Index   Back Top Print

[ FR  - IT  - PT  - SW ]

HOTUBA YA BABA MTAKATIFU YOHANE PAULO II
KUHUSU UFASIRI WA BIBLIA KATIKA KANISA

Ijumaa, 23 Aprili 1993

 

Hotuba hii imetolewa siku ya Ijumaa, 23 Aprili 1993 katika mkutano wa kuadhimisha miaka mia moja ya Ensiklika Providentissimus Deus wa Leo XIII, na miaka hamsini ya Ensiklika Divino afflante Spiritu wa Pius XII, ambazo zote mbili zahusu masuala ya Biblia.
Mkutano ulifanyika katika Ukumbi wa Klementina wa Jumba la Kitume, huko Vatikano, mbele ya wajumbe wa Jopo la Makardinali, Bodi ya Mabalozi walioidhinishwa kwa Kiti Kitakatifu, Tume ya Kipapa ya Biblia na Bodi ya Wahadhiri wa Chuo cha Kipapa cha Biblia.
Wakati wa mkutano, Kardinali J. Ratzinger alionyesha kwa Baba Mtakatifu hati ya Tume ya Biblia kuhusu ufasiri wa Biblia katika Kanisa.

 

Wahashamu Makardinali,
Waheshimiwa Mabalozi,
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Biblia,
Waheshimiwa Wahadhiri wa Chuo cha Kipapa cha Biblia,

1. Namshukuru kwa moyo wote Kardinali Ratzinger kwa hisia alizoonyesha sasa hivi akinitambulisha hati iliyoandaliwa na Tume ya Kipapa ya Biblia kuhusu ufasiri wa Biblia katika Kanisa. Kwa furaha ninapokea hati hiyo, tunda la kazi ya pamoja iliyoanzishwa kutokana na nia yenu, Bwana Kardinali, na kuendelezwa kwa miaka kadhaa. Inaitikia suala ninalojali sana, kwa sababu ufasiri wa Maandiko Matakatifu ni wa umuhimu wa pekee kwa imani ya kikristo na kwa maisha ya Kanisa. “Maana katika Vitabu Vitakatifu – ulivyotukumbusha vizuri Mtaguso – Baba aliye mbinguni anawajia watoto wake kwa upendo mkubwa na anaongea nao. Katika Neno la Mungu umo uweza na nguvu nyingi, kiasi kwamba Neno hilo huwa ni egemeo na nguvu kwa Kanisa na pia uthabiti wa imani, chakula cha roho na chemchemi safi na ya daima ya maisha ya kiroho kwa watoto wa Kanisa.” (Dei Verbum, 21). Namna ya kufasiri matini za Biblia kwa ajili ya wanaume na wanawake wa leo ina matokeo moja kwa moja kuhusu uhusiano wao binafsi, na kwa pamoja, na Mungu, na pia imefungamana kikamilifu na utume wa Kanisa. Inahusu suala lenye uhai, linalostahili uangalifu wenu wote.

2. Kazi yenu imetimilika wakati wa kufaa sana, kwa sababu inanipa fursa ya kuadhimisha pamoja nanyi kumbukumbu mbili zilizojaa maana: miaka mia ya Ensiklika Provvidentissimus Deus, na miaka hamsini ya Ensiklika Divino afflante Spiritu, zote mbili zenye kukusudia masuala ya Biblia. Tarehe 18 Novemba 1893 Baba Mtakatifu Leo XIII, akiangalia sana masuala ya kiakili, alitangaza Ensiklika yake kuhusu mitaala ya Maandiko Matakatifu, “kwa kusudi – alikuwa akiandika – ya kuihimiza na kuihamasisha” na pia ya “kuielekeza kwa jinsi ya kufaa zaidi mahitaji ya nyakati” (Enchiridion Biblicum, 82). Miaka hamsini baadaye, Baba Mtakatifu Pius XII aliwatia upya moyo wafafanuzi wakatoliki, katika Ensiklika yake, pamoja na kuwapa pia miongozo mipya. Wakati huohuo, Majisterio ya kipapa ilidhihirisha uangalifu wake wa daima mintarafu masuala yahusuyo Maandiko, kwa njia ya kujihusisha mara nyingi. Mwaka 1902 Leo XIII alianzisha Tume ya Biblia; mwaka 1909 Pius X alianzisha Chuo cha Biblia. Mwaka 1920 Benedikto XV aliadhimisha ukumbusho wa miaka 1500 wa kifo cha Mt. Yeronimo kwa njia ya Ensiklika kuhusu ufasiri wa Biblia. Msukumo wenye nguvu uliotolewa hivyo kwa mitaala ya kibiblia, umethibitishwa kikamilifu katika Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, hata Kanisa nzima limenufaika. Hati ya kidogma Dei Verbum huangaza kazi ya wafafanuzi wakatoliki, na kualika wachungaji na waamini kujilisha kwa dhati zaidi na neno la Mungu lililomo katika Maandiko.

