Index

Back Top Print

[BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

Dikrii juu ya
malezi ya Waseminari

Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso Mkuu
ataka haya yakumbukwe daima

 

UTANGULIZI

Mtaguso Mkuu unatambua sana kwamba upyaisho wa Kanisa lote unaotamaniwa (Optatam Totius), kwa sehemu kubwa hutegemea huduma ya kipadre chini ya uongozi wa Roho wa Kristo[1], na kwa dhati Mtaguso unathibitisha umuhimu mkubwa wa malezi ya kipadre. Mtaguso unaeleza kanuni za msingi ambamo maagizo ambayo yamekwisha jaribiwa kwa mang’amuzi ya karne na karne yanathibitishwa upya na yanaongezewa marekebisho mapya ambayo yanakwenda sambamba na dikrii na konstitusio za Mtaguso Mkuu pamoja na hali za mabadiliko za siku zetu hizi. Kwa sababu ya umoja wa tabia ya upadre katika Kanisa Katoliki, malezi haya ya kipadre yahitajika kwa mapadre wote, wawe wa kijimbo, wa kitawa au wa riti yoyote. Hivyo, ingawa miongozo hii inahusika moja kwa moja kwa malezi ya mapadre wa kijimbo, inatakiwa, kwa ulinganifu unaofaa, itumike kwa wote.

I - MWONGOZO WA MALEZI YA KIPADRE KATIKA NCHI MBALIMBALI

Malezi yalingane na mazingira

1. Kwa kuwa, kutokana na utofauti mkubwa wa mataifa na nchi inawezekana kutunga sheria zilizo za jumla tu, kila nchi au riti iwe na “utaratibu wa malezi ya kipadre” (Sacerdotalis Institutionis Ratio) wake pekee. Utaratibu huu unatakiwa kuandaliwa na Mabaraza ya Maaskofu[2] na kuchunguzwa kila baada ya muda fulani na kuthibitishwa na Kiti cha Kitume. Katika mwongozo huo, sheria za jumla zirekebishwe kulingana na mazingira maalum ya wakati na mahali ili kwamba malezi ya kipadre kila mara yawe yanafuata mahitaji ya kichungaji kwa mahali husika ambapo uchungaji huo utakuja kufanywa.

II - ULAZIMA WA KUKUZA MIITO YA KIPADRE

Wakristo wote wajiwajibishe

2. Wajibu wa kukuza miito mitakatifu[3] ni wa jumuiya nzima ya kikristo, na inatakiwa kuutekeleza hasa kwa kuishi maisha bora ya kikristo. Mchango mkubwa unatolewa na familia zikiongozwa na roho ya imani, upendo na uchaji wa Mungu, ambazo hufanywa kama ndiyo seminari ya kwanza; vilevile na parokia zenye uhai tele, ambamo vijana wenyewe wanashiriki. Walimu na wote ambao, kwa namna moja au nyingine, wanahusika katika kutoa malezi kwa watoto na vijana – hasa katika vyama vya kikatoliki – watakiwa kujitahidi katika kuwafundisha vijana waliokabidhiwa ili kutambua wito mtakatifu na kuufuata kwa hiari. Mapadre wote watakiwa kuonyesha juhudi zao za kitume katika kuiendeleza miito mitakatifu zaidi iwezekanavyo, na kuivutia mioyo ya vijana waume kupenda upadre kwa maisha yao ya upole, yenye bidii, wanayoishi kwa furaha, pamoja na mifano ya upendo kati yao mapadre na ushirikiano wa kidugu.

Ni wajibu wa Maaskofu kuwatia moyo watu wao kuiendeleza miito na kuona kwamba nguvu zao zote na shughuli zao zote zinafungamana. Ni wajibu wao pia kujitolea bila kikomo, mfano wa baba, ili kuwasaidia wale ambao wanawatambua kuwa wameitwa katika huduma ya Bwana.

Ushirikiano huu thabiti wa watu wote wa Mungu katika kuiendeleza miito mitakatifu, ni itikio kwa Maongozi ya Mungu, ambayo hugawa tunu bora zitakiwazo na kusaidia kwa neema yake wale ambao wamechaguliwa na Mungu kushiriki Upadre wa Kristo kidaraja. Maongozi hayo ya Mungu huwaaminisha wahudumu halali wa Kanisa wajibu wa kuwaita wateule watamanio utume huo mkubwa kwa moyo radhi na kwa uhuru wote, baada ya kuthibitishwa kufaa, na kuwawekwa wakfu kwa muhuri wa Roho Mtakatifu kwa ajili ya ibada ya Mungu na ya huduma ya Kanisa[4].

Awali ya yote, Mtaguso Mkuu unapendekeza misaada ya kimapokeo ya ushirikiano huo ambayo ni: sala ya daima, toba ya kikristo, na uchambuzi wa mafundisho kwa waamini, unaopatikana kwa mahubiri, katekesi, na vyombo mbalimbali vya upashanaji habari, na ambapo umuhimu, maumbile na ubora wa wito wa upadre unasisitizwa. Mtaguso Mkuu pia unatoa maelekezo ili kwamba Vyama vya kuendeleza miito (Opera vocationum) ambavyo vimekuwepo, au ambavyo vinatarajia kuwepo, katika majimbo mbalimbali, kanda au nchi mbalimbali kulingana na hati za kipapa viunganishe na kuratibu kazi zote za kichungaji kwa ajili ya miito mitakatifu pamoja na kuziendeleza kwa busara kubwa na jitihada, vikiitumia misaada yote ya kisaikolojia na ya kisosiolojia ya siku hizi[5].

Ni muhimu kwamba Chama hicho cha kuichochea miito [mitakatifu] kifanye kazi kwa moyo wa upendo. Kinatakiwa kuvuka mipaka ya Jimbo moja hadi jingine, nchi, mashirika ya kitawa na riti na, kwa kutazama mahitaji ya Kanisa zima, hukusudiwa kusaidia hasa katika maeneo yale ambayo watenda kazi wanahitajika kwa namna ya pekee katika shamba la Bwana.

Malezi ya kiroho na kielimu katika seminari ndogo

3. Katika seminari ndogo ambazo zimeundwa ili kuotesha mbegu za wito, wanafunzi wanatakiwa kutayarishwa kwa malezi pekee ya kidini na hasa kwa uongozi wa kiroho wa kufaa, kufuata Kristo Mkombozi kwa roho pendevu na mioyo mikunjufu. Chini ya uongozi wa kibaba wa wakubwa wao, wakisaidiwa na wazazi kwa namna ya kufaa, wanafunzi waelekezwe kuongoza maisha yao kulingana na umri, fikra na maendeleo ya vijana. Namna yao ya maisha inatakiwa kujaa maelekezo kwa kila kiwango cha saikolojia njema pamoja na kuwa na mang’amuzi bora kwa mambo ya kawaida kwa maisha ya kila siku na mahusiano na familia zao[6]. Zaidi ya hayo, yote ambayo yameandikwa katika sura zinazofuata kwa ajili ya seminari kubwa yanatakiwa kuingizwa, baada ya kuyalinganisha, katika seminari ndogo pia, pale itakapoonekana kuwa inafaa kufanya hivyo kadiri ya lengo na tabia zake. Utaratibu wa masomo unatakiwa kupangwa ili kwamba wanafunzi waweze kuyaendeleza bila madhara hata katika sehemu nyingine, pale ambapo watapendelea kuifuata njia nyingine ya maisha.

