[BE
-
CS -
DE -
EN -
ES -
FR -
IT -
HU -
LA -
PT -
SW -
ZH]
Konstitusio ya kidogma juu ya Fumbo la Kanisa
Paulo Askofu Mtumishi wa watumishi wa Mungu pamoja
na Mababa wa Mtaguso mkuu ataka haya yakumbukwe daima
Sura ya Kwanza
FUMBO LA KANISA
Kanisa ni sakramenti katika Kristo
1. MWANGA WA MATAIFA (Lumen Gentium) ndiye Kristo. Ndiyo maana
Mtaguso huu Mkuu, uliokusanyika katika Roho Mtakatifu, watamani mno
kuwaangaza watu wote kwa mng’ao wake Kristo ung’arao juu ya uso wa Kanisa,
kwa njia ya kuitangaza Injili kwa kila kiumbe (taz. Mk 16:15). Katika Kristo
Kanisa ni kama sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu
kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Kwa hiyo [Mtaguso
huu], ukiendeleza mafundisho ya Mitaguso iliyotangulia, unadhamiria
kuwaeleza kinaganaga zaidi waamini wake na ulimwengu wote pia, maumbile yake
na utume wake kwa ajili ya watu wote. Mazingira ya nyakati hizi yanafanya
wajibu huu wa Kanisa uwe wa sharti zaidi sasa hivi, ili watu wote wanaozidi
kuunganika siku za leo kwa vifungo vya kijamii, kiteknolojia na kiutamaduni,
wapate kuufikia pia umoja kamili ndani ya Kristo.
Azimio la wokovu la Mungu Baba kwa ajili ya ulimwengu wote
2. Baba wa milele aliumba ulimwengu kwa azimio la hiari na la siri lenye
hekima na wema, akaamua kuwainua wanadamu hadi kuwashirikisha uhai wake wa
kimungu. Na pindi wanadamu walipoanguka katika Adamu, hakuwaacha kabisa,
bali aliwapatia sikuzote misaada ya wokovu kwa kumtazamia Kristo Mkombozi
“ambaye yu mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote”
(Kol 1:15). Maana wale wote walio wateule wake tangu milele, Mungu Baba
“aliwajua, akawachagua wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe
mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi” (Rum 8:29). Tena, [Baba]
aliazimia kuwakusanya [wote] wamwaminio Kristo katika Kanisa takatifu,
lililoashiriwa (praefigurata) tangu mwanzo wa ulimwengu, na
kutayarishwa kwa namna ya ajabu katika historia ya taifa la Israeli na
katika agano la kale[1]. Katika
nyakati za mwisho [Kanisa hilo] liliwekwa na kudhihirishwa kwa mmiminiko wa
Roho Mtakatifu, na tena mwishoni mwa karne litakamilishwa kwa utukufu. Hapo,
kama walivyoandika Mababa watakatifu wa Kanisa, wote wenye haki, kuanzia
Adamu, “na tangu Abili hata mteule wa mwisho”[2],
watakusanyika aliko Baba ndani ya Kanisa zima (Ecclesia universali).
Utume na kazi ya Mwana
3. Basi akaja Mwana ametumwa na Baba, naye Baba ndiye aliyetuteua katika
Yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, akatangulia kutuchagua ili
tufanywe wanawe; kwa maana ilimpendeza Baba kuvijumlisha vitu vyote katika
Yeye (taz. Efe 1:4-5 na 10). Hivyo Kristo, ili kuyatimiza mapenzi ya Baba,
akauzindua ufalme wa mbinguni hapa duniani, akatufunulia mafumbo yake Baba,
akafanya ukombozi kwa utii wake. Kanisa, ambalo ndilo ufalme wa Kristo
uliopo tangu sasa kati yetu katika fumbo, linakua wazi hapa duniani kwa
uwezo wa Mungu. Mwanzo na kukua kwa Kanisa vimeonyeshwa kwa ishara za damu
na maji zilizotoka katika ubavu uliochomwa wa Yesu msulibiwa (taz. Yn
19:34); vivyo hivyo vimebashiriwa na maneno ya Bwana yahusuyo kifo chake
msalabani, “Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu” (Yn
12:32). Kila mara inapoadhimishwa altareni sadaka ya msalaba – ambayo kwayo
“Kristo Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka” (1Kor 5:7) – kazi ya
ukombozi yatekelezwa. Pamoja na hayo, kwa sakramenti ya mkate wa Ekaristi
hudokezwa na kuundwa umoja wa waamini walio mwili mmoja katika Kristo (taz.
1Kor 10:17). Watu wote wanaitwa katika umoja huo na Kristo aliye nuru ya
ulimwengu; nasi tunatoka kwake Yeye, tunaishi kwa ajili yake, na kumwelekea
Yeye.
Roho Mtakatifu hulitakatifuza Kanisa
4. Pale ilipotimilika kazi Baba aliyomkabidhi Mwana afanye duniani
(taz. Yn 17:4), basi Roho Mtakatifu akatumwa siku ya Pentekoste ili
kulitakatifuza Kanisa siku hadi siku, na waamini wapate njia ya kumkaribia
Baba kwa Kristo katika Roho mmoja (taz. Efe 2:18). Huyo ndiye Roho wa uzima
au chemchemi ya maji yabubujikiayo uzima wa milele (taz. Yn 4:14; 7:38-39).
Kwa njia yake Baba anawahuisha wanadamu, walio wafu kwa sababu ya dhambi,
mpaka atakapofufua ndani ya Kristo [pia] miili yao iliyo katika hali ya kufa
(taz. Rum 8:10-11). Roho hukaa ndani ya Kanisa na ndani ya mioyo ya waamini
kama katika hekalu (taz. 1Kor 3:16; 6:19); naye huomba ndani yao na
kushuhudia ya kuwa walifanywa kuwa wana (taz. Gal 4:6; Rum 8:15-16 na 26).
Naye huliongoza Kanisa kwenye kweli yote (taz. Yn 16:13), hulifanya kuwa
moja katika ushirika na huduma, na kulifadhili vipawa mbalimbali vya
kihierarkia na vya kikarama, ambavyo kwavyo huliongoza na kulipamba kwa
matunda yake (taz. Efe 4:11-12; 1Kor 12:4; Gal 5:22). Kwa nguvu ya Injili
hulitia tena Kanisa ujana wake, hulitengeneza upya daima na kuliongoza
lipate kuunganika kikamilifu na Bwanaarusi wake[3].
Maana Roho na Bibiarusi wamwambia Bwana Yesu, “Njoo!” (taz. Ufu 22:17).
Hivyo Kanisa zima ulimwenguni linajionyesha kuwa “taifa lililokusanywa na
umoja wa Baba, wa Mwana na wa Roho Mtakatifu”[4].
Ufalme wa Mungu
5. Fumbo la Kanisa takatifu linajidhihirisha katika kuanzishwa kwake
lenyewe. Maana Bwana Yesu alianzisha Kanisa lake kwa kuihubiri habari njema,
yaani ujio wa ufalme wa Mungu, ulioahidiwa tangu karne nyingi katika
Maandiko: “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia” (Mk 1:15; taz. Mt
4:17). Ufalme huo unang’aa wazi mbele ya watu katika Neno la Kristo, katika
matendo yake na uwepo wake. Neno la Bwana linafananishwa na mbegu
iliyopandwa shambani (taz. Mk 4:14): wanaolisikiliza kwa imani na kuhesabiwa
katika kundi dogo la Kristo (taz. Lk 12:32) wameupokea ufalme wenyewe wa
Mungu. Halafu mbegu hiyo, kwa nguvu yake yenyewe, ikamea na kukua hata
wakati wa mavuno (taz. Mk 4:26-29). Hata miujiza ya Yesu yathibitisha ya
kuwa ufalme umekwisha fika duniani: “Ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha
Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia” (Lk 11:20; taz. Mt 12:28).
Lakini kwanza kabisa ufalme wajionyesha katika nafsi ya Kristo mwenyewe
aliye Mwana wa Mungu na Mwana wa Adamu, ambaye alikuja “kutumika na kutoa
nafsi yake iwe fidia ya wengi” (Mk 10:45).
Na hatimaye Yesu alipofufuka, baada ya kufa msalabani kwa ajili ya
wanadamu, alijidhihirisha ya kuwa amewekwa kuwa Bwana na Kristo na Kuhani
milele (taz. Mdo 2:36; Ebr 5:6; 7:17-21), akawamwagia wanafunzi wake Roho
Mtakatifu aliyeahidiwa na Baba (taz. Mdo 2:33). Hivyo Kanisa ambalo
lilijaliwa vipaji vyema vya Mwanzilishi wake na kushika kwa uaminifu amri
zake za upendo, unyenyekevu na kujitolea, lakabidhiwa utume wa kuutangaza
ufalme wa Kristo na wa Mungu, na kuusimika kati ya mataifa. Nalo Kanisa hapa
duniani li chipukizi na chanzo cha ufalme huo. Wakati linapokua polepole
lautazamia kwa shauku ufalme mkamilifu, na kwa nguvu zake zote latumaini na
kutamani kujiunga na Mfalme wake katika utukufu.
Mifano ya Kanisa
6. Katika Agano la kale ufunuo wa ufalme wa Mungu umetolewa mara
nyingi kwa njia ya mifano. Vivyo hivyo sasa maumbile ya ndani ya Kanisa
hujidhihirisha kwetu kwa ishara mbalimbali, zitokanazo na maisha ya
wachungaji na wakulima, kama vile na kazi ya kujenga, au na maisha ya
familia na arusi. Na ishara hizo zimewahi kutayarishwa katika vitabu vya
Manabii.
Hivyo Kanisa ni zizi, ambalo mlango wake mmoja tu na wa
lazima ndiye Kristo (taz. Yn 10:1-10). Nalo ni pia kundi la kondoo, ambalo
Mungu mwenyewe alihubiri tangu zamani ya kwamba atakuwa mchungaji wake (taz.
Isa 40:11; Eze 34:11nk). Kondoo wake, ijapokuwa wanachungwa na wanadamu,
huongozwa na kulishwa na Kristo mwenyewe aliye Mchungaji mwema na Mkuu wa
wachungaji (taz. Yn 10:11; 1Pet 5:4), ambaye aliutoa uhai wake kwa ajili ya
kondoo (taz. Yn 10:11-15).
Kanisa ni ardhi iliyolimwa, ni shamba la Mungu (taz. 1Kor 3:9).
Katika shamba hilo mzeituni ule wa zamani hukua, ambao shina lake takatifu
ni Mababu, na ndani yake upatanisho wa Wayahudi na wa Mataifa umeletwa na
utaendelea kuletwa (taz. Rum 11:13-26). Mzeituni huu ulipandwa na Mkulima wa
mbinguni kama shamba la mizabibu lililoteuliwa (taz. Mt 21:33-43//; Isa
5:1nk). Kristo ndiye mzabibu wa kweli anayeyajalia matawi, yaani sisi, uhai
na uwezo wa kuzaa; nasi, kwa njia ya Kanisa, twakaa ndani yake, na pasipo
yeye hatuwezi kufanya neno lolote (taz. Yn 15:1-5).
Mara nyingi zaidi Kanisa huitwa jengo la Mungu (taz. 1Kor 3:9). Bwana
mwenyewe alijifananisha na jiwe walilokataa waashi, nalo lakini limekuwa
jiwe kuu la pembeni (taz. Mt 21:42//; Mdo 4:11; 1Pet 2:7; Zab 118:22). Na
Kanisa lilijengwa na Mitume juu ya msingi huo (taz. 1Kor 3:11), na kutoka
kwake lapata uimara na muungano. Jengo hilo huelezwa kwa majina mbalimbali:
nyumba ya Mungu (taz. 1Tim 3:15), inamokaa familia yake, maskani ya
Mungu katika roho (taz. Efe 2:19-22), “maskani ya Mungu pamoja na wanadamu”
(Ufu 21:3). Na hasa laitwa hekalu takatifu, ambalo ishara zake ni
mahali patakatifu palipojengwa kwa mawe, ambalo limesifiwa na Mababa
watakatifu, na katika Liturujia hufananishwa kwa haki na Mji mtakatifu, ndio
Yerusalemu mpya[5]. Maana ndani
yake sisi tumejengwa hapa duniani kama mawe yaliyo hai (taz. 1Pet 2:5). Mji
huo mtakatifu Yohane anautazama, wakati ulimwengu unapofanywa upya, kama
ulioshuka kutoka mbinguni kwa Mungu, nao umewekwa tayari kama Bibiarusi
aliyekwisha kupambwa kwa mumewe (Ufu 21:1nk).
Hatimaye Kanisa huitwa pia “Yerusalemu ya juu” na “mama yetu” (Gal 4:26;
taz. Ufu 12:17), na kuelezwa kama Bibiarusi asiye na mawaa wa Mwanakondoo
asiye na mawaa (taz. Ufu 19:7; 21:2 na 9; 22:17). Kristo “alilipenda
...akajitoa kwa ajili yake, kusudi alitakase” (Efe 5:25-26), akaliunganisha
naye kwa agano lisilovunjika, daima “analilisha na kulitunza” (Efe 5:29).
Basi alipokwisha kulitakasa alitaka liunganike naye na kumtii katika upendo
na uaminifu (taz. Efe 5:24); hatimaye akalijaza vipaji vya mbinguni hata
milele ili sisi tupate kuujua upendo wa Mungu na wa Kristo kwa ajili yetu,
upitao kila ufahamu (taz. Efe 3:19). Wakati Kanisa linaposafiri hapa duniani
mbali na Bwana (taz. 2Kor 5:6), hujiona kuwa ni mgeni, hata likatafute na
kuyazingatia yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,
ambapo uhai wa Kanisa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu, mpaka
[Kanisa] litakapofunuliwa pamoja na Bwana arusi wake katika utukufu (taz.
Kol 3:1-4).
Kanisa ni mwili wa Kristo
7. Mwana wa Mungu, katika hali ya kibinadamu aliyofungamana nayo,
aliposhinda mauti kwa kifo chake na ufufuko wake, alimkomboa mwanadamu,
akamgeuza kuwa kiumbe kipya (taz. Gal 6:15; 2Kor 5:17). Maana kwa
kuwashirikisha Roho wake, anawafanya ndugu zake waitwao kutoka katika
mataifa yote kuwa mwili wake katika fumbo.
Ndani ya mwili huo uhai wa Kristo hutiwa katika waamini, ambao kwa
njia ya sakramenti wanaunganishwa, kwa jinsi ya siri na ya kweli, na Kristo
aliyeteswa na kutukuzwa[6]. Maana
kwa ubatizo tumefananishwa na Kristo: “Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote
tulibatizwa kuwa mwili mmoja” (1Kor 12:13). Katika ibada hii takatifu
ushirikiano wetu na kifo cha Kristo na ufufuko wake huonyeshwa kwa ishara na
kutekelezwa: “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti
yake”; na “kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika
tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake” (Rum 6:4-5). Kwa kushiriki kweli
mwili wa Bwana katika kumega mkate wa Ekaristi, twainuliwa hadi tuufikie
ushirikiano naye na kati yetu, “Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu
mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja” (1Kor
10:17). Hivyo sisi sote tumekuwa viungo vya mwili ule (taz. 1Kor 12:27), “na
sisi tu viungo, kila mmoja kwa mwenzake” (Rum 12:5).
Kama vile viungo vyote vya mwili wa kibinadamu, ijapo ni vingi, ni
mwili mmoja, vivyo hivyo na waamini katika Kristo (taz. 1Kor 12:12). Hata
katika kujenga mwili wa Kristo kuna tofauti za viungo na za kazi zake. Roho
ni mmoja agawiaye karama zake mbalimbali kwa ajili ya manufaa ya Kanisa,
kadiri ya utajiri wake mwenyewe na hitaji la huduma. Neema waliyopewa Mitume
ni bora zaidi kati ya karama hizo, na Roho mwenyewe aliwatiisha chini ya
mamlaka yao pia wale waliojaliwa karama za pekee (taz. 1Kor 14). Roho
huyohuyo akiunganisha katika umoja mwili huu, kwa njia yake mwenyewe, kwa
uweza wake na kwa muungano wa ndani wa viungo vyake, hutengeneza na
kuchochea umoja kati ya waamini. Kwa hiyo kiungo kimoja kikiumia, viungo
vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi
pamoja nacho (taz. 1Kor 12:26).
Kichwa cha mwili huo ndiye Kristo. Naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana,
na katika yeye vitu vyote viliumbwa. Yeye amekuwako kabla ya vyote, na vitu
vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha Kanisa;
naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi
katika yote (taz. Kol 1:15-18). Kwa ukuu wa uweza wake atawala juu ya vitu
vyote vilivyo mbinguni na duniani, na kwa ukamilifu wake upitao vyote na kwa
utendaji wake aujaza mwili wote kwa utajiri wa utukufu wake (taz. Efe
1:18-23)[7].
Viungo vyote lazima viundwe ili kufanana na Kristo, hata yeye aumbike ndani
yao (Gal 4:19). Kwa sababu hiyo sisi, tuliopata kufanana naye, tuliokufa pamoja
naye na kufufuliwa pamoja naye, tumeingizwa katika mafumbo ya maisha yake, hata
tutakapotawala pamoja naye (taz. Flp 3:21; 2Tim 2:11; Efe 2:6; Kol 2:12; n.k.).
Nasi tungali wasafiri bado hapa duniani, tunapofuata nyayo zake katika dhiki na
dhuluma, tunaunganishwa na mateso yake kama vile mwili unavyounganika na kichwa,
na tunateswa pamoja naye ili tupate kutukuzwa pamoja naye (taz. Rum 8:17).
“Kwa yeye mwili wote ukiruzukiwa na kuungamanishwa kwa viungo na
mishipa, hukua kwa maongeo yatokayo kwa Mungu” ( Kol 2:19). Yeye katika
mwili wake, yaani Kanisa, anagawa daima karama za huduma. Nasi kwa msaada wa
karama hizi tunatumikiana sisi kwa sisi kwa nguvu yake mwenyewe, ili
tuokoke, na tukiushika ukweli katika mapendo tukue hata tumfikie yeye katika
yote, aliye kichwa chetu (taz. Efe 4:11-16).
Aidha ili tufanywe wapya daima ndani yake (taz. Efe 4:23),
alitushirikisha Roho wake ambaye ni mmoja na yuleyule katika kichwa na
katika viungo. Naye Roho huuhuisha na kuungamanisha na kuusukuma mwili wote
hivi kwamba kazi yake ilifananishwa na Mababa watakatifu na kazi itendayo
roho ndani ya mwili wa mtu, ambayo ndiyo asili ya uzima wake[8].
Kristo analipenda Kanisa kama Bibiarusi wake, akawa mfano wa mume
anayempenda mke wake kama mwili wake mwenyewe (taz. Efe 5:25-28). Kwa upande
wake Kanisa hukitii kichwa chake (taz. Efe 5:23-24). Maadamu “katika yeye
unakaa utimilifu wote wa Mungu kwa jinsi ya kimwili” (Kol 2:9), basi
utimilifu wake hulijaza Kanisa, lililo mwili wake na utimilifu wake, kwa
vipaji vyake vya kimungu (taz. Efe 1:22-23), ili lipate kuuelekea na
kuufikia utimilifu wote wa Mungu (taz. Efe 3:19).
Kanisa lionekanalo na lisiloonekana
8. Kristo, aliye mshenga pekee, aliliweka duniani Kanisa lake
takatifu, lililo jumuiya ya imani, matumaini na mapendo, kama muundo (compaginem)
unaoonekana; na daima hulilisha[9]
na kwa njia yake hueneza kwa watu wote ukweli na neema. Jamii iliyoundwa na
viungo vya kihierarkia na mwili wa fumbo la Kristo; kusanyiko linaloonekana
na jumuiya ya kiroho; Kanisa lililopo duniani na Kanisa lililokwisha pata
urithi wa mema mbinguni; mambo hayo yasihesabiwe kuwa ni mambo mawili
tofauti, bali ni jambo moja tu, changamano linalounganisha sehemu moja ya
kibinadamu na sehemu nyingine ya kimungu[10].
Kwa hiyo kwa ulinganifu ulio mzuri Kanisa hufananishwa na fumbo la Neno
lililofanyika mwili. Maana, kama vile maumbile [ya kibinadamu] yaliyotwaliwa
na Neno wa Mungu na kuunganika naye kwa njia isiyotengeka yanavyomtumikia
kama chombo cha wokovu chenye uhai, vivyo hivyo muundo wa kijamii wa Kanisa
unamtumikia Roho wa Kristo anayeuhuisha, kwa ajili ya kuukuza mwili (taz.
Efe 4:16)[11].
Hilo ndilo Kanisa pekee la Kristo tunalolikiri katika kanuni ya
imani kwamba ni moja, takatifu, katoliki na la mitume[12].
Mwokozi wetu, baada ya ufufuko wake, alilikabidhi kwa Petro ili alilishe
(taz. Yn 21:17); akamwagiza yeye na mitume wengine walieneze na kuliongoza
(taz. Mt 28:18 n.k.); akaliweka kwa nyakati zote kama nguzo na msingi wa
kweli (taz. 1Tim 3:15). Kanisa hilo, lililoundwa na kupangwa kama jamii
katika ulimwengu huu, linaendelea kuwepo (subsistit) katika Kanisa
katoliki, linalotawaliwa (gubernata) na Halifa wa Petro na Maaskofu
katika ushirika naye[13].
Lakini pia nje ya muundo huu unaoonekana, hupatikana mambo mengi ya
kutakatifuza na ya ukweli, ambayo, kama vipaji vilivyo mali ya Kanisa la
Kristo, husukuma kwenye umoja wa kikatoliki.
Kama vile Kristo alivyotimiza kazi yake ya ukombozi katika hali ya
umaskini na madhulumu, vivyo hivyo Kanisa laitwa kushika njia hiyohiyo ili
kuwashirikisha watu matunda ya wokovu. Yesu Kristo “ambaye yeye mwanzo
alikuwa yuna namna ya Mungu...alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya
mtumwa” (Flp 2:6-7); na kwa ajili yetu “ingawa alikuwa tajiri, akajifanya
maskini” (2Kor 8:9). Vilevile Kanisa, ingawa linahitaji misaada ya wanadamu
kwa kutekeleza utume wake, halikuwekwa ili kutafuta utukufu wa kidunia, bali
kusudi lifahamishe [pote] unyenyekevu na roho ya kujihinisha
(abnegationem),
hata kwa kutoa mfano wake lenyewe. Kristo alitumwa na Baba “kuwahubiri
maskini habari njema...kuwaponya waliovunjika moyo” (Lk 4:18), na “kutafuta
na kuokoa kilichopotea” (Lk 19:10). Vivyo hivyo Kanisa huwahurumia kwa
mapendo yake wanaotaabika kwa udhaifu wa kibinadamu; zaidi hutambua katika
maskini na wateswa sura ya Mwasisi wake aliyekuwa naye maskini na mteswa;
tena hujishughulisha kuinua umaskini wao, na hunuia kumtumikia Kristo ndani
yao. Kristo aliye “mtakatifu, asiye na uovu, asiye na waa lolote” (Ebr
7:26), hakujua dhambi (taz. 2Kor 5:21), bali alikuja tu “ili afanye suluhu
kwa dhambi za watu” (taz. Ebr 2:17). Lakini Kanisa, ambalo huwakumbatia
wakosefu ndani yake, na wakati uleule ni takatifu na linahitaji kutakaswa,
haliachi kamwe kutubu na kujitengeneza upya.
Kanisa “linaendelea mbele katika kuhiji kwake katikati ya
madhulumu ya ulimwengu na faraja za Mungu”[14],
likitangaza msalaba na mauti ya Bwana hata ajapo (taz. 1Kor 11:26). Kwa
uwezo wa Bwana aliyefufuka linapata nguvu ya kuzishinda, kwa saburi na
upendo, taabu na shida za ndani na za nje, na ya kuufunulia ulimwengu, kwa
uaminifu, fumbo la Bwana, ingawa bado lipo katika kivuli, mpaka mwisho wa
nyakati litakapodhihirishwa katika ukamilifu wa mwanga wake.
Sura ya Pili
TAIFA LA MUNGU
Agano jipya na taifa jipya
9. Kila wakati na katika kila taifa mtu amchaye Mungu na kutenda haki
hukubaliwa na yeye (taz. Mdo 10:35). Lakini ilimpendeza Mungu kuwatakatifuza
na kuwaokoa watu, siyo mmoja mmoja na pasipo muungano kati yao, bali kwa
kuwaunda kama taifa moja, lenye kumjua katika ukweli na kumtumikia
kitakatifu. Kwa hiyo alijichagulia watu wa Israeli kuwa taifa lake, akafunga
agano na taifa hilo, akalifundisha polepole kwa kujidhihirisha katika
historia yake yeye mwenyewe na kufunulia kusudio la mapenzi yake, naye
akaliweka wakfu kwa ajili yake. Lakini hayo yote yalitokea kama matayarisho
na mfano wa lile agano lililo jipya na kamilifu ambalo lilitakiwa kufungwa
katika Kristo, na wa ule ufunuo mtimilifu wa kuletwa na Neno wa Mungu
mwenyewe aliyejifanya mwili. “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana,
nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda... Nitatia
sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu
wao, nao watakuwa watu wangu... Watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo
miongoni mwao, hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana” (Yer 31:31-34).
Kristo aliliweka agano hilo jipya, yaani Agano Jipya katika damu yake (taz.
1Kor 11:25), akiwaita watu kutoka Wayahudi na mataifa, ili waungane siyo kwa
kadiri ya mwili, bali katika Roho, na wawe taifa jipya la Mungu. Maana
wamwaminio Kristo waliozaliwa mara ya pili, si kwa mbegu iharibikayo, bali
kwa ile isiyoharibika, kwa Neno la Mungu lenye uzima (taz. 1Pet 1:23), si
kwa mwili, bali kwa maji na kwa Roho Mtakatifu (taz. Yn 3:5-6); hawa
walifanywa kuwa “mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa
milki ya Mungu... waliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu”
(1Pet 2:9-10).
Kichwa cha taifa hili la kimasiya ni Kristo, “ambaye alitolewa kwa ajili ya
makosa yetu, na kufufuliwa ili tupate kuhesabiwa haki” (Rum 4:25). Naye sasa
atawala kwa utukufu mbinguni, baada ya kupata jina lipitalo kila jina. Taifa
hilo, hali yake ni heshima na uhuru wa watoto wa Mungu, ambao ndani ya mioyo yao
Roho Mtakatifu hukaa kama katika hekalu lake. Sheria yake ni amri mpya ya
kupendana kama Kristo mwenyewe alivyotupenda (taz. Yn 13:34). Na hatimaye kikomo
chake ndicho ufalme wa Mungu, ulioanzishwa duniani na Mungu mwenyewe, na
unaopaswa kupanuliwa zaidi hata utimizwe naye mwisho wa nyakati, Kristo
atakapofunuliwa, aliye uhai wetu (taz. Kol 3:4), na “viumbe vyenyewe navyo
vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru
wa utukufu wa watoto wa Mungu” (Rum 8:21). Kwa hiyo taifa hili la kimasiya,
ijapo kwa kweli halijawachukua ndani yake watu wote, na mara nyingi huonekana
kuwa kundi dogo tu, lakini ni mbegu thabiti sana ya umoja, tumaini na wokovu kwa
jamii nzima ya wanadamu. Nalo limewekwa na Kristo katika ushirika wa maisha, wa
upendo na wa ukweli, likatwaliwa naye kuwa chombo cha ukombozi wa watu wote,
likatumwa ulimwenguni mwote kuwa nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia (taz. Mt
5:13-16).
Kama vile taifa la Israeli kadiri ya mwili lenye kutangatanga
jangwani, lilivyoitwa Kanisa la Mungu (taz. Neh 13:1; Hes 20:4; Kum 23:1nk),
vivyo hivyo taifa jipya la Israeli lenye kusafiri wakati huu likiutafuta mji
ujao na udumuo (taz. Ebr 13:14), huitwa Kanisa la Kristo (taz. Mt 16:18).
Kristo alilinunua kwa damu yake mwenyewe (taz. Mdo 20:28), akalijaza Roho
wake, akalijalia misaada inayofaa kwa ajili ya umoja uonekanao na wa
kijamii. Mungu alikusanya kusanyiko la wenye kumtazama kwa imani Yesu aliye
mtendaji wa wokovu na asili ya umoja na amani; naye akawaweka kuwa Kanisa
ili Kanisa hilo liwe, kwa ajili ya wote na kwa kila mmoja, sakramenti
inayoonekana ya umoja huu uletao wokovu[15].
Kanisa, likitakiwa kuenea mahali pote, huingia katika historia ya watu,
lakini wakati huohuo linavuka mipaka ya nyakati na ya mataifa. Kanisa hilo
likisafiri katika majaribu na dhiki hutiwa nguvu na uwezo wa neema ya Mungu
iliyoahidiwa na Bwana, lisije likatindikiwa uaminifu kamili kwa ajili ya
udhaifu wa kibinadamu, bali lidumu kuwa Bibiarusi stahivu wa Bwana wake;
wala lisiache kujitengeneza upya kwa msaada wa Roho Mtakatifu, hadi
liifikie, kwa njia ya msalaba, nuru isiyojua kuchwa.
Ukuhani wa waamini wote
10. Kristo Bwana ndiye Kuhani Mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu (taz. Ebr
5:1-5), alilifanya taifa hili jipya kuwa “ufalme na makuhani kwa Mungu Baba
yake” (Ufu 1:6; taz. 5:9-10). Maana, kwa kuzaliwa mara ya pili na kupakwa mafuta
ya Roho Mtakatifu, waliobatizwa wanawekwa wakfu kuwa makao ya kiroho na ukuhani
mtakatifu, ili kutoa dhabihu za kiroho kwa njia ya matendo yote ya kila mkristo,
na kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita watoke gizani na waingie katika nuru
yake ya ajabu (taz. 1Pet 2:4-10). Kwa hiyo wanafunzi wote wa Kristo, wakidumu
katika kusali na kumsifu Mungu pamoja (taz. Mdo 2:42-47), wajitoe wenyewe wawe
dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu (taz. Rum 12:1); tena
wamshuhudie Kristo popote duniani na wamjibu kila mtu awaulizaye habari za
tumaini la uzima wa milele lililo ndani yao (taz. 1Pet 3:15).
Ukuhani wa waamini wote na ukuhani wa kidaraja au wa kihierarkia, ingawa
huhitilafiana kadiri ya kiini chake na siyo kadiri ya cheo tu, huelekezana
kati yake kwa sababu zote mbili, na kila mmoja kwa namna yake, hushiriki
ukuhani mmoja wa Kristo[16].