Nataka leo kuweka wazi vipengere kadhaa vya mafundisho ya Ensiklika hizo mbili, na manufaa ya kudumu ya maelekeo yao katika mazingira mbalimbali geugeu, ili kuweza vizuri zaidi kunufaika na mchango wao.

 

I.
Kutokana na “Providentissimus Deus”
hadi “Divino afflante Spiritu”

3. Awali ya yote, inaonekana tofauti muhimu kati ya hati hizo mbili. Inahusu sehemu ya mbishano – au vizuri zaidi sehemu ya utetezi – ya Ensiklika hizo mbili. Naam, zote mbili zinaonyesha jukumu la kujibu mapigo dhidi ya ufasiri wa kikatoliki wa Biblia, lakini mapigo hayo hayakuenda yote kwa mwelekeo mmoja. Waraka Providentissimus Deus, kwa upande mmoja, ulitaka hasa kulinda ufasiri wa kikatoliki wa Biblia toka kwa mapigo ya ufasiri wa kisayansi wa kiurazini; kwa upande mwingine, waraka Divino afflante Spiritu, ulijali hasa kutetea ufasiri wa kikatoliki dhidi ya mapigo yanayopinga matumizi ya sayansi kwa upande wa wafafanuzi waliotaka kulazimisha ufasiri usio wa kisayansi, ulioitwa kwa haraka “wa kiroho”, wa Maandiko Matakatifu.

Mabadiliko hayo katakata ya matazamio yalitokana, bila shaka, na hali ya mazingira ya nyakati zile. Waraka Providentissimus Deus ulitangazwa katika wakati ulioathiriwa na mabishano makali dhidi ya imani ya Kanisa. Ufafanuzi huria (liberal exegesis) uliwapa mabishano hayo tegemeo muhimu, kwani ulitumia vifaa vyote vya kisayansi, toka uhakiki wa matini hadi jiolojia, na kupita kwenye filolojia ya kiuhakiki ya fasihi, historia ya dini, akiolojia na fani nyingine pia. Kinyume chake, waraka Divino afflante Spiritu ulitangazwa muda mfupi baada ya mabishano tofauti kabisa, yalioongozwa hasa katika nchi ya Italia, dhidi ya mitaala ya kisayansi ya Biblia. Kijitabu, kinachohifadhi jina la mwandishi, kilichoenezwa kwa upana ili kuangalisha dhidi ya yale kinayochora kama “hatari kubwa sana kwa Kanisa na roho za watu: yaani mbinu ya kihistoria-kiuhakiki katika kuchunguza na kufasiri Maandiko Matakatifu, maelekeo yake mabaya yenye hatari, na makengeuko yake.”

4. Kwa suala la kwanza na la pili, msimamo wa Majisterio ulikuwa wa maana, kwa sababu, mbali na kutoa jibu la kujilinda tu, ulichimba kiini cha suala, na hivyo kuonyesha (tuseme wazi mara moja) imani ya Kanisa kuhusu fumbo la Umwilisho.

Dhidi ya mapigo ya ufafanuzi huria, uliotangaza maelezo yake kana kwamba ni uamuzi uliotegemea matokeo hakika ya sayansi, ingaliwezekana mara kujibu kwa kutupa laana juu ya matumizi ya sayansi katika kufasiri Biblia, na kuwapa amri wafafanuzi wakatoliki ya kushika maelezo “ya kiroho” ya matini.

Waraka Providentissimus Deus hauchukui njia hii. Kinyume chake, Ensiklika hiyo hualika kwa msisitizo wafafanuzi wakatoliki kujipatia ujuzi halisi wa kisayansi, ili kuweza kushinda maadui katika uwanja wao wenyewe. “Njia ya kwanza” ya kujikinga, husema, “hupatikana katika kujifunza lugha za kale za Mashariki, na vilevile katika mazoezi ya uhakiki wa kisayansi” (EB, 118). Kanisa haliogopi uhakiki wa kisayansi. Linaogopa tu kauli za upendeleo, ambazo zinadai kuwa na msingi katika sayansi, kumbe, kwa kweli, zinaipotosha kwa ujanja sayansi, hata itoke nje ya uwanja wake.

