[BE
-
CS -
DE -
EN -
ES -
FR -
IT -
HE -
HU -
LA -
PT -
SW -
ZH]
Konstitusio ya kidogma juu ya
ufunuo wa kimungu
Paulo Askofu Mtumishi wa watumishi
wa Mungu pamoja na Mababa wa Mtaguso mkuu ataka haya yakumbukwe daima
UTANGULIZI
1. Katika kusikiliza kwa uchaji NENO LA MUNGU (Dei Verbum) na
kulitangaza kwa tumaini thabiti, Mtaguso Mkuu unaungana na Mtakatifu Yohane
asemaye: “Tunawahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba,
ukadhihirika kwetu: hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi, ili
nanyi pia mpate kushirikiana nasi, na ushirika wetu ni pamoja na Baba na
pamoja na Mwana wake Yesu Kristo” (1Yoh. 1:2-3). Kwa hiyo, [Mtaguso huu],
ukifuata nyayo za Mtaguso wa Trento na Vatikano I, unadhamiria kueleza
mafundisho halisi juu ya ufunuo wa kimungu na kurithishwa (transmissione)
kwake. Mtaguso unataka ulimwengu usikie mbiu ya wokovu, ili kwa kusikia
uweze kusadiki, na kwa kusadiki uweze kutumaini, na kwa kutumaini uweze
kupenda[1].
Sura ya Kwanza
UFUNUO WENYEWE
Maumbile na maana ya ufunuo
2. Ilimpendeza Mungu, katika wema na hekima yake, kujifunua mwenyewe na
kulidhihirisha fumbo la mapenzi yake (taz. Efe 1:9); katika fumbo hilo, kwa
njia ya Kristo, Neno la Mungu aliyefanyika mwili, katika Roho Mtakatifu,
wanadamu wanapata njia ya kumwendea Baba na kushirikishwa hali ya kimungu (taz.
Efe 2:18; 2Pet 1:4). Kwa njia ya ufunuo huo Mungu asiyeonekana (taz. Kol
1:15; 1Tim. 1:17) katika upendo wake usio na mipaka anaongea na wanadamu
kama na marafiki (taz. Kut 33:11; Yn 15:14-15), tena hukaa nao (taz. Bar
3:38) ili kuwaalika na kuwapokea katika ushirika naye. Mpango huu wa ufunuo
hutimizwa kwa matukio na kwa maneno. Haya yameunganika kwa ndani kabisa,
kiasi kwamba kazi zilizotimizwa na Mungu katika historia ya wokovu
zinaonyesha na kuthibitisha mafundisho na yale yote yaliyomo katika maneno;
na maneno yanatangaza kazi na kuliangaza fumbo lililomo ndani yake. Aidha,
kwa njia ya ufunuo huo, ukweli kamili juu ya Mungu na juu ya wokovu wa
wanadamu unang’ara kwetu katika Kristo, ambaye Yeye mwenyewe ndiye mshenga
na utimilifu wa ufunuo wote[2].
Matayarisho ya ufunuo wa kiinjili
3. Mungu, anayeviumba na kuvihifadhi vitu vyote kwa njia ya Neno [wake] (taz.
Yn 1:3), anaendelea kuwapatia wanadamu ushuhuda juu yake mwenyewe katika
vitu vilivyoumbwa (taz. Rum 1:19-20). Tena, alipotaka kuifungua njia ya
wokovu wa kimungu, tangu mwanzo alijidhihirisha kwa wazazi wetu wa awali.
Baada ya kuanguka kwao, aliwainua tena katika tumaini la wokovu kwa ahadi ya
ukombozi (taz. Mwa 3:15), naye alikuwa na utunzo wa daima kwa jamii ya
wanadamu, ili awapatie uzima wa milele wale wote ambao wanautafuta wokovu
kwa saburi katika kutenda mema (taz. Rum 2:6-7). Kwa wakati wake alimwita
Ibrahimu, ili kumfanya yeye kuwa taifa kubwa (taz. Mwa 12:2-3), ambalo baada
ya Mababu, alilifundisha kwa njia ya Musa na Manabii, ili wamtambue Mungu
kuwa ndiye Mungu peke yake, mwenye uhai na ukweli, Baba mwenye kuwatunza na
hakimu mwenye haki. Tena aliwafundisha kumngojea Mwokozi aliyeahidiwa. Kwa
jinsi hii Mungu aliiandaa njia ya Injili katika mwenendo wa karne.
Kristo anakamilisha ufunuo
4. Mungu, baada ya kusema zamani katika Manabii mara nyingi na kwa njia
nyingi, “mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana” (Ebr 1:1-2).
Maana alimtuma Mwanawe, yaani Neno wa milele, anayewaangazia watu wote, ili
akae kati ya wanadamu na kuwafunulia siri za Mungu (taz. Yn 1:1-18). Kwa
hiyo Yesu Kristo, Neno aliyefanyika mwili, aliyetumwa kwetu kama “mwanadamu
kwa wanadamu”[3], “huyanena
maneno ya Mungu” (Yn 3:34) na kutimiza kazi ya wokovu ambayo Baba alimpa ili
aitende (taz. Yn 5:36; 17:4). Kwa hiyo Yeye mwenyewe, ambaye tumwonapo
twamwona Baba (taz. Yn 14:9), alitimiza na kukamilisha ufunuo na
kuuthibitisha kwa ushuhuda wa kimungu. Hayo aliyafanya kwa uwepo wake
kamili, kwa kujidhihirisha mwenyewe, kwa maneno na matendo, kwa ishara na
miujiza na hasa kwa kifo na ufufuko wake mtukufu kutoka katika wafu, na
hatimaye kwa kumtuma Roho wa kweli. Alitufunulia kwamba Mungu yupo pamoja
nasi ili atukomboe kutoka katika giza la dhambi na mauti na kutufufua kwa
uzima wa milele.
