Index

Back Top Print

[AR - BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

TAMKO JUU YA ELIMU YA KIKRISTO

Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso Mkuu
ataka haya yakumbukwe daima

 

Utangulizi

UMUHIMU MAHUSUSI WA ELIMU (Gravissimum Educationis) kwa maisha ya binadamu na athari yake izidiyo kuwa kubwa katika usitawi wa jamii yetu ni mambo ambayo yanazingatiwa kwa makini na Mtaguso Mkuu wa kiekumeni.[1] Malezi ya vijana na elimu ya kujiendeleza ya watu wazima pia, kwa kweli vinapatikana kwa urahisi zaidi na tena vimekuwa vya lazima zaidi katika mazingira ya wakati huu. Watu, hali wamejipatia ufahamu uliokomaa wa hadhi yao na wa wajibu wao, watamani kuchukua nafasi inayowafaa ya kufanya kazi katika jamii, hasa katika nyanja za uchumi na za siasa[2]. Tena maendeleo ya kushangaza ya kiteknolojia na ya uchunguzi wa kisayansi, vyombo vipya vya upashanaji habari, hayo yote yanawapa watu – hasa kwa sababu wanapata fursa nyingi zaidi – uwezo wa kunufaika zaidi kwa urithi wa kitamaduni na wa kiroho na kufurahia kwa kuunganika kati yao kwa njia ya mahusiano mbalimbali, pia ya kimataifa.

Ndiyo sababu inazidi kuonekana popote mipango ya kuanzisha miradi ihusuyo elimu; na haki za msingi za wanadamu, kwa habari ya elimu, zatungwa na kutolewa katika hati rasmi, hasa haki zinazowahusu watoto na wazazi[3]. Kadiri idadi ya wanafunzi inavyoongezeka kwa kasi, ndivyo shule zinavyofunguliwa na kusitawishwa, na taasisi za malezi zinaanzishwa. Kutokana na mang’amuzi mapya mitindo ya kuelimisha na ya kufundisha yakamilishwa, na juhudi kubwa kweli hufanywa ili kuwaelimisha na kuwafunza watu wote, ijapo ni kweli kwamba watoto na vijana wanaokosa bado elimu ya msingi ni wengi sana, na wengine wengi hawajaridhia elimu iliyo kamili, ile inayosisitiza kwa pamoja ukweli na upendo.

Mama Kanisa, kwa upande wake, ili kutimiliza utume aliotumwa na Mwanzilishi wake wa kimungu, yaani kuwahubiria watu wote fumbo la wokovu na kujumlisha viumbe vyote katika Kristo, anapaswa kushughulikia maisha mazima ya wanadamu, hata yale ya kidunia, kwa vile yanahusiana na wito wao unaowaelekeza mbinguni[4], na hivyo ana wajibu wa pekee minajili ya maendeleo na ya usitawi wa elimu. Ndiyo sababu Mtaguso Mkuu hutangaza kanuni kadha wa kadha za msingi kuhusu elimu ya kikristo, hasa ile ambayo hutolewa shuleni, kanuni ambazo itakuwa ni wajibu wa tume maalum – baada ya kazi za Mtaguso kumalizika – kuzipanua na kufafanua zaidi. Kisha itakuwa juu ya Mabaraza ya Maaskofu kuzitekeleza katika mazingira ya mahali mbalimbali.

Haki ya wanadamu wote ya kujipatia elimu na maana ya elimu

1. Wanadamu wote, wa taifa lolote, cheo chochote, na umri wowote, kwa mujibu wa hadhi yao ya kibinadamu wanayo haki isiyofutika ya kupata elimu[5]. Elimu hiyo iwe inafaa kwa shabaha ya maisha yao[6], ilingane na tabia yao, utofauti wa jinsia, utamaduni na desturi za taifa lao; pia iwasaidie kwa ushirikiano wa maisha ya kindugu na watu wa mataifa mengine, ili kuthibitisha umoja na amani ya kweli hapa duniani. Elimu ya kweli itahamasisha malezi ya binadamu kwa mtazamo wa kikomo chake, na ya mafaa ya jamii mbalimbali, ambazo kila mwanadamu ni mwanachama, na ambamo, akiwa amepevuka, atakuwa ana wajibu wa kutimiza.

Kwa hiyo, huku yakithaminiwa sawasawa maendeleo katika saikolojia, pedagojia na ufundishaji, watoto na vijana lazima wasaidiwe kusitawisha utaratibu johari za kimwili, za kimaadili na za kiakili, na pia kujipatia hatua kwa hatua hisia zilizokomaa za majukumu kwa ajili ya kuinua maisha yao – kwa utaratibu na kwa vitendo visivyokoma – na kwa kutafuta uhuru wa kweli, hali wameshinda vipingamizi vyote kwa uhodari na uvumilivu. Kadiri wanavyokua, lazima wapewe kwa busara elimu ya uzazi iliyo na tunu nzuri. Waingizwe pia katika maisha ya kijamii, ili wakiwa na yale yote yanayohitajika na ya kufaa kwa lengo hili, waweze kuingia kwa mafanikio katika nyanja zote za maisha ya kijamii, na wawe tayari kwa dialogia na wengine, na watoe mchango wao kwa ajili ya kukuza mafaa ya ushirika.