Bidii kama hiyo ifanyike pia ili kuchochea mbegu za miito ya vijana wadogo na ya vijana wasomao katika taasisi maalum ambazo kulingana na mazingira ya mahali zinasaidia pia kutimiza malengo yaleyale ya seminari ndogo. Vilevile ifanyike bidii pia kati ya wavulana waliosoma katika shule nyinginezo au katika mitindo mingine ya elimu. Vyuo vya miito katika umri mkubwa na shughuli nyinginezo kwa kusudi hilohilo vyatakiwa kuendelezwa kwa makini.

III - UTARATIBU WA SEMINARI KUU

Malezi ya kichungaji

4. Seminari kuu ni za lazima kwa malezi ya kipadre. Katika hizo, malezi yote kwa wanafunzi lazima yalenge katika kuwafanya wachungaji wa kweli wa roho [za watu] kwa mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliye Mwalimu, Kuhani, na Mchungaji[7]. Hivyo wanatakiwa kuandaliwa kwa huduma ya Neno ili kwamba wapate ufahamu siku hadi siku wa Neno la Mungu lililofunuliwa, kulifanya kuwa lao kwa tafakari, na kutoa ufafanuzi wake na kwa njia ya maneno na maisha yao. Wanatakiwa kulelewa kwa huduma ya ibada na ya kutakatifuza, ili kwamba kwa sala na maadhimisho ya liturujia takatifu waendeleze kazi ya wokovu kwa njia ya sadaka ya Ekaristi pamoja na Sakramenti. Wanatakiwa kufunzwa kufanya huduma ya kichungaji ili kufahamu namna ya kumwakilisha Kristo kwa watu, ambaye “hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi (Mk 10:45; taz. Yn 13:12-17), na kwamba, wakiisha kujifanya watumishi wa wote, wawapate wengi (taz. 1Kor 9:19).

Kwa hiyo, fani zote za malezi yao, kiroho, kiakili, kimaadili, zatakiwa kujumlishwa kwa lengo hili la kichungaji. Ili kulipata lengo hili, walezi wote na walimu wanatakiwa kwa juhudi na mshikamano kufanya kazi hii kwa utii chini ya mamlaka ya Askofu.

Uchaguzi wa wakuu wa seminari na maprofesa

5. Malezi ya waseminari hayategemei sheria zenye busara tu, bali hasa walezi wenye uwezo. Kwa hiyo, wakuu wa seminari na maprofesa wanatakiwa kuchaguliwa kati ya wale walio bora sana[8], na waandaliwe kwa uangalifu katika mafundisho sahihi, mang’amuzi ya kichungaji ya kufaa, na malezi ya pekee katika maisha ya kiroho na mbinu mbalimbali za ufundishaji. Katika kutoa mafunzo haya, vyuo maalum vinatakiwa kuanzishwa, au walau mafunzo ya kufaa yaandaliwe, na tena mikutano ya mara kwa mara ya wakuu wa seminari iitishwe.

Wakuu wa seminari na maprofesa, wanatakiwa kukumbuka kila mara jinsi maoni yao na matendo yao yanavyoweza kuathiri mafanikio ya malezi ya waseminari. Chini ya uongozi wa Gombera wanatakiwa kujenga mshikamano kiroho na kimatendo, na wao wenyewe pamoja na wanafunzi waunde familia inayolingana na sala ya Bwana: “ili wawe na umoja” (taz. Yn 17:11), pamoja na kuchochea katika mioyo ya waseminari hali ya furaha kwa wito wao. Askofu, kwa upendeleo mkubwa usiokoma awatie moyo wale wanaofanya kazi seminarini, na ajionyeshe mwenyewe kama baba wa kweli katika Kristo kwa wanafunzi. Hatimaye mapadre wote wanatakiwa kuiona seminari kama ndiyo moyo halisi wa jimbo na kuitegemeza kwa hiari[9].

Kutathmini nia njema

6. Kila mkandidati anatakiwa kuchunguzwa wazi, kwa kuzingatia umri na ukomavu wake, katika nia yake njema na uhuru wa kuchagua, maisha yake kiroho, ufahamu wake kiakili, afya yake njema kimwili na kisaikolojia, ubora katika maadili na akili tambuzi, pamoja na mambo ambayo yawezekana kuwa ameyarithi [kwa wazazi wake]. Upimwe uwezo wa mkandidati katika kuyakabili majukumu ya upadre na kutekeleza wajibu wa kazi za kichungaji[10].

Bila kujali tatizo la uhaba wa mapadre, inabidi kuwa na msimamo katika kuwachunguza waseminari na kuwatathmini[11]. Mungu hawezi kuliacha Kanisa lake likose wahudumu, kama wale wanaofaa watapandishwa cheo, na wale wasiofaa [katika huduma] wanaongozwa kwa upendo wa kibaba kuufuata wito mwingine bila kukawia. Hao waelekezwe kwa namna ambayo itawasaidia, hali wamegundua wito wao wa kikristo, waweze kujibidisha kwa ari katika utume wa walei.

Seminari za kimajimbo

7. Pale ambapo jimbo moja linashindwa kuendesha seminari yake pekee, seminari za kimajimbo au za nchi nzima ziundwe na kuimarishwa. Kwa njia ya hizo mchango mzuri utatolewa kwa malezi thabiti ya waseminari, ambayo ni ya muhimu sana katika suala hili. Seminari hizi ambazo ni za eneo fulani au nchi nzima, lazima ziendeshwe kufuatana na kanuni inayotolewa na Maaskofu husika[12] na kuthibitishwa na Kiti cha Kitume.

Katika seminari ambazo idadi ya wanafunzi ni kubwa, wanafunzi wanatakiwa kupangwa katika vikundi, ili kila mwanafunzi aweze kuangaliwa ipasavyo, na wakati huohuo umoja wa uongozi na wa malezi kwa wote uzingatiwe.

