Index

  Back Top Print

SINODI YA MAASKOFU

________________________________________________________

MKUTANO MKUU WA DHARURA WA 3

CHANGAMOTO ZA KICHUNGAJI KUHUSU FAMILIA
KATIKA MAZINGIRA YA UINJILISHAJI

Hati ya Kimaandalizi

Mji wa Vatikano, 2013

________________________________________________________

 

I – SINODI: FAMILIA NA UINJILISHAJI

Utume wa kuihubiri Injili kwa viumbe vyote umekabidhiwa moja kwa moja na Bwana kwa wanafunzi wake, na Kanisa limekuwa likitekeleza utume huo katika historia, karne kwa karne. Mgogoro wa kijamii na wa kiimani ulio dhahiri sana katika ulimwengu wa hivi leo, unakuwa changamoto ya kichungaji kwa utume wa kiuinjilishaji kuhusu familia, ambayo ni kiini na kijenzi chenye uhai cha jamii na cha jumuiya ya kikanisa. Kutangaza Injili ya familia katika mazingira hayo ni kazi ambayo inaonekana ya haraka na ya lazima sana kuliko zamani. Umuhimu wa mada hii unaakisiwa na tendo la Baba Mtakatifu la kuamua kuitisha Sinodi ya Maaskofu, ambao utakuwa na utaratibu wa kazi katika awamu mbili: awamu ya kwanza, Mkutano mkuu wa dharura mnamo mwaka 2014, unaolenga kubainisha “status quaestionis” (hali halisi ya suala zima) na kukusanya mang’amuzi na mapendekezo ya Maaskofu katika kuitangaza na kuiishi kwa namna inayoaminika Injili ya familia; awamu ya pili, Mkutano mkuu wa kawaida utakaoadhimishwa mwaka 2015, ili kutafuta miongozo ya kiutendaji kwa ajili ya uchungaji wa nafsi ya kibinadamu na wa familia.

Yapo leo mbele yetu masuala ambayo hayakuwepo mpaka miaka michache iliyopita, kuanzia kuenea kwa zoezi la watu kukaa kinyumba, ambao hawafungi sakramenti ya ndoa na mara nyingine wanalikataa kabisa wazo lenyewe la ndoa kama sakramenti, hadi miungano ya watu wa jinsia moja, ambao si mara chache wanaruhusiwa kuasili watoto. Kati ya mazingira mapya mengi yanayodai uangalifu na bidii ya kiuchungaji ya Kanisa inatosha kukumbuka: ndoa za mseto (kati ya watu wa madhehebu au dini tofauti); familia zinazobaki na mzazi mmoja tu; ndoa za wake wengi; ndoa zinazopangwa, na tatizo linalotokana nazo la mahari, ambayo mara nyingine inaeleweka kama gharama ya kumnunua mwanamke; mfumo wa matabaka; desturi ya kutokuwajibika na ya kudhani kuwa kifungo cha ndoa si cha kudumu; mitindo ya kupigania haki za wanawake yenye uhasama kwa Kanisa; watu wengi kuhamia nchi nyingine na marekebisho ya dhana yenyewe ya familia; mfumo wa kukubali dhana nyingi na tofauti juu ya ndoa; athari za vyombo vya habari juu ya utamaduni wa watu katika namna ya kuielewa ndoa na maisha ya kifamilia; mielekeo ya fikra iliyopo chinichini ya mapendekezo ya kisheria ambayo inadhalilisha kudumu na uaminifu wa agano la ndoa; kukithiri kwa mazoea ya kukodisha tumbo la uzazi (wombs for hire, kuzaa badala ya mwingine); namna mpya za kufafanua haki za kibinadamu. Lakini hasa ndani ya Kanisa (mazingira mapya ni) kudhoofika au kupotea kabisa kwa imani katika hali ya kisakramenti ya ndoa na katika uwezo wa kuponya wa Sakramenti ya Kitubio.