Kwa hiyo azimio la kikristo, kwa sababu ni Agano Jipya na la mwisho,
halitapita kamwe. Na hakuna ufunuo mwingine mpya wa hadharani unaongojewa
kabla ya ujio mtukufu wa mwisho wa Bwana wetu Yesu Kristo (taz. 1Tim 6:l4 na
Tit 2:13).
Ufunuo upokelewe kwa imani
5. Utii wa imani lazima apewe Mungu anayejifunua (Rum 16:26; taz.
Rum 1:5; 2Kor 10:5-6). Kwa imani mwanadamu hujikabidhi kikamilifu na kwa
uhuru mikononi mwa Mungu, akitoa kwa Mungu mwenye kufunua “heshima kuu ya
akili na utashi”[4], na akikubali
kwa hiari ufunuo anaopewa na Yeye. Ili imani hii iweze kutekelezwa, mtu hana
budi kutanguliwa na kusaidiwa na neema ya Mungu. Kadhalika hana budi kuwa na
msaada wa ndani wa Roho Mtakatifu anayesukuma moyo na kumwelekeza kwa Mungu,
na anayefunua macho ya akili na anayewapa “watu wote utamu katika kuukubali
na kuuamini ukweli”[5]. Roho
Mtakatifu huyohuyo hukamilisha imani daima kwa njia ya mapaji yake ili
ufunuo ueleweke kwa undani zaidi.
Kweli zilizofunuliwa
6. Kwa njia ya ufunuo wa kimungu, Mungu alitaka kujifunua na kujishirikisha
nasi na pia kutufunulia na kutushirikisha maazimio ya mapenzi yake ya milele
kuhusu wokovu wa wanadamu, “yaani kushirikisha fadhili za kimungu, ambazo
zinapita kabisa ufahamu wa akili za kibinadamu”[6].
Mtaguso Mkuu hukiri kwamba “Mungu, asili na utimilifu wa vitu vyote,
anaweza kufahamika kwa hakika kwa mwanga wa kawaida wa akili ya kibinadamu
kwa njia ya ulimwengu ulioumbwa (taz. Rum 1:20); tena [Mtaguso Mkuu]
hufundisha ya kuwa ni kwa sababu ya ufunuo wake Mungu kwamba “mambo yale ya
kimungu ambayo kwa yenyewe hayavuki upeo wa akili ya kibinadamu, yanaweza
pia katika hali ya siku hizi ya wanadamu, kufahamika kwa wote upesi, kwa
hakika thabiti na bila mchanganyiko wa kosa”[7].
Sura ya Pili
URITHISHAJI WA UFUNUO WA KIMUNGU
Mitume na waandamizi wao ni watangazaji wa Habari Njema
7. Kwa wema wake mkuu, Mungu alipanga kwamba yale aliyoyafunua kwa ajili ya
wokovu wa mataifa yote yadumu daima kama yalivyo na yarithishwe kwa vizazi
vyote. Kwa hiyo Kristo Bwana, ambaye ndani yake ufunuo wote wa Mungu
Mwenyezi unatimilika (taz. 2Kor 1:30 na 3:16-4:6), aliwaamuru Mitume
kuwahubiria wote Injili ambayo iliisha ahidiwa kwa njia ya Manabii, na
ambayo aliitimiliza mwenyewe na kuitangaza kwa kinywa chake
[8]. Kwa njia hii waliwashirikisha watu wote vipaji vya kimungu. Injili
hii iliwekwa kama chemchemi ya kila ukweli uletao wokovu na ya kila nidhamu
yenye maadili. Tendo hilo lilitimizwa kiaminifu na Mitume, ambao kwa
kuhubiri kwa maneno, kwa mifano na kwa kuunda jumuiya mbalimbali
waliwajulisha watu wote yale waliyopokea kutoka katika kinywa cha Kristo,
kwa kuishi pamoja naye na kwa matendo yake; na pia yale waliyojifunza kwa
uvuvio wa Roho Mtakatifu. Tena, tendo hilo lilitimizwa pia na wale, Mitume
na wengine walioishi nao, ambao, kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu mwenyewe,
waliandika ujumbe wa wokovu[9].
Mitume waliweka Maaskofu kuwa waandamizi wao ili Injili ihifadhiwe daima
ikiwa nzima na yenye uhai katika Kanisa, “wakiwakabidhi nafasi zao wenyewe
za mamlaka-fundishi (magisterii)”[10].
Hivyo basi, Mapokeo hayo Matakatifu pamoja na Maandiko Matakatifu ya Maagano
yote mawili ni kama kioo ambacho, kwa njia yake, Kanisa linalohiji hapa
duniani humtazama Mungu, ambaye kutoka kwake hupewa yote mpaka litakapomwona
uso kwa uso kama alivyo (taz. 1Yoh 3:2).
Mapokeo Matakatifu
8. Kwa hiyo, mahubiri ya kitume, yanapatikana kwa namna ya pekee katika Vitabu
Vitakatifu, ilikuwa lazima yaendelee kuhifadhiwa kwa mfululizo wa kupokezana
mpaka mwisho wa nyakati. Hivyo basi, Mitume, wanapowarithisha wengine yale
waliyopokea, wanawasihi waamini wahifadhi mapokeo waliyopewa ama kwa maneno
au kwa maandishi (taz. 2The 2:15). Na pia waliwasihi wapiganie imani
waliyopewa mara moja tu na kwa daima (taz. Yda 3)[11].
Yale ambayo Mitume waliyarithisha, ndani yake yamo yote yenye kulifanya
Taifa la Mungu kuishi katika utakatifu na kukuza imani yake. Hivyo Kanisa,
katika mafundisho yake na katika maisha na ibada zake, linaendeleza daima na
kuvirithisha vizazi vyote ukweli juu yake, na pia juu ya yale anayoyaamini.
