HALMASHAURI YA KIPAPA Wakristo na Waislam: UJUMBE KWA AJILI YA MWISHO WA RAMADHAN
Wapendwa marafiki Waislam, 1. Mwisho wa mwezi wa Ramadhan unavyokaribia, kufuatia mapokeo mema yaliyoanzishwa vizuri sana, ninayo furaha kuwaletea matashi mema kabisa ya Halmashauri ya Kipapa kwa ajili ya Mazungumzano na Dini mbalimbali. Ndani ya mwezi huu Wakristo walio karibu nanyi wameshiriki tafakari zenu na maadhimisho mbalimbali ya familia zenu; mazungumzano na urafiki vimeimarishwa. Mungu atukuzwe! 2. Kama ilivyokuwa nyakati zilizopita, mkutano wa kirafiki wa aina hii unatupatia fursa kutafakari pamoja juu ya mada yenye manufaa kwetu sote itakayotajirisha kubadilishana kwetu na kufahamiana vizuri zaidi katika tunu zile tunazoshirikiana na hata zile tofauti zetu. Mwaka huu ningependa kupendekeza mada inayohusu familia. 3. Moja ya Hati za Mtaguso wa Pili wa Vatikano, Furaha na Matumaini (Gaudium et Spes) inayoshughulika na Kanisa katika ulimwengu wa leo, inasema: ÂÂUsitawi wa mtu binafsi na wa jamii ya kibinadamu na ya Kikristo hufungamana kabisa na hali njema ya jumuiya ya kindoa na ya kifamilia. Kwa hiyo Wakristo, pamoja na wote wenye kuiheshimu sana jumuiya hiyo, wanaifurahia kwa moyo mkunjufu misaada mbalimbali ambayo kwayo wanadamu wa siku za leo waweza kuendelea katika kuisitawisha jumuiya hiyo ya upendo, na katika kuuheshimu uhai na kwa njia hiyo inawasaidia watu wa ndoa na wazazi katika kutekeleza jukumu lao muhimu, na kutoka misaada hiyo wao hutarajia kupata manufaa yaliyo bora zaidi, pamoja na kufanya juhudi ili itoleweÂÂ (n. 47). 4. Maneno haya yanatupatia fursa maalum kwamba maendeleo ya mtu binafsi na ya jamii hutegemea sana usitawi wa familia! Wako watu wangapi wanaobeba, na mara nyingi kwa maisha yao yote, uzito wa majeraha ya msingi mgumu au wenye maumivu ya kifamilia? Wanaume wangapi na wanawake wangapi sasa walio katika dimbwi la madawa ya kulevya au vurugu wanatafuta bure kuondokana na maumivu waliyoyapata toka utotoni? Wakristo na Waislam wanaweza, na hawana budi kufanya kazi pamoja kulinda heshima ya familia, leo na baadaye. 5. Kwa kuwa Waislam na Wakristo wote wanaheshimu sana familia, tumekwishapata nafasi nyingi za kufanya kazi pamoja katika eneo hili, kuanzia kiwango mahalia hadi cha kimataifa. Familia, mahali pale ambapo upendo na uhai, heshima kwa jirani na ukarimu vinapatikana na kuendelezwa, ndicho ÂÂkiini cha msingi wa jamii.ÂÂ 6. Waislam na Wakristo kamwe wasisite, si kuzisaidia tu familia zilizo katika magumu, bali pia kushirikiana na wale wote wanaotegemeza udumifu wa familia kama asasi na utendaji wa wajibu wa wazazi, kwa namna ya pekee katika eneo la elimu. Sina budi kuwakumbusha kwamba familia ndiyo skuli ya kwanza ambamo mtu hujifunza kuwaheshimu watu wengine, akijali utu na tofauti ya kila mtu. Mazungumzano kati ya Dini Mbalimbali na matumizi ya uraia hayawezi kufaidisha isipokuwa kutokana na hilo. 7. Marafiki wapendwa, sasa kwa kuwa mfungo wenu unakaribia kumalizika, ninatumaini kwamba ninyi, pamoja na familia zenu na wale walio karibu nanyi, mkiwa mmetakaswa na kufanywa wapya kwa njia ya mazoezi yale ambayo yanapendwa sana na dini yenu, mjaliwe kujua utulivu na usitawi katika maisha yenu. Naye Mungu Mwenyezi awajaze Rehema Yake na Amani. Jean-Louis Kardinali Tauran Askofu Mkuu Pier Luigi Celata
PONTIFICAL COUNCIL FOR INTERRELIGIOUS DIALOGUE
|
|