[BE
-
CS -
DE -
EN -
ES -
FR -
IT -
HU -
LA -
PT -
SW -
ZH]
KONSTITUSIO YA KICHUNGAJI JUU YA
KANISA KATIKA ULIMWENGU WA LEO[1]
Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja
na Mababa wa Mtaguso mkuu
ataka haya yakumbukwe daima
UTANGULIZI
Ushirika wa kiundani wa Kanisa na familia nzima ya wanadamu
1. FURAHA NA MATUMAINI (Gaudium et Spes), uchungu na fadhaa ya
wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote
ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Wala
hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao.
Maana jumuiya yao imefanywa na wanadamu ambao, wakijumuika pamoja katika
Kristo, huongozwa na Roho Mtakatifu katika hija yao inayouelekea Ufalme wa
Baba; nao wamepewa tangazo la ukombozi lililowekwa kwa wote. Kwa hiyo
[jumuiya ya wakristo] inajisikia kuwa inashikamana kweli na kwa ndani na
binadamu na historia yake.
Ni akina nani wanaoelekezewa maneno ya Mtaguso
2. Kwa sababu hiyo Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano, ukishapenya
kwa undani zaidi fumbo la Kanisa, bila kusita unalielekeza neno lake si kwa
watoto wa Kanisa tu, wala si kwa wale wote wanaoliitia jina la Kristo tu,
bali kwa wanadamu wote bila kutofautisha. Hivyo basi, Mtaguso unatamani
kuwawekea wazi mtazamo wake mintarafu kuwepo kwa Kanisa na kazi yake katika
ulimwengu wa nyakati zetu.
Kwa hiyo Mtaguso unauzingatia ulimwengu wa wanadamu, yaani jamii nzima ya
kibinadamu katika mazingira yote ambamo huishi ndani yake. Nao ni ulimwengu
ulio mandhari ya historia ya binadamu; tena unaleta alama ya juhudi zake,
kushindwa na kushinda kwake. Huu ndio ulimwengu ambao wakristo huamini kuwa
umeumbwa na unaendelea kutunzwa kwa njia ya mapendo ya [Mungu] Muumba. Tena
ni ulimwengu ambao umeanguka katika utumwa wa dhambi, lakini ambao
umeokolewa na Kristo Msulibiwa na Mfufuka aliyevunja mamlaka ya yule mwovu.
[Kwa njia hiyo, ulimwengu huu] unapata kutengenezwa upya kadiri ya azimio la
Mungu, na kufikia utimilifu wake.
Kumtumikia binadamu
3. Nyakati zetu binadamu, akipigwa na butwaa kwa sababu ya magunduzi na
uwezo wake, huyatokeza masuala yenye kufadhaisha juu ya maendeleo ya kisasa
ya ulimwengu; tena juu ya nafasi na wajibu wa binadamu hapa duniani (orbe
universo); juu ya maana ya juhudi za kila mmoja na za wote pamoja; kisha
juu ya kikomo cha mambo yote na cha wanadamu. Kwa sababu hiyo, Mtaguso
unashuhudia na kuieleza imani ya taifa zima la Mungu lililojumuishwa na
Kristo; hivyo hauwezi kutoa kielelezo kilicho wazi cha mshikamano, heshima
na upendo wake kwa ajili ya jamii nzima ya kibinadamu ambamo linaishi ndani
yake kuliko kuanzisha majadiliano ya pamoja (colloquium) na jamii hii
kuhusu masuala mbalimbali yaliyodokezwa hapo juu. [Katika majadiliano haya]
Mtaguso unaleta mwanga utokao katika Injili na unaweka wazi kwa wanadamu
nguvu ziletazo wokovu ambazo Kanisa, likiongozwa na Roho Mtakatifu,
linazipokea kutoka kwa Mwasisi wake. Maana binadamu ndiye aliye lazima
akombolewe, na jamii ya kibinadamu ndiyo hiyo lazima ijengwe. Hivyo basi,
kiini cha maelezo yetu yote ni binadamu: lakini kila binadamu katika hali
yake nzima, yaani katika umoja wa mwili na roho, wa moyo na dhamiri, wa
akili na utashi.
Kwa hiyo Mtaguso Mkuu, ukitangaza ukuu wa wito wa binadamu, tena
ukithibitisha kuwemo ndani yake kwa mbegu ya kimungu, basi unatoa kwa
binadamu msaada (cooperationem) wa Kanisa utolewao kwa moyo mweupe
ili kuimarisha udugu ule kati ya wanadamu wote unaolingana na wito huo.
Kanisa halisukumwi na tamaa yoyote ya makuu ya kidunia, bali linalenga
katika hilo tu: likiongozwa na Roho Mtakatifu, kuendeleza kazi ya Kristo
mwenyewe ambaye alikuja ulimwenguni ili kuushuhudia ukweli[2],
tena kukomboa wala si kuhukumu, kutumikia wala si kutumikiwa[3].
Maelezo ya kitangulizi
HALI YA BINADAMU KATIKA ULIMWENGU WA SASA
Matumaini na fadhaa
4. Ili kutekeleza jukumu hilo, ni wajibu wa kudumu wa Kanisa
kuchunguza ishara za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa Injili hivi
kwamba, kwa namna inayolingana na kila kizazi, liweze kuyajibu masuala
yarudiayo siku zote mintarafu umaana wa maisha ya kisasa na yale ya wakati
ujao, tena namna yanavyohusiana kati yao. Maana hatuna budi kujua na kuelewa
ulimwengu tunamoishi kama vile matazamio na matarajio yake, kisha tabia yake
iletayo mara nyingi fadhaa. Haya yafuatayo ni maelezo yanayoweza kutolewa
kuhusu masuala yenye uzito zaidi katika ulimwengu wa kisasa.
Binadamu anaishi leo katika kipindi kipya cha historia yake,
chenye mabadiliko ya haraka na ya ndani yanayoenea polepole ulimwenguni
kote. [Mabadiliko] hayo husababishwa na akili na harakati za ugunduzi wa
binadamu. Nayo yanamgeukia yeye mwenyewe, yaani mawazo yake, maazimio yake
ya kibinafsi na ya kijamii, namna ya kufikiri na namna ya kutenda, kuhusu
vitu na watu. Hivyo twaweza kuzungumzia mageuzi halisi ya kijamii na ya
kitamaduni yenye kuleta matokeo yake hata katika maisha ya kidini.
Kama inavyotokea kila mara mageuzi yanapofanyika katika harakati za
kimaendeleo, hata mabadiliko ya namna hii huleta matatizo makubwa. Hivyo
wakati binadamu anapoukuza uwezo wake, ndipo wakati huohuo mara nyingi
anashindwa kuuweka chini ya mamlaka yake. Tena binadamu anapofanya bidii ili
kujipenyeza zaidi na zaidi katika nafsi yake, mara nyingi huonyesha hali ya
kusitasita juu yake mwenyewe. Naye anagundua polepole kwa uwazi zaidi sheria
za maisha ya kijamii, lakini anaendelea kuwa mtu mwenye mashaka kuhusu
mahali pa kuzielekeza.
Haijatokea wakati wowote kuwa binadamu amefaidika kwa mali nyingi namna hii,
pamoja na kuwa na uwezo wa kiuchumi; na hata hivyo sehemu iliyo kubwa ya
wanadamu inataabika kwa njaa na umaskini; makundi makubwa ya watu
wasiohesabika hawajui kabisa kusoma na kuandika. Wala haijatokea kamwe
wanadamu kuutilia maanani uhuru kama ilivyo leo, na wakati huohuo mitindo
mipya ya utumwa wa kijamii na wa kifikara inazidi kustawi. Tena wakati
ulimwengu unaoelewa wazi umoja wake na ulazima wa mshikamano, ambapo kwao
watu wake wanategemezana wao kwa wao, ulimwengu unasukumwa kwa nguvu na
kugawanyika katika pande zinazopingana; maana bado yanaendelea mapigano
makali ya kisiasa, ya kijamii, ya kiuchumi, ya kikabila na ya kiitikadi.
Wala haijatoweka hatari ya vita vya ulimwengu vyenye uwezo wa kuangamiza
kila kitu. Ingawa mawasiliano ya mawazo yanazidi kusitawi, maneno yenyewe
yanayoeleza fikra zile muhimu hushika maana zilizo tofauti sana katika
itikadi (ideologiis) mbalimbali. Mwishowe, kwa kila jitihada binadamu
hutaka kujenga mfumo wa kidunia ulio mkamilifu zaidi, lakini bila kwenda
sambamba na mfumo wa maendeleo ya kiroho.
Basi, watu wengi sana wa kizazi chetu, wakizama katika hali za kupingana
namna hii, wanashindwa kugundua tunu halisi na za kudumu ili wapate
kuzilinganisha ipasavyo na zile zinazogunduliwa katika mwenendo wa
kihistoria. Kwa sababu hiyo wanasongwa na uzito wa mashaka na kuhangaishwa
kati ya matumaini na fadhaa, hasa wakati wanapojihoji mintarafu mwenendo wa
kisasa wa ulimwengu. Na mwenendo huo ndio unaomkabili binadamu, tena
humshurutisha ajipatie jibu.
Mabadiliko ya ndani
5. Fadhaa ya kiroho ya nyakati zetu na mabadiliko ya hali ya maisha
vinahusiana na geuzo la kimsingi linalojitokeza katika muundo wa elimu.
Maana muundo huu mpya kwa upande mmoja watilia mkazo zaidi sayansi za
kihesabu, kifizikia, au sayansi zinazomhusu binadamu mwenyewe; na kwa upande
wa kimatendo inategemea teknolojia itokanayo na sayansi zilizotajwa hapo
juu. Mtazamo huo wa kisayansi unaunda kwa mtindo ulio tofauti na ule wa
zamani utamaduni na tabia ya kimawazo. Aidha, teknolojia imesonga mbele
kiasi kwamba imeugeuza uso wa dunia na kuufuatilia utawala wa anga.
Tena akili ya binadamu kwa namna fulani inakuza utawala wake hata juu ya
nyakati: juu ya nyakati zilizopita kwa njia ya uchunguzi wa kihistoria; juu
ya nyakati zijazo kwa ustadi katika kuona mbele na kuratibu mambo. Basi,
maendeleo ya kisayansi, ya kibayolojia, ya kisaikolojia, na ya kijamii
yanampatia binadamu uwezo wa kujitambua vizuri zaidi. Na licha ya hayo,
maendeleo hayo yanampa pia mbinu za kiteknolojia ili kuyatengeneza moja kwa
moja maisha ya kijamii. Vilevile binadamu anajishughulisha zaidi na zaidi
kutathmini mbele na kudhibiti ongezeko la watu.
Kutokana na hayo, mwenendo wa historia unaharakishwa kiasi kwamba kila
binadamu hawezi kufuatilia mwenendo huo kirahisi. Kikomo cha jamii ya
wanadamu kinapata kuwa kimoja pasipo kutofautiana tena katika historia
mbalimbali. Na hivyo binadamu anapita kutoka utaratibu wa kutogeukageuka, na
kuingia katika utaratibu wa kimkikimkiki na wa kusonga mbele. Jambo hilo
linasaidia kuzuka kwa wingi kwa matatizo mapya ambayo yanadai bidii za
uchunguzi na usanisi mpya.
Mabadiliko katika mfumo wa kijamii
6. Kutokana na hayo yote, mabadiliko ya ndani yanazidi kutokea
katika jamii mahalia za jadi – kama vile jamaa, koo, kabila na vijiji – na
pia katika makundi mbalimbali na mahusiano ya maisha ya kijamii.
Jamii zinazotegemea viwanda zinaenea polepole, nazo zaleta ukwasi
(opulentiam) wa kiuchumi kwa baadhi ya nchi na zinabadilisha kiundani
mitazamo na hali za maisha ya kijamii zilizokuwepo tangu karne zilizopita.
Vilevile tamaa na bidii kwa mfumo wa maisha ya mjini zinakua; tamaa na bidii
hizo zinasukumwa na ongezeko la miji na wakazi wake, na pia zinatokana na
kuenea kwa [ruwaza za] maisha ya mjini kati ya wakazi wa vijijini.
Tena vyombo vipya na vizuri zaidi vya upashanaji habari vinaleta
taarifa kuhusu matukio mbalimbali kwa haraka na kufika sehemu zilizo mbali
za dunia. Pia vinasaidia kushamiri kwa mawazo na hisia, pamoja na kuzusha
mjibizo (repercussiones) wa mlolongo.
Kisha, usipunguzwe uzito wa kwamba watu wengi sana, wakisukumwa
kwa sababu mbalimbali kuhamia katika sehemu mbalimbali, hubadilisha namna
zao za kuishi.
Hivyo mahusiano kati ya wanadamu yanaendelea kuongezeka; na kwa upande
wake kuhusiana huko, au ujamiisho (socializatio), kunaunda tena
mawasiliano mapya; lakini mara chache tu kuhusiana huko kunakwenda sambamba
na kukomaa kwa mtu na kusaidia uhusiano wa kila mtu na mwenzake (personalizatio).
Maendeleo ya namna hii yanajitokeza wazi zaidi katika nchi zenye
viwango vya juu vya kiuchumi na kiteknolojia. Lakini yanayasukuma mbele hata
mataifa yale yanayoendelea na ambayo yanakusudia kupata manufaa kutokana na
viwanda na miji. Na mataifa hayo, hasa yakifungamana na mapokeo ya zamani,
yanajitahidi vilevile kujitengenezea upya mazoea ya uhuru yaliyokomaa na
yenye kumwajibisha kila mtu.
Mabadiliko ya kisaikolojia, kimaadili na kidini
7. Mabadiliko ya fikra na mifumo mara nyingi hujadili desturi za
kimapokeo, hasa kati ya vijana ambao mara nyingi hawana saburi na pengine
wanakuwa waasi kwa sababu ya kutoridhika. Nao, wakielewa umuhimu wao katika
maisha ya kijamii, hutamani kuchukua wadhifa wao mapema iwezekanavyo. Kwa
sababu hiyo mara nyingi wazazi na walezi wao wanakumbana kila siku na
matatizo makubwa zaidi katika kutekeleza jukumu lao.