Hali kadhalika, Mtaguso Mkuu hutangaza kuwa watoto na vijana wanayo haki ya kusaidiwa kuzitathmini kwa dhamiri nyofu na kuzipokea kwa ukubaliano wa hiari tunu za kimaadili, pia kumjua na kumpenda Mungu kwa ukamilifu zaidi. Kwa sababu hiyo, huwasihi na kuwaonya wanaotawala mataifa ama wanaosimamia elimu, wafanye bidii ili vijana wasije wakanyimwa kamwe haki hiyo tukufu. Aidha, huwahimiza wanakanisa wote wafanye kazi kwa juhudi katika nyanja zote za elimu, hasa kusudi manufaa makubwa ya elimu na ya mafunzo kwa wote yaenezwe upesi katika dunia nzima[7].

Elimu ya kikristo

2. Wakristo wote, kwa vile wamezaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, na wamekuwa viumbe vipya[8], na hivyo wakawa kwa jina na kwa kweli watoto wa Mungu, wanayo haki ya kupata elimu ya kikristo. Maana yake siyo tu kule kupevuka kibinadamu, bali hasa ni ile haki inayowafanya waliobatizwa, walioanza kujua fumbo la wokovu hatua kwa hatua, wajali zaidi na zaidi kipaji cha imani walichopokea: wajifunze kumwabudu Mungu Baba katika Roho na kweli (taz. Yn 4:23) hasa kwa njia ya Liturujia; wafundishwe kuishi maisha yao kulingana na utu mpya katika haki na utakatifu wa kweli (Efe 4:22-24), mpaka kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo (taz. Efe 4:13), na hivyo kutoa mchango wao kwa ajili ya kukuza mwili wake wa fumbo. Aidha, wakizingatia wito wao, wanatakiwa kujizoesha kutoa ushuhuda kwa tumaini lililo ndani yao (taz. 1Pet 3:15), na pia kuhimiza dhana ya kikristo ulimwenguni, kusudi tunu za kimaumbile – zikilinganishwa na mtazamo halisi wa utu uliokombolewa na Kristo – zinufaishe jamii yote[9]. Kwa hiyo Mtaguso Mkuu huwakumbusha wachungaji wa roho ule wajibu mkuu wa kuandaa kila kitu ili waamini wote wapate hiyo elimu ya kikristo, na hasa vijana, walio tumaini la Kanisa[10].

Wenye wajibu wa kutoa elimu

3. Wazazi, kwa sababu kuishi kwa wanao kumetokana nao, wanashika wajibu mkuu wa kuwalea wazao wao: hivyo watazamwe kuwa walezi wao wa kwanza na wenye maana zaidi[11]. Jukumu lao hilo la kuwa walezi ni muhimu sana, kiasi kwamba usipotimizwa ni vigumu sana kuziba pengo hilo. Ni juu ya wazazi kuandaa katika familia yao mazingira ya upendo halisi na ya utauwa kwa Mungu na ya huruma kwa watu, ambavyo vitasaidia kuwaelimisha kikamilifu watoto wao kibinafsi na kijamii. Hivyo familia ni shule ya kwanza ya fadhila za kijamii, ambazo jamii zote za wanadamu huzihitaji. Katika familia, hasa ya kikristo, yenye kutajirishwa kwa wadhifa na neema za sakramenti ya ndoa, watoto chipukizi, kutokana na imani waliyopewa katika ubatizo, wanatakiwa kujifunza kuhisi hali ya kimungu na kumwabudu, na pia kuwapenda majirani zao. Ndani ya familia yao, hung’amua kwa mara ya kwanza jamii iliyo bora ya kibinadamu na ya Kanisa. Hatimaye, tena kwa njia ya familia, wanaongozwa kutambua maana ya kuwemo miongoni mwa umma na katika taifa la Mungu. Kwa sababu hiyo wazazi hawana budi kuzingatia umuhimu wa familia iliyo ya kikristo kwelikweli kwa ajili ya maisha na ya usitawi wa taifa lenyewe la Mungu[12].

Wajibu wa kulea, ulio kwanza kabisa juu ya familia, huhitaji msaada wa jumuiya yote. Ndiyo sababu, pamoja na haki za wazazi na za wale wanaokabidhiwa nao sehemu ya wajibu ya kuelimisha, zipo haki na wajibu nyinginezo zihusuzo serikali, kwa maana ni juu yake kupanga yale yote yanayohitajika kwa manufaa ya wote hapa duniani. Mmoja kati ya wajibu zake ni kusaidia kwa namna mbalimbali malezi ya vijana: yaani kutetea wajibu na haki za wazazi na za wengine wanaohusika katika kazi za kuwaelimisha vijana, na pia kuwasaidia mahitaji. Pale panapokosekana uwezo wa wazazi na wa jumuiya nyinginezo, ni juu ya serikali, kutokana na kanuni ya auni, kusitawisha elimu, kwa kuridhia matakwa ya wazazi. Pia ni juu ya serikali kufungua shule na taasisi za kwake, kiasi kile kinachodaiwa na manufaa ya wote[13].

