Index

Back Top Print

[BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

Dikrii juu ya 
marekebisho ya maisha ya wakfu

PAULO ASKOFU
MTUMISHI WA WATUMISHI WA MMUNGU
PAMOJA NA MABABA  WA MTAGUSO MKUU
ATAKA HAYA YAKUMBUKWE DAIMA 

  

Utangulizi

1. MAPENDO KAMILI (Perfectae Caritatis) kwa kufuata mashauri ya kiinjili ni mada ambayo Mtaguso Mkuu umewahi kuonyesha hapo kwanza, katika konstitusio ambayo maneno ya kwanza ni “Mwanga wa mataifa”. Nayo chimbuko lake ni mafundisho na mifano ya Mwalimu wa kimungu, na yanaonekana kuwa ishara angavu ya Ufalme wa mbinguni. Hivi sasa, Mtaguso huohuo unakusudia kushughulikia maisha na nidhamu ya mashirika yale, ambayo wanashirika wake huahidi usafi wa moyo, umaskini na utii; hali kadhalika hukusudia kutegemeza mahitaji yake, kulingana na nyakati zetu.

Tangu mwanzoni mwa Kanisa walikuwepo watu, wanaume na wanawake, ambao kwa kutekeleza mashauri ya kiinjili walinuia kumfuata Kristo kwa hiari zaidi na kumwiga kwa karibu, na walienenda, kila mmoja kwa jinsi yake, katika maisha ya wakfu kwa Mungu. Wengi miongoni mwao, kwa kufuata msukumo wa Roho Mtakatifu, waliishi maisha ya upweke, au walianzisha familia za kitawa, ambazo Kanisa kwa mamlaka yake lilizikubali kwa moyo na kuziidhinisha. Hivyo, kwa mpango wa kimungu, wingi wa ajabu wa mashirika ya kitawa ukasitawi, nayo yamechangia sana ili Kanisa lisiwe tu limekamilishwa lipate kutenda kila tendo jema (taz. 2Tim 3:17), na liwe limeandaliwa hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe (taz. Efe 4:12), bali pia, liwe linapendeza kwa wingi wa karama mbalimbali za wanae, nalo lionekane pia kama bibiarusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe (taz. Ufu 21:2), na kwa njia yake hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane (taz. Efe 3:10).

Katika wingi huu wa karama, wale wote wanaoitwa na Mungu kutekeleza mashauri ya kiinjili na kuyatimiza kiaminifu, wanajiweka wakfu kwa Bwana kwa namna ya pekee, kwa kumfuasa Kristo ambaye, akiwa bikira na maskini (taz. Mt 8:20; Lk 9:58), aliwakomboa wanadamu na kuwatakatifuza kwa njia ya utii wake mpaka kufa msalabani (taz. Flp 2:8). Vivyo hivyo nao watu, walihimizwa na pendo ambalo Roho Mtakatifu amemimina mioyoni mwao (taz. Rum 5:5) wanaishi zaidi na zaidi kwa ajili ya Kristo na kwa ajili ya Mwili wake ulio Kanisa (taz. Kol 1:24). Kwa hiyo, kama wanavyojiunga kwa ari na Kristo kwa njia ya kujitolea kwao maisha yote, ni kadiri hiyohiyo maisha ya Kanisa yananufaika na utume wake unazidi kuwa na nguvu za kuleta matunda.

Kusudi thamani kuu ya maisha ya wakfu kwa njia ya uprofesi (professionem) wa mashauri ya kiinjili, pamoja na huduma zake muhimu katika mazingira ya leo, vilete manufaa makubwa katika Kanisa, Mtaguso huu Mkuu unaidhinisha kanuni zifuatazo, zihusuzo misingi ya kijumla tu ya upyaisho wa maisha na wa nidhamu unaotakiwa katika mashirika ya kitawa, na vilevile katika jamii za maisha ya pamoja pasipo nadhiri, na katika mashirika ya kilimwengu (secularium), hata ingawa kila taasisi inatakiwa kudumisha tabia yake. Sheria za pekee, zihusuzo maelezo na utendaji wa kanuni hizi zitatolewa na mamlaka ya Kanisa baada ya Mtaguso kufunga.