Mapokeo hayo yanayotoka kwa Mitume hukua katika Kanisa kwa msaada wa Roho
Mtakatifu[12]: unakua, kwa
kweli, utambuzi wa mambo na pia wa maneno yanayorithishwa. Nao, unakua kwa
tafakuri na kusoma kwa moyo kwa waamini, ambao wanayaweka na kuyafikiri
mioyoni mwao (Lk 2:19 na 51). Na pia unakua kwa njia ya ujuzi wa ndani wa
mambo ya kiroho wanaoung’amua; na kwa mahubiri ya wale waliopewa fadhili
halisi ya ukweli kwa njia ya uandamizi wa kiaskofu. Yaani Kanisa, katika
mfululizo wa karne, linaelekea kwenye utimilifu wa ukweli wa kimungu hadi
maneno ya Mungu yatakapotimia ndani yake.
Mafundisho ya Mababa watakatifu yanathibitisha uwepo hai wa Mapokeo hayo.
Hazina ya Mapokeo hayo inamiminwa ndani ya matendo na maisha ya Kanisa
linaloamini na kusali. Mapokeo yenyewe yanalijulisha Kanisa kanoni, au
orodha, nzima ya Vitabu Vitakatifu (integer Sacrorum Librorum canon),
na kuwezesha kuvielewa kwa undani zaidi. Na pia yanasaidia Maandiko
Matakatifu ili yaendelee kutenda kazi daima; hivyo Mungu, aliyeongea zamani,
hakomi kuongea na Bibiarusi wa Mwanae mpendwa. Na Roho Mtakatifu, ambaye kwa
njia yake sauti hai ya Injili husikika katika Kanisa, na kwa njia ya Kanisa
katika ulimwengu, anawaingiza waamini katika ukweli wote na kufanya Neno la
Kristo likae kwa wingi ndani yao (taz. Kol 3:16).
Uhusiano hai baina ya Mapokeo na Maandiko
9. Kwa hiyo Mapokeo Matakatifu na Maandiko Matakatifu yameshikamana pamoja
na kushirikiana. Kwa sababu yote mawili yanabubujika kutoka katika chemchemi
ileile ya kimungu na hivyo huungana na kuwa kitu kimoja na kuelekea lengo
moja. Kwa kweli, Maandiko Matakatifu ndilo Neno la Mungu ambalo liliandikwa
kwa uvuvio wa Roho wa Mungu. Neno la Mungu lililokabidhiwa kwa Mitume na
Kristo Bwana na Roho Mtakatifu linarithishwa li zima na Mapokeo Matakatifu
kwa waandamizi wao, ili, wakiangazwa na Roho wa kweli, kwa njia ya kuhubiri
kwao, walihifadhi kiaminifu, walifafanue na kulieneza. Hivyo Kanisa
halichoti uhakika wake juu ya mambo yote yaliyofunuliwa kutokana na Maandiko
Matakatifu peke yake. Kwa hiyo Maandiko Matakatifu na Mapokeo Matakatifu
lazima yapokelewe na kuheshimiwa kwa hisia sawa, za uchaji na heshima[13].
Uhusiano kati ya Mapokeo, Maandiko Matakatifu, Kanisa lote na Uongozi
wake
10. Mapokeo Matakatifu na Maandiko Matakatifu yanaunda hazina moja takatifu
ya Neno la Mungu iliyokabidhiwa kwa Kanisa. Taifa lote takatifu pamoja na
Wachungaji wake likishikamana na hazina hiyo, linadumu daima aminifu katika
Mafundisho ya Mitume na katika ushirika, katika kumega mkate na katika
kusali (taz. Mdo 2:42), ili, katika kuitunza, kuiishi na kuikiri imani
iliyorithishwa, uwepo umoja wa pekee wa kiroho kati ya Maaskofu na waamini[14].
Jukumu (Munus) la kutoa ufafanuzi halisi wa Neno la Mungu
lililoandikwa au kupokewa[15]
umekabidhiwa tu kwa Majisterio hai ya Kanisa[16],
ambayo mamlaka yake inatekelezwa kwa jina la Yesu Kristo. Lakini Majisterio
hiyo ya kufundisha haiko juu ya Neno la Mungu, bali [Majisterio] ni mtumishi
wa Neno hilo, na hufundisha yale tu iliyorithi. Kwani, kwa amri ya Mungu na
kwa msaada wa Roho Mtakatifu, hulisikiliza Neno kwa uchaji, hulihifadhi
kitakatifu na kulielezea kiaminifu, na huchota katika hazina hii moja ya
imani yale yote inayoyatangaza ili yaaminiwe kwa kuwa yalifunuliwa na Mungu.
Ni dhahiri kwamba Mapokeo Matakatifu, Maandiko Matakatifu na Majisterio ya
Kanisa, kwa maamuzi yenye hekima sana ya Mungu, yameshikamana na kuunganika
pamoja kiasi kwamba moja haliwezi kusimama peke yake bila mengine. Bali,
yote kwa pamoja, na kila moja kwa namna yake, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu
aliye mmoja, hutoa mchango wake kwa wokovu wa watu.
Sura ya Tatu
UVUVIO WA KIMUNGU NA UFAFANUZI WA MAANDIKO MATAKATIFU
Uvuvio na ukweli katika Maandiko Matakatifu (Biblia)
11. Kweli zilizofunuliwa na Mungu zilizomo na zinazoelezwa katika matini ya
Maandiko Matakatifu, zimeandikwa chini ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. Mama
Kanisa mtakatifu, akitegemea imani ya [nyakati za] Mitume, anavipokea rasmi
kama vitakatifu vitabu vyote vizima vya Agano la Kale na Jipya, tena katika
sehemu zao zote, kwa misingi hii kwamba, kwa vile viliandikwa kwa uvuvio wa
Roho Mtakatifu (taz. Yn 20:31; 2Tim 3:16; 2Pet 1:19-21; 3:15-16), Mungu
mwenyewe ndiye mtunzi wake; na katika hali hiyo vimekabidhiwa kwa Kanisa
lenyewe[17]. Kwa kutunga Vitabu
Vitakatifu, Mungu aliwachagua watu fulani aliowatumia, katika vipaji na
nguvu zao[18], ili, akifanya
kazi ndani yao na kwa njia yao[19]
kama watunzi wa kweli waandike kila kitu alichotaka kiandikwe bila kitu cha
ziada[20].
