Index

Back Top Print

[BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

Dikrii juu ya 
vyombo vya upashanaji habari 

PAULO ASKOFU
MTUMISHI WA WATUMISHI WA MUNGU
PAMOJA NA MABABA WA MTAGUSO MKUU
ATAKA HAYA YAKUMBUKWE DAIMA 

  

UTANGULIZI

Maana ya istilahi

1. KATI YA MAMBO YA AJABU (Inter Mirifica) ya kitekniki ambayo akili ya mwanadamu, ikiongozwa na Mungu, imevumbua kutoka kwa vitu vilivyoumbwa, hasa siku hizi, Mama Kanisa anapendezwa na kupokea kwa namna ya pekee hasa yale ambayo yanahusiana moja kwa moja na roho ya mwanadamu, na kufungua njia mpya za kuwasiliana habari, maoni na maelekezo ya aina zote, kwa urahisi zaidi. Baadhi ya njia hizo zinazochukua umuhimu wa kwanza ni zile ambazo kwa hali zao zinaweza kufikia na kuathiri si mtu mmoja mmoja tu, bali watu wengi kwa pamoja na hata jamii nzima ya wanadamu. Njia hizo ni vitabu na magazeti, sinema, redio, televisheni na nyinginezo zinazofanana nazo. Hizi ndizo zinazostahili kuitwa “vyombo vya upashanaji habari”.

Sababu zifanyazo Mtaguso Mkuu uliongelee suala hili

2. Mama Kanisa anajua kwamba vyombo hivi kama vikitumiwa vizuri, vyaweza kuleta faida kwa binadamu. Vinatoa mchango mkubwa katika ukuzaji na ustawishaji wa nafsi za watu na pia katika uenezaji na uimarishaji wa ufalme wa Mungu. Lakini anajua pia kuwa binadamu waweza kuvitumia vyombo hivyo kwa mitindo ambayo ni kinyume na lengo la Mungu Muumbaji, na hivyo kujidhuru wenyewe kwavyo. Kwa kweli [Kanisa] husikitishwa kwa huzuni ya kimama na uharibifu huo, ambao matumizi maovu ya vyombo hivyo huharibu jumuiya ya watu.

Mtaguso huu Mkuu hushiriki uangalifu na juhudi za Mapapa na Maaskofu katika suala hilo la umuhimu mkubwa, na unadhani kuwa ni wajibu wake kujadili matatizo makubwa yaletwayo na vyombo vya upashanaji habari. Pia unaamini kwamba mafundisho na maagizo yaliyomo katika hati hii yatafaa siyo kwa wokovu wa waamini tu, ila pia kwa maendeleo ya jamii nzima ya binadamu.

Sura ya Kwanza

MWONGOZO KWA MATUMIZI MANYOFU YA VYOMBO VYA UPASHANAJI HABARI

Wajibu wa Kanisa

3. Kanisa Katoliki, lililoanzishwa na Kristo Bwana kwa madhumuni ya kuleta wokovu kwa watu wote, linasukumwa na wajibu wa kuihubiri Injili. Kwa jinsi hii Kanisa linasadiki kuwa jukumu lake ni kuhubiri habari njema ya wokovu kwa kutumia pia vyombo vya upashanaji habari, na pia kuwafundisha watu kuvitumia vyombo hivi kwa namna inayofaa.

Ni haki ya msingi ya Kanisa kuvitumia na kuvimiliki vyombo hivyo ambavyo ni muhimu au vya kufaa kwa malezi ya kikristo, na kwa kushughulikia wokovu wa watu. Ni wajibu wa Wachungaji kuwafundisha na kuwaongoza waamini kusudi, kwa msaada pia wa vyombo hivyo, watamani na kuuelekea wokovu wao wenyewe na wa familia nzima ya wanadamu.

Aidha, ni wajibu hasa wa walei kuimarisha vyombo hivyo kwa roho ya kiutu na ya kikristo ili kweli viweze kusaidia matarajio makubwa ya watu, kulingana na mpango wa Mungu.