  

Kanuni za kijumla kwa ajili ya upyaisho ufaao

2. Upyaisho wa maisha ya kitawa unadai kurudi kwa daima kwenye chemchemi za maisha ya kikristo na za roho ya mwanzoni ya mashirika, na wakati huohuo kujilinganisha kwa mashirika yenyewe na mazingira ya nyakati yaliyobadilika. Upyaisho huo, chini ya msukumo wa Roho Mtakatifu na ya uongozi wa Kanisa, unatakiwa utekelezwe kadiri ya kanuni hizi za msingi:

   a) Kwa vile kanuni ya msingi ya maisha ya kitawa ni kumfuata Kristo kadiri ya agizo la Injili, basi hiyo inabidi iwe kanuni kuu ya kila shirika.

   b) Ni faida kwa Kanisa lenyewe kwamba mashirika yawe na tabia na huduma ya pekee. Kwa hiyo inafaa roho na lengo maalum la waanzilishi vifahamike na kuhifadhiwa, hali kadhalika mapokeo yanayofaa, kwa sababu hayo yote ni urithi wa kila shirika.

   c) Mashirika yote yashiriki katika maisha ya Kanisa na, kadiri ya tabia yake, yapokee na kuchangia kadiri ya uwezo wake, katika juhudi ya utendaji na malengo ya Kanisa lenyewe, katika mambo mbalimbali, kama vile ya kibiblia, kiliturujia, kidogma, kichungaji, kiekumeni, kimisioni na ya kijamii.

   d) Mashirika yawapatie wanashirika wake ufahamu wa kufaa wa hali ya nyakati na ya binadamu, kama vile ya mahitaji ya Kanisa, kusudi wenyewe, huku wakiweza kutambua kwa busara hali ya ulimwengu wa leo kadiri ya mwanga wa imani na wakiwaka ari ya kitume waweze kuleta manufaa kwa wengine kwa mafanikio makubwa.

   e) Kwa vile awali ya yote maisha ya kitawa yanalenga kuwawezesha wanachama wake wamfuate Kristo na waunganike na Mungu kwa kutimiliza mashauri ya kiinjili, lazima izingatiwe kwamba aina zozote zile za marekebisho, ziwe bora namna gani, hazitafanikisha, kama zisipoongozwa na upyaisho wa rohoni, ambao una nafasi ya kwanza katika kazi mbalimbali za utume wa nje pia.

   

Vigezo vya kimatendo vya upyaisho

3. Utaratibu wa maisha, wa sala na wa utendaji unapaswa kulinganishwa na hali ya leo ya kimwili na ya kisaikolojia ya watawa. Vilevile unatakiwa kulinganishwa na uhitaji wa kitume, na madai ya utamaduni, na mazingira ya kijamii na ya kiuchumi, kadiri ya tabia ya kila shirika. Na itakuwa hivyo popote pale, lakini hasa katika maeneo ya kimisioni.

 

Pia namna ya utawala katika mashirika inatakiwa ichunguzwe kadiri ya vigezo hivyohivyo.

Kwa sababu hiyo, katiba, “miongozo” (“directoria”), vitabu vya desturi, vya sala na vya maadhimisho, na sheria nyinginezo za aina hiyo zitengenezwe kwa namna inayofaa, ili, kwa kufuta kanuni zisizolingana na wakati huu, zibadilishwe kufuatana na hati mbalimbali zilizotolewa na Mtaguso huu Mkuu.

   

Wahusika wa kutimiliza upyaisho huu ni akina nani?

4. Upyaisho wa kufaa na marekebisho ya kweli haviwezi kutekelezwa pasipo ushirikiano wa wanashirika wote.

Kuweka kanuni za marekebisho na kutunga sheria zake, pamoja na kujipatia muda wa kutosha kibusara wa kuzijaribu, ni wajibu wa mamlaka halali tu, hasa mikutano mikuu, bila kusahau, kila inapotakiwa, kupewa idhini na Kiti Kitakatifu au na Askofu wa mahali, kwa mujibu wa sheria. Wakuu [wa shirika], katika yale yote yahusuyo maendeleo ya shirika zima, washauriane na wanashirika wenzao na kuwasikiliza kwa namna nzuri.

Kwa ajili ya upyaisho wa monasteri za wamonaki wa kike (monialium), inawezekana kupata kura na mashauriano ya mikutano ya shirikisho au ya mikutano mingine inayoitiwa kihalali.

Lakini lazima wote wakumbuke kwamba upyaisho unaotarajiwa upo katika kushika kikamilifu kanuni na katiba, kuliko kuongeza sheria juu ya sheria.

    

Madokezo ya awali yaliyo sawa katika kila aina ya maisha ya kitawa

5. Kabla ya yote, wanashirika wa shirika lolote wakumbuke kwamba waliitikia wito wa Mungu kwa kuweka nadhiri za mashauri ya kiinjili, ili kwamba wao wenyewe, wakiwa wamekufa kwa dhambi (taz. Rum 6:11), na pia wamekataa ulimwengu, wanaishi kwa ajili ya Mungu peke yake. Maisha yao yote yamekuwa kwa ajili ya kumtumikia Mungu, nayo ni aina ya pekee ya kujiweka wakfu yenye msingi imara katika uwakfu wa ubatizo, nako ni ufafanuzi wake uliokamilika hasa.

Na kwa vile Kanisa limepokea hayo majitoleo yao, wajue wenyewe kwamba nao wako katika utumishi wa Kanisa.

