Index

Back Top Print

[AR - BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

Tamko juu ya uhuru wa dini

 Haki ya mtu binafsi na ya jumuiya 
ya kuwa na uhuru wa kijamii na wa kiserikali
katika masuala ya dini
 

Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso mkuu
ataka haya yakumbukwe daima

  

UTANGULIZI

1. Wanadamu wa nyakati hizi wanazidi kuwa macho sana kuhusu HESHIMA YA KIUTU (Dignitatis Humanae)[1]; na inaongezeka idadi ya wale wanaodai kuwa binadamu wafanye mashauri yao wenyewe na washike wajibu wao kwa uhuru katika vitendo vyao na wasiwe watendaji wa kulazimishwa, bali waongozwe na hisia ya wajibu wao. Wakati huohuo wanadai kikomo cha kisheria cha nguvu ya serikali ili kuzuia kubanwa mno kwa uhuru wa kila mmoja na jumuiya. Dai hili kwa ajili ya uhuru katika jumuiya za watu linahusika hasa na mema ya kiroho katika mtu, na hasa yale yanayohusu matendo huru ya dini katika jamii. Mtaguso huu Mkuu unazingatia kwa uangalifu hamu hizo za moyoni na ukiazimia kutamka jinsi zinavyoendana na ukweli na haki, unachunguza Mapokeo matakatifu na mafundisho ya Kanisa ambako huchotwa vitu vipya ambavyo mara zote hulingana na vile vya zamani.

Mtaguso Mkuu kwanza unakiri kwamba Mungu mwenyewe amedhihirisha kwa binadamu wote njia ambayo binadamu wanaweza kuokolewa katika Kristo na kufikishwa kwenye heri ya milele, kwa kumtumikia yeye. Tunaamini kwamba dini hii moja iliyo ya kweli yadumu katika Kanisa Katoliki la Mitume ambalo Bwana Yesu Kristo alilikabidhi wajibu wa kuieneza kwa watu wote, alipowaambia Mitume wake, “Basi, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu, mkiwafundisha kushika yote niliyowaamuru” (Mt 28:19-20). Watu wote yawapasa kutafuta ukweli, hasa unaomhusu Mungu na Kanisa lake, kuukubali kwa moyo na kushikamana nao baada ya kuujua.

Vilevile Mtaguso Mkuu unakiri kwamba masharti haya hugusa na kufunga dhamiri ya binadamu. Ukweli unatawala wenyewe katika mawazo ya binadamu, kwa nguvu ya ukweli wenyewe tu ambao hupenya ufahamu wote kwa upole na nguvu. Uhuru wa dini ambao binadamu wanaudai katika kutimiliza wajibu wao wa kumwabudu Mungu, unaendana na uhuru kutoka kwa shurutisho lolote la serikali. Kwa hiyo, haudhuru mfululizo wa mafundisho ya kikatoliki kuhusu wajibu wa kimaadili wa kila mmoja na wa jamii kuelekea kwenye dini ya kweli na Kanisa lililo moja la Kristo. Zaidi ya hayo katika kulishughulikia suala hili la uhuru wa dini, Mtaguso Mkuu unaazimia kuendeleza mafundisho ya Mapapa waliotangulia hivi karibuni kuhusu haki za binadamu zisizoondoleka, na katika sheria za muundo wa jamii.

I - UHURU WA DINI KWA UJUMLA

Maana na misingi ya uhuru wa dini

2. Mtaguso Mkuu unatangaza (declarat) kwamba binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubaliwa kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Aidha Mtaguso unatangaza kwamba haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili.[2] Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia.

Ni kutokana na hadhi yao kwamba watu wote, kwa sababu wao ni binadamu, yaani wamejaliwa kipaji cha akili na utashi na hivyo wanao wajibu binafsi, wanasukumwa na maumbile yao na kanuni za kimaadili kuutafuta ukweli, hasa unaohusu dini. Wanasukumwa pia kuambatana na ukweli, baada ya kuujua, na kuyaelekeza maisha yao yote kwenye matakwa ya ukweli. Lakini binadamu hawawezi kuitimiliza kanuni hii katika njia inavyodaiwa na maumbile yao, wasipopata uhuru wa ndani na kinga dhidi ya mashurutisho ya nje. Kwa hiyo haki ya uhuru wa dini, msingi wake si katika hisia za mtu binafsi (subiectiva personae dispositione), bali katika maumbile yake yenyewe (in ipsa eius natura). Kwa sababu hii, haki ya kinga hiyo hudumu hata kwa wale ambao hawalitimizi sharti la kutafuta ukweli na kuambatana nao. Utekelezaji wa haki hii hauwezi kuzuiwa iwapo hauleti ghasia katika jamii.