Taasisi mbalimbali [za kuliongoza taifa], sheria, namna za
kufikiri na kuhisi ambazo zimerithiwa kutoka nyakati zilizopita, si kila
mara zinaonekana kuweza kulingana vema na hali ya kisasa. Kwa sababu hiyo
machafuko mazito katika tabia na kanuni zenyewe za kimaadili hutokea.
Kisha, hata maisha ya kidini husongwa na hali hii mpya. Kwa upande mmoja,
uwezo mkubwa zaidi wa kuyapambanua mambo unayasafisha maisha ya kidini na
mitazamo ya mazingaombwe na ushirikina ya ulimwengu inayoendelea kuwepo hadi
leo. Tena [uwezo huo mkubwa] hudai daima ambato (adhaesionem) la kila
mmoja na la kimatendo kwa imani. Na hivyo ni wengi wanaofikia hatua ya
kuhisi kiundani zaidi juu ya Mungu. Lakini kwa upande mwingine umati wa watu
wanatengana na dini kimatendo. Tofauti na nyakati zilizopita, suala la
kumkana Mungu ama dini, au kutomjali Mungu si suala linalotokea kwa nadra na
kwa mtu mmoja mmoja. Maana siku za leo tabia hii mara nyingi inaonyeshwa
kama dai la maendeleo ya kisayansi au kama mtindo mpya wa “humanismi” (humanismus).
Katika nchi nyingi haya yote yanajitokeza si tu katika masuala ya
wanafalsafa, bali hupenya kwa vikubwa katika fasihi, sanaa, ufafanuzi wa
sayansi ya kibinadamu na wa historia; kisha hupenya pia katika sheria za
kijamii hivi kwamba watu wengi hukanganywa.
Tofauti na migongano katika ulimwengu wa nyakati zetu
8. Mabadiliko ya haraka namna hii, ambayo mara nyingi yanaendeshwa
kiholela, pamoja na mang’amuzi ya undani zaidi ya hitilafu zilizomo
ulimwenguni huzalisha na kuongeza kinzano na migongano.
Awali ya yote katika mtu mwenyewe mara nyingi huonekana mgongano
kati ya fikra za kisasa kimatendo na mfumo wa mawazo kinadharia. Nayo mawazo
yanashindwa kuutawala na kuuratibu katika muhtasari wa kufaa ujumla wa mambo
anayofahamu. Vilevile hujitokeza mgongano kati ya juhudi kwa mafanikio ya
kimatendo na madai ya dhamiri kuhusu maadili. Mara nyingi [kutolingana huko
hujitokeza] pia kati ya hali za maisha ya pamoja na madai yatokanayo na
uwezo wa kufikiri, na pengine wa kutafakari, wa kila mtu. Na tokea hapo,
ndipo unapozaliwa mgongano kati ya ubingwa katika kazi mbalimbali za
wanadamu na mtazamo kwa ujumla wa mambo.
Aidha, katika familia mivutano hutokana na hali ngumu za idadi ya
watu, za kiuchumi na za kijamii; tena, hutokana na matatizo yanayozuka kati
ya vizazi vinavyofuatana; kisha hutokana na uhusiano mpya katika jamii kati
ya mwanamume na mwanamke.
Mivutano mikubwa huzuka pia kati ya makabila na hata kati ya
tabaka mbalimbali katika jamii; kati ya mataifa tajiri, na yale yenye uwezo
mdogo, na yale maskini; mwisho kabisa kati ya taasisi za kiulimwengu,
zilizoanzishwa kutokana na hamu ya mataifa ya kupata amani, na tamaa ya
kuieneza itikadi yake pamoja na ubinafsi wa kijamii uliopo katika mataifa au
katika taasisi nyinginezo.
Tokea hapo huzaliwa kutoaminiana, uadui, vita na uchungu. Chanzo cha hayo
yote ni binadamu mwenyewe, na ni binadamu mwenyewe mwenye kudhurika.
Matarajio ya binadamu yaliyoenea zaidi
9. Wakati huohuo linazidi kuaminiwa wazo la kwamba binadamu siyo
tu anaweza na anapaswa kuimarisha utawala wake juu ya viumbe, bali pia
kwamba ni juu yake kuunda mpango wa kisiasa, kijamii na wa kiuchumi ambao
utaweza kuwasaidia watu binafsi na makundi ya watu mbalimbali kupandikiza na
kuendeleza hadhi yao.
Tokea hapo hujitokeza madai ya wengi ambao wanaamini kabisa kuwa
wamenyimwa mali zao bila haki ama kwa mgawanyo usio sawa. Nchi zinazoendelea
au zile zilizoufikia uhuru hivi karibuni zinatamani kushiriki manufaa ya
ustaarabu wa kisasa katika vipengele vya kisiasa na kiuchumi. Tena hutamani
kutekeleza kwa uhuru wajibu wao katika ulimwengu, lakini wakati huohuo
umbali wao na mara nyingi hata kutegemea kwao kiuchumi nchi tajiri,
zinazoendelea upesi zaidi, vinazidi kukua siku kwa siku. Mataifa
yanayosongwa na njaa yanaziita na kuzihoji nchi tajiri. Wanawake wanadai
kuwa sawa na wanaume, si tu kinadharia, bali katika haki na hata katika
matendo, pale ambapo usawa haupo. Wafanyakazi na wakulima hawataki kuridhika
kwa mahitaji yao ya lazima tu katika maisha, bali wanataka kuendeleza haiba
yao kwa njia ya kazi, na hivyo kushika nafasi zao katika mpango wa maisha ya
kiuchumi, ya kijamii, ya kisiasa na ya kiutamaduni. Kwa mara ya kwanza
katika historia ya wanadamu mataifa yote siku hizi yanasadiki kwamba mapato
ya ustaarabu yanaweza na yanapaswa kufikishwa kwa wote.
Chini ya madai hayo yote imejificha hamu ya ndani na ya upote zaidi: watu
binafsi na makundi wanayo kiu ya maisha yaliyo ya uhuru kamili,
yanayoustahili utu na yanayoyaweka chini ya utawala wao yale yote ambayo
ulimwengu huu unaweza kuyatoa kwa ajili yao kwa wingi. Mataifa nayo
yanafanya juhudi zaidi na zaidi ili kuufikia muungano wa kiulimwengu kwa
namna fulani.
Mambo yakiwa hivyo, ulimwengu wa leo unajionyesha kwa wakati mmoja kuwa
wenye nguvu na mdhaifu, wenye uwezo wa kutenda yaliyo bora au yaliyo mabaya
sana. Na wakati huohuo zinafunguliwa mbele yake njia za uhuru au utumwa,
maendeleo au kurudi nyuma, udugu au chuki. Licha ya hayo binadamu anaelewa
kuwa ni juu yake kuelekeza kwa unyofu nguvu ambazo yeye mwenyewe aliziamsha
na ambazo zinaweza kumdhuru ama kumtumikia. Na kwa sababu hiyo anajihoji.
Maswali mazito zaidi ya binadamu
10. Kwa kweli makinzano yanayoutesa ulimwengu wa leo yanahusiana na lile
la ndani zaidi lenye mizizi yake katika moyo wa binadamu. Ndani ya binadamu
mwenyewe mambo mengi hupingana yenyewe kwa yenyewe. Maana, kwa upande mmoja
kiumbe hung’amua kwa namna nyingi mipaka yake; na kwa upande mwingine
hujihisi kuwa hana mipaka katika matarajio yake na kuwa ameitwa kwa maisha
ya juu zaidi. Akivutwa na tamaa nyingi, hulazimika daima kuzichagua baadhi
yake na kuziacha nyingine. Tena, akiwa mdhaifu na mkosefu, mara nyingi
hutenda yale ambayo asingetaka kuyatenda na hatendi yale ambayo angetaka
kuyatenda[4]. Kwa hiyo huteswa na
mgawanyiko huo uliopo ndani yake mwenyewe ambao kutokana nao huzuka pia
fitina nyingi na kubwa katika jamii. Hakika watu wengi sana wanaoishi
kimatendo katika hali ya uyakinifu (materialismus) wako mbali katika
kuelewa vizuri tatizo hilo sugu, au walau wakisongwa na umaskini huzuiliwa
kuitafakari hoja hiyo. Wengi hudhani ya kuwa watapata amani kwa njia ya
fafanuzi mbalimbali za mambo zilizoletwa kwa namna nyingi. Tena wengine
hungoja ukombozi ulio halisi na mkamilifu kutokana na juhudi za kibinadamu
tu; nao wameshawishiwa kuwa ufalme ujao wa kibinadamu hapa duniani utakidhi
matarajio yote ya mioyo yao. Wala hawakosekani wale ambao, wakishakata tamaa
juu ya umaana wa maisha yao, huusifu ujasiri wa wengine ambao, wakiona kuwa
maisha ya binadamu hayana umaana halisi, basi hujitahidi kuyafanya yawe na
maana kamili kwa njia ya akili yao tu. Hivyo mbele ya mageuzo ya ulimwengu
wa kisasa wanazidi kuwa wengi wale wanaojihoji au wanaojihisi kwa mang’amuzi
mapya maswali ya kimsingi kama haya yafuatayo: Je, binadamu ni nani? Je,
nini maana ya uchungu, uovu na mauti, ambayo yanaendelea kuwepo ingawa kuna
maendeleo katika kila fani? Je, ni kwa ajili ya nini mafanikio haya
yanayogharimiwa namna hii? Je, mwanadamu atoe mchango gani kwa ajili ya
jamii? Je, naye atarajie kupata nini kutokana nayo? Je, baada ya maisha haya
ya kidunia kitafuata nini?
Basi, Kanisa huamini kuwa Kristo, aliyekufa na kufufuka kwa ajili
ya wote[5], anampa binadamu
mwanga na nguvu kwa njia ya Roho wake ili binadamu mwenyewe aweze kuuitikia
wito wake ulio bora. Wala hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa
wanadamu liwapasalo wao kuokolewa kwalo[6].
Kadhalika, Kanisa linaamini kupata katika Bwana wake na Mwalimu ufunguo,
kiini na kikomo cha historia yote ya binadamu. Aidha, Kanisa linakiri kwamba
licha ya mabadiliko yote yapo mambo mengi yasiyobadilika; nayo yanapata
msingi wake halisi katika Kristo ambaye ndiye Yeye yule jana na leo na hata
milele[7]. Na hivyo, katika nuru
ya Kristo, aliye sura ya Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe
vyote[8], Mtaguso unadhamiria
kunena na watu wote ili kuwaeleza fumbo la binadamu na kushirikiana nao
katika utafiti ili kulipata suluhisho la matatizo muhimu zaidi ya nyakati
zetu.
SEHEMU YA KWANZA
KANISA NA WITO WA BINADAMU
Kuitikia misukumo ya Roho Mtakatifu
11. Taifa la Mungu linasukumwa na imani, ambayo kwayo linaamini
kuwa huongozwa na Roho wa Bwana anayeujaza ulimwengu. Nalo linayashiriki
matukio, madai na matarajio pamoja na wanadamu wote wa nyakati zetu. Katika
hayo linajibidisha kuzitambua ni zipi ishara halisi za kuwepo kwa Mungu au
za mpango wake. Maana imani inayang’arisha mambo yote kwa mwanga mpya, na
kuyafunua maazimio ya Mungu mintarafu wito mzima wa binadamu; na hivyo
inaiongoza akili kwa masuluhisho ambayo ni ya kiutu kabisa.
Katika mwanga huo, Mtaguso unadhamiria kwanza kuzichambua tunu
zinazoheshimiwa sana siku hizi, na kuzielekeza tena katika chemchemi yake ya
kimungu. Maana tunu hizo kwa zenyewe ni bora kwa sababu zinatokana na akili
ya kibinadamu iliyo kipaji kutoka kwa Mungu. Lakini mara nyingi, kutokana na
upotovu wa moyo wa binadamu tunu hizo zinaharibiwa kutoka hali zake halisi,
na hivyo zinahitaji kusafishwa.
Je, Kanisa linafikiria nini kuhusu binadamu? [sura ya 1]. Je, ni hatua
zipi zinazohimizwa kwa ujenzi wa jamii ya siku hizi? [sura ya 2]. Je, ni
nini maana ya ndani ya harakati za binadamu katika ulimwengu? [sura ya 3].
Majibu kwa maswali hayo yanasubiriwa. Baada ya hayo itaonekana wazi zaidi
kuwa taifa la Mungu na wanadamu wote ambao kati yao taifa la Mungu linaishi,
wanatumikiana wenyewe kwa wenyewe. Hivyo, utume wa Kanisa utajidhihirisha
kuwa na tabia ya kidini, na kwa sababu hiyohiyo kuwa pia na tabia halisi ya
kibinadamu [sura ya 4].
Sura ya Kwanza
HESHIMA YA BINADAMU
Binadamu ni sura ya Mungu
12. Waamini na wasio waamini hukubaliana karibu kwa kauli moja
kwamba yote yaliyomo duniani yamefanywa kwa ajili ya binadamu aliye kiini na
kilele chake.
Lakini, je, binadamu ni nani? Naye mwenyewe ametoa, na anaendelea kutoa,
maoni mengi juu yake; ambayo pengine hupingana. Maana, ama anajikuza na
kujiweka kuwa kama kanuni inayoviongoza vitu vyote, ama anajidhili hata
kukata tamaa na hivyo kuingia katika mashaka na fadhaa. Basi Kanisa
linajihusisha kiundani kwa matatizo hayo na linaweza kutoa jawabu, likiisha
kufundishwa na ufunuo wa Mungu. Nalo jibu linaweza kueleza hali halisi ya
binadamu, kuutia maana udhaifu wake, na wakati huohuo kumsaidia binadamu
kutambua kwa haki hadhi yake na wito wake.
Maana Maandiko Matakatifu hufundisha kuwa binadamu ameumbwa “kwa mfano na
sura ya Mungu”, mwenye uwezo wa kumjua na kumpenda Muumba wake. Tena
[hufundisha] kwamba binadamu aliwekwa na Mungu juu ya viumbe vyote vya
duniani kama mtawala wake[9] ili
aviongoze na kuvitumia kwa utukufu wa Mungu[10].