Kuhani wa kidaraja, kwa mamlaka takatifu aliyo nayo, hulea na kuliongoza
taifa la kikuhani, huadhimisha sadaka ya Ekaristi katika nafsi ya Kristo na
kuitolea kwa Mungu kwa jina la taifa lote. Waamini wanashiriki sadaka ya
Ekaristi kwa nguvu ya ukuhani wao wa kifalme[17],
watekeleza ukuhani huo kwa kupokea sakramenti, kusali na kutoa shukrani, kwa
ushuhuda wa maisha matakatifu, kwa kujikana na kwa upendo wenye utendaji.
Kutekelezwa kwa ukuhani wa waamini wote katika sakramenti
11. Tabia takatifu ya jumuiya ya kikuhani inatekelezwa, pamoja na
muundo wake wenye utaratibu, kwa njia ya sakramenti na fadhila. Waamini,
waliofanywa kuwa viungo vya Kanisa kwa ubatizo, kwa muhuri (charactere)
wa ubatizo wameteuliwa na wameagizwa kutoa ibada ya dini ya kikristo, na
maadamu walizaliwa upya kuwa watoto wa Mungu, yawapasa kuikiri mbele ya watu
imani waliyoipokea kwa Mungu kwa njia ya Kanisa[18].
Kwa sakramenti ya kipaimara waunganishwa na Kanisa kikamilifu zaidi na
kujaliwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu; kwa hiyo wanawajibika zaidi
kuieneza na kuitetea imani kwa neno na kwa matendo, kama mashahidi wa kweli
wa Kristo[19]. Wakishiriki
sadaka ya Ekaristi, iliyo chemchemi na kilele cha maisha yote ya kikristo,
wanamtolea Mungu dhabihu ya kimungu na kujitoa wenyewe pamoja nayo[20].
Hivyo wote, kwa kutoa sadaka au kwa kupokea Komunyo takatifu, wanatenda kazi
yao katika Liturujia, wala si wote sawasawa, bali kila mmoja kwa namna yake.
Tena wakiimarishwa kwa kula mwili wa Kristo katika kusanyiko (synaxi)
takatifu, wadhihirisha wazi umoja wa taifa la Mungu, ambao huonyeshwa kwa
jinsi ifaayo na kufanyizwa kwa namna ya ajabu kwa sakramenti hii tukufu
sana.
Wanaoijongea sakramenti ya kitubio hupokea humo kutoka huruma ya Mungu
ondoleo la makosa yaliyotendwa dhidi yake, na papo hapo hupatanishwa na
Kanisa, ambalo dhambi yao imelijeruhi, na ambalo kwa mapendo, mfano na sala
huhangaikia wongofu wao. Kwa mpako mtakatifu wa wagonjwa na sala ya mapadre,
Kanisa lote linawakabidhi wagonjwa kwa Bwana aliyeteswa na kutukuzwa, ili
awainue na kuwaokoa (taz. Yak 5:14-16); waama linawasihi hasa wajiunge kwa
hiari na mateso na kifo cha Bwana (taz. Rum 8:17; Kol 1:24; 2Tim 2:11-12;
1Pet 4:13), ili walifaidie taifa la Mungu. Tena, wale miongoni mwa waamini
wanaopokea Daraja takatifu, wanawekwa kwa jina la Kristo kulichunga Kanisa
kwa Neno la Mungu na neema yake. Na hatimaye, wakristo wafunga ndoa, ambao
kwa nguvu ya sakramenti yao ya ndoa waisharisha na kulishiriki fumbo la
umoja na la upendo wenye kuzaa kati ya Kristo na Kanisa (taz. Efe 5:32),
wanasaidiana kuufikia utakatifu katika maisha ya ndoa na katika kuwapokea na
kuwalea watoto wao; kwa hiyo katika hali na hadhi ya maisha yao wana karama
yao ya pekee ndani ya taifa la Mungu[21].
Maana katika ndoa hii hutokea familia ambayo ndani yake wanazaliwa raia
wapya wa jamii ya kibinadamu, ambao kwa neema ya Roho Mtakatifu wanafanywa
kuwa watoto wa Mungu kwa ubatizo, ili kuliendeleza taifa lake Mungu karne
kwa karne. Katika familia, iliyo kama Kanisa la kinyumbani, yawapasa wazazi
kuwa watangazaji wa kwanza wa imani kwa ajili ya watoto wao, kwa neno na
mfano wao, na kusaidia wito maalum wa kila mmoja, na kwa uangalifu wa pekee
hasa ule wito mtakatifu.
Kwa kuimarika na misaada ya wokovu mingi namna hii na ya ajabu,
waamini wote wa kila hali na hadhi wanaitwa na Bwana, kila mmoja kwa njia
yake, kwenye ukamilifu wa utakatifu kama Baba mwenyewe alivyo mtakatifu.
Hisia ya imani na karama katika taifa la Mungu
12. Taifa takatifu la Mungu laishiriki pia kazi ya unabii wa Kristo,
linapoueneza ushuhuda wake ulio hai hasa kwa njia ya maisha ya imani na
upendo, na kumpa Mungu dhabihu ya sifa, tunda la midomo iliungamayo jina
lake (taz. Ebr 13:15). Waamini wote waliopakwa mafuta na Yeye aliye
Mtakatifu (taz. 1Yoh 2:20 na 27) hawawezi kukosa katika mambo ya imani; nao
hudhihirisha tabia yao hiyo ya pekee, isiyo ya dunia hii, kwa njia ya
utambuzi wa imani (sensu fidei) ya taifa lote, pale ambapo “kuanzia
maaskofu hadi waamini walei wa mwisho”[22]
wanaonyesha makubaliano (consensum) ya wote kuhusu mambo ya imani na
ya adili. Maana kwa hisia hiyo ya imani iliyoamshwa na kutegemezwa na Roho
wa ukweli, taifa la Mungu, chini ya uongozi wa Majisterio takatifu
linayoifuata kwa uaminifu, hulipokea si neno la wanadamu, bali hakika Neno
la Mungu (taz. 1The 2:13). Tena huishika daima “imani waliyokabidhiwa
watakatifu mara moja tu” (Yda 3), na kwa hukumu iliyo nyofu huipenya kwa
undani zaidi na kuitia kikamilifu katika maisha yake.
Na Roho Mtakatifu mwenyewe, licha ya kutakatifuza taifa la Mungu
na kuliongoza na kulipamba kwa fadhila mbalimbali kwa njia ya sakramenti na
huduma, atoa pia karama za pekee miongoni mwa waamini wa kila hadhi kwa
“kumgawia kila mtu peke yake karama zake kama apendavyo yeye” (1Kor 12:11);
na kusudi lake ndilo kuwafanya wafae na kuwa tayari kuzishika kazi na huduma
mbalimbali zenye kuleta manufaa kwa ajili ya matengenezo ya Kanisa na
maongezo yake, kadiri ilivyoandikwa, “Kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa
kufaidiana” (1Kor 12:7). Karama hizo zisizo za kawaida au zile za kawaida
ambazo zimesambazwa kwa kiasi kikubwa, hazina budi kupokelewa kwa shukrani
na faraja, maadamu ni zenye kufaa sana na kusaidia kwa mahitaji ya Kanisa.
Lakini karama hizi zisizo za kawaida zisiombwe bila uchaji, wala matunda ya
kazi za kitume yasitumainiwe kwa ujuvi kutokana nazo. Lakini kuamua uhalisi
wake na matumizi yake yenye utaratibu ni juu ya wale wanaosimamia katika
Kanisa, ambao yawapasa hasa siyo kumzimisha Roho, bali kujaribu mambo yote
na kulishika lililo jema (taz. 1The 5:12 na 19-21).
Kuenea kwa taifa pekee la Mungu popote duniani
13. Watu wote waitwa kuliingia taifa jipya la Mungu. Kwa hiyo
taifa hili, likiendelea kuwa moja na pekee, inabidi lienee ulimwenguni pote
na kwa karne zote, ili litimizwe azimio la mapenzi ya Mungu, ambaye awali
aliumba maumbile ya kibinadamu kuwa kitu kimoja, akaamua kuwakusanya watoto
wake waliotawanyika ili wawe wamoja (taz. Yn 11:52). Kwa kusudi hilo Mungu
akamtuma Mwanae, aliyemweka kuwa mrithi wa yote (taz. Ebr 1:2), ili awe
Mwalimu, Mfalme na Kuhani wa watu wote, kichwa cha taifa jipya na la popote
duniani la watoto wa Mungu. Ndiyo sababu Mungu akamtuma pia Roho wa Mwanae,
aliye Bwana na Mleta uzima, ambaye ndiye asili ya muungano na umoja kwa
Kanisa zima na kwa waamini wote na kwa kila mmoja wao, katika fundisho la
Mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali (taz.
Mdo 2:42).
Hivyo taifa lile moja la Mungu lipo sasa katika mataifa yote ya dunia,
maadamu Mungu hutwaa katika mataifa raia wake, walio raia wa ufalme ambao
kwa maumbile yake si wa kidunia, bali wa kimbingu. Kwa hiyo waamini wote
waliotawanyika ulimwenguni washirikiana wao kwa wao katika Roho Mtakatifu,
na hivyo “yule akaaye Rumi ajua kuwa Wahindi ni viungo vyake”[23].
Lakini, maadamu ufalme wa Kristo si wa ulimwengu huu (taz. Yn 18:36), Kanisa
au taifa la Mungu liletalo ufalme huu, halilinyimi taifa lolote chochote cha
mali yake ya kidunia, bali kinyume chake husaidia na kupokea uwezo, utajiri
na desturi vya mataifa, kwa kadiri vilivyo vyema, na katika kuvipokea
huvitakasa, huviimarisha na kuviinua. Maana lakumbuka kwamba linapaswa
kukusanya pamoja na Mfalme yule aliyepewa mataifa kuwa urithi wake (taz. Zab
2:8), nayo mataifa yanaleta vipawa vyao na sadaka zao katika mji wake (taz.
Zab 72:10; Isa 60:4-7; Ufu 21:24). Tabia hii, ya kuenea pote duniani,
ilipambayo taifa la Mungu ndiyo kipaji cha Bwana mwenyewe, na kwa njia yake
Kanisa katoliki, kwa mafanikio na bila kukoma, laelekea kuwajumlisha
wanadamu wote pamoja na mema yao yote chini ya Kristo aliye kichwa, katika
umoja wa Roho wake[24].
Kwa nguvu ya ukatoliki (catholicitatis) huu kila sehemu
huvipeleka vipaji vyake yenyewe kwa sehemu nyingine na kwa Kanisa lote, hivi
kwamba sehemu zote pamoja, na kila moja pia, hukithiri kwa kushirikiana
zenyewe kwa zenyewe na kufanya juhudi ili kupata ukamilifu katika umoja.
Tokea hapo yajiri kuwa taifa la Mungu, licha ya kujikusanya kutoka katika
mataifa mbalimbali, ndani yake lenyewe pia linajipanga kwa madaraja
mbalimbali. Kwa maana kati ya viungo vyake kuna utofauti wa kazi, kwani
wengine wanatumikia kwa huduma takatifu kwa ajili ya manufaa ya ndugu zao,
au tena kuna utofauti wa hali na mpango wa maisha, kwani wengi katika hali
ya kitawa wanawachochea ndugu kwa mfano wao wakinuia kuufikia utakatifu kwa
njia nyembamba zaidi. Hivyo katika ushirika wa kikanisa yapo pia kwa halali
Makanisa maalum (Ecclesiae particulares) yashikayo mapokeo yao
yenyewe, bila kuathiri mamlaka kuu ya Kiti cha Petro kinachosimamia ushirika
wote wa mapendo[25], hulinda
tofauti za haki zilizopo, na wakati uleule huangalia ili yaliyo ya pekee
yasidhuru umoja bali yautumikie zaidi. Na hatimaye, kutokana na hayo,
vinakuwepo vifungu vya ushirika wa kindani kati ya sehemu mbalimbali za
Kanisa kuhusu utajiri wa kiroho, wafanyakazi wa kitume na misaada ya
kidunia. Kwa maana viungo vya taifa la Mungu vyaitwa kushirikiana katika
mema, na maneno haya ya Mtume Paulo yahusu pia kila Kanisa, “Kila mmoja kwa
kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana, kama mawakili wema wa
neema mbalimbali za Mungu” (1Pet 4:10).
Hivyo watu wote waitwa kwenye umoja huu wa kikatoliki wa taifa la
Mungu, ambao huashiria na kuhamasisha amani timilifu. Na katika umoja huo
kwa namna mbalimbali huhusianishwa au hukusudiwa kuingia waamini wakatoliki
na hata wengine wamwaminio Kristo, na hatimaye pia watu wote wanaoitwa kwa
neema ya Mungu kupata wokovu.
Waamini wakatoliki
14. Mtaguso huu mtakatifu huwaangalia kwanza waamini wakatoliki.
Ukijitegemeza juu ya Maandiko Matakatifu na Mapokeo, [Mtaguso] hufundisha
kuwa Kanisa hili linalohiji hapa duniani, ni la lazima kwa kupata wokovu.
Maana Kristo peke yake ndiye Mshenga na njia ya wokovu, yeye ambaye yupo
hapa kwa ajili yetu katika mwili wake, ulio Kanisa. Na Yeye mwenyewe
alisisitiza kwa maneno wazi ulazima wa imani na ubatizo (taz. Mk 16:16; Yn
3:5), na papo hapo akathibitisha ulazima pia wa Kanisa, ambamo watu
wanaingia kwa ubatizo kama kwa mlango. Kwa sababu hiyo, hawawezi kuokoka
watu wale ambao, ingawa wanajua ya kwamba Kanisa katoliki limeasisiwa na
Mungu kwa njia ya Yesu Kristo kama la lazima, wanakataa au kuingia ndani ya
Kanisa au kudumu ndani yake.
Basi wanaingizwa kikamilifu katika jumuiya ya Kanisa wale ambao,
wakiwa na Roho wa Kristo, wanakubali muundo wake mzima na njia zote za
wokovu lilizopewa. Tena, katika mpangilio wake uonekanao, wanaunganika na
Kristo – aliongozaye Kanisa kwa njia ya Baba Mtakatifu na Maaskofu – kwa
vifungo vya ungamo la imani, sakramenti, uongozi wa Kanisa na ushirika.
Lakini yule ambaye hadumu katika upendo na akaa ndani ya Kanisa kwa ‘mwili’
na si kwa ‘moyo’, ijapo ameingizwa katika Kanisa, hataokoka[26].
Basi, watoto wote wa Kanisa wakumbuke kuwa hali yao bora hutokana siyo na
mastahili yao, bali na neema ya pekee ya Kristo. Ikiwa hawaiitikii neema
hiyo kwa wazo, kwa neno na kwa tendo, sio tu hawataokoka, bali pia
watahukumiwa kwa ukali zaidi[27].
Wakatekumeni ambao, wakiongozwa na Roho Mtakatifu, wanatamani kwa mapenzi
dhahiri kuingizwa katika Kanisa, waunganishwa nalo kwa tamaa hiyo yenyewe,
naye Mama Kanisa huwakumbatia tayari kama [wana] wake kwa upendo na matunzo.
Kanisa na wakristo wasio wakatoliki
15. Kanisa lajua kwamba limeunganika kwa sababu nyingi na wale
waliobatizwa, ambao wamepewa heshima ya jina la wakristo, ingawa hawakiri
imani iliyo kamili, au hawatunzi umoja wa ushirika chini ya Halifa wa Petro[28].
Kwa maana wapo wengi ambao huyaheshimu Maandiko Matakatifu kama kanuni ya
imani na ya maisha, huonyesha juhudi ya kweli ya kidini, na kumwamini kwa
upendo Mungu Baba Mwenyezi na Kristo aliye Mwana wa Mungu na Mwokozi[29].
Tena walitiwa muhuri wa ubatizo, ambao kwa njia yake wameunganishwa na
Kristo, na zaidi wazikubali sakramenti nyingine pia na kuzipokea katika
Makanisa yao au jumuiya za kikanisa. Wengi miongoni mwao wanao pia Uaskofu,
huadhimisha Ekaristi Takatifu na kuwa na moyo wa ibada kwa ajili ya Bikira
Mama wa Mungu[30]. Aidha kuna
ushirika wa sala na fadhila nyingine za kiroho, na zaidi kuna hali ya umoja
wa kweli katika Roho Mtakatifu, kwa kuwa Roho kwa nguvu yake iletayo
utakatifu hutenda kazi pia ndani yao kwa njia ya vipawa na neema, tena
baadhi yao akawatia nguvu hadi kumwaga damu yao. Hivyo Roho huchochea ndani
ya wanafunzi wa Kristo hamu na matendo ili wote, kadiri ilivyopangwa na
Kristo, wajiunge kwa amani katika kundi moja chini ya mchungaji mmoja[31].
Mama Kanisa hakomi kusali, kutumaini na kutenda ili kupata jambo hilo, tena
huwasihi wanawe wajitakase na kujitengeneza upya, ili ishara ya Kristo
ing’ae wazi zaidi juu ya uso wa Kanisa.
Kanisa na wasio wakristo
16. Hatimaye wale ambao hawajapokea Injili huhusiana na taifa la Mungu
kwa njia mbalimbali[32]. Kwanza
kabisa taifa lile, lililopewa maagano na ahadi, ambalo katika hilo alitoka
Kristo kwa jinsi ya mwili (taz. Rum 9:4-5). Hilo ndilo taifa lililo penzi
kwa ajili ya Mababa zake, kwa habari ya kule kuchaguliwa, kwa sababu karama
za Mungu hazina majuto, wala mwito wake (taz. Rum 11:28-29). Lakini mpango
wa wokovu huwakumbatia pia wanaomtambua Muumba, na kati yao wa kwanza
Waislamu: hao wakiri ya kuwa wanashika imani ya Ibrahimu, na pamoja nasi
wanamwabudu Mungu mmoja, mwenye huruma, atakayewahukumu watu siku ya mwisho.
Naye Mungu mwenyewe hayupo mbali na wengine wanaomtafuta katika vivuli na
sanamu Mungu asiyejulikana, kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na
vitu vyote (taz. Mdo 17:25-28), naye ndiye Mwokozi anayetaka watu wote
waokolewe (taz. 1Tim 2:4). Kwa maana wanaweza kupata wokovu wa milele wale
ambao, bila hatia, hawaifahamu Injili ya Kristo wala Kanisa lake, lakini
hata hivyo wanamtafuta Mungu kwa moyo mnyofu, na kwa mvuto wa neema
wanajitahidi kutimiza kwa matendo yao mapenzi ya Mungu wanayotambua kwa njia
ya sauti ya dhamiri[33].
Maongozi ya Mungu hayakatai kuwapa misaada inayohitajika kwa ajili ya wokovu
wale ambao, bila hatia yao, hawajaufikia ufahamu wazi wa Mungu, nao
wanajitahidi, kwa neema ya Mungu, kuishi maisha manyofu. Kwa maana lolote
lililo jema na la kweli lipatikanalo kati yao, lahesabiwa na Kanisa kuwa
kama matayarisho ya Injili[34],
na limetolewa na Yule amwangazaye kila mtu ili mwishowe apate uzima. Lakini
mara nyingi wanadamu, wakidanganywa na Ibilisi, walipotea katika mawazo yao,
wakaibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakiabudu kiumbe badala ya Muumba
(taz. Rum 1:21 na 25). Au tena wakiishi na kufa pasipo Mungu hapa duniani,
wanaelekea mwishoni kukata tamaa. Kwa hiyo Kanisa, likikumbuka amri ya
Bwana: “Hubirini Injili kwa kila kiumbe” (Mk 16:15), husitawisha kwa
uangalifu mkuu misioni, kwa ajili ya utukufu wa Mungu na wokovu wa watu hawa
wote.
Tabia ya kimisionari ya Kanisa
17. Maana kama Mwana alivyotumwa na Baba, Yeye naye aliwatuma Mitume
(taz. Yn 20:21) akisema, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa
wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na
kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja
nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari” (Mt 28:19-20). Kanisa limepokea
kutoka kwa Mitume amri hii ya Kristo, yenye umuhimu, ya kuuhubiri ukweli wa
wokovu, ili kuitimiza hata mwisho wa dunia (taz. Mdo 1:8). Nalo Kanisa
lashika maneno ya Mtume kana kwamba ni yake lenyewe, “Ole wangu
nisipoihubiri Injili!” (1Kor 9:16), kwa hiyo huendelea kuwatuma wamisionari
bila kukoma mpaka Makanisa mapya (novellae Ecclesiae) yatakapokwisha
wekwa tayari, nayo yenyewe yapate kuendeleza tendo la uinjilishaji. Maana
Kanisa huongozwa na Roho Mtakatifu kushiriki kazi ili kutimiliza azimio la
Mungu aliyemweka Kristo kuwa asili ya wokovu kwa ulimwengu mzima. Kwa njia
ya kuhubiri Injili Kanisa huwavuta wasikilizaji kuipokea na kuikiri imani,
huwaandaa wapate ubatizo na kuwatoa katika utumwa wa upotovu, na kuwafanya
kuwa viungo vya mwili wa Kristo, ili wakue ndani yake katika upendo hata
ukamilifu. Matokeo ya kazi yake ni kwamba wema wowote upatikanao kuwa
umepandwa katika moyo na nia za watu, na katika ibada na tamaduni za
mataifa, zisipotee, bali ziponywe, ziinuliwe na kukamilishwa kwa ajili ya
utukufu wa Mungu, aibu ya Shetani na heri ya mwanadamu. Kila mwanafunzi wa
Kristo, kwa upande wake, huwajibika kuieneza imani[35].
Lakini, ijapo kila mmoja aweza kuwabatiza waaminio, ni juu ya padre tu
kulitimiza jengo la Mwili kwa njia ya sadaka ya Ekaristi, akitekeleza maneno
aliyoyasema Mungu kwa kinywa cha nabii, “Tokea maawio ya jua hata machweo
yake jina langu ni kuu katika mataifa; na katika kila mahali unatolewa
uvumba na dhabihu safi kwa jina langu” (Mal 1:11)[36].
Hivyo Kanisa husali na kutenda kazi pia ili ukamilifu wa ulimwengu wote
uingizwe katika Taifa la Mungu, lililo Mwili wa Bwana na Hekalu la Roho
Mtakatifu. Tena, ili katika Kristo, aliye kichwa cha wote, heshima yote na
utukufu wote vitolewe kwa Muumba na Baba wa ulimwengu.
Sura ya Tatu
MUUNDO WA KIHIERARKIA WA KANISA
NA HASA UASKOFU
Utangulizi
18. Kristo Bwana, kusudi kulichunga na kuzidi kuliongeza Taifa la Mungu,
aliweka katika Kanisa lake huduma mbalimbali, zinazolenga wema wa Mwili
wote. Kwa maana wahudumu, waliopewa uwezo mtakatifu, wanawatumikia ndugu
zao, ili wote walio watu wa Taifa la Mungu, na hivyo wamejaliwa heshima ya
kweli ya kikristo, wakielekea shabaha ileile kwa hiari na kwa utaratibu,
wakaufikie wokovu.
Sinodi hii takatifu hufuata nyayo za Mtaguso Mkuu wa Vatikani wa
I, hufundisha na kutangaza pamoja nao ya kwamba Yesu Kristo, aliye Mchungaji
wa milele, alijenga Kanisa takatifu, akawatuma Mitume kama Yeye mwenyewe
alivyotumwa na Baba (taz. Yn 20:21), tena akataka waandamizi wao, yaani
Maaskofu, wawe wachungaji wa Kanisa lake hata ukamilifu wa nyakati. Kusudi
Uaskofu wenyewe uwe mmoja na usiogawanyika, akamweka Mt. Petro juu ya Mitume
wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi udumuo na uonekanao wa umoja
wa imani na wa ushirika[37].
Mtaguso Mtakatifu huwatolea tena waamini wote fundisho hilo la uanzishaji,
udumifu, nguvu na tabia ya mamlaka tukufu ya Papa na ya Majisterio yake
isiyoweza kukosa, ili liaminike kwa uthabiti. Tena, katika kuendelea kwa
njia hiyohiyo, linaamua kukiri na kutangaza mbele ya wote fundisho juu ya
Maaskofu walio waandamizi wa Mitume, ambao pamoja na mwandamizi wa Petro,
aliye Wakili wa Kristo[38] na
kichwa kionekanacho cha Kanisa zima, waiongoza nyumba ya Mungu aliye hai.
Kuitwa na kuwekwa kwa Thenashara
19. Bwana Yesu, baada ya kumwomba Baba, aliwaita aliowataka mwenyewe,
akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume
kuhubiri ufalme wa Mungu (taz. Mk 3:13-19; Mt 10:1-42). Na Mitume hawa (taz.
Lk 6:13) akawaweka wawe kama urika (ad modum collegii) au kundi la
kudumu (coetus stabilis), ambalo kiongozi wake alimweka Petro,
aliyemteua miongoni mwao (taz. Yn 21:15-17). Akawatuma kwanza kwa wana wa
Israeli, kisha kwa mataifa yote (taz. Rum 1:16), ili, wakishiriki katika
uwezo wake Yesu, wawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wake, wawatakatifuze
na kuwaongoza (taz. Mt 28:16-20; Mk 16:15; Lk 24:45-48; Yn 20:21-23), na
hivyo walieneze Kanisa na kulichunga wakihudumia chini ya uongozi wa Bwana,
siku zote hata ukamilifu wa dahari (taz. Mt 28:20). Nao walithibitishwa
kikamilifu katika utume huo siku ya Pentekoste (taz. Mdo 2:1-36) kadiri ya
ahadi ya Bwana, “Mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu;
nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na
Samaria, na hata mwisho wa nchi” (Mdo 1:8). Aidha Mitume, wakihubiri
kotekote Injili (taz. Mk 16:20), ipokelewayo na wasikilizaji kwa kazi ya
Roho Mtakatifu, hulikusanya Kanisa lote ulimwenguni, ambalo Bwana aliasisi
juu ya msingi wa Mitume na kulijenga juu ya Mt. Petro, kiongozi wao, naye
Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni (taz. Ufu 21:14; Mt 16:18; Efe
2:20)[39].
Maaskofu ni waandamizi wa mitume
20. Utume ule wa kimungu, uliokabidhiwa na Kristo kwa Mitume,
utadumu hata mwisho wa nyakati (taz. Mt 28:20), maadamu Injili wanayopaswa
kuipeleka (tradendum) ni, kwa ajili ya Kanisa, asili ya maisha yake
sikuzote. Kwa sababu hiyo Mitume, katika jamii hii iliyopangwa kihierarkia,
walijitahidi kuwaweka waandamizi.
Kwa maana, licha ya kuwa na wasaidizi katika huduma yao[40],
waliwaachia wasaidizi wao wa karibu zaidi, kama wosia, wajibu wa kulitimiza
na kuimarisha tendo lililoanzishwa nao[41],
ili utume uliokabidhiwa kwao uendelezwe baada ya kifo chao. Wakasisitiza
walitunze kundi lote, ambalo Roho Mtakatifu aliwaweka ndani yake wapate
kulilisha Kanisa lake Mungu (taz. Mdo 20:28). Basi, wakawaweka watu hawa na
baadaye wakaagiza kwamba watu wengine wenye kukubaliwa wapokee huduma yao
baada ya kufa kwao[42]. Kati ya
huduma mbalimbali zinazotekelezwa katika Kanisa tangu siku za kwanza, kama
vile Mapokeo yashuhudiavyo, inashika nafasi ya kwanza kazi ya wale
waliowekwa katika Daraja ya Uaskofu, ambao, kwa uandamizi unaoendelea tangu
awali[43], wanayo matawi ya
shina la Mitume[44]. Hivyo
basi, Mt. Ireneus ashuhudiavyo, Mapokeo ya kitume hujidhihirisha[45]
na kutunzwa[46] ulimwenguni
mwote kwa njia ya wale waliosimikwa na Mitume kuwa Maaskofu na kwa njia ya
waandamizi wao mpaka sasa.
Basi, Maaskofu wamekabidhiwa huduma ya jumuiya pamoja na msaada wa
Mapadre na mashemasi[47],
wakiliongoza kundi lake kwa niaba ya Mungu[48],
ambalo wao ni wachungaji wake, wakiwa kama walimu wa mafundisho, makuhani wa
ibada takatifu, wahudumu wa uongozi[49].
Aidha, kama vile udumuvyo wajibu uliokabidhiwa na Bwana kwa Petro tu, mkuu
wa Mitume, unaotakiwa kupitishwa kwa waandamizi wake, vivyo hivyo hudumu
wajibu wa Mitume wa kulichunga Kanisa, ambao inabidi utimizwe bila katizo na
Daraja takatifu ya Maaskofu[50].
Kwa hiyo Mtaguso Mkuu mtakatifu hufundisha kwamba Maaskofu waliwekwa mahali
pa Mitume kwa amri ya kimungu[51],
ili wawe wachungaji wa Kanisa, ambao awasikilizaye wao amsikiliza Kristo,
naye awakataaye wao amkataa Kristo na yule aliyemtuma Kristo (taz. Lk 10:16)[52].
Hali ya kisakramenti ya Uaskofu
21. Basi, katika nafsi za Maaskofu, wanaosaidiwa na mapadre, yupo
katikati ya waamini Bwana Yesu Kristo, aliye Kuhani Mkuu. Maana wakati
anapoketi kuume kwa Mungu Baba, haiachi jumuiya ya makuhani wake wakuu[53],
bali kwanza kwa njia ya huduma yao mashuhuri huyatangazia mataifa yote neno
la Mungu na kuwapa waamini sakramenti za imani bila kikomo. Tena kwa
uangalifu wao wa kibaba (taz. 1Kor 4:15) huviunganisha viungo vipya na Mwili
wake kwa kuvizaa upya kutoka juu. Mwishowe kwa hekima na busara yao
hulielekeza na kuliongoza taifa la agano jipya katika safari yake ya
kuelekea uheri wa milele. Wachungaji hawa, walioteuliwa ili kulichunga kundi
la Bwana, ndio watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu (taz. 1Kor
4:1); nao walikabidhiwa huduma ya kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu
(taz. Rum 15:16; Mdo 20:24), na huduma ya Roho na ya haki katika utukufu
(taz. 2Kor 3:8-9).