Uhuru wa dini na umuhimu wa uhusiano wa binadamu na Mungu

3. Hayo yajionyesha kwa wazi zaidi kama mmoja atazingatia kwamba kanuni ya kipeo ya maisha ya binadamu ni sheria ya Mungu pekee, yenye umilele, iliyo na ukweli ndani yake yenyewe na inayoongoza viumbe vyote, ambayo Mungu kwa njia yake hupanga, huongoza na kutawala dunia yote, na njia za maisha ya jamii kulingana na azimio la busara na upendo wake. Mungu anawashirikisha binadamu sheria yake ili kwamba kwa azimio amana la maongozi yake binadamu waweze kujua zaidi na zaidi ule ukweli usiobadilika[3]. Kwa sababu hii kila mmoja anao wajibu na haki ya kutafuta ukweli katika masuala ya dini ili kwamba kwa njia za kufaa aweze kwa busara kutoa maamuzi ya dhamiri yake ambayo ni amini na kweli.

Hata hivyo, utafutaji wa ukweli unatakiwa kufanywa kwa mtindo ambao unalingana na hadhi ya binadamu na maumbile yake ya kijamii, yaani njia ya utafiti huru kwa msaada wa mafundisho, au maelekezo, mawasiliano na mijadala. Ni kwa njia hizi ambapo binadamu huelezana ukweli waliougundua, au ambao wanafikiri kuwa wameugundua, kwa lengo la kusaidiana wao kwa wao katika utafutaji wa ukweli. Kwa ukweli ambao wameugundua binadamu lazima washikamane nao kikamilifu na kwa dhati.

Ni kwa njia ya dhamiri yake ambapo binadamu huona na kugundua madai ya sheria za kimungu. Anawajibika katika kufuata dhamiri hii kwa uaminifu katika shughuli zake zote, ili aweze kufika kwa Mungu ambaye ndiye kikomo chake. Hivyo anatakiwa asilazimishwe kutenda kinyume na dhamiri yake. Wala asizuiliwe katika kutenda kulingana nayo, hasa katika masuala ya dini. Sababu ni kwamba, matendo ya dini kwa maumbile yake ni matendo ya hiari na uhuru wa ndani ambapo mtu hujielekeza moja kwa moja kwa Mungu. Matendo ya namna hii hayawezi kuamrishwa au kukatazwa na mtu yeyote mwenye mamlaka[4]. Lakini maumbile yake ya mahusiano hudai binadamu aonyeshe nje pia matendo haya ya ndani yaliyo ya kidini na awasiliane na wengine katika masuala hayo na kuishuhudia dini yake katika jumuiya.

Kwa sababu hiyo, kumkatalia binadamu matendo huru ya dini katika jamii, wakati sheria za haki zinazolinda haki ya taifa zinazingatiwa, ni kumkosea haki binadamu na mpango mzima uliowekwa na Mungu kwa ajili yake pia.

Zaidi ya hayo, matendo ya binafsi na ya hadhara ya dini ambayo watu hujielekeza wenyewe kwa Mungu kwa uamuzi wa dhamiri zao, hushinda mpango wa mambo ya kidunia na yenye kupita. Kwa hiyo serikali, ambayo ndiyo yenye kutunza manufaa ya wote hapa duniani, lazima igundue na itazame kwa jicho la upendeleo maisha ya kidini ya raia. Lakini kama itathubutu kudhibiti, au kuzuia matendo ya dini, lazima isemwe kuwa imevuka mipaka ya kikomo chake cha utawala.

Uhuru wa dini wa jumuiya

4. Uhuru au kinga dhidi ya kulazimishwa katika mambo ya dini, ambayo ni haki ya kila mtu, lazima pia wapewe watu wanapotenda kijumuiya. Jumuiya za kidini ni hitaji la maumbile ya kijamii ya binadamu na ya dini yenyewe.

Iwapo masharti ya haki ya usalama katika jamii yanatunzwa, haki za jumuiya hizo zikingwe kisheria. Nazo ni haki ya kupewa ruhusa ya kujitengenezea muundo wake kulingana na kanuni zake zenyewe; haki ya kumwabudu Mungu kwa ibada za hadhara; haki ya kusaidia wanajumuiya wake kuendesha dini yao, na kuwakuza kwa mafundisho ya kidini; na kuanzisha idara ambazo wanajumuiya wake watashikamana katika kupanga maisha yao kulingana na kanuni zao za kidini.

Kadhalika, jumuiya za kidini zina haki za kutokuzuiliwa kwa njia za kisheria au kwa matendo ya utawala kutoka katika upande wa serikali, katika kuchagua, katika kufunza, kuwaweka na kuwahamisha wahudumu wake, katika kuwasiliana na wakuu wa jumuiya za kidini wanaoishi nchi nyingine za dunia, kujenga majengo kwa ajili ya masuala ya dini, na katika kujipatia na kutumia mali wanazohitaji.