“Mtu ni kitu gani hata umkumbuke? Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya
mdogo punde kuliko malaika, umemvika taji ya utukufu na heshima; umemtawaza
juu ya kazi za mikono yako. Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake” (Zab
8:4-6).
Lakini Mungu hakumwumba binadamu na kumwacha peke yake, bali tangu mwanzo
“mwanamume na mwanamke aliwaumba” (Mwa 1:27), na muungano wao umeunda mtindo
wa kwanza wa ushirika kati ya watu. Maana binadamu kwa mtima wa maumbile
yake ni kiumbe ambaye anahitaji kushirikiana na wengine; naye hawezi kuishi
wala kuvitokeza vipawa vyake pasipo mahusiano na wenzake.
Kwa sababu hiyo Mungu, kama tena ilivyoandikwa kwenye Maandiko
Matakatifu, aliona “kila kitu alichokifanya, na tazama, kilikuwa chema sana”
(Mwa 1:31).
Juu ya dhambi
13. Ingawa binadamu aliumbwa na Mungu katika hali ya haki, hata hivyo
akishawishiwa na Shetani, tangu mwanzo wa historia aliutumia vibaya uhuru
wake. Naye akajikweza dhidi ya Mungu na kutamani sana kupata tarajio lake (finem
suum) nje ya Mungu. Ijapo walikuwa wamemfahamu Mungu, wanadamu
hawakumtukuza kama Mungu, bali mioyo yao isiyo na hekima ilitiwa giza, nao
wakakitumikia kiumbe badala ya Muumba[11].
Na yale tunayoarifiwa na ufunuo wa Mungu hulingana na ung’amuzi wenyewe.
Maana kama binadamu hujichunguza moyoni mwake anajitambua kuwa anauelekea
ubaya na kuzama katika mabaya mengi, ambayo kwa hakika hayawezi kutoka kwa
Muumba [wake] ambaye ni mwema. Mara nyingi binadamu, kwa kukataa kumkiri
Mungu kama asili yake, umevunja utaratibu uliokuwa wa kufaa kwa kikomo
chake, na wakati huohuo utaratibu mzima ndani yake, na pia katika uhusiano
wake na watu wenzake na viumbe vyote.
Hivyo binadamu amegawanyika ndani yake mwenyewe. Hivyo maisha yote ya
binadamu, mmoja mmoja na pamoja, hujidhihirisha kama pambano, tena lililo
kali, kati ya wema na uovu, kati ya mwanga na giza. Zaidi, binadamu
anajikuta hawezi kushinda kabisa peke yake mashambulio ya uovu, hivi kwamba
kila mmoja hujisikia kama amefungwa minyororo. Lakini Bwana mwenyewe amekuja
kumkomboa binadamu na kumtia nguvu akimwumba upya ndani yake na kumfukuza
“mkuu wa ulimwengu huu” (Yn 12:31), aliyekuwa amemfunga katika utumwa wa
dhambi[12]. Kwa sababu dhambi
humshusha binadamu mwenyewe, ikimzuia asiufikilie utimilifu wake.
Basi, katika mwanga wa Ufunuo huo, wito mkuu na pia udhaifu mkubwa,
ambavyo binadamu huvionja, vinapata maana yake halisi.
Maumbile ya binadamu
14. Binadamu ni umoja wa mwili na roho. Hivyo kwa hali yake ya kimwili
anajumlisha ndani yake vitu asili vya ulimwengu unaoonekana ili kwamba hivyo
[vitu] kwa njia yake viweze kuufikia utimilifu wake na kupata sauti ya
kumsifu Muumba kwa hiari
[13].
Ndiyo maana binadamu haruhusiwi kuudharau uzima wa mwili. Zaidi, anapaswa
kuutazama mwili wake kama mwema na wenye kustahili heshima kwa sababu
uliumbwa na Mungu na utafufuliwa siku ya mwisho. Japo hivyo, binadamu
aliyejeruhiwa na dhambi huonja maasi ya mwili. Kwa hiyo, ni heshima yenyewe
ya binadamu inayomdai amtukuze Mungu katika mwili wake
[14],
wala asiuruhusu ujitumikishe kwa maelekeo mapotovu ya moyo wake.
Lakini binadamu hakosi anapojitambua kuwa yeye ni mkuu kuliko viumbe
vingine vyenye mwili, wala anapojijali zaidi kuliko chembe ndogo tu ya
ulimwengu, au kuliko mwanajumuiya asiyetambuliwa katika jamii ya watu. Maana
binadamu katika undani (interioritate) wake huzidi viumbe vyote; naye
anaingia tena katika undani huo anapourudia moyo wake. Ndimo ambamo Mungu
anamngojea, Yeye ambaye ndiye mwenye kuichunguza mioyo[15];
tena, ambamo binadamu mbele ya macho ya Mungu huamua bahati yake. Kwa hiyo
[binadamu] akitambua kuwa ana nafsi ya kiroho isiyokufa, hakubali kuhadaiwa
na mawazo madanganyifu yanayotokana tu na hali za kimaumbile au za kijamii;
bali, kinyume chake hufikia kugusa kiundani ukweli wenyewe wa mambo.
Heshima ya akili, ukweli, na hekima
15. Binadamu anayo haki kujitambua kuwa mkubwa kuliko viumbe vyote kwa
sababu ya akili yake, ambayo kwayo hushiriki nuru ya fikra (
mentis)
ya Mungu. Kwa kujibidisha kuitumia akili yake katika mfululizo wa karne,
binadamu hakika amejiendeleza katika fani za sayansi, za kiuchunguzi, katika
sanaa za kiufundi na za kitaalamu (
artibus technicis et liberalibus).
Aidha, nyakati zetu binadamu amefanikiwa kwa vikubwa hasa katika kuutafiti
na kuutawala ulimwengu. Na hata hivyo ametafuta na kuuvumbua daima ukweli
ulio wa kina zaidi. Maana akili ya binadamu haimalizi kazi yake katika mambo
ya ulimwengu huu yanayoonekana tu, bali inamudu kuufikia ukweli unaoweza
kueleweka kwa uhakika halisi, ijapokuwa kutokana na dhambi imetiwa kivuli na
kudhoofishwa.
Kisha maumbile ya kiakili ya binadamu, yanaufikia ukamilifu wake kadiri
ipasavyo kwa njia ya hekima; nayo humvutia kwa upole binadamu ili atafute na
kupenda yaliyo kweli na mema. Na hekima hiyo, binadamu akijazwa nayo,
humwongoza kwa njia ya yale yaonekanayo kufikia yale yasiyoonekana.
Nyakati zetu zinahitaji hekima hiyo kuliko nyakati zilizopita, ili magunduzi
yote mapya yalingane zaidi na hali ya kibinadamu. Kwa kweli mustakabali wa
ulimwengu upo katika hatari, kama wasipojitokeza watu wenye hekima zaidi.
Licha ya hayo, haina budi kusisitizwa kwamba kuna mataifa mengi, ambayo
kiuchumi ni maskini zaidi kuliko mengine, lakini ni matajiri zaidi katika
hekima, yanayoweza kuyachangia mengine msaada mkubwa.
Aidha, kwa paji la Roho Mtakatifu, binadamu huweza kuifikia katika imani
hatua ya kutazama na kulionja fumbo la mpango wa Mungu[16].
Heshima ya dhamiri ya kimaadili
16. Ndani kabisa ya dhamiri yake binadamu hugundua sheria ambayo
hakujiwekea mwenyewe, lakini ambayo lazima aitii. Sauti [ya sheria hiyo]
inamwita daima kupenda na kutenda mema, na kuepuka uovu; nayo yasikika
kusema moyoni mwake wakati unaotakiwa, “fanya hili, epukana na lile”. Kwa
kweli binadamu anayo sheria moyoni mwake iliyoandikwa na Mungu; kuitii ndiyo
heshima yenyewe ya binadamu, na kadiri ya hiyo atahukumiwa[17].
Dhamiri ndicho kiini cha siri zaidi cha binadamu, na hekalu lake. Humo yeye
yumo peke yake pamoja na Mungu, ambaye sauti yake ndimo inamosikika[18].
Tena, kwa njia ya dhamiri inajijulisha kwa namna ya ajabu sheria ile ambayo
yapata utimilifu wake katika upendo wa Mungu na wa jirani[19].
Katika uaminifu kwa dhamiri [yao] wakristo wanajiunga na wanadamu wengine,
ili kutafuta ukweli na kuyatatua masuala mengi ya kimaadili yanayozuka
katika maisha ya binafsi na ya jamii. Kwa hiyo, kadiri dhamiri inavyozidi
kuwa nyofu, ndivyo watu na vikundi vinavyozidi kujitenga na uamuzi kipofu na
hujaribu kulingana na sheria halisi za uadilifu. Hata hivyo, pengine
inatokea kwamba dhamiri inadanganyika kwa sababu ya ujinga usioponyeka; ila
ijapo hivi haipotezi heshima yake. Lakini mambo haya hayawezi kusemwa ikiwa
binadamu anazembea katika kuutafuta ukweli na wema, tena iwapo dhamiri
[yake] karibu imepofuka kutokana na uzoefu wa dhambi.
Ubora wa uhuru
17. Lakini binadamu anaweza kuugeukia wema katika uhuru tu. Watu wa
nyakati zetu wanauzingatia sana uhuru huo na kuutafuta kwa shauku. Na katika
hilo wanayo haki. Lakini mara nyingi wanaushughulikia kwa namna isiyofaa,
kana kwamba yote yanaruhusiwa ilimradi yapendeze, hata yakiwa ni mabaya.
Bali uhuru halisi ndiyo ishara iliyo bora ya sura ya kimungu katika
binadamu. Maana Mungu alitaka kumwacha binadamu “aifuate nia yake”[20],
hivi kwamba amtafute Muumba wake kwa hiari; na hatimaye aufikie ukamilifu
ulio bora na wenye heri, pasipo shuruti na kwa kuambatana naye [Mungu]. Kwa
hiyo, hadhi ya binadamu yamtaka atende kadiri ya chaguo lake kwa kujua na
kwa uhuru; yaani awe amesukumwa na kuhimizwa kutoka ndani, wala si kwa
misukumo yenye upofu ya ndani yake, au kwa shuruti tu za nje. Lakini
binadamu anapewa hadhi hiyo anapoliweka mbele lengo lake kwa kuchagua kwa
hiari lililo jema, akijibandua mwenyewe na kila utumwa wa tamaa. Kwa juhudi
na bidii anajipatia njia zinazofaa lengo lake. Uhuru wa binadamu
uliojeruhiwa na dhambi, unaweza kufanikisha kikamilifu mpango huo
unaomwelekea Mungu kwa msaada wa neema ya Mungu tu. Aidha, kila binadamu
atapaswa kutoa hesabu ya maisha yake mbele ya mahakama ya Mungu, kwa mambo
yote aliyoyatenda, kwamba ni mema au mabaya[21].
Fumbo la mauti
18. Mbele ya kifo fumbo la hali ya binadamu hupata kuwa kubwa sana. Binadamu
anafadhaika si tu anapofikiria juu ya kukaribia kwa uchungu na uozo wa
mwili, bali zaidi anaposhikwa na hofu juu ya mambo yote kukoma moja kwa
moja. Lakini silka (
instinctu) ya moyo wake inamfanya apambanue mambo
kwa unyofu, hasa anapolichukia wazo la uharibifu wote na la mwisho kabisa wa
utu wake. Mbegu ya umilele iliyo ndani yake, isiyoweza kugeuzwa kuwa kitu
tu, hiyo basi huinuka dhidi ya mauti. Juhudi zote za teknolojia, ingawa
zinafaa sana, haziwezi kutuliza fadhaa ya binadamu; kurefusha maisha ya
kimwili hakuwezi kukidhi hamu ya maisha ya baadaye isiyozimika, iliyomo
moyoni mwa binadamu.
Wakati ambapo kila kuwaza kunakoma mbele ya kifo na mauti, hapo Kanisa,
likifundishwa na Ufunuo wa kimungu, hukiri kwamba binadamu ameumbwa na Mungu
kwa kikomo chenye heri kinachovuka mipaka ya udhaifu wa dunia hii. Zaidi ya
hayo, imani ya kikristo hufundisha kwamba kifo cha kimwili, ambacho binadamu
angezuiliwa kama asingalitenda dhambi[22],
kitashindwa kabisa. Nalo litatimizwa wakati binadamu atakaporudishwa na
uweza na huruma ya Mkombozi katika hali aliyoipoteza kwa sababu ya dhambi.
Maana Mungu alimwita na anaendelea kumwita binadamu aambatane naye kwa
maumbile yake yote katika ushirika wa milele na uzima wa kimungu usioweza
kuharibika. Kristo ndiye aliyeupata ushindi huo alipofufuka yu mzima, baada
ya kumkomboa binadamu na mauti kwa njia ya kifo chake[23].
Kwa hiyo imani, ikijiweka mbele ya watu kwa mafundisho yenye misingi imara,
inawapa wote wanaotaka kutafakari jibu kwa fadhaa zao mintarafu maisha
yajayo. Tena wakati huohuo imani inawawezesha kushirikiana katika Kristo na
ndugu zao waliokwisha kufa. Nayo [imani] inawapa tumaini la kwamba ndugu
hawa wamekwisha fikia uzima wa Mungu.
Namna za ukani Mungu (atheismus), na sababu zake
19. Hadhi ya binadamu kwanza kabisa imo katika wito wake wa kuwa na
ushirika na Mungu. Tangu mwanzo wa uwepo wake, binadamu anaitwa kuongea na
Mungu; kwani kama binadamu anakuwepo, ni kwa sababu aliumbwa na Mungu kwa
upendo [wake]; tena kwa upendo huo anatunzwa naye; wala binadamu hawezi
kuishi kikamilifu kulingana na ukweli ikiwa hautambui kwa uhuru upendo huo
na hamtegemei Muumba wake. Lakini wengi wa watu wa nyakati zetu hawakielewi
katu au wanakikataa waziwazi kiungo hiki cha ndani na kiletacho uzima na
Mungu [kwa binadamu]. Hivyo, ukani Mungu lazima utazamwe kama moja ya
masuala yaliyo mazito sana ya nyakati zetu, nao unapaswa kuchunguzwa kwa
uangalifu mkubwa.