Kwa vile yale yote ambayo watunzi waliovuviwa au waandishi watakatifu (hagiographi)
wanayasema, inabidi yapokelewe kama yanasemwa na Roho Mtakatifu, lazima
kukiri kwamba vitabu vya Maandiko Matakatifu vinafundisha kwa nguvu, kwa
uaminifu thabiti na bila hitilafu ukweli ambao Mungu alitaka ukabidhiwe kwa
Maandiko Matakatifu kwa ajili ya wokovu wetu[21].
Kwa hiyo “kila Andiko lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa
kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika
haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo
jema” (2Tim 3:16-17).
Mwongozo kuhusu ufafanuzi wa Biblia
12. Maadam Mungu katika Maandiko Matakatifu ameongea kwa njia ya wanadamu
na kwa mtindo wa kibinadamu[22],
mfafanuzi wa Maandiko Matakatifu, ili afahamu vizuri yale Mungu aliyotaka
kutushirikisha, lazima atafute kwa makini yale ambayo waandishi watakatifu
walitaka kumaanisha na yale ambayo Mungu alitaka kutufunulia kwa njia ya
maneno yao.
Ili kuelewa nia ya waandishi watakatifu lazima tujali pia, kati ya mengine,
mitindo ya fasihi yao (genera litteraria).
Maana ukweli unaelezwa na kuonyeshwa kwa namna tofauti katika matini za
kihistoria, za kinabii au za kishairi au za mitindo mingine ya kifasihi. Kwa
hiyo ni lazima mfafanuzi atafute maana ile iliyoandikwa, aliyotaka kueleza
mwandishi mtakatifu katika nafasi fulani, kadiri ya hali ya wakati na
utamaduni wake, kwa njia ya mitindo ya fasihi iliyotumika wakati ule[23].
Maana, ili kuelewa kwa hakika alichotaka kusema mwandishi mtakatifu katika
maandishi, lazima kujali sana jinsi alivyoguswa na mambo mbalimbali,
alivyojieleza na kusimulia kadiri ya utamaduni na nyakati za mwandishi
mtakatifu, na pia kadiri ya mitindo iliyokuwa imeenea kati ya jamii
mbalimbali[24].
Lakini, Maandiko Matakatifu lazima yasomwe na kufunuliwa kwa msaada wa Roho
Mtakatifu mwenyewe ambaye kwa njia yake yaliandikwa[25].
Kwa sababu hiyo, ili kupata kwa hakika maana ya matini takatifu, hatuna budi
kujali sana na kwa makini yale yaliyomo katika Maandiko Matakatifu yote na
umoja wake, pamoja na kutilia maanani Mapokeo hai ya Kanisa lote na
ulinganifu wa imani (analogiae fidei). Ni wajibu wa wafafanuzi
kusaidia, kadiri ya mwongozo huu, kuelewa na kufasiri kwa undani zaidi maana
ya Maandiko Matakatifu ili, kwa chunguzi zilizo za namna ya matayarisho,
uamuzi wa Kanisa uthibitike. Kwa kweli hayo yote yanayohusu jinsi ya
kufasiri Maandiko Matakatifu yapo chini ya uamuzi wa Kanisa, ambaye hutimiza
amri ya Mungu na huduma yake ya kuhifadhi na kulifafanua Neno la Mungu[26].
Kushirikishwa kwa wanadamu Hekima ya Mungu
13. Katika Maandiko Matakatifu, ukweli na utakatifu wa Mungu ukiwa imara
daima, hisani (condescensio) ya ajabu ya Hekima ya milele
inadhihirishwa, “ili tufahamu ukarimu usioelezeka wa Mungu na pia jinsi Yeye,
ambaye yupo tayari daima kuyashughulikia maumbile yetu, alivyojishusha
katika maneno yetu”[27]. Maana,
maneno ya Mungu yaliyotamkwa kwa lugha za kibinadamu yameingia katika maneno
ya wanadamu, kama vile Neno wa Baba wa Milele alivyojifanya mtu, akichukua
udhaifu wa maumbile ya kibinadamu.
Sura ya Nne
AGANO LA KALE
Historia ya wokovu yahifadhiwa katika vitabu vya Agano la Kale
14. Mungu, katika upendo wake mkuu, akiazimu na kutayarisha kwa makini
wokovu wa watu wote, alijichagulia kwa mpango wa pekee Taifa, ili alikabidhi
ahadi zake. Maana, baada ya kufunga Agano na Ibrahimu (taz. Mwa 15:18), pia
na Taifa la Israeli kwa njia ya Musa (taz. Kut 24:8), alijifunua kwa maneno
na matendo kwa taifa alilojipatia, kama Mungu mmoja wa kweli na hai, ili
[Taifa la] Israeli ling’amue njia za Mungu kati ya wanadamu; pia Mungu
mwenyewe alinena kwa vinywa vya Manabii ili Israeli azielewe kwa undani na
kwa wazi zaidi, tena azijulishe kwa upana zaidi kwa Mataifa yote (taz. Zab
22:27-28; 96:1-3; Isa 2:1-4; Yer 3:17). Mpango wa wokovu uliotabiriwa,
ukasimuliwa na kuelezwa na watunzi watakatifu, unajitokeza (exstat)
kama Neno la kweli la Mungu katika vitabu vya Agano la Kale. Ndiyo sababu
vitabu hivyo vilivyoandikwa kwa uvuvio wa kimungu vinahifadhi thamani ya
daima: “Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha
sisi; ili kwa saburi na faraja ya Maandiko tupate kuwa na tumaini” (Rum
15:4).