Zaidi ya hayo, jumuiya za kidini zina haki ya kutokuzuiliwa kufundisha na kutoa ushuhuda hadharani kwa imani yao, kwa maneno na maandishi. Hata hivyo, katika kueneza imani ya dini [yao] na katika kuziingiza kawaida za dini, lazima wakati wote kuepukana na kitendo chochote kinachoonekana kitashurutisha, au kukosesha uaminifu, au kushawishi kwa namna isiyofaa, hasa wakati wanaposhughulikiwa wale wasiosoma au maskini. Kutenda vile lazima kufikiriwe kuwa ni matumizi mabaya ya haki ya binafsi na uvunjaji wa haki za wengine.

Inaendana na uhuru wa dini haki ya jumuiya za kidini kutokuzuiliwa katika kuonyesha thamani halisi ya mafundisho yake katika kutengeneza jamii na kuhuisha matendo yote ya binadamu. Mwishowe, ile haki ya watu ambao, wakisukumwa na hisia zao za kidini, waweza kwa uhuru kufanya mikutano au kuanzisha makundi yenye shabaha ya kulea kielimu, kiutamaduni, kiufadhili, na kijamii, inajengwa juu ya tabia ya binadamu ya kushikamana na wengine na juu ya maumbile yenyewe ya kidini.

Uhuru wa dini wa familia

5. Kila familia ni jamii yenye haki zake pekee za msingi. Familia ina haki ya kupanga kwa uhuru maisha yake ya kidini katika nyumba kwa uongozi wa wazazi. Hawa wana haki ya kuamua kulingana na imani yao mtindo wa kufundisha watoto wao dini. Kwa hiyo, serikali lazima itambue haki ya wazazi ya kuchagua kwa uhuru halisi shule au njia nyingine ya kujipatia elimu. Kwa njia moja au nyingine wazazi wasitwishwe mizigo inayoweza kuathiri uhuru wao wa kuchagua. Zaidi ya hayo, haki za wazazi zinavunjwa kama watoto wao watalazimishwa kujifunza masomo ambayo hayaendani na imani ya wazazi wao au kama wanalazimishwa mfumo mmoja tu wa elimu ambamo malezi yoyote ya dini hayamo ndani yake.

Kuhifadhi uhuru wa dini

6. Manufaa ya wote katika jamii yamo katika jumla ya njia za maisha ya kijamii ambazo zinawawezesha watu kupata utimilifu wao kwa urahisi zaidi. Manufaa hayo yamo hasa katika kulinda haki na wajibu wa binadamu[5]. Kwa sababu hiyo ulinzi wa haki ya uhuru wa dini ni wajibu wa kila mmoja kama raia, wa makundi ya kijamii, wa serikali, wa Kanisa pamoja na jumuiya nyingine za kidini. Kila moja ya hizo ina wajibu katika masuala yanayohusiana na utendaji wake halisi katika kuyakuza manufaa ya wote.

Ulinzi na uendelezaji wa haki za msingi za binadamu ni wajibu wa lazima wa kila serikali[6]. Kwa hiyo serikali ni lazima ishughulike katika kulinda uhuru wa dini kwa raia wote kwa sheria za haki na njia nyinginezo zenye kuleta mafanikio. Serikali ni lazima isaidie kuanzisha hali bora katika kuimarisha maisha ya kidini ili kwamba raia wawe kweli katika nafasi ya kutenda haki zao za kidini na kutimiza wajibu wao ili jamii yenyewe ifurahie mafaa ya haki na amani ambayo huanzia kutoka katika uaminifu wa watu kwa Mungu na kwa utashi wake mtakatifu[7].

Kama, kutokana na mazingira ya pekee ya mataifa fulani, katika mfumo wa kisheria wa jamii fulani, jumuiya mojawapo ya kidini inapewa idhini mahsusi na serikali, lazima wakati huohuo raia wote na jumuiya nyinginezo za kidini zitambuliwe na kuheshimiwa kama zina haki nazo pia katika masuala ya dini.

Hatimaye, serikali lazima isimamie usawa wa raia mbele ya sheria, ambao unahusu nao pia manufaa ya wote katika jamii, ili usidhuriwe kamwe, wala kwa uwazi, wala kwa siri, kwa sababu za kidini; na kwamba usiwepo ubaguzi kati ya raia.

Kutokana na hilo ni wazi kwamba si halali serikali kuwalazimisha raia wake kwa nguvu au kwa kutisha, au kwa njia nyingine yoyote, kukiri au kuasi dini, au kumzuia mtu yeyote kujiunga au kujitenga na jumuiya ya kidini. Tena, ni kosa kubwa zaidi dhidi ya mapenzi ya Mungu na dhidi ya haki tukufu za mtu binafsi na za jumuiya ya mataifa, pale nguvu inapotumika kwa namna yoyote kufuta au kukandamiza dini, iwe kwa dunia nzima au katika sehemu moja tu, au katika jumuiya fulani.

Mipaka ya uhuru wa dini

7. Haki ya uhuru katika masuala ya dini inatumika katika jamii ya watu. Kwa sababu hii matumizi yake yanapangwa na sheria fulani.