Kwa neno “ukani Mungu”, au “atheismi”, hutajwa mambo kadhaa yanayotofautiana
sana kati yao. Maana wengine wanamkana Mungu waziwazi; wengine tena hudhani
kwamba binadamu hawezi kufahamu neno lolote juu yake; aidha wapo wengine
ambao huichunguza hoja kuhusu Mungu kwa njia inayoleta wazo kwamba suala
hilo halionekani kuwa na maana yoyote. Wengi, wanavuka isivyofaa mipaka ya
sayansi, ama hudai kuyafafanua mambo yote kwa mtazamo wa kisayansi tu; au,
kinyume chake, hawakubali kuwa ukweli ulio halisi unaweza kupatikana. Tena
wengine wanamtukuza binadamu kiasi ambacho imani kwa Mungu inadhoofishwa;
nao inavyoonekana wanapendelea kumkweza binadamu kuliko kumkana Mungu
waziwazi. Aidha wengine hujitungia wenyewe mawazo juu ya Mungu kwa namna
ambayo hayalingani na ukweli wa Injili, na hivyo fikra mintarafu Mungu
wanazozikataa haziwezi kwa namna yoyote ile kumhusu Mungu wa Injili. Kisha
wapo wengine ambao hawajishughulishi kamwe na suala juu ya Mungu, kwa sababu
hawaonekani kuhisi fadhaa yoyote kuhusu dini na wanashindwa kuelewa kwa nini
ingewapasa wajishughulishe nayo. Aidha, mara nyingi kumkana Mungu kuna asili
yake katika kuupinga vikali uovu uliopo ulimwenguni; au pengine pale ambapo
tunu za kibinadamu zinatiliwa ubora unaozifaa kweli za kimungu (
ipsius
absoluti) tu; na hivyo tunu hizo za kibinadamu zinachukua nafasi ya
Mungu. Mara nyingi pia ustaarabu wa kisasa unaweza kuleta ugumu katika
kumkaribia Mungu, si kwa sababu yake wenyewe, bali kwa kuwa unafungamana mno
na mambo ya dunia hii.
Bila shaka wale ambao kwa makusudi wanapania kumfunga Mungu mbali na
mioyo yao na kuepukana na hoja za kidini na hivyo wasiufuate mwongozo wa
dhamiri yao, hawa basi hawana budi kuwa na kosa. Lakini mara nyingi katika
fani hii hata waamini wamechangia. Kwa maana ukani Mungu ukitazamwa kwa
ujumla si jambo lililokuwepo tangu asili (non est quid originarium)
bali unatokana na sababu mbalimbali. Kati ya hizo [kisa kimojawapo] ni
upinzani wenye msingi wake katika malalamiko dhidi ya dini mbalimbali, na
hasa, katika nchi kadha wa kadha, dhidi ya dini ya kikristo. Kwa sababu
hiyo, katika vyanzo vya ukani Mungu waamini wanaweza kuchangia kwa sehemu
ambayo si ndogo. Maana, ama huzembea katika mafunzo ya imani; au hufafanua
mafundisho yake kwa namna isiyo sahihi; au kwa makasoro yao katika maisha
yao ya kidini, ya kimaadili au ya kijamii. [Kwa sababu hizo zote] hakuna
budi kusema kuwa waamini pengine wanauficha uso halisi wa Mungu na wa dini,
kuliko kuufunua.
Ukani Mungu wa kimpango
20. Mara nyingi ukani Mungu wa nyakati zetu hujidhihirisha kwa namna ya
mpango kamambe. Kadiri ya mpango huo, licha ya sababu nyingine, mvuto wa
binadamu kujitawala unakazwa sana, hivi kwamba unaleta ugumu katika
kumtegemea Mungu kwa namna yoyote ile. Watu wanaoshikilia nadharia hii ya
ukani Mungu hudai kuwa uhuru kwa binadamu ni kuwa mwenyewe kikomo chake (
homo
sibi ipse sit finis), yaani yeye peke yake ndiye mtengenezaji na mratibu
wa historia yake. Hao hudhani kwamba mtazamo huo haupatani na imani kwa
Bwana aliye Muumba na kikomo cha mambo yote; au pengine tu unaifanya batili
kabisa [imani hiyo]. Nadharia hiyo yaweza kuhamasishwa na hisia ya kuwa na
uwezo mkubwa ambayo inatiwa moyoni mwa binadamu na maendeleo ya
kiteknolojia.
Kati ya mitindo mbalimbali ya ukani Mungu wa nyakati zetu, hauna budi
kuzingatiwa ule unaotarajia ukombozi wa binadamu kutokana hasa na ukombozi
wa kiuchumi na wa kijamii. Inadaiwa kuwa dini kwa maumbile yake yenyewe ni
kipingamizi kwa ukombozi huo, kwa maana inaelekeza tumaini la binadamu kwa
maisha ya baadaye na yenye udanganyifu, na hivyo inamwondoa binadamu katika
harakati za kujenga mji wa dunia hii. Kwa hiyo, wafuasi wa itikadi hiyo
wanapofikia hatua ya kushika hatamu za uongozi katika nchi, wanaipinga dini
kwa nguvu na kueneza ukani Mungu, kwa kutumia pia vyombo vyao vya dola
vinavyowaelemea raia, hasa katika elimu ya vijana.
Msimamo wa Kanisa mbele ya ukani Mungu
21. Kanisa likijishughulisha kiaminifu na wajibu wake mbele za Mungu na
wanadamu, halina budi kuyapinga kwa uchungu na kwa nguvu mafundisho na
matendo hayo yenye kudhuru, kama lilivyofanya huko nyuma[24].
[Mafundisho na matendo] hayo yanapingana na akili na mang’amuzi ya kawaida
ya wanadamu, pamoja na kumwangusha binadamu kutoka cheo chake cha heshima
alichoumbiwa.
Lakini Kanisa linajibidisha kuvumbua sababu za kumkana Mungu zinazojificha
akilini mwa wakana Mungu; nalo likitambua uzito mkubwa wa masuala
yanayozushwa na ukani Mungu, tena likisukumwa na upendo kwa ajili ya watu
wote, hudhani kuwa masuala haya yanastahili uchunguzi wenye uzingativu na wa
ndani zaidi.
Kanisa linaamini kwamba kumkiri Mungu hakupingi hata kidogo hadhi ya
binadamu, kwa vile hadhi hiyo husimikwa na kutimilizika katika Mungu; maana
binadamu hupokea kutoka kwa Mungu Muumba vipawa vya akili na uhuru; tena
huwekwa kuwa huru katika jamii; lakini hasa huitwa kuungana na Mungu
mwenyewe kama mwana [wake] na kushiriki heri yake Yeye. Aidha [Kanisa]
linafundisha kuwa tumaini kwa maisha yajayo (
spem eschatologicam)
halipunguzi umuhimu wa shughuli za kidunia, bali hutoa sababu mpya
zinazosaidia utekelezaji wake. Kinyume chake, ukikosekana msingi wa kimungu
na tumaini la uzima wa milele, basi hadhi ya binadamu inaudhiwa sana, kama
inavyoonekana mara nyingi siku za leo. Hoja za maisha na mauti, za dhambi na
uchungu, huendelea kuwa mafumbo yasiyo na ufumbuzi, kiasi kwamba mara nyingi
wanadamu huzama katika kukata tamaa.
Wakati huohuo binadamu hubaki kuwa kwake mwenyewe suala lisilo na ufumbuzi,
na analolihisi kwa gizagiza. Maana hakuna anayeweza kuepukana kabisa na
suala hilo la kujihojihoji katika wakati fulani wa maisha yake, na hasa
katika matukio yaliyo mazito zaidi. Mungu peke yake anaweza kutoa jawabu
kamili na timilifu kwa hoja hiyo; Yeye ambaye humwita binadamu kwenye fikra
za juu na kwenye uchunguzi wenye hali ya kunyenyekea.
Dawa kwa ukani Mungu haina budi kutokana na fafanuzi za kufaa za
mafundisho ya Kanisa, na pia kutokana na maisha yake na ya wanajumuiya yake.
Maana ni juu ya Kanisa kuleta uwepo wa Mungu Baba na wa Mwanae aliyetwaa
mwili, na kuudhihirisha. Na litafanya hivyo likijitengeneza upya na
kujirekebisha bila kukoma chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu[25].
Hilo litapatikana kwa ushuhuda wa imani iliyo hai na komavu, yaani imani
ambayo imelelewa vizuri hivi kwamba iweze kuyakabili matatizo kwa upambanuzi
na kuyashinda. Na mashahidi wengi sana walitoa na wanatoa ushuhuda mtukufu
wa imani hiyo. Nayo haina budi kudhihirisha uwezo wake na kuzaa matunda
tele, kwa kupenya mfumo mzima wa maisha ya waamini pia katika harakati zake
za kidunia. Tena kwa kuwasukuma kufuatilia haki na upendo hasa kwa wahitaji.
Kisha, linalochangia kwa vikubwa kuutambua uwepo wa Mungu ndio upendo wa
kidugu kati ya waamini ambao kwa roho moja hushirikiana katika kazi kwa
ajili ya imani ya Injili[26] na
kujidhihirisha kuwa alama ya umoja.
Aidha, ingawa Kanisa linaukataa kabisa ukani Mungu, hata hivyo linatambua
kwa moyo mweupe kwamba wanadamu wote, waamini na wasio waamini, wanapaswa
kuchangia katika ujenzi wa haki wa ulimwengu huu, ambapo wanaishi wote
pamoja. Nalo haliwezi kufanikishwa bila ya mjadala, au dialogia, unaofanyika
kwa moyo mnyofu na kwa busara. Kwa hiyo Kanisa hulaumu ubaguzi kati ya
waamini na wasio waamini, ambao baadhi ya serikali za nchi zinauingiza
pasipo haki. Na sababu yake ni kwamba [serikali hizo] hazitaki kuzitambua
haki zile za msingi za binadamu. Tena Kanisa linadai uhuru wa kweli kwa
waamini, ili waruhusiwe kulijenga pia hekalu la Mungu katika dunia hii. Na
hatimaye linawaalika wakana Mungu wakubali kuizingatia (considerent)
Injili ya Kristo kwa moyo ulio wazi.
Kanisa linajua vizuri kabisa kwamba ujumbe wake huuwiana vema na
matarajio ya siri kabisa ya moyo wa binadamu linapotetea hadhi ya wito wa
binadamu, na hivyo linawarudishia tumaini wale wote waliokata tamaa ya
kwamba kuna kikomo kilicho bora kwa ajili yao. Ujumbe wa Kanisa hauwanyimi
binadamu kitu chochote, bali unaleta mwanga, uzima na uhuru kwa ajili ya
maendeleo yake. Nje ya ujumbe huo hakuna liwezalo kuuridhisha moyo wa
binadamu : “Umetuumba kwa ajili yako, ee Bwana, na moyo wetu hautulii, mpaka
utulie ndani yako”[27].
Kristo, aliye Mtu Mpya
22. Kwa kweli ni katika fumbo la Neno aliyefanyika mwili tu kwamba fumbo
la binadamu linaangazwa. Maana Adamu, mtu wa kwanza, alikuwa mfano wa yule
atakayekuja[28], yaani Kristo
Bwana. Naye Kristo, aliye Adamu mpya, akilifunua fumbo la [Mungu] Baba na la
upendo wake, hudhihirisha kikamilifu kwa binadamu, binadamu alivyo, na
kumjulisha wito wake mkuu. Kwa hiyo, sasa, hakuna la kushangaza ikiwa kweli
zote zilizokwisha elezwa hapo juu hupata chemchemi yake katika Kristo na
[katika Yeye] kukifikia kilele chake.
Naye ndiye “mfano wa Mungu asiyeonekana” (Kol 1:15)[29].
Tena ndiye mtu mkamilifu, aliyewarudishia wana wa Adamu kufanana kwao na
Mungu, yaani ile sura iliyoumbuka tangu awali kwa sababu ya dhambi. Maadam
katika Kristo hali ya kibinadamu imechukuliwa bila kumezwa[30],
basi, vivyo hivyo, hali hiyo imekuzwa hata katika sisi kwenye hadhi iliyo
kuu. Kwa njia ya umwilisho [wake] Mwana wa Mungu amejiunga kwa namna fulani
na kila binadamu. Alifanya kazi kwa mikono ya kibinadamu, alifikiri kwa
akili ya kibinadamu, alitenda kwa utashi wa kibinadamu[31],
na alipenda kwa moyo wa kibinadamu. Akizaliwa na Bikira Maria alijifanya
kweli mmoja kati yetu, akifanana nasi katika yote isipokuwa katika dhambi[32].
Mwanakondoo asiye na kosa, alitustahilisha uzima kwa damu yake aliyoimwaga
kwa hiari; na katika yeye Mungu alitupatanisha naye na kati yetu
[33]
na alitupokonya katika utumwa wa shetani na wa dhambi. Hivyo kila mmoja wetu
anaweza kutamka pamoja na Mtume [Paulo]: Mwana wa Mungu “alinipenda akajitoa
nafsi yake kwa ajili yangu” (Gal 2:20). Akiteswa kwa ajili yetu, alituachia
kielelezo ili tufuate nyayo zake
[34],
na pia alitufungulia njia ili tunapoifuata, uzima na mauti vitakatifuzwe na
kupata maana mpya.
Aidha, mkristo, akiisha fananishwa na sura ya Mwana aliye mzaliwa wa
kwanza miongoni mwa ndugu wengi[35],
hupokea “malimbuko ya Roho” (Rum 8:23), ambayo kwayo huwezeshwa kutimiza
sheria mpya ya upendo[36]. Kwa
njia ya Roho huyo aliye “amana ya urithi wetu” (Efe 1:14), mtu mzima huumbwa
upya kiundani mpaka kufikia “ukombozi wa mwili [wake]” (Rum 8:23): “Ikiwa
Roho wake Yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, Yeye
aliyemfufua Kristo katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya
kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu” (Rum 8:11)[37].