Utumishi huo kwa Mungu utachochea na kusitawisha utekelezaji wa fadhila, hasa wa unyenyekevu na utii, wa nguvu na wa usafi wa moyo, ambao kwao inawezekana kushiriki katika kujinyenyekeza kwa Kristo (taz. Flp 2:7-8) na pia uzima wake katika Roho (taz. Rum 8:1-13).

Hivyo watawa, kwa kuwa waaminifu katika nadhiri zao, wakiacha vyote kwa ajili ya upendo wa Kristo (taz. Mk 10:28), wamfuate yeye (taz. Mt 19:21) kama ndiye kile kitu kimoja tu kinachotakiwa (taz. Lk 10:42), wakisikiliza maneno yake (taz. Lk 10:39) na kujishughulisha kwa mambo yake (taz. 1Kor 7:32).

Kwa hiyo ni muhimu watawa wa shirika lolote, huku wakimtafuta Mungu peke yake kuliko yote, waunganishe taamuli, ambayo kwayo waweza kuambatana na Mungu kwa akili na kwa moyo, na ari ya kitume, ambayo inawahimiza kusaidia katika kazi ya ukombozi na kueneza ufalme wa Mungu.

   

Maisha ya kiroho yana nafasi ya kwanza

6. Wenye kuweka nadhiri za mashauri ya kiinjili, kabla ya yote wamtafute na kumpenda Mungu aliyewapenda kwanza (taz. 1Yoh 4:10), na katika mazingira yote wafanye bidii kulisha uhai uliofichwa pamoja na Kristo katika Mungu (taz. Kol 3:3), ambamo huchimbuka na kukuzwa upendo wa jirani kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu na ujenzi wa Kanisa. Mapendo hayo ni moyo na uongozi wa utekelezaji wa mashauri ya kiinjili.

Kwa sababu hiyo wanashirika watawa wasitawishe kwa makini kuu roho ya sala na sala zenyewe, wakiyachota haya katika chemchemi zilizo safi za elimuroho (spiritualitatis) ya kikristo. Awali ya yote, kila siku washike mikononi Maandiko Matakatifu, ili kwa njia ya kusoma na kutafakari vitabu vitakatifu wajifunze “uzuri usio na kiasi wa kumjua Yesu Kristo” (Flp 3:8). Waadhimishe liturujia takatifu, hasa fumbo tukufu la Ekaristi kwa moyo na vitendo vinavyolingana na mwongozo wa Kanisa, na wakinywesha maisha yao ya kiroho kwenye chemchemi hii yenye utamu tele.

Kwa namna hiyo, wakiwa wanajilisha katika meza ya sheria ya kimungu, na ya altare takatifu wawapende kindugu viungo vya Kristo; kwa roho ya kimwana wawaheshimu na kuwapenda wachungaji [wa Kanisa]; wapate zaidi na zaidi kuishi na kuwa na nia moja na Kanisa na wajitolee kabisa katika huduma ya utume wake.

   

Mashirika ya taamuli

7. Mashirika ambayo yajishughulisha muda wote na taamuli, kiasi kwamba wanashirika wake wanamtafuta Mungu tu katika upweke na katika ukimya, katika sala za daima na matendo ya toba kwa moyo, ingawa taabu za kazi za kitume zinaelemea vikali, yanastahili kuendelea kuwa na nafasi yenye kuheshimiwa katika Mwili wa fumbo wa Kristo, ambamo “viungo vyote havitendi kazi moja” (Rum 12:4). Maana watawa hao wamtolea Mungu sadaka ya sifa iliyo bora na, kwa kuzaa matunda tele ya utakatifu, wanakuwa fahari na mfano kwa watu wa Mungu, ambao watapata usitawi kwa njia ya uzalishaji wa utume [unaotekelezwa] katika fumbo. Kwa hiyo [wao] wanaonekana kuwa ni utukufu wa Kanisa na chemchemi ya neema ya kimungu. Lakini hata mtindo wao wa maisha uchunguzwe kadiri ya kanuni na vigezo vya upyaisho vilivyoelezwa hapa juu; lakini kwa uangalifu mkubwa mbele ya utaratibu wa maisha yao ya kujitenga na ulimwengu na wa mazoezi ya kawaida ya maisha ya taamuli.

   

Mashirika yenye kufanya kazi ya kitume

8. Katika Kanisa yapo mashirika mengi, ya kikleri au ya kilei, yenye kujishughulisha na kazi za kitume; nayo yana karama mbalimbali kulingana na neema yalizopewa, “ikiwa tuna karama ya huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kurehemu, kwa furaha” (Rum 12:7-8). “Basi, pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule” (1Kor 12:4).