Katika matumizi ya uhuru wowote, watu lazima waheshimu kanuni ya kimaadili ya uwajibikaji wa binafsi na wa kijamii. Katika kutumia haki zake, mtu binafsi na makundi ya kijamii, kwa mujibu wa sheria ya kimaadili, lazima kuzijali haki za wengine, na pia wajibu wao kwa wengine na manufaa ya wote kwa pamoja. Watu wote lazima watendeane kwa haki na kiutu.

Zaidi ya hayo, kutokana na kwamba jamii inayo haki ya kujilinda dhidi ya madhulumu yanayofanywa kwa udhuru wa uhuru wa dini, wajibu wa kutoa ulinzi huo umo hasa mikononi mwa serikali tawala. Hata hivyo, hilo lisifanywe kwa hiari mbovu (modo arbitrario) au kwa matendo yasiyo halali ya upendeleo, bali kulingana na sheria ambazo zinaendana na utaratibu wa maadili halisi. Sheria hizo zinahitajika kwa ulinzi mahsusi wa haki za raia wote, na kwa maafikiano yao ya amani. Ni za lazima pia kwa ulinzi wa kufaa wa usalama wa haki ambao hupatikana katika mahali ambapo watu wanaishi pamoja kwa mpangilio wao bora katika haki ya kweli, na zahitajika pia kwa ajili ya kulinda maadili ya wote. Hayo yote ni misingi ya manufaa ya wote na yanatambulikana kijumla kwa jina la usalama katika jamii (ordinis publicis). Kwa maana lazima ihifadhiwe kawaida iliyopo juu ya uhuru kamili katika jamii, ambayo kwayo mtu apewe uhuru mpana zaidi iwezekanavyo, tena bila kupunguzwa isipokuwa pale ionekanapo kuwa ni lazima kufanya hivyo.

Kulea katika matumizi halali ya uhuru

8. Binadamu wa sasa wanasongwa kwa namna mbalimbali na wapo katika hatari ya kuzuiwa kuyafuata maamuzi yao huru (libero consilio). Kwa upande mwingine, wapo wengi ambao wanasingizia uhuru huo, wakikaribia kukataa maongozi yoyote na kupunguza uzito wa wajibu wa utii.

Kwa sababu hiyo, Mtaguso huu wa Vatikano unamsihi kila mmoja, hasa wale wenye wajibu wa kuelimisha wengine, kujitahidi kuwalea watu ambao kwa kuheshimu maadili na kutii mamlaka iliyo halali, wawe wapenzi wa uhuru wa kweli; yaani watu ambao watafanya maamuzi yao katika mwanga wa ukweli, wenye kuelekeza shughuli zao katika roho ya uwajibikaji, wakifanya juhudi kufuatilia yaliyo ya kweli na ya haki, wakishirikiana kwa hiari na wengine.

Kwa hiyo, uhuru wa dini watakiwa kuwa na lengo na nia ya kuwafanya watu kutenda kazi zao katika maisha ya kijamii kwa uwajibikaji mkubwa zaidi.

II - UHURU WA DINI KATIKA MWANGA WA UFUNUO

Mafundisho juu ya uhuru wa dini yana misingi yake katika Ufunuo

9. Tamko la Mtaguso Mkuu mintarafu haki ya binadamu ya uhuru wa dini, msingi wake ni hadhi ya mwanadamu, ambayo madai yake yamezidi kueleweka wazi katika akili ya binadamu kwa mang’amuzi ya karne nyingi. Zaidi ya hayo, mafundisho haya juu ya uhuru wa dini, mzizi wake ni Ufunuo wa kimungu, na kwa sababu hiyo wakristo wana wajibu wa kuuheshimu kwa juhudi zao zote. Ingawa Ufunuo hautamki wazi haki ya uhuru kutoka katika mashurutisho ya nje katika masuala ya dini, hata hivyo huonyesha wazi hadhi ya binadamu katika undani wake wote. Vilevile hutuonyesha heshima ya Kristo kwa uhuru ambao binadamu anao katika kutekeleza wajibu wake wa kuliamini Neno la Mungu, na hutufundisha roho ambayo wafuasi wa [Bwana wetu Yesu Kristo aliye] Mwalimu wanapasika kuitambua na kuifuata katika mambo yote. Kwa hayo yote zaelezwa kanuni za jumla ambamo mafundisho ya hati hii kuhusu uhuru wa dini yanao msingi wake. Zaidi ya yote, uhuru wa dini katika jamii upo bega kwa bega na uhuru wa kutenda kulingana na imani ya kikristo.