IV - MSISITIZO WA PEKEE KATIKA MALEZI YA KIROHO

Umuhimu wa maisha ya kiroho

8. Malezi ya kiroho (Institutio spiritualis) lazima yaende sambamba na mafundisho ya imani (doctrinali) na malezi ya kichungaji (pastorali). Kwa namna ya pekee kwa msaada wa baba wa roho[13], malezi haya yatakiwa kuendeshwa kwa namna ambayo wanafunzi watajifunza kuishi katika muungano thabiti na usiotetereka na Mungu Baba, kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo katika Roho Mtakatifu. Wale ambao watafanana na Kristo kuhani kwa upadirisho mtakatifu wanatakiwa kujenga mazoea ya kuwa wameunganika naye kama marafiki katika kila undani wa maisha yao[14]. Wanatakiwa kuliishi Fumbo la kipasaka la Kristo kwa namna ambayo watajua kuwaingiza ndani yake watu ambao watakabidhiwa kwao. Wanatakiwa kufundishwa kumtafuta Kristo katika tafakuri aminifu la Neno la Mungu na katika kushiriki kikamilifu katika Mafumbo matakatifu ya Kanisa, hasa Ekaristi Takatifu, na katika sala ya vipindi (officio divino)[15]; [na kumtafuta Kristo] katika Askofu ambaye kwa njia yake wanatumwa, na katika watu ambao wanatumwa kwao, hasa maskini, watoto wadogo, wadhaifu, wakosefu, na wasiomwamini Mungu. Kwa matumaini ya kimwana wanatakiwa kumpenda na kumheshimu Mama mbarikiwa sana Bikira Maria, ambaye alitolewa na Yesu Kristo alipokuwa kifoni msalabani kuwa mama kwa mwanafunzi.

Mazoezi ya uchaji ( pietatis exercitia) ambayo yamekubaliwa na mapokeo ya Kanisa yanatakiwa kuchochewa kwa bidii, lakini uangalifu uwepo ili kwamba malezi ya kiroho yasitegemee hayo tu, wala kuelekea katika kionjo cha kidini peke yake. Zaidi ya hayo waseminari wanatakiwa kujifunza kuishi kiinjili, kujengeka na kuimarika katika imani, matumaini na mapendo, ili kwamba kwa kuishi kadiri ya fadhila hizo wajipatie roho ya sala [16], wauimarishe na kuulinda wito wao na kuchochea fadhila nyinginezo, na kupanua juhudi yao katika kuwavuta watu wote kwa Kristo.

Malezi kwa hisia ya Kanisa na utii

9. Waseminari wanatakiwa kupenywa kiundani na Fumbo la Kanisa, ambalo Mtaguso huu Mtakatifu umejitahidi kulifafanua, ili kwa kuunganika na upendo wa kimwana na Wakili wa Kristo, na baada ya upadirisho kwa kuambatana na Askofu wao kama wajoli wake waaminifu, na katika mshikamano na mapadre wenzao, waweze kwa njia hiyo kutoa ushuhuda wa umoja ule unaowavuta watu kwa Kristo[17]. Wanatakiwa kujifunza kushiriki kwa hamu kubwa maisha ya Kanisa kwa ujumla, wakizingatia maneno ya Mtakatifu Augustino: “Mtu anampata Roho Mtakatifu kwa kipimo kile anacholipenda Kanisa”[18]. Wanafunzi lazima watambue vizuri kwamba lengo lao si ubwana wa maisha wala kusifiwa, bali kujitolea wenyewe kwa nafsi yao yote katika kumtumikia Mungu na huduma ya kichungaji. Kwa malezi ya pekee wanatakiwa kufundishwa katika utii wa kipadre, kiwango cha maisha cha ufukara na roho ya majikatalio[19], ili kwamba waweze kujizoesha kuishi kadiri ya Kristo Msulibiwa na kujinyima kwa hiari vile vitu ambavyo ni halali lakini si vya lazima.

Wanafunzi wanatakiwa kujulishwa wajibu wanaouendea, na pasiwepo neno gumu katika maisha ya upadre linalofichwa kwao. Hata hivyo, wasitishwe mno na hatari katika maisha ya utume wao wa baadaye, bali wafundishwe namna ya kuimarisha maisha yao ya kiroho yajuayo kujipatia nguvu kutokana na kazi yao yenyewe ya kitume.

Malezi kwa usafi wa moyo

10. Wanafunzi ambao wanafuata mapokeo ya useja wa kipadre kama ulivyowekwa na sheria takatifu na za kudumu za riti yao, wanatakiwa kulelewa kwa uangalifu sana juu ya hali hiyo. Kwa njia ya useja huo, wanajinyima ndoa kwa sababu ya Ufalme wa mbinguni (taz. Mt 19:12), na kuambatana kikamilifu na Bwana wao kwa pendo lisilogawanyika [20], ambalo hupatikana kwa mshikamano na Agano Jipya, wanatoa ushuhuda kwa ufufuko wa maisha yajayo (taz. Lk 20:36) [21] na kupata msaada wa kufaa katika mazoezi ya siku hadi siku kwa mapendo yale kamili ambayo kwayo wataweza kuwa yote kwa watu wote katika maisha ya huduma yao ya kipadre [22]. Wanatakiwa kugundua kwa makini ni kwa shukrani gani wanazotakiwa kuishi hali hiyo, si tu kama jambo linalotakiwa na sheria ya Kanisa, bali kama zawadi ya Mungu yenye thamani kubwa ambayo wanatakiwa kuiomba kwa unyenyekevu na kuitikia upesi, kwa hiari na upendo wakihimizwa na kusaidiwa na neema ya Roho Mtakatifu.

Wanafunzi wanatakiwa kuwa na ufahamu wa kufaa kuhusu wajibu na heshima ya ndoa ya kikristo, ambayo ni mfano wa upendo uliopo kati ya Kristo na Kanisa (taz. Efe 5:22-33). Lakini wanatakiwa kugundua ukuu wa ubikira uliowekwa wakfu kwa Kristo[23], ili wajitolee wenyewe kwa hiari na uchaguzi mkomavu, pamoja na kujikabidhi kabisa mwili na roho kwa Bwana.

Wanatakiwa kuonywa kuhusu hatari ambazo zinaweza kudhuru usafi wao wa moyo, hasa kutokana na hali ya jamii ya siku hizi[24]. Wanatakiwa kujifunza, wakisaidiwa na njia bora za kimungu na za kibinadamu, jinsi kujikatalia kwao kwa ndoa kunavyoweza kuunganishwa na tabia ya maisha yao, ili kwamba matendo yao yasipungukiwe kutokana na useja, bali wao wenyewe wajifunze kujitawala kikamilifu, kiroho na kimwili, wakue katika ukomavu na waweze kupata heri zilizoahidiwa katika Injili.

Kujitawala

11. Kanuni za elimu ya kikristo zinatakiwa kuzingatiwa kiaminifu na kuongezewa tafiti za kisaikolojia na kipedagojia zilizo njema za siku hizi. Kwa hiyo, utaratibu wa malezi wenye busara utalenga katika kuwaendeleza wanafunzi kufikia kiwango halisi cha ukomavu wa kiutu. Ukomavu huu utahakikishwa hasa na msimamo wa tabia, na uwezo wa kutengeneza maamuzi yaliyopimwa kiangalifu, pamoja na uwezo wa kupambanua watu na matukio. Wanafunzi wanatakiwa kujizoesha kukamilisha tabia yao, kukuza uimara wa moyo, na kwa ujumla wajifunze kuheshimu fadhila zile ambazo huthaminiwa sana na binadamu na kuwafanya wahudumu wa Kristo wakubalike[25]. Fadhila hizo ni ukweli, heshima ya kudumu ya haki, uaminifu wa ahadi, heshima katika matendo, kiasi na upendo katika mazungumzo.