Kanuni za kimaadili

4. Ili vyombo hivyo vitumiwe kwa usahihi, ni lazima wale wote wanaotumia wajue kanuni za kimaadili na kuzitekeleza kiaminifu katika uwanja huo. Kwanza kabisa wanatakiwa kuyazingatia yale yote yanayoletwa na kila chombo kulingana na tabia yake, wote wanatakiwa kuwa macho juu ya mazingira – yaani lengo, watu, mahali, wakati, n.k. – ya mawasiliano. Mazingira ambayo yaweza kubadilisha, au kupindua kabisa, tunu za kimaadili za mawasiliano yenyewe. Kati yake, izingatiwe hasa jinsi kila chombo kinavyotenda, yaani nguvu zake za kushawishi, ambazo zaweza kuwa kubwa sana, kiasi kwamba watu, hasa kama hawajatayarishwa vya kutosha, wataweza kuzihisia na kuzitawala kwa shida tu, wala wasingeweza kuzipinga itakiwapo.

Haki ya upashanaji habari

5. Ni lazima wote wanaohusika waunde dhamiri nyofu katika matumizi ya vyombo hivyo, hasa kuhusiana na masuala kadhaa yenye ubishani mkubwa siku hizi.

Suala la kwanza lahusu taarifa, yaani utafutaji wa habari na usambazaji wake. Kutokana na maendeleo ya jamii ya kisasa na ongezeko la mahusiano ndani yake, ni wazi kuwa upashanaji wa taarifa umekuwa ni muhimu sana, na kwa sehemu kubwa ni wa lazima. Kama habari na matukio vyapashwa hadharani na upesi, kila mmoja ataweza kupata ufahamu wa kufaa na hivyo kuwezeshwa kutoa mchango kikamilifu kwa manufaa ya wote. Zaidi ya hayo, wote wataweza kuhamasisha kwa urahisi ustawi na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Kwa hiyo jamii ya watu ina haki ya upashanaji habari kwa mada zinazohusu watu, awe mtu mmoja mmoja au kama kundi la watu, kulingana na mazingira. Utekelezaji wa halali wa haki hiyo hudai yale yaliyomo katika upashanaji habari yawe kila mara ya kweli na, kwa kutunza haki na mapendo, makamilifu. Hatimaye, yatakiwa yatangazwe kiaminifu na kwa kufaa. Hii ina maana kwamba katika ukusanyaji na usambazaji wa habari, sheria za kimaadili, na haki halali pamoja na hadhi ya binadamu vyatakiwa kuhifadhiwa. Sio ujuzi wowote unaleta faida, “bali upendo hujenga” (1Kor 8:1).

Sanaa na maadili

6. Suala la pili hutoka katika uhusiano kati ya haki za sanaa – inavyosemeka – na masharti ya maadili. Mabishano ambayo suala hili huzidi kuzusha, mara nyingi mwanzo wake ni kuielewa vibaya elimu ya maadili na elimu ya ujumi (aesthetica). Kwa sababu hiyo, Mtaguso Mkuu unatangaza kwamba watu wote wanapasika kuukubali ubora wa mpango wa kimaadili, ambao pekee hupita na kuratibu mipango mingine yote ya kazi za kibinadamu, pasipo kuacha sanaa, licha ya ubora wake. Ni mpango wa kimaadili tu unaomgusa binadamu katika utu wake wote kama kiumbe wa Mungu, mwenye akili na utashi, ambaye huitwa kushiriki hadhi ya kimungu. Kama mpango wa kimaadili utafuatwa vizuri na kiaminifu, utamwongoza mwanadamu katika ukamilifu na utimilifu wa heri.

Onyesho la ubaya wa kimaadili

7. Hatimaye simulizi, maelezo au viigizo vya ubaya wa kimaadili, kwa njia pia ya vyombo vya upashanaji habari, bila shaka huweza kusaidia kufahamu na kupekua kwa undani zaidi utu wa binadamu, kudhihirisha na kukuza fahari ya ukweli na ya wema, pamoja na kunufaika matokeo mazuri zaidi ya kitamthiliya. Lakini, ili hivyo visilete madhara zaidi kuliko faida kiroho, sheria za maadili zinatakiwa kufuatwa kwa makini hasa wakati vinaposhughulikia masuala yanayodai heshima yake, au masuala ambayo huwasha kwa urahisi zaidi tamaa ovu za binadamu, aliyejeruhiwa na dhambi ya asili.

Maoni ya umma

8. Siku hizi maoni ya umma yanaathiri kwa vikubwa na kwa nguvu maisha ya raia wote, yawe ya kibinafsi, ama ya kijumuiya. Kwa hiyo lazima wahusika wote katika jamii watimize wajibu wao wa haki na mapendo, hata katika uwanja huo. Hivyo, inawapasa kujenga na kueneza maoni ya umma yaliyo manyofu pia kwa njia ya vyombo hivyo.  