Uhuru wa kutenda kulingana na imani

10. Kati ya vipengere vya msingi vya mafundisho ya kikatoliki, ukweli ambao umo katika neno la Mungu, na ambao mara kwa mara umehubiriwa na mababa[8], ni kwamba itikio la binadamu kwa Mungu katika imani latakiwa kuwa huru, na kwa hiyo yeyote asilazimishwe kuifuata imani kinyume na matashi yake[9]. Tendo la imani, kwa maumbile yake, ni tendo la hiari. Mwanadamu aliyekombolewa na Kristo Mwokozi na kuitwa katika Yesu Kristo kufanywa mwana[10], hawezi kushikamana na Mungu anayejifunua kwake, mpaka awe amevutwa na Baba[11], asipomtolea Mungu heshima ya imani iliyo kamili na huru. Kwa hiyo hulingana na msingi wa imani kwamba, katika masuala ya dini, kila aina ya shurutisho lifanywalo na watu yatakiwa kuondolewa. Hivyo, kanuni ya uhuru wa dini huchangia kwa vikubwa sana kwa maendeleo ya mazingira ambamo watu wanaweza kukaribishwa kwa urahisi katika imani ya kikristo, na wanaweza kuishikilia kwa hiari na kutoa ushuhuda wao kwa matendo katika kila uwanja wa maisha yao.

Namna ya kutenda ya Kristo na Mitume

11. Mungu anawaita binadamu kumtumikia katika roho na ukweli. Kwa sababu hiyo wanafungwa na dhamiri yao lakini hawashurutishwi. Mungu anaijali hadhi ya binadamu ambaye alimwumba. Binadamu anatakiwa kujiongoza kwa maamuzi yake mwenyewe na kuufurahia uhuru wake. Ukweli huu ulipata utimilifu wake katika Kristo Yesu, ambamo Mungu alijifunua yeye mwenyewe pamoja na njia zake kikamilifu. Kwa Kristo ambaye ndiye Mwalimu wetu na Bwana[12], na wakati huohuo yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo[13], alitenda kwa uvumilivu katika kuwavuta na kuwakaribisha wafuasi wake[14]. Alitegemeza na kuthibitisha mahubiri yake kwa miujiza ili kuanzisha na kuimarisha imani kwa wasikilizaji wake, lakini bila kutaka kuwashurutisha[15]. Hakika alilaumu kutokuamini kwa wasikilizaji wake, lakini aliacha kisasi kwa Mungu katika siku ya hukumu[16]. Alipowatuma Mitume wake ulimwenguni aliwaambia, “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa” (Mk 16:16). Alielewa kwamba magugu yamepandwa pamoja na ngano, lakini aliamuru kuyaacha yakue mpaka wakati wa mavuno siku ya mwisho[17]. Hakutaka kuwa Masiya wa kisiasa ambaye angewatawala watu kwa nguvu[18], lakini alipendelea kujiita Mwana wa Adamu aliyekuja kutumikia na “kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” (Mk 10:15). Alijionyesha mwenyewe kama Mtumishi mwaminifu wa Mungu[19] ambaye “mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima” (Mt 12:20). Aliijali serikali na haki zake pale alipoamuru kutoa kodi kwa Kaisari, lakini alionya wazi kwamba haki za Mungu zilizo kubwa zaidi lazima ziheshimiwe: “Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu” (Mt 22:21). Hatimaye alikamilisha ufunuo wake alipotimiza msalabani kazi ya ukombozi ambayo ilileta wokovu na uhuru halisi kwa wanadamu. Kwani aliushuhudia ukweli[20] lakini hakutaka kuwatwisha kwa nguvu wale walioupinga. Ufalme wake haudai kutumia nguvu[21], bali hujengwa kwa kushuhudia ukweli na kuusikiliza; pia hukua kwa njia ya upendo ambao Kristo aliyeinuliwa msalabani huwavuta watu wote kwake[22].

Wakiongozwa na neno la Kristo na mifano yake, Mitume walifuata njia ileile. Tangu mwanzo kabisa wa Kanisa, wafuasi wa Kristo walipigania kuwaongoza watu kumkiri Kristo kama Bwana. Hata hivyo, si kwa kutumia nguvu, au kwa mbinu zisizostahi Injili bali hasa kwa nguvu ya neno la Mungu[23]. Kwa uthabiti walihubiri kwa watu wote mpango wa Mungu Mwokozi, “ambaye hutaka watu wote waokolewe na kupata kujua yaliyo kweli.” (1Tim 2:4). Wakati huohuo lakini, waliwaheshimu wadhaifu hata kama walikuwa katika makosa, na kwa njia hii waliweka wazi ya kuwa “kila mtu miongoni mwetu atatoa hesabu zake mwenyewe mbele ya Mungu” (Rum 14:12)[24] na kwa sababu hiyo ana wajibu wa kufuata dhamiri yake tu. Kama [alivyofanya] Kristo, Mitume walijaribu siku zote kutoa ushuhuda kwa ukweli wa Mungu na walionyesha uthabiti mkubwa katika kunena “neno la Mungu kwa ujasiri” (Mdo 4:31)[25] mbele ya watu wa kawaida na watawala. Kwa imani madhubuti waliamini kwamba Injili yenyewe ni nguvu halisi ya Mungu kwa wokovu wa wote waaminio[26], kwa hiyo wakadharau “silaha zote za kidunia”[27] na kufuata mfano wa upole na wema wa Kristo, wakahubiri neno la Mungu kwa ujasiri wakiwa na imani katika nguvu za kimungu za neno hilo, ambazo huvunja nguvu za adui zake Mungu[28] na kuwaongoza watu kuamini na kumtumikia Kristo[29]. Kama Mwalimu wao, Mitume pia walitambua mamlaka halali za kiserikali: “Kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu” anafundisha Mtume, ambaye tena anaagiza: “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; ... ampingaye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu” (Rum 13:1-2)[30]. Lakini wakati huohuo hawakuogopa kubisha serikali iliyopingana na matashi matakatifu ya Mungu: “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu” (Mdo 5:29)[31]. Hii ndiyo njia ambayo mashahidi na waamini wasio na idadi wameifuata kwa karne zote katika dunia yote.