Nidhamu katika maisha ya seminari yatakiwa izingatiwe si tu kama hifadhi ya maisha ya pamoja na ya upendo, lakini pia kama sehemu ya lazima ya mfumo mzima ya malezi. Lengo lake ni kuwafundisha vijana njia za kujilinda, kukuza ukomavu madhubuti wa kiutu pamoja na malezi ya tunu za tabia ambazo ni muhimu zaidi, ili kuratibisha matendo ya Kanisa yapate kutoa matunda. Lakini nidhamu hiyo inatakiwa kutumiwa kwa njia ambazo zitajenga katika moyo wa wanafunzi utayari wa kukubali madaraka ya wakubwa wao kwa moyo radhi, au kwa sababu ya dhamiri (taz. Rum 13:5) au kwa sababu zinazopita ufahamu wa kibinadamu. Viwango vya nidhamu vyatakiwa kutumika vikizingatia umri wa wanafunzi, ili kwamba siku hadi siku wakijifunza kujitawala, wakati huohuo watapata mazoea ya kutumia uhuru wao kwa busara, kukuza moyo wa utendaji[26], pamoja na kushirikiana na waseminari wenzao na walei.

Mpango mzima wa seminari unatakiwa uratibiwe vizuri, kusudi katika mazingira yake ya uchaji na utulivu na wajibu wake wa ushirikiano wa pamoja, uweze kuwa maandalizi mazuri kwa maisha ya baadaye kama mapadre.

Mazoezi ya kichungaji

12. Ili kuleta msingi imara katika malezi ya kiroho kwa waseminari, na kuwawezesha kufanya uchaguzi wa wito wao kwa hiari, ni juu ya Maaskofu kuweka muda kwa kuboresha maandalizi ya kiroho. Ni juu yao pia kupima kwa uangalifu faida ya kukatisha masomo, au kupanga uanagenzi (tirocinio) wa kufaa wa uchungaji, ili kutathmini vizuri mkandidati wa upadirisho. Vivyo hivyo ni jukumu la Maaskofu kuamua kuongeza, au la, umri utakiwao na sheria ya Kanisa wa kupokea Daraja takatifu na pia kujadili kama ni vema, au sivyo, kuweka utaratibu kuwa baada ya kumaliza masomo ya teolojia wanafunzi wabaki kwa kipindi fulani kama mashemasi kabla ya kupandishwa katika daraja ya upadre.

V - MAREKEBISHO YA MASOMO YA KIKANISA

Elimu sanaa

13. Kabla ya waseminari kuanza masomo maalum ya Kanisa, wanatakiwa kuwa wamepata ile elimu sanaa na elimu sayansi (humanistica et scientifica institutione) ambazo ni za lazima kwa vijana ili kuingia masomo ya juu katika nchi zao mbalimbali. Zaidi ya hayo wanatakiwa kujua lugha ya Kilatini ambayo itawasaidia kujua na kutumia machimbuko (fontes) ya taaluma mbalimbali na hati za Kanisa[27]. Somo la lugha maalum ya kiliturujia kadiri ya riti latakiwa kufikiriwa kama hitaji muhimu, pamoja na elimu ya kufaa katika kujua lugha za Maandiko Matakatifu na ya Mapokeo.

Kuelekeza kwenye teolojia

14. Katika marekebisho ya masomo ya kikanisa, lengo muhimu litakiwalo kuzingatiwa ni ule ulinganifu wa falsafa na teolojia, ili kwamba kila moja liwe ni kijalizo kwa lingine katika kuleta upanuzi wa akili wa waseminari kwa Fumbo la Kristo, ambalo huathiri mfumo mzima wa historia ya wanadamu, na kupenya daima utendaji wa Kanisa, na kutenda kazi hasa kwa njia ya huduma ya kipadre[28].

Mtazamo huo unatakiwa kutolewa kwa waseminari tangu mwanzo kabisa mwa malezi yao. Kwa hiyo, masomo yao ya kikanisa yatakiwa kuanza na kozi tangulizi ya muda wa kufaa. Katika kozi hiyo, Fumbo la wokovu latakiwa kuelezwa kwa njia ambayo waseminari wataelewa maana, mpango na lengo la kichungaji kwa masomo hayo ya kikanisa, na wakati huohuo wasaidiwe kuifanya imani kuwa ndio msingi na mwongozo wa ndani katika maisha yao yote na waimarishwe katika kukubali wito wao kwa moyo wa furaha pamoja na kujitoa kwa dhati.

Masomo ya falsafa

15. Masomo ya falsafa yatakiwa kufundishwa kwa namna ambayo itawafanya waseminari wapate elimu imara na halisi ya mwanadamu, ya ulimwengu na ya Mungu. Waseminari wanatakiwa kuutegemea urithi wa falsafa ambao ni bora sikuzote[29], lakini pia wajifunze falsafa za kisasa hasa zile zenye athari kubwa katika nchi zao, bila kusahau maendeleo ya sayansi za kisasa. Hivyo, kutokana na ufahamu sahihi wa mawazo ya kisasa, waseminari watakuwa wamejiandaa kuingia katika dialogia na watu wa nyakati hizi[30].

Historia ya falsafa yatakiwa kufundishwa katika mtindo ambao utawafanya waseminari watambue kanuni za msingi za mifumo mbalimbali ya falsafa wakiendelea kuzizingatia tunu zile ambazo zimehakikishwa kuwa ni za kweli; na wakati huohuo wakitambua na kupinga mawazo yale ambayo yana makosa.

Namna ya kufundisha itoe hamasa kwa waseminari katika kupenda uchunguzi wa kina wa ukweli, kuutazama na kuuthibitisha, pamoja na ukubaliano mnyofu juu ya ufinyu wa ufahamu wa kibinadamu. Uangalifu mkubwa utumiwe kwa mahusiano kati ya falsafa na matatizo mbalimbali ya maisha, pamoja na maswali yanayosumbua akili za waseminari. Hao wenyewe wasaidiwe kung’amua muunganiko uliopo kati ya masuala ya kifalsafa na mafumbo ya wokovu ambayo yatatazamwa katika mwanga mkuu wa imani kwenye masomo ya teolojia.

Masomo ya teolojia

16. Masomo ya teolojia yafundishwe katika mwanga wa imani, chini ya uongozi wa Majisterio ya Kanisa[31], kwa namna ambayo wanafunzi wataweza kupata kwa makini mafundisho ya kikatoliki mintarafu Ufunuo wa kimungu. Waseminari wataweza kuingia ndani ya maana yake halisi wakiyafanya kuwa chakula cha maisha yao ya kiroho[32], na kujifunza kuyatangaza, kuyafafanua, na kuyalinda katika huduma yao ya kipadre.