Miaka hamsini baadaye, Papa Pius XII aliweza kutambua mafanikio ya miongozo ya Providentissimus Deus: “Kwa sababu ya kujua vizuri zaidi lugha za Biblia na yote yahusuyo Mashariki... masuala kadhaa yaliyozuka wakati wa Papa Leo XIII dhidi ya uhalisi, ukale, ukamilifu, na thamani ya kihistoria ya Vitabu Vitakatifu [...] leo yamefunuliwa na kutatuliwa” (EB, 546). Kazi ya wafasiri wakatoliki, “waliotumia kwa usahihi vyombo vya kielimu vya wapinzani wao” (EB, 562), imeleta mazao yake. Na ni kwa sababu hiyo kuwa Divino afflante Spiritu unaonekana hauna mahangaiko, ambayo ulikuwa nayo Providentissimus Deus, dhidi ya mapigo ya msimamo wa ufafanuzi wa kiurazini.

5. Lakini ilipaswa kuyajibu mapigo yaliyotoka kwa waliotaka ufafanuzi ulioitwa wa “kifumbo” (mystical) (EB, 552), waliotaka Majisterio iilaani juhudi ya ufafanuzi wa kisayansi. Ensiklika ilijibuje? Ingaliweza kufika tu kukazia faida na hata “ulazima” wa juhudi hizo kwa kulinda imani, kitu ambacho kingalinufaisha aina ya mgawanyiko kati ya ufafanuzi wa kisayansi, uliokusudiwa kwa matumizi ya nje, na ufasiri wa kiroho, uliotumika ndani ya Kanisa. Katika Divino afflante Spiritu, Pius XII aliepa makusudi kutumia njia hii. Bali alitetea muungano thabiti kati ya njia hizo mbili; kwa upande mmoja alikaza uzito wa “kitheolojia” wa maana sisisi, ya kuchunguzwa kwa mbinu maalum (EB, 551); na, kwa upande mwingine, alikiri kuwa, ili ipate kukubaliwa kama maana ya matini ya Biblia, maana ya kiroho lazima itoe uthibiti wa uhakika. Hisia tu ya binafsi haitoshi. Lazima kuthibitisha kuwa ni maana “aliyoitaka Mungu mwenyewe”, maana ya kiroho “iliyotolewa na Mungu” kwa matini iliyovuviwa (EB, 552-553). Kuhakikisha maana ya kiroho, basi, kunapatikana nako katika uwanja wa sayansi ya ufafanuzi.

Tunatambua, hivyo, kuwa, ijapo tofauti kati ya mambo ya kujadili ni kubwa, nyaraka hizo mbili zinaunganika kikamilifu katika kina. Zinakataa, zote mbili, kuvunja uhusiano kati ya yaliyo ya kibinadamu na yaliyo ya kimungu, kati ya utafiti wa kisayansi na mtazamo wa imani, kati ya maana sisisi na maana ya kiroho. Na hivyo, zote mbili, zinaonyesha kuwa zinalingana kabisa na fumbo la Umwilisho.

 

II.
Ulinganifu kati ya ufafanuzi wa kikatoliki
na fumbo la Umwilisho

6. Uhusiano wa karibu unaounganisha matini za Biblia zilizovuviwa na fumbo la Umwilisho ulidhihirishwa katika Ensiklika Divino afflante Spiritu kwa maneno hayo: “Jinsi Neno aliye na tabia ya kimungu alivyojifanya mfano wa wanadamu katika yote, ila dhambi, vivyo hivyo maneno ya Mungu, yaliyotamkwa kwa lugha za kibinadamu, yanalingana na lugha ya binadamu katika yote, ila kosa” (EB, 559). Ushuhuda huo, uliochukuliwa karibu neno kwa neno katika hati ya Mtaguso Dei Verbum (n. 13), unaangaza usambamba uliojaa maana.

Kweli, kuweka maneno ya Mungu katika maandishi, kwa kuongozwa na karama ya uvuvio wa Maandiko, imekuwa hatua ya kwanza kuelekea Umwilisho wa Neno la Mungu. Naam, maneno hayo yaliyoandikwa, yamekuwa njia ya kudumu ya mawasiliano na ushirikiano kati ya taifa teule na Bwana wake pekee. Kwa upande mwingine, ni kwa sababu ya hali ya unabii ya maneno hayo, kwamba imewezekana kutambua kukamilika kwa mpango wa Mungu, pale ambapo “Neno la Mungu alifanyika mwili akakaa kwetu” (Yn 1:14). Baada ya kutukuzwa mbinguni kwa ubinadamu wa Neno aliyejifanya mtu, ni tena kwa maneno yaliyoandikwa kwamba kukaa kwake kati yetu kumebaki kukishuhudiwa kwa namna ya kudumu. Yakiunganishwa na Maandiko yaliyovuviwa ya Agano la Kwanza, Maandiko yaliyovuviwa ya Agano Jipya, yamekuwa njia bayana ya mawasiliano na ushirikiano kati ya taifa la waamini na Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Njia hiyo haiwezi kamwe kutengwa na mto wa uzima wa kiroho uliobubujika kutoka kwa moyo wa Yesu na unaoenea kwa njia ya sakramenti za Kanisa. Hata hivyo, ina msimamo wake wenyewe hapohapo, yaani katika matini zilizoandikwa, zenye kuihakikisha.