Kusudi wapate kutimiza kazi hizo kubwa namna hiyo, Mitume
walitajirishwa na Kristo kwa mmiminiko wa pekee wa Roho Mtakatifu
aliyewajilia (taz. Mdo 1:8; 2:4; Yn 20:22-23); nao wenyewe kwa kuwekea
mikono yao waliwapa wasaidizi wao kipaji hicho cha Roho (taz. 1Tim 4:14;
2Tim 1:6-7), ambacho ndicho kimepitishwa mpaka kwetu kwa njia ya kuwekwa
wakfu kwa Maaskofu[54]. Mtaguso
mtakatifu unafundisha kwamba kwa kuwekwa wakfu kwa Maaskofu hujaliwa
ukamilifu wa sakramenti ya upadre, yaani ukamilifu ule ambao, katika mapokeo
ya kiliturujia ya Kanisa, na katika lugha ya Mababa wa Kanisa, huitwa
ukuhani mkuu, ulio kilele cha huduma takatifu[55].
Uwakfu wa Maaskofu hukabidhi pia, pamoja na jukumu la kutakatifuza, majukumu
ya kufundisha na ya kuongoza, ambayo lakini, kwa maumbile yake, yaweza
kutekelezwa tu katika ushirika wa kihierarkia na kichwa na viungo vingine
vya urika [huo]. Kwa maana kutokana na mapokeo, yajidhihirishavyo hasa
katika ibada za kiliturujia na desturi za Kanisa la Mashariki na la
Magharibi, huonekana wazi kwamba, kwa njia ya kuwekea mikono na kutaja
maneno ya uwakfu, hujaliwa neema ya Roho Mtakatifu[56]
na kutiwa muhuri (characterem) takatifu[57],
kiasi kwamba Maaskofu, kwa namna bora na dhahiri, wanashika nafasi ya Kristo
mwenyewe aliye Mwalimu, Mchungaji na Kuhani mkuu, na kutenda katika nafsi
yake (in Eius persona)[58].
Tena ni juu ya Maaskofu, kwa njia ya sakramenti ya Daraja takatifu,
kuwaingiza wateuliwa wapya katika umoja wa Maaskofu.
Urika wa Maaskofu na mkuu wake
22. Kama vile Mt. Petro na wale Mitume wengine wameunganika, kwa
agizo la Bwana, katika urika mmoja tu wa kitume, kwa jinsi iliyo sawa (pari
ratione), Baba Mtakatifu aliye mwandamizi wa Petro, na Maaskofu walio
waandamizi wa Mitume, wanaungana pamoja. [Yapo mambo mawili] yaonyeshayo
tabia na maumbile ya kiurika ya Daraja ya uaskofu: yaani nidhamu ya kale,
ambayo kufuatana nayo Maaskofu wa ulimwengu mzima walishirikiana wao kwa wao
na pamoja na Askofu wa Roma, katika kifungo cha umoja, upendo na amani[59];
na vilevile kukusanyika kwa Mitaguso[60]
ili kuamua pamoja masuala yaliyo muhimu[61],
baada ya kutia maanani na kuchunguza maoni ya wengi[62].
Tena Mitaguso ya Kanisa iadhimishwayo katika mfululizo huthibitisha kwa
udhahiri maumbile hayo, ambayo imekwisha kudokezwa pia na desturi iliyopo
tangu zamani ya kuwashirikisha Maaskofu wengi katika kumwinua mteuliwa mpya
kwenye Daraja ya ukuhani mkuu. Basi, mmoja hufanywa mshiriki wa Umoja wa
Maaskofu kwa nguvu ya uwakfu wa kisakramenti (vi sacramentalis
consecrationis) na kwa ushirika wa kihierarkia (hierarchica
communione) pamoja na Kichwa cha Urika [huo] (Collegii Capite) na
viungo vyake.
Urika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba
Mtakatifu, aliye mwandamizi wa Petro, naye ndiye kichwa chake, ambaye
mamlaka ya ukuu wake hudumu kabisa juu ya wote, wachungaji kwa waamini. Kwa
maana Baba Mtakatifu, kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na
Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu
kabisa na iwahusuyo wote (plenam, supremam et universalem potestatem),
ambayo anaweza kuyatimiza kwa uhuru. Urika wa Maaskofu (Ordo Episcoporum)
ni urithi wa urika wa Mitume katika kufundisha na katika uongozi wa
kichungaji; na ndani yake umoja wa Mitume huendelezwa katika nyakati. [Urika
huo wa Maaskofu] pamoja na Kichwa chake aliye Baba Mtakatifu, na kamwe
pasipo yeye, una mamlaka ya juu kabisa na kamili juu ya Kanisa lote[63].
[Mamlaka hiyo] yaweza kutekelezwa tu kwa idhini ya Baba Mtakatifu. Bwana
alimweka Simoni Petro tu kuwa mwamba na mshika ufunguo wa Kanisa (taz. Mt
16:18-19), akamweka kuwa Mchungaji wa kundi lake zima (taz. Yn 21:15nk);
lakini wadhifa wa kufunga na kufungua aliopewa Petro (taz. Mt 16:19),
ulikabidhiwa pia kwa Urika wa Mitume uliounganika na mkuu wake (taz. Mt
18:18; 28:16-20)[64]. Urika huo
maadamu umeundwa na wengi, huonyesha hali ya Taifa la Mungu ya kuwa la namna
nyingi na la ulimwengu mzima; maadamu ulikusanyika chini ya kiongozi mmoja
tu, huonyesha umoja wa kundi la Kristo. Ndani yake Maaskofu, wakiheshimu kwa
uaminifu mamlaka na ukuu wa mkuu wao, hutumia mamlaka yao wenyewe kwa ajili
ya mema ya waamini wao, na zaidi, ya Kanisa zima, ambalo Roho Mtakatifu
huzidi kuimarisha muundo wake wenye utaratibu na upatano wake. Mamlaka kuu
juu ya Kanisa lote uliyopewa Urika huo wa Maaskofu hutekelezwa kwa jinsi
iliyo rasmi katika Mitaguso Mikuu. Hakuna Mtaguso Mkuu usipothibitishwa au
walau kukubaliwa na mwandamizi wa Petro; tena ni haki ya Kuhani Mkuu wa Roma
kuiitisha Mitaguso hii, kuiongoza na kuiidhinisha[65].
Mamlaka hiyohiyo ya Urika [wa Maaskofu] yaweza kutekelezwa na Maaskofu
walioko pande zote za dunia wakishirikiana na Baba Mtakatifu, ilimradi mkuu
wa Urika awe amewaita kutenda kiurika, au walau aidhinishe au kukubali kwa
hiari tendo la pamoja la Maaskofu waliotawanyika, ili lipate kuwa kweli
tendo la kiurika (actus collegialis).
Mahusiano ya Maaskofu ndani ya urika wao
23. Umoja wa kiurika huonekana pia katika mahusiano ya kila Askofu na
Makanisa faridi na Kanisa lote zima. Kuhani Mkuu wa Roma, kama mwandamizi wa
Petro, ni chanzo na msingi udumuo na uonekanao wa umoja wa Maaskofu na wa
kundi la waamini[66]. Maaskofu,
kila mmoja peke yake, ni chanzo na msingi uonekanao wa umoja katika Makanisa
yao faridi[67], yaliyowekwa kwa
mfano wa Kanisa lote zima, na katika hayo na kutokana na hayo lipo Kanisa
katoliki lililo moja na pekee[68].
Kwa sababu hiyo kila Askofu huwakilisha Kanisa lake mwenyewe, na Maaskofu
wote pamoja na Baba Mtakatifu, huwakilisha Kanisa lote katika kifungo cha
amani, upendo na umoja.
Maaskofu wote, kila mmoja wao, waliowekwa juu ya Makanisa faridi, wanatumia
madaraka yao ya kichungaji juu ya sehemu ya taifa la Mungu waliyokabidhiwa,
si juu ya Makanisa mengine wala juu ya Kanisa zima. Lakini Maaskofu, maadamu
ni viungo vya Umoja wa Maaskofu na waandamizi halali wa Mitume, kwa mpango
na agizo la Kristo, wanapaswa, kila mmoja, kulishughulikia Kanisa lote[69].
Shughuli hiyo, ijapo haitekelezwi kwa mamlaka ya kisheria, lakini huchangia
sana katika kuleta manufaa ya Kanisa zima. Kwa maana Maaskofu wote
huwajibika kukuza na kuhifadhi umoja wa imani na nidhamu iliyo moja kwa
Kanisa lote; tena huwafundisha waamini wawe na upendo kwa Mwili wote wa
fumbo wa Kristo, hasa kwa viungo vilivyo maskini, vyenye kuteswa na kuudhiwa
kwa ajili ya haki (taz. Mt 5:10). Mwishowe huwajibika kuendeleza utendaji
wowote unaohusu Kanisa lote, hasa kusudi imani ipate kukua na mwanga wa
ukweli kamili uwazukie watu wote. Aidha, ni kweli kwamba [Maaskofu],
wakiongoza vizuri kila mmoja Kanisa lake kama sehemu ya Kanisa zima,
wanachangia kwa manufaa ustawi wa Mwili wote wa fumbo, ambao ni mwili
unaofanywa na Makanisa pia[70].
Juhudi ya kutangaza Injili popote duniani ni juu ya Umoja wa Wachungaji,
ambao Kristo aliwapa amri wote kwa pamoja, akiweka wajibu ulio wa pamoja,
kama vile Baba Mtakatifu Selestino alivyowasisitizia Mababa wa Mtaguso wa
Efeso[71]. Hivyo Maaskofu, kila
mmoja kwa upande wake, kwa kadiri utekelezaji wa wajibu wao wa pekee
uwawezeshavyo, wanapaswa kushirikiana katika kazi wao kwa wao na pamoja na
Halifa wa Petro, ambaye alikabidhiwa kwa namna ya pekee jukumu kuu la
kueneza jina la Kristo[72]. Kwa
hiyo inabidi [Maaskofu] watoe watenda kazi wa mavuno na pia misaada ya
kiroho na ya kimwili, kwa nguvu zao zote kwa ajili ya misioni, au moja kwa
moja wao wenyewe, au katika kuuchochea ushirikiano wenye bidii wa waamini.
Hatimaye Maaskofu, wakifuata mfano mstahiki wa zamani, katika ushirika wa
upendo usio na mipaka, watoe kwa moyo msaada wa kidugu kwa Makanisa mengine,
hasa yale yaliyo jirani zaidi au maskini zaidi.
Kwa Maongozi ya Mungu imetokea kwamba baadhi ya Makanisa
yaliyoasisiwa mahali mbalimbali na Mitume na waandamizi wao, katika mwenendo
wa karne yalijiweka katika makundi mengi yenye kuunganika kwa utaratibu.
Makundi hayo, wakati unapohifadhiwa umoja wa imani na muundo pekee wa
kimungu wa Kanisa zima, yanatumia nidhamu, mazoea ya kiliturujia na urithi
wa kiteolojia na wa kiroho yao yenyewe. Baadhi yao, hasa Makanisa ya zamani
ya kipatriarka, kama mama katika imani, yamezaa mengine yaliyo kama binti
zao, nayo hufungamana mpaka siku ya leo kwa kifungo cha upendo katika maisha
ya kisakramenti na kwa kuheshimiana katika haki zao na wajibu zao[73].
Utofauti huo wa Makanisa mahalia yaliyo na umoja kati yao waonyesha kwa
udhahiri zaidi ukatoliki wa Kanisa lisilogawanyika. Vivyo hivyo Mabaraza ya
Maaskofu siku hizi yanaweza kusaidia kwa njia nyingi na zenye kuzaa matunda,
ili roho ya umoja ipate kuwa na matokeo yaonekanayo.
Huduma ya Maaskofu
24. Maaskofu, kwa kuwa ni waandamizi wa Mitume, wakabidhiwa na Bwana,
aliyepewa mamlaka yote mbinguni na duniani, utume wa kuyafundisha mataifa
yote na kuihubiri Injili kwa kila kiumbe, ili watu wote wapate wokovu kwa
njia ya imani, ubatizo na kuzishika amri (taz. Mt 28:18-20; Mk 16:15-16; Mdo
26:17nk). Ili wapate kuutimiza utume huo Kristo Bwana aliwaahidia Mitume
Roho Mtakatifu, na siku ya Pentekoste alimtuma kutoka mbinguni, ili kwa
nguvu ya Roho huyo wapate kuwa mashahidi wake mpaka mwisho wa dunia, mbele
ya mataifa, jamii za watu na wafalme (taz. Mdo 1:8; 2:1nk; 9:15). Wajibu huo
Bwana alioukabidhi kwa wachungaji wa taifa lake ni utumishi wa kweli, ambao
katika Maandiko Matakatifu huitwa kwa neno lenye maana “diakonia” au huduma
(taz. Mdo 1:17 na 25; 21:19; Rum 11:13; 1Tim 1:12).
Utume wa kikanisa (missio canonica) wa Maaskofu waweza
kufanyika kadiri ya desturi halali, zisizokanushwa na mamlaka ya juu kabisa
ya Kanisa yanayolihusu Kanisa lote zima, au kwa sheria ziwekwazo au
kukubaliwa na mwenye mamlaka hiyohiyo, au moja kwa moja na Halifa wa Petro
mwenyewe. Ikiwa huyo anapinga au anakataa ushirika wa kitume, Maaskofu
hawawezi kukubaliwa kwenye madaraka[74].
Jukumu la kufundisha
25. Kati ya majukumu ya Maaskofu yaliyo muhimu zaidi, kuhubiri Injili
hushika nafasi ya kwanza[75].
Maana Maaskofu ndio watangazaji wa imani wawaletao wanafunzi wapya kwa
Kristo, na walimu halisi waliojaliwa mamlaka ya Kristo, ambao wanawahubiria
watu waliokabidhiwa kwao imani. Imani hiyo inawapasa kuishika na kuiishi
katika mwenendo wao. Tena, wanaieleza imani hiyo katika mwanga wa Roho
Mtakatifu, wakitoa katika hazina ya Ufunuo vitu vipya na vya kale (taz. Mt
13:52), wakaufanya uzae matunda na wanalichunga kundi lao ili kufukuza
makosa yanayolihatarisha (taz. 2Tim 4:1-4). Maaskofu wanaofundisha katika
ushirika na Baba Mtakatifu, lazima waheshimiwe na wote kama mashahidi wa
ukweli ulio wa kimungu na wa kikatoliki; aidha, waamini wapaswa kuukubali
uamuzi wa Askofu wao, utolewao kwa jina la Kristo kuhusu imani na maadili,
na kuambatana nao kwa roho ya utii wa kidini. Lakini utii huo wa kidini ulio
wa utashi na wa akili inabidi wautoe kwa namna ya pekee kwa Majisterio
halisi ya Baba Mtakatifu, hata wakati asiposema “ex cathedra”, ili
Majisterio yake kuu ikubalike kwa heshima, na hukumu zitolewazo naye
zipokelewe kwa moyo wa dhati, kadiri anavyojulisha nia na mapenzi yake,
ambayo yanaonekana hasa kwa tabia ya hati, au kwa kurudiwa mara nyingi
mafundisho yaleyale, au kwa namna ya kusema kwake.
Ingawa kila Askofu peke yake hana fadhila ya kutokosea (infallibilitas),
lakini Maaskofu hutangaza fundisho la Kristo bila kukosa[76]
pale ambapo, ijapo wametawanyika ulimwenguni, watunza kifungo cha ushirika
kati yao na pamoja na Halifa wa Petro, katika mafundisho yao halisi kuhusu
mambo ya imani na maadili, wanakubaliana juu ya fundisho (sententia)
linalotakiwa kulipokea kama la kweli na la mwisho. Jambo hilo ni dhahiri
zaidi wanapokusanyika katika Mtaguso Mkuu, nao ni walimu na waamuzi wa imani
na maadili kwa ajili ya Kanisa lote, na maamuzimkataa (definitionibus)
yao yapaswa yashikwe kwa utii na imani[77].
[Fadhila hii ya] kutokosea ambayo Mkombozi aliye Mungu alitaka Kanisa
lake lijaliwe kila linapoamua kuhusu mafundisho ya imani na maadili, inaenea
kadiri ya amana (depositum) ya Ufunuo wa Mungu ieneavyo, ambayo
lazima itunzwe kwa uchaji na kuelezwa kwa uaminifu. Baba Mtakatifu wa Roma,
aliye kichwa cha Urika wa Maaskofu, hujaliwa fadhila hiyo ya kutokosea, kwa
nguvu ya wadhifa wake, wakati anapotangaza kwa mkataa (definitivo actu)
fundisho kuhusu imani au maadili[78],
hali akiwa mchungaji mkuu na mwalimu wa waamini wote, anayewaimarisha ndugu
zake katika imani (taz. Lk 22:32). Kwa hiyo maamuzimkataa (definitiones)
yake huitwa kwa haki [maamuzi] yasiyokosoleka (irreformabiles) kwa
tabia yake yenyewe na siyo kwa kibali cha Kanisa, kwa kuwa yametangazwa kwa
msaada wa Roho Mtakatifu, ulioahidiwa kwake katika nafsi ya Mtakatifu Petro.
Kwa hiyo [maamuzi yake] hayahitaji idhini yoyote ya wengine wala haiwezekani
kukata rufaa kwa baraza jingine. Kwa maana hapo Baba Mtakatifu hatoi hukumu
zake kama mtu binafsi, bali anaeleza au kulinda mafundisho ya imani katoliki[79]
kama mwalimu mkuu wa Kanisa zima aliyejaliwa katika nafsi yake karama ya
kutokosea iliyo ya Kanisa lenyewe. [Karama hii ya] kutokosea iliyoahidiwa
kwa Kanisa imo pia katika Umoja wa Maaskofu unapotekeleza Majisterio kuu
pamoja na Halifa wa Petro. Ukubali wa Kanisa hauwezi kukosekana kwa
maamuzimkataa haya kwa sababu ya tendo la Roho Mtakatifu mwenyewe lenye
kutunza na kuendeleza kundi lote la Kristo katika umoja wa imani[80].
Baba Mtakatifu wa Roma na Umoja wa Maaskofu pamoja naye
wanapoelezea fundisho fulani, wanalitoa kadiri ya Ufunuo wenyewe, ambao wote
wanatakiwa kuukubali na kuufuata. Ufunuo huo, kwa njia ya Maandiko
[Matakatifu] au ya Mapokeo hurithishwa kikamilifu na uandamizi halali wa
Maaskofu (per legitimam Episcoporum successionem), na kwanza na
uangalizi wa Baba Mtakatifu mwenyewe, tena hutunzwa kitakatifu na kuelezwa
kiaminifu katika Kanisa kwa mwanga wa Roho wa ukweli[81].
Baba Mtakatifu na Maaskofu, kwa sababu ya wadhifa wao na umuhimu wa jambo
lenyewe, wanajitahidi kwa bidii na kwa njia zifaazo, ili kuuchunguza Ufunuo
huo barabara na kuueleza inavyofaa[82];
ila hawapati ufunuo mpya wa hadhara kana kwamba unaihusu amana ya kimungu ya
imani[83].
Jukumu la kutakatifuza
26. Askofu, aliyepewa ukamilifu wa sakramenti ya Daraja takatifu, ndiye
“wakili wa neema ya ukuhani mkuu”[84],
hasa katika Ekaristi anayotolea mwenyewe au kuagiza itolewe[85],
na kwa njia ya hiyo Kanisa daima huishi na kukua. Kanisa hilo la Kristo limo
kweli ndani ya jumuiya za mahali za waamini zilizo halali, ambazo,
zikiunganika na wachungaji wao, zaitwa nazo pia, katika Agano Jipya,
Makanisa[86]. Maana hayo,
katika mahali pao, ndilo Taifa jipya lililoitwa na Mungu katika Roho
Mtakatifu na uthibitifu mwingi (taz. 1The 1:5). Ndani yao kwa njia ya
kuhubiri Injili ya Kristo waamini wanakusanywa, na fumbo la Karamu ya Bwana laadhimishwa, “ili kwa mwili na damu ya Bwana udugu wa Mwili wote
ufungamanishwe”[87]. Katika
kila jumuiya inayoshiriki altare, chini ya huduma takatifu ya Askofu[88],
hutolewa ishara ya mapendo yale na “umoja ule wa Mwili wa fumbo, ambao
pasipo huo, haiwezekani kuwepo wokovu”[89].
Katika jumuiya hizo, ingawa mara nyingi ni ndogo na maskini, au
zimetawanyika kama uamishoni, yumo Kristo, ambaye kwa nguvu zake, Kanisa
lililo moja, takatifu, katoliki na la Mitume launganishwa[90].
Kwa maana, “ushirika wa mwili na damu ya Kristo haufanyi lolote jingine
zaidi ya kwamba sisi tunageuzwa kuwa kile tunachopokea”[91].
Aidha, kila adhimisho halali la Ekaristi lasimamiwa na Askofu anayekabidhiwa
wajibu wa kumtolea Mungu Mtukufu ibada ya dini ya kikristo na kuipanga
kadiri ya amri za Bwana na sheria za Kanisa, zinazoainishwa zaidi, kwa
habari ya Jimbo lake, na uamuzi wake mwenyewe.
Hivyo Maaskofu, kwa njia ya sala na kazi kwa ajili ya watu, wamimina
ukamilifu wa utakatifu wa Kristo kwa namna mbalimbali na kwa wingi. Kwa
huduma ya Neno wawashirikisha waaminio uweza wa Mungu uuletao wokovu (taz.
Rum 1:16), na kwa njia ya sakramenti, ambazo kwa mamlaka yao wanapanga
utoaji wake wenye utaratibu na matunda[92],
wawatakatifuza waamini. Wao wenyewe wasimamia utoaji wa ubatizo, ambao kwao
unajaliwa ushirika katika ukuhani wa kifalme wa Kristo. Nao ni wahudumu
halisi (ministri originarii) wa kipaimara, watoaji wa Daraja
takatifu, wapangao utaratibu wa nidhamu ya kitubio, na kwa juhudi wawaonya
na kuwafundisha watu wao ili washike nafasi zao kwa imani na uchaji katika
Liturujia na hasa katika sadaka takatifu ya Misa. Mwisho inawapasa
kuwasaidia kwa mfano wa mtindo wa maisha yao wale wanaowasimamia,
wakiiepusha mienendo yao na mabaya, na kuigeuza kuwa mizuri, iwezekanavyo
kwa msaada wa Mungu, ili wachungaji wapate kuufikia uzima wa milele, pamoja
na kundi lililokabidhiwa kwao[93].
Jukumu la kuongoza
27. Maaskofu huyaongoza Makanisa faridi waliyokabidhiwa kama mawakili na
wajumbe wa Kristo[94], kwa
mashauri, maonyo na mifano, na pia kwa mamlaka na uwezo mtakatifu, ambao
lakini hawautumii ila kwa kulijenga kundi lao katika ukweli na utakatifu,
wakikumbuka kuwa aliye mkubwa na awe kama aliye mdogo, na mwenye kuongoza
kama yule atumikaye (taz. Lk 22:26-27). Uwezo huo, wanaotumia wenyewe kwa
jina la Kristo, ni halisi, wa kawaida na wa kujitegemea, ingawa mwishowe
utekelezaji wake waongozwa na mamlaka kuu ya Kanisa, na waweza kutiwa mipaka
fulani kwa ajili ya manufaa ya Kanisa au ya waamini. Kwa nguvu ya uwezo huu
Maaskofu wanayo haki takatifu na wajibu mbele ya Mungu wa kutoa sheria na
hukumu kwa waliowekwa chini yao, na wa kusimamia yale yahusuyo utaratibu wa
ibada na wa utume.
Nao wanakabidhiwa kwa ukamilifu huduma ya kichungaji, yaani utunzaji wa
kundi lao wa daima na wa kila siku, wala wasihesabiwe kuwa mawakili wa
Mababa Watakatifu wa Roma, kwa sababu wanatumia uwezo ulio wao wenyewe na
huitwa kweli wasimamizi wa watu wanaowaongoza[95].
Mamlaka yao hayaondolewi na mamlaka kuu ya Kanisa zima, bali, kinyume chake,
huthibitishwa, huimarishwa na hulindwa nayo[96],
kwa maana Roho Mtakatifu hutunza bila hitilafu muundo wa uongozi uliowekwa
na Kristo Bwana katika Kanisa lake.
Askofu, aliyetumwa na Baba wa nyumba kuiongoza familia yake, aweke mbele
ya macho mfano wa Mchungaji Mwema asiyekuja kutumikiwa, bali kutumika (taz.
Mt 20:28; Mk 10:45) na kuutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo (taz. Yn 10:11).
Yeye, aliyetwaliwa katika wanadamu na kuwa katika hali ya udhaifu, aweza
kuwachukulia wasiojua na wenye kupotea (taz. Ebr 5:1-2). Asikatae
kuwasikiliza walio chini yake anaowatunza kama watoto wake wa kweli na
kuwaonya wamsaidie kwa bidii. Kwa vile atatoa hesabu kwa Mungu kwa ajili ya
roho zao (taz. Ebr 13:17), afanye juhudi kwa ajili yao, kwa sala, mahubiri,
na matendo yote ya mapendo, pia kwa ajili ya wale wasio bado wa kundi lile
moja, ambao awaone kama watu waliokabidhiwa kwake katika Bwana. Naye, kwa
kuwa huwiwa na wote, kama Mtume Paulo awe tayari kuihubiri Injili kwa wote
(taz. Rum 1:14-15) na kuwahimiza waamini wake wawe na utendaji wa kitume na
wa kimisioni. Na waamini kwa upande wao yawapasa kuambatana na Askofu kama
Kanisa na Yesu Kristo, na kama Yesu Kristo na Mungu Baba, ili yote
yaunganishwe katika umoja[97]
na kuzidi kwa wingi kwa ajili ya utukufu wa Mungu (taz. 2Kor 4:15).
Mapadre: mahusiano yao na Kristo, na Maaskofu, na umoja wa mapadre na
Taifa la kikristo
28. Kristo, ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni (taz. Yn 10:36),
kwa njia ya Mitume wake aliwashirikisha katika uwakfu na utume wake
waandamizi wao, yaani Maaskofu[98],
ambao waliwakabidhi kihalali watu wengine katika Kanisa wadhifa wa huduma
yao kwa daraja mbalimbali. Hivyo huduma ya kikanisa iliyoasisiwa na Mungu
hutekelezwa katika daraja mbalimbali na wale waitwao tangu zamani Maaskofu,
Mapadre, Mashemasi[99].
Mapadre, ingawa hawana kilele cha ukuhani, na katika kutumia uwezo wao wapo
chini ya Maaskofu, lakini waunganika nao katika heshima ya kikuhani[100],
na kwa nguvu ya Daraja takatifu[101],
kwa mfano wa Kristo aliye Kuhani mkuu na wa milele (taz. Ebr 5:1-10; 7:24;
9:11-28), wawekwa wakfu, kama makuhani wa kweli wa Agano Jipya, kwa ajili ya
kuihubiri Injili, kuwachunga waamini na kuadhimisha ibada kwa Mungu[102].
Wakishiriki kazi ya Mpatanishi, aliye mmoja, Kristo (taz. 1Tim 2:5), katika
daraja ya huduma yao, wawahubiria wote Neno la Mungu. Nao hutekeleza jukumu
lao tukufu hasa katika ibada au kusanyiko la Ekaristi, ambapo wakitenda
katika nafsi ya Kristo[103],
na kulitangaza fumbo lake, huunganisha matoleo ya waamini na sadaka ya
Kichwa chao, na katika sadaka ya Misa huidhihirisha na kuitekeleza[104],
hata Bwana ajapo (taz. 1Kor 11:26), sadaka ile ya Agano Jipya iliyo moja,
yaani sadaka ya Kristo, aliyejitoa nafsi yake mara moja tu kwa Mungu Baba
kuwa sadaka isiyo na mawaa (taz. Ebr 9:11-28). Tena, kwa ajili ya waamini
watubu au wagonjwa, hutimiza kwa nguvu yote huduma ya upatanisho na faraja,
na kumtolea Mungu Baba mahitaji na sala za waamini (taz. Ebr 5:1-4).
Wakiitekeleza huduma ya Kristo aliye Mchungaji na Kichwa, kwa kadiri ya
mamlaka yao[105], huikusanya
familia ya Mungu kama jumuiya ya ndugu iliyopenywa na roho ya umoja[106],
na kwa njia ya Kristo katika Roho huiongoza kwa Mungu Baba. Katikati ya
kundi lao humwabudu katika roho na kweli (taz. Yn 4:24). Hatimaye
hujitaabisha kwa kuhutubu na kufundisha (taz. 1Tim 5:17), wakisadiki
waliyoyasoma na kuyatafakari katika sheria ya Bwana, wakifundisha
waliyosadiki na kuyafuata waliyofundisha[107].
Mapadre, washiriki wenye busara wa Daraja ya Uaskofu[108],
na msaada na chombo chake, waitwao kutumikia taifa la Mungu, wanakuwa umoja,
au presbiterio (presbyterium), pamoja na Askofu wao[109],
ijapokuwa umoja huu una wadhifa mbalimbali. Katika kila jumuiya ya waamini
ya mahali [mapadre hao] wanafanya kwa namna fulani awepo Askofu, ambaye
wanashirikiana naye kwa roho pana na yenye tumaini, na wanashika, kwa kiasi
fulani, majukumu yake na uangalizi wake na kuzitekeleza kwa juhudi za kila
siku. Nao, chini ya mamlaka ya Askofu, hutakatifuza na kuongoza fungu la
kundi la Bwana walilokabidhiwa, hulifanya Kanisa lote zima lionekane wazi
mahali pao na kutenda kazi ifaayo hata Mwili mzima wa Kristo ujengwe (taz.
Efe 4:12). Wakiangalia daima mema ya wana wa Mungu wajitahidi kuchangia
matendo yao katika kazi ya uchungaji ya Jimbo zima, na zaidi, ya Kanisa
lote. Kwa sababu ya ushirikiano huo katika ukuhani na utume, Mapadre wamkiri
kweli Askofu kama baba yao na kumtii kwa heshima. Na Askofu awahesabu
Mapadre, walio wasaidizi wake, kama wana na rafiki, kama vile Kristo
anavyowaita wanafunzi wake si tena watumwa, bali rafiki (taz. Yn 15:15). Kwa
sababu ya Daraja yao na huduma yao Mapadre wote wa kijimbo na wa kitawa,
washirikishwa katika umoja wa Maaskofu, na kadiri ya wito wao na neema
waliyopewa, wahudumia mema ya Kanisa zima.