Kutokana na hayo yote, inaeleweka jinsi ilivyo muhimu kwamba Maaskofu wa dunia nzima waitwe kukusanyika “cum et sub Petro” (chini na pamoja na Papa) ili kukabili changamoto hizo. Kama, kwa mfano, tukilifikiria suala kwamba katika mazingira ya sasa watoto na vijana wengi, waliozaliwa katika ndoa zisizo kadiri ya kanuni za kikristo, hawataweza kamwe kuwaona wazazi wao kusogea kwenye sakramenti, inaeleweka jinsi zilivyo za haraka changamoto ambazo mazingira ya siku hizi yanazusha kwa uinjilishaji, nayo ni mazingira ambayo yameenea pande zote za “kijiji dunia” (global village). Inaendana kwa namna ya pekee kabisa na jambo hilo jinsi yanavyopokelewa wazi siku hizi mafundisho juu ya huruma ya Mungu na upendo kwa watu waliojeruhiwa, kijamii au kimaisha: Hivyo, matarajio yanayojitokeza kuhusu maamuzi ya kiuchungaji yatakayofanywa mintarafu familia ni mengi sana. Tafakari ya Sinodi ya Maaskofu juu ya mada hizo inaokeana kwamba inahitajika na ni ya haraka, tena inadaiwa kama namna ya kuonyesha upendo wa Wachungaji kwa wale waliokabidhiwa kwao na kwa familia nzima ya kibinadamu.

II - KANISA NA INJILI YA FAMILIA

Habari njema ya upendo wa Mungu inabidi itangazwe kwa wale wanaoishi mang’amuzi hayo ya msingi ya kibinadamu. Wanaoyaishi kama watu binafsi, kama jozi na kama watu wenye ushirika ulio wazi katika kupokea zawadi ya watoto, ushirika ambao ni jumuiya ya kifamilia. Mafundisho ya imani kuhusu ndoa inabidi yaelezwe kwa namna iliyo rahisi kuielewa na yenye mafanikio, ili yenyewe yaweze kuifikia mioyo na kuigeuza kadiri ya mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa katika Kristo Yesu.

Kuhusu kukumbusha vyanzo vya kibiblia juu ya ndoa na familia, katika hati hii tunatoa marejeo ya msingi tu. Vilevile kuhusu hati za Majisterio inaonekana kuwa inafaa kudokeza tu hati zile zenye mafundisho ya Kanisa kwa Wakristo wote duniani kote, kwa kuongeza matini chache za Baraza la Kipapa la Familia na itaachwa juu ya Maaskofu watakaoshiriki Sinodi kazi ya kuzikumbusha hati nyingine za taasisi zao za kiaskofu.

Katika nyakati zote na katika tamaduni mbalimbali haijawahi kukosekana wala mafundisho wazi ya wachungaji wala ushuhuda halisi wa waamini, wanaume kwa wanawake, ambao katika mazingira tofauti tofauti waliishi Injili ya familia kama tunu isiyopimika kwa maisha yao na ya watoto wao. Bidii kwa ajili ya Sinodi ya dharura ijayo inasukumwa na kutegemezwa na hamu ya kuwashirikisha wote, kwa nguvu zaidi, katika huo ujumbe, kwa kutumaini kwamba hivyo “hazina ya ufunuo iliyokabidhiwa kwa Kanisa ijaze zaidi na zaidi mioyo ya waamini” (DV, 26).

Mpango wa Mungu, Muumba na Mkombozi

Uzuri wa ujumbe wa Biblia juu ya familia una mzizi wake katika kuumbwa kwa mwanamume na mwanamke, wote wawili wakiwa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (rej. Mwa 1:24-31; 2:4b-25). Wakiwa wamefungwa na kifungo cha kisakramenti kisichoweza kufunguliwa, watu wa ndoa wanaishi uzuri wa upendo, wa ubaba, wa umama na wa ile hadhi iliyo kuu ya kushiriki hivyo kazi ya Mungu ya kuumba.

Katika zawadi ya tunda la muungano wao, wanapokea jukumu la kuwakuza na kuwalea watu wengine kwa ajili ya mustakabali wa wanadamu. Kupitia uzazi, mwanamume na mwanamke hutekeleza katika imani wito wa kushiriki pamoja na Mungu katika utunzaji wa dunia na katika ukuzaji wa familia ya wanadamu.