Ulazima wa Agano la Kale kwa Wakristo
15. Mpango wa Agano la Kale ulikusudia hasa kutayarisha, kutangaza
kiutabiri (taz. Lk 24:44; Yn 5:39; 1Pet 1:10) na kuashiria kwa jinsi za
mifano (taz. 1Kor 10:11) ujio wa Kristo Mkombozi wa ulimwengu na ujio wa
Ufalme wa kimasiya. Aidha, vitabu vya Agano la Kale, kadiri ya hali ya jamii
ya wanadamu kabla ya nyakati za wokovu ulioletwa na Kristo,
vinawadhihirishia watu wote ujuzi juu ya Mungu na juu ya binadamu na pia
jinsi Mungu mwenye haki na huruma anavyojihusisha na watu. Vitabu hivyo,
ingawa vina ndani yake mambo ambayo hayajakamilishwa na ya muda, ni dhahiri
kwamba vinaonyesha mafundisho (paedagogia) halisi ya kimungu[28].
Kwa hiyo waamini ni lazima wapokee kwa heshima vitabu hivyo ambavyo
vinaonyesha jinsi ya kumcha Mungu, mafundisho makuu juu ya Mungu, hekima
iletayo wokovu kwa maisha ya binadamu, na pia hazina za ajabu za sala. Ndani
ya vitabu hivyo limefichika fumbo la wokovu wetu.
Umoja wa Maagano yote mawili
16. Mungu, mvuviaji na mtunzi wa vitabu vya Maagano yote mawili, alipanga
kwa hekima ili Agano Jipya lifichike ndani ya Agano la Kale na Agano la Kale
lifunuliwe katika Agano Jipya[29].
Kwa sababu hiyo, hata kama Kristo alifanya Agano Jipya katika damu yake
(taz. Lk 22:20; 1Kor 11:25), vitabu vyote vya Agano la Kale, vikichukuliwa
katika hali yao nzima[30]
katika ujumbe wa Injili, vinapata na kuonyesha maana yao timilifu katika
Agano Jipya (taz. Mt 5:17; Lk 24:27; Rum 16:25-26; 2Kor 3:14-16), navyo
[vitabu vya Agano la Kale] pia, kwa upande wao, vinaliangaza na kulieleza
Agano Jipya.
Sura ya Tano
AGANO JIPYA
Ubora wa Agano Jipya
17. Neno la Mungu, ambalo ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye
(taz. Rum 1:16), linajidhihirisha na kuonyesha nguvu yake kikamilifu katika
Maandiko ya Agano Jipya. Hata ulipowadia utimilifu wa wakati (taz. Gal 4:4),
Neno alifanyika mwili akakaa kwetu akiwa amejaa neema na kweli (taz. Yn
1:14). Kristo alileta Ufalme wa Mungu hapa duniani, akamfunua Baba yake na
pia akajifunua mwenyewe kwa matendo na maneno. Pia alikamilisha kazi yake
kwa kifo, ufufuko na kupaa kwake kwa utukufu mbinguni na kumpeleka Roho
Mtakatifu. Akiinuliwa juu ya nchi anawavuta wote kwake (taz. Yn 12:32), Yeye
tu aliye na maneno ya uzima wa milele (taz. Yn 6:68). Fumbo hili
havikujulishwa vizazi vingine kama walivyofunuliwa Mitume wake watakatifu na
Manabii zamani hizi katika Roho Mtakatifu (taz. Efe 3:4-6), ili waihubiri
Injili na kuchochea imani katika Yesu Kristo na Bwana na kulikusanya Kanisa.
Maandishi ya Agano Jipya ni ushuhuda wa daima na wa kimungu wa mambo hayo
yote.
Asili ya kitume ya Injili
18. Wote wanafahamu kwamba kati ya Maandiko yote, pia ya Agano Jipya,
Injili kwa haki zina ubora wa pekee kwa sababu ni ushuhuda mahsusi wa maisha
na mafundisho ya Neno aliyefanyika mwili, Mwokozi wetu.
Kanisa daima na popote huamini na kukiri kwamba Injili zote nne zina asili
yao kutoka kwa Mitume. Yale ambayo Mitume walihubiri kwa kuagizwa na Kristo,
baadaye, kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu (Divino afflante Spiritu), wao
wenyewe na wengine walioishi nao walitupatia sisi, kama msingi wa imani,
[ujumbe uleule waliouhubiri,] katika maandishi. Huo ndiyo Injili
inayosimuliwa kwa namna nne kadiri ya Mathayo, Marko, Luka na Yohane[31].
Tabia ya kihistoria ya Injili
19. Mama Kanisa mtakatifu, kwa nguvu na daima amesadiki na hukiri kwamba
Injili nne zilizotajwa hapo juu, ambazo anaamini bila kusita kwamba ni za
kweli, zinasimulia kiaminifu yale ambayo Yesu Mwana wa Mungu aliyatenda
kwelikweli na kufundisha kwa ajili ya wokovu wa milele, wakati alipoishi
kati ya wanadamu hadi siku ile alipopaa mbinguni (taz. Mdo 1:1-2). Mitume,
baada ya Bwana kupaa mbinguni, waliwatangazia watu yale aliyokuwa ameyasema
na kuyatenda, kwa ujuzi kamili waliojaliwa[32]
baada ya kufundishwa na matukio matukufu ya Kristo na kuangazwa na mwanga wa
Roho wa ukweli[33]. Hatimaye
watunzi watakatifu waliandika Injili nne wakichagua mengine kati ya mengi
yaliyokuwa yamesimuliwa kwa maneno au kwa maandishi, wakifupisha mambo
mengine, au kuyafafanua wakilenga hasa hali ya Makanisa. Tena waliandika
wakilinda mtindo uleule wa kuhubiri, lakini daima wakisimulia mambo ya kweli
na kwa uaminifu kuhusu Yesu[34].