Waseminari wanatakiwa kufundishwa kwa uangalifu na bidii katika Maandiko Matakatifu, ambayo yatakiwa kuwa ndio mtima (anima) wa teolojia yote[33]. Baada ya kupata kozi ya utangulizi wa kufaa, wanatakiwa kufundishwa mtindo wa ufafanuzi (exegeseos methodum), wajifunze kiundani mada za msingi za Ufunuo wa kimungu, na wapate himizo na lishe katika kusoma na kutafakari kila siku Vitabu Vitakatifu[34].

Utaratibu ufuatao watakiwa kuzingatiwa katika kushughulikia somo la Dogma (theologia dogmatica): mada zenyewe za kibiblia zipewe kipaumbele; halafu waseminari waonyeshwe jinsi Mababa wa Kanisa la Mashariki na la Magharibi walivyotoa mchango wao katika kurithisha kwa uaminifu na kuchambua kila ukweli wa Ufunuo wa kimungu; halafu historia ya Dogma, ikijumlishwa na uhusiano wake na historia ya Kanisa[35]; mwishowe, ili kutoa mwanga mtimilifu iwezekanavyo katika mafumbo ya wokovu, waseminari wajifunze kiundani kwa njia ya utafiti (ope speculationis) vipengele vyote vya mafumbo hayo, na kuona uhusiano kati yake, wakisaidiwa na ufafanuzi wa Mt. Tomaso [wa Akwino], aliye mwalimu[36]. Wafundishwe kuyatambua na kuyaona kuwa ndiyo yaliyomo na yanayotenda daima katika maadhimisho ya Liturujia[37], na katika maisha yote ya Kanisa. Wafundishwe kutafuta utatuzi wa matatizo ya binadamu katika mwanga wa Ufunuo, na kuzitumia kweli za milele katika hali ya kigeugeu ya ulimwengu huu, na kutoa ufafanuzi katika lugha ambayo watu wa nyakati hizi wataifahamu[38].

Katika namna kama hiyo masomo mengine ya Teolojia yanatakiwa yafanyiwe marekebisho kwa njia ya mshikamano hai na Fumbo la Kristo na historia ya wokovu. Uangalifu mkubwa ufanyike katika kulifanya somo la teolojia maadili (Theologiae morali) liwe kamilifu. Fafanuzi zake za kisayansi zilenge kwa uwazi zaidi katika mafundisho ya Biblia takatifu na zitoe mwanga juu ya ubora wa wito wa waamini katika Kristo, na juu ya wajibu wao wa kuzaa matunda katika mapendo kwa uzima wa ulimwengu. Vivyo hivyo, katika kufafanua sheria za Kanisa (iure canonico) na kufundisha historia ya Kanisa, lizingatiwe Fumbo la Kanisa kama ilivyoelezwa katika Konstitusio ya kidogma “De Ecclesia” [Mwanga wa Mataifa] ambayo ilitolewa rasmi na Mtaguso huu Mkuu. Liturujia Takatifu, ambayo yatakiwa kuzingatiwa kama ndiyo chemchemi ya kwanza na ya lazima ya roho halisi ya kikristo, na ifundishwe kama ilivyoelezwa katika vipengere 15 na 16 vya Konstitusio juu ya Liturujia[39].

Kulingana na hali za nchi mbalimbali, waseminari waelekezwe kwenye ufahamu halisi wa Makanisa na wa Jumuiya za kikanisa zilizojitenga na Kiti cha Kitume cha Roma, ili waweze kutoa mchango katika kukuza urudishaji wa umoja kati ya wakristo wote kadiri ya miongozo ya Mtaguso huu Mkuu[40].

Waingizwe pia katika ufahamu wa dini nyinginezo zilizopo katika eneo hili au lile, ili waweze kutambua vizuri zaidi zina mema na ukweli kiasi gani kadiri ya mpango wa Mungu; na wajifunze jinsi ya kukosoa makosa ziliyo nayo; na waweze kuleta mwanga wa ukweli kwa wale wasio nao.

Kurekebisha mitindo ya ufundishaji

17. Mafunzo hayo ya mafundisho [ya Kanisa] yasielekee kuwa uhawilishaji (communicationem) tupu wa dhana, bali yawe malezi halisi na ya ndani kwa waseminari. Mitindo ya ufundishaji yatakiwa kurekebishwa. Marekebisho hayo yahusu mihadhara, majadiliano na semina au mazoezi. Vilevile wanafunzi wasaidiwe na mitindo hiyo mipya katika kusoma kwao kibinafsi na katika vikundi. Uangalifu mkubwa uchukuliwe katika kupata umoja na uimara wa mafunzo yote kwa ujumla, kwa kuepuka mlundikano wa masomo na mihadhara na kwa kuacha masuala ambayo yana umuhimu mdogo siku hizi au ambayo yangetakiwa kupangwa kwa ajili ya masomo ya juu zaidi.

Masomo ya juu zaidi

18. Ni wajibu wa Maaskofu kuwapeleka vijana wenye tabia njema, fadhila na akili katika taasisi maalum, vitivo au vyuo vikuu ili mahitaji mbalimbali ya kichungaji yaweze kutoshelezwa na mapadre walioandaliwa katika viwango vya juu kisayansi, kuhusu taaluma takatifu na mengine ya kufaa. Lakini malezi ya kiroho na ya kichungaji ya vijana hawa, hasa kama bado hawajapata upadre, yasiachwe kwa sababu yoyote iwayo.

VI - MWONGOZO WA MALEZI MAHUSUSI YA KICHUNGAJI

Kufunza usikivu

19. Ari ya kichungaji ambayo yafaa kuwa kama tabia ya malezi ya waseminari[41] pia hutakiwa kufundishwa kwa uangalifu hasa katika vipengele vyake vyote ambavyo vinafaa katika huduma takatifu. Vipengele hivi ni kama katekesi, kuhubiri, ibada za kiliturujia na utoaji wa sakramenti, matendo ya huruma, wajibu wa kuwakaribia wale walio katika makosa na wasioamini bado, na shughuli nyinginezo nyingi za kichungaji. Wanatakiwa kufundishwa vizuri katika mbinu za kuziongoza roho za watu. Kwa hiyo basi, wataweza kuwa tayari kuwaongoza waana wote wa Kanisa katika maisha ya kikristo ambayo yamejaa utambuzi na roho ya kichungaji. Watakiwa pia kuwajaza waamini moyo wa uwajibikaji katika kutimiza wajibu wa hali zao. Kwa bidii sawia wanatakiwa kujifunza kuwasaidia watawa wa kiume na wa kike, kudumu katika neema ya wito wao na kukua kadiri ya roho ya kila Shirika[42].

Kwa ujumla, inatakiwa kusitawisha mielekeo ile ya tabia katika waseminari inayosaidia kukuza dialogia na watu, ambayo kati yake ni uwezo wa kuwasikiliza wengine, na uwezo wa kufungua mioyo katika roho ya mapendo kwa mahitaji mbalimbali ya jumuiya[43].