Hatimaye, kwa namna ya pekee sana, wajibu wa kuelimisha ni juu ya Kanisa, kwa sababu lenyewe laonekana kama jamii ya kibinadamu liwezalo kuleta elimu, lakini hasa kwa sababu lenyewe lina wajibu wa kuwatangazia watu wote njia ya wokovu na kuwashirikisha waamini katika uzima wa Kristo, likiwasaidia kwa bidii isiyokoma kuufikia utimilifu wa uzima huo[14]. Kanisa, mfano wa mama, lapaswa kuwapatia hao watoto wake elimu maalum, inayofanya maisha yao yote yapenywe na roho ya Kristo. Wakati huohuo lajitolea kwa mataifa yote kuhamasisha ukamilifu wa tabia za kibinadamu, kukuza mema ya jamii ya kidunia na kujenga ulimwengu unaostahi zaidi utu wa wanadamu[15].

Taratibu za elimu ya kikristo

4. Minajili ya kutimiza wajibu wake wa kuelimisha, Kanisa latumia vyombo vyote vifaavyo, hasa likijali vile vilivyo vyake pekee. Cha kwanza kati ya hivyo, mafundisho ya dini (katekesi)[16], yaletayo mwanga na nguvu kwa imani, hulisha maisha kufuatana na roho ya Kristo, huongoza waamini katika kushiriki fumbo la kiliturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu wa moyo[17], na huhimiza kazi za kitume. Vilevile Kanisa latathmini na lajaribu kuvipenya kwa roho yake na kuvikuza vyombo vingine, vilivyo urithi wa jumuiya ya wanadamu wote, navyo vinafaa kwa ajili ya kuwakamilisha kimaadili na kuwajenga kiutu. Vyombo hivyo hasa ni vyombo vya upashanaji habari[18], halafu makundi yanayohusika katika mafunzo ya kiutamaduni na kimwili, vyama vya vijana, na hasa mashule.

Umuhimu wa shule

5. Kati ya vyombo vyote vya kukuza elimu shule inao umuhimu wa pekee [19]. Kutokana na lengo na wajibu wake, pamoja na kupevusha kwa bidii nyingi wepesi wa akili, inakuza pia uwezo wa kubainisha mambo. Inashirikisha urithi wa utamaduni wa vizazi vilivyotangulia; inasisitiza umuhimu wa tunu mbalimbali; inaandaa kwa maisha ya kikazi. Pamoja na hayo hustawisha uhusiano wa kirafiki kati ya wanafunzi wenye tabia na hali zinazotofautiana, na hivyo inakuza uelewano kati yao. Aidha, shule yenyewe inakuwa kituo ambapo kazi na usitawi wake lazima visimamiwe kwa ushirikiano wa wazazi, walimu, vyama vya aina mbalimbali vyenye malengo ya kiutamaduni, kisiasa ama kidini, serikali na jamii yote kwa jumla.

Ule wito wa wale wote ambao, kwa kushirikiana na wazazi katika wajibu wao na kwa kufanya kazi kwa niaba ya jumuiya nzima, wanajipatia wajibu wa kufundisha shuleni, kweli ni wito bora na wenye maana kubwa. Wito wa namna hiyo unahitaji vipaji vya pekee vya akili na vya moyo, maandalizi ya makini sana, uwezo mwepesi na wa kudumu wa kujifanya upya na kujirekebisha.

Wajibu na haki za wazazi

6. Wazazi, kwa vile wanao wajibu na haki za msingi zisizofutika za kuwalea watoto wao, lazima wapewe uhuru kweli katika kuchagua shule [watakakojifunza]. Kwa sababu hiyo, mamlaka ya serikali ambayo yana wajibu wa kuhifadhi na kulinda uhuru wa raia wote, kwa mujibu wa haki-mgawanyo ( iustitiae distributive) lazima wahakikishe kwamba misaada ya kiserikali inatolewa kwa jinsi iliyo halali ili wazazi waweze kuwachagulia watoto wao shule zinazopendeza, kwa uhuru zaidi, kulingana na dhamiri yao [20].

Walakini, ni juu ya serikali kuwafanya raia wote waweze kujipatia elimu, na kuifaidia inavyofaa, na hivyo kuandaliwa kushika wajibu na haki zao za kijamii. Serikali hupaswa kuhifadhi haki za watoto za kupewa elimu ya kufaa shuleni, kuwa makini mintarafu ustadi wa walimu na uwezo wa kufundisha, kukinga afya ya wanafunzi, na kusimamia kwa jumla utaratibu wote wa kishule. Serikali itatekeleza hayo kwa kufuatia kanuni ya auni (principio subsidiarii officii), na kuzuia kila uwezo wa kuhodhi shule, kupinganako na haki za msingi za raia, maendeleo na uenezaji wa elimu, hupinga amani katika kuishi kwa pamoja kwa raia, na ule mseto [wa fikra] (pluralismo) uliopo siku hizi katika jamii nyingi za watu[21].

Mtaguso Mkuu unawasihi waamini wafanye bidii kusaidiana katika kutafuta mbinu za kuelimisha na taratibu za masomo zifaazo, na katika kuwaandaa walimu watakaojua kufundisha vema vijana. Hali kadhalika, kwa njia ya vyama mbalimbali vya wazazi, watoe mchango wao kwa mfululizo, ili kutimiza wajibu wa shule, hasa kwa upande wa kujenga maadili, ambako ni juu yake kutekeleza[22].

