The Holy See
back up
Search
riga

HALMASHAURI YA KIPAPA
KWA AJILI YA MAZUNGUMZANO NA DINI MBALIMBALI
  

Wakristo na Waislam:
Kwa pamoja kuutokomeza umasikini
 

UJUMBE KWA AJILI YA MWISHO WA RAMADHAN

‘Id al-Fitr 1430 H. / 2009 A.D.

 

 

Wapendwa Marafiki Waislam,                       

1. Kwa nafasi ya sikukuu yenu inayohitimisha mwezi wa Ramadhan, ningependa kuwafikishia matashi yangu mema kabisa  ya amani na furaha, na pia, kwa njia ya Ujumbe huu napendekeza mada hii kwa ajili ya tafakari yetu: Wakristo na Waislam: kwa pamoja katika kuutokomeza umasikini.

2. Ujumbe huu wa  Halmashauri ya Kipapa kwa ajili ya Mazungumzano na Dini Mbalimbali umekuwa ni mapokeo yanayohifadhiwa kwa upendo mkubwa na sisi sote, ambao  unangojewa kila mwaka na kwa hakika hiki ni chanzo cha furaha. Kwa miaka sasa, imekuwa ni fursa ya kukutana kwa moyo wa mapendo katika nchi nyingi baina ya Wakristo na Waislam. Mara nyingi unashughulikia jambo linalotuhangaisha sisi sote. Jambo ambalo linatusukuma kubadilishana mawazo kwa imani na uwazi. Hayo  yote yanayoonjwa kama alama za urafiki baina yetu, kwa nini tusimshukuru Mungu?.

3. Tukija kwenye mada ya mwaka huu, mwanadamu katika hali ya ufukara kwa hakika ni jambo lililo katikati ya kiini cha amri ambazo, katika imani mbalimbali,  wote tunakipenda. Uangalifu, huruma na msaada ambao sisi sote, kaka na dada katika ubinadamu, tunaweza kumwezesha mtu aliye masikini  kupata nafasi yake katika jamii ya watu, ni ushahidi hai wa Mapendo ya Mwenyezi, kwa sababu ni mtu kama huyo ambaye Yeye anatutaka tumpende na kumsaidia, bila ubaguzi wa jinsia.

Wote tunajua kwamba umasikini una nguvu ya kunyanyasa na kusababisha mateso yasiyovumilika, mara nyingi ni chanzo cha upweke, hasira, hata chuki na shauku ya kulipa kisasi. Unaweza kuchochea vitendo vya uhasama kwa kutumia  njia zozote zile  zinazopatikana, hata kutafuta kuzihalalisha kwa misingi ya kidini, au  kutwaa mali ya mtu mwingine, pamoja na amani yake na usalama, kwa jina la kile kinachodaiwa kuwa ni “haki ya Mungu”. Hii ndiyo sababu kukabiliana na suala la misimamo  isiyo na ukadiri na vurugu inahusu kukabiliana na umasikini kwa njia ya kusukuma maendeleo kamili ya mwanadamu, yale ambayo Papa Paulo VI aliyaainishia kama “ jina jipya kwa ajili ya  amani” (Encyclical Letter Populorum Progessio , 1975, n. 76).

Katika Waraka wake wa Kiinsiklika wa hivi karibuni Caritas in veritate juu ya maendeleo kamili ya mwanadamu katika upendo na ukweli, Papa Benedikto XVI, akizingatia muktadha wa sasa wa juhudi za kukuza maendeleo, anatilia mkazo hitaji la  “usanisi mpya wa ubinadamu” (n. 21) ambao unalinda uwazi wa mtu kwa Mungu, unaompa  mtu mahali pake duniani kama “kiini na kilele” (n. 57) . Maendeleo ya kweli, basi, hayana budi kupangiliwa hivi kwa ajili ya “ mtu mzima na kwa kila binadamu” (Populorum Progressio, n. 42).