Kufunza roho ya kimisionari

20. Waseminari wafundishwe kutumia ipasavyo misaada itolewayo na sayansi za pedagojia, saikolojia na sosiolojia[44], kadiri ya mitindo iliyo sahihi na kanuni za Mamlaka ya Kanisa. Wanatakiwa pia kufundishwa kwa uangalifu namna ya kukuza na kuchochea kazi za kitume za walei[45] na kuinua aina mbalimbali zilizo bora za utume; pamoja na kujazwa ile roho ya kweli ya kikatoliki ambayo hutupa macho yake pia nje ya mipaka ya jimbo, taifa au riti, ili kufikia mahitaji ya Kanisa zima, wakitayarishwa katika roho yao kuhubiri Injili ya Kristo mahali popote[46].

Mazoezi ya kimatendo nje ya seminari

21. Waseminari wajifunze mbinu ya kuutekeleza utume siyo tu kinadharia, bali katika matendo na wawe tayari kufanya hivyo kwa moyo wa kujituma wenyewe, na katika ushirikiano na wengine. Kwa lengo hili waingizwe katika kazi za kichungaji kama sehemu ya kozi yao ya masomo, pia katika wakati wa likizo, kwa mazoezi mazuri yatakayopangwa. Mazoezi hayo yalingane na umri wa waseminari na mazingira ya mahali, kadiri ya uamuzi wenye busara wa Maaskofu, yatekelezwe kwa mitindo ya kufaa na chini ya uongozi wa mabingwa katika mambo ya kichungaji, ukizingatiwa daima kwamba uwezo mkubwa ni wa misaada ya Mungu[47].

VII - MAFUNZO BAADA YA UPADIRISHO

Kujiendeleza kinadharia na kimatendo

22. Mafunzo ya kipadre, hasa katika muono wa mazingira ya siku hizi, yanatakiwa kuendelezwa na kukamilishwa hata baada ya kumaliza kozi za masomo katika seminari[48]. Itakuwa ni wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu katika kila nchi kuandaa na kutoa njia za kufaa kwa mwendelezo huo wa masomo. Mifano ya njia hizo ni: Taasisi za kichungaji zikishirikiana na parokia fulani ambazo zimeteuliwa kwa lengo hilo; kuitisha mikutano kwa kipindi cha muda fulani uliokubaliwa; na mazoezi ya kufaa ambayo kwayo mapadre wapya wataingizwa polepole, kwa upande wa roho, wa akili, na wa uchungaji, katika maisha ya upadre na katika kazi ya kitume, pamoja na kuweza kuendelezwa na kukamilishwa katika hayo mawili.

HITIMISHO

Mababa wa Mtaguso Mkuu, wakiendeleza kazi iliyoanzishwa na Mtaguso wa Trento, kwa matumaini wanawaaminisha wakuu na maprofesa wa seminari wajibu wa kulea mapadre wa Kristo wa kesho katika roho ya marekebisho ambayo yamehimizwa na Mtaguso Mkuu wenyewe. Wakati huohuo wanawasihi sana wale wanaojiandaa kwa huduma ya kipadre kuendeleza ufahamu thabiti kwamba matumaini ya Kanisa na wokovu wa nafsi [za watu] vimekabidhiwa kwao, na wakipokea kwa hiari na ari miongozo iliyomo katika dikrii hii, wazae matunda mengi na ya kudumu.

 

Mambo yote yaliyoamuliwa katika dikrii hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

 

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 28 Oktoba 1965

 

Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki

(zinafuata sahihi za Mababa)

 
[1] Maendeleo ya Taifa zima la Mungu, kwa mapenzi ya Kristo mwenyewe, huitegemea hasa huduma ya mapadre. Jambo hilo ni dhahiri kwa maneno ambayo Bwana aliyasema alipowaweka Mitume na waandamizi wao pamoja na washiriki wao kuwa watangazaji wa Injili, viongozi wa Taifa teule jipya na watoaji wa mafumbo ya Mungu. Hilo lathibitishwa hata na maelezo ya Mababa wa Kanisa, na ya watakatifu na pia na hati kadha wa kadha za Mababa Watakatifu.

Taz. hasa: Mt. Pius X, Exhortatio ad Clerum Haerent animo, 4 agosti 1908: S. Pii X Acta, IV, uk. 237-264. – Pius XI, Litt. Encicl. Ad catholici Sacerdotii, 20 desemba 1935: AAS 28 (1936), hasa uk. 37-52. – Pius XII, Adhortatio Apost. Menti Nostrae, 23 septemba 1950: AAS 42 (1950), uk. 657-702. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Sacerdotii Nostri primordia, 1 agosti 1959: AAS 51 (1959), uk. 545-579. – Paulus VI, Epistula Apost. Summi Dei Verbum, 4 novemba 1963: AAS 55 (1963), uk. 979-995.