Katika mashirika hayo kazi za kitume na matendo ya huruma ni sehemu rasmi ya maisha yao ya kitawa, kwa vile hizo kazi ni huduma takatifu na tendo maalum la upendo ambalo wamekabidhiwa na Kanisa na lazima litimizwe kwa jina la Kanisa. Kwa sababu hiyo, maisha yote ya kitawa ya wanashirika wake yatakiwa kupenywa na roho ya kitume, na kazi zote za kitume zipenywe na roho ya ibada. Na kusudi watawa hao kabla ya yote waitikie wito wao wa kumfuasa Kristo na kumtumikia yeye katika viungo vyake, inabidi kazi za kitume zitekelezwe katika muungano kamili na Bwana Yesu. Kwa njia hiyo mapendo kwa Mungu na jirani yazidi kuongezeka.

Mashirika hayo yalinganishe kanuni na desturi zao na mahitaji ya utume yanaoutekeleza. Na kwa vile mitindo ya maisha ya kitawa yenye kujishughulisha na kazi za kitume ni ya aina nyingi, marekebisho yanatakiwa kufanywa kwa kuzingatia utofauti huo, na pia kwamba katika mashirika mbalimbali maisha ya watawa walio katika huduma ya Kristo yategemezwe kwa vyombo vinavyowafaa na vinavyoendana na lengo lenyewe.

   

Kutunza maisha ya kimonaki na ya kikonventi

9. Uasisi wenye kusifika wa maisha ya kimonaki, ambao katika namna nyingi umejipatia heshima kuu katika Kanisa na katika jamii ya watu, uhifadhiwe kiaminifu na upate kuangaza zaidi na zaidi katika roho yake halisi katika Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Wajibu wa kwanza wa wamonaki ni kumtolea Mungu mkuu utumishi mnyenyekevu na mtukufu ndani ya kuta za monasteri, ama kwa kujitolea kabisa kwa ibada takatifu katika maisha ya faraghani, au kwa kujibebesha kihalali tendo fulani la kitume au la mapendo ya kikristo. Kwa kushika tabia maalum ya shirika lao, wamonaki wafanye upya mapokeo ya siku nyingi yenye mafaa, na wayarekebishe kulingana na mahitaji ya leo ya roho za watu, ili kuwezesha monasteri ziwe kama vitalu vyenye kuotesha wakristo.

Hali kadhalika mashirika ya kitawa, ambayo kwa mujibu wa kanuni au wa katiba yanaunganisha maisha ya kitume na wajibu wa kusali pamoja yakitunza desturi za kimonaki, yalinganishe utaratibu wa maisha yao na madai ya utume ule unaowafaa, ili kwamba mtindo wa maisha utunzwe kiaminifu, kwa vile ni wa manufaa makubwa kwa Kanisa.

   

Watawa walei

10. Maisha ya kitawa ya walei, wanaume kwa wanawake, ni hali iliyokamilika ya uprofesi wa mashauri ya kiinjili. Mtaguso Mkuu una heshima kubwa kwa maisha haya ya kitawa ya walei kwa sababu yanaleta manufaa makubwa kwa kazi ya kichungaji ya Kanisa katika uwanja wa malezi ya vijana, wa kuwatunza wagonjwa, na wa huduma nyinginezo. Kwa hiyo Mtaguso huu pamoja na kuwathibitisha katika wito wao wanachama wa mtindo wa namna hii ya maisha ya kitawa, unawahimiza pia walinganishe maisha yao na mahitaji ya siku hizi.

Mtaguso Mkuu unasema kwamba hakuna kizuio kwa mashirika ya kitawa ya kiume, kwa uamuzi wa Mkutano mkuu, wanachama wachache wasipokee sakramenti ya Daraja takatifu, kwa lengo la kusaidia katika nyumba zake mahitaji ya huduma ya kipadre, bila kubadilisha tabia yake ya msingi ya kuwa ya kilei.

  

Mashirika ya kilimwengu

11. Mashirika ya kilimwengu (Instituta saecularia), yangawa si mashirika ya kitawa, hata hivyo yanakuwa yana uprofesi wa kweli na kamili wa mashauri ya kiinjili katika ulimwengu, uliokubaliwa na Kanisa. Uprofesi huu unawapa [wanashirika wote] wanaume na wanawake, walei kwa wakleri, wanaoishi katika ulimwengu, hali ya wakfu. Kwa hiyo hao, kabla ya yote wanuie kujitolea kikamilifu kwa Mungu katika mapendo kamili, na mashirika yenyewe [hayo] yahifadhi tabia yao ya pekee, yaani ile ya kuwa ya kilimwengu, ili kuweza kutimiza kwa mafanikio popote katika ulimwengu na kama wangekuwa wa ulimwengu, ule utume ambao yaliundwa kwa ajili ya kuutekeleza.

Lakini itambulikane kuwa haiwezekani kutimiza wajibu huu muhimu namna hii kama wanashirika wake wasipopewa malezi katika mambo ya kimungu na ya kibinadamu, ili wawe kweli chachu katika ulimwengu kwa ajili ya kuimarisha na kukuza Mwili wa Kristo. Kwa hiyo wakubwa wao waangalie sana ili wanachama wao wapatiwe mafunzo hasa ya kiroho, na wasitawishe malezi yao.