Elimu ya kimaadili na ya kidini katika shule zote

7. Kanisa, likijali wajibu wake muhimu sana wa kusimamia kwa makini elimu ya kimaadili na ya kidini ya wanae wote, halina budi kukaribia kwa upendeleo mahususi na kwa msaada wake, wale watoto wake wengi, wanaosoma katika shule zisizo za kikatoliki. Latekeleza wajibu huo ama kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya walimu na wakubwa wao, ama pia kwa kazi za kitume za wenzao[23], au hasa kwa huduma watoayo mapadre na walei wanaowafundisha njia ya wokovu kwa mtindo unaolingana na umri na mazingira mengineyo, na wanawapatia msaada wa kiroho kwa njia ya uanzishaji unaofaa kwa mahitaji ya wakati na mazingira.

Kanisa pia linawakumbusha wazazi kuhusu wajibu wao mkuu wa kupanga, au pia kudai, ili katika yote watoto wao waweze kunufaika na misaada hiyo, na wakue katika elimu ya kikristo sambamba na elimu ya kidunia. Kanisa lasifu serikali na jamii ambazo, zinapojali mseto wa jamii ya kisasa na kulinda uhuru wa dini, zinasaidia familia ili mafunzo ya wana wao yatolewe katika shule zote kulingana na misingi ya maadili na ya dini ya familia hizo zenyewe[24].

Shule za kikatoliki

8. Uwepo wa Kanisa katika uwanja wa kishule unadhihirika hasa katika shule za kikatoliki. Kwa kweli shule hizo hazina upungufu wa juhudi, zikilinganishwa na shule nyinginezo, katika kuimarisha utamaduni na malezi ya vijana. Lakini, wajibu wa pekee wa shule za kikatoliki ni kuunda mazingira bora katika jumuiya za shule yenye roho ya uhuru na upendo iliyo na msingi katika Injili, pia ni kuwawezesha vijana ili wakati wa kujengeka utu wao wakue kulingana na hali ya kuwa kiumbe kipya waliyoipata kwa ubatizo. Hatimaye, hufanya utamaduni mzima wa binadamu ulingane na ujumbe wa wokovu ili ufahamu wa dunia, wa maisha, wa watu waupatao wanafunzi hatua kwa hatua, uangazike katika imani[25]. Hivyo, shule za kikatoliki – kama ulivyo wajibu wake – zikitilia maanani hali ya maendeleo ya siku hizi, huwaandaa wanafunzi wake kuchangia kwa vikubwa katika mema ya watu wa dunia na huwaandaa kwa huduma ya kueneza Ufalme wa Mungu, ili kwa mfano wa maisha yao na ya kitume wawe chachu ya wokovu katika jumuiya.

Hivyo, shule za kikatoliki, kwa vile zaweza kutoa mchango mkubwa sana ili kutimiza utume wa taifa la Mungu na kuwa chombo kwa ajili ya dialogia kati ya Kanisa na jamii, kwa faida ya pande zote mbili, zina umuhimu mahususi pia katika nyakati hizi. Ndiyo sababu, Mtaguso Mkuu husisitiza kuwa ni haki ya Kanisa kuanzisha kwa hiari shule za aina zote na za kila kiwango, na kuzisimamia, haki ambayo tayari imetangazwa na Majisterio ya Kanisa katika hati nyingi [26]. Husisitiza pia kwamba utimilifu wa haki hiyo una umuhimu mkubwa zaidi kwa kulinda uhuru wa dhamiri, haki za wazazi na kwa kukuza utamaduni wenyewe.

Kwa upande wao, walimu wapaswa kukumbuka kwamba wanategemewa ili shule za kikatoliki ziweze kutimiza malengo yake na juhudi za utendaji wao[27]. Kwa hiyo wanatakiwa kujiandaa kwa kazi yao kwa uangalifu wa pekee, ili wawe na ustadi unaofaa wa kidunia na wa kidini unaothibitishwa na shahada zinazohusika, pia kuwa na ujuzi katika maarifa ya elimu inayolingana na ugunduzi wa maendeleo ya kisasa. Walimu wakiunganishwa na kifungo cha mapendo kati yao na wanafunzi wao, wakijazwa na roho ya kitume wanatakiwa kutoa ushuhuda kwa maisha yao na kwa mafundisho yao kwa Mwalimu pekee ambaye ni Kristo. Zaidi ya yote washirikiane na wazazi, katika mpango mzima wa elimu, wajali sana utofauti wa kijinsia na wa wajibu pekee ambao msichana ama mvulana amepewa na Mungu katika familia na katika jamii. Wajitahidi kuchochea ari ya wanafunzi wao, na hata baada ya hao kuhitimu masomo, waendelee kuwasaidia kwa mashauri yao, kwa urafiki, na kwa uundaji wa makundi maalum ya wanafunzi waliomaliza shule yenye kujaa roho halisi ya kikanisa. Mtaguso Mkuu unatangaza rasmi kuwa huduma za walimu hao ni utume kweli wa kufaa sana na kuhitajika pia katika nyakati zetu, na wakati huohuo ni huduma kweli kwa jamii. Wazazi wakatoliki wanakumbushwa wajibu wao wa kupeleka watoto wao katika shule za kikatoliki kila inapowezekana, kutoa misaada kulingana na uwezo wao na kushirikiana nazo kwa mafaa ya watoto wao[28].