Hakika mkristo anasongwa na haja ya kuupinga ubaya akipitia katika matatizo
mengi, na hatimaye kufa. Lakini akiungana na fumbo la kipasaka na
kushirikishwa kifo cha Kristo ataulaki ufufuko akiimarishwa na tumaini[38].
Jambo hilo haliwahusu wakristo tu bali pia wanadamu wote wenye mapenzi mema,
ambao neema ya Mungu hufanya kazi mioyoni mwao, kwa namna isiyoonekana
[39].
Maana Kristo alikufa kwa ajili ya watu wote
[40]
na wito halisi wa binadamu ndio mmoja, ule wa kimungu. Kwa hiyo lazima tuwe
na wazo kwamba Roho Mtakatifu anawajalia watu wote uwezekano wa kushiriki
fumbo la kipasaka, kwa jinsi anayoijua Mungu.
Fumbo la binadamu ni kuu na la namna ambayo huangazwa machoni pa waamini
kwa njia ya Ufunuo wa kikristo. Kwa njia ya Kristo na katika Kristo hata
fumbo la uchungu na mauti hupata nuru, nalo ambalo pasipo Injili
hutufadhaisha. Kristo amefufuka na kuangamiza mauti kwa mauti yake, naye
ametupatia uzima[41] ili,
tukiwa wana katika Mwana, tulie katika Roho: Aba, yaani, Baba![42].
Sura ya Pili
JUMUIYA YA WANADAMU
Madhumuni ya Mtaguso
23. Mandhari mojawapo ya muhimu zaidi katika ulimwengu wa sasa ni
kuongezeka kwa mawasiliano kati ya watu, nako kunachangiwa kwa vikubwa na
maendeleo ya kiteknolojia ya nyakati zetu. Hata hivyo, mjadala wa kidugu
kati ya wanadamu hautimiliki katika maendeleo hayo, bali kwa undani zaidi
katika jumuiya ya watu. Nayo inadai heshima kati yao na kwa hadhi kamilifu
ya roho [ya kila mtu]. Ufunuo wa kikristo unasaidia sana usitawi wa ushirika
kati ya watu; wakati huohuo unatuongoza kufahamu kwa undani zaidi sheria
zinazoongoza maisha ya kijamii na zilizoandikwa na Muumba katika maumbile ya
kiroho na ya kimaadili ya binadamu.
Hati za Majisterio ya Kanisa zilizotolewa hivi karibuni zilifafanua kwa
upana zaidi mafundisho ya kikristo kuhusu jamii ya kibinadamu
[43].
Kwa sababu hiyo Mtaguso unakumbushia tu baadhi ya kweli zilizo muhimu zaidi
na kueleza misingi yake katika mwanga wa Ufunuo. Aidha, unasisitiza baadhi
ya mambo yanayotokana na kweli hizo, na yaliyo muhimu zaidi kwa nyakati
zetu.
Tabia ya kijumuiya ya wito wa binadamu katika mpango wa Mungu
24. Mungu, mwenye kutunza watu wote kama baba, alitaka wanadamu wote waunde
familia moja na kutendeana [wao kwa wao] kwa roho ya kidugu. Maana, wote
wameumbwa kwa sura ya Mungu ambaye “alifanya kila taifa la wanadamu kutoka
katika mtu mmoja, ili wakae juu ya uso wa nchi yote” (Mdo 17:26); nao huitwa
kwa kikomo kimoja kilekile, yaani Mungu mwenyewe.
Kwa hiyo, upendo wa Mungu na wa jirani ndiyo amri ya kwanza na iliyo kuu
kuliko zote. Maana tunafundishwa na Maandiko Matakatifu ya kuwa upendo wa
Mungu hauwezi kutenganishwa na upendo wa jirani. “Na amri nyingine yoyote
inajumlishwa katika neno hili: Mpende jirani yako kama nafsi yako. Kwa hiyo,
utimilifu wa sheria ndio upendo” (Rum 13:9-10; taz. 1Yoh 4:20). Na jambo
hilo lajidhihirisha kuwa la muhimu sana kwa wanadamu wanaozidi kutegemezana
wao kwa wao; tena kwa ulimwengu unaozidi kuunganika siku baada ya siku.
Zaidi, Bwana Yesu akimwomba Baba ili “wote wawe na umoja, kama sisi nasi
tulivyo umoja” (Yn 17:21-22) anatuwekea upeo mpya uliofumbika kwa akili ya
binadamu. Na papo hapo anatudokezea ufanano kati ya umoja wa nafsi [tatu] za
Mungu na umoja wa wana wa Mungu katika ukweli na upendo. Ufanano huo
unadhihirisha kuwa binadamu, ambaye hapa duniani ni kiumbe pekee alichotaka
Mungu kwa ajili yake chenyewe, hawezi kuvumbua kikamilifu ukweli wake,
isipokuwa kwa kujitolea mwenyewe kwa moyo mweupe[44].
Kutegemezana baina ya mtu na jamii
25. Tabia ya kijamii ya binadamu huonyesha kuwa kukamilishwa kwa ubinadamu
na maendeleo ya jamii yenyewe vinategemezana. Hivyo binadamu, kwa vile ni
yeye ambaye kwa maumbile yake huhitaji sana maisha ya kijamii, ndiye yeye,
na lazima awe yeye, msingi, kiini na lengo la taasisi zote za kijamii
[45].
Maadamu maisha ya kijamii si kitu kilicho nje ya mtu, basi binadamu hukua
katika vipawa vyake vyote na kuweza kuuitikia wito wake kwa mawasiliano na
wenzake, kwa kutimiza wajibu zake kwa ajili ya wengine, na kwa mjadala wa
kindugu.
Kati ya miungano ya kijamii inayokusaidia kukamilishwa kwa binadamu,
mingine, kama vile familia na jamii ya kisiasa, inalingana moja kwa moja na
tabia ya ndani ya mtu. Mingine tena inatokana zaidi na utashi wake ulio
huru. Katika nyakati zetu hizi kuwasiliana na kutegemezana kati ya watu
kunaongezeka kwa sababu nyingi; na kutokana na kuongezeka huko vyama na
taasisi mbalimbali huundwa, viwe vya kijamii ama vya kibinafsi (
sive
publici sive privati iuris). Tendo hilo, liitwalo “ujamiisho” (
socializatio),
halina budi kuandamana na hatari zake, lakini pia linaleta manufaa mengi
katika kuimarisha na kukuza vipaji vya binadamu na katika kutetea haki zake
[46].
Kwa hiyo basi, watu wanapewa mambo mengi kutokana na maisha haya ya
kijamii ili kuutimiliza wito wao, hata wa kidini. lakini, kwa upande
mwingine, haipingiki kwamba mara nyingi wanadamu wanapotoshwa katika kutenda
mema na kusukumwa kutenda mabaya kutokana na mazingira yenyewe ya kijamii
wanamoishi na kuzoea tangu utotoni. Ni yakini kwamba machafuko yanayozuka
mara kwa mara katika utaratibu wa kijamii husababishwa kwa kiasi fulani na
mivutano itokanayo na mifumo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Lakini kwa
undani zaidi machafuko haya asili yake ni katika kiburi na ubinafsi wa
binadamu, vinavyoathiri mazingira ya kijamii. Na pale ambapo utaratibu wa
mambo huharibiwa kwa matokeo ya dhambi, ndipo binadamu, anayeuelekea ubaya
tangu kuzaliwa kwake, hupata misukumo mipya ya kutenda dhambi. Nayo haiwezi
kushindwa bila ya bidii nyingi na pasipo msaada wa neema [ya Mungu].
Kustawisha manufaa ya wote
26. Kutegemezana [kati ya watu] kunazidi kuwaunganisha wanadamu na kuenea
polepole ulimwenguni kote. Hivyo hutokea kwamba manufaa ya wote – yaani
ujumla wa hali za maisha ya kijamii zinazowawezesha watu, au kama makundi,
au kama mtu mmoja mmoja, kufikia utimilifu wao kikamilifu na upesi zaidi –
yanazidi kuwahusisha watu wa dunia nzima mintarafu haki na wajibu kwa
wanadamu wote. Kwa sababu hiyo, kila kundi lazima lizingatie mahitaji na
matarajio ya makundi mengine na pia manufaa ya wote katika familia nzima ya
kibinadamu
[47].
Wakati huohuo watu wanazidi kuelewa hadhi kuu ya utu wa binadamu, aliye
mkubwa kuliko vitu vyote na ambaye wajibu na haki zake zinawahusu wote na
haziwezi kuvunjwa. Kwa hiyo, inabidi binadamu aweze kuvipata vitu vyote vile
vinavyohitajika ili kuendesha maisha yaistahiliyo hadhi yake ya kibinadamu,
kama vile chakula, nguo, makazi, haki ya kujichagulia kwa uhuru hali ya
maisha, ya kuunda familia, ya kupata elimu, kazi, sifa nzuri, heshima, ujuzi
wa habari unaotakiwa, uwezo wa kutenda kadiri ya mwongozo mnyofu utokanao na
dhamiri yake; kisha haki ya kulinda maisha ya binafsi na kuishi katika uhuru
ulio na haki pia katika masuala ya dini.
Kwa hiyo, mfumo wa kijamii na maendeleo yake havina budi kuyapa kipaumbele
manufaa ya watu. Maana katika kuyaratibu mambo lazima kuyalinganisha na
utaratibu wa watu, wala si kinyume chake. Na ndivyo alivyoelekeza Bwana
mwenyewe aliposema kuwa sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si
mwanadamu kwa ajili ya sabato
[48].
Basi utaratibu huo unadaiwa kuendelezwa zaidi na zaidi, kuasisiwa katika
ukweli, kutekelezwa katika haki; tena lazima uhuishwe na upendo, na
kurekebishwa ili uzidi kuuwiana zaidi na zaidi na hali ya kibinadamu katika
uhuru
[49]. Ili kulifikia lengo
hilo yapasa kuanzisha matengenezo ya fikira na mageuzo ya ndani ya jamii.
Roho wa Mungu ambaye, kwa maongozi ya ajabu, huongoza mwenendo wa nyakati
na kutengeneza upya uso wa dunia, anasimamia maendeleo hayo. Basi, chachu ya
Injili ilichochea na inaendelea kuchochea kiu hii isiyozimika ya heshima
[kwa binadamu].
Heshima kwa binadamu
27. Mtaguso ukiyazingatia yale yanayotokana na mawazo hayo na yahitajiyo
kukabiliwa upesi zaidi, unakazia sana ile heshima kwa binadamu, ili kwamba
kila mmoja amwone jirani yake, bila kubagua, kama “nafsi yake” nyingine. Na
afanye hivyo akizingatia maisha yake na njia za kuyaishi inavyostahili
[50].
Wala asimwige yule tajiri ambaye hakumshughulikia katu Lazaro aliyekuwa
maskini
[51].
Siku za leo hasa linatusonga sharti la kujifanya jirani wa kila binadamu na
la kutoa huduma kimatendo kwa yule anayepita karibu nasi. [Na ndivyo
tutakavyomtendea kila mhitaji], awe mzee aliyeachwa na wote au mfanyakazi
mgeni anayedharauliwa pasipo haki, au mhamiaji, au mtoto aliyezaliwa na
ujamiano usio halali na ambaye anateswa bila kustahili kwa dhambi ambayo
hakuitenda mwenyewe; kisha awe mwenye njaa anayehoji dhamiri yetu
akikumbushia sauti ya Bwana isemayo: “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao
ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” (Mt 25:40).
Aidha, kila tendo linalodhuru uhai wenyewe ndiyo aibu kabisa kama vile
kila aina ya uuaji: uuaji wa kabila zima, utoaji mimba, euthanasia au uuaji
wa mtu asiyeweza kuponywa, na pia kujiua makusudi. [Tena ni aibu] matendo
yote yanayoathiri uzima wa mtu kama vile kutia vilema, kutesa kimwili na
kiakili, bidii ya kugandamiza dhidi ya roho ya mtu. [Kisha ni aibu] kila
tendo linalovunja heshima ya kibinadamu kama vile hali zile za maisha
zisizostahili kwa mtu, [kwa mfano] kufungwa bila hukumu, kuhamishwa, utumwa,
ukahaba, uuzaji wa wanawake na vijana; tena hali nyonge ya kazi
inayosababisha wafanyakazi watazamwe kama vyombo viletavyo faida tu, wala si
kama watu walio huru na wawajibikaji. Haya yote na mengine yanayofanana na
hayo huuchafua ustaarabu wa kibinadamu na hasa huwaharibu wenye kuyatenda
kuliko wale wenye kuteswa nayo. Kisha huipinga heshima ya Muumba.
Heshima na upendo kwa maadui
28. Heshima na upendo ni lazima viwafikie pia wale wenye kufikiri au
kutenda tofauti na sisi katika masuala ya kijamii, kisiasa, na hata ya dini.
Maana kadiri tutakavyozidi kupenya katika namna zao za kufikiri, kwa ukarimu
na upendo mkubwa, ndivyo tutakavyofanikiwa kirahisi kuingia katika mijadala
nao.
Ni kweli kwamba upendo na ukarimu wa namna hii hauwezi kutufanya kwa
vyovyote tusiujali ukweli na wema. Naam, ni upendo wenyewe unaowasukuma
wafuasi wa Kristo wawatangazie watu wote ukweli wenye kukomboa. Lakini
lazima kupambanua baina ya kosa, ambalo daima hukataliwa, na mwenye kukosa
ambaye daima hushika hadhi ya kiutu hata pale anapochafuliwa na mawazo
madanganyifu na yasiyo kamili kuhusu dini
[52].
Mungu peke yake ndiye hakimu na mwenye kuichunguza mioyo; kwa hiyo
anatukataza kuhukumu hatia ya ndani ya mtu yeyote
[53].