   

Usafi wa moyo

12. Usafi wa moyo “kwa ajili ya ufalme wa mbinguni” (Mt 19:12), ambao watawa wanauwekea nadhiri, uheshimiwe kama karama ya pekee ya neema. Usafi wa moyo unaweka huru moyo wa mtu kwa namna ya pekee (taz. 1Kor 7:32-35) ili uzidi kuwaka mapendo kwa Mungu na kwa watu wote. Ni mfano wa pekee wa mema ya mbinguni, na pia njia inayowafaa sana watawa ili waweze kujitoa kwa moyo wote kwa utumishi wa Mungu na kwa kazi za kitume. Kwa namna hiyo watawa wanakumbusha mbele ya waamini wote ule uhusiano wa kindoa aliopanga Mungu – ambao utadhihirika waziwazi katika ulimwengu ujao – ambao umefanya Kanisa liwe na Kristo kama bwanaarusi wake pekee.

Kwa hiyo inatakiwa watawa, huku wakifanya bidii kudumu waaminifu kwa nadhiri zao, wayasadiki maneno ya Bwana na, kwa kutegemea msaada wa Mungu, wasijidai kufanikisha kwa nguvu zao binafsi, bali wajizoeshe katika kujihinisha na kujitawala kihisia. Wala wasiache kutumia misaada ya kawaida, yenye kufaa kwa siha ya akili na ya mwili. Hivyo hawataathiriwa na mafundisho mapotovu yenye kudai kuwa usafi kamili hauwezekani au huleta madhara kwa ukamilishaji wa binadamu, ila, kwa aina ya hisia ya kiroho, watafukuza yote yanayohatarisha usafi wa moyo. Aidha, wote, hasa Wakubwa wa mashirika, wafahamu kuwa usafi wa moyo utatunzwa kwa uhakika zaidi kama kati ya watawa unakuwepo upendo wa kweli wa kidugu katika maisha yao ya pamoja.

Kwa vile kutunza usafi kamili kunahusiana kwa ndani sana na mielekeo ya ndani ya hulka ya binadamu, makandidati wa kuweka nadhiri ya usafi wa moyo wasiambatane na hali hiyo, wala wasikubaliwe kwa hiyo, isipokuwa baada ya muda wa kutosha kweli wa kujaribu na baada ya kuwa wamekomaa kwa upande wa saikolojia na wa upendohisia. Waonywe kuhusu hatari zitakazokabili usafi wa moyo, pia wafundishwe kutunza daima usafi wa moyo ulio kwa ajili ya Mungu kama hali ya kuleta mema kwa uzima wa utu wao wenyewe.

  

Umaskini

13. Umaskini wa hiari kwa ajili ya kumfuata Kristo, ambao ni ishara yake yenye kusifiwa sana siku hizi, usitawishwe kwa makini na watawa; tena, ikitakiwa, utekelezwe kwa mitindo mipya. Ni njia ya kushiriki umaskini wa Kristo, ambaye amekuwa maskini kwa ajili yetu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba sisi tupate kuwa matajiri kwa umaskini wake (Taz. 2Kor 8:9; Mt 8:20).

Kwa habari ya nadhiri ya umaskini, haitoshi watawa wajiweke chini ya maagizo ya wakubwa kuhusu matumizi ya mali tu, ila inabidi watimize umaskini wa mali na wa roho, huku wakijiwekea hazina mbinguni (taz. Mt 6:20).

Wajione katika shughuli zao wamewekwa chini ya sheria ya kawaida ya kufanya kazi, na katika hayo pamoja na kujipatia riziki za maisha na za matendo yao wafukuze mahangaiko yasiyofaa na wayategemee Maongozi ya Baba wa mbinguni (taz. Mt 6:25).

Mashirika ya kitawa katika katiba zao yaweze kuruhusu wanashirika kujinyima urithi waliopata au watakaoupata.

Mashirika yenyewe, kwa kuzingatia mazingira ya mahali, yafanye bidii ili kutoa ushuhuda – kama kwa pamoja – wa umaskini, na kwa hiari watoe sehemu za mali zao kwa ajili ya mahitaji mengine ya Kanisa na kwa msaada kwa maskini, ambao watawa wote watakiwa kuwapenda kwa upendo wa Kristo (taz. Mt 19:21; 25:34-46; Yak 2:15-16; 1Yoh 3:17). Maprovinsi na nyumba mbalimbali za mashirika ya kitawa yaishirikiane katika mali zao za dunia, kusudi nyumba zile zilizo na mali nyingi zisaidie zile zenye mahitaji.

Mashirika, ingawa yanayo haki ya kumiliki yote yanayohitajika kwa maisha yake ya kidunia na kwa matendo yake, kadiri ya sheria na katiba zao, yaepukane na kila aina ya anasa, na mali za kupita kiasi na hamu ya kujilundikia mali nyingi.