Kwa nguvu ya upadirisho mtakatifu na ya utume ulio sawasawa Mapadre wote
hufungamana katika udugu wa ndani, unaopaswa kujionyesha kwa hiari na kwa
moyo katika kusaidiana katika mambo ya kiroho na ya kimwili, ya kichungaji
na ya binafsi, katika mikutano na katika ushirikiano wa maisha, wa kazi na
wa upendo.
Kama baba katika Kristo wawaangalie waamini wao waliowazaa kiroho kwa
Ubatizo na mafundisho (taz. 1Kor 4:15; 1Pet 1:23). Wakijifanya kwa moyo
vielelezo vya kundi lao (taz. 1Pet 5:3) waongoze na kuitumikia jumuiya yao
ya mahali, ili yenyewe istahili kuitwa kwa jina lile ambalo kwalo taifa lile
lililo moja na zima la Mungu lasifiwa, yaani Kanisa la Mungu (taz. 1Kor 1:2;
2Kor 1:1; n.k.). Wakumbuke katika mwenendo na uangalizi wao wa kila siku
kuwaonyesha waamini na wasio waamini, wakatoliki na wasio wakatoliki, sura
ya huduma ya kweli ya kikuhani na ya kichungaji, na ya kwamba inawapasa
kuwashuhudia wote ukweli na uzima, na kama wachungaji wema, kuwatafuta pia
wale (taz. Lk 15:4-7) ambao, ijapokuwa walibatizwa katika Kanisa katoliki,
waliacha kupokea sakramenti, au hata kukosa imani.
Kwa kuwa siku hizi wanadamu wanazidi kufungamana wao kwa wao katika
maisha ya kiraia, ya kiuchumi na ya kijamii, yawapasa Mapadre, kwa
kuunganisha juhudi na kazi zao chini ya uongozi wa Maaskofu na wa Baba
Mtakatifu, waondoshe kila sababu ya mfarakano (dispersionis), kusudi
wanadamu wote waongozwe kwenye umoja wa familia ya Mungu.
Mashemasi
29. Kwenye daraja iliyo chini katika Hierarkia wapo Mashemasi, ambao
wamewekewa mikono “siyo kwa ajili ya ukuhani, bali kwa utumishi”[110].
Kwa maana, wakiwa wamethibitika kwa neema ya sakramenti wanalitumikia taifa
la Mungu katika ushirika na Askofu na umoja wa Mapadre wake, katika huduma (diaconia)
ya liturujia, ya Neno na ya upendo. Ni wajibu wa Shemasi, kadiri
atakavyokabidhiwa na mamlaka halali, kutoa Ubatizo rasmi, kuitunza Ekaristi
na kuigawa, kuisimamia Ndoa na kuibariki kwa jina la Kanisa, kuwapelekea
Komunyopamba walio katika hatari ya kufa, kuwasomea waamini Maandiko
Matakatifu, kuwafundisha na kuwaonya watu, kuongoza ibada na sala za
waamini, kugawa visakramenti, kuongoza ibada ya maziko na mazishi.
Mashemasi, waliowekwa kwa matendo ya huruma na ya usimamizi, walikumbuke
onyo la Mt. Polikarpo, “Wawe na huruma, wenye bidii, wakienenda katika
ukweli wa Bwana, aliyejifanya mtumishi wa wote”[111].
Maadamu wajibu hizo zilizo za lazima sana kwa maisha ya Kanisa
zinaweza kutekelezeka kwa shida katika nchi nyingi kadiri ya utaratibu wa
sasa wa Kanisa la Roma, kwa siku za mbele Ushemasi unaweza tena kuwekwa kama
Daraja halisi na ya kudumu ya Hierarkia. Ni juu ya Mabaraza halali ya
Maaskofu ya nchi mbalimbali kwa kibali cha Baba Mtakatifu mwenyewe, kuamua
kama inafaa na katika mahali gani Mashemasi wa namna hii waasisiwe kwa
huduma ya kiroho. Kwa idhini ya Askofu wa Roma Ushemasi huu waweza kutolewa
kwa wanaume wa umri wa kukomaa kutosha pia wakiishi katika ndoa, na vilevile
kwa vijana wafaao ambao sheria ya useja lazima kwao idumu kuwa na nguvu.
Sura ya Nne
WALEI
Walei katika Kanisa
30. Mtaguso Mkuu, ukiisha kueleza majukumu ya Hierarkia unafurahi
kuelekeza moyo kwenye hali ya waamini wakristo wenye kuitwa walei, ingawa
yote yaliyosemwa juu ya Taifa la Mungu huwahusu walei, sawasawa kama watawa
na wakleri. Lakini mambo mengine huwahusu kwa namna ya pekee walei, wanaume
kwa wanawake, sababu ya hali yao na utume wao. Misingi ya mambo hayo
inatakiwa kuchunguzwa kinaganaga zaidi, sababu ya mazingira ya pekee ya siku
hizi. Maana wachungaji wenye Daraja takatifu wanajua sana jinsi walei
wanavyosaidia usitawi wa Kanisa lote. Maana wachungaji wanajua kwamba
hawakuasisiwa na Kristo ili wajitwalie peke yao utume wote wenye wokovu
ambao Kanisa liliupokea kwa ajili ya ulimwengu, bali kwamba huduma yao
tukufu ndiyo kuwachunga waamini na kutambua huduma zao na karama zao ili
wote, kila mmoja kadiri ya kipaji chake, wasaidiane kwa pamoja katika kazi
moja. Kwa maana yatupasa sisi sote “tuishike kweli katika upendo na kukua
hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili
wote ukiungamanishwa na kushikamanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa
kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga
wenyewe katika upendo” (Efe 4:15-16).
Tabia na utume wa walei
31. Kwa jina la walei humaanishwa hapa waamini wote isipokuwa wale wenye
Daraja takatifu, na wenye hali ya kitawa iliyokubaliwa na Kanisa. Yaani,
waamini ambao kwa vile walipata kuwa viungo vya mwili wa Kristo kwa ubatizo,
na kufanywa kuwa Taifa la Mungu na kushirikishwa kwa namna yake katika
huduma ya kikuhani, ya kinabii na ya kifalme ya Kristo, watekeleza, kadiri
ya uwezo wao, utume wa Taifa lote la kikristo katika Kanisa na katika
ulimwengu.
Tabia ya kidunia ndiyo tabia halisi na pekee ya walei. Maana wenye
Daraja takatifu, ingawa mara nyingine waweza kuyashughulikia mambo ya
kidunia, hata kufanya kazi ya kidunia, lakini kwa sababu ya wito wao wa
pekee waelekezwa kimsingi na hasa (precipue et ex professo) ili
kutimiza huduma takatifu; na watawa, kwa hali yao, watoa ushuhuda mwangavu
na bora wa kwamba ulimwengu hauwezi kugeuzwa na kutolewa kwa Mungu pasipo
roho ya heri nane. Ni juu ya walei, kutokana na wito wao, kuutafuta ufalme
wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia na kuyaelekeza kadiri ya Mungu.
Wanaishi ulimwenguni, yaani katika kazi zozote na shughuli za kidunia na
katika mazingira ya kawaida ya maisha ya kifamilia na ya kijamii, ambayo
maisha yao yamefungamanishwa nayo. Hapo wanaitwa na Mungu kusaidia
kuutakatifuza ulimwengu, kama kutoka kwa ndani, mithili ya chachu, katika
kuyatimiza majukumu yao wenyewe, wakiongozwa na roho ya kiinjili, na hivyo
wamdhihirishe Kristo kwa wengine, waking’aa hasa kwa ushuhuda wa maisha yao,
imani, matumaini na mapendo. Kwa hiyo yawahusu hao kwa namna ya pekee
kuyaangaza na kuyapanga mambo yote ya kidunia, ambayo wamefungamana nayo,
hili daima yafanyike na kukua kadiri ya Kristo na kuwa kwa sifa ya Muumba na
Mkombozi.
Hadhi ya walei katika Taifa la Mungu
32. Kwa asasi ya Mungu Kanisa takatifu lapangwa na kuongozwa kwa
namna mbalimbali ajabu. “Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo
vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; vivyo hivyo na sisi tulio
wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake” (Rum
12:4-5).
Basi, Taifa teule la Mungu ni moja tu: “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo
mmoja” (Efe 4:5); hadhi moja ya viungo kwa kuzaliwa upya katika Kristo,
neema moja ya kuwa watoto, wito mmoja wa kuwa wakamilifu, wokovu mmoja,
tumaini moja na upendo usiogawanyika. Basi katika Kristo na katika Kanisa
haiko tofauti mintarafu jamaa au taifa, hali ya kijamii au jinsia, kwa kuwa
“hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala
mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa “mmoja” katika Kristo Yesu” (Gal
3:28; taz. Kol 3:11).
Basi, ingawa ndani ya Kanisa sio wote wanaoshika njia ileile, lakini wote
waitwa kuwa watakatifu na wamepata imani ileile katika haki ya Mungu (taz.
2Pet 1:1). Ijapo wengine kwa mapenzi ya Kristo waliwekwa kuwa walimu,
mawakili wa mafumbo na wachungaji kwa ajili ya wengine, lakini upo kati ya
wote usawa wa kweli kuhusu hadhi na utendaji wa pamoja wa waamini wote kwa
ajili ya kuujenga Mwili wa Kristo. Tofauti iliyowekwa na Bwana kati ya wenye
Daraja takatifu na wengine wa Taifa la Mungu, inaleta yenyewe muungano kwa
kuwa wachungaji na waamini wengine wamefungamana wao kwa wao kwa sababu kila
mmoja anamhitaji mwenzake. Wachungaji wa Kanisa, wakiufuata mfano wa Bwana,
watumikiane wao kwa wao na wawatumikie waamini; nao waamini wafanye kazi kwa
juhudi pamoja na wachungaji na walimu. Hivyo katika kutofautiana wote
wanaushuhudia umoja wa ajabu katika Mwili wa Kristo: kwa maana utofauti
wenyewe wa neema, huduma na utendaji unawakusanya watoto wa Mungu katika
umoja, kwa kuwa “kazi hizi zote huzitenda Roho huyu mmoja, yeye yule” (1Kor
12:11).
Kwa hiyo walei, kama vile kwa hisani ya Mungu wanaye kama ndugu Kristo,
ambaye ijapokuwa ni Bwana wa vyote hakuja kutumikiwa bali kutumika (taz. Mt
20:28), vivyo hivyo wanao kama ndugu zao wale wenye Daraja takatifu ambao
wanaichunga familia ya Mungu wakifundisha, wakitakatifuza na kuiongoza kwa
mamlaka ya Kristo, ili amri mpya ya upendo itimizwe na wote. Mtakatifu
Augustino aeleza hayo vizuri sana: “Ikiwa kunanitisha [kujitambua] mimi ni
nani kwa ajili yenu, kunanifariji [kujitambua] mimi ni nani pamoja nanyi.
Maana kwa ajili yenu, mimi ni Askofu; pamoja nanyi, mimi ni mkristo. Lile ni
jina la wajibu, hili ni la neema; lile ni jina la hatari, hili ni la wokovu”[112].
Utume wa walei
33. Walei, waliokusanyika katika Taifa la Mungu na kuwekwa katika
Mwili mmoja wa Kristo chini ya kichwa kimoja, wawao wote waitwa, kama viungo
vyenye uhai, kutolea nguvu zao zote walizopewa na ufadhili wa Muumbaji na
neema ya Mkombozi, ili kulikuza Kanisa na kulitakatifuza daima.
Utume wa walei ndio kushiriki utume wa Kanisa lenyewe uletao wokovu; na
kuutimiza utume huo ni agizo ambalo wote wanapewa na Mungu mwenyewe kwa njia
ya Ubatizo na Kipaimara. Kwa sakramenti, hasa kwa Ekaristi takatifu, mapendo
kwa Mungu na kwa watu, yaliyo roho ya utume wote, yanashirikishwa na
kulishwa. Lakini walei waitwa kwa namna ya pekee kuonyesha uwepo wa Kanisa
na utendaji wake mahali pale na katika mazingira yale ambamo lenyewe
haliwezi kuwa chumvi ya dunia, isipokuwa kwa njia yao tu[113].
Hivyo kila mlei, kwa sababu ya vipaji vyenyewe alivyopewa, anakuwa shahidi
na wakati huohuo chombo hai cha utume wa Kanisa lenyewe “kwa kadiri ya
kipimo cha kipawa chake Kristo” (Efe 4:7).
Licha ya utume huo uwahusuo moja kwa moja waamini wakristo wote, walei
wanaweza kuitwa kwa njia mbalimbali kuushiriki kwa karibu zaidi utume wa
Hierarkia[114], kadiri ya
mfano wa wanaume na wanawake wale waliomsaidia Mtume Paulo katika
kuishindania Injili, na kutenda kazi katika Bwana (taz. Flp 4:3; Rum
16:3nk). Aidha wana uwezo wa kuwekwa na Hierarkia ili kutimiza kazi kadhaa
za Kanisa kwa ajili ya shabaha ya kiroho.
Basi, walei wote wametwishwa mzigo wenye heshima wa kufanya kazi ili
azimio la wokovu la Mungu liwafikie zaidi na zaidi watu wote wa nyakati zote
na wa mahali pote duniani. Kwa sababu hiyo wafunguliwe kila njia ili wao nao
wapate kushiriki kwa bidii tendo la wokovu la Kanisa kadiri ya nguvu zao na
mahitaji ya nyakati.
Jukumu ya kikuhani na ya kiibada
34. Yesu Kristo, aliye Kuhani mkuu na wa milele, akitaka
kuendeleza ushuhuda wake na huduma (servitium) yake kwa njia ya walei
pia, huwahuisha kwa Roho wake na kuwahimiza bila kukoma watimize tendo
lolote lililo jema na kamili.
Kwa maana hao aliowaunganisha kwa ndani na maisha yake na huduma yake
akawajalia pia sehemu ya jukumu lake la kikuhani ili watimize ibada ya
kiroho, ili Mungu atukuzwe na watu waokolewe. Kwa sababu hiyo walei, maadamu
wametunukiwa kwa Kristo (Christo dicati) na kupakwa Roho Mtakatifu,
kwa namna ya ajabu waitwa na kufundishwa ili Roho azae kila siku matunda
mengi sana ndani yao. Kwa maana matendo yao yote, sala zao na shughuli zao
za kitume, maisha yao ya ndoa, na ya familia, kazi zao za kila siku,
burudani za roho na za mwili, kama zikitimilizwa katika Roho, na hata taabu
za maisha, zikichukuliwa kwa uvumilivu, zinageuka kuwa dhabihu za roho
zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo (taz. 1Pet 2:5). Katika
adhimisho la Ekaristi dhabihu hizo zatolewa kwa uchaji wote kwa Baba pamoja
na sadaka ya Mwili wa Bwana. Hivyo walei pia, huku wakitenda kazi kila
mahali katika utakatifu kama waabudu, wauweka wakfu kwa Mungu ulimwengu
wote.
Jukumu la kinabii na ushuhuda
35. Kristo, aliye Nabii mkuu, alitangaza ufalme wa Baba kwa
ushuhuda wa maisha yake na kwa nguvu ya neno, naye hutimiza kazi yake ya
kinabii hadi ufunuo mkamilifu wa utukufu wake, si kwa njia ya Hierarkia peke
yake, inayofundisha kwa jina na uwezo wake, bali pia kwa njia ya walei. Kwa
sababu hiyo huwaweka walei kuwa mashahidi wake na kuwapa utambuzi wa imani (sensu
fidei) na neema ya Neno (taz. Mdo 2:17-18; Ufu 19:10) ili nguvu ya
Injili ing’ae katika maisha ya kila siku, ya kifamilia na ya kijamii. Nao
wanajionyesha kuwa wana wa ahadi, wakiwa wamethibitika katika imani na
matumaini, wakiukomboa wakati wa sasa (taz. Efe 5:16; Kol 4:5) na kungojea
kwa saburi utukufu ujao (taz. Rum 8:25). Na matumaini haya wasiyafiche
moyoni mwao, bali wayaonyeshe katika miundo ya maisha ya kidunia, wakiongoka
daima na kushindana “juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo
wabaya” (Efe 6:12).
Kama vile sakramenti za Sheria Mpya, zinazolisha maisha na utume
wa waamini hudokeza mbingu mpya na nchi mpya (taz. Ufu 21:1), vivyo hivyo
walei huwa watangazaji wenye nguvu wa imani ya mambo yatarajiwayo (taz. Ebr
11:1), ikiwa hawasiti kuunganisha ungamo la imani na maisha kadiri ya imani.
Kuhubiri Injili, yaani kumtangaza Kristo kwa ushuhuda wa maisha na kwa neno,
hupata tabia maalum na nguvu ya pekee kwa sababu hutekelezwa katika hali za
kawaida za dunia.
Katika jukumu hilo hali ile ya maisha iliyotakatifuzwa na
sakramenti maalum, yaani maisha ya ndoa na ya kifamilia, huonekana kuwa na
thamani kubwa. Humo mna utekelezaji na shule bora ya utume wa walei, ambapo
dini ya kikristo hupenya mpango wote wa maisha na kuugeuza zaidi siku kwa
siku. Humo watu wa ndoa wana wito wao maalum wa kushuhudiana wao kwa wao na
kwa watoto imani na upendo wa Kristo. Familia ya kikristo hutangaza kwa
sauti kubwa nguvu za Ufalme wa Mungu zilizopo sasa, pamoja na matumaini ya
uzima wa heri ujao. Hivyo kwa mfano na ushuhuda wake huuhakikisha ulimwengu
kwa habari ya dhambi na kuwaangaza wautafutao ukweli.
Basi walei, hata wanaposhughulikia mambo ya kidunia, waweza na kupaswa
kutekeleza utendaji bora kwa ajili ya uinjilishaji wa ulimwengu. Hata kama
baadhi yao wanatoa huduma takatifu fulani kadiri ya uwezo wao kama mawakili,
wenye Daraja wakikosekana au wakizuiwa kwa madhuluma, au ikiwa wengi kati
yao wanatumia nguvu zao zote katika kazi ya kitume, lakini inawapasa wote
kusaidia kazi ya kueneza Ufalme wa Kristo duniani na kuukuza. Kwa hiyo walei
wajitahidi kwa bidii kuufahamu zaidi na zaidi ukweli uliofunuliwa, na
kumsihi Mungu kwa ari awajalie kipaji cha hekima.
Jukumu ya kifalme
36. Kristo, aliyekuwa mtii hata mauti na kwa hiyo Baba
alimwadhimisha mno (taz. Flp 2:8-9), akaingia katika utukufu wa ufalme wake.
Vitu vyote vimetiishwa chini yake mpaka atakapojitiisha yeye mwenyewe na
kuvitiisha viumbe vyote kwa Baba, ili kwamba Mungu awe yote katika yote
(taz. 1Kor 15:27-28). Naye aliwashirikisha wanafunzi wake uwezo huu ili nao
pia wawekwe katika uhuru wa kifalme na washinde ndani yao wenyewe utawala wa
dhambi kwa kujikana wenyewe na kwa utakatifu wa maisha yao (taz. Rum 6:12),
na zaidi, wakimtumikia Kristo katika watu wengine, kwa unyenyekevu na saburi
wawapeleke ndugu zao kwa Mfalme yule, ambaye kumtumikia yeye ndiko kutawala.
Kwa maana Bwana anapenda kuueneza ufalme wake kwa njia pia ya walei waamini,
yaani ufalme “wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa
haki, mapendo na amani”[115];
katika ufalme huo viumbe vyenyewe vitatolewa katika utumwa wa uharibifu,
hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu (taz. Rum 8:21).
Wanafunzi wamepewa yakini ahadi kuu na amri kuu, yaani “vyote ni vyenu,
nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu” (1Kor 3:21 na 23).
Basi, yawapasa waamini kutambua maumbile halisi ya viumbe vyote, thamani
yake na mpango wake unaoielekea sifa ya Mungu, na kusaidiana wao kwa wao
kuishi maisha matakatifu zaidi pia kwa njia ya matendo ya kidunia, ili
ulimwengu upenywe na Roho wa Kristo ili ufanikiwe kufikia kikomo chake
katika haki, upendo na amani. Katika kuutimiza wajibu huu kwa ajili ya wote,
walei wanashika nafasi ya kwanza. Kwa hiyo, kwa ustadi wao katika maarifa ya
kidunia na kwa utendaji wao ulioinuliwa kwa ndani na neema ya Kristo,
wachangie kwa bidii matendo yao ili mema yaliyoumbwa yasitawishwe kwa kazi
ya kibinadamu, kwa ufundi na maarifa kwa ajili ya manufaa ya watu wote
kabisa, kadiri ya mpango wa Muumbaji na mwanga wa Neno lake. Tena mema hayo
yagawanyike kati ya watu kwa haki inavyofaa na, kwa namna yake, yasaidie
maendeleo ya watu wote katika uhuru wa kibinadamu na wa kikristo. Hivyo
Kristo kwa njia ya viungo vya Kanisa ataiangaza zaidi na zaidi jamii nzima
ya kibinadamu kwa mwanga wake uletao wokovu.
Aidha, yawapasa walei, kwa kuunganisha nguvu zao, waponye taasisi na hali za
maisha za ulimwengu, ikiwa zinachochea dhambi katika desturi, hivi kwamba
hizo zote ziweze kufuata kanuni za haki na kurahisisha kutenda fadhila
badala ya kuwa kizuizi. Kwa kufanya hivyo watapenyeza thamani ya kimaadili
katika utamaduni na kazi za binadamu. Kwa namna hiyo shamba la dunia
laandaliwa vizuri zaidi kwa ajili ya mbegu iliyo Neno la Mungu, na pamoja na
hayo, milango ya Kanisa itakuwa ni wazi zaidi, ili tangazo la amani liuingie
ulimwengu.
Kwa ajili ya mpango wa wokovu waamini wajifunze kwa uangalifu
kutofautisha kati ya haki na wajibu ambao wanazo, maadamu wameunganika na
Kanisa, na zile ziwapasazo kama washiriki wa jamii ya kibinadamu.
Wajibidishe kuzioanisha kati yao, wakikumbuka kwamba katika mambo yote ya
kidunia yawabidi kuongozwa na dhamiri ya kikristo, kwa sababu hakuna
utendaji wa kibinadamu, hata katika mambo ya kidunia, uwezao kuondolewa
katika utawala wa Mungu. Katika nyakati zetu inatakiwa hasa kwamba
utofautishaji huu pamoja na ulinganifu huu zing’ae kwa namna iliyo dhahiri
zaidi iwezekanavyo katika mwenendo wa waamini, ili utume wa Kanisa uweze
kuzikabili kikamilifu hali za pekee za ulimwengu wa sasa. Kwa maana, kama
vile lazima kukubali ya kwamba mji wa kidunia, ushughulikiao kwa haki mambo
ya kidunia, huongozwa na kanuni zake, vivyo hivyo hukataliwa kwa haki
mafundisho yale mabaya yatakayo kuijenga jamii bila kuijali dini na kuupinga
uhuru wa dini wa raia, na kuuangamiza[116].
Mahusiano na Hierarkia
37. Walei, kama vile waamini wakristo wote, wana haki ya kupokea kwa
wingi, kutoka kwa wachungaji wenye Daraja takatifu, mema ya kiroho ya
Kanisa, hasa misaada ya Neno la Mungu na ya sakramenti[117].
Basi, wawajulishe wachungaji mahitaji yao na matakwa yao kwa uhuru na
matumaini yanavyowapasa watoto wa Mungu na ndugu katika Kristo. Kwa kadiri
ya elimu, umahiri na ubora walivyo navyo, wanayo haki, pengine hata wajibu,
ya kuyaeleza maoni yao juu ya yale yahusuyo manufaa ya Kanisa[118].
Ikiwa inafaa, hilo litendeke kwa njia ya taasisi zilizopangwa na Kanisa kwa
ajili hiyo, na daima [litendeke] katika ukweli, uthabiti na busara, kwa
heshima na mapendo kwa wale wanaowakilisha nafsi ya Kristo kutokana na
huduma zao takatifu.
Walei, kama vile waamini wakristo wote, washike kwa utii wa kikristo na kwa
moyo yale ambayo wachungaji wenye Daraja takatifu, walio mawakili wa Kristo,
wanayaamuru kama walimu na viongozi katika Kanisa. Hivyo wanaufuata mfano wa
Kristo ambaye, kwa utii wake hata mauti aliwafungulia watu wote njia yenye
heri ya uhuru wa watoto wa Mungu. Wala wasiache kuwaombea viongozi wao kwa
Mungu, maana wao wanakesha kwa ajili zetu, kama watu watakaotoa hesabu, ili
kwamba wafanye hivyo kwa furaha, wala si kwa kuugua (taz. Ebr 13:17).
Na wachungaji wenye Daraja takatifu watambue na kukuza hadhi na
madaraka ya walei katika Kanisa; watumie kwa moyo mashauri yao yenye busara,
wawakabidhi kazi kwa huduma ya Kanisa huku wakiwaamini, wawaachie uhuru na
nafasi ya utendaji, zaidi wawatie moyo ili waanzishe matendo kwa hiari yao
pia. Kwa uangalifu katika Kristo na upendo wa kibaba wayafikirie makusudio,
maombi na mapendekezo yatolewayo na walei[119].
Aidha, wachungaji wataukubali kwa heshima ule uhuru wa haki uwahusuo wote
katika mji wa dunia hii.
Mema mengi yatarajiwa kwa ajili ya Kanisa kutokana na mahusiano haya ya
karibu kati ya walei na wachungaji. Kwa njia hii hisia ya madaraka yao
wenyewe yaimarika ndani ya walei, juhudi zachochewa na nguvu za walei
zaunganika kwa urahisi zaidi na kazi ya wachungaji. Wachungaji nao, kwa
msaada wa mang’amuzi ya walei, wanaweza kutoa hukumu yao kwa dhahiri na kwa
kufaa zaidi katika mambo ya kiroho na ya kidunia; na hivyo Kanisa lote
likithibitishwa na viungo vyake vyote, lipate kutimiza utume wake kwa ajili
ya uzima wa ulimwengu kwa mafanikio makubwa zaidi.
Walei, roho ya ulimwengu
38. Kila mlei hupaswa kuwa mbele ya ulimwengu shahidi wa ufufuko na
maisha ya Bwana Yesu na ishara ya Mungu aliye hai. Yawapasa wote kwa pamoja,
na kila mmoja kwa upande wake, kuulisha ulimwengu matunda ya kiroho (taz.
Gal 5:22) na kueneza ndani yake ile roho iwahuishayo maskini, wapole na
wapatanishi, ambao Bwana aliwatangaza katika Injili kuwa wenye heri (taz. Mt
5:3-9). Kwa neno moja, “kama vile roho ilivyo mwilini, ndivyo wakristo wawe
ulimwenguni”[120].
Sura ya Tano
WITO WA WATU WOTE KATIKA KANISA KUWA WATAKATIFU
Utakatifu katika Kanisa
39. Kanisa, ambalo fumbo lake laelezwa na Mtaguso Mkuu, huaminika kuwa
daima takatifu. Kwa maana Kristo, Mwana wa Mungu, anayetangazwa pamoja na
Baba na Roho Mtakatifu kwamba ni “peke yake mtakatifu”[121],
amelipenda Kanisa kama Bibiarusi wake, akajitoa mwenyewe kwa ajili yake ili
alitakatifuze (taz. Efe 5:25-26), akaliunganisha naye kama mwili wake,
akalijazia kipaji cha Roho Mtakatifu, kwa utukufu wa Mungu. Kwa hiyo wote
katika Kanisa, wawe watu wa hierarkia au wawe waongozwao nayo, waitwa kuwa
watakatifu, kadiri anavyosema Mtume [Paulo], “Haya ndiyo mapenzi ya Mungu,
kutakaswa kwenu” (1The 4:3; taz. Efe 1:4). Utakatifu huu wa Kanisa
hujidhihirisha bila kukoma, tena ni lazima ujidhihirishe katika matunda ya
neema anayozaa Roho ndani ya waamini. Hujieleza kwa njia mbalimbali katika
kila mmoja mwenye kujitahidi kuufikia ukamilifu wa upendo katika hali yake
ya kawaida ya maisha yake, akiwajenga wengine; kwa namna yake ya pekee
hujionyesha katika kutimiza mashauri yaitwayo kwa kawaida ya kiinjili.
Utekelezaji huo wa mashauri wanaojitwalia wakristo wengi kwa msukumo wa Roho
Mtakatifu, au wenyewe peke yao au katika hali au mpango ulivyokubaliwa na
Kanisa, huleta ulimwenguni, tena lazima ulete, ushuhuda na mfano bora wa
utakatifu wake [Kanisa].
Wito wa watu wote kuwa watakatifu
40. Bwana Yesu, aliye mwalimu na mfano wa kimungu wa ukamilifu wote,
aliwahubiria wanafunzi wake wote na kila mmoja peke yake wenye hali yoyote,
utakatifu wa maisha ambao Yeye mwenyewe ndiye mwanzishaji na mtimilizaji
wake, “Ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo
mkamilifu” (Mt 5:48)[122].
Akawapelekea wote Roho Mtakatifu ili awasukume kwa ndani kumpenda Mungu kwa
moyo wote, kwa roho yote, kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote (taz. Mk
12:30), na kupendana kama vile Kristo alivyowapenda (taz. Yn 13:34; 15:12).
Wafuasi wa Kristo walioitwa na Mungu siyo kadiri ya matendo yao, bali kadiri
ya azimio na neema yake na kuhesabiwa haki katika Bwana Yesu, katika ubatizo
wa imani walifanywa kweli watoto wa Mungu na washiriki wa tabia ya Mungu, na
hivyo watakatifu halisi. Kwa hiyo yawapasa, kwa msaada wa Mungu, kuushika na
kuutimiliza katika maisha yao utakatifu huu waliopewa. Waonywa na Mtume
waishi “kama iwastahilivyo watakatifu” (Efe 5:3), na “kwa kuwa wamekuwa
wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, wajivike moyo wa rehema, utu mwema,
unyenyekevu, upole, uvumilivu” (Kol 3:12), na wawe na matunda ya Roho ili
wafanywe watakatifu (taz. Gal 5:22; Rum 6:22). Kwa kuwa twajikwaa sisi sote
pia katika mambo mengi (taz. Yak 3:2) tunahitaji daima huruma ya Mungu na
tunapaswa kusali kila siku, “Utusamehe madeni yetu” (Mt 6:12)[123].