Mwenye Heri Yohane Paulo II alieleza suala hili katika Familiaris Consortio: “Mungu aliumba mwanadamu katika sura na mfano wake (taz. Mwa 1:26nk): kama vile alivyomwita katika uhai kwa sababu ya upendo, vilevile alimwita kwa ajili ya upendo. Mungu ni upendo (rej. 1Yoh 4:8) na anaishi ndani yake binafsi fumbo la ushirika wa upendo. Kwa kuwaumba watu kwa sura yake na kuwatunza daima katika uzima, Mungu anaweka ndani ya mwanamume na mwanamke wito wa upendo na umoja, na hivyo hata uwezo na wajibu (wa kutekeleza wito huo) (rej. GS, 12). Hivyo, upendo ni wito wa msingi na wa awali wa kila mwanadamu” (FC, 11).

Mpango wa Mungu muumba, ambao dhambi imeuharibu (rej. Mwa 3:1-24), umedhihirika katika historia kupitia matukio ya taifa teule hadi utimilifu wa nyakati, wakati Mwana wa Mungu kwa kufanyika mwili si kwamba alithibitisha tu matakwa ya Mungu ya kuokoa, lakini pia alithibitisha ukombozi unaojalia neema ya kuyatii matakwa hayo.

Mwana wa Mungu, Neno aliyefanyika mwili (rej. Yn 1:14) katika tumbo la Mama Bikira, aliishi na kukua katika familia ya Nazareti, na alishiriki arusi ya Kana ambapo aliitunukia sherehe kwa “ishara” yake ya kwanza (rej. Yn 2:1-11). Yeye alipokea kwa furaha ukaribishaji wa kindugu wa wanafunzi wake wa kwanza (rej. Mk 1:29-31; 2:13-17) na aliifariji familia ya rafiki zake huko Bethania wakati wa msiba (rej. Lk 10:38-42; Yn 11,1-44). Yesu Kristo alitengeneza upya uzuri wa ndoa kwa kutangaza tena mpango mzima wa Mungu, uliokuwa umeachwa kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya wanadamu, hata katika mapokeo ya taifa la Israeli (rej. Mt 5:31-32; 19:3-12; Mk 10:1-12; Lk 16:18). Kwa kurudia kwenye mpango wa asili Yesu aliufundisha umoja na uaminifu wa watu wa ndoa, akikataa talaka na uzinzi.Hasa kwa kupitia uzuri wa ajabu wa upendo wa kibinadamu – ambao ulikuwa umeshaadhimishwa katika Wimbo Ulio Bora kwa mikazo iliyovuviwa – na kwa kupitia uzuri wa kifungo cha ndoa – kilichodaiwa na kulindwa na Manabii kama Hosea (rej. Hos 1:2, 3:3) na Malaki (rej. Mal 2:13-16) – Yesu aliithibitisha hadhi ya asili ya upendo wa kindoa wa mwanamume na wa mwanamke.

Mafundisho ya Kanisa mintarafu familia

Hata katika jumuiya za awali za Kikristo familia ilionekana kuwa “Kanisa la nyumbani” (rej. KKK, 1655). Katika sehemu zile zinazojulikana kama “kanuni za familia” za Nyaraka za Mitume za Agano Jipya, familia pana za dunia ya kale (ancient world) inaeleweka kuwa ni mahali pa mshikamano thabiti baina ya waume na wake, baina ya wazazi na watoto, na baina ya wenye nacho na walio maskini (rej. Efe 5:21-6:9; Kol 3:18-4:1; 1Tim 2:8-15; Tit 2:1-10; 1Pet 2:13-3:7; rej. pia Waraka kwa Filemoni). Hususan, Waraka kwa Waefeso unatambua upendo wa kindoa baina ya mwanamume na mwanamke kama “siri kubwa”, inayodhihirisha duniani upendo wa Kristo na wa Kanisa (rej. Efe 5:31-32).