Kanisa linafuata nyayo za Kristo na Mitume

12. Kwa hiyo Kanisa, aminifu kwa ukweli wa Injili, linaifuata njia ya Kristo na ya Mitume pale linapoutambua uhuru wa dini kwamba unalingana na hadhi ya binadamu, pia na ufunuo wa kimungu, na linapoutegemeza. Kwa karne zote Kanisa limehifadhi na kurithisha mafundisho ambayo limepokea kutoka kwa Mwalimu wake na Mitume. Ingawa katika maisha ya Taifa la Mungu, katika kuhiji kwake ndani ya mabadiliko ya kihistoria ya kibinadamu, mara nyingine kumetokea mfumo wa tabia usiolingana na roho ya Injili, tena wakati fulani umepingana nayo, hata hivyo mafundisho ya Kanisa yamebaki kwamba mtu yeyote asishurutishwe katika kuishikilia imani.

Kwa hiyo chachu ya Injili imekuwa kwa muda mrefu ikifanya kazi katika fikra za binadamu na imetoa mchango mkubwa kwa karne zote kuitambua kwa upana zaidi hadhi yao kama binadamu. Imetoa mchango pia katika makuzi ya sadikisho ya kuwa katika masuala ya dini binadamu anatakiwa kuwa huru kutoka katika shurutisho lolote ndani ya jamii.

Uhuru wa Kanisa

13. Kati ya mambo ambayo yanahusiana na manufaa ya Kanisa, waama kwa manufaa ya jamii yote hapa duniani, mambo ambayo ni lazima kila mahali na kwa nyakati zote kuhifadhiwa na kulindwa kutoka katika madhara yoyote, hakika la muhimu ni kuwa Kanisa lifurahie uhuru wa kutenda, unaodaiwa kwa ajili ya kushughulikia wokovu wa wanadamu[32]. Huu ndio uhuru mtukufu ambao Mwana pekee wa Mungu alilijalia Kanisa alilolinunua kwa damu yake. Kwa kweli uhuru huo unahusika sana na Kanisa, kiasi kwamba wanaoukataa wanapinga matashi ya Mungu. Uhuru wa Kanisa ni kanuni ya msingi ya mahusiano kati ya Kanisa na mamlaka ya kiserikali na mfumo wote wa kijamii.

Katika jamii ya watu na mbele ya kila serikali Kanisa linadai uhuru wake, kwa vile ni lenye mamlaka ya kiroho, lililoasisiwa na Kristo Bwana aliyelipatia agizo na wajibu wa kwenda duniani pote kuhubiri Injili kwa kila kiumbe[33]. Hali kadhalika, Kanisa linadai kwake uhuru kwa vile ni jumuiya ya watu wenye haki ya kuishi katika jamii kuendana na sheria za imani ya kikristo[34].

Wakati muundo wa uhuru wa dini hautangazwi tu kwa maneno au kuidhinishwa tu kisheria, bali hutendeka kweli, hapo tu ndipo Kanisa huifurahia kisheria na kimatendo hali ya kudumu ya uhuru unaohitajika katika kutimiliza utume wa kimungu. Mamlaka ya Kanisa imesisitiza zaidi na zaidi katika kudai uhuru wake katika jamii[35]. Wakati huohuo wakristo, vilevile kama watu wengine, wanayo haki ya kisheria ya kutokuzuiliwa kuishi kadiri ya dhamiri yao. Kuna mlingano, kwa hiyo, kati ya uhuru wa Kanisa na ule uhuru wa dini ambao lazima utambuliwe kama haki ya watu wote na wa jumuiya zote, na usio na budi kuidhinishwa kisheria.

Utume wa Kanisa

14. Kanisa Katoliki, ili kutimiza amri ya Mungu: “Mkayafanye mataifa yote kuwa wanafunzi” (Mt 28:19), lazima litumie nguvu zote ili “Neno la Mungu liendelee na kutukuzwa” (2The 3:1).

Kwa hiyo Kanisa huhimiza kwa ari watoto wake ili kwanza kabisa zifanyike “dua na sala, na maombezi na shukrani kwa ajili ya watu wote... Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele ya Mungu Mwokozi wetu, ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli” (1Tim 2:1-4).