Ni dhahiri kwa wote kwamba waamini wote wakristo wa hali yoyote au
daraja lolote huitwa kufikia utimilifu wa maisha ya kikristo na ukamilifu wa
upendo[124]: kwa utakatifu
huu huhamasishwa kiwango cha maisha kiwafaacho zaidi wanadamu, hata katika
jamii ya kidunia. Kwa lengo la kuufikia ukamilifu huo waamini watumie nguvu
walizopata kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo, ili wakifuata nyayo
zake na kufananishwa na mfano wake, wakiyatii mapenzi ya Baba katika mambo
yote, wajitoe kwa moyo wote kwa ajili ya utukufu wa Mungu na huduma ya
jirani. Hivyo utakatifu wa Taifa la Mungu utazidi kuzaa matunda tele, kama
ilivyoonyeshwa wazi katika historia ya Kanisa kwa njia ya maisha ya
watakatifu wengi.
Namna nyingi za kutekeleza utakatifu ulio mmoja
41. Katika aina na wajibu mbalimbali za maisha utakatifu mmoja
husitawishwa na wote waongozwao na Roho wa Mungu na, wakiitii sauti ya Baba
na kumwabudu Mungu Baba katika roho na kweli, wanamfuata Kristo aliye
maskini, mnyenyekevu na mwenye kuchukua msalaba, ili wastahili kushiriki
utukufu wake. Yampasa kila mmoja, kadiri ya vipawa vyake na majukumu yake,
kuendelea mbele bila kusitasita katika njia ya imani iliyo hai, iamshayo
matumaini na kutenda kwa mapendo.
Wachungaji wa kundi la Kristo wapaswa kwanza kabisa, kwa mfano wa Kuhani
Mkuu na wa milele, Mchungaji na Mwangalizi (Episcopi) wa roho zetu,
kutekeleza kwa utakatifu na shauku, kwa unyenyekevu na uthabiti huduma yao,
ambayo ikiwa imetimizwa hivi, itakuwa njia bora ya kujitakatifuza wao
wenyewe pia. Wameteuliwa kwa utimilifu wa ukuhani, na wanajaliwa neema ya
kisakramenti ili watimize jukumu kamili la upendo wa kichungaji, katika
kusali, kujitoa na kuhubiri, na kwa kila mtindo wa uangalizi na huduma ya
kiaskofu[125], wasihofu kutoa
uhai wao kwa ajili ya kondoo na, wakijifanya vielelezo kwa lile kundi (taz.
1Pet 5:3), walihamasishe Kanisa liufikie utakatifu mkubwa zaidi siku kwa
siku, kwa mfano wao pia.
Mapadre, kwa kulandana na Daraja la Maaskofu, ambao ni taji lake la
kiroho[126], huku wakishiriki
neema ya huduma yao kwa njia ya Kristo, aliye Mshenga wa milele na pekee,
wakue katika upendo wa Mungu na wa jirani kwa kutimiza wajibu wao kila siku,
watunze kifungo cha ushirika kati ya mapadre, wajae mema yote ya kiroho na
watoe kwa wote ushuhuda hai wa Mungu[127],
huku wakiwaiga wale mapadre ambao, katika mkondo wa karne nyingi, walitoa
mfano mwangavu wa utakatifu, katika huduma iliyokuwa mara nyingi nyenyekevu
na iliyositirika. Sifa yao yadumu katika Kanisa la Mungu. Kutokana na wajibu
wao, husali na kutoa sadaka kwa ajili ya watu wao na kwa ajili ya taifa lote
la Mungu, kwa kufahamu wanayotenda na kuiga wanayoshika[128].
Badala ya kuzuiliwa na shughuli za kitume, na hatari na dhiki, kwa njia ya
yayo hayo wakwee kwenye utakatifu wa juu zaidi, wakilisha na kuchochea
utendaji wao kwa wingi wa kutafakari, kwa ajili ya faraja ya Kanisa zima la
Mungu. Mapadre wote, na hasa waitwao wakleri wa Jimbo kwa hadhi ya pekee ya
upadirisho wao, wakumbuke jinsi gani umoja mwaminifu na ushirikiano mkubwa
na Askofu wao unavyosaidia utakatifu wao.
Wahudumu pia wa Daraja iliyo chini zaidi wanashiriki kwa namna ya pekee
utume na neema ya ukuhani mkuu, na wa kwanza kati yao ni Mashemasi, ambao,
kwa kuwa wanayatumikia mafumbo ya Kristo na ya Kanisa[129],
wapaswa kujikinga na kila hatia ya uovu na kumpendeza Mungu na kutenda mema
yote mbele ya watu (taz. 1Tim 3:8-10 na 12-13). Wakleri wanaoitwa na Bwana
na kutengwa ili wawe fungu lake, chini ya uangalizi wa wachungaji wao, na
wanaojiandaa kwa wajibu wa wahudumu, wanatakiwa kulinganisha akili zao na
mioyo yao na [lengo] la uteule wao mtukufu, wakidumu katika kusali, wakiwa
na juhudi katika upendo, wakitafakari mambo yoyote yaliyo ya kweli, yaliyo
ya haki na yenye sifa njema, wakitekeleza yote kwa utukufu na heshima ya
Mungu. Wanaunganika nao wale walei walioteuliwa na Mungu, ambao wanaitwa na
Askofu kusudi wajitoe kabisa kwa matendo ya kitume na wanataabika katika
shamba la Mungu wakizaa matunda mengi[130].
Watu wa ndoa na wazazi walio wakristo wapaswa, wakifuata njia yao
wenyewe, kutegemezana kwa upendo mwaminifu katika neema kwa muda wote wa
maisha yao. Wawafundishe watoto wao waliopokea kutoka kwa Mungu kwa upendo,
katika mafundisho ya kikristo na fadhila za kiinjili. Hivyo wanatoa mfano wa
upendo usiolegea na wenye ukarimu, wanajenga udugu wa mapendo na wanakuwa
mashahidi na washiriki wa uzaaji wa Mama Kanisa, kama ishara na ushirika wa
upendo ule, ambao kwao Kristo alimpenda Bibiarusi wake akajitoa kwa ajili
yake[131]. Mfano wa aina hii
unatolewa kwa namna nyingine na watu wajane na wasiofunga ndoa, [wanawake
kwa wanaume], ambao wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya
utakatifu na utendaji wa Kanisa. Na wale wanaojishughulisha katika kazi
zilizo mara nyingi zenye taabu, wapaswa kwa njia ya matendo ya kibinadamu
kujikamilisha wenyewe, kuwasaidia raia, kuhamasisha jamii yote na viumbe
vyote viifikie hali bora zaidi. Tena, kwa upendo wenye matendo, huku
wakifurahi katika matumaini na kuchukuliana mizigo wao kwa wao, wapaswa
kumwiga Kristo, ambaye mikono yake ilizoea kushika vyombo vya kazi na pamoja
na Baba daima anatenda kazi kwa ajili ya wokovu wa watu wote; na kwa kazi
yao ya kila siku waufikie utakatifu wa juu zaidi, hata ule wa kitume.
Na wale wanaolemewa na umaskini, udhaifu, maradhi na taabu mbalimbali au
wanaoudhiwa kwa ajili ya haki, wajue kuwa wanaunganika kwa namna ya pekee na
Kristo atesekaye kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Bwana katika Injili
aliwatangaza kuwa wenye heri, na “Mungu wa neema yote, aliyetuita kuingia katika
utukufu wake wa milele katika Kristo, wakiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye
mwenyewe atawatengeneza na kuwathibitisha na kuwatia nguvu” (1 Pet 5:10).
Basi wakristo wote waamini katika hali, wajibu au mazingira ya maisha
yao, na kwa njia ya mambo hayo yote, watatakatifuzwa zaidi na zaidi siku kwa
siku ikiwa wanapokea yote kwa imani kutoka kwa mkono wa Baba wa mbinguni na
kushirikiana na mapenzi ya Mungu, wakiwaonyesha wote, katika huduma hiyo ya
kidunia, upendo ule ambao kwao Mungu aliupenda ulimwengu.
Njia za utakatifu
42. “Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na
Mungu hukaa ndani yake” (1Yoh 4:16). Mungu amemimina pendo lake katika mioyo
yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi (taz. Rum 5:5); kwa sababu
hiyo kipaji cha kwanza na cha lazima zaidi ni upendo, ambao kwao tunampenda
Mungu kupita yote na jirani kwa ajili ya Mungu. Lakini kusudi upendo ukue
rohoni kama mbegu nzuri na kuzaa matunda, yampasa kila mwamini kusikiliza
kwa hamu Neno la Mungu, na kwa msaada wa neema yake kutimiza mapenzi yake
kwa matendo, kushiriki mara kwa mara sakramenti, hasa Ekaristi na ibada
takatifu, na kujitia kwa uthabiti katika kusali, kujinyima, kuwahudumia
ndugu kwa bidii, na kutekeleza fadhila zote. Kwa maana upendo, ulio kifungo
cha ukamilifu na utimilifu wa sheria (taz. Kol 3:14; Rum 13:10), huziongoza
njia zote za kutakatifuza, huzikamilisha na kuzielekeza zifikie kikomo chake[132].
Kwa hiyo, upendo kwa Mungu na kwa jirani ndio muhuri aliotiwa kila mfuasi wa
kweli wa Kristo.
Kwa kuwa Yesu, Mwana wa Mungu, amedhihirisha upendo wake kwa kutoa uhai
wake kwa ajili yetu, hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kutoa
uhai wake kwa ajili yake Yesu na ndugu zake (taz. 1Yoh 3:16; Yn 15:13).
Tangu awali wakristo wengine waliitwa, tena wataitwa sikuzote, kutoa
ushuhuda huu mkubwa sana mbele ya watu wote, hasa mbele ya wadhulumu. Kwa
hiyo kifodini (martyrium) ambacho kwa njia yake mwanafunzi
anafananishwa na mwalimu wake aliyekubali kwa hiari kufa kwa ajili ya wokovu
wa ulimwengu, na kulinganishwa naye katika kuimwaga damu, kinathaminiwa na
Kanisa kuwa karama bora na uhakikisho mkuu wa upendo. Ingawa ni wachache
wanaojaliwa [neema hii ya kifodini], lakini wote wanapaswa wawe tayari
kumkiri Kristo mbele ya watu, na kumfuata katika njia ya msalaba kati ya
madhulumu ambayo hayakosekani kamwe katika Kanisa.
Tena utakatifu wa Kanisa hutukuzwa kwa namna ya pekee kwa njia ya mashauri
ya aina nyingi ambayo Bwana anawapa wafuasi wake katika Injili ili wayashike[133].
Bora katika hayo ni karama yenye thamani ya neema ya Mungu waliyojaliwa
wengine na Baba (taz. Mt 19:11; 1Kor 7:7) ya kujiweka wakfu kwa Mungu tu
katika ubikira au katika useja[134]
kwa urahisi zaidi na kwa moyo usiogawanyika (taz. 1Kor 7:32-34). Kujinyima
huko kikamilifu kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni huheshimiwa daima na Kanisa
kwa namna ya pekee kama ishara na msukumo wa mapendo na kama chemchemi
maalum yenye uwezo wa kuzaa kiroho ulimwenguni.
Kanisa lakumbuka pia onyo la Mtume anayewahimiza waamini wawe na mapendo
na kuwaonya kuwa na nia iyo hiyo ndani yao, ambayo ilikuwamo ndani ya Kristo
Yesu “aliyejifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa… akawa mtii
hata mauti” (Flp 2:7-8) na kwa ajili yetu “amekuwa maskini ingawa alikuwa
tajiri” (2Kor 8:9). Ingawa yawapasa wanafunzi kuuiga daima na kuushuhudia
upendo huu na unyenyekevu wa Kristo, Mama Kanisa hufurahi kuwa ndani yake
kuna idadi kubwa ya wanaume na wanawake wanaofuata kujinyenyekesha kwake
Mwokozi kwa karibu zaidi na kukuonyesha wazi zaidi, kwa kushika umaskini kwa
uhuru wa wana wa Mungu na kukana mapenzi yao wenyewe. Yaani hao wajitiisha
chini ya mtu kwa ajili ya Mungu, na hivi wanakwenda mbele zaidi ya kiasi
kilichomo katika amri kuhusu ukamilifu, ili wafanane kikamilifu zaidi na
Kristo aliye mtii[135].
Basi waamini wote waalikwa na kupasika kuuelekea utakatifu na
ukamilifu kwa kadiri ya hali yao. Kwa hiyo wajitahidi wote kuliongoza
pendohisia (affectus) lao inavyotakiwa, ili katika kutumia vitu vya
kiulimwengu na kushikwa na tamaa ya mali iliyo kinyume na roho ya umaskini
wa kiinjili, wasije wakazuiliwa kuyaelekea mapendo kamili. Kwa maana Mtume
aonya, “Wale wautumiao ulimwengu huu [wawe] kama hawautumii sana; kwa maana
mambo ya ulimwengu huu yanapita” (1Kor 7:31)[136].
Sura ya Sita
WATAWA
Mashauri ya kiinjili katika Kanisa
43. Mashauri ya kiinjili ya usafi wa moyo uliowekwa wakfu kwa Mungu,
umaskini na utii, yaliyo na misingi juu ya maneno na mifano ya Bwana na
kupendekezwa na Mitume, Mababa, Walimu na Wachungaji wa Kanisa, ni kipaji
cha Mungu ambacho Kanisa limepewa na Bwana wake na kukitunza daima kwa neema
yake. Mamlaka ya Kanisa, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, yalifanya bidii
kuyafafanua [mashauri hayo], kuratibisha utekelezaji wake na kuasisi,
kutokana nao, miundo thabiti ya maisha. Basi ikawa kama ilivyo katika mti
uliopandwa na mbegu ya Mungu na kutoa matawi katika shamba la Bwana kwa
namna za ajabu nyingi, ziliongezeka njia mbalimbali za maisha ya upweke na
ya pamoja, na familia mbalimbali, zinazositawi kwa ajili ya manufaa ya
washiriki wake, na kwa ajili ya wema wa Mwili wote wa Kristo[137].
Kwa maana familia hizo huwapatia washiriki wake misaada ya uthabiti mkubwa
wa mwenendo wa maisha, ya mafundisho yakubalikayo kwa kuufikia ukamilifu, ya
ushirika wa kidugu katika utumishi wa kiaskari wa Kristo, ya uhuru
uimarishwao na utii, kusudi waweze kutimiza salama nadhiri zao za kitawa (professionem
religiosam) na kuzitunza kwa uaminifu na kuendelea kwa furaha ya kiroho
katika njia ya mapendo[138].
Tukizingatia mfumo wa kimungu na wa kihierarkia wa Kanisa, hali
hiyo ya kitawa haiko kati ya hali ya kikleri na ya kilei, bali katika
makundi haya mawili waamini kadha wa kadha huitwa na Mungu ili wajaliwe
kipaji hiki cha pekee katika maisha ya Kanisa, na kuusaidia, kila mmoja kwa
namna yake, utume wa Kanisa uletao wokovu[139].
Maumbile na umuhimu wa hali ya kitawa
44. Kwa nadhiri, au vifungo vingine vitakatifu vinavyofanana nazo
kwa jinsi zake, ambazo mwamini ajilazimisha kwa hizo kuyashika yale mashauri
matatu ya kiinjili yaliyotajwa hapo juu, yeye ajitoa kabisa kwa Mungu aliye
mpendwa wake kupita yote, hata awekwe kwa huduma na heshima ya Mungu kwa
hadhi mpya na ya pekee. Kwa ubatizo amefia dhambi na kuwekwa wakfu kwa
Mungu, lakini kusudi aweze kuzalisha matunda tele zaidi ya neema ya ubatizo,
kwa uprofesi (professione) wa mashauri ya kiinjili katika Kanisa
ananuia kuopolewa na mapingamizi yawezayo kumzuia kuwa na ari ya upendo na
ukamilifu wa ibada kwa Mungu, naye ajiweka wakfu kwa undani zaidi kwa
utumishi wa Mungu[140].
Uwakfu huu utazidi kuwa mkamilifu kwa kadiri vitakavyokuwa imara na thabiti
vifungo vimwonyeshavyo Kristo afungamanaye kwa namna isiyotanguka na Kanisa
aliye Bibiarusi wake.
Kwa kuwa mashauri ya kiinjili, kwa njia ya upendo yanaouelekezea[141],
yawaunganisha kwa namna ya pekee wale wanaozitimiza na Kanisa na fumbo lake,
maisha yao ya kiroho yapaswa kutolewa pia kwa ajili ya manufaa ya Kanisa
zima. Unatokana na hayo wajibu wao wa kufanya kazi, kadiri ya nguvu zao na
aina ya wito wao, kwa ajili ya kupandikiza na kuthibitisha Ufalme wa Kristo
katika roho za watu, kwa sala na matendo, na kuueneza katika nchi zote. Kwa
sababu hiyo Kanisa huhifadhi na kusimamia tabia ya pekee ya mashirika
mbalimbali.
Basi uprofesi wa mashauri ya kiinjili unaonekana kuwa kama ishara
inayoweza na kupaswa kuwavuta kwa namna ya kufaa wanakanisa wote watimize
kwa juhudi wajibu za wito wa kikristo. Maana, kwa kuwa taifa la Mungu halina
mji udumuo hapa duniani, bali hutafuta ule ujao, hali ya kitawa iwafanyayo
wale waliyoishika kuwa huru zaidi na shughuli za kidunia, hudhihirisha kwa
ajili ya waamini wote uwepo wa mema ya mbinguni yaliyopo tayari katika
ulimwengu huu; na huushuhudia uzima mpya na wa milele unaopatikana kwa njia
ya ukombozi wa Kristo, na kutangaza ufufuko ujao na utukufu wa Ufalme wa
mbinguni. Hali ya kitawa huiga pia kwa uaminifu zaidi, na daima huonyesha
katika Kanisa, hali ile ya maisha aliyotwaa Mwana wa Mungu alipoingia
ulimwenguni ili kuyafanya mapenzi ya Baba, na aliyoipendekeza kwa wanafunzi
wake waliomfuata. Hatimaye, huonyesha kwa namna ya pekee Ufalme wa Mungu
unavyoinuka juu ya mambo yote ya dunia, na yalivyo madai yake makuu; na
kudhihirisha kwa ajili ya watu wote ubora wa ukuu wa uweza wake Kristo
Mtawala, na uwezo usio na mipaka wa Roho Mtakatifu atendaye kazi kwa ajabu
katika Kanisa.
Basi hali hiyo [ya maisha] inayoundwa kwa uprofesi wa mashauri ya
kiinjili, ingawa haingii katika muundo wa kihierarkia wa Kanisa, lakini
inahusu kwa hakika maisha yake na utakatifu wake.
Mamlaka ya Kanisa na hali ya kitawa
45. Kwa kuwa wajibu wa Hierarkia ya Kanisa ni kulichunga taifa la
Mungu na kuliongoza kwenye malisho mema (taz. Eze 34:14), inaipasa
kuratibisha kwa hekima kwa njia ya sheria zake utekelezaji (praxim)
wa mashauri ya kiinjili ambayo kwa njia yake ukamilifu wa mapendo kwa Mungu
na kwa jirani huchochewa kwa namna ya pekee[142].
Nayo pia ikifuata kwa usikivu misukumo ya Roho Mtakatifu, hupokea kanuni
zilizotolewa na wanaume na wanawake mashuhuri, na zikiisha pangwa hata
zaidi, hutoa idhini kwa uthabiti. Kwa mamlaka yake yenye uangalizi na utunzo
huzisimamia pia mashirika yaliyoasisiwa popote duniani ili kujenga Mwili wa
Kristo, yapate kukua na kusitawi kadiri ya roho ya waanzishaji.
Kwa lengo la kusaidia zaidi mahitaji ya kundi zima la Bwana, shirika
lolote la kitawa (perfectionis Institutum), na wanashirika wake mmoja
mmoja, huweza kuondolewa kutoka kwa mamlaka ya wakuu wa mahali, kwa idhini
ya Baba Mtakatifu kwa sababu ya ukuu wake juu ya Kanisa lote, na kuwekwa
chini yake tu, kwa ajili ya mafaa ya wote[143].
Vilevile huweza kuachiliwa au kuwekwa (relinqui aut committi) chini
ya mamlaka ya [Maaskofu wao wakuu waitwao] Mapatriarka. Wanashirika wenyewe,
katika kutimiza wajibu wao kwa akili ya Kanisa kulingana na aina yao ya
pekee ya maisha, wapaswa kuwaheshimu na kuwatii Maaskofu, kadiri ya sheria
za Kanisa, kwa sababu ya mamlaka yao ya kichungaji juu ya Makanisa [yao]
faridi na kwa ajili ya umoja na ulinganifu (concordiam) uhitajikao
katika kazi ya kitume[144].
Kanisa kwa idhini yake haliinui tu nadhiri za kitawa kuwa na hadhi
ya hali ya kikanuni (ad status canonici dignitate), lakini kwa
adhimisho lake la kiliturujia huziweka katika hali ya uwakfu kwa Mungu. Kwa
maana Kanisa lenyewe, kwa mamlaka liliyokabidhiwa na Mungu, hupokea nadhiri
za maprofesi (profitentium vota suscipit), huwaombea kwa sala ya
hadharani [wajaliwe] misaada na neema ya Mungu, huwaweka mikononi mwa Mungu
na kuwapa baraka ya kiroho, likiunganisha matoleo yao na sadaka ya Ekaristi.
Ukuu wa kujiweka wakfu kwa Mungu
46. Watawa wafanye bidii sana ili kwa njia yao wenyewe Kanisa
limdhihirishe kwa uwazi zaidi siku kwa siku, kwa waamini na wasioamini,
Kristo, ama [kama yuko katika hali ya] kutafakari mlimani, au akiuhubiria
umati Ufalme wa Mungu, ama akiwaponya wagonjwa na wenye jeraha, au
akiwaongoa wakosefu wazae matunda mema, au akiwabariki watoto na kuwatendea
mema watu wote, akiyatii daima mapenzi ya Baba aliyemtuma[145].
Mwishowe wote wajue kwamba uprofesi wa mashauri ya kiinjili, ingawa
unasababisha kuacha mambo yenye heshima yanayothamanika sana, lakini
haupingi maendeleo ya kweli ya nafsi ya kibinadamu, bali kwa tabia yake
huifaidia sana. Kwa maana mashauri haya, yakipokelewa kwa hiari kadiri ya
wito wa kila mmoja, husaidia sana takaso la moyo na uhuru wa kiroho, huwasha
daima moto wa mapendo na hasa huweza kumlinganisha mkristo na aina ile ya
maisha ya kibikira na kimaskini aliyojichagulia Kristo Bwana na ambayo Mama
yake Bikira aliifuata, kama ilivyothibitishwa na mifano ya waanzishaji (fundatorum)
wengi watakatifu. Mtu yeyote asidhani kwamba watawa kwa kujiweka wakfu
wamekuwa wageni kwa watu na wasiofaa katika mji wa kidunia. Kwa maana, ijapo
wengine hawakai pamoja (non directe adsistunt) na watu wa wakati wao,
lakini wanawakumbuka kwa namna ya kindani zaidi katika mtima wa Kristo, na
kushirikiana nao kiroho ili jengo la mji wa kidunia liwe daima na msingi
katika Bwana na kumwelekea Yeye, isije ikatokea kwamba wanafanya kazi bure
waujengao[146].
Kwa sababu hiyo Mtaguso Mtakatifu huwathibitisha na kuwasifu
wanaume na wanawake, ndugu wa kiume na ndugu wa kike, ambao monasterini au
katika mashule na hospitali, au mishenini, kwa uaminifu mdumifu na
mnyenyekevu katika uwakfu wao, wanampamba Bibiarusi wa Kristo na kuwahudumia
watu wote kwa moyo na kwa namna nyingi.
Kuhimiza udumifu
47. Kila mmoja aitwaye kwa uprofesi wa mashauri, afanye juhudi kubwa ili
kudumu na kuwa bora zaidi katika wito ule ambao Mungu alimwita, ili Kanisa
lipate utakatifu mkubwa zaidi, na kwa ajili ya utukufu mwingi zaidi wa Utatu
mmoja na usiogawanyika, ulio chemchemi na asili ya utakatifu wote katika
Kristo na kwa njia ya Kristo.
Sura ya Saba
TABIA YA KIESKATOLOJIA YA KANISA LINALOSAFIRI
NA UMOJA NA KANISA LILILO MBINGUNI
Tabia ya kieskatolojia ya wito wetu
48. Kanisa, ambalo sisi sote twaitwa kwake katika Kristo Yesu na
ndani yake tunapata utakatifu kwa neema ya Mungu, halitapata utimilifu wake
isipokuwa katika utukufu wa mbinguni, hata zije zamani za kufanywa upya vitu
vyote (taz. Mdo 3:21). [Na wakati huo], pamoja na jamii ya watu ulimwengu
wote pia, ambao umeunganika kwa undani na mwanadamu (intime cum homine
coniungitur), na kwa njia yake unafikilia shabaha yake, utajumlishwa (instaurabitur)
kikamilifu katika Kristo (taz. Efe 1:10; Kol 1:20; 2Pet 3:10-13).
Kristo alipoinuliwa juu ya nchi aliwavuta wote kwake (taz. Yn 12:32);
akiisha kufufuka katika wafu (taz. Rum 6:9) akamtuma ndani ya wanafunzi wake
Roho wake mleta uzima, na kwa njia yake akauweka Mwili wake ulio Kanisa kuwa
sakramenti ya wokovu kwa wote. Akikaa kuume kwa Baba, daima hutenda kazi
ulimwenguni ili awaongoze wote kwenye Kanisa na kwa njia yake awaunganishe
naye zaidi na, kwa kuwalisha Mwili wake na Damu yake mwenyewe,
kuwashirikisha katika maisha ya utukufu wake. Basi kule kutengeneza upya
tulikoahidiwa na tunakongojea, kumekwisha anza tayari katika Kristo,
kunaendelezwa mbele kwa utume wa Roho Mtakatifu, na kudumu kwa njia yake
katika Kanisa. Ndani yake [Kanisa] twafundishwa kwa imani maana ya maisha
yetu ya muda, hadi tuimalize kwa tumai la mema yajayo, kazi tuliyokabidhiwa
na Baba katika ulimwengu huu, na kutimiza wokovu wetu wenyewe (taz. Flp
2:12).
Basi, miisho ya zamani imekwisha kutufikia (taz. 1Kor 10:11), kufanywa upya
kwa ulimwengu kumekwisha wekwa bila kutenguliwa, na kwa hakika kabisa
kumeanza kuonjwa kweli toka sasa; kwa kweli Kanisa hata hapa duniani
limepambwa utakatifu wa kweli ingawa si mkamilifu. Lakini mpaka hapo
zitakapokuwepo mbingu mpya na dunia mpya ambamo haki yakaa ndani yake (taz.
2Pet 3:13), Kanisa linalosafiri, katika sakramenti zake na taasisi zake
zilizo za wakati huu, linachukua sura ya ulimwengu huu unaopita na linaishi
kati ya viumbe ambavyo vinaugua na vina utungu hata sasa na vinatazamia kwa
shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu (taz. Rum 8:19-22).
Tukiwa tumeunganishwa na Kristo katika Kanisa na kutiwa muhuri wa Roho
Mtakatifu “aliye arbuni ya urithi wetu” (Efe 1:14), twaitwa kweli wana wa
Mungu, na ndivyo tulivyo (taz. 1Yoh 3:1), lakini hatujafunuliwa bado pamoja
na Kristo katika utukufu (taz. Kol 3:4) ambao ndani yake tutafanana na Mungu
kwa maana tutamwona kama alivyo (taz. 1Yoh 3:2). Kwa hiyo, “wakati tuwapo
hapa katika mwili, tunakaa mbali na Bwana” (2Kor 5:6) na sisi wenyewe tulio
na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu (taz. Rum 8:23) na
tunatamani kwenda zetu tukae na Kristo (Flp 1:23). Upendo wenyewe
hutubidisha tuishi zaidi kwa ajili yake Yeye aliyekufa na kufufuka (taz.
2Kor 5:15). Kwa hiyo twajitahidi kumpendeza Bwana katika yote (taz. 2Kor
5:9) na twazivaa silaha zote za Mungu tupate kuweza kuzipinga hila za
shetani na kushindana siku ya uovu (taz. Efe 6:11-13). Kwa kuwa hatujui siku
wala saa yatupasa kukesha daima kama Bwana anavyotuonya ili, ikishamalizika
safari iliyo moja tu ya maisha yetu duniani (taz. Ebr 9:27), tustahili
kuingia pamoja naye katika karamu ya arusi na kuhesabiwa miongoni mwao
waliobarikiwa [na Mungu] (taz. Mt 25:31-46) na wala asituamuru kama watumwa
wabaya na walegevu (taz. Mt 25:26) kwenda katika moto wa milele (taz. Mt
25:41) na katika giza la nje ambako “ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”
(Mt 22:13 na 25:30). Kwa maana, kabla ya kutawala pamoja na Kristo mtukufu,
sisi sote tutadhihirishwa “mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu
apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni
mema au mabaya” (2Kor 5:10), na mwisho wa dunia “watatoka, wale waliofanya
mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu”
(Yn 5:29; taz. Mt 25:46). Basi tukiyahesabu “mateso ya wakati huu wa sasa
kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu” (Rum 8:18; taz. 2Tim
2:11-12), kwa imani thabiti twalitazamia “tumaini lenye baraka na mafunuo ya
utukufu wa Kristo Yesu, Mungu Mkuu na Mwokozi wetu” (Tit 2:13),
“atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa
utukufu” (Flp 3:21), na atakayekuja “ili kutukuzwa katika watakatifu wake,
na kustaajabiwa katika wote waliosadiki” (2The 1:10).
Ushirika wa Kanisa la mbinguni na Kanisa linalosafiri
49. Mpaka Bwana atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote pamoja
naye (taz. Mt 25:31), na vitu vyote kutiishwa chini ya miguu yake baada ya
kubatilishwa mauti (taz. 1Kor 15:26-27), wanafunzi wake wengine husafiri
duniani, wengine walioaga dunia hii hutakaswa, na wengine wanatukuzwa
wakimtazama katika nuru timilifu Mungu huyu mmoja katika nafsi tatu, jinsi
alivyo[147]Lakini sisi
sote, ingawa kwa hatua na namna mbalimbali, tunashirikiana katika upendo
uleule wa Mungu na jirani na kumwimbia Mungu wetu utenzi uleule wa utukufu.
Kwa maana wale wote walio wa Kristo, walio na Roho wake, waungamanishwa
katika Kanisa moja na kushikanishwa katika Yeye (taz. Efe 4:16). Kwa hiyo,
umoja wa wale wanaosafiri duniani na wa ndugu waliolala katika amani ya
Kristo haukatiki hata kidogo, kinyume chake, kadiri ya imani ya daima ya
Kanisa [umoja huo] huimarishwa kwa kubadilishana mema ya kiroho[148].