Aina mbalimbali za shule za kikatoliki

9. Hata kama shule za kikatoliki zinaweza kubuni njia mbalimbali kulingana na mazingira ya mahali, shule zote ambazo kwa namna yoyote hulitegemea Kanisa zinatakiwa zilingane na mfano huo wa shule za kikatoliki kadiri iwezekanavyo [29]. Aidha Kanisa huambatisha umuhimu wa pekee kwa shule zile za kikatoliki ambazo zinahudhuriwa pia na wanafunzi wasio wakatoliki, hasa katika nchi ambapo Kanisa linaanzishwa siku hizi.

Na tena katika kuanzisha na kuziongoza shule za kikatoliki yatakiwa kutazama mahitaji ya maendeleo ya kisasa. Ndiyo sababu, licha ya kufanya bidii kuanzisha shule za msingi na za sekondari, ambazo hutoa misingi ya elimu, lazima zipewe umuhimu mkubwa sana zile ambazo zinadaiwa hasa katika mazingira ya siku hizi, kama vile: shule za ufundi na vyuo vya aina mbalimbali[30], taasisi za elimu ya watu wazima, taasisi za uandaaji kwa huduma za jamii, taasisi ya wasiojiweza wanaohitaji misaada ya pekee, vyuo vya mafunzo kwa ajili ya walimu, vyuo vya kidini, na vyuo vya matawi mengine ya elimu.

Mtaguso Mkuu unawahimiza wachungaji wa Kanisa na waamini wote kujitolea kikamilifu katika kuzisaidia shule za kikatoliki, ili kutimiza zaidi na zaidi jukumu lao, hasa katika kuwasaidia maskini, wanaokosa msaada na upendo wa kifamilia, na kwa wale wasio na kipaji cha imani.

Vitivo na vyuo vikuu vya kikatoliki

10. Kanisa vilevile linakuwa na uangalifu mkubwa kwa elimu ya juu, hasa kwa vyuo vikuu na vitivo mbalimbali. Kwa hakika katika vile vyote vinavyosimamiwa nalo, Kanisa linajaribu kwa utaratibu kuboresha masomo yote kulingana na kanuni na taratibu zake, katika uhuru wa utafiti wa kisayansi. Lengo lake ni kwamba mwendelezo wa ufahamu wa ndani upatikane, na kwa kuchunguza kwa makini masuala mapya na utafiti wa siku hizi za mabadiliko, itambulike waziwazi jinsi imani na akili zinavyokutana katika ukweli ulio mmoja. Njia hiyo hufuata msingi wa walimu wa Kanisa, na hasa Mt. Tomaso wa Akwino[31]. Kwa hiyo mtazamo wa kikristo upatikane, tuseme, hadharani, daima na popote kwa njia ya vyuo vikuu vya kikatoliki, katika jukumu zima la kukuza elimu ya juu. Wale wanafunzi kutoka katika vyuo hivi, wawe wamekamilika katika elimu, tayari kuchukua wajibu mkubwa katika jamii, na kuwa mashahidi wa imani ya kweli katika dunia[32].

Katika vyuo vikuu vya kikatoliki ambavyo havina kitivo cha teolojia, kunatakiwa kuwa na taasisi au somo la teolojia ambamo mihadhara mbalimbali itatolewa hata kwa wanafunzi walei. Kutokana na kwamba elimu ya juu inaendelezwa hasa na utafiti maalum wenye umuhimu wa pekee kisayansi, kila jitihada yatakiwa kufanywa katika vyuo vikuu na vitivo vya kikatoliki, ili kustawisha idara zinazoendeleza utafiti wa kisayansi.

Mtaguso Mkuu unahimiza kwa ari kuanzisha vyuo vikuu na vitivo vya kikatoliki kwa kuvigawanya kwa namna inayofaa katika mabara yote ya dunia, lakini vinatakiwa kuwa vyenye staha, si kwa idadi yao tu, bali kwa bidii ya taaluma. Kuingia katika vyuo hivyo kufanywe kuwa rahisi kwa wanafunzi wenye kuonyesha dalili ya kufaulu, hata kama hali zao ni za kawaida, hasa kwa wale wanaotoka katika nchi zinazoendelea.

Kutokana na kwamba mafaa ya jamii na ya Kanisa yana uhusiano wa ndani na maendeleo ya wanafunzi wanaofuata masomo ya juu[33], wachungaji wa Kanisa wanatakiwa wasijishughulishe tu na maisha ya kiroho ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu vya kikatoliki, bali katika juhudi yao kwa malezi ya kiroho ya wana wao wote, kwa njia ya makubaliano yanayofaa kati ya Maaskofu, wanatakiwa kuanzisha makazi (convictus) na vituo vya kikatoliki hata katika vyuo vikuu vingine visivyo vya kikatoliki. Huko mapadre, watawa na walei, ambao wamechaguliwa kwa uangalifu, na waliotayarishwa kwa kazi hiyo, waweze kutoa kwa wanafunzi vijana wa vyuo msaada wa kudumu wa kiroho na kiakili. Msisitizo wa pekee unatakiwa kuelekezwa kwa vijana, ambao ndio wenye uwezo, wawe wanafunzi wa vyuo vikuu vya kikatoliki au vyuo vikuu vingine, ambao waonekana kufaa kufundisha na kufanya uchunguzi, wanatakiwa kutiwa moyo kuchagua ualimu.