Aidha wakristo, katika kujenga dhamiri zao, wanatakiwa kuzingatia kwa makini mafundisho matakatifu na ya hakika ya Kanisa[36]. Kwa sababu Kanisa Katoliki ni mwalimu wa ukweli kwa mapenzi ya Kristo, na ni wajibu wake kuhubiri na kufundisha kwa nguvu na bila woga Ukweli ambao ni Kristo mwenyewe, na wakati huohuo kutangaza na kuthibitisha kwa mamlaka yake kanuni za muundo wa kimaadili ambazo hutokana na maumbile yenyewe ya binadamu. Aidha wakristo watakiwa kuwakaribia kwa busara wale walio nje, “katika Roho Mtakatifu, katika upendo usio unafiki, katika neno la kweli” (2Kor 6:6-7), na wanatakiwa kujibidiisha, hata kama itawapasa kumwaga damu, katika kueneza mwanga wa uzima kwa ujasiri wote[37] na nguvu ya kitume.

Mwanafunzi anao wajibu mkubwa kwa Kristo Mwalimu wake, wa kujua zaidi na zaidi ukweli aliopokea kutoka kwake, wa kuwa mwaminifu katika kuutangaza na kuulinda kwa juhudi bila kutumia njia zinazokwenda kinyume na roho ya Injili. Wakati huohuo upendo wa Kristo humbidiisha kuwatendea kwa upendo, busara na uvumilivu wale ambao wapo katika makosa au kutokujua kuhusu imani[38]. Kwa hiyo hana budi kuzingatia wajibu wake kwa Kristo, Neno aletaye uzima, ambaye hutakiwa kuhubiriwa, na pia haki za binadamu, na kipimo cha neema ambayo Mungu, kwa njia ya Kristo, hutoa kwa kila mtu, amwitaye kukubali na kuikiri imani kwa uhuru.

Hitimisho

15. Ni hakika, kwa hiyo, kwamba wanadamu wa sasa wanapenda kukiri dini yao kwa uhuru kibinafsi au hadharani. Na kwa hakika ni kweli kwamba uhuru huo wa dini umekwisha tangazwa kama haki ya kisheria katika Katiba [za nchi] zilizo nyingi na umetambuliwa kwa dhati katika hati za kimataifa[39].

Lakini kuna miundo ya serikali ambayo, hata kama uhuru wa dini katika kuabudu umetambulika katika Katiba zao, serikali zenyewe zinapigania kuwakataza raia katika kukiri dini yao, na kufanya maisha ya jumuiya za kidini kuwa magumu na ya hatari.

Mtaguso Mkuu, pamoja na kuzifurahia hizo ishara pendevu za nyakati hizi, na kulaumu kwa uchungu matendo yale yenye lawama, unawasihi waamini wakatoliki na kuwaalika watu wote ili watafakari kwa makini jinsi uhuru wa dini unavyohitajika, hasa katika mazingira ya kisasa kwa familia ya wanadamu.

Ni dhahiri kwamba watu wote wa mataifa yote huzidi kuunganika pamoja, na watu wa tamaduni na dini mbalimbali wanafungamana katika mahusiano ya ndani zaidi. Pamoja na hayo, utambuzi wa wajibu wake hukua ndani ya kila mmoja. Ndiyo sababu, ili yaweze kuwepo na kukua mahusiano yenye amani na uelewano katika jamii nzima ya watu, inatakiwa kwamba uhuru wa dini ulindwe na kuhifadhiwa kwa njia ya sheria za kufaa, na ziheshimiwe wajibu na haki za msingi za binadamu zinazomwezesha kuishi kwa uhuru katika jamii maisha yanayolingana na dini yake.

Mungu aliye Baba wa wote ajalie kwamba familia ya wanadamu [wote], kwa njia ya kuheshimu kwa makini utekelezaji wa uhuru wa dini katika jamii, kwa neema ya Kristo na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, iongozwe mpaka kuingia katika ule “uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu” (Rum 8:21) ulio bora sana na wa milele.

 

Mambo yote yaliyoamuliwa katika tamko hili, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

 

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 7 Desemba 1965

 

Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki

(zinafuata sahihi za Mababa)

 

     


[1] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Pacem in terris, 11 Apr. 1963: AAS 55 (1963) uk.279; ibid. uk.265; Pius XII, Nuntius radiophonicus, 24 Dec. 1944: AAS 37 (1945) uk.14.

[2] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Pacem in terris, 11 Apr. 1963: AAS 55 (1963) uk.260-261; Pius XII, Nuntius radiophonicus, 24 Dec. 1942: AAS 35 (1943) uk.19; Pius XI, Litt. Encycl. Mit Brennender Sorge, 14 Mar. 1937: AAS 29 (1937) uk.160; Leo XIII, Litt. Encycl. Libertas praestantissimum, 20 Jun. 1888: Acta Leonis XIII 8 (1888) uk.237-238.

[3] Taz. Mt. Thomas, Summa Theol., I II, q. 91, a. 1; q. 93, a. 1-2.