Hivyo wale walio mbinguni, kwa kuwa wameunganika na Kristo kwa undani zaidi,
wanaliimarisha Kanisa lote katika utakatifu kwa uthabiti zaidi, wanakuza
ibada zinazotolewa nalo kwa Mungu hapa duniani na kusaidia kulijenga zaidi
na zaidi kwa njia mbalimbali (taz. 1Kor 12:12-27)[149].
Kwa maana, baada ya kupokelewa mbinguni na kukaa pamoja na Bwana (taz. 2Kor
5:8), kwa njia yake, pamoja naye na ndani yake, hawaachi kutuombea kwa Baba[150],
wakimtolea mastahili yao waliyojipatia duniani kwa njia ya Kristo Yesu aliye
Mpatanishi pekee kati ya Mungu na wanadamu (taz. 1Tim 2:5), kwa kumtumikia
Bwana katika yote na kuyatimiliza katika miili yao yale yaliyopungua ya
mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, yaani, Kanisa (taz. Kol 1:24)[151].
Hivyo udhaifu wetu husaidiwa sana na juhudi yao ya kidugu.
Mahusiano kati ya Kanisa linalosafiri duniani na Kanisa la mbinguni
50. Kanisa la wale wanaosafiri, huku likiufahamu vizuri ushirika
huu wa Mwili mzima wa Fumbo wa Yesu Kristo, tangu awali ya dini ya kikristo
lilikuza kwa heshima kubwa ukumbusho wa marehemu[152]
na, kwa sababu “ni wazo takatifu na la kicho kufanya upatanisho kwa wafu ili
wafunguliwe dhambi zao” (taz. 2Mak 12:46), likatolea maombezi kwa ajili yao.
Kanisa limesadiki daima kwamba mitume na mashahidi wa Kristo, waliotoa
ushuhuda mkubwa wa imani na mapendo kwa kumwaga damu yao, wameunganika nasi
kwa namna ya pekee katika Kristo; likawaheshimu kwa upendo wa pekee pamoja
na Bikira Maria Mwenye heri na malaika watakatifu[153]
na kuwaomba kwa uchaji msaada wa maombezi yao. Baadaye wamehesabika pamoja
nao wengine pia walioiga kwa karibu zaidi ubikira na umaskini wa Kristo[154],
na mwishowe wengine ambao utimizaji wao bora wa fadhila za kikristo[155]
na karama za Mungu ziliwapendekeza kwa waamini hata wawaheshimu kwa utauwa
na kuwaiga[156].
Kwa maana tukiangalia maisha ya wale waliomfuata Kristo kiaminifu,
tunahimizwa upya kuutafuta Mji ule ujao (taz. Ebr 13:14 na 11:10), na pamoja
na hayo twafundishwa njia salama kabisa ya kuufikia, kati ya mabadiliko ya
ulimwengu, umoja kamili na Kristo, ndio utakatifu, kila mmoja kadiri ya wito
wake na hali yake[157].
Katika maisha ya wale wanaobadilishwa wafanane kikamilifu zaidi na mfano wa
Kristo (taz. 2Kor 3:18), ijapo wanashiriki hali yetu ya kibinadamu, Mungu
huwadhihirishia watu wazi uwepo wake na uso wake. Ndani yao Yeye mwenyewe
husema nasi na kutuonyesha alama ya Ufalme wake[158],
ambao tunavutwa kwake kwa nguvu, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la
mashahidi namna hii (taz. Ebr 12:1) na kuwa na ushuhuda wa namna hii wa
ukweli wa Injili.
Lakini hatuheshimu kumbukumbu ya watakatifu wa mbinguni kwa sababu ya mfano
[wao] tu, bali zaidi ili umoja wa Kanisa zima katika Roho [Mtakatifu]
uimarishwe kwa zoezi la mapendo ya kidugu (taz. Efe 4:16). Kwani, kama vile
ushirika kati ya [wakristo] wasafirio [duniani] unavyotusogeza karibu zaidi
na Kristo, vivyo hivyo umoja na watakatifu unatuunganisha na Kristo, ambaye
kwake yeye, kama Chemchemi na Kichwa, hutoka neema zote na uzima wenyewe wa
taifa la Mungu[159]. Kwa hiyo
yafaa kabisa tuwapende rafiki hawa wa Yesu Kristo na warithi pamoja naye,
walio ndugu na wafadhili wetu wakuu, na tumshukuru Mungu ipasavyo kwa ajili
yao[160] na “tuwasihi sana na
kuyakimbilia maombezi yao, nguvu zao na msaada wao ili tujaliwe na Mungu
fadhili zake kwa njia ya Mwana wake Yesu Kristo, Bwana wetu aliye peke yake
Mkombozi wetu na Mwokozi wetu”[161].
Kwa maana kila kielezo halisi cha upendo wetu kwa ajili ya watakatifu,
kadiri ya tabia yake, humwelekea Kristo na kutekelezwa kwake yeye aliye
“taji la watakatifu wote”[162],
na kwa njia yake kwa Mungu aliye wa ajabu katika watakatifu wake na
kutukuzwa ndani yao[163].
Umoja wetu na Kanisa la mbinguni hutimizwa kwa njia bora tunapoadhimisha
sifa ya Mungu Mwenyezi kwa shangwe moja, hasa katika Liturujia takatifu,
ambamo uwezo wa Roho Mtakatifu hutenda kazi ndani yetu kwa ishara za
sakramenti[164], na sisi
sote, watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa tulionunuliwa kwa damu
ya Kristo (taz. Ufu 5:9), tuliokusanyika katika Kanisa moja, twamtukuza
Mungu aliye Mmoja na Utatu Mtakatifu kwa wimbo mmoja wa sifa. Kwa hiyo
katika kuadhimisha sadaka ya Ekaristi tunaunganika sana na ibada ya Kanisa
la mbinguni tukishirikiana nalo, na tukimheshimu na kumkumbuka kwanza Maria
mtukufu Bikira daima, na pia Yusufu mwenye heri, na Mitume na mashahidi
wenye heri na watakatifu wote[165].
Maagizo ya kichungaji ya Mtaguso Mkuu
51. Mtaguso huu Mtakatifu huipokea kwa utauwa mkubwa imani hii
stahivu ya mababa wetu mintarafu muungano wetu wenye uhai na ndugu ambao
wapo katika utukufu wa mbinguni au wapo bado katika kutakaswa baada ya kufa
kwao, na kukumbusha tena Maagizo ya Mtaguso wa pili wa Nikea[166],
ya Mtaguso wa Florenzia[167]
na Trento[168]. Pamoja na
haya kwa bidii yake ya kichungaji unawaonya wote wanaohusika wajitahidi
kuepuka au kusahihisha desturi mbaya, mambo yapitayo kiasi au yaliyo na
mapungufu fulani, ambayo labda yameingia hapa na pale, na wayatengeneze upya
yote, ili Kristo na Mungu wasifiwe kikamilifu zaidi. Wawafundishe waamini
kwamba heshima ya kweli ya watakatifu (sanctorum cultum) hutegemea
siyo wingi wa matendo mbalimbali ya nje, bali nguvu ya upendo wetu wenye
utendaji, ambao kwao twatafuta, kwa manufaa yetu na ya Kanisa, “mfano katika
maisha yao, urafiki kwa kuungana nao na msaada kwa njia ya maombezi yao”[169].
Kwa upande mwingine yapasa kuwafundisha waamini kwamba uhusiano wetu na wale
[watakatifu] walio mbinguni, mradi umefahamika katika mwanga mkubwa zaidi wa
imani, haupunguzi ibada ya kumwabudu Mungu Baba itolewayo kwake kwa njia ya
Kristo katika Roho, bali kinyume chake huzidi kuisitawisha[170].
Kwa maana sisi sote tulio watoto wa Mungu na kuwa familia moja katika
Kristo (taz. Ebr 3:6), tunaposhirikiana sisi kwa sisi katika kupendana na
katika kutoa sifa moja kwa Utatu Mtakatifu, tunaitikia wito halisi wa Kanisa
na kushiriki Liturujia ya utukufu kamili, tukiionja tangu sasa[171].
Kwa maana Kristo atakapotokea na wafu wakifufuka kwa utukufu, fahari ya
Mungu itautilia nuru mji wa mbinguni na taa yake itakuwa ni Mwanakondoo
(taz. Ufu 21:23). Ndipo Kanisa lote la watakatifu, katika heri kubwa ya
mapendo, litakapomwabudu Mungu na “Mwanakondoo aliyechinjwa” (Ufu 5:12)
likitangaza kwa sauti moja: “Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye
aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwanakondoo, hata milele na milele”
(Ufu 5:13).
Sura ya nane
BIKIRA MARIA MWENYE HERI MAMA WA MUNGU
KATIKA FUMBO LA KRISTO NA LA KANISA
I. UTANGULIZI
52. Mungu mwenye fadhili na hekima tele, akitaka kuutimiza ukombozi wa
ulimwengu, “ulipowadia utimilifu wa wakati alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa
na mwanamke... ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana” (Gal 4:4-5). Naye
“ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu
wetu, akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria”[172].
Fumbo hili la wokovu la Mungu limefunuliwa kwetu na kuendelezwa katika
Kanisa, ambalo Bwana ameweka kuwa mwili wake, na ndani yake waamini,
wanaoambatana na Kristo aliye Kichwa [chao] na kushirikiana na watakatifu
wake wote, wapaswa pia “kumheshimu kwanza Maria mtukufu daima Bikira, Mama
wa Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo”[173].
Maria na Kanisa
53. Bikira Maria, aliyepokea kwa ujumbe wa Malaika Neno wa Mungu moyoni
mwake na mwilini mwake na kuuletea ulimwengu Uzima, anatambuliwa na
kuheshimiwa kuwa kweli Mama wa Mungu na wa Mkombozi. Yeye aliyekombolewa kwa
njia bora sana kwa kutazamiwa mastahili ya Mwanae, na kuunganika naye kwa
kifungo imara kisichofungulika, amejaliwa cheo kikuu na hadhi ya kuwa Mzazi
wa Mwana wa Mungu, na kwa sababu hiyo ndiye binti mpenzi wa Baba na hekalu
la Roho Mtakatifu. Kwa ajili ya kipaji hiki cha neema kuu anavizidi sana
viumbe vingine vyote vilivyo mbinguni na duniani. Pamoja na hayo anaonekana
ameunganika, katika uzao wa Adamu, na watu wote wanaohitaji wokovu; na
zaidi, yeye ni pia “mama kweli wa viungo (vya Kristo) ... kwa sababu …
alishiriki kwa mapendo yake ili waamini wazaliwe katika Kanisa, ambao ndio
viungo vya Kichwa hicho[174].
Kwa sababu hiyo husalimiwa kama kiungo kikuu na cha pekee cha Kanisa na
mfano wake mtimilifu (typus) na kielelezo (exemplar) chake
bora sana katika imani na katika mapendo; na Kanisa katoliki, likifundishwa
na Roho Mtakatifu, humheshimu kwa upendo na heshima wa kimwana kama mama
yake mpenzi sana.
Madhumuni ya Mtaguso Mkuu
54. Mtaguso Mkuu katika kutoa mafundisho mintarafu Kanisa ambamo Mkombozi
Mungu hutenda wokovu, unanuia kueleza kwa uangalifu dhima ya Bikira Mwenye
heri katika fumbo la Neno aliyefanyika mwili na la Mwili wake wa fumbo. Pia
[unataka kufafanua] wajibu wa watu waliokombolewa kumhusu Mama wa Mungu (Deiparam),
aliye mama wa Kristo na mama wa wanadamu, hasa wa waamini. Lakini Mtaguso
hauna nia ya kutoa mafundisho yaliyotimilika juu ya Maria, wala kukata
masuala yasiyoelezwa bado wazi na kazi ya wanateolojia. Kwa hiyo yanabaki
halali (in suo iure) maoni yapendekezwayo katika shule katoliki
mintarafu yule anayeshika katika Kanisa takatifu mahali pa kwanza baada ya
Kristo, na pa karibu zaidi nasi[175].
II. DHIMA YA BIKIRA MARIA KATIKA MPANGO WA WOKOVU
Mama wa Masiya katika Agano la Kale
55. Maandiko Matakatifu ya Agano la Kale na ya Agano Jipya na Mapokeo ya
kale yaonyesha wazi zaidi na zaidi dhima ya Mama wa Mwokozi katika mpango wa
wokovu, na kuiweka mbele yetu tuifikirie. Vitabu vya Agano la Kale vyaeleza
historia ya wokovu ambayo ndani yake hutayarishwa polepole ujio wa Kristo
ulimwenguni. Maandiko hayo ya Kale, yanavyosomwa katika Kanisa na kufahamika
katika mwanga wa ufunuo kamili wa baadaye, hatua kwa hatua yabainisha zaidi
na zaidi sura ya yule mwanamke aliye Mama wa Mkombozi. Katika mwanga huu
anabashiriwa kinabii katika ahadi ya ushindi juu ya nyoka waliyopewa wazazi
wa kwanza baada ya kutenda dhambi (taz. Mwa 3:15). Vilevile yeye ni Bikira
yule atakayepata mimba na kumzaa Mtoto mwanamume ambaye jina lake ataitwa
Emanueli (taz. Isa 7:14; Mik 5:2-3; Mt 1:22-23). Yeye anashika nafasi ya
kwanza miongoni mwa wanyenyekevu na maskini wa Bwana, ambao, kwa matumaini
ya imani wanangojea na wanapata wokovu kwake. Hatimaye, kwa yeye, Binti
mtukufu wa Sayuni aliye bora sana, baada ya kungojea ahadi kwa muda mrefu,
nyakati zilitimia na mpango mpya wa wokovu ukawekwa, hapo Mwana wa Mungu
alipotwaa maumbile ya kibinadamu kutoka kwake, ili amkomboe mwanadamu katika
dhambi kwa mafumbo ya mwili wake.
Maria katika kutangazwa habari njema
56. Mungu wa huruma alitaka Umwilisho utanguliwe na ukubali wake yeye
aliyeteuliwa tangu milele awe Mama, ili kama vile mwanamke alivyoshiriki
kuileta mauti, kadhalika mwanamke asaidie kuuleta uzima. Hayo yamhusu kwa
namna ya pekee Mama wa Yesu aliyeuzalia ulimwengu Uzima wenyewe, utengenezao
yote upya, naye alitajirishwa na Mungu kwa karama zenye kustahili jukumu
hili kubwa hivi. Kwa hiyo hatuwezi kushangaa ikiwa Mababa Watakatifu
walizoea kumwita Mama wa Mungu kuwa “Mtakatifu kabisa”, bila doa lolote la
dhambi, kama aliyetengenezwa na Roho Mtakatifu na kufanywa kuwa kiumbe kipya[176].
Hali amepambwa tangu nukta ya kwanza ya kutungwa kwake mimba kwa mng’aro wa
utakatifu wa pekee kabisa, Bikira huyu wa Nazareti aliamkiwa na Malaika
mhubiri (Angelo nuntiante), kwa amri ya Mungu, kuwa “amejaa neema” (gratia
plena) (taz. Lk 1:28), naye akamjibu mjumbe wa mbinguni, “Tazama, mimi
ni mjakazi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyosema” (Lk 1:38). Hivyo Maria,
binti Adamu, kwa kulikubali Neno la Mungu amekuwa Mama wa Yesu, na
akiyakumbatia kwa roho yake yote, na bila kushikwa na dhambi yoyote, mapenzi
ya Mungu yenye wokovu, akajitoa kabisa kama mjakazi wa Bwana kwa ajili ya
nafsi ya Mwanawe na kwa kazi yake, akilihudumia fumbo la ukombozi chini yake
na pamoja naye, kwa neema ya Mungu Mwenyezi. Kwa hiyo Mababa Watukufu huona
kwa haki kuwa Maria hakutumiwa na Mungu katika hali ya kutendwa tu, bali
alishiriki kuleta wokovu wa binadamu kwa imani [yake] na utii [wake] wa
hiari. Kwa maana, kama vile Mt. Ireneus asemavyo, yeye “kwa kutii amekuwa
sababu ya wokovu kwa ajili yake na kwa ajili ya kizazi chote cha wanadamu”[177].
Ndiyo sababu, Mababa wa Kanisa wasio wachache hupenda kueleza katika
mahubiri yao kwamba “fundo la kutotii kwa Hawa limefunguliwa kwa utii wa
Maria; na kile ambacho Hawa bikira alifunga kwa kutosadiki kwake, Bikira
Maria alikifungua kwa imani yake”[178].
Wakimfananisha [Maria] na Hawa, wanamwita Maria “Mama wa walio hai”[179],
na mara nyingi wanatangaza, “Mauti kwa njia ya Hawa; kwa njia ya Maria
uzima”[180].
Maria wakati wa utoto wa Yesu
57. Umoja huu wa Maria na Mwanawe katika kazi ya wokovu unaonekana tangu
dakika ile Bikira alipotunga mimba Kristo mpaka kifo chake. Kwanza, Maria
alipoondoka kwenda kwa haraka kumwamkia Elisabeti akasalimiwa naye kuwa
mwenye heri kwa imani yake katika wokovu ulioahidiwa, na mtangulizi akaruka
ndani ya tumbo la mama yake (taz. Lk 1:41-45); tena, wakati wa kuzaa, Mama
wa Mungu alipowaonyesha wachungaji na mamajuzi kwa furaha Mwana wake mzaliwa
wa kwanza, asiyepunguza ukamilifu wa ubikira wake, bali akautakatifuza[181].
Na alipomtolea Bwana hekaluni, pamoja na sadaka ya maskini, alimsikia
Simeoni akiagua kwamba Mwanae atakuwa ishara itakayonenewa, na kwamba upanga
utaingia moyoni mwake mama ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi (taz. Lk
2:34-35). Walipomkosa mtoto Yesu na kumtafuta kwa huzuni, wazazi wake
wakamwona hekaluni akiyashughulikia yale yaliyo ya Baba yake, wala
hawakuelewa na neno la Mwana. Lakini mama yake aliyaweka haya yote moyoni
mwake akiyatafakari (taz. Lk 2:41-51).
Maria katika maisha ya hadharani ya Yesu
58. Katika maisha ya hadharani ya Yesu, mama yake alijionyesha tangu
mwanzo kwa njia ya pekee katika arusi ya Kana ya Galilaya, aliposababisha
kwa huruma yake chanzo cha ishara za Yesu aliye Masiya, kwa njia ya maombezi
yake (taz. Yn 2:1-11). Wakati wa kuhubiri kwake Mwanae, alipokea maneno
ambayo kwayo yeye, akiuinua Ufalme juu ya mahusiano na vifungo vya mwili na
damu, alitangaza kuwa wenye heri wale wanaolisikia na kulitunza Neno la
Mungu (taz. Mk 3:35; Lk 11:27-28), kama alivyofanya Maria kwa uaminifu (taz.
Lk 2:19 na 51). Hivyo Bikira Maria pia aliendelea mbele katika safari ya
imani, alihifadhi kwa uaminifu muungano wake na Mwanawe, mpaka kufika penye
msalaba (taz. Yn 19:25), ambapo alisimama imara, kwa mpango wa Mungu;
aliteswa kikatili pamoja na Mwanawe wa pekee, na alijiunganisha kwa moyo
wake wa kimama na sadaka yake. Alikubali kwa upendo sadaka aliyojitoa yule
dhabihu aliyemzaa mwenyewe. Mwishowe alikabidhiwa na Yesu mwenyewe akifa
msalabani kama mama yake kwa mwanafunzi kwa maneno haya, “Mama, tazama
mwanao” (taz. Yn 19:26-27)[182].
Maria baada ya kupaa kwake Bwana
59. Kwa kuwa ilimpendeza Mungu sakramenti ya wokovu wa wanadamu
isidhihirishwe kitukufu kabla ya kumimina Roho aliyeahidiwa na Kristo,
tunawaona Mitume kabla ya siku ya Pentekoste “wakidumu kwa moyo mmoja katika
kusali, pamoja nao wanawake na Maria, Mama yake Yesu, na ndugu zake” (Mdo
1:14). Hata Maria aliomba kwa sala zake paji la Roho ambaye alimfunika
tayari kama kivuli siku ya kutangazwa kwake. Mwishowe, Bikira asiye na doa,
aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili[183],
akishamaliza mwendo wa maisha yake duniani, aliinuliwa katika utukufu wa
mbinguni pamoja na mwili [wake] na pamoja na roho [yake][184];
akatukuzwa na Bwana kama Malkia wa ulimwengu, ili afananishwe kikamilifu
zaidi na Mwanawe, aliye Bwana wa mabwana (taz. Ufu 19:16) na mshindi wa
dhambi na mauti[185].
III. BIKIRA MWENYE HERI NA KANISA
Kristo aliye mpatanishi wa pekee na Maria
60. Mpatanishi wetu ni mmoja tu kadiri ya maneno ya Mtume, “Mungu ni
mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo
Yesu, ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote” (1Tim
2:5-6). Huduma ya kimama ya Maria kwa watu haiutilii giza upatanisho huu wa
pekee wa Kristo, wala kuupunguza kwa namna yoyote ile, bali yaonyesha nguvu
zake. Kwa kweli kila mvuto wa wokovu kwa upande wa Bikira Mwenye heri kwa
watu hautoki katika lazima fulani bali katika mapenzi ya Mungu, na
kububujika kutoka wingi wa mastahili ya Kristo. Una msingi wake katika
upatanisho wake, na huutegemea kabisa, huchota toka humo nguvu yake yote,
wala hauzuii kwa namna yoyote muungano wa moja kwa moja wa waamini na
Kristo, bali unausaidia.
Maria anashiriki katika kazi ya ukombozi
61. Bikira Mwenye heri aliyeteuliwa tangu milele kuwa Mama wa Mungu,
pamoja na [azimio la] umwilisho wa Neno wa Mungu, kwa mpango wa Maongozi ya
Mungu amekuwa hapa duniani Mama Mtukufu wa Mkombozi aliye Mungu, mwenzi
mwenye moyo mkuu kwa namna ya pekee kuliko wote, na mjakazi mnyenyekevu wa
Bwana. Kwa kumtunga mimba na kumzaa Kristo, kwa kumlisha, kumtolea kwa Baba
hekaluni, kwa kuteswa pamoja na Mwanae aliyekufa msalabani, alishiriki kwa
namna iliyo ya pekee kabisa kazi ya Mwokozi kwa utii wake na imani,
matumaini na mapendo yake yenye kuwaka, ili uzima wa kimungu utengenezwe
upya katika roho [za wanadamu]. Kwa sababu hiyo amekuwa mama kwa ajili yetu
katika mpango wa neema.
Mwombezi kwa ajili ya wokovu
62. Umama huu wa Maria katika mpango wa neema unadumu bila kukatizwa
tangu nukta ile ya ukubali aliotoa kwa imani wakati wa tangazo [la kuzaliwa
Bwana] na alioushikilia bila kusita chini ya msalaba, hadi ukamilifu wa
milele wa wateule wote. Kwa kweli, akiwa amepalizwa mbinguni, hakuacha
huduma hii ya wokovu, bali kwa njia ya maombezi yake ya namna nyingi
anaendelea kupata kwa ajili yetu mapaji ya wokovu wa milele[186].
Kwa mapendo yake ya kimama, huwaangalia ndugu wa Mwanawe wanaohiji bado na
kuishi katika hatari na taabu, mpaka watakapofikishwa kwenye makao yenye
furaha. Kwa sababu hiyo, Bikira mwenye heri huombwa katika Kanisa kwa majina
haya ya heshima: Mtetezi, Msaidizi, Mfadhili na Mpatanishi[187].
Lakini haya yaeleweke vizuri, ili kitu chochote kisipunguze au kuongeza
hadhi na uwezo wa Kristo aliye Mpatanishi peke yake[188].
Kwa maana hakuna kiumbe chochote kiwezacho kulinganishwa na Neno
aliyejifanya mwili na Mkombozi; lakini kama vile ukuhani wa Kristo
unavyoshirikishwa kwa namna mbalimbali kwa wahudumu [watakatifu] na kwa watu
waamini, na kama vile wema wa pekee wa Mungu unavyoenea kweli kwa namna
mbalimbali katika viumbe, ndivyo upatanisho pekee wa Mkombozi hauzuii, bali
unaamsha katika viumbe ushirikiano wa namna mbalimbali unaochotwa katika
chemchemi moja tu.
Kanisa halisiti kuikiri wazi huduma hii ya Maria iliyowekwa chini [ya ile
ya Kristo], huionja daima na kuikabidhi mioyoni mwa waamini, ili,
wakitegemezwa na msaada huu wa kimama, waambatane kwa undani zaidi na
Mpatanishi na Mkombozi.
Maria bikira na mama, mfano mtimilifu wa Kanisa
63. Bikira Mwenye heri, kwa kipaji na dhima ya umama wa kimungu
unaomwunganisha na Mwanae Mkombozi, na kwa neema zake na huduma zake za
pekee, ameunganika pia kwa undani na Kanisa. Mama wa Mungu ni kielezo (typus)
cha Kanisa, kwa habari ya imani, mapendo na umoja kamili na Kristo, kama
alivyowahi kufundisha Mt. Ambrosi[189].
Kwa maana katika fumbo la Kanisa ambalo pia laitwa kwa haki mama na bikira,
Bikira Maria mwenye heri ametangulia kwa njia bora na ya pekee kutoa mfano
wa kuwa bikira na kuwa mama[190].
Katika kuamini na kutii kwake alimzaa duniani Mwana mwenyewe wa Baba,
asimjue mtu, akitiwa kivuli na Roho Mtakatifu, akiwa kama Hawa mpya
asiyemwamini nyoka wa zamani, bali amwaminiye mjumbe wa Mungu kwa imani
isiyochafuliwa na shaka lolote. Akamzaa Mwana ambaye Mungu alimweka [awe]
mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi (taz. Rum 8:29), yaani waamini,
ambao Maria anashiriki kwa upendo wa kimama katika kuzaliwa kwao na kulelewa
kwao.
Kanisa bikira na mama
64. Hata Kanisa, kwa kuutazama utakatifu wenye siri wa Maria, na kuyaiga
mapendo yake na kuyatimiza kiaminifu mapenzi ya Baba, kwa kulipokea Neno la
Mungu kwa uaminifu, linakuwa pia mama; kwani kwa mahubiri na ubatizo linazaa
watoto waliotungwa kwa [uwezo wa] Roho Mtakatifu na kuzaliwa kwa Mungu, kwa
uzima mpya usiokufa. Nalo pia ni Bikira anayehifadhi kwa ukamilifu na usafi
wa moyo ile imani aliyomwahidia Bwanaarusi wake, na kwa kumwiga Mama wa
Bwana wake, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, hutunza kibikira (virginaliter)
imani kamili, tumaini thabiti na mapendo manyofu[191].
Kanisa linapaswa kuuiga utakatifu wa Maria
65. Kanisa limekwisha kuufikia, ndani ya nafsi ya Bikira mwenye heri sana
ukamilifu unaoliweka kuwa bila waa wala kunyanzi (taz. Efe 5:27); ila
waamini wa Kristo wanajibidisha bado kukua katika utakatifu wakishinda
dhambi. Kwa sababu hiyo wayainua macho yao kwa Maria anayeng’aa mbele ya
jumuiya ya wateule kama mfano wa fadhila. Kanisa likimfikiria yeye kwa
utauwa na kumtazama katika mwanga wa Neno aliyefanyika mwili, hupenya kwa
heshima na kwa undani zaidi fumbo kuu la umwilisho, na kupata kufanana zaidi
na zaidi na Bwanaarusi wake. Maana Maria, aliyeingia kabisa ndani ya
historia ya wokovu, anaunganisha ndani yake kwa namna fulani maazimio (placita)
makuu ya imani na kuyaakisi kama kioo; hivyo, anapohubiriwa na kuheshimiwa,
huwavuta waamini kwa Mwanawe, kwa sadaka yake na kwa upendo wa Baba. Nalo
Kanisa, likiufuatia utukufu wa Kristo, lapata kufanana zaidi na zaidi na
kielezo (typus) chake kitukufu, na kuendelea bila kukoma katika
imani, matumaini na mapendo, likitafuta na kuyashika mapenzi ya Mungu katika
yote. Kwa hiyo Kanisa, pia katika kazi yake ya kitume, linamtazama kwa haki
yeye aliyemzaa Kristo ambaye alichukuliwa mimba kwa Roho Mtakatifu na
kuzaliwa na Bikira, kusudi [halafu] azaliwe na kukua katika mioyo ya waamini
kwa njia ya Kanisa. Bikira huyo alikuwa katika maisha yake kielezo cha ule
upendo wa kimama ambao wapaswa kuwa nao rohoni wale wote wanaoshiriki katika
kazi ya utume ya Kanisa ili watu wazaliwe upya.
IV. IBADA KWA BIKIRA MARIA KATIKA KANISA
Tabia na msingi wa ibada
66. Maria alitukuzwa kwa neema ya Mungu, baada ya Mwanawe, kupita malaika
wote na wanadamu wote, kwa maana yeye ni Mama mtakatifu sana wa Mungu
aliyeshiriki mafumbo ya Kristo. [Kwa sababu hiyo Bikira Maria] anaheshimiwa
kwa haki na Kanisa kwa ibada ya pekee. Kwa kweli, tangu nyakati za kale
zaidi, Bikira Mwenye heri anaheshimiwa kwa cheo cha “Deipara” [yaani “Mama
wa Mungu”], nao waamini wanaukimbilia ulinzi wake, wakimwomba katika hatari
zao zote na mahitaji yao[192].
Hasa tokea Mtaguso wa Efeso ibada ya taifa la Mungu kwa Maria imekua kwa
njia ya ajabu katika kumheshimu na kumpenda, katika kumwomba na kumwiga,
kadiri ya maneno yake mwenyewe yenye utabiri, “Vizazi vyote wataniita
mbarikiwa, kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu” (Lk 1:48-49). Ibada
hiyo, kama ilivyokuwa daima katika Kanisa, ingawa ni ya pekee kabisa, ni
tofauti kimsingi na ibada ya kuabudu inayotolewa kwa Neno aliyejifanya
mwili, pia kwa Baba na kwa Roho Mtakatifu; na ibada [kwa Maria] pia inaikuza
[ibada ile ya kuabudu]. Aina mbalimbali za heshima kwa Mama wa Mungu ambazo
Kanisa amezikubali kufuatana na mafundisho yenye uzima na halisi, kadiri ya
mazingira ya nyakati na mahali, kadiri ya tabia na hali za waamini, zaleta
kwamba, Mama anapoheshimiwa, Mwana hupata kujulishwa, kupendwa na kutukuzwa
inavyostahili, na amri zake kushikwa, kwa kuwa katika Yeye vitu vyote
viliumbwa (taz. Kol 1:15-16) na “katika yeye ilimpendeza Baba wa milele
utimilifu wote ukae” (Kol 1:19).