Mafundisho ya Kristo yanatudai sisi tuyasamehe pia matukano[54],
na yanawahusisha katika amri ya upendo maadui wote. Amri hiyo ndiyo amri ya
sheria mpya, “Mmesikia kwamba imenenwa: Umpende jirani yako, na umchukie
adui yako. Lakini mimi nawaambia: Wapendeni adui zenu, watendeeni mema
wanaowachukia; waombeeni wanaowaudhi na kuwasengenya” (Mt 5:43-44).
Usawa wa msingi kati ya wanadamu wote, na haki ya kijamii
29. Wanadamu wote wamejaliwa nafsi yenye akili na wameumbwa kwa sura ya
Mungu; tena wanashiriki maumbile yaleyale na asili ileile; nao, wakiisha
kombolewa na Kristo, wanafurahia wito uleule na kikomo kilekile. Kwa hiyo
basi, ni sharti kuzidi kuutambua usawa wa msingi kati ya watu wote.
Kwa kweli watu wote si sawa kufuatana na uwezo mbalimbali wa kimwili na
tofauti za nguvu, za akili na kimaadili. Lakini hata hivyo kila mtindo wa
ubaguzi katika haki za msingi za binadamu – uwe katika uwanja wa kijamii au
wa kitamaduni, kuhusu jinsia, kabila, rangi, hali ya kijamii, lugha au dini
– lazima uachwe na kung’olewa kama kinyume cha mpango wa Mungu. Kweli,
yatupasa kusikitika kwa kuwa haki zile za msingi za binadamu hazijapata
kuheshimiwa mahali pote. Kwa mfano mwanamke anaponyimwa fursa ya kuchagua
kwa uhuru mume wake, au kuambata hali fulani ya maisha, au tena kuwahi
katika elimu na utamaduni unaokubaliwa kwa mwanamume tu.
Licha ya hayo, ingawa kati ya wanadamu zipo tofauti zenye haki, hata
hivyo usawa wao wa hadhi kama binadamu wataka tupiganie hali ya maisha iliyo
ya haki na ya kiutu zaidi. Maana kuwepo kwa tofauti nyingi mno za kiuchumi
na kijamii kati ya wanajamii na kati ya mataifa ya familia iliyo moja ya
kibinadamu kunaleta taksiri, au kikwazo. Nako kunaipinga haki ya kijamii,
usawa na hadhi ya binadamu, kadhalika amani ya kijamii na kimataifa.
Taasisi za kibinadamu, ziwe za binafsi ama za umma, zifanye juhudi ili
zipate kuitumikia hadhi ya binadamu na kikomo chake. Na wakati huohuo
zikinze kwa ujasiri kila mtindo wa utumikishaji wa kijamii na wa kisiasa, na
pia zizitetee haki za msingi za wanadamu walio chini ya dola yoyote ile.
Zaidi, taasisi hizi hupaswa polepole kujilinganisha na ile hali ya kiroho
iliyo juu kuliko mambo mengine yote, ijapo pengine zitachukua muda mrefu
kulifikia lengo linalotarajiwa.
Ulazima wa kuishinda tabia ya kibinafsi
30. Hatua za mabadiliko ni za kina na za haraka kiasi kwamba zinadai kwa
upesi zaidi asiwepo mtu awaye yote ambaye, akiufumbia macho mkondo wa
matukio na kutoujali kwa uvivu, anashikilia tabia ya kibinafsi tu. Wajibu wa
haki na upendo utazidi kutimizwa ikiwa kila mmoja atatoa mchango wake kwa
ajili ya manufaa ya wote, kulingana na uwezo wake ya mahitaji ya wengine. Na
hivyo, atazihamasisha na kuzisaidia pia taasisi za umma na za binafsi
zilizopo kwa minajili ya kukuza hali za maisha ya wanadamu. Wapo watu ambao,
ingawa wanakiri mawazo mapana na yaliyojaa ukarimu, lakini kimatendo huishi
daima kama wasingejali kabisa mahitaji ya jamii. Zaidi, walio wengi katika
nchi mbalimbali wanapuuzia sheria na maagizo ya kijamii. Wasio wachache tena
hawaoni aibu kuepa zile kodi zilizo halali – kwa mbinu mbalimbali za
udanganyifu na ulaghai – au masharti mengine ya kijamii. Hatimaye, wengine
hawazingatii kanuni kadhaa za maisha ya kijamii kama vile zile zilizowekwa
kwa afya ya wote, au zinazoratibisha uendeshaji wa magari. [Kwa kufanya
hivyo] hawaelewi kuwa wanahatarisha maisha yao wenyewe na ya wengine kwa
uzembe wao.
Ni tendo takatifu kwa wote kuyaingiza masharti ya kijamii katika wajibu
zilizo muhimu zaidi za mtu wa kisasa, na kuzitimiza. Maana, kadiri ulimwengu
unavyozidi kuunganika, vivyo hivyo ni wazi kuwa masharti ya wanadamu
yanavuka mipaka ya makundi mbalimbali na kuenea polepole ulimwenguni kote.
Na jambo hilo haliwezekani ikiwa watu binafsi na makundi yao hawashughulikii
ndani yao usitawi wa fadhila za kimaadili na za kijamii na kuzishamirisha
katika ujamii. Nalo lilenge katika kujitokeza kwa kizazi kipya cha wanadamu
wenye kujenga ubinadamu mpya, kwa msaada ulio wa lazima wa neema ya kimungu.
Uwajibikaji na ushirikiano
31. Ili kila mtu apate kuutimiza kwa bidii zaidi wajibu wa dhamiri yake (
conscientiae
officium) mbele yake mwenyewe na mbele ya makundi mbalimbali ambapo
anashiriki, basi lazima kila mmoja alelewe kwa makini na kuelekezwa katika
nafsi yake kwenye uwanja wa ustaarabu ulio mpana zaidi. [Kwa kusudi hilo]
vitumiwe vyombo vile vingi vinavyopatikana siku za leo kwa binadamu. Awali
ya yote, mfumo wa malezi ya vijana wanaotoka katika kila tabaka la kijamii
hauna budi kulenga katika kuandaa wanaume na wanawake si zaidi wenye elimu
ya juu sana bali hasa walio imara katika utu wao, kama inavyodaiwa kwa nguvu
na nyakati zetu.
Lakini binadamu anaifikia hisia hii ya uwajibikaji kwa shida, kama hali za
maisha hazimwezeshi kuitambua hadhi yake na kuuitikia wito wake katika
huduma ya Mungu na ya wengine. Kwa kweli mara nyingi uhuru wa binadamu
unadhoofishwa iwapo binadamu anakabiliana na umaskini mtupu. Vilevile yeye
naye hudunishwa anapokubali kuishi maisha ya raha mno na hivyo kujifungia
katika upweke unaojitosheleza. Kinyume chake, [uhuru wa binadamu] unaimarika
wakati mtu anapokubali kupambana na magumu yasiyoepukika ya maisha ya
kijamii; tena anapokidhi madai yaliyo mengi ya maisha ya pamoja, kisha
anapojihusisha kuitumikia jumuiya ya watu.
Kwa hiyo ni lazima kuamsha utashi wa wote ili wachukue nafasi zao katika
shughuli za pamoja; Aidha ni lazima kuisifu mifumo ile ya mataifa ambayo
huruhusu wengi wa raia wao kushiriki katika uongozi wa maisha ya umma katika
hali ya uhuru kamili. Hata hivyo haina budi kuzingatiwa hali halisi ya kila
taifa na uimara wa lazima wa madaraka ya kiserikali. Aidha, ili raia wote
waweze kukubali kushiriki maisha ya makundi mbalimbali yanayoiunda jamii,
basi ni lazima wapate katika makundi hayo mambo mema yawezayo kuvutia na ya
kuwaweka tayari kuwatumikia wengine. Kwa hiyo ni halali kudhani kwamba siku
zijazo za binadamu zimo mikononi mwa wale walio na uwezo wa kuvipa vizazi
vijavyo sababu za kuishi na za kutumaini.
Neno aliyefanyika mwili na mshikamano wa binadamu
32. Kama vile Mungu alivyowaumba wanadamu si kusudi waishi kama watu
binafsi, bali wawekwe ili kuunda umoja wa kijamii, vivyo hivyo “ilimpendeza
Mungu kuwatakatifuza na kuwaokoa watu, sio mmoja mmoja na pasipo muungano
kati yao, bali kwa kuwaunda kama taifa moja lenye kumjua katika ukweli na
kumtumikia kitakatifu”[55].
Tangu mwanzo wa historia ya wokovu Mungu mwenyewe aliwateua watu si kama
watu binafsi tu, bali pia kama wana wa jumuiya fulani. Maana Mungu, akifunua
azimio lake, akawaita wateule hawa “watu wake” (Kut 3:7-12) ambao alifunga
Agano nao katika mlima Sinai[56].
Tabia hii ya kijumuiya imekamilishwa na kutimizwa na kazi ya Yesu Kristo.
Neno wa Mungu mwenyewe aliyefanyika mwili alitaka kushiriki katika umoja wa
wanadamu. Alihudhuria arusi ya Kana, akaingia nyumbani mwake Zakayo, akala
pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi. Alifunua upendo wa Baba na wito
bora wa wanadamu akiyazingatia masuala ya kawaida zaidi ya maisha ya kijamii
na kutumia lugha na mifano ya maisha ya kila siku. Aliyatakatifuza mahusiano
kati ya wanadamu, na kabla ya yote yale ya kifamilia, ambayo katika hayo
hutoka mahusiano ya kijamii; kwa hiari alizitii sheria za taifa lake.
Alitaka kuishi maisha ya mfanyakazi wa nyakati zake na ya nchi yake.
Tena katika kuhubiri kwake aliwaamuru wazi wana wa Mungu wazingatiane wao
kwa wao kama ndugu. Katika sala yake akaomba wanafunzi wake wote wawe “kitu
kimoja”. Zaidi, Yeye mwenyewe alijitoa kwa ajili ya watu wote hata mauti,
akiwa Mkombozi wa wote. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu
kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yn 15:13). Aidha, akawaamuru
Mitume watangaze habari ya Injili kwa mataifa yote, ili wanadamu wapate kuwa
familia ya Mungu, ambapo utimilifu wa sheria utakuwa upendo.
Mzaliwa wa kwanza kati ya ndugu wengi, baada ya kifo na ufufuko wake aliunda
kwa paji la Roho wake jumuiya mpya ya kidugu kati ya wale wote wanaompokea
kwa imani na upendo. Nayo ndiyo jumuiya ya Mwili wake, yaani Kanisa, ambamo
washirika wake kama viungo wahudumiane wao kwa wao kadiri ya vipawa
mbalimbali walivyojaliwa.
Na mshikamano huu ni lazima uwe unakuzwa zaidi na zaidi hata kufikia siku
ya kutimilizwa kwake. Hapo ndipo ambapo wanadamu, wakishaokolewa kwa neema,
watampa Mungu utukufu uliokamilika, kama familia iliyopendwa naye, pia na
Kristo aliye ndugu yao.
Sura ya Tatu
UTENDAJI WA BINADAMU ULIMWENGUNI
Kuwekwa kwa suala
33. Kwa njia ya kazi na maarifa yake binadamu daima amefanya bidii ili
kuyaendeleza maisha yake. Aidha, leo, hasa kwa msaada wa sayansi na
teknolojia, amepanua na anaendelea kuupanua utawala wake karibu juu ya
ulimwengu mzima. Tena, hasa kwa msaada wa ongezeko la njia mbalimbali za
mawasiliano kati ya mataifa, familia ya wanadamu imeifikia polepole hatua ya
kujitambua na kujitengeneza kama jumuiya moja katika dunia nzima. Matokeo
yake ni kwamba sasa binadamu kwa maarifa na nguvu zake tu hujipatia vitu
vingi ambavyo hapo zamani alikuwa akivingojea kutoka nguvu za juu.
Mbele ya bidii hii kubwa sana ambayo siku hizi inawasukuma watu wote,
masuala mengi yanajitokeza kati ya wanadamu. Je, maana na thamani ya kazi ya
binadamu ni ipi? Je, tuvitumieje vitu hivi vyote? Je, hizi juhudi za watu
binafsi na za umma zinalenga wapi? Kanisa linahifadhi hazina ya Neno la
Mungu na kuchota miongozo ndani yake kwa taratibu za kimaadili na za kidini.
Lakini si mara zote Kanisa linalo jibu lililo tayari kwa masuala yote; hivyo
linatamani kuunganisha mwanga wa Ufunuo pamoja na mang’amuzi ya watu wote
kusudi liangaze njia ambayo wanadamu wameiingia hivi karibuni.
Thamani ya utendaji wa binadamu
34. Jambo hili ni la hakika kwa waamini: utendaji wa binadamu, wa binafsi
na wa pamoja, ukitazamwa kwa wenyewe hulingana na azimio la Mungu. Nao ndio
ile bidii kubwa ambayo kwayo wanadamu katika mfululizo wa karne hufanya
juhudi ili kuboresha hali ya maisha yao. Maana binadamu, aliyeumbwa kwa sura
ya Mungu, alipewa amri ili aitiishe dunia na vyote viijazavyo na kuutawala
ulimwengu katika haki na utakatifu[57].
Kadhalika, aliamriwa kumrejea Mungu mwenyewe na kuurudisha ulimwengu mzima
kwake, akimtambua Yeye kama Muumba wa viumbe vyote ili kwamba kwa njia ya
utawala wa binadamu juu ya viumbe vyote, jina la Mungu litukuzwe duniani
kote[58].
Jambo hili linazihusu pia kazi za kila siku. Maana wanaume kwa wanawake
hupata mahitaji kwa ajili yao na ya familia wakifanya kazi, na hivyo pia
hutoa huduma ifaayo kwa jamii. Nao huweza kwa haki kufikiri kwamba kwa kazi
yao huendeleza kazi ya Muumba, hutoa huduma kwa ndugu zao, pamoja na mchango
wa kila mmoja ili kutimiliza mpango wa Mungu katika historia
[59].