Katika karne zote, hasa katika enzi za sasa hadi siku hizi, Kanisa halijakosa kufundisha daima na kuendeleza mafundisho yake mintarafu familia na ndoa, ambazo zinaliunda. Mmoja wa misemo mikuu kuhusu familia na ndoa ulipendekezwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano katika Konstitusyo ya Kichungaji Gaudium et Spes, ambao, katika kuainisha baadhi ya masuala nyeti, ulitumia sura moja nzima ili kusisitiza hadhi ya ndoa na ya familia, kama inavyoonekana katika maelezo ya thamani yake kwa ajili ya kujenga jamii: “Familia ni mahali ambapo vizazi vilivyo tofauti vinakutana na kusaidiana kati yao kuifikia busara ya kibinadamu iliyo kamili zaidi, na kuunganisha pamoja haki za mtu binafsi na madai mengine ya maisha ya kijamii. Hivyo familia ndiyo msingi wa jamii” (GS, 52). Mwito wake wa kuweka Kristo kama kiini cha maisha ya kiroho na kiimani ya wanandoa umesisitizwa sana kwa namna inayogusa: “Wanandoa wenyewe, walioumbwa kwa sura ya Mungu aliye hai, na waliowekwa kwenye hadhi halisi ya kila mtu, na waungane kwa upendo ulio sawa wa kila mmoja kwa mwenzie, na nia moja na hatimaye na utakatifu wa pamoja. Na hivyo watamfuata Kristo aliye asili ya uzima katika furaha na majitoleo ya wito wao. Na kwa njia ya upendo wao mwaminifu wapate kuwa mashahidi wa lile fumbo la pendo ambalo Bwana amelifunua kwa ulimwengu, kwa njia ya kifo na ufufuko wake” (GS, 52).

Baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano, waandamizi wa Mt. Petro walitajirisha mafundisho hayo mintarafu ndoa na familia, hususan Papa Paulo wa VI katika Insiklika Humanae Vitae, ambayo inatoa kanuni na miongozo mahususi. Baadaye, katika Mausia yake ya Kitume Familiaris Consortio, Papa Yohane Paulo wa II alikazia kusisitiza mpango wa Mungu katika kweli ya asili ya upendo wa kindoa na ya familia: “ ‘Mahali’ pa pekee ambapo majitoleo hayo yanawezeshwa katika ukweli wake wote ni ndoa, yaani agano la upendo wa kijozi lililofungwa kwa hiari na kwa kusudi, ambamo mwanamume na mwanamke wanakubali ushirika wa ndani wa maisha na upendo uliotakwa na Mungu mwenyewe (rej. GS, 48), nao katika mwanga huu tu huonyesha maana yake ya kweli. Asasi ya ndoa si kuingilia kati kusikotakiwa kwa upande wa jamii au mamlaka, wala si kulazimisha muundo fulani unaotoka nje. Bali ndoa ni hitaji la ndani la agano la upendo wa kijozi, agano ambalo lathibitishwa hadharani kuwa ni moja na pekee, kwa kusudi la kuishi katika uaminifu kamili kwa mpango wa Mungu, aliye Muumba. Uhuru wa mtu, mbali na kubanwa na madai ya uaminifu huo, hulindwa dhidi ya kila aina ya unafsia (subjectivism) au relativizimi (“nionavyo mimi”), na hufanywa kuwa mshiriki katika Hekima mbunifu” (FC, 11).

Katekisimu ya Kanisa Katoliki hukusanya pamoja vipengele vya msingi vya mafundisho hayo: Agano la ndoa, ambalo kwalo mume na mke huunda kati yao jumuiya ya ndani ya uzima na mapendo, limeanzishwa na kupewa sheria zake na Muumba. Kwa maumbile yake limepangwa kwa ajili ya mema ya wanandoa, pia kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Kristo Bwana aliiinua ndoa baina ya wabatizwa katika hadhi ya sakramenti [rej. Mtaguso wa Pili wa Vatikano, GS, 48; Sheria Kanuni ya Kanisa, 1055, 1]” (KKK 1660).