Wajibu wa wapokeaji

9. Wajibu wa pekee wanao wapokeaji wote, yaani, wasomaji, watazamaji na wasikilizaji, ambao kwa uchaguzi wao binafsi na wa hiari wanapokea mawasiliano yanayotolewa na vyombo hivyo. Uchaguzi sahihi unawadai wapendelee kwa namna zote yale yaliyo bora kimaadili, kiutamaduni na kisanaa. Vilevile unawadai waepuke chochote ambacho kinakuwa ni sababu au fursa ya madhara ya kiroho, au kinachoweza kuwahatarisha wengine kwa mifano mibaya, au kinachozuia mawasiliano yenye manufaa na kurahisisha yale maovu. Haya huwa yanatokea wakati ambapo mchango wa fedha unatolewa kwa wale ambao wanatumia vyombo hivyo kwa kutaka faida ya binafsi tu.

Kwa hiyo wapokeaji, ili kutimiza sheria za kimaadili, wasipuuze wajibu wa kujipatia upesi iwezekanavyo habari za maamuzi yanayofanywa na kamati inayohusika, na kuyafuata kulingana na miongozo ya dhamiri njema. Wanatakiwa kuchukua hatua zifaazo kuongoza na kuunda dhamiri zao ili kwamba waweze kuzuia kwa urahisi zaidi vishawishi visivyo vinyofu na kuvichochea vile vilivyo vyema.

Wajibu wa vijana na wazazi

10. Wapokeaji, hasa vijana, wajizoeshe kutumia kwa kiasi na kwa nidhamu vyombo hivyo. Wawe na lengo la kuelewa sawasawa kila wakionacho, wakisikiacho, na wakisomacho. Wanatakiwa kujadili pamoja na walezi wao na wataalamu wa masuala haya ili wajifunze kuvitathmini inavyofaa. Wazazi kwa upande wao wanatakiwa kukumbuka kwamba ni wajibu wao kuona kuwa burudani, magazeti, n.k., ambavyo vyaweza kudhuru imani na uadilifu, visiingie nyumbani mwao na watoto wao wasipate kuvikuta wala mahali pengine.

Wajibu wa watunzi

11. Wajibu wa pekee wa kimaadili kwa matumizi mema ya vyombo vya upashanaji habari unawahusu waandishi wa habari na wa vitabu, waigizaji, watunzi, wahariri na watoaji, wasambazaji, wagawaji na wauzaji, wahakiki na wengine wote ambao wanashiriki katika utengenezaji na usambazaji wa habari kwa namna yoyote ile. Ni dhahiri kuwa wahusika hawa wote wanao wajibu mkubwa sana katika ulimwengu wa leo: wao wanao uwezo wa kuielekeza jamii ya wanadamu kwenye mwelekeo unaofaa au hata kuipotosha kwa njia ya ushawishi walio nao pamoja na taarifa wanazozitoa.

Ni wajibu wao pia kuratibisha faida yao binafsi ya kiuchumi, kisiasa na kisanaa kwa namna ambayo haipingani na manufaa ya wote. Ili kufanikisha jambo hili kwa uhakika zaidi, itakuwa vizuri kuunda vyama kulingana na taalumakazi (professione) zao mbalimbali, ambavyo – kwa njia ya kuweka kiapo maalum, kama inatakiwa, cha kushika “kanuni ya kimaadili” – vina uwezo wa kuwawajibisha wahusika wake kuziheshimu sheria za kimaadili katika shughuli na wajibu vya ustadi wao.

Aidha, hawana budi kutambua daima kwamba sehemu kubwa ya wasomaji na watazamaji ni vijana ambao wanahitaji makala zinazochapishwa pamoja na burudani ambavyo vinaleta maburudisho halali na kuongoza pia roho zao kwa makusudio ya juu. Aidha, wahakikishe kuwa utoaji wa vipindi vya dini [kwa njia ya vyombo hivyo] unakabidhiwa kwa watu wanyofu na wenye ujuzi unaotakiwa, na uandaliwe kwa heshima ya kufaa.

Wajibu wa serikali

12. Serikali ina wajibu wa pekee katika uwanja huu kwa manufaa ya wote ambayo vyombo hivyo vipo kwa ajili ya hayo. Ni juu ya serikali yenyewe, kwa wadhifa wake, kulinda, na kuhifadhi, hasa kuhusu uchapishaji uhuru wa kweli na wa haki wa mawasiliano unaodaiwa na jamii ya kisasa kwa ajili ya maendeleo yake. Serikali yatakiwa kukuza thamani za kidini, za kiutamaduni, na za kisanaa. Yatakiwa kuwahakikishia wapokeaji matumizi huru ya haki zao halali. Zaidi ya hayo, wajibu wa serikali ni kutoa msaada katika miradi ambayo, ingawa ni ya kufaa sana, hasa kwa vijana, haiwezi kufanikiwa [bila msaada huo].