Kwa hiyo wakristo hawapinganishi kabisa matokeo ya maarifa na uwezo wa
binadamu dhidi ya uweza wa Mungu, kana kwamba kiumbe chenye akili kingekuwa
mshindani wa Muumba. Bali kinyume chake [wakristo] husadiki kuwa ushindi wa
binadamu ni alama ya ukuu wa Mungu na tunda la mpango wake wa ajabu. Na
kadiri uwezo wa wanadamu unavyozidi kukua, ndivyo uwajibikaji wao wa binafsi
na wa pamoja unavyozidi kupanuka. Tokea hapo huonekana kwamba ujumbe wa
kikristo, mbali na kuwatoa wanadamu katika wajibu wao wa kuijenga dunia,
tena mbali na kuwahimiza kutojali manufaa ya wenzao, huwahusisha na hayo
yote kwa sharti linalowafungamanisha zaidi[60].
Utaratibu wa utendaji wa binadamu
35. Kwa kweli utendaji wa binadamu, kama vile unavyotokana na binadamu,
vivyo hivyo hulenga katika binadamu. Maana binadamu anapofanya kazi
hatengenezi tu mambo na jamii, bali pia hujikamilisha mwenyewe. Anajifunza
mengi, anakuza uwezo wake, anasukumwa kutoka katika ubinafsi wake, na
kuongeza kipawa chake. Maendeleo hayo, yakieleweka vizuri, yana thamani
kubwa kuliko utajiri wa nje unaoweza kulimbikizwa. Binadamu thamani yake ni
alivyo, kuliko alivyo navyo
[61].
Hali kadhalika yale yote wayatendayo wanadamu ili kupata haki iliyo kubwa
zaidi, udugu ulio mpana zaidi, na mfumo wa mahusiano ya kijamii yaliyo ya
kiutu zaidi, haya yana thamani kubwa kuliko maendeleo ya kiteknolojia. Nayo
maendeleo ya kiteknolojia yatupatia dutu (
materiam) kwa maendeleo ya
binadamu, lakini peke yake hayawezi kwa namna yoyote kuyatimiliza [maendeleo
ya binadamu].
Hii ndiyo kanuni ya utendaji wa kibinadamu: kwamba utendaji huo ulingane
na manufaa halisi ya wanadamu, kadiri ya mpango wa Mungu na mapenzi yake;
tena umwezeshe kila binadamu kama mtu binafsi na kama mshirika wa jamii
kuusitawisha na kuutekeleza wito wake kikamilifu.
Uhalali wa kujiratibisha kwa mambo ya dunia
36. Watu wengi wa siku hizi wanaonekana kuhofia kwamba, kama mahusiano kati
ya utendaji wa binadamu na dini yanafungamamishwa mno, uwezekano wa
kujitawala wa binadamu, jamii na sayansi utazuiliwa.
Pengine tunaweza kuelewa kwamba “[tendo la] kujiratibisha kwa mambo ya
dunia” (
terrenarum rerum autonomiam) lina msingi kwamba vitu
vilivyoumbwa pamoja na jamii zenyewe vina sheria na tunu zake; na binadamu
anapaswa polepole kuzivumbua tunu hizo, kuzitumia na kuzipanga. Ikiwa
tutaelewa hivyo, basi tendo hilo ni dai lililo halali. Tena dai hilo
halitakiwi tu na wanadamu wa nyakati zetu, bali linalingana na mapenzi yake
Muumba. Maana ni kwa nguvu yenyewe ya kuumbwa kwao, kwamba viumbe vyote
vinapata uthabiti wao wa pekee, ukweli na wema wao pamoja na sheria na
utaratibu wao. Mwanadamu apaswa kuyaheshimu hayo yote kwa kuzitambua mbinu
mahususi za kila sayansi na ufundi. Kwa hiyo, utafiti wenye mpango
ukifanyika katika nyanja mbalimbali za ujuzi, hautapingana kweli na imani,
kama ukifanyika kweli kisayansi na kufuata taratibu za kimaadili. Maana
mambo ya kidunia na yale ya kiimani, asili yake ni katika Mungu yuleyule
[62].
Tena yule ajibidishaye kuzichunguza siri za mambo kwa unyenyekevu na saburi,
hata asipojua, mkono wa Mungu ndio unaomwongoza. Maana Mungu ndiye
anayevitunza vitu vyote na kuvifanya viwe kama vilivyo. Tupate hapa nafasi
ya kulaumu namna kadhaa za fikra, ambazo pengine hazikosekani hata kati ya
wakristo, zinazotokana na kutokueleweka kwa kutosha uhalali wa sayansi
kuzifuata kanuni zake. Fikra hizo zimezua mapingano, mabishano na kuwavuta
wengi mpaka wakafikia hatua ya kudhani kwamba sayansi na imani vinapingana
kati yake
[63].
Lakini, ikiwa kwa usemi “tendo la kujiratibisha kwa mambo ya dunia”
inaeleweka kuwa vitu vilivyoumbwa havimtegemei Mungu, tena kuwa binadamu
huweza kuvitumia bila ya kuvielekeza kwa Muumba, [basi ikieleweka hivyo,]
wale wote wenye kumwamini Mungu wanahisi jinsi kauli hizo zilivyo za
udanganyifu. Maana kiumbe bila Muumba hutoweka. Kwa vyovyote, wote wenye
kuamini dini yoyote ile, wamegundua daima sauti ya Mungu na ufunuo wake
katika lugha za viumbe. Zaidi, kwa kumsahau Mungu, kiumbe chenyewe kinatiwa
giza.
Utendaji wa binadamu ulioharibiwa na dhambi
37. Maandiko Matakatifu, ambayo mang’amuzi ya karne nyingi hupatana nayo,
yanawafundisha watu kuwa, ijapo maendeleo yao ni kitu chema sana kwa
binadamu, huleta kishawishi kikubwa ndani yake. Maana mpangilio wa tunu [za
binadamu] (
ordine valorum) umevurugwa, ubaya na wema
vimechanganyikana, watu binafsi na makundi mbalimbali wanazingatia mambo yao
wenyewe tu, wala si yale ya wengine. Hivyo dunia inakoma kuwa mahali pa
mahusiano ya kidugu, wakati ambapo kuongezeka kwa uwezo wa kibinadamu
kunatishia kuangamiza watu wote.
Maana historia yote ya binadamu imejaa mapambano magumu dhidi ya nguvu za
giza. Mapambano haya yalianza tangu mwanzo wa dunia, nayo yataendelea,
asemavyo Bwana, mpaka siku ya mwisho
[64].
Binadamu, akiwa katika vita hivi, lazima apambane bila kukoma ili aweze
kuambatana na mema; wala hataweza kuufikia umoja wake wa ndani, bila juhudi
kubwa, pamoja na msaada wa neema ya Mungu.
Kwa sababu hiyo Kanisa la Kristo, likiutegemea mpango wa Muumba, linakubali
kuwa maendeleo ya kibinadamu yanaweza kuisaidia heri halisi ya wanadamu.
Lakini wakati huohuo halina budi kuyatangaza maneno ya Mtume [Paulo]:
“Msitake kuifuatisha namna ya dunia hii” (Rum 12:2), yaani ile roho ya
ubatili na ya uovu inayopotosha utendaji wa binadamu uliolengwa katika
utumishi wa Mungu na wa mtu, kuwa chombo cha dhambi.
Kama mtu angalituuliza, “Je, ni kwa njia gani hali hii duni ingeweza
kushindwa?” Wakristo tungejibu kuwa utendaji wote wa kibinadamu,
unaohatarishwa kila siku na kiburi na kujipenda kusiko na utaratibu, lazima
usafishwe na kukamilishwa kwa njia ya msalaba na ufufuko wa Kristo. Maana
binadamu, akishaokolewa na Kristo na kuwa kiumbe kipya katika Roho
Mtakatifu, anaweza na anapaswa kuvipenda pia vitu vile alivyoviumba Mungu.
Anavipata kutoka kwa Mungu, anavitazama na kuviheshimu kana kwamba vinatoka
wakati huohuo mikononi mwa Mungu. Anamshukuru [Mungu] Mhisani kwa hivyo; na
akivitumia na kuvifurahia viumbe hivi katika ufukara na uhuru wa kiroho,
huingizwa katika utawala wa ulimwengu kana kwamba ni mtu asiye na kitu, bali
yu mwenye vitu vyote[65]:
“Maana vyote ni vyenu: nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu” (1Kor
3:22-23).
Utendaji wa binadamu hufikishwa katika ukamilifu wake kwenye fumbo la
Pasaka
38. Neno wa Mungu, ambaye kwa njia yake vitu vyote viliumbwa, aliutwaa
mwili Yeye mwenyewe, akaja kukaa katika dunia ya wanadamu[66],
akaingia katika historia ya ulimwengu kama binadamu kamili, na akaichukua na
kuijumlisha ndani yake[67].
Naye hutufunulia kuwa “Mungu ndiye upendo” (1Yoh 4:8) na hutufundisha kuwa
sheria ya msingi ya utimilifu wa binadamu, na pia ya mageuzo ya ulimwengu,
ndiyo amri mpya ya upendo. Kwa hiyo wale wote wanaouamini upendo wa Mungu,
wanahakikishiwa naye kuwa njia ya upendo imewekwa wazi kwa watu wote. Tena
wanathibitishwa kwamba juhudi zinazokusudia kutimiza udugu wa wote, si za
bure. Vilevile [Neno wa Mungu] anatuhimiza tusienende kwenye njia ya upendo
katika mambo makubwa tu, bali hasa katika mazingira ya kawaida ya maisha.
Akiyastahimili mauti kwa ajili yetu sisi sote wenye dhambi[68],
hutufundisha kwa mfano wake kuwa tunapaswa pia kubeba msalaba. Huo ndio ule
msalaba ambao mwili na ulimwengu (caro et mundus) huwatwisha mabegani
mwao wote watafutao amani na haki. Kwa njia ya ufufuko wake aliwekwa kuwa
Bwana, Yeye aliye Kristo, na akapewa mamlaka yote duniani na mbinguni[69].
Naye anaendelea kufanya kazi hadi leo mioyoni mwa wanadamu kwa nguvu ya Roho
wake, si kwa kuamsha tu ari ya ulimwengu ujao, bali pia kwa kuhamasisha,
kusafisha, na kuimarisha matarajio mema. Ni kwa njia ya matarajio hayo
kwamba familia ya wanadamu inajitahidi kuyafanya maisha yake yawe ya kiutu
zaidi na kuitiisha dunia nzima kwa kusudi hilo. Lakini vipawa vya Roho ni
vya aina nyingi: watu wengine anawaita kutoa ushuhuda wazi wa makao ya
mbinguni kwa njia ya hamu yao [ya kutaka kufika huko]. Kwa njia hiyo
wataifanya [hamu hiyo] iendelee kuwa hai kati ya wanadamu. Tena wengine
anawaita kujitoa kwa utumishi wa wanadamu hapa duniani ili kwamba kwa huduma
hiyo wapate kuzitayarisha njia za ufalme wa mbinguni. Lakini Roho Mtakatifu
huwafanya wote wawe watu huru, wenye kukataa ubinafsi na kuzishirikisha
nguvu zote za kidunia katika maisha ya kibinadamu. Hivyo [nao] wataweza
kujielekeza kwenye maisha yajayo ambapo watu wote watapata kuwa sadaka
inayokubalika kwa Mungu[70].
Bwana amewaachia wafuasi wake amana ya tumaini hilo na chakula cha safari
katika sakramenti ile ya imani ambayo ndani yake vitu vya kawaida
vinavyolimwa na binadamu hugeuzwa kuwa Mwili na Damu yake tukufu. Hiyo ndiyo
karamu ya ushirika wa kidugu na kama onjo la karamu ya mbinguni.
Dunia mpya na mbingu mpya
39. Sisi hatujui wakati wa utimilifu wa dunia na wa ubinadamu
[71],
wala hatujui jinsi ulimwengu utakavyobadilika. Sura ya ulimwengu huu
ulioharibiwa na dhambi inapita
[72].
Lakini twafundishwa [toka katika ufufuo] kuwa Mungu anatayarisha makao mapya
na dunia mpya itakamotawala haki
[73],
na ambamo heri yake itashibisha na kupita tamaa zote za amani ziibukazo
mioyoni mwa watu
[74]. Hapo
ndipo mauti itakaposhindwa, wana wa Mungu watafufuliwa katika Kristo, na
kile kilichopandwa katika udhaifu na uharibifu kitaivaa hali ya kutokufa
[75].
Upendo na matunda yake ndivyo vitakavyobaki
[76],
na mambo yote yaliyoumbwa na Mungu kwa ajili ya binadamu yataokolewa na
utumwa wa ubatili
[77].
Bila shaka tunaonywa kuwa hakuna linalomfaa mtu, ikiwa anaupata ulimwengu
wote, lakini anajipoteza mwenyewe
[78].
Hata hivyo kungojea dunia mpya, mbali na kuidhoofisha juhudi katika kazi
inayoihusu dunia ya sasa, huichochea; mwili wa familia mpya ya wanadamu
hukua, ambao tayari unaweza kutoa sura ambayo ni kivuli cha ulimwengu mpya.
Kwa sababu hiyo, ni lazima kutofautisha kwa makini maendeleo ya kidunia na
ongezeko la Ufalme wa Kristo. Hata hivyo maendeleo hayo yana umuhimu mkubwa
kwa Ufalme wa Mungu
[79], kwa
kadiri yanavyoweza kuchangia kuratibisha vizuri zaidi jamii ya kibinadamu.
Maana, baada ya sisi kueneza duniani [kote] matunda yote mema ya maumbile
na utendaji wetu – yaani hadhi ya binadamu, udugu na uhuru – katika Roho wa
Bwana na kadiri ya amri yake, basi tutayapata tena baadaye yakiwa sasa
yameshafishwa na kila doa, yameng’arishwa na yamegeuzwa, Kristo
atakapomkabidhi Baba Ufalme wa milele na wa ulimwengu mzima: “ambao ni
ufalme wa ukweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki,
mapendo na amani”[80]. Basi,
hapa duniani Ufalme huo tayari upo katika fumbo; lakini katika ujio wa Bwana
utaufikia utimilifu wake.