Mafundisho yanayotolewa katika Katekisimu inagusia kwa upande mmoja kanuni za msingi za kitheolojia, na pia, kwa upande mwingine, mienendo ya kimaadili, kwa kuielezea chini ya vipengele viwili tofauti: Sakramenti ya Ndoa (na. 1601-1658) na Amri ya Sita (na. 2331-2391). Kwa kusoma kwa makini vipengele hivyo vya Katekisimu hupatikana uelewa wa kisasa wa mafundisho ya kiimani, unaosaidia kazi ya Kanisa mbele ya changamoto za siku hizi. Huduma ya kiuchungaji ya Kanisa inapata msukumo katika ukweli wa kutazama ndoa kama sehemu ya mpango wa Mungu, aliyeumba mume na mke, na ambaye, katika utimilifu wa nyakati, aliufunua katika Yesu ukamilifu wa upendo wa kindoa kwa kuuinua kwenye hadhi ya sakramenti. Ndoa ya Kikristo yenye misingi yake katika agano, hupewa pia matokeo yake, yaani mema na wajibu wa wanandoa. Wakati huohuo, ndoa haina kinga dhidi ya athari za dhambi (rej. Mwa 3:1-24), ambayo huweza kusababisha majeraha makubwa na pia matumizi mabaya ya hadhi ya sakramenti.

Insiklika ya hivi karibuni ya Papa Fransisko, Lumen Fidei, inaongea juu ya familia katika muktadha wa tafakari kuhusu namna imani inavyofunua “jinsi vinavyoweza kuwa imara vifungu kati ya watu pale ambapo Mungu yu katikati yao” (LF, 50). “Mazingira ya kwanza ambamo imani inamulika mji wa binadamu ni familia. Ninaufikiria kwanza kabisa na hasa umoja wa kudumu wa mume na mke katika ndoa. Umoja huo umezaliwa na upendo wao, nao ni ishara ya upendo wa Mungu mwenyewe, na ya ukubali na upokezi wa wema wa utofauti wa kijinsia, ambamo wanandoa wanaweza kuwa mwili mmoja (rej. Mwa 2:24) na wanawezeshwa kuzaa kiumbe mpya mwenye uhai, dhihirisho la wema wa Muumba, la hekima yake na la mpango wake wa upendo. Kwa kuwa na misingi katika upendo huo, mume na mke huweza kuahidiana upendo kwa kitendo kinachohusisha maisha yao yote na kuakisi fani nyingi za imani. Kuahidi upendo wa daima kunawezekana pale ambapo tunatambua kuwepo mpango ulio mkubwa kuliko mawazo na matendo yetu wenyewe, mpango unaotutegemeza na kutuwezesha kukabidhi mustakabali wetu wote kwa yule tumpendaye” (LF, 52). “Imani si kimbilio la waoga, bali ni jambo ambalo linakuza maisha yetu. Inatuwezesha kutambua mwito wa ajabu, wito wa upendo. Inatuhakikishia kwamba upendo huo ni aminifu, na kwamba inafaa kuambatana nao, kwani una misingi yake katika uaminifu wa Mungu, ulio thabiti kuliko udhaifu wetu wowote” (LF, 53).

 

III. Maswali

Maswali yafuatayo yatayasaidia Makanisa mahalia kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya Sinodi hii ya Dharura, ambayo inalenga kutangaza Injili mbele ya changamoto za kiuchungaji za leo zinazohusu familia.

1. Kuhusu uenezi wa Mafundisho juu ya Familia kama yanavyopatikana katika Maandiko Matakatifu na Majisterio ya Kanisa

a) Eleza jinsi yanavyoeleweka na watu siku hizi mafundisho ya Kanisa Katoliki juu ya thamani ya familia yanavyopatikana katika Biblia, “Gaudium et Spes”, “Familiaris Consortio” na nyaraka nyingine za Mafundisho Maalum (Majisterio) ya Kanisa baada ya Mtaguso Mkuu. Kwa namna gani waamini wetu wanaelimishwa kuhusu maisha ya familia kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa?

b) Pale ambapo mafundisho ya Kanisa yanajulikana, je, yanakubaliwa kikamilifu au yanatokea matatizo wakati wa utekelezaji wa mafundisho haya? Matatizo yapi?

c) Kwa njia gani mafundisho ya Kanisa yanaenezwa katika muktadha wa mipango ya kiuchungaji kwa ngazi ya taifa, jimbo na parokia? Je, katekesi ipi inatolewa kuhusu familia katika ngazi hizi?

d) Kwa kiwango gani – na hasa juu ya vipengele gani – mafundisho haya yanajulikana kweli, yanakubalika, kukataliwa na/au kukosolewa katika mazingira nje ya Kanisa? Je, ni vipengele gani vya kitamaduni vinavyoyazuia mapokezi kamili ya mafundisho ya Kanisa juu ya familia?