Hatimaye, serikali yenyewe ambayo ndiyo yenye wajibu juu ya ustawi wa raia, yatakiwa pia kuhakikisha kwa uadilifu na makini, kwamba maadili ya taifa yasifishwe kutokana na matumizi mabaya ya vyombo hivyo. Hali hii huweza kufikiwa kwa kutunga sheria na kuzizingatisha kwa mafanikio. Uhuru wa mtu binafsi na wa vikundi, haukandamizwi na sheria hizo, hasa pale ambapo uhakika wa kutosha hautolewi na wale wanaotumia vyombo hivyo vya upashanaji habari minajili ya kazi yao.

Uangalifu wa pekee hauna budi kuzingatiwa katika kulinda vijana wadogo dhidi ya magazeti na burudani vinavyodhuru rika lao.

Sura ya Pili

VYOMBO VYA UPASHANAJI HABARI NA KAZI YA KITUME YA KANISA

Kazi ya Wachungaji na ya waamini

13. Wanakanisa wote wanatakiwa kufanya juhudi ya mashauri ya pamoja kuhakikisha kwamba vyombo vya upashanaji habari vinatumiwa kwa huduma mbalimbali za kichungaji bila kuchelewa na kwa juhudi zote ziwezekanazo, mahali na nyakati vihitajiwapo. Wanatakiwa kuwahi pale ambapo kuna miradi ambayo inaelekea kuleta uharibifu, hasa katika maeneo ambayo maendeleo ya kimaadili na ya kidini yanadai kuingilia kati pasipo kukawia.

Kwa hiyo Wachungaji wa Kanisa wanatakiwa kujibidisha sana katika uwanja huu kwani fani hii imefungamana na wajibu wao wa kuhubiri Injili. Walei wafanyao kazi za kiufundi kwa vyombo hivyo wajitahidi kutoa ushuhuda kwa Kristo. Awali ya yote kwa kufanya kazi yao kwa umahiri na kwa roho ya kitume, kwa kushirikiana moja kwa moja, kila mmoja kwa uwezo wake, katika kazi ya kichungaji ya Kanisa, kwa kutoa huduma zao za kitekniki, za kiuchumi, za kiutamaduni na za kisanaa.

Utendaji wa waamini

14. Kwanza kabisa uchapishaji mnyofu unatakiwa kuhimizwa. Ili kuwaundia wasomaji roho halisi ya kikristo, uchapishaji thabiti wa kikatoliki unatakiwa kuundwa na kusaidiwa. Uchapishaji kama huo, uwe umeanzishwa na kuongozwa na mamlaka ya Kanisa yenyewe au na watu wakatoliki (catholicis viris), utolewe kwa lengo wazi la kuunda, kuimarisha na kukuza maoni ya umma yanayolingana na sheria za asili, na mafundisho na maadili ya kikatoliki. Unatakiwa kusambaza na kufafanua kwa usahihi taarifa zinazohusu maisha ya Kanisa. Waamini wanatakiwa kukumbushwa juu ya umuhimu wa kusoma na kuyaeneza makala za kikatoliki ili kuweza kuchambua matukio yote katika mtazamo wa kikristo.

Matengenezo na maonyesho ya filamu ambazo zatoa burudani na ambazo zina ubora kiutamaduni na kisanaa, yatakiwa kukuzwa na kuhakikishwa kwa juhudi, kwa njia ya misaada mbalimbali ya kufaa, hasa zile zinazokusudiwa kwa vijana. Hayo yanatimizwa kwa ubora kutokana na kutegemeza na kuratibisha vyombo na miradi vya watengenezaji na wasambazaji wanyofu, kwa kuzisifu filamu nzuri kwa njia ya ukubali wa wahakiki na kwa zawadi, kwa kuzitegemeza na kuzishirikisha sinema zinazoendeshwa na watu wakatoliki na wanyofu.