   

Utii

14. Watawa kwa kuweka nadhiri ya utii wamtolea Mungu kabisa utashi wao kama sadaka ya nafsi zao, na kwa njia ya sadaka hiyo wajiunga na mapenzi ya Mungu yenye kuokoa, kwa namna ya kudumu na halisi. Kwa hiyo, kwa kuufuata mfano wa Yesu Kristo aliyekuja kufanya mapenzi ya Baba (taz. Yn 4:34; 5:30; Ebr 10:7; Zab 40:7-8) na “kwa kutwaa namna ya mtumwa” (Flp 2:7), kwa mateso yaliyompata alijifunza kutii (taz. Ebr 5:8); watawa kwa msukumo wa Roho Mtakatifu wanajiweka kwa moyo wa imani chini ya wakubwa [wao], watendao badala ya Mungu, na kwa njia yao waongozwa kuwatumikia ndugu wote katika Kristo, kama Kristo mwenyewe, kwa kujinyenyekesha kwake kwa Baba, alivyokuja kuwatumikia ndugu wote na kutoa nafsi yake kuwa fidia ya wengi (taz. Mt 20:28; Yn 10:14-18). Kwa njia hiyo wanajifunga zaidi na zaidi na utumishi wa Kanisa na wajibidisha kukifikia cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo (taz. Efe 4:13).

Kwa hiyo watawa, wakishika mapenzi ya Mungu kwa roho ya imani na ya upendo, kadiri ya kanuni na katiba, wawaheshimu kwa unyenyekevu wakubwa wao, wakitumia nguvu za akili na utashi, na fadhila za tabia na za neema katika kutimiza maagizo na kutekeleza wajibu waliokabidhiwa, wakitambua kwamba wanasaidia kujenga Mwili wa Kristo kadiri ya mpango wa Mungu. Kwa namna hiyo nadhiri ya utii, mbali na kupunguza hadhi ya mtu, inamwongoza kwa upeo wake, kwa vile inaupanua uhuru wa wana wa Mungu.  

Wakubwa [wa mashirika], kwa vile siku moja wataitwa na Mungu kutoa hesabu ya roho walizokabidhiwa (taz. Ebr 13:17), wakiwa watiifu kwa mapenzi ya Mungu katika kutimiza wajibu wao, watekeleze madaraka kwa moyo wa kujitolea kwa ndugu zao ili wapate kuonyesha mapendo ambayo kwayo Mungu anawapenda. Wawatawale watawa kama wana wa Mungu wakijali heshima ya utu, wakifanya bidii ili wakubali kwa hiari kuongozwa. Kwa hiyo wawaachie uhuru unaofaa hasa kuhusu masuala ya sakramenti ya kitubio na ya uongozi wa dhamiri. Wawaelekeze wanashirika kushirikiana nao kwa utii wenye utendaji na uwajibikaji katika kutekeleza wajibu wao na kuanzisha shughuli mpya. Kwa hiyo wakubwa wawasikilize kwa moyo wanashirika na wahimize umoja wa nguvu zao kwa manufaa ya shirika na ya Kanisa, licha ya kwamba inadumu mamlaka yao ya kukata shauri na ya kutoa amri ya utekelezaji.

Mikutano mikuu na halmashauri zitekeleze kwa uaminifu wajibu wao ziliokabidhiwa wa kuongoza; na taasisi hizi, kila moja kwa namna yake, iwe chombo cha ushirikiano na jitihada ya watawa wote kwa ajili ya manufaa ya shirika zima.

   

Maisha ya pamoja

15. Kulingana na mfano wa Kanisa la kwanza ambapo jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja (taz. Mdo 4:32), maisha ya pamoja yatakiwa kujilisha kwa mafundisho ya Injili, Liturujia takatifu, hasa Ekaristi, na kudumu katika kusali na katika ushirika wa roho ileile (taz. Mdo 2:42). Watawa, kama viungo vya Kristo, katika kuishi pamoja kama ndugu, wawatangulize wenzao kwa heshima (taz. Rum 12:10) wakichukuliana mizigo yao wao kwa wao (taz. Gal 6:2). Kwa maana, kwa vile upendo wa Mungu umemiminwa katika mioyo na Roho Mtakatifu (taz. Rum 5:5), basi jumuiya mithili ya familia halisi iliyokusanyika katika jina la Bwana inafurahia kuwepo kwake (taz. Mt 18:20). Mapendo ni utimilifu wa sheria (taz. Rum 13:10) na kifungo cha ukamilifu (taz. Kol 3:14), na kwa njia yake sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani (taz. 1Yoh 3:14). Tena umoja wa ndugu ni dhihirisho la ujio wa Kristo (taz. Yn 13:35; 17:21), na chemchemi ya nguvu nyingi kwa utume.