2. Juu ya ndoa kwa mujibu wa sheria ya maumbile

a) Je, dhana ya sheria ya maumbile (Natural Law) inashika nafasi gani katika utamaduni wa jamii: kwa ngazi ya kitaasisi, ya kielimu na ya kitaalamu na kwa ngazi ya umma? Ni maoni gani ya kianthropolojia yanaongoza majadiliano juu ya msingi ya kimaumbile ya familia?

b) Dhana ya sheria ya maumbile juu ya muungano kati ya mwanamume na mwanamke kwa kawaida imekubaliwa kwa wabatizwa kwa ujumla?

c) Kwa namna gani sheria ya maumbile juu ya muungano kati ya mwanamume na mwanamke kwa lengo la kuijenga familia inakosolewa au kupingwa katika maisha na katika nadharia? Kwa jinsi gani inapendekezwa na kuendelezwa katika taasisi ya kiserikali na ya kikanisa?

d) Kwa namna gani zinashughulikiwa changamoto za kiuchungaji ikiwa Wakatoliki wasioshiriki au wanaojitambua kama wasiosadiki wanaomba adhimisho la sakramenti ya ndoa?

3. Utume wa kifamilia katika mazingira ya uinjilishaji

a) Je, ni uzoefu gani uliojitokeza katika miaka (miongo) hii ya hivi karibuni kwa ajili ya maandalizi ya sakramenti ya ndoa? Juhudi gani zimetafutwa ili kuchochea kazi ya uinjilishaji wa wanandoa na familia? Kwa njia gani ufahamu wa familia kama “Kanisa la nyumbani” huweza kukuzwa?

b) Umefanikiwa kupendekeza njia za sala katika familia, ambazo zinadumu licha ya utata wa maisha ya leo na utamaduni uliopo?

c) Katika hali iliyopo sasa katika mtikisiko kati ya vizazi, kwa namna gani familia za Kikristo zimekuwa zikitimiza wito wao wa kurithisha imani?

d) Kwa namna gani Makanisa mahalia na vyama vya kiroho vya familia vimeunda mikakati maalum ya kiutendaji?

e) Wanandoa na familia wanaweza kutoa mchango maalum upi ili kueneza mtazamo kamili wa wanandoa na wa familia ya Kikristo unaoaminika leo?

f) Ni mambo gani ambayo Makanisa yamejitahidi kuyatekeleza kwa ajili ya kuyasaidia malezi ya wanandoa wapya na wanandoa wenye matatizo?

4. Juu ya huduma ya kiuchungaji kwa ajili ya kuzisaidia baadhi ya hali ngumu za wanandoa

a) Kukaa kinyumba bila ndoa kama majaribio (ad experimentum) ni hali muhimu katika Kanisa mahalia lako? Kwa asilimia gani mnaweza kuthamini hali hii kati ya wanaooana?

b) Ipo miungano ambayo haitambuliwi wala kwa kibali cha kidini wala cha kiserikali? Zipo takwimu kamili za miungano hiyo?

c) Walioachana na waliopeana talaka ni wengi katika Kanisa mahalia lako? Kwa asilimia gani mnaweza kutathmini tatizo hilo? Kwa njia gani au kwa mikakati ya kiuchungaji gani inawezekana kuwasaidia wanandoa hawa?

d) Katika hali hizo zote zisizo halali, waliobatizwa wanaishi kwa namna gani tatizo lao? Wanalitambua hilo? Hawajali tu tatizo hilo? Wanajisikia kutengwa na wanaishi na mateso hali ya kutokuwa na uwezo wa kupokea sakramenti?

e) Je, masuala gani watu wa talaka na waliooa tena wanaleta kwa Kanisa kuhusu upokeaji wa sakramenti ya Ekaristi na ya Upatanisho? Wangapi wanaomba sakramenti hizi kati ya watu hao wanaojikuta katika hali kama hiyo?

f) Kurahisisha sheria ya Kanisa kwa upande wa utambuzi wa tamko la ubatili wa kifungo cha ndoa kungeweza kutoa mchango chanya kwa ufumbuzi wa matatizo ya watu wanaohusika? Kama ndiyo, kwa namna gani?

g) Upo utume kwa kuwasaidia watu wenye matatizo hayo? Kwa namna gani kazi hii ya kiuchungaji inatekelezwa? Kuna mikakati kuhusu matatizo hayo kwa ngazi ya kitaifa na ya kijimbo? Kwa ajili ya wale waliotengana na watu wa talaka waliooa au kuolewa tena kwa jinsi gani wanatangaziwa huruma ya Mungu, na kwa jinsi gani Kanisa linawasaidia watu hawa katika safari yao ya kiimani?