[2] Malezi yote ya mapadre, yaani utaratibu wa seminari, malezi ya kiroho, mpango wa masomo, maisha ya pamoja, nidhamu na mazoezi ya kichungaji, lazima yalinganishwe na hali ya mahali. Kanuni za msingi za malinganisho haya zitungwe, kwa kawaida, kwa ajili ya mapadre wasio watawa na Mabaraza ya Maaskofu, na kwa ajili ya mapadre watawa na Wakuu halali. (taz. S. Congr. De Religiosis, Const. Apost. Sedes Sapientiae, pamoja na Katiba za jumla zilizoambatanishwa nayo, art. 19, ed. 2 a,, Roma, 1957, uk. 38 s.)
[3] Kati ya shida kuu zilitaabishazo Kanisa siku hizi, hasa huonekana upungufu wa miito. Taz. Pius XII, Adhortatio Apost. Menti Nostrae: “...Idadi ya mapadre katika nchi za kikatoliki na katika nchi za kimisioni, haitoshi kwa mahitaji yaendeleayo kuongezeka”: AAS 42 (1950), uk. 682. – Ioannes XXIII: “Suala la miito ya mapadre na watawa ni hangaiko la kila siku la Baba Mtakatifu... Ni kite cha sala yake, shauku yenye bidii nyingi ya nafsi yake”: toka hotuba kwenye Kongamano la I la kimataifa la miito ya maisha ya kitawa, 16 desemba 1961: AAS 54 (1962), uk. 33.
[4] Taz. Pius XII, Const. Ap. Sedes Sapientiae, 31 maggio 1956: AAS 48 (1956),uk. 357. – Paulus VI, Epistula Apost. Summi Dei Verbum, 4 novemba 1963: AAS 55 (1963), uk. 984 ss.
[5] Taz. hasa: Pius XII, Motu proprio Cum nobis, kuhusu kusimikwa kwa Shirika la Kipapa kwa miito ya kipadre kwenye Idara Takatifu kwa Seminari na Vyuo Vikuu, 4 novemba 1941: AAS 33 (1941), uk. 479; pamoja na maambatano Katiba na Miongozo zilizoidhinishwa na Idara Takatifu hiyohiyo tarehe 8 septemba 1943. – Id., Motu proprio Cum supremae, kuhusu Shirika la Kipapa kwa miito ya kitawa, 11 februari 1955: AAS 47 (1955), uk. 266; pamoja na maambatano Katiba na Miongozo zilizoidhinishwa na Idara Takatifu kwa watawa ( ibid., uk. 298-301). – Conc. Vat. II, Decretum de accommodata renovatione vitae religiosae, Perfecta Caritatis, n. 24. – Id., Decretum de pastorali Episcoporum munere in Ecclesia, Christus Dominus, n. 15.
[6] Taz. Pius XII, Adhortatio Apost. Menti Nostrae, 23 septemba 1950: AAS 42 (1950), uk. 685.
[7] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. de Ecclesia, Lumen Gentium, n. 28: AAS 57 (1965), uk. 34.
[8] Taz. Pius XI, Litt. Encicl. Ad catholici Sacerdotii, 20 desemba 1935: AAS 28 (1936), uk. 37. “Kwanza kabisa wachaguliwe kwa uangalifu wakuu na walimu... Wawekeni katika seminari zenu mapadre wenye maadili bora, wala msisite kuwatoa katika kazi zionekanazo kuwa na umuhimu mkubwa zaidi, kwa sababu hakuna kazi iwezayo kulinganishwa na jambo hilo kuu lisilo na kifani, wala kujitia mahali pake”. Kanuni hii ya kuwachagua wale walio bora zaidi ilisisitizwa na Pius XII katika Waraka wa Kitume kwa Maaskofu wa Brazili ya tarehe 23 aprile 1947: Discorsi e radiomessaggi IX, uk. 579-580.
[9] Kuhusu wajibu wa mapadre wote wa kuzipa seminari msaada wao, taz. Paulus VI, Epistula Apost. Summi Dei Verbum, 4 novemba 1963: AAS 55 (1963), uk. 984.
[10] Taz. Pius XII, Adhortatio Apost. Menti Nostrae, 23 septemba 1950: AAS 42 (1950), uk. 684. – Taz. pia Idara Takatifu ya Masakramenti, Litt. circulares Magna equidem kwa Maaskofu wa mahali, 27 desemba 1935, n. 10. – Kwa upande wa watawa taz. Katiba za jumla zilizoambatishwa na Const. Ap. Sedes Sapientiae, 31 maggio 1956, art. 33. – Paulus VI, Epistula Apost. Summi Dei Verbum, 4 novemba 1963: AAS 55 (1963), uk. 987 s.
[11] Taz. Pius XI, Litt. Encicl. Ad catholici Sacerdotii, 20 desemba 1935: AAS 28 (1936), uk. 41.
[12] Imeamriwa ya kwamba Maaskofu wote wahusika washirikiane katika kutunga Sheria za seminari za kikanda au za kitaifa, kufuatana na can. 1357, § 4, CIC.
[13] Taz. Pius XII, Adhortatio Apost. Menti Nostrae, 23 septemba 1950: AAS 42 (1950), uk. 674. – Idara Takatifu kwa Seminari na Taaluma za Vyuo Vikuu, La formazione spirituale del candidato al sacerdozio, Città del Vaticano, 1965.
[14] Taz. Mt. Pius X, Exhortatio ad Clerum Haerent animo, 4 agosti 1908: S. Pii X Acta, IV, uk. 242-244. – Pius XII, Adhortatio Apost. Menti Nostrae, 23 septemba 1950: AAS 42 (1950), uk. 659-661. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Sacerdotii Nostri primordia, 1 agosti 1959: AAS 51 (1959), uk. 550 s.
[15] Taz. Pius XII, Litt. Encicl. Mediator Dei, 20 novemba 1947: AAS 39 (1947), uk. 547 ss. na 572 s. – Ioannes XXIII, Adhortatio Apost. Sacrae Laudis, 6 jenuari 1962: AAS 54 (1962), uk. 69. – Conc. Vat. II, Const. de Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, art. 16 na 17: AAS 56 (1964), uk. 104 s. – Idara Takatifu kwa Madhehebu ya Ibada, Mwongozo Inter oecumenici kwa utekelezaji kamili wa Const. de Sacra Liturgia, 26 septemba 1964, nn. 14-17: AAS 56 (1964), uk. 880 s.
[16] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Sacerdotii Nostri primordia, 1 agosti 1959: AAS 51 (1959), uk. 559 s.
[17] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. de Ecclesia, Lumen Gentium, n. 28: AAS 57 (1965), uk. 35 s.
[18] Mt. Augustinus, In Ioannem tract. 32, 8: PL 35, 1646.
[19] Taz. Pius XII, Adhort. Apost. Menti Nostrae, 23 septemba 1950: AAS 42 (1950), uk. 662 s., 685, 690. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Sacerdotii Nostri primordia, 1 agosti 1959: AAS 51 (1959), uk. 551-553, 556 s. – Paulus VI, Litt. Enycl. Ecclesiam suam, 6 agosti 1964: AAS 56 (1964), uk. 634 s. – Conc. Vat. II, Const. dogm. de Ecclesia, Lumen Gentium, hasa n. 8: AAS 57 (1965), uk. 12.
[20] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Sacra Virginitas, 25 machi 1954: AAS 46 (1954), uk. 165 ss.
[21] Taz. Mt. Cyprianus, De habitu virginum, 22: PL 4, 475. – Mt. Ambrosius, De virginibus, I, 8, 5: PL 16, 202 s.
[22] Taz. Pius XII, Adhort. Apost. Menti Nostrae: AAS 42 (1950), uk. 663.
[23] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Sacra Virginitas, l.c., uk. 170-174.
[24] Taz. Pius XII, Adhort. Apost. Menti Nostrae: l.c., uk. 664 na 690 s.
[25] Taz. Paulus VI, Epistula Apost. Summi Dei Verbum, 4 novemba 1963: AAS 55 (1963), uk. 991.
[26] Taz. Pius XII, Adhort. Apost. Menti Nostrae: l.c., uk. 686.
[27] Taz. Paulus VI, Epistula Apost. Summi Dei Verbum, l.c., uk. 993.
[28] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. de Ecclesia, Lumen Gentium, nn. 7 na 28: AAS 57 (1965), uk. 9-11 na 33.
[29] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Humani generis, 12 agosti 1950: AAS 42 (1950), uk. 571-575.
[30] Taz. Paulus VI, Litt. Enycl. Ecclesiam suam, 6 agosti 1964: AAS 56 (1964), uk. 637 ss.
[31] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Humani generis, 12 agosti 1950: AAS 42 (1950), uk. 567-569. – Id., Allocutio Si diligis, 31 mei 1954: AAS 46 (1954), uk. 314 s. – Paulus VI, Hotuba kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorianum, 12 machi 1964: AAS 56 (1964), uk. 364 s. – Conc. Vat. II, Const. dogm. de Ecclesia, Lumen Gentium, n. 25: AAS 57 (1965), uk. 29-31.
[32] Taz. Mt. Bonaventura, Itinerarium mentis in Deum, Prol., n. 4: “Mtu asidhani kwamba inatosha kusoma pasipo kutiwa mafuta, kuchunguza pasipo moyo wa ibada, kutafuta pasipo mshangao, kukagua pasipo shauku, kujitahidi pasipo uchaji wa Mungu, kuwa na elimu bila upendo, akili bila unyenyekevu, bidii ya kusoma bila neema, mwigo bila hekima itokayo kwa Mungu”: (Mt. Bonaventura, Opera Omnia, V, Quaracchi, 1891, uk. 296.
[33] Taz. Leo XIII, Litt. Encicl. Providentissimus Deus, 18 novemba 1893: ASS 26 (1893-94), uk. 283.
[34] Taz. Tume ya Kipapa ya taaluma ya Biblia, Instructio de Sacra Scriptura recte docenda, 13 mei 1950: AAS 42 (1950), uk. 502.
[35] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Humani generis, 12 agosti 1950: AAS 42 (1950), uk. 568 s.: “....Taaluma takatifu zapata upya ujana kwa mtaala wa machimbuko matakatifu; kinyume chake utafiti usiojali uchunguzi wa ndani wa amana takatifu, hakiwezi kuzaa, kama tujuavyo kutoka mang’amuzi”.
[36] Taz. Pius XII, Hotuba kwa wanafunzi wa Maseminari, 24 juni 1939: AAS 31 (1939), uk. 247: “Bidii ya mwigo, … katika kutafuta na kueneza ukweli haikomeshwi bali yachochewa na kuongozwa kwa njia thabiti kwa msaada wa mafundisho ya Mt. Tomaso”. – Paulus VI, Hotuba kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorianum, 12 machi 1964: AAS 56 (1964), uk. 365: “[Walimu]... waisikilize kwa heshima sauti ya Walimu wa Kanisa, ambao kati yao Mt. Tomaso ashika nafasi ya kwanza. Kwa maana uwezo wa akili yake ni kubwa sana, upendo wa ukweli ni mnyofu, na pana ni hekima ya kuzichunguza zile kweli kuu sana, ya kuzieleza na ya kuziunganisha kwa kifungo cha umoja kifaacho, kiasi kwamba mafundisho yake ni chombo chenye nguvu sana, licha ya kuiweka salama misingi ya imani, hata ya kupata matunda ya maendeleo bora kwa faida na usalama”. – Taz. pia id., Hotuba kwenye Kongamano la VI la kimataifa ya kielimu-Tomaso, 10 septemba 1965: AAS 57 (1965), uk. 788-792.
[37] Taz. Conc. Vat. II, Const. de Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, nn. 7 na 16: AAS 56 (1964), uk. 100s. na 104s.
[38] Taz. Paulus VI, Litt. Enycl. Ecclesiam suam, 6 agosti 1964: AAS 56 (1964), uk. 640s.
[39] Taz. Conc. Vat. II, Const. de Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, nn. 10, 14, 15, 16. – Idara Takatifu kwa Madhehebu ya Ibada, Mwongozo Inter oecumenici kwa utekelezaji kamili wa Const. de Sacra Liturgia, 26 septemba 1964, nn. 11 na 12: AAS 56 (1964), uk. 879 s.
[40] Taz. Conc. Vat. II, Decretum de Oecumenismo, Unitatis redintegratio, nn. 1, 9, 10: AAS 57 (1965), uk. 90 na 98 s.
[41] Taswira kamili ya mchungaji inapatikana katika hati Mababa Watakatifu za hivi karibuni zenye kueleza habari za maisha, za tunu na za malezi ya mapadre, hasa: Mt. Pius X, Exhortatio ad Clerum Haerent animo: S. Pii X Acta, IV, uk. 237 ss. – Pius XI, Litt. Encicl. Ad catholici Sacerdotii: AAS 28 (1936), uk. 5 ss. – Pius XII, Adhortatio Apost. Menti Nostrae: AAS 42 (1950), uk. 657 ss. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Sacerdotii Nostri primordia: AAS 51 (1959), uk. 545 ss. – Paulus VI, Epistula Apost. Summi Dei Verbum: AAS 55 (1963), uk. 979 ss.