7. Kutokana na hayo, Ensiklika zote mbili zinadai wafasiri wakatoliki kukaa katika ulingano kamili na fumbo la Umwilisho, lililo fumbo la muungano wa umungu na ubinadamu katika maisha ya mmoja aliyeishi katika wakati unaojulikana kabisa. Maisha ya Yesu hapa duniani hayadhihirishwi tu na mahali na tarehe ya mwanzoni mwa karne ya kwanza katika Yudea na Galilaya, lakini pia kwa njia ya kusimika katika historia ndefu kwa taifa dogo la Mashariki ya Kati ya kale, pamoja na udhaifu wake, na makubwa yake, na watu wake walio wa Mungu na wakosefu wake, na kwa maendeleo yake ya polepole ya utamaduni, na mabadiliko ya kisiasa, kwa ushinde na ushindi wake, kwa hamu zake kwa amani na kwa ufalme wa Mungu. Kanisa la Kristo linajali sana ukweli wa kuguswa wa Umwilisho na, kwa sababu hiyo, linatilia mkazo sana umuhimu wa uchunguzi wa “kihistoria-kiuhakiki” wa Biblia. Kwa kuacha mbali kuukataa, kama wangalitaka wanaotia maanani ufafanuzi wa “kifumbo” (mystical), watangulizi wangu waliukubali kwa nguvu. “Artis criticae disciplinam – aliandika Leo XIII – quippe percipiendae penitus hagiographorum sententiae perutilem, Nobis vehementer probantibus, nostri (exegetae, scilicet, catholici) excalant” [“Mbinu ya uhakiki ni mbinu ya kufaa sana ili kufahamu matini za waandishi watakatifu, wataalamu wetu (yaani wafafanuzi wakatoliki) wachochewa kuitumia. Maana Sisi tunaikubali kwa harara”] (Waraka wa kitume Vigilantiae, kwa uzinduzi wa Tume ya Biblia, 30 Oktoba 1902: EB, 142). “Harara” hiyohiyo ya kuidhinisha, na kielezi chenyewe (“vehementer”) anachotumia, vinapatikana pia katika Divino afflante Spiritu kuhusu chunguzi za uhakiki wa matini (taz. EB, 548).

8. Ensiklika Divino afflante Spiritu, inavyojulikana, iliwashauri hasa wafafanuzi kujifunza tanzu za fasihi andishi zinaotumika katika Vitabu Vitakatifu, hata kufikia kukiri kuwa mfafanuzi mkatoliki sharti “apate uhakika kuwa sehemu hii ya kazi yake haiwezi kupuuzwa bila kuathiri vibaya sana ufafanuzi wa kikatoliki” (EB, 560). Onyo hilo hutegemea juhudi ya kufahamu maana za matini kwa usahihi na ukamilifu wote uwezekanavyo, na hivyo pia katika mazingira yake ya kiutamaduni na kihistoria. Dhana danganyifu juu ya Mungu na Umwilisho husukuma wakristo kadhaa kuchukua mwelekeo ulio kinyume. Wanaelekea kusadiki kuwa, kwa vile Mungu ni Yule Aliye Juu Pekee, kila neno toka kwake lina thamani pekee kabisa, hata mbali na kanuni za lugha ya kibinadamu. Hakuna haja, wanavyofikiri hao, ya kujifunza kanuni hizo ili kuainisha maneno, jambo ambalo lingalipunguza uzito wa maneno yenyewe. Lakini hii inamaanisha kujisingizia na kukataa, kwa kweli, mafumbo ya uvuvio wa Maandiko na Umwilisho, kwa kuutegemea ufahamu wa uongo kuhusu Aliye Mkuu. Mungu wa Biblia si Yule aliye Mkuu Pekee, ambaye kwa kukanyaga yote anayogusa, angefuta tofauti zote na hata zile ndogondogo. Kumbe, Yeye ni Mungu Muumba, aliyeumba viumbe katika tofauti zao za ajabu “kila kitu kwa jinsi yake” linavyosema na kuandika simulizi la Mwanzo (Mwa 1). Mbali na kufuta tofauti, Mungu anaziheshimu na kuzitumia vizuri (taz. 1Kor 12:18.24.28). Ingawa anatumia lugha ya kibinadamu, Mungu hataki kulipa kila tamko maana ya namna moja, bali anatumia kila tofauti ndogondogo kwa urahisi sana, na vilevile anaikubali mipaka ya lugha. Hili linasababisha jukumu la wafafanuzi kuwa la taabu sana, la lazima na la kuamsha hamu! Hakuna kati ya mandhari za kibinadamu za lugha hata moja inayoweza kuachwa. Mafanikio ya siku hizi kuhusu utafiti wa lugha, fasihi na hemenetiki, yamefanya ufafanuzi wa Biblia kufikia kwenye kuziongezea tanzu za fasihi mitazamo mingine mingi (wa kibalagha, wa kisimulizi, na wa kisemiotiki). Sayansi nyingine za kibinadamu, kama saikolojia, sosholojia, pia zimekubaliwa ili zitoe mchango wao. Kwa hayo yote linaweza kukabidhiwa onyo ambalo Leo XIII aliwapa wajumbe wa Tume ya Biblia: “Wasidhanie kisihusike na kazi yao chochote kile kipya ambacho wasomi wa leo walikipata kwa bidii ya utafiti wao; bali, wawahi kuyatumia, bila kuchelewa, yale manufaa ambayo ufafanuzi wa Biblia huletewa katika kila wakati” (Vigilantiae, EB, 140). Uchunguzi wa mazingira ya kibinadamu ya neno la Mungu, lazima uhimizwe kufanywa kwa hamu iliyo daima mpya.