Wao wenyewe, wakichota kutoka katika kumbukumbu yao na pia ushuhuda wa wale
ambao “tangu mwanzo walikuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile
neno”, waliandika kusudi watujulishe “ukweli” (taz. Lk 1:2-4) wa mambo
tuliyoelezewa.
Maandishi mengine ya Agano Jipya
20. Kanoni ya Agano Jipya, zaidi ya Injili nne, ina pia nyaraka za Mtume
Paulo na maandiko mengine ya Mitume yaliyotungwa kwa uvuvio wa Roho
Mtakatifu. Kwa njia ya Maandiko hayo, kwa azimio lenye hekima la Mungu, yale
yote yamhusuyo Kristo Bwana yanathibitishwa, mafundisho yake halisi
yanaelezwa kinaganaga zaidi, na uweza uletao wokovu wa kazi ya kimungu ya
Kristo unahubiriwa. Tena, maisha ya kwanza ya Kanisa na kuenea kwake kwa
ajabu vinasimuliwa, na utimilifu wake mtukufu unatabiriwa.
Maana, Bwana Yesu alitenda kazi pamoja na Mitume wake kama alivyoahidi
(taz. Mt 28:20) na akawapelekea Roho Mtakatifu Msaidizi, mwenye kuwaongoza
na kuwaingiza kwenye kweli yote (taz. Yn 16:13).
Sura ya Sita
MAANDIKO MATAKATIFU KATIKA MAISHA YA KANISA
Kanisa huheshimu Maandiko Matakatifu
21. Kanisa limeheshimu daima Maandiko Matakatifu kama lilivyoheshimu Mwili
wa Bwana, wala halikukosa kamwe, hasa katika Liturujia takatifu, kujilisha
mkate wa uzima na kuwapa waamini kutoka katika meza moja ya Neno la Mungu na
pia ya Mwili wa Kristo. Kanisa limeyaamini daima na linaendelea kuyaamini
Maandiko Matakatifu, pamoja na Mapokeo Matakatifu, kuwa ndiyo kanuni kuu
kuliko zote ya maisha yake ya imani; kwa kweli Maandiko hayo, yaliyovuviwa
na Mungu na kutungwa mara moja kwa daima, yanatushirikisha bila hitilafu
yoyote Neno la Mungu mwenyewe; tena yanatusikiza sauti ya Roho Mtakatifu
katika maneno ya Manabii na Mitume. Kwa hiyo mahubiri yote ya Kanisa, kama
vile na dini yenyewe ya kikristo, lazima yalishwe na kuongozwa na Maandiko
Matakatifu. Maana katika Vitabu Vitakatifu Baba aliye mbinguni anawajia
watoto wake kwa upendo mkubwa na anaongea nao. Katika Neno la Mungu umo
uweza na nguvu nyingi, kiasi kwamba Neno hilo huwa ni egemeo na nguvu kwa
Kanisa na pia uthabiti wa imani, chakula cha roho na chemchemi safi na ya
daima ya maisha ya kiroho kwa watoto wa Kanisa. Kwa hiyo, haya yaliyoandikwa
ya kwamba “Neno la Mungu ni hai, tena lina nguvu” (Ebr 4:12), “laweza
kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa” (Mdo 20:32; taz.
1The 2:13), haya basi huyahusu kabisa Maandiko Matakatifu.
Tafsiri za Biblia lazima ziwe sahihi na aminifu
22. Ni lazima waamini wafunguliwe kwa wingi Maandiko Matakatifu. Kwa sababu
hiyo Kanisa la awali lilipokea kama mali yake tafsiri ya zamani ya kigriki
ya Agano la Kale iitwayo ya LXX [Septuajinta au “Watu Sabini”]; pia
liliheshimu daima tafsiri nyingine za Mashariki na za Kilatini, hasa ile
iitwayo Vulgata. Kwa vile Neno la Mungu lazima lipatikane kwa watu wote wa
nyakati zote, basi Kanisa, kwa upendo wa kimama, linafanya kila jitihada ili
zitayarishwe tafsiri zifaazo na zenye kuaminika katika lugha mbalimbali hasa
kutoka lugha za asili za Vitabu Vitakatifu. Kama itaonekana kuwa inafaa
kutayarisha tafsiri hizo pamoja na wakristo waliojitenga, kwa kibali cha
mamlaka ya Kanisa, basi tafsiri hizo zinaweza kutumiwa na wakristo wote.
Wajibu wa kitume wa wataalamu
23. Bibiarusi wa Neno aliyefanyika mwili, yaani Kanisa, akifundishwa na
Roho Mtakatifu, hujibidisha kufikia zaidi na zaidi ujuzi wa ndani wa
Maandiko Matakatifu ili kuwalisha watoto wake kila wakati kwa maneno ya
kimungu. Kwa hiyo, kwa haki anahimiza kuwajua zaidi Mababa Watakatifu wa
Mashariki na wa Magharibi na aina mbalimbali za Liturujia takatifu. Ni
lazima wafafanuzi Wakatoliki na pia wanateolojia wengine washirikiane kwa
bidii na kujitahidi kusoma na kufasiri Maandiko Matakatifu kwa namna ifaayo
chini ya uangalizi wa Majisterio takatifu. Kwa njia hii wahudumu wengi zaidi
wa Neno la Mungu waweze kwa mafanikio zaidi kulipatia Taifa la Mungu chakula
chake, yaani Maandiko yaangazayo akili, yanayoimarisha utashi na kuwasha
mioyo ya wanadamu ili wampende Mungu[35].
Mtaguso Mkuu unawahimiza wana wa Kanisa wapenzi wa taaluma za kibiblia, ili
wadumu katika kutimiza kwa nguvu mpya na kwa juhudi kubwa kazi ile
waliyoianza vizuri kadiri ya lengo la Kanisa[36].