Kanuni za kichungaji
67. Mtaguso Mtakatifu unatoa mafundisho hayo ya kikatoliki baada ya
kufikiri sana, na wakati huohuo unawaonya wana wote wa Kanisa wahamasishe
kwa moyo mkuu ibada kwa Bikira Mwenye heri, hasa ile ya kiliturujia.
Wathamini sana desturi na mazoezi ya ibada kwake, vilivyopendekezwa na
Majisterio [ya Kanisa] katika mfululizo wa karne, na washike kwa makini yale
yaliyoamriwa zamani juu ya kuziheshimu sanamu (de cultu imaginum) za
Kristo, za Bikira Maria na za watakatifu[193].
Tena unawaonya sana wanateolojia na wahubiri wa Neno la Mungu waepukane kwa
makini na kila chuku ya uongo (falsa superlatione), pia na choyo ya
akili (a nimia mentis angustia) katika kuheshimu hadhi ya pekee ya
Mama wa Mungu[194]. Kwa
kusoma Maandiko Matakatifu, vitabu vya Mababa na vya Walimu Watakatifu, na
kuchunguza Liturujia za Kanisa chini ya uongozi wa Majisterio, waeleze sawa
majukumu na majaliwa ya Bikira Mwenye heri, ambayo kikomo chake daima ni
Kristo, ambaye ni asili ya ukweli wote, utakatifu wote na utauwa wote.
Wajihadhari sana wasije wakawakosesha kwa maneno na kwa matendo ndugu
waliojitenga au watu wengine kuhusu mafundisho ya kweli ya Kanisa. Waamini,
kwa upande wao, wakumbuke kwamba ibada ya kweli si kuwa na vionjo (affectu)
vipitavyo tu visivyo na matunda, wala si wepesi wa kuamini bila ushuhuda,
bali hutokana na imani ya kweli ambayo twaongozwa nayo kuutambua ubora wa
Mama wa Mungu, na kuhimizwa kumpenda kimwana huyo Mama yetu na kuziiga
fadhila zake.
V. MARIA NI ISHARA NA TUMAINI THABITI
NA YA FARAJA KWA TAIFA LA MUNGU LISAFIRILO
Maria ni ishara ya taifa la Mungu
68. Mama wa Yesu, akiwa amekwisha tukuzwa mbinguni mwili na roho, ni sura
na mwanzo wa Kanisa ambalo litapata utimilifu wake katika ulimwengu ujao.
Kadhalika anang’aa duniani kama alama ya hakika ya matumaini na ya faraja
kwa taifa la Mungu lililo safarini, mpaka siku ya Bwana itakapokuja (taz.
2Pet 3:10).
Maria auombee umoja wa wakristo
69. Mtaguso huu Mkuu unaona furaha kubwa na faraja kwa kuwa hata kati ya
ndugu waliojitenga hawakosi kuwapo wanaomtolea Mama wa Bwana na Mwokozi
heshima stahili, hasa kati ya wakristo wa Mashariki, wanaoshirikiana nasi
katika kumheshimu Mama wa Mungu aliye Bikira daima, kwa bidii ya ari na moyo
wa ibada[195]. Waamini wote
wakristo wamsihi kwa nguvu Mama wa Mungu na Mama wa wanadamu, ili yeye
aliyeusaidia mwanzo wa Kanisa kwa maombezi yake, pia sasa aliyetukuzwa
mbinguni, juu ya Wenye heri na Malaika, awaombee kwa Mwanawe katika Ushirika
wa Watakatifu wote, mpaka jamaa zote za mataifa zilizopambwa jina la Kristo
au zisizomjua bado Mwokozi wao, zikusanyike kwa furaha kuwa Taifa moja la
Mungu katika amani na mapatano, kwa utukufu wa Utatu Mtakatifu sana
usiogawanyika.
Mambo yote yaliyoamuliwa katika konstitusio hii, na kila moja kati
yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume
tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho
Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote
yaliyoamuliwa kwa pamoja katika Sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa utukufu wa
Mungu.
Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 21 Novemba 1964
Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki
(zinafuata sahihi za Mababa)
______________
Kutoka maandishi ya Mtaguso Mkuu Vatikano II (Taarifa zilizotolewa na
Katibu wa Mtaguso katika mkusanyo wa 123, tarehe 16 novemba 1964).
Limeulizwa swali kuhusu maana ya kiteolojia ya mafundisho yaliyotolewa
katika kiwatiko (Schemate) juu ya Kanisa yenye kupigiwa kura ya maoni.
Kamati ya kimafundisho, kuhusu swali juu ya utathmini wa Hoja za
marekebisho (Modis) zihusuzo Sura ya Tatu ya kiwatiko juu ya Kanisa, imetoa
jibu hili lifuatalo:
“Kama ilivyo dhahiri kwa yenyewe, fasuli ya Mtaguso hutakiwa kufasiriwa
kulingana na kanuni za kawaida, zinazojulikana kwa wote.
Wakati huohuo kamati ya kimafundisho hurejesha kwenye Tamko lake la
tarehe 6 machi 1964, ambalo tunalinukulu hapa chini:
“Kulingana na desturi za Mitaguso na pia na malengo ya kichungaji ya
Mtaguso huu wa sasa, Sinodi hii takatifu huagiza kwamba ni yenye nguvu ya
faradhi yale tu ambayo, katika nyanja za dini na desturi, au maadili,
yenyewe itatamka wazi kuwa na tabia hiyo.
Mambo mengine ambayo Sinodi takatifu inapendekeza na kufundisha,
kama mafundisho ya Majisterio kuu ya Kanisa, waamini, wote na kila mmoja,
watakiwa kuyapokea na kuyashika kadiri ya nia ya Sinodi takatifu yenyewe,
nia ambayo inadhihirishwa katika mada yenyewe inayoongeleka na maneno
yenyewe yanayoielezea, kufuatana na kanuni za ufafanuzi wa kiteolojia”.
Kwa agizo la Mamlaka kuu yanatolewa kwa Mababa maelezo mafupi ya
utangulizi wa Hoja za marekebisho juu ya Sura ya Tatu ya kiwatiko juu ya
Kanisa. Kadiri ya nia na maneno ya maelezo hayo inabidi kufafanua na kuelewa
mafundisho yaliyotolewa katika sura hiyo ya tatu.
Maelezo mafupi ya utangulizi (Nota esplicativa praevia)
Kamati imeamua kutanguliza kabla ya kutazama Hoja za marekebisho,
maangalizo haya ya jumla:
1) Neno “Urika” halieleweki kwa maana iliyo “ya kisheria
finyufinyu”, kama kundi la walio sawa, ambao kabidhi mamlaka yao kwa mkuu
wao, bali kundi la kudumu ambalo muundo wake na mamlaka yake vinatakiwa
kukisiwa (deduci debet) kutoka kwa Ufunuo wa kimungu. Kwa hiyo katika
jibu kwa Hoja namba 12 inasemwa wazi juu ya Thenashara kwamba Bwana
aliwaweka “kama Urika au kundi la kudumu”. Taz. pia Hoja n. 53c. – Kwa
sababu hiyohiyo, mintarafu Urika wa Maaskofu hutumika pia maneno kama
“Daraja” (Ordo), au “Umoja” (Corpus). Ufanano kati ya Petro na
Mitume wengine kwa upande mmoja, na Baba Mtakatifu na Maaskofu kwa upande
mwingine, hauleti maana ya kurithishwa mamlaka ya pekee ya Mitume kwa
waandamizi wao, wala – kama ilivyo dhahiri – “usawa” (aequalitatem)
kati ya Kichwa na viungo vya Urika, ila tu uwiano (proportionalitatem)
kati ya uhusiano wa kwanza (Petro - Mitume) na uhusiano mwingine (Baba
Mtakatifu - Maaskofu). Kwa hiyo kamati imeamua kuandika katika n. 22 sio
jinsi “ileile” (eadem ratione), bali “iliyo sawa” (pari). Taz.
Hoja 57.
2) Mmoja anakuwa “mwanaurika” kwa njia ya kupewa uwakfu wa Daraja
ya Uaskofu, na ya ushirika wa kihierarkia na Mkuu wa Urika na viungo vyake.
Taz. n. 22 § 1, mwishoni.
Katika kuwekwa wakfu, Askofu hupewa ushirikiano halisi katika
majukumu “matakatifu”, kama inavyoonekana kutokana na mapokeo, pia ya
kiliturujia. Kwa kusudi limetumiwa neno “majukumu” (munerum), wala si
“mamlaka” (potestatum), kwa sababu hili la mwisho lingetambulika
pengine kama mamlaka “iliyo huru kutumiwa” (ad actum expedita).
Lakini, ili kuwepo uhuru huo wa kutumia mamlaka, inatakiwa liwepo “agizo
wazi la kisheria”, au la kikanisa (iuridica determinatio) kutoka kwa
mamlaka ya kihierarkia. Na agizo hilo juu ya mamlaka laweza kuhusu ama
idhini kwa ofisio maalum, ama kukabidhiwa kundi la waamini, nalo linatolewa
kadiri ya “miongozo” iliyoidhinishwa na mamlaka ya juu kabisa. Kanuni hii ya
nyongeza inadaiwa na hali halisi ya jambo lenyewe (ex natura rei),
kwa vile yanaongelewa hapa majukumu ya kutekelezwa na “watendaji wengi
wengi”, wanaoshirikiana katika ngazi ya kihierarkia, kwa mapenzi ya Kristo.
Ni dhahiri kwamba “ushirika” huo “katika maisha” ya Kanisa umetekelezwa hapo
awali kadiri ya mazingira ya nyakati, kabla ya kupangwa katika kanuni na
sheria (in iure).
Ndiyo sababu imesemwa wazi kwamba inatakiwa ushirika “wa kihierarkia” na
Kichwa cha Kanisa na viungo vyake. “Ushirika” ni neno lenye heshima sana
katika Kanisa la zamani (na hata sasa, hasa huko Mashariki). Kwa neno hili
halimaanishwi “upendo-hisia” wa juujuu, bali “utaratibu lenye mpangilio” (realitate
organica), udaio muundo wa kisheria na vilevile hutendwa na mapendo.
Kwa hiyo, kamati – kwa makubaliano ya wanakamati karibu wote –
imeamua iandikwe hivi: “Katika ushirika wa kihierarkia”. Taz. Hoja 40 na pia
yale yaliyosemwa juu ya “utume wa kikanisa” (missione canonica),
katika n. 24.
Hati za Mababa Watakatifu wa hivi karibuni mintarafu mamlaka ya
kisheria ya Maaskofu zinapaswa kufasiriwa kwa kuendana na hilo agizo juu ya
mamlaka linalotakiwa.
3) “Urika”, ambao haupo pasipo Kichwa, husemwa kuwa nao una
“mamlaka kubwa sana na kamili” juu ya Kanisa lote. Na jambo hilo lazima
likubalike, ili usiathiriwe utimilifu wa mamlaka ya Baba Mtakatifu. Maana,
Urika daima na kwa maumbile yake, unahusisha pia Kichwa, au Mkuu, wake
“ambaye katika Urika ana daima wadhifa wa Wakili wa Kristo na Mchungaji wa
Kanisa lote”. Kwa maneno mengine: kumeainishwa kati ya Baba Mtakatifu akiwa
peke yake, na Baba Mtakatifu akiwa pamoja na Maaskofu; sio baina ya Baba
Mtakatifu peke yake, na Maaskofu wakiwa wao pamoja. Lakini, kwa vile Baba
Mtakatifu wa Roma ni “Kichwa” (Caput) cha Urika, anao uwezo wa
kutenda matendo (actus) ambayo hayamo katika mamlaka ya Maaskofu,
k.v. kuitisha na kuongoza Urika, kuidhinisha kanuni za utendaji, n.k. Taz.
Hoja 81. Ni juu ya uamuzi wa Baba Mtakatifu, ambaye amekabidhiwa uangalizi
juu ya kundi lote la Kristo, kuelezea, kadiri ya mahitaji ya Kanisa
yanayobadilika katika mlolongo wa karne, kanuni za kutekeleza uangalizi huo,
ama kwa peke yake, ama kiurika. Baba Mtakatifu, katika kuamuru, kuhimiza,
kuidhinisha utendaji wa kiurika, anafuata utambuzi wake (discretionem)
akitazamia manufaa ya Kanisa.
4) Baba Mtakatifu, kama Mchungaji Mkuu wa Kanisa, anaweza kutumia
mamlaka yake wakati wowote kwa hiari yake, kadiri inavyodaiwa na majukumu
yake. Lakini Urika, ungawa daima upo, hata hivyo hautendi daima matendo ya
kiurika “kwelikweli” (stricte), kama inavyoonekana katika Mapokeo ya
Kanisa. Kwa maneno mengine: haupo daima “katika utendaji timilifu” (in
acto pleno); na kwa kweli unatenda kiurika kwelikweli kwa nafasi tu, na
“kwa kibali cha Kichwa” (consentiente Capite), inasemwa “kwa kibali
cha Kichwa” ili isifikiriwe kuwa ni suala la “kumtegemea mgeni”; neno
“kibali” linarejea kwenye maana ya “ushirika” uliopo kati ya Kichwa na
viungo, na inamaanisha kuwa “tendo” ambalo kwa asili ni ya Kichwa
lahitajika. Jambo hilo liko wazi katika n. 22, § 2, napo mwishoni
linaelezwa. Usemi wa kukanusha “isipokuwa” (nonnisi) inaelekea ibara
zote, kwa hiyo ni dhahiri kwamba “kanuni” zilizoidhinishwa na mamlaka ya juu
zatakiwa kushikwa daima. Taz. Hoja 84.
Lakini inaonekana katika sehemu zote kwamba unaongelewa “muungano”
(coniunctionem) wa Maaskofu na Kichwa chao, wala kamwe matendo ya
Maaskofu bila ya Baba Mtakatifu. Ingalikuwa hivyo, kwa vile ingekosekana
utendaji wa Kichwa, Maaskofu hawawezi kutenda kama Urika, kadiri
inavyoeleweka kwa maana yenyewe ya “Urika”. Hakika ushirika huo wa
kihierarkia wa Maaskofu wote na Baba Mtakatifu ni wa kawaida katika Mapokeo.
N.B. Bila ushirika wa kihierarkia majukumu ambayo yanaendana na
sakramenti na maumbile (munus sacramentale-ontologicum), ambayo ni
kitu kingine na maana ya kikanuni na kisheria (ab aspectu
canonico-iuridico), “hayawezi” kutekelezwa. Kamati imeona vema
kutokuingia katika masuala ya “uhalali” na “uthabiti” ambayo yameachwa kwa
majadiliano ya wanateolojia, hasa kwa ambo yale yahusuyo mamlaka ambayo
yakini inatumiwa na ndugu wa Mashariki waliojitenga, na ambayo kuna maelezo
mbalimbali ya ufasiri wake.
+ Pericle Felici Askofu Mkuu wa Samosata
Katibu mkuu wa Mtaguso
[1]Taz. Mt. Cyprianus,
Epist. 64,4: PL 3, 1017; CSEL
(Hartel), III B, uk. 720. – Mt. Hilarius Pict., In Mt. 23,6:
PL 9, 1047. – Mt. Augustinus, passim. – Mt. Cyrillus Alex.,
Glaph. in Gen. 2,10: PG 69, 110A.
[2]Mt. Gregorius M., Hom. in
Evang. 19,1:
PL 76, 1154B. – Taz. Mt. Augustinus, Serm. 341,9,11: PL
39, 1499 s. – Mt. Ioannes Dam., Adv. Iconocl. 11: PG 96,
1357.
[3] Taz. Mt. Irenaeus, Adv.
Haer.III,24,1: PG 7, 966B; Harvey 2,131; ed.Sagnard,
Sources Chr., uk. 398
[4]Mt. Cyprianus, De Orat.
Dom. 23: PL 4, 553; Hartel, III A, uk. 285. – Mt. Augustinus,
Serm. 71,20,33: PL 38, 463 s. – Mt. Ioannes Dam., Adv.
Iconocl. 12: PG 96, 1358D.
[5]Taz. Origenes, In Mt.
16,21: PG 13, 1443C. – Tertullianus, Adv. Marc. 3,7: PL
2, 357C; CSEL 47,3, uk. 386. – Kuhusu matini za kiliturujia, taz.
Sacramentarium Gregorianum: PL 78, 160B; au C. Moehlberg,
Liber Sacramentorum Romanae Ecclesiae, Romae 1960, uk. 111, XC: “Ee
Mungu, ujijengaye makao ya milele kwa tangamano lote la watakatifu....”.
Utenzi Urbs Ierusalem baeata katika Breviari ya kimonaki, na
Coelestis urbs Ierusalem, katika Breviari ya Kiroma (Sala ya
Kanisa).
[6]Taz. Mt. Thomas, Summa
Theol.III, q.62, a.5, ad i.
[7]Taz. Pius XII, Enc. Mystici
Corporis, 29 juni 1943: AAS 35 (1943) uk. 208.
[8]Taz. Leo XIII, Enc.
Divinum illud, 9 mei 1897: AAS 29 (1896-97) uk. 650. – Pius
XII, Enc. Mystici Corporis, l.c., uk. 219-220; Denz. 2288 (3808).
– Mt. Augustinus, Serm. 268,2: PL 38, 1232 na nyingine. –
Mt. Ioannes Chrys., In Eph., Hom. 9, 3: PG 62, 72. –
Didymus Alex., Trin. 2, 1: PG 39, 449 s. – Mt.
Thomas, In Col. 1, 18, lect. 5: Ed. Marietti, II, n. 46: “Kama
ulivyowekwa mwili mmoja kutoka kwa umoja wa roho ( animae), vivyo
hivyo Kanisa kutoka kwa umoja wa Roho...”.
[9]Taz. Leo XIII, Enc.
Sapientiae Christianae, 10 jenuari 1890: AAS 22 (1889-90) uk.
392. Id., Epist. Enc. Satis cognitum, 29 juni 1896: AAS 28
(1895-96) uk. 710 na 724 ss. – Pius XII, Enc. Mystici Corporis,
l.c., uk. 199-200.
[10]Taz. Pius XII, Enc.
Mystici Corporis, l.c., uk. 221 ss. Id., Enc. Humani generis,
12 agosti 1950: AAS 42 (1950) uk. 571.
[11]Taz. Leo XIII, Epist.
Enc. Satis cognitum, 29 juni 1896: AAS 28 (1895-96) uk.
713.
[12]Taz. Symbolum Ap.:
Denz. 6-9 (10-30); Symb. Nic.Const.: Denz. 86 (150); coll. Prof.
fidei Trid.: Denz. 994 na 999 (1862 na 1868).
[13] Laitwa “Kanisa la
kiroma, takatifu (katoliki, la Mitume)”, katika Prof. fidei Trid.,
l.c. na katika Conc. Vat. I, Sess. III, Const. dogm. Dei Filius:
Denz. 1782 (3001).
[14]Taz. Mt. Augustinus,
De Civ.Dei
XVIII, 51, 2: PL 41, 614.
[15]Taz. Mt. Cyprianus,
Epist. 69,6: PL 3, 1142B; CSEL
(Hartel), III B, uk. 754: “Sakramenti ya umoja isiyotengeka”.
[16] Taz. Pius XII, Alloc.
Magnificate Dominum, 2 novemba 1954: AAS 46 (1954) uk. 669.
Id., Litt. Enc.
Mediator Dei, 20 novemba 1947: AAS 39 (1947) uk. 555.
[17] Taz. Pius XI, Litt. Enc.
Miserentissimus Redemptor, 8 mei 1928: AAS 20 (1928) uk. 171
s. – Pius XII, Alloc. Vous nous avez, 22 septemba 1956: AAS
48 (1956) uk. 714.
[18]Taz. Mt. Thomas, Summa
Theol. III, q.63, a.2.
[19]Taz. Mt. Cyrillus
Hieros., Catech. 17, kuhusu Roho Mtakatifu, II, 35-37:
PG 33, 1009-1012. – Nic.Cabasilas, De vita in Christo, lib. III,
kuhusu manufaa ya Krisma (Mpako mtakatifu, au kipaimara): PG 150,
569-580. – Mt. Thomas, Summa Theol. III, q.65, a.3 na q.72, a.1
na 5.
[20]Taz. Pius XII, Litt. Enc.
Mediator Dei, 20 novemba 1947: AAS 39 (1947) hasa uk. 552 s.
[21]Taz. 1Kor 7:7: “Kila mtu
ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi”. –
Mt. Augustinus, De Dono Persev. 14, 37: PL
45, 1015s.: “Ni kipaji cha Mungu si kutawala tamaa tu, bali pia usafi wa
moyo wa watu wa ndoa”.
[22]Taz. Mt. Augustinus,
De Praed.Sanct.14, 27: PL 44, 980.
[23]Taz. Mt. Ioannes Chrys.,
In Io., Hom. 65, 1: PG 59, 361.
[24]Taz. Mt. Irenaeus,
Adv.Haer.III,16,6; III,22,1-3: PG 7, 925C-926A na 955C-958A;
Harvey 2,87 s. na 120-123; ed. Sagnard, Sources Chr., uk. 290-92
na 372 ss.
[25]Taz. Mt. Ignatius M.,
Ad Rom., Praef.: ed. Funk, I, uk. 252.
[26]Taz. Mt. Augustinus,
Bapt. c. Donat., V,28, 39: PL 43, 197: “Hakika ni dhahiri
kwamba liitwalo katika Kanisa ndani na nje, lazima lifikiriwe moyoni,
wala si mwilini”. – Id., ib.III,19,26: col. 152; V,18,24: col. 189;
In Io., Tr. 61,2: PL 35, 1800, na mara nyingi mahali pengine.
[27] Lk 12:48: “Kila
aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi”. Taz. Mt 5:19-20; 7:21-22;
25:41-46; Yak 2:14.
[28] Taz. Leo XIII, Epist.
Apost. Praeclare gratulationis, 20 juni 1894: AAS 26
(1893-94) uk. 707.
[29]Taz. Leo XIII, Epist.
Enc. Satis cognitum, 29 juni 1896: AAS 28 (1895-96) uk.
738. – Id. Epist. Enc. Caritatis studium, 25 julai 1898: AAS
31 (1898-99) uk. 11. – Pius XII, Nuntius radioph. Nell’alba, 24
desemba 1941: AAS 34 (1942) uk.21.
[30]Taz. Pius XI, Litt. Enc.
Rerum Orientalium, 8 septemba 1928: AAS
20 (1928) uk. 287. – Pius XII, Litt. Enc. Orientalis Ecclesiae, 9
aprili 1944: AAS 36 (1944) uk. 137.
[31]Taz. Instr. S.S.C.S.
Officii, 20 desemba 1949: AAS 42 (1950) uk. 142.
[32]Taz. Mt. Thomas, Summa
Theol.III, q.8, a.3, ad l.
[33] Taz. Epist.
S.S.C.S. Officii kwa Askofu Mkuu wa Boston: Denz. 3869-72.
[34] Taz. Eusebius Caes.,
Praeparatio Evangelica. 1,1: PG 21, 28AB.
[35]Taz. Benedictus XV,
Epist. Apost. Maximum illud, 30 novemba 1919: AAS
11 (1919) uk. 440, hasa 451 ss. – Pius XI, Litt. Enc. Rerum Ecclesiae,
28 februari 1926: AAS 18 (1926) uk. 68-69. – Pius XII, Litt. Enc. Fidei
Donum, 21 aprile 1957: AAS 49 (1957) uk. 236-237.
[36] Taz. Didachè, 14:
ed. Funk, I, uk. 32 – Mt. Iustinus, Dial 41: PG 6, 564. –
Mt. Irenaeus, Adv. Haer.IV,17,5: PG 7, 1023; Harvey 2,199
s. – Conc. Trid., Sess. 22, cap. 1: Denz. 939 (1742).
[37]Taz. Conc. Vat.I, Const.
dogm.De Ecclesia Christi, Pastor aeternus: Denz. 1821 (3050 s.).
[38] Taz. Conc. Flor.,
Decretum pro Graecis: Denz. 694 (1307) na Conc. Vat. I, ib.:
Denz. 1826 (3059).
[39] Taz. Liber
sacramentorum Mt. Gregorii, Praef. in natali Mt. Matthiae et Mt.
Thomae: PL 78, 51 na 152; taz. Cod. Vat. lat. 3548, f.18 – Mt.
Hilarius Pict., In Ps. 67,10: PL 9, 450; CSEL 22,
uk.286. – Mt. Hieronymus, Adv. Iovin. 1,26: PL
23, 247A.-S. – Mt. Augustinus, In Ps. 86,4: PL 37, 1103. –
Mt. Gregorius M., Mor. in Iob XXVIII,V: PL 76, 455-456. –
Primatius,
Comm. in Apoc. V: PL 66, 924BC. – Paschasius Radb., In Mt.
L.8, cap.16: PL 120, 561C. – Taz.Leo XIII, Epist. Et sane,
17 desemba 1888: AAS 21 (1888) uk. 321.
[40]Taz. Mdo 6:2-6; 11:30;
13:1; 14:23; 20:17; 1The 5:12-13; Flp 1:1; Kol 4:11 na sehemu nyingine.
[41]Taz. Mdo 20:25-27; 2Tim
4:6s. pamoja na 1Tim 5:22; 2Tim 2:2; Tit 1:5; Mt. Clem. Rom., Ad
Cor. 44,3: Ed. Funk, I, uk. 156.
[42]Taz. Mt. Clem. Rom.,
Ad Cor. 44,2: Ed. Funk, I, uk. 154 s.
[43]Taz. Tertullianus,
Praescr. Haer. 32: PL 2, 52 s. – Mt. Ignatius M., sehemu
mbalimbali.
[44]Taz. Tertullianus,
Praescr. Haer. 32: PL 2, 53.
[45]Taz. Mt. Irenaeus,
Adv. Haer. III,3,1: PG 7, 848A; Harvey 2,8; ed. Sagnard,
Sources Chr., uk. 100 s.: “manifestatam” (= hudhihirishwa).
[46]Taz. Mt. Irenaeus,
Adv. Haer. III,2,2: PG 7, 847; Harvey 2,7; ed. Sagnard,
Sources Chr., uk. 100: “custoditur” (= hutunzwa), taz. hiyohiyo
IV,26,2; coll. 1053; Harvey 2,236, na IV,33,8 coll. 1077; Harvey 2,262.
[47]Taz. Mt. Ignatius M.,
Ad Philad., Praef.: ed. Funk, I, uk. 264.
[48]Taz. Mt. Ignatius M.,
Ad Philad. 1,1;
Ad Magn. 6,1: ed. Funk, I, uk. 264 na 234.
[49] Taz. Mt. Clem. Rom.,
l.c. 42,3-4; 44,3-4; 57,1-2: Ed. Funk, I, uk. 152, 156, 171 s. – Mt.
Ignatius M., Ad Philad. 2; Ad Smyrn. 8; Ad Magn. 3;
Ad Trall. 7: ed. Funk, I, uk. 265 s.; 282; 232; 246 s. n.k. – Mt.
Iustinus, Apol., 1,65: PG 6, 428. – Mt. Cyprianus,
Epist., sehemu mbalimbali.
[50] Taz. Leo XIII, Epist.
Enc. Satis cognitum, 29 juni 1896: AAS 28 (1895-96) uk.
732.
[51]Taz. Conc. Trid., Decr.
De sacr. Ordinis, cap. 4: Denz. 960 (1768); Conc. Vat.I, Const.
dogm.De Ecclesia Christi, Pastor aeternus, cap. 3: Denz. 1828
(3061). Pius XII, Litt. Enc. Mystici Corporis, 29 juni 1943:
AAS 35 (1943) uk. 209 na 212. CIC, can. 329 §1.
[52]Taz. Leo XIII, Epist. Et
sane, 17 desemba 1888: AAS 21 (1888) uk. 321 s.
[53]Taz. Mt. Leo M., Serm.
5,3: PL 54, 154.
[54]Taz. Conc. Trid., Sess.
23, cap. 3. hutaja maneno ya 2Tim 1:6-7, ili kuonyesha kuwa Daraja
takatifu ndiyo sakramenti ya kweli: Denz. 959 (1766).
[55]Katika Trad. Apost.
3: ed. Botte, Source Chret., uk. 27-30, Askofu hupewa “primatus
sacerdotii = ukuu wa ukuhani”. Taz. Sacramentarium Leonianum, ed.
C. Moehlberg, Sacramentarium Veronense, Romae, 1955, uk. 119:
“hadi huduma ya ukuhani mkuu... kamilisha ndani ya makuhani wako fumbo
lako”; vilevile Liber Sacramentorum Romanae Ecclesiae, Romae,
1960, uk. 121-122: “Uwape, Ee Bwana, kiti cha Uaskofu, walichunge Kanisa
lako na watu wote”.Taz. PL 78, 224.
[56] Taz. Trad. Apost.
2: ed. Botte, uk. 27.
[57] Taz. Conc. Trid., Sess.
23, cap. 4, hufundisha kwamba Daraja takatifu hutia alama isiyofutika ( characterem):
Denz. 960 (1767). Taz. Ioannes XXIII, Alloc. Iubilate Deo, 8 mei
1960: AAS 52 (1960) uk. 466.Paulus VI, Homilia in Bas. Vaticana,
20 oktoba 1963: AAS 55 (1963), uk. 1014.
[58]Mt. Cyprianus, Epist.
63,14: PL 4, 386; Hartel, III B, uk. 713: “Kuhani hutenda kweli
mahali pa Kristo”. – Mt. Ioannes Chrys., In 2 Tim., Hom. 2, 4:
PG 62, 612: Kuhani ndiye “sumbolon” ya Kristo. – Mt. Ambrosius,
In Ps. 38,25-26: PL 14, 1051-52:
CSEL 64,203-204. – Ambrosiaster, In 1 Tim. 5,19: PL 17,
479C na In Eph. 4,11-12: col. 387C. – Theodorus Mops., Hom.
Katech. XV,21 na 24: ed. Tonneau, uk. 497 na 503. – Hesychius
Hieros., In Lev. L. 2,9,23: PG 93, 894B.