Vyuo vya teolojia

11. Kanisa linatumainia faida kubwa kutokana na utendaji wa vitivo vya taaluma za kidini [34]. Kwani kwavyo Kanisa linakabidhi wajibu mkubwa wa kutayarisha wanafunzi wake siyo tu kwa huduma ya kipadre, bali hasa kwa kufundisha katika taasisi za masomo ya juu ya kikanisa, au kwa kuendelea katika mafunzo kwa uchunguzi wa peke yao, au kwa kushika wajibu mzito wa utume wa kifikra ( apostolatus intellectualis). Ni kazi pia ya vyuo hivyo kuongeza uchunguzi katika nyanja mbalimbali za mafunzo ya kikanisa. Lengo lake ni kuhakikisha kwamba ujuzi wa ndani zaidi wa ufunuo wa kimungu upatikane, na kwamba urithi wa hekima ya kikristo, uliopokelewa kutoka kwa vizazi vilivyotangulia ukaguliwe vizuri, na pia dialogia na ndugu waliojitenga nasi, na wale wasio wakristo, ihimizwe, na kwamba masuala yanayotokana na maendeleo ya kitamaduni yatatuliwe kwa ufasaha [35].

Kwa hiyo, vitivo vya kikanisa, vikiisha kuzikagua sheria zao inavyofaa, vihamasishe sana usitawi wa taaluma za kikanisa, pamoja na nyinginezo zinazohusiana nazo; na kwa kuweka njia na misaada ya kisasa vyatakiwa kuwafunza wanafunzi wao kwa uchunguzi wa juu zaidi.

Umuhimu wa uratibu katika uwanja wa elimu

12. Kama vile ushirikiano unavyozidi kuwa wa umuhimu siku kwa siku na wenye nguvu zaidi kimajimbo, kitaifa na kiulimwengu, ni wa lazima sana pia katika uwanja wa kielimu. Kila jitihada ichukuliwe katika kuweka uratibu wa kufaa kati ya shule za kikatoliki; na ushirikiano kati ya shule hizo na nyinginezo wafaa pia kuendelezwa kwa faida ya jamii nzima[36].

Kutokana na kiwango kikubwa cha uratibu na kutokana na kazi hiyo ya ushirikiano, yatazaliwa matunda bora, hasa katika uwanja wa taasisi za kitaaluma. Kwa hiyo, katika kila chuo kikuu, vitivo mbalimbali vyatakiwa kusaidiana kadiri uwanja wake unavyoruhusu. Hali kadhalika, vyuo vikuu vyenyewe vyatakiwa kushirikiana sana kwa maungano ya dhati, kwa mfano kuitisha makongamano ya kimataifa, kupeana taarifa juu ya uchunguzi wa kisayansi, kuwasiliana juu ya matokeo ya utafiti wao, kubadilishana wahadhiri kwa muda, na kukuza njia zote ambazo zinafaidia ushirikiano kati yao.

Hatima

Mtaguso Mkuu unahimiza kwa nguvu wanafunzi wenyewe kuheshimu ubora wa jukumu la kuelimisha ( muneris educandi) na kuwa tayari kuupokea kwa moyo wote, hasa katika nchi zile ambapo elimu ya vijana ipo katika hali ngumu kwa sababu ya upungufu wa walimu.

Vilevile, Mtaguso Mkuu unatoa shukrani za dhati kwa mapadre, watawa wa kiume na wa kike na walei ambao wamejitolea kwa roho ya kitume kwa kazi zote katika elimu kwa shule za aina zote za kila kiwango. Mtaguso unawahimiza kuendelea kwa upendo kutoa huduma hii na kuzidi kujibidisha katika kuwajaza wanafunzi wao roho ya Kristo, katika ustadi wao wa kufundisha, na katika jitihada za kujiendeleza ili wasikuze tu matengenezo ya Kanisa ndani yake, lakini pia wadumishe na kuongeza mafaa ya uwepo wake katika ulimwengu wa leo, hasa katika uwanja wa elimu.

 

Mambo yote yaliyoamuliwa katika tamko hili, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 28 Oktoba 1965

Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki

(zinafuata sahihi za Mababa)  [1] Kati ya hati zilizo nyingi sana zinazoeleza juu ya elimu ya kikristo, tazama hasa: Benedictus XV, Ep. Apost. Communes Litteras, 10 apr. 1919: AAS 11 (1919) uk. 172. – Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, 31 dec. 1929: AAS 22 (1930) uk.49-86. – Pius XII, Hotuba kwa vijana wa Aksio Katoliki wa Italia, 20 apr. 1946: Discorsi e Radiomessaggi VIII, uk. 53-57; id. Hotuba kwa akina baba wa Ufaransa, 18 sept. 1951: Discorsi e Radiomessaggi XIII, uk. 241-245. – Yoannes XXIII, Tangazo la redio katika kutimiza mwaka wa 30 wa waraka kwa watu wote Divini Illius Magistri, 30 dec. 1959: AAS 52 (1960) uk. 57-59. – Paulus VI, Hotuba kwa wanachama F.I.D.A.E. (Federazione Istituti Dipendenti dall'Autorità Ecclesiastica = Umoja wa Taasisi zilizo chini ya Mamlaka ya Kikanisa), 30 dec. 1963: Encicliche e Discorsi di S.S. Paolo VI, I, Roma 1964, uk. 601-603.