Vilevile, vipindi vya redio na televisheni vinavyofaa, havina budi kutegemezwa kwa juhudi, hasa vile vinavyofaa kwa familia. Tena uhimizwe kwa bidii utangazaji wa kikatoliki ambao unakaribisha wasikilizaji na watazamaji kushiriki katika maisha ya Kanisa na kushika kweli za kidini. Vituo vya kikatoliki vyatakiwa kuanzishwa pale ambapo panafaa. Urushajihabari (transmissiones) wake uwe bora zaidi kwa njia ya ufundi sanifu wa kutosha na thabiti.

Bidii zifanyike ili sanaa ya zamani na bora ya tamthilia inayoenezwa kwa wazi kwa vyombo vya upashanaji habari, isaidie kukuza utamaduni na maadili kwa watazamaji.

Mafunzo ya watunzi

15. Mapadre, watawa na walei wanatakiwa kufunzwa mara moja juu ya mahitaji yaliyoelezwa hapo juu. Wanatakiwa kupata ujuzi wa kufaa ili kuvitumia vyombo hivyo kwa lengo la kichungaji.

Kwanza, walei wafunzwe ufundi, elimu ya imani, na maadili kwa njia ya kuzidi kuanzisha shule, vitivo na taasisi, ambamo waandishi wa habari, watunzi wa filamu na wanaohusika na usambazaji wa habari kwa njia ya redio na televisheni, pamoja na wengine wote wanaohusika na shughuli hizo, waweze kupewa mafunzo ya kutosha pamoja na mafundisho yenye roho ya kikristo, hasa katika uwanja wa mafundisho ya Kanisa juu ya jamii. Waigizaji wanatakiwa pia kuelekezwa na kusaidiwa ili kwamba sanaa yao inufaishe jamii. Hatimaye, wahakiki wa fasihi, wa filamu, wa redio, wa televisheni, n.k., waandaliwe kwa uangalifu, ili kwamba waweze kujitosheleza kwa ustadi wao katika fani yao na waweze kufunzwa na kutiwa moyo kusudi siku zote wajali inavyofaa maadili katika uchambuzi wao.

Malezi ya wapokeaji

16. Wapokeaji wa vyombo vya upashanaji habari wanatofautiana katika umri na kiwango cha elimu. Kwa hiyo, matumizi halali ya vyombo hivyo yanadai waandaliwe kinadharia na kimatendo, kwa namna maalum na za kufaa. Hivyo miradi inayoundwa ili kutoa huduma hii – hasa inayowaelekea vijana – yatakiwa kutiwa moyo na kuongezwa kwa wingi katika shule za kikatoliki za kila kiwango, katika seminari na katika vyama vya kitume vya walei, pia yatakiwa kuongozwa kadiri ya kanuni za maadili ya kikristo. Ili kupata upesi mafanikio, mafundisho na miongozo ya kikatoliki juu ya suala hili itolewe na kufafanuliwa katika katekisimu.

Vifaa na misaada

17. Kitakuwa ni kitendo cha aibu kama wanakanisa wanaruhusu neno la wokovu likwame na kupewa pingamizi kwa sababu ya ukosefu wa ufundi, au kwa gharama, iliyo kubwa mno, ya vyombo hivyo. Kwa sababu hii Mtaguso Mkuu unawakumbusha wakatoliki kwamba wanao wajibu wa kutegemeza na kusaidia magazeti ya kikatoliki, majarida, miradi ya filamu, vituo vya redio na televisheni, pamoja na urushaji wake wa habari. Lengo kubwa kwa hivi vyote ni kueneza na kulinda ukweli pamoja na kuwezesha mpenyezo wa malezi ya kikristo katika jamii za watu. Wakati huohuo yanakaribishwa kwa mikono miwili makundi au mtu mmoja mmoja, wenye uwezo katika teknolojia au katika uchumi, kutoa kwa hiari na kwa ukarimu hazina zao na ujuzi wao kwa vyombo hivyo, maadamu wanayo malengo ya kuhudumia utamaduni na uchungaji.

“Siku” ya upashanaji habari kila mwaka

18. Ili kufanya uchungaji wa Kanisa katika kipengere hiki cha vyombo vya upashanaji habari katika jamii kuwa thabiti, “Siku” maalum yafaa kupangwa katika kila mwaka kwa kila jimbo ulimwenguni, kwa maelekezo ya Maaskofu, ambapo waamini watakumbushwa wajibu zao katika fani hii. Waalikwe kusali kwa nia hiyo, na kutoa mchango wao kwa lengo hilo, mchango ambao hakika utatumika kutegemeza na kusitawisha taasisi na miradi ya Kanisa katika uwanja huo, kulingana na mahitaji ya ulimwengu wa kikatoliki.