4.  Katika mazungumzo yake katika nafasi ya Siku ya Kiulimwengu ya Amani tarehe 1 Januari 2009, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alitofautisha aina mbili za umasikini: umaskini unaotakiwa kupigwa vita na umasikini unaotakiwa kuukumbatiwa.

Umaskini unaotakiwa kupigwa vita uko mbele ya macho ya kila mtu: njaa, kukosa maji safi na salama, uhaba wa matibabu, ukosefu wa makazi, kutotosheleza kwa miundo mbinu ya elimu na tamaduni, kutojua kusoma na kuandika, bila kutaja pia miundo mipya ya umasikini “katika jamii zilizoendelea sana kwa utajiri, kuna ushahidi wa umasikini wa kuwekwa pembezoni, wa kupendelewa, kimaadili, na  kiroho” (Message for the World Day of Peace, 2009, n. 2).

Umasikini wa kukumbatiwa ni mtindo ule wa maisha ambayo ni ya kawaida na muhimu, kuzuia ubadhirifu na kujali mazingira na uzuri wa viumbe. Umasikini huu unaweza pia kuwa, walau katika vipindi fulani vya mwaka, ule wa kudunduliza na kufunga. Ni umasikini tunaouchagua unaotuwezesha kwenda nje yetu wenyewe, tukipanua moyo wetu.

5. Kama waumini, hamu ya kufanya kazi pamoja kwa ajili ya jawabu la haki na la kudumu la balaa la umasikini hakika inajumuisha kutafakari juu ya matatizo mazito ya zama zetu, na inapowezekana, kushirikishana msimamo wa pamoja wa kuyatokomeza. Kwa hali hiyo, rejea za hali zile za umasikini zinazohusiana na masuala ya utandawazi wa jamii zetu zina maana za kiroho na kimaadili, kwa sababu wote wanaposhiriki wito wa kujenga familia ya mwanadamu – mtu mmoja moja ,  makabila, na mataifa – wanajiweka  kufuatana na misingi ya udugu na madaraka.

6. Mafunzo makini ya hali ngumu ya umasikini yanatupeleka moja kwa moja hasa  kwenye vianzo na ukosefu wa heshima ya hadhi ya kuzaliwa nayo ya mwanadamu na kututaka  mshikamano wa jumla, kwa mfano kwa njia ya kuchukua  “kanuni ya jumla ya kimaadili: (Yohane Paulo II,   Address to ThePontifical  Academy of Sociail Sciences, 27 April 2001, n.4) ambazo taratibu zake  zisingekuwa tu na hali ya mapatano, bali pia kwa vyovyote zingesimikwa katika sheria ya maumbile iliyoandikwa na Muumba katika dhamiri ya kila mwanadamu (rej. Rum 2, 14-15).

7. Inaonekana kwamba katika  nafasi mbalimbali za ulimwengu tumevuka kutoka kuvumiliana   hadi kukutana pamoja, kuanzia mang’amuzi ya jumla tunayoishi na mahangaiko tuliyoshirikiana. Hii ni hatua muhimu kwa kuendelea mbele.

Katika kumpa kila mmoja utajiri wa maisha unaotokana na sala, kufunga na mapendo ya mmoja kwa mwingine, je, isingewezekana kufanya mazungumzano kuchota nguvu hai za wale wanaosafiri kumwendea Mungu?

Masikini wanatuuliza, wanatupa changamoto, lakini juu ya yote wanatutaka kushirikiana katika daawa ya heshima:  kuutokomeza umaskini!

Heri ya ‘Id al-Fitr!

 

Jean-Louis Kardinali TauranRais

Askofu Mkuu Pier Luigi Celata
Katibu

 

 

Pontifical Council for Interreligious Dialogue
00120 Vatican City
Tel: +39.06.6988 4321 / 06.6988 3648
Fax: +39.06.6988 4494
E-mail: dialogo@interrel.va

  

  

top