9. Walakini, uchunguzi huo hautoshi. Ili kujali usahihi wa imani ya Kanisa na uvuvio wa Maandiko, ufafanuzi wa kikatoliki unapaswa kujitahadhari usitazame fani za kibinadamu tu za matini za Biblia. Hutakiwa kuwa, pia na hasa, usaidie taifa la Wakristo kutambua wazi zaidi neno la Mungu katika matini hizo, ili waweze kulipokea vizuri zaidi, ili kuishi kikamilifu katika ushirika na Mungu. Kwa kusudi hilo, ni wazi kuwa ni lazima mfafanuzi mwenyewe atambue katika matini neno la Mungu, na hii haiwezekani isipokuwa kazi yake ya kielimu itegemezwe na mwamko wa maisha ya kiroho.

Tegemeo hilo likikosekana, utafiti wa kiufafanuzi utakuwa umekatika; unapoteza lengo lake muhimu na kujiwekea kwenye kazi ya pembeni. Unaweza kugeuka kuwa aina ya utoro. Uchunguzi wa kisayansi kuhusu miundo ya kibinadamu tu ya matini unasaidia kufikia kusahau kuwa neno la Mungu linamwalika kila mtu kujiondokea toka ubinafsi ili kuishi katika imani na upendo.

Ensiklika Providentissimus Deus, hapo ilikumbuka tabia ya pekee ya Maandiko Matakatifu na sharti linalotokana nayo la ufasiri wake: “Vitabu Vitakatifu – ilisema – haviwezi kufananishwa na maandiko ya kawaida, bali, kwa sababu vimetolewa na Roho Mtakatifu mwenyewe, na kwa kuwa vinashika ndani mambo ya hali ya juu sana, ya kifumbo na magumu kwa namna mbalimbali, sisi tunahitaji daima – ili tupate kuyafahamu na kuyaeleza – ujio wa Roho Mtakatifu, yaani mwanga wake na neema yake, tunazopaswa kuziomba kwa sala nyenyekevu na kuzidumisha kwa njia ya maisha matakatifu” (EB, 89). Kwa maneno machache, yaliyochukuliwa kutoka kwa Mt. Augustino, Divino afflante Spiritu ilieleza sharti hilohilo: “Wasali, ili wapate kufahamu!” (EB, 569).

Ndiyo, ili kuufikia ufasiri ulio sahihi kabisa wa maneno yaliyovuviwa na Roho Mtakatifu, lazima mtu kwanza aongozwe na Roho Mtakatifu, kwa hiyo ni lazima kusali kwa hilo, kusali sana, kuomba katika sala mwanga wa Roho umwangaze kwa ndani, na kuupokea kwa moyo mtiifu mwanga huo; kuomba upendo, ambao peke yake unawezesha kufahamu lugha ya Mungu, ambaye “ni Upendo” (1Yoh 4:8.16). Wakati wa kazi ya ufasiri, lazima kudumu, zaidi inavyowezekana, mbele ya Mungu.