[59]Taz. Eusebius Caes.,
Hist.Eccl.,
V,24,10: GCS II,1, uk. 495; ed. Bardy, Sources Chret.
II, uk. 69. – Dionysius, kufuata Eusebius Caes., ib. VII,5,2:
GCS II,2, uk. 638 s.; ed. Bardy, Sources Chret. II, uk. 168
s.
[60]Taz. kuhusu Mitaguso ya
zamani, Eusebius Caes., Hist.Eccl.,
V,23-24: GCS II,1, uk. 488 ss.; ed. Bardy, Sources Chret.
II, uk. 66 ss. na sehemu nyingine. Conc. Nicaenum, can. 5: COD
uk. 7.
[61]Taz.
Tertullianus, De Ieiunio, 13: PL 2, 972B; CSEL
20, uk. 292, lin. 13-16.
[62]Taz. Mt. Cyprianus,
Epist. 56,3: Hartel, III B, uk. 650; Bayard, uk. 154.
[63]Taz. Relatio officialis
Zinelli, katika Conc. Vat.I: Mansi 52, 1109C.
[64]Taz. Conc. Vat.I, Schema
Const. Dogm. II, de Ecclesia Christi, c. 4: Mansi 53, 310. Taz.
Relatio Kleutgen kuhusu Schemate reformato: Mansi 53, 321B-322B na
declaratio Zinelli: Mansi 52, 1110A. Taz. pia Mt. Leo M., Serm.
4,3:
PL 54, 151A.
[65]Taz. CIC, can. 222
na 227.
[66]Taz. Conc. Vat.I, Const.
dogm.De Ecclesia Christi, Pastor aeternus: Denz. 1821 (3050 s.).
[67]Taz. Mt. Cyprianus,
Epist. 66,8: Hartel, III,2, uk. 733: “Askofu katika Kanisa, na
Kanisa katika Askofu”.
[68]Taz. Mt. Cyprianus,
Epist. 55,24: Hartel, uk. 642, lin. 13: “Kanisa lililo moja
hugawanyika katika viungo vingi ulimwenguni mwote”. Epist. 36,4:
Hartel, uk. 575, lin. 20-21.
[69]Taz. Pius XII, Litt. Enc.
Fidei Donum, 21 aprile 1957: AAS 49 (1957) uk. 237.
[70]Taz. Mt. Hilarius Pict.,
In Ps. 14,3: PL 9, 206; CSEL 22, uk.86. – Mt.
Gregorius M., Moral. IV,7,12: PL 75, 643C. – Ps. Basilius,
In Is. 15,296: PG 30, 637C.
[71]Taz. Mt. Coelestinus,
Epist. 18,1-2, ad Conc. Eph.: PL 50, 505AB; Schwartz, Acta
Conc. Oec. I,1,1, uk.22. Taz. Benedictus XV, Epist. Apost.
Maximum illud, 30 novemba 1919: AAS 11 (1919) uk. 440. – Pius XI,
Litt. Enc. Rerum Ecclesiae, 28 februari 1926: AAS 18
(1926) uk. 69. – Pius XII, Litt. Enc. Fidei Donum, l.c.
[72] Taz. Leo XIII, Epist.
Enc. Grande munus, 30 septemba 1880: AAS 13 (1880) uk.
145. Taz. CIC, c. 1327; c. 1350 §2.
[73]Kuhusu haki za
Upatriarka, taz. Conc. Nicaenum, can. 6 kwa habari ya Alexandria na
Antiochia, na can. 7 kwa habari ya Hierosolymis: COD, uk. 8. –
Conc.Later. IV, mwaka 1215, Constit.V: De dignitate Patriarcharum:
COD, uk. 212. – Conc.Ferr.-Flor.: COD, uk. 504.
[74]Taz. Cod. Iuris Can.
pro Eccl. Orient., c. 216-314: kuhusu Mapatriarka; c. 324-339:
kuhusu Maaskofu wakuu; c. 362-391: kuhusu wenye madaraka wengine; hasa
c. 238 §3; 216; 240; 251; 255: kuhusu Mapatriarka kuwateua
Maaskofu.*Tunaona vema kueleza hivi dondoo hili: Taz. Pius XII, Motu
proprio Cleri sanctitati, 2 juni 1957: AAS 49 (1957) uk.
497-527 (cc. 216-314: kuhusu Mapatriarka), uk. 530-534 (cc. 324-339:
kuhusu Maaskofu wakuu), uk. 540-547 (cc. 362-391: kuhusu wenye madaraka
wengine); hasa uk. 497-510 (cc. 238 §3; 216; 240; 251; 255: kuhusu
Mapatriarka kuwateua Maaskofu). ( N.d.R.)
[75]Taz. Conc. Trid., Decr.
de reform., Sess. V, c. 2, n. 9 na Sess. XXIV, can. 4; COD, uk
645 na 739).
[76]Taz. Conc. Vat.I, Const.
dogm. Dei Filius, 3: Denz. 1792 (3011). Taz. maelezo yaliyomo
katika kiwatiko (=“Schema”) (yaliyochukuliwa kutoka kwa Mt. Roberto
Bellarmino): Mansi 51, 579C; na pia kiwatiko kilichosahishwa Const. II
De Ecclesia Christi, pamoja na maelezo yake Kleutgen: Mansi 53,
313AB. – Pius IX, Epist. Tuas libenter: Denz. 1683 (2879).
[77]Taz. CIC, c.
1322-1323.
[78]Taz.
Conc. Vat. I, Const. dogm., Pastor aeternus: Denz. 1839 (3074).
[79]Taz. ufafanuzi wa Gasser
katika Conc. Vat.I: Mansi 52, 1213AC.
[80]Taz. Gasser, ib.: Mansi
1214A.
[81]Taz. Gasser, ib.: Mansi
1215CD, 1216-1217A.
[82]Taz. Gasser, ib.: Mansi
1213.
[83]Taz. Conc. Vat. I, Const.
dogm., Pastor aeternus, 4: Denz. 1836 (3070).
[84]Sala ya kuweka wakfu
Askofu katika riti ya kigriki: Euchologion to mega, Romae, 1873,
uk. 139.
[85]Taz. Mt. Ignatius M.,
Ad Smyrn.8,1: ed. Funk, I, uk. 282.
[86] Taz. Mdo 8:1; 14:22-23;
20:17 na sehemu nyingine.
[87] Sala ya kimozarabi:
PL
96, 759B.
[88]Taz. Mt. Ignatius M.,
Ad Smyrn.8,1: ed. Funk, I, uk. 282.
[89]Mt. Thomas, Summa
Theol. III, q.73, a.3.
[90]Taz. Mt. Augustinus,
C. Faustum, 12,20: PL 42, 265; Serm.
57,7: PL 38,89, n.k.
[91]Mt. Leo M., Serm.
63,7: PL 54, 357C.
[92] Taz. Trad. Apost.
Hippolyti, 2-3: ed. Botte, uk. 26-30.
[93] Taz. fasulu ya
uchunguzi
mwanzoni mwa kumweka wakfu Askofu, na sala mwishoni mwa Misa hiyo
ya kumweka wakfu, baada ya Ta Deum.
[94]Benedictus XIV, Br.
Romana Ecclesia, 5 oktoba 1752, §1: Bullarium Benedicti XIV,
t. IV, Romae, 1758, 21: “Askofu ni mfano wa Kristo, hutekeleza jukumu
lake”. – Pius XII, Enc. Mystici Corporis, l.c.; uk. 211:
“Wanalisha na kuchunga kwa jina la Kristo makundi waliyokabidhiwa, kila
mmoja kundi lake”.
[95] Taz. Leo XIII, Epist.
Enc. Satis cognitum, 29 juni 1896: AAS 28 (1895-96) uk.
732. Idem, Epist. Officio sanctissimo, 22 desemba 1887: AAS
20 (1887) uk. 264. – Pius IX, Litt. Apost. ad Episcopos Germaniae, 12
machi 1875, na Alloc. Consist. 15 machi 1875: Denz. 3112-3117, katika
toleo jipya tu.
[96]Taz. Conc. Vat. I, Const.
dogm., Pastor aeternus, 3: Denz. 1828 (3061). Taz. Relatio
Zinelli: Mansi 52, 1114D.
[97]Taz. Mt. Ignatius M.,
Ad Ephes.5,1: ed. Funk, I, uk. 216.
[98]Taz. Mt. Ignatius M.,
Ad Ephes.6,1: ed. Funk, I, uk. 218.
[99]Taz. Conc. Trid., Decr.
De sacr. Ordinis, cap. 2: Denz. 958 (1765), na can. 6: Denz. 966
(1776).
[100]Taz. Innocentius I,
Epist. ad Decentium: PL 20, 554A; Mansi 3, 1029; Denz. 98
(215): “Mapadre, ingawa ni makuhani wa Daraja ya pili, lakini hawana
kilele cha ukuhani”. – Mt. Cyprianus, Epist. 61,3: ed. Hartel,
uk. 696.
[101]Taz. Conc. Trid.,
l.c.: Denz. 956a-968 (1763-1778), na hasa can. 7: Denz. 967 (1777). –
Pius XII, Const. Apost. Sacramentum Ordinis: Denz. 2301
(3857-61).
[102]Taz. Innocentius I,
l.c. – Mt. Gregorius Naz., Apol. II,22: PG
35, 432B. – Ps.Dionysius, Eccl. Hier., 1,2: PG 3, 372D.
[103]Taz. Conc. Trid.,
Sess. 22: Denz. 940 (1743). – Pius XII, Litt. Enc. Mediator Dei,
20 novemba 1947: AAS 39 (1947) uk. 553: Denz. 2300 (3850).
[104]Taz. Conc. Trid.,
Sess. 22: Denz. 938 (1739-40). – Conc. Vat. II, Const. de Sacra
Liturgia, Sacrosanctum Concilium, n.7 na n.47: AAS 56
(1964) uk. 100-113.
[105]Taz. Pius XII, Litt.
Enc. Mediator Dei, l.c., kwenye dondoo n. 103.
[106]Taz. Mt. Cyprianus,
Epist. 11,3: PL 4, 242B; Hartel, II, 2, uk. 497.
[107]Taz. Pontificale
romanum, katika kuweka wakfu Mapadre, wakati wa kuvalisha mavazi ya
ibada.
[108]Taz. Pontificale
romanum, katika kuweka wakfu Mapadre; utangulizi.
[109]Taz. Mt. Ignatius M.,
Ad Philad., 4: ed. Funk, I, uk. 266. – Mt. Cornelius I, kufuata Mt.
Cyprianus, Epist. 48,2; Hartel, III, 2, uk. 610.
[110] Constitutiones
Ecclesiae aegyptiacae, III,2: ed. Funk, Didascalia,
II, uk. 103 . Statuta Eccl. Ant. 37-41: Mansi 3, 954.
[111] Taz. Mt. Polycarpus,
Ad Phil., 5,2: ed. Funk, I, uk. 300: Kristo aitwa “aliyejifanya
mtumishi wa wote”. – Taz. Didachè, 15,1: ed. Funk, I, uk. 32. –
Mt. Ignatius M., Ad Trall. 2,3: ed. Funk, I, uk. 242. –
Constitutiones Apostolorum, 8,28,4: ed. Funk, Didascalia,
I, uk. 530 .
[112]Taz. Mt. Augustinus,
Serm. 340,1: PL 38, 1483.
[113]Taz. Pius XI, Litt.
Enc. Quadragesimo anno, 15 mei 1931: AAS 23 (1931) uk. 221
s. – Pius XII, Alloc. De quelle consolation, 14 oktoba 1951:
AAS 43 (1951) uk. 790 s.
[114] Taz. Pius XII, Alloc.
Six ans se sont écouléss, 5 oktoba 1957: AAS 49 (1957) uk.
927.
[115]Missale romanum,
kutoka Utangulizi wa Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme.
[116] Taz. Leo XIII, Epist.
Enc. Immortale Dei, 1 novemba 1885: AAS 18 (1885) uk. 166
ss. – Id. Litt. Encicl. Sapientiae christianae, 10 jenuari 1890:
AAS 22 (1889-90) uk. 397 ss. – Pius XII, Alloc. Alla vostra
filiale, 23 machi 1958: AAS 50 (1958) uk. 220: “Hali ya ulei
safi na wa halali ya serikali”.
[118] Taz. Pius XII, Alloc.
De quelle consolation, l.c., uk. 789: “Katika mapigano mkataa
katika vita, mara nyingi juhudi zenye mafanikio zatoka kwa upande wa
mbele wa jeshi...”. Id., Alloc. L’importance de la presse catholique,
17 februari 1950: AAS 42 (1950) uk. 256.
[119]Taz. 1The 5:19 na 1Yoh
4:1.
[120] Epist. Ad
Diognetum, 6: ed. Funk, I, uk. 400 – Taz. Mt. Ioannes Chrys., In
Mt., Hom. 46(47), 2: PG 58, 478, kwa mfano wa chachu katika
donge.
[121] Missale romanum,
Gloria in excelsis. Taz. Lk 1:35; Mk 1:24; Lk 4:34; Yn 6:69 (Ð §gioj toà
Qeoà); Mdo 3:14; 4:27 na 30; Ebr 7:26; 1Yoh 2:20; Ufu 3:7.
[122] Taz. Origenes,
Comm. Rom. 7,7: PG 14, 1122B. – Ps. Macarius, De Oratione
11:
PL 34, 861AB. – Mt. Thomas, Summa Theol. II-II, q.184, a.3.
[123]Taz. Mt. Augustinus,
Retract. II, 18: PL 32, 637 s. – Pius XII, Enc. Mystici
Corporis, 29 juni 1943: AAS 35 (1943) uk. 225.
[124]Taz. Pius XI, Litt.
Enc. Rerum omnium, 26 jenuari 1923: AAS 15 (1923) uk. 50
na 59-60. – Id., Litt. Enc. Casti Connubii, 31 desemba 1930:
AAS 22 (1930) uk. 548. – Pius XII, Const. Apost. Provida Mater,
2 februari 1947: AAS 39 (1947) uk. 117. – Id., Alloc. Annus
sacer, 8 desemba 1950: AAS 43 (1951) uk. 27-28. – Id., Alloc.
Nel darvi, 1 julai 1956: AAS 48 (1956) uk. 574 s.
[125]Taz. Mt. Thomas,
Summa Theol. II-II, q.184, a.5 na 6. – Id., Perf. vitae spir.
c. 18. – Origenes, In Is. Hom. 6,1: PG 13, 239.
[126] Taz. Mt. Ignatius M.,
Ad Magn. 13,1: ed. Funk, I, uk. 241.
[127]Taz. Mt. Pius X,
Exort. Haerent animo, 4 agosti 1908: ASS 41 (1908) uk 560
s.. – CIC can. 124. – Pius XI, Litt. Enc. Ad catholici
sacerdotii, 20 desemba 1935: AAS 28 (1936) uk. 22.
[128]Taz. Pontificale
romanum, katika kuweka wakfu Mapadre; katika mawaidha ya mwanzoni.
[129]Taz. Mt. Ignatius M.,
Ad Trall. 2,3: ed. Funk, I, uk. 244.
[130] Taz. Pius XII, Alloc.
Sous la maternelle protection, 9 desemba 1957: AAS 50 (1958)
uk. 36.
[131]Taz. Pius XI, Litt.
Enc. Casti Connubii, 31 desemba 1930: AAS 22 (1930) uk.
548 s. – Mt. Ioannes Chrys., In Eph., Hom. 20, 2: PG 62,
136 ss.
[132]Taz. Mt. Augustinus,
Enchir. 121, 32: PL 40, 288. – Mt. Thomas, Summa Theol.
II-II, q.184, a.1. – Pius XII, Adhort. Apost. Menti nostrae, 23
septemba 1950: AAS
42 (1950) uk. 660.
[133]Kuhusu mashauri kwa
ujumla, taz.Origenes, Comm. Rom. X,14: PG 14, 1275B. – Mt.
Augustinus, De S. Virginitate, . 15, 15: PL 40, 403.
– Mt. Thomas, Summa Theol.I-II, q.100, a.2C (mwishoni); II-II,
q.44, a.4, ad 3.
[134] Kuhusu ubora wa
ubikira mtakatifu, taz. Tertullianus, Exhort. Cast. 10: PL
2, 925C. – Mt. Cyprianus, Hab. Virg. 3 na 22: PL 4, 443B
na 461A s..– Mt. Athanasius (?), De Virg.: PG 28, 252 ss.
– Mt. Io. Chrys., De Virg.: PG 48, 533 ss.
[135]Kuhusu umaskini wa
kiroho, taz. Mt 5:3 na 19:21; Mk 10:21; Lk 18:22; kuhusu utii, hutolewa
mfano wa Kristo: Yn 4:34 na 6:38; Flp 2:8-10¸Ebr 10:5-7. Maandishi ya
Mababa na ya waanzilishi wa mashirika yapo mengi.
[136]Kuhusu kutekeleza
mashauri ya kiinjili kusikowalazimisha watu wote, taz. Mt. Ioannes
Chrys., In Mt., Hom. 7(7), 2: PG 57, 81 s. – Mt.
Ambrosius, De Viduis, 4,23: PL 16, 241 s.
[137]Taz. Rosweydus,
Vitae Patrum, Antwerpias, 1628. – Apophtegmata Patrum: PG
65. – Palladius, Historia Lausiaca: PG 34, 995ss.: ed.C.
Butler, Cambridge, 1898 (1904). – Pius XI, Const. Apost. Umbratilem,
8 julai 1924: AAS 16 (1924) uk. 386-387. – Pius XII, Alloc.
Nous sommes heusereux, 11 aprili 1958: AAS 50 (1958) uk. 283.
[138] Taz. Paulus VI,
Alloc. Magno gaudio, 23 mei 1964: AAS 56 (1964) uk. 566.
[139] Taz. CIC, c.
487 na 488, 4 °. – Pius XII, Alloc. Annus sacer, 8
desemba 1950: AAS 43 (1951) uk. 27 s. – Id., Const. Apost.
Provida Mater, 2 februari 1947: AAS 39 (1947) uk. 120 ss.
[140] Taz. Paulus VI, l.c.,
uk. 567.
[141]Taz. Mt. Thomas,
Summa Theol.II-II, q.184, a.3 na q.188, a.2. – Mt. Bonaventura,
Opusc . XI, Apologia Pauperum, c. 3,3: ed. Opera,
Quaracchi, t. 8, 1898, uk. 245 a.
[142]Taz. Conc. Vat.I,
Schema De Ecclesia Christi, cap. XV na dondoo n.48: Mansi 51, 549 s. na
619 s. – Taz. Leo XIII, Epist. Au milieu des consolations, 23
desemba 1900: AAS 33 (1900-01) uk. 361. – Pius XII, Const.Apost.
Provida Mater, l.c., uk. 114 s.
[143] Taz. Leo XIII, Const.
Romanus Pontefices, 8 mei 1881: ASS 13 (1880-81) uk. 483. –
Pius XII, Alloc. Annus sacer, 8 desemba 1950: AAS 43
(1951) uk. 28 s.
[144] Taz. Pius XII, Alloc.
Annus sacer, l.c., uk. 28. – Id., Const. Apost. Sede Sapientiae,
31 mei 1956: AAS 48 (1956) uk. 355. – Paulus VI, Alloc. Magno
gaudio, 23 mei 1964: AAS 56 (1964) uk. 570-571.
[145]Taz. Pius XII, Litt.
Enc. Mystici Corporis, 29 juni 1943: AAS 35 (1943) uk. 214
s.
[146] Taz. Pius XII, Alloc.
Annus sacer, l.c., uk. 30. – Id., Alloc. Sous la maternelle
protection, 9 desemba 1957: AAS 50 (1958) uk. 39 s..
[147]Taz. Conc. Flor.,
Decretum pro Graecis: Denz. 693 (1305).
[148]Licha ya hati za
zamani dhidi ya aina yoyote ya kuwapandisha pepo, tangu wakati wa
Iskanda IV (27 septemba 1258), taz. Encicl. S.S.C.S. Officii, De
magnetismi abusu, 4 agosti 1856: ASS (1856) uk. 177-178,
Denz. 1653-54 (2823-2825); jibu S.S.C.S. Officii, 24 aprile 1917: AAS
(1917) uk. 268, Denz. 2182 (3642).
[149]Muhtasari wa
mafundisho ya Mt. Paulo Mtume hupatikana katika: Pius XII, Litt. Enc.
Mystici Corporis, 29 juni 1943: AAS 35 (1943) uk. 200, na
nyingine.
[150]Taz. k.m. Mt.
Augustinus, Enarr. in Ps. 85,24: PL 37, 1099. – Mt.
Hieronymus, Liber contra Vigilantium, 6: PL 23, 344. – Mt.
Thomas, In quattrom Sent., d. 45, q. 3, a. 2. – Mt.
Bonaventura, In quattrom Sent., d. 45, a. 3, q.2; n.k.
[151]Taz. Pius XII, Enc. Mystici
Corporis, 29 juni 1943: AAS 35 (1943) uk. 245.
[152]Taz. miandiko mingi
iliyomo katika makatakombi huko Roma.
[153]Taz. Gelasius I,
Decretalis De libris recipiendis, 3: PL 59, 160, Denz. 165
(353).
[154]Taz. Mt. Methodius,
Symposion, VII, 3: GCS (Bonwetsch) uk. 74.
[155]Taz. Benedictus XV,
Decretum approbationis virtutum in Causa beatificationis et
canonizationis Servi Dei Ioannis Nepomuceni Neumann: AAS 14
(1922) uk. 23 – Hotuba nyingi za Pius XII juu ya watakatifu: Inviti
all’eroismo, katika Discorsi e Radiomessaggi, tt.I-III,
Romae, 1941-42, sehemu nyingi; Id., Discorsi e Radiomessaggi, t.
10, 1949, uk. 37-43.
[156]Taz. Pius XII, Litt.
Enc. Mediator Dei, 20 novemba 1947: AAS 39 (1947) uk. 581.
[157] Taz. Ebr 13:7; YbS
44-50; Ebr 11:3-40. Taz. pia Pius XII, Litt. Enc. Mediator Dei,
20 novemba 1947: AAS 39 (1947) uk. 582 s.
[158]Taz. Conc. Vat.I,
Const. dogm. De fide catholica, Dei Filius, cap. 3: Denz. 1794
(3013).
[159]Taz. Pius XII, Enc.
Mystici Corporis, 29 juni 1943: AAS 35 (1943) uk. 216.
[160]Kuhusu ushukrani kwa
ajili ya watakatifu, taz. E. Diehl, Inscriptiones latinae christianae
veteres, I, Berolini, 1925, nn. 2008, 2382 na nyingine.
[161]Taz. Conc. Trid.,
Decr. De invocatione...Sanctorum: Denz. 984 (1821).
[162]Breviarum romanum,
mwaliko katika sherehe ya Watakatifu Wote.
[163]Taz. k.m. 2The 1:10.
[164]Conc. Vat. II, Const.
de Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, cap. 5, n. 104: AAS
56 (1964) uk. 125-126.
[165] Missale romanum,
Kanuni ya Misa.
[166]Conc. Nicaenum II,
Act. VII: Denz. 302 (600).
[167]Conc. Flor., Decretum
pro Graecis: Denz. 693 (1304).
[168]Conc.Trid., Decr.
De invocatione, veneratione et reliquiis Sanctorum et sacris imaginibus:
Denz. 984-988 (1821-1824). – Id., Decr. De Purgatorio: Denz 983
(1820). – Id., Decr. De Iustificatione, can. 30: Denz 840 (1580).
[169] Missale romanum,
katika Utangulizi wa sherehe ya Watakatifu, uliotolewa kwa idhini kwa
ajili ya majimbo kadha wa kadha (ya Ufaransa).
[170] Taz. Mt. Petrus
Canisius, Catechismus Maior seu Summa Doctrinae christianae, cap.
III (ed. crit. F. Streicher), sehemu ya I, uk. 15-16, n. 44 na uk.
100-101, n. 49.
[171]Taz. Conc. Vat. II,
Const. de Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, cap. 1, n. 8:
AAS 56 (1964) uk. 401.
[172]Symbolum
Constantinopolitanum: Mansi 3, 566. Taz. Conc.Ephesinum, ibid. 4,
1130 (na pia ibid. 2, 665 na 4, 1071); Conc. Chalcedonense, ibid. 7,
111-116; Conc.Constantinopolitanum II, ibid. 9, 375-396; Missale
romanum, katika “Nasadiki”.
[173] Missale romanum,
Kanuni ya Misa.
[174]Mt. Augustinus, De
S. Virginitate, . 6:
PL 40, 399.
[175] Taz. Paulus VI,
Allocutio in Concilio, 4 desemba 1963: AAS 56 (1964) uk. 37.
[176]Taz. Mt. Germanus
Const., Hom. in Annunt. Deiparae: PG 98, 328A – Id., In
Dorm. 2: col. 357 – Anastasius Anthioc., Serm. 2 de Annunt.,
2: PG 89, 1377AB – Id., Serm. 3,2: col. 1388C. – Mt.
Andreas Cret., Can. in B.V. Nat. 4: PG 97, 1321B. – Id.,
In B.V. Nat., 1: col. 812A. – Id., Hom. in Dorm. 1:
col. 1068C. – Mt. Sophronius, Hor. 2 in Annunt., 18: PG
87 (3), 3237BD.
[177]Mt. Irenaeus,
Adv.Haer.III, 22,4: PG 7, 959A; Harvey 2,123.
[178]Mt. Irenaeus, ibid.;
Harvey 2,124.
[179]Mt. Epiphanius,
Haer. 78, 18: PG 42, 728CD-729AB.
[180]Mt. Hieronymus,
Epist. 22, 21: PL 22, 408. – Taz. Taz. Mt. Augustinus,
Serm. 51,2,3: PL 38, 335. – Id., Serm. 232,2: 1108. –
Mt. Cyrillus Hieros., Catech. 12, 15: PG 33, 741AB. – Mt.
Ioannes Chrys., In Ps. 44, 7: PG 55, 193. – Mt. Ioannes
Dam., Hom. 2 in Dorm. B. M. V., 3: PG 96, 728.
[181]Taz. Conc. Lateranense
(mwaka 649), can. 3: Mansi 10, 1151. – Mt. Leo M., Epist. ad Flav.:
PL 54, 759. – Conc.Chalcedonense: Mansi 7, 462. – Mt. Ambrosius,
De instit. Virg.: PL
16, 320.
[182]Taz. Pius XII, Enc. Mystici
Corporis, 29 juni 1943: AAS 35 (1943) uk. 247-248.
[183] Taz. Pius IX, Bulla
Ineffabilis, 8 desemba 1854: Acta Pii IX, 1, I, uk. 616; Denz.
1641 (2803).
[184]Taz. Pius XII, Const.
Apost. Munificentissimus, 1 novemba 1950: AAS 42 (1950);
Denz. 2333 (3903). – Mt. Ioannes Dam., Enc. in Dorm.Dei genitricis,
Hom. 2 na 3: PG 96, 721-761, hasa col. 728B. – Mt. Germanus
Const., In. S. Dei gen. Dorm., Serm. 1: PG 98 (6),
340-348; ibid., Serm. 3: col. 361. – Mt. Modestus Hier., In Dorm. SS.
Deiparae:
PG 86 (2), 3277-3312.
[185] Taz. Pius XII, Litt.
Enc. Ad coeli Reginam, 11 oktoba 1954: AAS 46 (1954) uk.
633-636; Denz. 3913 ss. – Taz. Mt. Andreas Cret., Hom 3 in Dorm.
SS.Deiparae: PG 97, 1089-1109. – Mt. Ioannes Dam., De fide
orth., IV, 14: PG
94, 1153-1161.
[186]Taz. Kleutgen, fasuli
iliyorekebishwa De mystero Verbi incarnati, cap.IV: Mansi 53,
290. – Taz. Mt. Andreas Cret., In nat. Mariae, sermo 4: PG
97, 865A. – Mt. Germanus Const., In Annunt. Deiparae: PG
98, 321BC. – Id., In Dorm. Deiparae, III: col. 361D. – Mt.
Ioannes Dam., In Dorm. B. M. V., Hom. 1, 8: PG 96,
712BC-713A.
[187]Taz. Leo XIII, Litt.
Enc. Adiutricem populi, 5 septemba 1895: AAS 28 (1895-96)
uk. 129. – Mt. Pius X, Litt.Encicl. Ad diem illum, 2 februari
1904: Acta, I, uk. 154; Denz. 1978a (3370). – Pius XI, Litt. Enc.
Miserentissimus Redemptor, 8 mei 1928: AAS 20 (1928) uk. 178.
– Pius XII, Nuntius radioph., 13 mei 1946: AAS 38 (1946)
uk. 266.
[188] Taz. Mt. Ambrosius,
Epist.
63: PL 16, 1218.
[189]Taz. Mt. Ambrosius,
Expos. Lc., II, 7: PL 15, 1555.
[190]Taz. Ps. Petrus Dam.,
Serm. 63: PL 144, 861AB. – Godefridus wa Mt. Victore, In
nat. B.M., Ms. Paris, Mazarine, 1002, fol. 109r. – Gerhohus Reich.,
De gloria et honore Filii hominis, 10: PL 194, 1105AB.
[191]Taz. Mt. Ambrosius,
Expos.Lc., II, 7 na X, 24-25: PL 15, 1555 na 1810. – Mt.
Augustinus, In Io., Tr. 13,12: PL 35, 1499. – Id.,
Serm. 191,2,3: PL
38, 1010; na nyingine. – Taz. pia Ven. Beda, In Lc. Expos. I, cap.
2: PL 92, 330. – Isaac de Stella, Serm.
51: PL 194, 1863A.
[192]Taz. Breviarium
romanum, ant. “Sub tuum praesidium”, ya Vesperi I ya Ofisyo Ndogo ya
Bikira Maria.
[193] Taz. Conc. Nicaenum
II, anno 787: Mansi 13, 378-379; Denz. 302 (600-601). – Conc. Trid.,
Sess. 25: Mansi 33, 171-172.
[194]Taz. Pius XII, Nuntius
radioph., 24 oktoba 1954: AAS 46 (1954) uk. 679. – Id., Litt.
Enc. Ad coeli Reginam, 11 oktoba 1954: AAS 46 (1954) uk.
637.
[195]Taz. Pius XI, Litt.
Enc. Ecclesiam Dei, 12 novemba 1923: AAS 15 (1923) uk. 581.
– Pius XII, Litt. Enc. Fulgens corona, 8 septemba 1953: AAS
45 (1953) uk. 590-591.
|
|