Aidha, ionwe Acta et Documenta Concilio Oecumenico Vaticano II apparando, series I, Antepraeparatoria, vol. III, uk. 363-364, 370-371, 373-374.

[2] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961) uk. 413, 415-417, 424; id. Litt. Encycl. Pacem in Terris, 11 apr. 1963: AAS 55 (1963), uk. 278s.
[3] Taz. Tamko la Haki za Binadamu (Déclaration des droits de l’homme) iliyoidhiniwa tarehe 10 des. 1948 na Baraza la Umoja wa Mataifa; pia, taz. Tamko la Haki za Watoto (Déclaration des droits de l’enfant), 20 nov. 1959; Hati ya nyongeza ya mapatano ya kuzilinda Haki za binadamu na Uhuru wa msingi (Protocole additionel à la convention de sauveguarde des droits de l’homme et des libertés fondamentales), Paris, 20 machi 1952; kuhusu hilo “Tamko la Haki za Binadamu”, taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Pacem in terris, 11 apr. 1963: AAS 55 (1963) uk. 295.
[4] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961) uk. 402. Taz. pia Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 17: AAS 57 (1965) uk. 21.
[5] Pius XII, Rediotangazo ya 22 des. 1942: AAS 35 (1943) uk. 12, 19. – Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Pacem in terris, 11 apr. 1963: AAS 55 (1963) uk.259s. Taz. pia Matamko ya Haki za Binadamu yaliyokaririwa katika dondoo n.3 hapo juu.
[6] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, 31 des. 1929: AAS 22 (1930) uk. 50s.
[7] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961) uk. 441.
[8] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, l.c., uk 83.
[9] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 36: AAS 57 (1965) uk. 41ss.
[10] Taz. Conc. Vat. II, Decretum de pastorali Episcoporum munere in Ecclesia, Christus Dominus, nn. 12-14: AAS 58 (1966) uk. 678-679.
[11] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, l.c., uk.59s.; Litt. Encycl. Mit brennender Sorge, 14 machi 1937: AAS 29 (1937) uk. 164s. – Pius XII, Hotuba iliyotolewa kwenye Kongamano la kwanza la kitaifa la Umoja wa Walimu Wakatoliki wa Italia (A.I.M.C.), 8 sep. 1946: Discorsi e Radiomessaggi, VIII, uk. 218.
[12] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 11 na 35: AAS 57 (1965) uk. 16 na 40s
[13] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, l.c., uk.63s. – Pius XII, Rediotangazo ya tarehe 1 juni 1941: AAS 33 (1941) uk. 200; Hotuba iliyotolewa kwenye Kongamano la kwanza la kitaifa la Umoja wa Walimu Wakatoliki wa Italia (A.I.M.C.), 8 sep. 1946: Discorsi e Radiomessaggi, VIII, uk. 218. – Kuhusu kanuni ya auni, taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Pacem in terris, 11 apr. 1963: AAS 55 (1963) uk.294.
[14] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, l.c., uk.53s, 56s. Litt. Encycl. Non abbiamo bisogno, 29 juni 1931: AAS 23 (1931) uk 311s. – Pius XII, Litt. Secretariae Status ad XXVIII Hebdomadam Soc. Ital., 20 sep. 1955: L’Osservatore Romano, 29 sep. 1955.
[15] Kanisa linayasifu mamlaka yale ya kiserikali, ya kimahali, ya kitaifa na ya kimataifa ambayo, kwa kuzingatia mahitaji ya lazima ya wakati wetu, hujishughulisha kwa nguvu zao zote ili watu wa mataifa yote wafaulu kujipatia elimu bora zaidi na kuinua kiwango cha maisha. Taz. Paulus VI, Hotuba kwa Baraza la Umoja wa Mataifa, 4 okt. 1965: AAS 57 (1965) uk. 877-885.
[16] Taz. Pius XI, Motu Proprio Orbem catholicum, 29 juni 1923: AAS 15 (1923) uk. 327-329; Decretum Provido sane, 12 jen. 1935: AAS 27 (1935) uk. 145-152. – Conc. Vat. II, Decretum de pastorali Episcoporum munere in Ecclesia, Christus Dominus, nn. 13 na 14: AAS 58 (1966) uk. 678-679.
[17] Taz. Conc. Vat. II, Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, n. 14: AAS 56 (1964) uk. 104.
[18] Taz. Conc. Vat. II, Decretum de instrumentis communicationis socialis, Inter mirifica, nn. 13 na 14: AAS (56 (1964) uk. 149s.
[19] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, l.c., uk. 76; Pius XII, Hotuba kwa Umoja wa Walimu Wakatoliki wa Bavaria (Ujermani), 31 des. 1956: Discorsi e Radiomessaggi, XVIII, uk. 746.