10. Utiifu kwa Roho Mtakatifu unazalisha na kuimarisha hali nyingine, iliyo ya lazima kwa maelekeo sahihi ya ufafanuzi: uaminifu kwa Kanisa. Mfafanuzi mkatoliki hashiki ndoto ya binafsi ya kutaka kusadiki kwamba, nje ya jumuiya ya waamini, inawezekana kuelewa vizuri zaidi matini za Biblia. Ukweli ni kinyume chake, kwa sababu matini hizo hazikutolewa kwa watafiti binafsi “ili washibishe utafiti wao, au ili kuwapa mada za taaluma na utafiti” (Divino afflante Spiritu, EB, 566), bali ziliaminishwa kwa jumuiya ya waamini, kwa Kanisa la Kristo, ili kulisha imani na kuongoza maisha ya mapendo. Kulinda upeo huu huhalalisha ukweli wa ufasiri. Waraka Providentissimus Deus umekumbusha ukweli huo wa kimsingi na kuangalisha kuwa, mbali na kuzuilia utafiti wa kibiblia, kujali jambo hilo hurahisisha maendeleo yake halisi (taz. EB, 108-109). Inafurahisha kutambua kuwa masomo ya falsafa ya kihemenetiki ya siku za karibuni yameleta hakika ya mtazamo huo wa mambo, na kwamba wafafanuzi wa madhehebu mbalimbali walifanya kazi katika mitazamo inayofanana, kwa kulikazia, kwa mfano, sharti la kufasiri kila matini ya Biblia kama sehemu ya Kanoni ya Maandiko iliyokubaliwa na Kanisa, au kwa kuangalia zaidi michango ya ufafanuzi wa Mababa wa Kanisa.

Naam, kuwa waaminifu kwa Kanisa, kunamaanisha kujiweka kwa nia thabiti katika mkondo wa Mapokeo makuu, ambayo chini ya mwongozo wa Majisterio, iliyohakikishwa na msaada wa pekee wa Roho Mtakatifu, yalitambua Maandiko yaliyo rasmi kikanoni kuwa neno la Mungu kwa taifa lake, na hayakuacha kamwe kuyatafakari na kugundua utajiri usiokwisha. Mtaguso Mkuu wa Vatikano II ulisisitiza: “Kwa kweli hayo yote yanayohusu jinsi ya kufasiri Maandiko Matakatifu yapo chini ya uamuzi wa Kanisa, ambaye hutimiza amri ya Mungu na huduma yake ya kuhifadhi na kulifasiri Neno la Mungu” (Dei Verbum, 12).

Na ni kweli pia, sio pungufu – unavyosisitiza tena Mtaguso, kwa kunukulu neno la Providentissimus Deus – kuwa “ni wajibu wa wafafanuzi kusaidia, kadiri ya mwongozo huu, kuelewa na kueleza kwa undani zaidi maana ya Maandiko Matakatifu ili, kwa chunguzi zilizo za namna ya matayarisho, uamuzi wa Kanisa uthibitike” (Dei Verbum, 12; taz. Providentissimus Deus, EB, 109: “ut, quasi praeparato studio, judicium Ecclesiae maturetur”, “ili, kwa njia ya mitaala iliyo kama mandalio, uamuzi wa Kanisa uivishwe”).

11. Ili kutekeleza vizuri zaidi wajibu huo wa kikanisa ulio muhimu sana, wafafanuzi watakujwa makini kubaki karibu na mahubiri ya neno la Mungu, kwa kutumia sehemu ya wakati wao kwa huduma hiyo, na tena kwa kuhusiana na wale walio wahudumu watendaji na kuwasaidia kwa njia ya kutunga maandishi ya ufafanuzi wa kiuchungaji (taz. Divino afflante Spiritu, EB, 551). Hivyo, wataepa kupotea katika kuzungukazunguka katika utafiti wa sayansi ya kinadharia, ambao utawapeleka mbali na maana ya kweli ya Maandiko. Kwani hiyo maana haitengani na lengo la Maandiko, yaani kufanya kila mwamini awe na uhusiano binafsi na Mungu.

 

III.
Hati mpya ya Tume ya Biblia

12. Kwa mitazamo hiyo – ilisema Providentissimus Deus – “uwanja mpana wa utafiti umefunuliwa kwa kazi binafsi ya kila mfafanuzi” (EB, 109). Miaka hamsini baadaye, Divino afflante Spiritu, ilirudia kusema, kwa maneno tofauti, jambo lilelile linalovutia sana: “Basi, yanabaki mambo mengi, na mengine ni muhimu sana, ambayo katika kuyajadili na kuyaeleza, kina cha akili na umahiri wa wafafanuzi wakatoliki vinaweza na vinapaswa kujitokeza kwa uhuru” (EB, 356).