Kwa lengo la kufanya kifungo cha udugu kati ya watawa kiwe cha ndani zaidi, wale wenye kuitwa mabradha walei (conversi), au wasaidizi, au kwa jina jingine, waunganishwe sana na maisha na kazi za jumuiya. Isipokuwa mazingira yanadai kufanya vinginevyo, inabidi katika mashirika ya kitawa ya kike ipatikane daraja moja tu ya masista. Na hivyo utofauti kati ya watu uwepo tu kulingana na kazi mbalimbali walizokabidhiwa masista ama kwa wito wa pekee wa Mungu, ama kwa mwelekeo wao wa pekee.  

Monasteri na mashirika ya kitawa ya kiume yasiyo ya kilei tu, yaweza kupokea, kadiri ya tabia yake, kwa mujibu wa katiba, wakleri na walei, kwa nafasi zilizo sawa na kwa haki na wajibu zilizo sawa, ila zile zitokanazo na Daraja takatifu.

   

Klausura ya wamonaki wa kike

16. Klausura ya kipapa ya wamonaki wa kike wa maisha ya taamuli tu iendelee kuwepo, lakini irekebishwe kadiri ya hali ya nyakati na mahali. Baada ya kusikiliza maoni ya monasteri zenyewe desturi zilizopitwa na wakati zitenguliwe.

Wamonaki (moniales) wengine, ambao kwa mujibu wa kanuni wanafanya kazi za kitume za nje waruhusiwe kuhusu klausura ya kipapa (= wapewe ruhusa ya kwenda nje ya ugo), ili waweze kutekeleza vema wajibu wao wa utume. Bali klausura [ya kawaida] ifuatwe kulingana na katiba yao.

   

Mavazi ya kitawa

17. Mavazi ya kitawa, kwa vile ni ishara ya kuwekwa wakfu, yasiwe ya umalidadi, bali ya unyenyekevu; ya umaskini lakini ya kufaa. Tena yalingane na mahitaji ya afya na kuyafaa mazingira ya wakati na mahali na mahitaji ya huduma. Mavazi ya watawa wa kiume na wa kike yasiyolingana na kanuni hizo, yabadilishwe.

  

Malezi ya wanashirika

18. Marekebisho ya mashirika yategemea kwa sehemu kubwa malezi ya wanashirika. Kwa sababu hiyo, watawa wenyewe wasio wakleri na masista wasitumwe kwenye kazi ya kitume mara tu baada ya kumaliza unovisi, bali inafaa kwamba malezi yao ya kiroho na ya kitume, ya mafundisho na ya ufundi, hadi kujipatia pia shahada maalum, yaendelezwe kwa namna ya kufaa katika nyumba zilizoandaliwa kwa kusudi hilo.

Ili marekebisho ya kulinganisha maisha ya kitawa na mahitaji ya siku hizi yasiwe ya nje tu, wala wenye kujishughulisha kwa mujibu wa kanuni katika utume wa nje wasishindwe katika wajibu wao, watawa wafundishwe inavyotakiwa, kadiri ya akili na tabia za kila mmoja, kuhusu fikra na desturi za maisha ya kijamii ya siku hizi. Malezi, kwa njia ya kuunganisha kwa mpangilio mzuri masomo yote, yafanyike kwa namna ambayo itasaidia watawa wenyewe kujipatia umoja wa maisha.

Kwa maisha yao yote watawa wafanye bidii kukamilisha kwa makini elimu hii ya kiroho, ya kimafundisho na ya kiufundi, na wakubwa [wao] wawapatie, kulingana na uwezo wao, fursa, misaada na nafasi ya muda kwa lengo hilo.

Pia ni wajibu wa wakubwa kuwa waangalifu sana katika kuchagua na kuwaandaa wakurugenzi, viongozi wa roho na walimu.

  

Uanzishaji wa mashirika mapya

19. Kuhusu suala la kuanzisha mashirika mapya, itafakariwe kwa makini kama kweli ni lazima au ina walau manufaa makubwa, na tena kama kuna uwezekano kwa usitawishaji wake, kusudi yasianzishwe pasipo busara mashirika yasiyofaa au yenye kukosa nguvu za kutosha. Kwa namna ya pekee bidii zifanyike ili kuanzisha na kusitawisha aina za maisha ya kitawa katika maeneo ambayo Kanisa linatia misingi siku hizi, na hayo yafanyike kwa kuzingatia tabia na desturi za wenyeji, vilevile pia mazingira na kawaida za mahali.

 

Kudumisha au kuacha kazi za mashirika

20. Mashirika yatunze kazi zilizo zao na kuzitimiza kwa uaminifu. Kwa kuzingatia ufanisi wa Kanisa zima na wa jimbo, kila shirika lizilinganishe kazi zenyewe na mahitaji ya wakati na mahali kwa kutumia nyenzo zifaazo hata kama ni mpya, na likiziacha zile kazi ambazo siku hizi hazilingani tena na roho na tabia halisi ya shirika.