Kamati maalum ya Kipapa

19. Katika kutekeleza huduma yake ya kichungaji katika uwanja wa vyombo vya upashanaji habari, Baba Mtakatifu anategemea Kamati maalum ya kipapa [1].

Madaraka ya Maaskofu

20. Ni wajibu wa Maaskofu kusimamia shughuli na miradi ya uwanja huu katika Majimbo yao, kuvikuza na kwa kiasi kinachohusu utume wa hadhara, kuiratibisha hata ile iliyo chini ya uongozi wa watawa wa kipapa (exemptorum).

Kamati za kitaifa

21. Utume fanisi katika taifa zima unahitaji ushirikiano katika lengo na nguvu. Kwa hiyo, Mtaguso huu Mkuu unathibitisha na kuamuru kwamba Kamati za kitaifa za uchapishaji, sinema, redio na televisheni ziundwe na kutegemezwa kwa njia zote. Wajibu mkubwa wa Kamati hizi utakuwa kutoa malezi ya dhamiri bora katika imani wakati wa kutumia vyombo hivyo, pamoja na kutia moyo na kusimamia kila kinachofanywa na wakatoliki katika kipengere hiki.

Katika kila nchi uongozi wa Kamati hizo ukabidhiwe kwa jopo la Maaskofu, au kwa Askofu mmoja aliyeteuliwa. Kamati hizo zatakiwa pia kuwa na walei miongoni mwa wajumbe wake, ambao wamefuzu katika mafundisho ya Kanisa katoliki na katika ufundi wa mambo haya.

Vyama vya kimataifa

22. Aidha, kwa vile uwezo wa vyombo vyenyewe unapita mipaka ya taifa ukiwafanya watu wote wa dunia hii kana kwamba ni raia wa nchi moja, miradi ya kitaifa katika uwanja huu yatakiwa kuratibishwa pia katika viwango vya kimataifa. Kamati zilizotajwa katika namba 21 hapo juu, zatakiwa kushirikiana kwa karibu sana na vyama vya kikatoliki vya kimataifa vinavyohusika. Vyama hivyo vya kikatoliki vya kimataifa vinathibitishwa na idhini ya Kiti Kitakatifu peke yake, na vinawajibika kwacho.

HITIMISHO

Taarifa ya kichungaji

23. Ili kuhakikisha kuwa kanuni na miongozo yote ya Mtaguso huu Mkuu [kuhusu vyombo vya upashanaji habari] vinatekelezwa, itolewe Taarifa ya kichungaji kwa agizo wazi la Mtaguso. Taarifa hiyo itungwe na Kamati ya Kipapa, iliyotajwa katika kifungo namba 19, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchi mbalimbali.

Himizo la mwishoni

24. Mwisho, Mtaguso huu Mkuu unayo matumaini kwamba wana wote wa Kanisa watazipokea na kuzizingatia kwa makini kanuni na miongozo iliyo katika hati hii. Hivyo, wao wenyewe kwa msaada wa vyombo hivi hawatapata madhara, bali watakuwa mfano wa chumvi na mwanga, na hivyo kuongeza ladha katika dunia na kuangaza ulimwengu. Zaidi ya hayo, Mtaguso unawaalika watu wote wenye mapenzi mema hasa wale wanaovidhibiti vyombo hivyo, wajitahidi kuvitumia kwa manufaa ya jamii ya binadamu ambao hali yao kila siku inategemea zaidi na zaidi matumizi manyofu ya vyombo hivyo. Kwa jinsi hii, kama kwa njia ya kazi bora za kisanaa za nyakati za kale, hali kadhalika kwa njia ya vyombo hivyo vilivyovumbuliwa siku hizi, Jina la Bwana litatukuzwa, kadiri ya neno la Mtume: “Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo na hata milele” (Ebr 13:8).

Mambo yote yaliyoamuliwa katika dikrii hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa Waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika Sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 4 Desemba 1963

 

Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki

(zinafuata sahihi za Mababa)


[1] Mababa wa Mtaguso, wakipokea rai ya “Ofisi ya Uchapishaji na Michezo” wanaomba kwa heshima kwa Baba Mtakatifu kwamba mamlaka na wajibu wa ofisi hiyo vipanuliwe, hata kuhusiana na vyombo vyote vya upashanaji habari, pamoja na uchapishaji, na waitwe kuiunda wataalamu wa nchi mbalimbali, walei wakiwemo miongoni mwao.