Kilichokuwa kweli mwaka 1943 bado nisawa siku hizi zetu, kwa sababu maendeleo ya utafiti yameleta ufumbuzi wa masuala kadhaa, na pamoja, masuala mapya ya kuchunguzwa. Katika ufafanuzi, kama vile katika sayansi nyingine, kadiri tunavyoendelea kupita mipaka ya yasiyojulikana, vile yanavyopanuka maeneo yanayohitaji kuchunguzwa. Miaka mitano tangu kutangaza Divino afflante Spiritu ilikuwa haijatimia, ndipo yale yaliyopatikana katika maandiko ya Kumrani yalileta mwanga mpya juu ya masuala mengi sana ya kibiblia, na kufungulia nyanja nyingine za utafiti. Baadaye, vumbuzi nyingi zilifanyika, na mbinu mpya za utafiti na uchanganuzi zilikamilishwa.

13. Badiliko hilo la hali lilisababisha ulazima wa uchambuzi mpya wa masuala. Tume ya Kipapa ya Biblia ilijiunganisha na juhudi hiyo na kutolea zao la kazi yake, lenye kichwa hiki: Ufasiri wa Biblia katika Kanisa.

Kinachoshtusha mara moja katika hati hiyo, ni upana wa mtazamo kwa jinsi ilivyodhamiriwa. Mbinu, njia na namna za ufafanuzi zinazotumika leo katika ufasiri zilichambuliwa na, licha ya mashaka mengine – mara nyingine ya maana sana – ambayo ni lazima kutokeza, zinakubaliwa karibu kila mara, kuwemo ndani yake misingi ya kufaa kwa ufasiri kamilifu ya matini ya Biblia.

Kwa sababu ufafanuzi wa kikatoliki hauna mbinu ya ufasiri iliyo yake na ya pekee, lakini, kwa kuanzia na msingi wa mbinu ya kihistoria-kiuhakiki ikiisha funguliwa na madai ya kifalsafa au mengine yaliyo kinyume cha ukweli wa imani yetu, unafaidika na mbinu zote za leo, ukitafuta katika kila moja yao “mbegu za Neno”.

14. Jambo jingine la pekee la muhtasari huo ni uwiano wake na utaratibu wake. Katika ufasiri wake wa Biblia unafaulu kuoanisha diakronia na sinkronia, kwa kutambua kuwa zote mbili zinakamilishana, na pia ni za lazima sana kwa kutokeza ukweli wote wa matini na kushibisha madai yaliyo haki yake msomaji wa leo.

Tena, ni muhimu zaidi kuwa ufafanuzi wa kikatoliki usijali tu fani za kibinadamu za ufunuo wa kibiblia, jambo ambalo mara nyingi ni kosa la mbinu ya kihistoria-kiuhakiki; au tena, fani za kimungu tu, wanavyotaka wenye imani kali (ufundamentalisti); bali unataka kuangaza fani za kwanza na za pili, jinsi zilivyoungana pamoja katika “hisani” (condescension) ya Mungu (Dei Verbum, 13), iliyo msingi wa Maandiko yote.

15. Mwishowe tungeweza kutambua mkazo uliowekwa katika hati hii, juu ya kwamba Neno la Biblia linatenda kazi kwa kusema na kila mtu, kila wakati, kila mahali. Ikiwa “Maneno ya Mungu [...] yameingia katika lugha za kibinadamu” (Dei Verbum, 13), ni kusudi yaeleweke na wote. Yatakiwa yasibaki mbali, “mazito mno kwako, wala mbali. ... Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya” (Kum 30,11.14).

Hilo ni lengo la ufasiri wa Biblia. Ikiwa jukumu la kwanza la ufafanuzi ni kuifikia maana halisi ya matini takatifu, ama pia maana zake mbalimbali, lazima baadaye upate kushirikisha maana hizo kwa mlengwa wa Maandiko Matakatifu, ambaye ndiye, ikiwezekana, kila binadamu.

Biblia inatenda nguvu yake katika mfululizo wa karne. Mchakato wa kudumu wa kuihusisha (actualization) na nyakati za leo unatengeneza ufasiri kwa kulingana na fikra na lugha ya watu wa wakati wake. Tabia thabiti na ya karibu sana ya lugha ya Biblia inarahisisha sana ulinganisho huo, ingawa kuwa imezaliwa katika utamaduni wa kale kunaleta matatizo mengi. Lazima, basi, daima kutafsiri wazo la kibiblia katika lugha ya sasa, ili liweze kusema kwa namna ya kuwafaa wasikilizaji. Utafsiri huo, lakini, lazima uwe mwaminifu kwa matini za asili, wala haiwezekani kuzilazimisha matini ili zifae kuendana na mbinu au njia ya ufasiri iliyozoeleka kwa wakati fulani tu. Lazima kuonyesha mwangaza wote wa neno la Mungu, ijapo limetamkwa “kwa lugha za kibinadamu” (Dei Verbum, 13).