Roho ya kimisionari idumishwe kikamilifu katika mashirika ya kitawa na, kadiri ya tabia ya pekee ya kila shirika, ilinganishwe na mazingira ya siku hizi, ili kwamba mahubiri ya Injili kwa mataifa yote yapate kuwa na nguvu zaidi.

  

Mashirika na monasteri zilizodhoofika

21. Kwa uamuzi wa Kiti Kitakatifu, baada ya kusikia maoni ya Wakuu wa mahali (Maaskofu) wahusika, mashirika na monasteri ambazo hazina tumaini la kusitawi tena, zizuiliwe kupokea tena manovisi kwa mbeleni. Ikiwezekana ziunganishwe na shirika au monasteri nyingine inayositawi yenye kutofautiana kidogo sana kwa habari ya lengo na roho yake.

  

Maunganisho ya mashirika ya kitawa

22. Mashirika na monasteri zinazojitawala (“sui iuris”), ikiwa inafaa na kwa idhini ya Kiti Kitakatifu, ziunde ‘mashirikisho’ (foederationes) kati yao, kama zinahusiana kwa namna fulani na familia ileile ya kitawa; au ziunde miungano, ikiwa katiba na kawaida zao zikifanana na kusukumwa na roho ileile, hasa kama zina watawa wachache tu; ziwe vyama (associationes), kama zinashughulikia kazi za kitume zilezile au zinazofanana.

   

Mabaraza ya viongozi wakuu

23. Mabaraza au halmashauri ya viongozi wakuu yaliyoidhinishwa na Kiti Kitakatifu yawepo. Mabaraza hayo yanaweza kuchangia kwa vikubwa ili kuleta fanaka ya malengo ya kila shirika binafsi, kuhimiza ushirikiano wenye nguvu kwa manufaa ya Kanisa, kuhakikisha ugawaji wa watenda kazi wa Injili katika eneo fulani, tena kujadili masuala yanayowahusu watawa wote. Pia yanaweza kusitawisha mitindo ifaayo ya uratibu na ushirikiano na Mabaraza ya Maaskofu kwa habari ya utekelezaji wa utume.

Mabaraza ya aina hiyo yaweza kuundwa pia kwa ajili ya mashirika ya kilimwengu.

  

Miito ya kitawa

24. Mapadre na walezi wa kikristo wafanye juhudi ili, kwa njia ya miito ya kitawa iliyochambuliwa kwa namna ya kufaa na kwa uangalifu, Kanisa lipate usitawi mpya unaolingana na mahitaji ya wakati huu. Pia katika mahubiri ya kawaida zigusiwe mara nyingi zaidi habari za mashauri ya kiinjili na za kuambatana na maisha ya kitawa. Wazazi, wakishughulikia elimu ya kikristo ya watoto wao, wakuze na kulinda mioyoni mwao wito wa kitawa.

 

Ni halali kwa mashirika, kwa lengo la kuchochea miito, kujijulisha hadharani na kutafuta makandidati, ilimradi hayo yafanyike kwa busara na kwa kuzingatia sheria zilizowekwa na Kiti Kitakatifu na Mkuu wa mahali.

Lakini watawa wakumbuke kwamba mifano ya maisha yao ni njia bora kuliko zote ya kuleta sifa kwa shirika lao na ya kualika [watu] kuambatana na maisha ya kitawa.

    

Hitimisho

25. Mashirika ambayo kwa ajili yake zimetolewa kanuni hizi za kujirekebisha yaitikie kwa utayari wito waliopokea kutoka kwa Mungu na wajibu ambao siku hizi yanatakiwa kuutekeleza katika Kanisa. Mtaguso Mkuu huheshimu sana mtindo wa maisha yao ya ubikira, ya umaskini na ya utii, ambayo Kristo Bwana mwenyewe ni mfano, na unaweka tumaini imara katika tendo lake hili lenye matunda, liwe kwa faragha na kwa wazi. Kwa sababu hiyo watawa wote, wawe wanasukumwa na imani thabiti, na mapendo kwa Mungu na kwa jirani, na upendo kwa msalaba, na matumaini katika utukufu ujao, waeneze popote duniani habari njema ya Kristo, kusudi ushuhuda wao uonekane mbele ya watu wote na Baba yetu aliye mbinguni apate kutukuzwa (taz. Mt 5:16). Kwa namna hiyo, kwa maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mungu (Deipara) mpole sana “ambaye maisha yake ni mafundisho na kielelezo kwa wote”[1], [watawa] wapate ongezeko siku kwa siku na kuleta utele wa matunda ya wokovu.

 

Mambo yote yaliyoamuliwa katika dikrii hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuriwa kwa pamoja katika Sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 28 Oktoba 1965

 

Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki

(zinafuata sahihi za Mababa) 


   


[1] Mt. Ambrosio, De Virginitate, l. II, c. II n. 15.