Ulazima wa Maandiko Matakatifu kwa Teolojia
24. Teolojia Takatifu hutegemea, kama msingi wake wa daima, Neno la Mungu
lililoandikwa, pamoja na Mapokeo Matakatifu. Na juu ya msingi huo wa Neno,
inapata kuimarishwa kwa nguvu na kufanywa upya zaidi ikitazama katika mwanga
wa imani kila kweli iliyomo katika fumbo la Kristo. Maandiko Matakatifu yote
yana Neno la Mungu ndani yake, na kwa vile yaliandikwa kwa uvuvio wa Roho
Mtakatifu, ni Neno la Mungu kweli kweli. Kwa hiyo, kujifunza Maandiko
Matakatifu kitakuwa ndicho kiini na roho ya Teolojia Takatifu[37].
Pia huduma ya Neno inajilisha kwa manufaa na kupania utakatifu kutoka kwa
Neno la Maandiko. Huduma hiyo ni: mahubiri ya kichungaji, katekesi na
mafundisho yote ya kikristo, na ndani yake homilia katika Liturujia lazima
ipewe nafasi ya pekee.
Kusoma Biblia kunahimizwa
25. Kwa hiyo makleri wote, hasa mapadre wa Kristo, mashemasi au makatekista
wanaoshiriki kwa rasmi huduma ya Neno, lazima wajizamishe katika Maandiko
Matakatifu kwa kuyasoma bila kuchoka na kwa makini, ili kati yao asiwepo
“mhubiri mtupu wa Neno la Mungu na wa nje tu, asiyezingatia Neno hilo moyoni
mwake”[38], yeye ambaye inabidi
awashirikishe waamini waliokabidhiwa kwake hazina tele ya Neno la Mungu,
hasa katika Liturujia takatifu. Vilevile Mtaguso Mkuu unawasihi kwa nguvu na
kwa bidii sana waamini wote, hasa watawa, wajifunze “uzuri usio na kiasi wa
kumjua Kristo Yesu” (Flp 3:8) kwa kusoma mara kwa mara Maandiko Matakatifu.
Maana “kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo”[39].
Kwa hiyo wakaribie kwa furaha na upendo Kitabu kitakatifu chenyewe [cha
Biblia] kwa njia ya Liturujia takatifu yenye utajiri wa Maneno ya Mungu; pia
wakikaribie kwa kukisoma kwa uchaji na kwa njia ya mazoezi yafaayo kwa lengo
hilo na kwa njia ya misaada mingine, ambayo, kwa kibali na kwa uangalizi wa
Wachungaji wa Kanisa, inaenea pote katika siku zetu kwa namna ya kusifika.
Lakini waamini wakumbuke kwamba kusoma Maandiko Matakatifu lazima kuwe
katika mazingira ya sala, ili Mungu na binadamu waweze kuongea pamoja; kwa
sababu “tunaongea naye tunaposali na tunamsikiliza tunaposoma Maneno
Matakatifu”[40].
Ni juu ya Maaskofu, “walio warithi wa mafundisho ya kitume”[41],
kuwafundisha waamini waliokabidhiwa kwao matumizi sahihi ya Vitabu
Vitakatifu, hasa Agano Jipya ambalo ndani yake Injili inashika nafasi ya
kwanza. Watafanya hilo kwa kuwapa waamini tafsiri za Maandiko Matakatifu
zenye maelezo ya lazima na ya kutosha, ili wana wa Kanisa waweze kuzoea
kushinda na Maandiko Matakatifu kwa hakika na kwa manufaa na pia ili
wakolezwe na roho zake.
Kisha, yatayarishwe matoleo ya Maandiko Matakatifu yenye maelezo ya kufaa
kwa matumizi pia ya wale wasio wakristo yalinganayo na hali yao. Lakini
Wachungaji wa kiroho na pia Wakristo wote waangalie ili matoleo hayo
yaenezwe kwa busara.
Hitimisho
26. Kwa njia hii, kwa kusoma na kujifunza Vitabu Vitakatifu “Neno la Bwana
liendelee na kutukuzwa” (2The 3:1), na hazina ya ufunuo iliyokabidhiwa kwa
Kanisa ijaze zaidi na zaidi mioyo ya waamini. Kama vile kushiriki mara
nyingi fumbo la Ekaristi kunavyokuza maisha ya Kanisa, vivyo hivyo tunaweza
kutumaini mwamko mpya wa maisha ya kiroho kutokana na kuheshimu zaidi Neno
la Mungu “linalodumu milele” (Isa 40:8; taz. 1Pet 1:23-25).
Mambo yote yaliyoamuliwa katika konstitusio hii, na kila moja kati yao,
yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume
tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho
Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote
yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa utukufu wa
Mungu.
Roma, katika Kanisa la Mtakatifu Petro, 18 Novemba 1965
Mimi mwenyewe Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki
(zinafuata sahihi za Mababa)
[1] Taz. Mt. Augustinus, De
Catechizandis Rudibus 4,8: PL 40, 316.
[2] Taz. Mt 11:27; Yn 1:14 na 17;
14:6; 17:1-3; 2Kor 3:16 na 4:6; Efe 1:3-14.
[3] Epist. ad Diognetum
7,4: Funk, Patres Apostolici, I, uk. 403.
[4] Conc. Vat. I, Const. Dogm. de
fide catholica Dei Filius, cap.3: Denz. 1789 (3008).
[5] Conc. Araus. II, can. 7:
Denz. 180 (377); Conc. Vat. I, l.c. :Denz. 1791 (3010).
[6] Conc. Vat. I, Const. Dogm. de
fide catholica Dei Filius, cap.2: Denz. 1786 (3005).
[7] Ibid.: Denz. 1785 na 1786
(3004 na 3005).
[8] Taz. Mt 28:19-20 na Mk 16:15.
Conc. Trid., Decr. De Canonicis Scripturis: Denz. 783 (1501).
[9] Taz. Conc. Trid., l.c.; Conc.
Vat. I, Const. Dogm. de fide catholica Dei Filius, cap. 2: Denz. 1787
(3006).