Biblia siku hizi imeenea katika mabara yote na mataifa yote. Lakini, ili utendaji wake uwe wa kina, lazima uwemo utamadunisho kadiri ya tabia halisi ya kila taifa. Huenda mataifa yasiyoguswa na maelekeo mabovu ya ustaarabu wa siku hizi wa Magharibi yataweza kufahamu ujumbe wa Biblia kwa urahisi zaidi, kuliko yale ambayo yamekwisha kugandamana mbele ya utendaji wa neno la Mungu kwa sababu ya kuelekea mambo ya dunia (secularisation) na kwa jinsi upuuzaji wa matakatifu (demythologisation) unavyozidi.

Siku hizi zetu ni lazima juhudi kubwa, sio tu kwa upande wa wasomi na wahubiri, bali hata kwa upande wa watangazaji wa mawazo ya kibiblia: hao wote wanapaswa kutumia vifaa vyote vilivyopo – na viko vingi sana leo hii – ili umuhimu wa Biblia ulio kwa watu wote, ukubaliwe kwa upana, na nguvu yake ya kuokoa idhihirike popote.

Kutokana na hati hiyo, ufasiri wa Biblia katika Kanisa utaweza kupata mwamko mpya, kwa manufaa ya ulimwengu mzima, ili kuangazia ukweli na kutukuza upendo mwanzoni mwa milenia ya tatu.

 

Hitimisho

16. Kwa kufunga, ninayo furaha ya kuweza kuwatolea, kama walivyofanya watangulizi wangu Leo XIII na Pius XII, kwa wafafanuzi wakatoliki, na hasa kwenu ninyi, wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Biblia, shukrani pamoja na kuwatia moyo.

Nawashukuruni kwa moyo wote kwa kazi bora mliyoifanya kwa huduma ya Mungu na ya taifa la Mungu: kazi ya utafiti, ya ufundishaji na ya uchapishaji; ni msaada mliotoa kwa theolojia, liturujia ya Neno na huduma ya kuhubiri; ni vifaa vinavyosaidia ekumeni na mahusiano mazuri kati ya Wakristo na Wayahudi; ni kushiriki juhudi ya Kanisa kwa matarajio na magumu ya ulimwengu wa leo.

Zaidi, ninaongezea kuwatia moyo, kwa hatua mpya inayotakiwa kuchukuliwa. Uchangamano unaoongezeka wa jukumu hili unadai juhudi ya wote, na ushirikiano mpana kati ya vitengo vinavyohusika. Katika ulimwengu ambamo utafiti wa kisayansi una umuhimu zaidi na zaidi katika nyanja mbalimbali, hakuna budi kuwa sayansi ya ufafanuzi ijiweke katika mstari unaofaa. Ni moja ya mbinu ya utamadunisho wa imani, ulio sehemu ya utume wa Kanisa, unaoendana na kupokea fumbo la Umwilisho.

Namwomba Yesu Kristo, aliye Neno wa Mungu aliyejifanya mtu, awaongoze katika tafiti zenu, yeye aliyewafunulia roho za wanafunzi wake kufahamu Maandiko (Lk 24:45)! Bikira Maria awe mfano wenu, sio tu kwa ukarimu wa utiifu wake kwa Neno la Mungu, lakini pia, awali ya yote, kwa namna alivyopokea yale ambayo Yeye alimwambia! Mt. Luka anatusimulia kuwa Maria aliyaweka moyoni mwake, akayafikiri, maneno ya Mungu na matukio yaliyotendeka “symballousa en tê kardia autes” (Lk 2:19). Kwa kupokea Neno, yeye ni mfano na mama wa wanafunzi (taz. Yn 19:27). Yeye awafundisheni kupokea kikamilifu neno la Mungu, sio tu kwa njia ya utafiti wa kiakili, bali pia kwa maisha yenu yote!

Ili kazi yenu na juhudi zenu zisaidie daima kuangaza zaidi nuru ya Maandiko, kwa moyo wangu wote nawapa Baraka yangu ya Kitume.

 

Yohane Paulo PP. II

 

© Copyright 1993 - Libreria Editrice Vaticana

 © Copyright - Libreria Editrice Vaticana