Kuhusu malezi ya kichungaji mengi yanapatikana pia katika Litt. Encycl. Mystici Corporis (1943), Mediator Dei (1947), Evangelii Praecones (1951), Sacra Virginitas (1954), Musicae Sacrae Disciplina (1955), Princeps Pastorum (1959), na pia katika Const. Apost. Sedes Sapientiae (1956) kwa ajili ya watawa.

Pius XII , Ioannes XXIII na Paulus VI wameelezea mara nyingi taswira ya mchungaji mwema, pia katika hotuba zao kwa waseminari.

[42] Kuhusu umuhimu wa hali hii iliyosimikwa na uprofesi wa mashauri ya kiinjili: taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. de Ecclesia, Lumen Gentium, cap. VI: AAS 57 (1965), uk. 49-53. – Conc. Vat. II, Decretum de accommodata renovatione vitae religiosae, Perfecta Caritatis, AAS 58 (1966), uk. 702-712.
[43] Taz. Paulus VI, Litt. Enycl. Ecclesiam suam, 6 agosti 1964: AAS 56 (1964), sehemu mbalimbali, hasa uk. 635 s. na 640 ss.
[44] Taz. hasa Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 401 ss.
[45] Taz. hasa Conc. Vat. II, Const. dogm. de Ecclesia, Lumen Gentium, n. 33: AAS 57 (1965), uk. 39.
[46] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. de Ecclesia, Lumen Gentium, n. 17: AAS 57 (1965), uk. 20 s.
[47] Hati nyingi za kipapa zinahadharisha dhidi ya hatari ya kuturufu lengo la kimungu katika kazi za kichungaji na ya kupunguza – walau kiutendaji – umuhimu wa misaada ya kimungu; taz. hasa hati zinazorejewa katika dondoo n. 41.
[48] Hati za hivi karibuni za Kiti Kitakatifu husihi kuwepo uangalizi wa pekee kwa mapadre wapya. Zinakumbukwa hasa:

Pius XII, Motu proprio Quandoquidem, 2 aprile 1949: AAS 41 (1949), uk. 165-167. – Id., Adhortatio Apost. Menti Nostrae: 23 septemba 1950: AAS 42 (1950), uk. 657-702. – Id., Const. Ap. (kwa watawa) Sedes Sapientiae, 31 maggio 1956, pamoja na Katiba za jumla zilizoambatishwa. – Id., Hotuba kwa Mapadre wa “Mkutano wa Barcellona”, 14 juni 1957: Discorsi e Radiomessaggi, XIX, uk. 271-273. – Paulus VI, Hotuba mbele ya Mapadre wa Shirika la “Gian Matteo Gilberti”, Jimbo la Verona, 11 machi 1964: L’Osservatore romano, 13 machi 1964.