[4] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Pacem in terris, 11 Apr. 1963: AAS 55 (1963) uk.270; Paulus VI, Nuntius radiophonicus, 22 Dec. 1964; AAS 57 (1965) uk. 181-182; Mt. Thomas, Summa Theologica, I-II, q. 91, a. 4 c.

[5] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl.  Mater et Magistra, 15 May 1961: AAS 53 (1961) uk. 417; Id., Litt. Encycl. Pacem in terris, 11 Apr. 1963: AAS 55 (1963) uk. 273.

[6] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl.  Pacem in terris, 11 Apr. 1963: AAS 55 (1963) uk. 273-274; Pius XII, Nuntius radiophonicus, 1 Jun. 1942; AAS 33 (1941) uk. 200.

[7] Taz. Leo XIII, Litt. encycl. Immortale Dei, 1 Nov. 1885:  AAS 18 (1885) uk.161.

[8] Taz. Lactantius, Divinarum Institutionum, Lib. V,19: CSEL 19, uk.463-464, 465;  PL 6, 614 et 616 (cap. 20); Mt. Ambrosius, Epistola ad Valentinianum Imp., Ep. 21: PL 16, 1005; Mt. Augustinus, Contra litteras Petiliani, lib. II, cap. 83: CSEL 52, uk.112; PL 33, 98; Id., Ep. 34: PL 33, 132; Id., Ep. 35, 135; Mt. Gregorius Magnus,  Epistola ad Virgilium et Theodorum Episcopos Massiliae Galliarum, Registrum Epistolarum I, 45: MGH, Ep. 1, uk. 72; PL 77, 510-511 (lib. I, ep. 47); Id., Epistola ad Iohannem Episcopum Constantinopolitanum, Registrum Epistolarum III, 52: MGH, Ep. 1, uk. 210; PL 77, 649 (lib. III, ep. 53); taz. D. 45, c.1(ed. Friedberg, col. 160); Conc. Tolet. IV, c.57: Mansi 10, 633; taz. D. 45, c.5 (ed. Friedberg, col. 161-162); Clemens III: X., V,6,9: (ed. Friedburg, col. 774); Innocentius III,  Epistola ad Arelatensem Archiepiscopum, X., III,42,3: (ed. Friedburg, col. 646).

[9] Taz. CIC, c.1351; Pius XII, Allocutio ad Praelatos auditores caeterosque officiales et administros Tribunalis S. Romanae Rotae, 6 Oct. 1946: AAS 38 (1946) uk.394; Id., Litt. Encycl. Mystici Corporis, 29 Jun. 1943: AAS 35 (1943) uk.243.

[10] Taz. Efe 1:5.

[11] Taz. Yn 6:44.

[12] Taz. Yn. 13:13.

[13] Taz. Mt 11:29.

[14] Taz. Mt 11:28-30; Yn 6:67-68.

[15] Taz. Mt. 9:28-29; Mk 9:23-24; 6:5-6; Paulus VI, Litt. Encycl. Ecclesiam suam, 6 Aug. 1964: AAS 56 (1964) uk.642-643.

[16] Taz. Mt 11:20-24; Rum 12:19-20; 2The 1:8.

[17] Taz. Mt 13:30, 40-42.

[18] Taz. Mt 4:8-10; Yn 6:15.

[19] Taz. Isa 42:1-4.

[20] Taz. Yn 18:37.

[21] Taz. Mt 26:51-53; Yn 18:36.

[22] Taz. Yn 12:32.

[23] Taz. 1Kor 2:3-5; 1The 2:3-5.

[24] Taz. Rum 14:1-23; 1Kor 8:9-13; 10:23-33.

[25] Taz. Efe 6:19-20.

[26] Taz. Rum 1:16.

[27] Taz. 2Kor 10:4; 1The 5:8-9.

[28] Taz. Efe 6:11-17.

[29] Taz. 2Kor 10:3-5.

[30] Taz. 1Pet 2:13-17.

[31] Taz. Mdo 4:19-20.

[32] Taz. Leo XIII, Litterae Officio sanctissimo, 22 Dec. 1887: AAS 20(1887) uk.269; Id., Litterae Ex litteris, 7 Apr. 1887: AAS 19(1886) uk.465.

[33] Taz. Mk 16:15; Mt 28:18-20; Pius XII, Litt. Encycl.  Summi Pontificatus, 20 Oct. 1939: AAS 31 (1939) uk.445-446.

[34] Taz. Pius XI, Litterae Firmissimam constantiam, 28 Mar. 1937: AAS 29(1937) uk.196.

[35] Taz. Pius XII, Allocutio Ci riesce, 6 Dec. 1953: AAS 45(1953) uk.802.

[36] Taz. Pius XII,  Nuntius radiophonicus, 23 Mar. 1952: AAS 44(1952) uk.270-278.

[37] Taz. Mdo 4:29.

[38] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Pacem in terris, 11 Apr. 1963: AAS 55(1963) uk.299-300.

[39] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Pacem in terris, 11 Apr. 1963: AAS 55(1963) uk.295-296.