[10] Mt. Ireneus, Adv. Haer.,
III, 3, 1: PG 7, 848; Harvey, 2, uk. 9.
[11] Taz. Conc. Nic. II: Denz.
303 (602). Conc. Const. IV, Sess. X, can. 1: Denz. 336 (650-652).
[12] Taz. Conc. Vat. I, Const.
Dogm. de fide catholica, Dei Filius, cap. 4: Denz. 1800 (3020).
[13] Taz. Conc. Trid., Decr.
De canonicis Scripturis: Denz. 783 (1501).
[14] Taz. Pius XII, Const.
Apost. Munificentissimus Deus, 1 nov. 1950: AAS 42 (1950) uk.
756, collatis verbis Mt. Cypriani, Epist. 66, 8: CSEL 3, 2,
733: “Ecclesia plebs Sacerdoti adunata et Pastori suo grex adhaerens”.
[15] Taz. Conc. Vat. I, Const
Dogm. de fide catholica Dei Filius, cap. 3: Denz. 1792 (3011).
[16] Taz. Pius XII, Litt.
Encycl. Humani Generis, 12 ago. 1950: AAS 42 (1950) uk.
568-569: Denz. 2314 (3886).
[17] Taz. Conc. Vat. I, Const.
Dogm. de fide catholica Dei Filius, cap. 2: Denz. 1787 (3006). Pont.
Comm. Biblica, Decr. 18 juni 1915: Denz. 2180 (3629); EB 420,
S.S.C.S. Officii, Epist. 22 des. 1923: EB 499.
[18] Taz. Pius XII, Litt.
Encycl. Divino afflante Spiritu, 30 sep.1943: AAS 35 (1943)
uk. 314; EB 556.
[19] In et per
hominem: Taz. Ebr 1:1 na 4:7 ( in): 2Sam 23:2; Mt 1:22 na passim ( per);
Conc. Vat. I: Schema de doctr. cath, nota 9: Coll. Lac. VII, 522.
[20] Leo XIII, Litt. Encycl.
Providentissimus Deus, 18 nov. 1893: Denz. 1952 (3293); EB 125.
[21] Taz. Mt. Augustinus, De
Gen. ad litt., 2, 9, 20: PL 34, 270-271; CSEL 28, 1, 46-47 na
Epist.
82, 3: PL 33,277; CSEL 34, 2, 354. – Mt. Thomas, De Ver., q.
12, a. 2, C. – Conc. Trid., Decr. De canonicis Scripturis: Denz. 783
(1501). – Leo XIII, Litt. Encycl. Providentissimus Deus: EB
121, 124, 126-127. – Pius XII, Litt. Encycl. Divino afflante Spiritu:
EB 539.
[22] Taz. Mt. Augustinus, De
Civ. Dei, XVII, 6, 2: PL 41, 573; CSEL 40, 2, 228.
[23] Taz. Mt. Augustinus, De
Doctr. Christ., III, 18, 26: PL 34, 75-76; CSEL 80, 95.
[24] Taz. Pius XII, l.c.: Denz.
2294 (3829-3830); EB 557-562.
[25] Taz. Benedictus XV, Litt.
Encycl. Spiritus Paraclitus, 15 sep. 1920: EB 469. - Mt.
Hieronymus, In Gal. 5, 19-21; PL 26, 417 A.
[26] Taz. Conc. Vat. I, Const.
Dogm. de fide catholica, Dei Filius, cap. 2: Denz. 1788 (3007).
[27] Mt. Ioannes Chrysostomus,
In Gen. 3, 8 (hom. 17, 1): PG 53, 134. “Attemperatio” kigiriki:
sugkatabasij.
[28] Taz. Pius XI, Litt.
Encycl.
Mit brennender Sorge, 14 machi 1937: AAS 29 (1937) uk. 151.
[29] Taz. Mt. Augustinus,
Quaest. in Hept. 2, 73: PL 34, 623.
[30] Taz. Mt. Irenaeus, Adv.
Haer., III, 21, 3: PG 7, 950; (25,1: Harvey, 2, uk. 115). Mt. Cyrillus
Hieros., Catech., 4, 35: PG 33, 497. Theodorus Mops., In Soph.,
1, 4-6: PG 66, 452D-453A.
[31] Taz. Mt. Irenaeus, Adv.
Haer., III, II, 8: PG 7, 885; ed. Sagnard uk.194.
[32] Taz. Yn 2:22; 12:16; na
pia 14:26; 16:12-13; 7:39.
[33] Taz. Yn 14:26; 16:13.
[34] Taz. Instructio Sancta
Mater Ecclesia a Pontificio Consilio Studiis Bibliorum provehendis
edita: AAS 56 (1964) uk. 175.
[35] Taz. Pius XII, Litt.
Encycl. Divino afflante Spiritu, 30 sep. 1943: EB 551, 553,
567. Comm. Biblica, Instructio de S. Scriptura in Clericorum Seminariis
et Religiororum Collegiis recte docenda, 13 mei 1950: AAS 42
(1950) uk. 495-505.
[36] Taz. Pius XII, ibidem:
EB
569.
[37] Taz. Leo XIII, Litt.
Encycl. Providentissimus Deus: EB 114; Benedictus XV, Litt.
Encycl. Spiritus Paraclitus, 15 sep. 1920: EB 483.
[38] Mt. Augustinus, Serm.
179, 1: PL 38, 966.
[39] Mt. Hieronimus, Comm.
in Is., Prol.: PL 24, 17. - Taz. Benedictus XV, Litt. Encycl.
Spiritus Paraclitus: EB 475-480. Pius XII, Litt. Encycl.
Divino afflante Spiritu: EB 544.
[40] Mt. Ambrosius, De
officiis ministrorum, I, 20, 88: PL 16, 50.
[41] Mt. Irenaeus, Adv.
Haer., IV, 32, 1: PG 7, 1071; (= 49, 2) Harvey, 2, uk. 255.
|
|