[20] Taz. Conc. Prov. Cincinnatense III, a. 1861: Collatio Lacensis, III, col. 1240, c/d; Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, l.c., uk. 60, 63s.
[21] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, l.c., uk. 63; Litt. Encycl. Non abbiamo bisogno, 29 juni 1931: AAS 23 (1931) uk. 305. – Pius XII, Litt. Secretariae Status ad XXVIII Hebdomadam Soc. Ital., 20 sep. 1955: L’Osservatore Romano, 29 sep. 1955. – Paulus VI, Hotuba kwa Umoja wa Wafanyakazi Wakatoliki wa Italia (A.C.L.I.), 6 okt. 1963: Encicliche e Discorsi di Paolo VI, I, Roma 1964, uk. 230.
[22] Taz. Ioannes XXIII, Tangazo la redio katika kutimiza mwaka wa 30 wa Waraka kwa watu wote (Litt. Encycl.) Divini Illius Magistri, 30 des. 1959: AAS 52 (1960) uk. 57.
[23] Kanisa linastahi sana walimu na wanafunzi wakatoliki wanaojimudu kufanya kazi ya kitume hata katika mashule hayo.
[24] Taz. Pius XII, Hotuba kwa Umoja wa Walimu Wakatoliki wa Bavaria (Ujermani), 31 des. 1956: Discorsi e Radiomessaggi, XVIII, uk. 745s.
[25] Taz. Conc. Prov.es Westminster I, a. 1852: Collectio Lacensis III, col. 1334, a/b. – Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, l.c., uk 77s. – Pius XII, Hotuba kwa Umoja wa Walimu Wakatoliki wa Bavaria (Ujermani), 31 des. 1956: Discorsi e Radiomessaggi, XVIII, uk. 746. – Paulus VI, Hotuba kwa wanachama F.I.D.A.E. (Federazione Istituti Dipendenti dall'Autorità Ecclesiastica = Umoja wa Taasisi zilizo chini ya Mamlaka ya Kikanisa), 30 dec. 1963: Encicliche e Discorsi di S.S. Paolo VI, I, Roma 1964, uk. 602s.
[26] Rej. kwanza kabisa hati zilizotajwa kwenye dondoo n. 1; licha ya hayo, haki hii ya Kanisa ilitamkwa na Mitaguso mingi ya kiprovinsi, na pia na Matamko mengi ya siku hizi ya Mabaraza ya Maaskofu.
[27] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Divini Illius Magistri, l.c., uk. 80s. – Pius XII, Hotuba kwa Umoja wa Walimu Wakatoliki wa Shule za sekondari wa Italia (U.C.I.I.M.), 5 jen. 1954: Discorsi e Radiomessaggi, XV, uk. 551-556. – Ioannes XXIII, Hotuba iliyotolewa kwenye Kongamano la VI la Umoja wa Walimu Wakatoliki wa Italia (A.I.M.C.), 5 sep. 1959: Discorsi, Messaggi, Colloqui, I, Roma 1960, uk. 427-431.
[28] Taz. Pius XII, Hotuba kwa Umoja wa Walimu Wakatoliki wa Shule za sekondari wa Italia (U.C.I.I.M.), 5 jen. 1954: l.c., uk. 555.
[29] Taz. Paulus VI, Hotuba kwa Tume la kimataifa la Elimu ya kikatoliki (O.I.E.C.), 25 feb. 1964: Encicliche e Discorsi di Paolo VI, II, Roma 1964, uk. 232.
[30] Taz. Paulus VI, Hotuba kwa Umoja wa Wafanyakazi Wakatoliki wa Italia (A.C.L.I.), 6 okt. 1963: Encicliche e Discorsi di Paolo VI, I, Roma 1964, uk. 229.
[31] Taz. Paulus VI, Hotuba iliyotolewa kwenye Kongamano la VI la kimataifa juu ya mfumo wa kifikra wa Mt. Tomaso wa Akwino ( = la kitomisti), 10 sep. 1965: AAS 57 (1965) uk. 788-792.
[32] Taz. Pius XII, Hotuba kwa walimu na wanafunzi wa Shule za sekondari za kikatoliki za Ufaransa, 21 sep. 1950: Discorsi e Radiomessaggi, XII, uk. 219-221; Waraka kwa Mkutano wa XXII wa “Pax Romana”, 12 ago. 1952: Discorsi e Radiomessaggi, XIV, uk. 567-569. – Ioannes XXIII, Hotuba kwa Umoja wa Vyuo Vikuu vya kikatoliki, 1 apr. 1959: Discorsi, Messaggi, Colloqui, I, Roma 1960, uk. 226-229. – Paulus VI, Hotuba kwa Halmashauri ya wazee ya Chuo Kikuu cha kikatoliki cha Milano, 5 apr. 1964: Encicliche e Discorsi di Paolo VI, II, Roma 1964, uk. 428-443.
[33] Taz. Pius XII, Hotuba kwa Halmashauri ya wazee pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Roma, 15 juni 1952: Discorsi e Radiomessaggi, XIV, uk. 208: “Uongozi wa taifa la kesho unategemea hasa elimu na moyo wa wanachuo wa leo”.
[34] Taz. Pius XI, Const. Apost. Deus Scientiarum Dominus, 24 mei 1931: AAS 23 (1931) uk. 245-247.
[35] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Humani generis, 12 ago. 1950: AAS 42 (1950) uk. 568s., 578. – Paulus VI, Litt. Encycl. Ecclesiam Suam, Pars III, 6 ago. 1964: AAS 56 (1964) uk. 637-659. – Conc. Vat. II, Decretum de Oecumenismo, Unitatis redintegratio: AAS 57 (1965) uk. 90-107.
[36] Taz Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Pacem in terris, 11 apr. 1963: AAS 55 (1963) uk.284 et passim.