5. Juu ya muungano wa watu wa jinsia moja

a) Je, kuna sheria katika nchi yako kwa ajili ya utambuzi wa kiraia kuhusu muungano kati ya watu wa jinsia moja, sheria ambayo inaupa hadhi sawasawa na ile ya ndoa?

b) Makanisa mahalia yanashika mtazamo gani juu ya serikali ambayo inakubali muungano kati ya watu wa jinsia moja, na pia juu ya watu wanaohusika katika aina hii ya muungano?

c) Misaada gani ya kiuchungaji inawezekana kutolewa kwa ajili ya watu ambao wameamua kuishi aina hii ya muungano?

d) Kama kuna muungano wa watu wa jinsia moja ambao wamewaasili watoto, inawezekana kufanya nini kiuchungaji kwa upande wa urithishaji wa imani?

6. Malezi ya watoto katika hali ya ndoa isiyo halali

a) Je, kuhusu kipengele hiki watoto na vijana wanayo idadi ya uwiano gani kulingana na watoto waliozaliwa na kukulia katika familia za Kikristo?

b) Kwa mtazamo gani wazazi wenye hali hiyo wanalielekea Kanisa? Wanaomba nini? Sakramenti tu au hata katekesi na mafundisho ya dini kwa ujumla?

c) Kwa namna gani Makanisa mahalia wanawasaidia wazazi wa watoto hawa kutoa elimu ya Kikristo kwa ajili ya watoto wao?

d) Kwa utaratibu gani sakramenti zinatolewa kwa watoto hawa: mafundisho, utoaji wa sakramenti zenyewe, na usindikizaji wa watoto wakiisha kupokea sakramenti?

7. Juu ya wanandoa na utetezi wa uhai

a) Je, Wakristo siku hizi wanao ufahamu gani kuhusu mafundisho ya Humanae Vitae na juu ya uzazi wenye uwajibikaji? Wanaweza kubainisha kimaadili mipango mbalimbali wa uzazi? Ufafanuzi gani unaweza kupendekezwa kuhusu mada hii kwa mtazamo ya kiuchungaji?

b) Mafundisho haya ya kimaadili yamekubaliwa? Vipengele vigumu gani vinazuia kukubaliwa kwa mafundisho hayo miongoni mwa asilimia kubwa ya majozi?

c) Mipango gani ya uzazi kwa njia ya asili inashauriwa na Makanisa ili kuwasaidia wanandoa kutekeleza mafundisho ya Humanae Vitae?

d) Je, una mang’amuzi gani kuhusu mada hii katika kushiriki Sakramenti ya Kitubio na ya Ekaristi?

e) Mawazo gani yanapingana kati ya mafundisho ya Kanisa na malezi ya kijamii kuhusu mada hii?

f) Kwa jinsi gani itawezekana kuchochea zaidi wazo na nia ya kuzaa? Kwa jinsi gani itawezekana kuhamasisha ukuaji wa idadi ya wanaozaliwa?

8. Juu ya uhusiano kati ya familia na mtu

a) Yesu Kristo hufunua fumbo na wito wa mtu. Jinsi gani familia huweza kuwa mahali pa pekee ili jambo hilo litimizwe?

b) Hali gumu gani za kifamilia katika dunia ya leo zinaweza kuwa kikwazo kwa mtu katika kumkuta Kristo?

c) Kwa kiasi gani mitikisiko ya imani ambayo watu wanaweza kung’amua inaathiri kwa kina na kwa mkazo maisha ya kifamilia?

9. Changamoto nyingine na mapendekezo

Kuna changamoto nyingine gani, au mapendekezo, kuhusu masuala yaliyochambuliwa katika maswali haya, ambazo mnazitambua kuwa ni ya haraka na muhimu kuzijadili?