Sura ya Nne
UTUME WA KANISA KATIKA ULIMWENGU WA SASA
Mahusiano ya Kanisa na ulimwengu
40. Yote tuliyoyazungumzia hapo juu mintarafu hadhi ya binadamu, jamii ya
watu, na maana ya ndani ya utendaji wa binadamu, ndio msingi wa mahusiano
kati ya Kanisa na ulimwengu na pia wa dialogia kati yao
[81].
Kwa sababu hiyo, katika mwanga wa yale yote yaliyokwisha kutangazwa rasmi na
Mtaguso kuhusu fumbo la Kanisa, katika sura hii [Mtaguso] unadhamiria
kutafakari juu ya Kanisa lililopo katika ulimwengu na linaloishi na kutenda
kazi pamoja nao.
Kanisa linalotoka katika upendo wa Baba wa milele[82],
limeanzishwa na Kristo Mwokozi katika ulimwengu wa nyakati, limekusanywa
katika Roho Mtakatifu[83], na
linalenga katika ukombozi wa maisha ya baadaye ambayo hayawezi kupatikana
kikamilifu isipokuwa katika ulimwengu ujao. Aidha, Kanisa lipo hapa duniani
na limeundwa na wanadamu ambao ni washiriki wa mji wa dunia hii. Nao huitwa,
kuanzia tayari katika historia ya binadamu, kuunda familia ya wana wa Mungu
inayopaswa kukua siku kwa siku mpaka Bwana atakapokuja. Familia hiyo,
iliyounganishwa kwa ajili ya mema ya mbinguni na inayotajirishwa nayo,
“iliundwa na kupangwa kama jamii katika ulimwengu huu”[84].
Nayo imepewa “misaada inayofaa kwa ajili ya umoja uonekanao na wa kijamii”[85].
Kwa hiyo, Kanisa ambalo kwa wakati mmoja ni “kusanyiko linaloonekana na
jumuiya ya kiroho”[86]
linatembea pamoja na wanadamu wote na linaionja pamoja na ulimwengu bahati
ileile ya kidunia. Vilevile Kanisa ni kama chachu na kama roho ya jamii ya
kibinadamu[87]
inayoelekea kufanyika upya katika Kristo na kugeuka kuwa familia ya Mungu.
Upenyezano wa namna hii kati ya mji wa duniani na mji wa mbinguni hauwezi
kuhisika kwa hakika ila kwa njia ya imani. Zaidi, fumbo la historia ya
kibinadamu linabaki; nayo historia itaendelea kuchafuliwa na dhambi hadi
mwangaza wa wana wa Mungu utakapodhihirika wazi. Ni kweli kwamba Kanisa
likifuatilia lengo lake la wokovu halimshirikishi binadamu maisha ya kimungu
tu, bali pia linaeneza mwanga wake unaoakisiwa kwa namna fulani duniani
kote. Na Kanisa linalifikia lengo hilo kwa sababu linaponya na kuinua hadhi
ya binadamu, linaimarisha jamii ya kibinadamu, na kutia maana ya ndani zaidi
na kusudi lake katika kazi za kila siku za wanadamu. Hivyo, Kanisa linaamini
kuwa, kwa njia ya kila mwanakanisa na ya jumuiya yake kwa pamoja, linaweza
kuchangia kwa vikubwa kuifanya familia ya wanadamu na historia yake viwe vya
kiutu zaidi.
Aidha, Kanisa katoliki kwa furaha linathamini mchango uliotolewa na
unaoendelea kutolewa na Makanisa mengine na jumuiya za kikanisa kwa kusudi
la kutekeleza jukumu lilelile. Wakati huohuo Kanisa linasadiki kuwa
ulimwengu unaweza kusaidia sana na kwa namna nyingi katika kuweka
matayarisho ya Injili. Yaani kila mtu, na jamii wa kibinadamu kwa ujumla,
huleta mchango wa vipawa na bidii zake. Basi, hapa Mtaguso unadhamiria
kufasiri baadhi ya miongozo iliyo muhimu zaidi ili kuhamasisha ipasavyo
katika kubadilishana na kupeana msaada mintarafu masuala ambayo kwa namna
fulani yahusu Kanisa na ulimwengu kwa pamoja.
Msaada unaonuiwa kutolewa na Kanisa kwa kila mtu
41. Binadamu wa siku hizi yupo katika njia inayoelekea kuupevusha
kikamilifu zaidi utu wake na inayomwezesha kuvumbua wazi zaidi haki zake na
kuzifuatilia. Lakini Kanisa limekabidhiwa wajibu wa kudhihirisha fumbo la
Mungu ambalo ndicho kikomo cha mwisho cha kila mtu. Kwa hiyo, wakati huohuo
Kanisa linamfunulia binadamu umaana wa maisha yake mwenyewe, yaani ukweli wa
ndani wa binadamu. Nalo hujua vema kuwa ni Mungu peke yake tu, ambaye kwa
utumishi wake linajitolea, anayetoa jibu kwa zile hamu zilizo za ndani zaidi
za moyo wa binadamu, usioweza kamwe kushibishwa kikamilifu na mali za
kidunia. Tena [Kanisa] hujua kuwa binadamu, akisukumwa pasipo kukoma na Roho
wa Mungu, hawezi kamwe kupuuzia suala la dini. Na ndivyo inavyoonyeshwa, si
tu na mang’amuzi ya karne zilizopita, bali pia na shuhuda nyingi za nyakati
zetu. Maana [binadamu] atatamani daima kujua, hata isivyo dhahiri, maana ya
maisha yake, ya kazi yake na ya kifo chake. Nalo Kanisa linakumbushia hoja
hizo kwa kuwepo kwake tu hapa duniani. Lakini Mungu peke yake, aliyemwumba
binadamu kwa sura yake na kumkomboa kutoka katika dhambi, anatoa jibu
maridhawa kabisa kwa masuala haya. Nalo jibu hutolewa kwa njia ya ufunuo
upatikanao katika Mwanae aliyefanyika mwili. Yeyote amfuataye Kristo, aliye
mtu kamili, yeye naye anazidi kujikamilisha katika utu wake.
Kutokana na imani hiyo, Kanisa linaweza kuopoa hadhi ya binadamu kutoka
katika kauli zile zote zenye hali ya kubadilikabadilika, kwa mfano zile
ambazo zinatweza mno mwili wa kibinadamu, ama kuukuza mno. Hakuna sheria ya
kibinadamu iwezayo kuiweka salama namna hii hadhi ya mtu na uhuru wake kama
ifanyavyo Injili ya Kristo iliyokabidhiwa kwa Kanisa. Maana Injili hii
inauhubiri na kuutangaza uhuru wa watoto wa Mungu, inakataa kila mtindo wa
utumwa utokanao na dhambi
[88],
inaheshimu hadhi ya dhamiri na hiari yake ya kuamua kama vitu vilivyo
vitakatifu. Tena Injili haikomi kuhamasisha kujiongezea talanta za
kibinadamu katika utumishi wa Mungu na kwa manufaa ya watu. Kisha,
inamkabidhi kila mmoja kwa wengine wote ili wampende
[89].
Jambo hilo linalingana na sheria ya msingi ya mpango wa kikristo. Maana
Mungu Mkombozi na Mungu Muumbaji ni Mungu yuleyule; tena Bwana wa historia
ya kibinadamu na Bwana wa historia ya wokovu ndiye Bwana yuleyule. Lakini
hata hivyo katika utaratibu huo wa kimungu, kujitawala kwa haki kwa kiumbe (
iusta
creatura autonomia), hasa kwa binadamu, hakuondolewi, bali zaidi
kunarudishwa katika hali ya hadhi yake na kuimarishwa katika hiyo.
Kwa sababu hiyo Kanisa, kwa nguvu ya Injili liliyokabidhiwa, linatangaza
haki za wanadamu, na linatambua na kuthamini sana juhudi zinazofanyika siku
za leo ili haki hizo zikuzwe popote. Lakini uamsho (motus) huo hauna
budi kupenywa na roho ya Injili, na kulindwa dhidi ya kila tabia danganyifu
inayodai binadamu ajitawale. Maana tunashawishiwa kufikiri kuwa haki za kila
mmoja wetu zinahifadhiwa pale tu ambapo tunafunguliwa na kila sharti la
sheria ya kimungu. Lakini kwa njia hii hadhi ya binadamu haiwezi kuokolewa;
ila zaidi inapotea.
Msaada unaonuiwa kutolewa na Kanisa kwa jamii ya kibinadamu
42. Muungano wa familia ya wanadamu unaimarishwa sana na kutimilizwa na
umoja wa familia ya watoto wa Mungu inayoasisiwa katika Kristo
[90].
Bila shaka utume maalum uliokabidhiwa na Kristo kwa Kanisa lake, haupo
katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, na kijamii. Maana lengo aliloliweka
Kristo kwa ajili ya Kanisa lipo katika uwanja wa kidini
[91].
Lakini kutokana na utume huo wa kidini hutiririshwa wajibu, mwanga na nguvu,
viwezavyo kuchangia katika kujenga na kuimarisha jamii ya wanadamu kadiri ya
sheria ya Mungu. Hivyo, pale panapohitajika na kadiri ya mazingira ya
nyakati na mahali, Kanisa nalo huweza na hupaswa kuamsha matendo yakusudiayo
katika utumishi wa watu wote, lakini hasa kwa wahitaji; kama vile kufanya
matendo ya huruma na mengine yanayofanana na hayo.
Aidha, Kanisa linayatambua yale mema yote yaliyopo katika mkikimkiki wa
kijamii (dynamismo sociali) wa siku za leo: na hasa huyatambua
maendeleo ya kuufikia umoja, ushirikisho ulio bora na muungano wa kijamii na
kiuchumi. Maana kuhamasisha umoja kunawiana na utume halisi wa Kanisa,
ambalo “katika Kristo ni kama sakramenti au ishara na chombo cha
kuwaunganisha watu kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote”[92].
Hivyo Kanisa lenyewe linauonyesha ulimwengu kwamba muungano halisi wa
kijamii [unaoonekana] kwa nje hutokana na muungano wa fikara na wa mioyo,
yaani hupatikana kutoka katika imani na upendo ambao kwao umoja wake una
msingi madhubuti katika Roho Mtakatifu. Maana nguvu ambazo Kanisa linaweza
kuzipenyeza katika jamii za kibinadamu za siku hizi ni imani na upendo
ambavyo vinapata kugeuzwa kuwa matendo katika maisha; wala nguvu hizo za
Kanisa hazimo katika kutawala milki yoyote ile ya kidunia kwa njia za
kibinadamu tu.
Aidha, kutokana na utume wake na maumbile yake, Kanisa halifungamani na
mtindo wowote wa utamaduni wa kibinadamu, au mfumo wa kisiasa, wa kiuchumi
au wa kijamii. Basi kwa sababu ya hali yake ya kuenea pote, Kanisa linaweza
kufungamanisha kwa namna ya pekee jamii za kibinadamu na pia mataifa,
ilimradi yawe na imani na Kanisa na kuutambua kimatendo uhuru wake halisi wa
kutimiliza utume wake. Ndiyo maana Kanisa linawaonya watoto wake, kama vile
wanadamu wote, kusuluhisha kila mgogoro kati ya mataifa na makabila katika
roho ile ya kifamilia ambayo ndiyo tabia ya watoto wa Mungu. Kadhalika
waimarishe kiundani vyama vya wanadamu vilivyo vya haki.
Basi, Mtaguso unazingatia kwa heshima kubwa kila kilicho cha kweli, chema
na cha haki, kipatikanacho katika taasisi mbalimbali ambazo wanadamu
wamejiundia na wanazoendelea kuzitengeneza. Aidha, Mtaguso unatangaza kuwa
Kanisa linataka kuzisaidia na kuzihamasisha taasisi hizo zote, kutegemeana
na uamuzi wake na kadiri zinavyolingana na utume wake. Hakuna lolote ambalo
Kanisa linalitamani zaidi kuliko kuyatumikia mafaa ya watu wote; tena kuliko
kupata uhuru wa kuenea chini ya mfumo wowote wa utawala (quovis regimine)
unaoziheshimu haki za msingi za binadamu na za familia na unaoyatambua madai
ya manufaa ya wote.
Msaada unaonuiwa kutolewa na Kanisa kwa utendaji wa binadamu kwa njia ya
wakristo
43. Mtaguso unawahimiza wakristo, walio raia wa miji yote miwili, [yaani
mji wa duniani na mji wa mbinguni], wafanye bidii kutekeleza kwa uaminifu
wajibu zao za kidunia, wakiongozwa na roho ya Injili. Wapo waamini ambao,
wakijua kuwa wao hawana uraia wa kudumu hapa duniani bali wanautafuta ule
ujao,[93] wanadhani kwamba kwa
sababu hiyo wanaweza kuzembea wajibu zao za kidunia. Hao basi wanakosa, wala
hawafikirii kuwa ni imani yenyewe inayowashurutisha zaidi kuzitekeleza,
kadiri ya wito wa kila mmoja[94].
Lakini vilevile wanakosa ambao, kinyume chake, hudhani kuwa wanaweza
kujizamisha kabisa katika shughuli za kidunia, kana kwamba hizo zingekuwa
geni sana kwa maisha ya kidini. Nayo hutazamwa tu machoni pao kama
mkusanyiko wa ibada mbalimbali na masharti kadhaa ya kimaadili. Utengano
unaoonekana katika fikra za wengi kati ya imani wanayoikiri na maisha yao ya
kila siku hauna budi kuhesabiwa kati ya makosa makubwa zaidi ya nyakati
zetu. Tangu Agano la Kale manabii walikuwa wanatoa kwa nguvu makaripio yao
dhidi ya kikwazo hicho[95]. Na
zaidi sana katika Agano Jipya, Yesu Kristo mwenyewe alitoa tishio la adhabu
kali [kwa wenye fikra za namna hii][96].
Kwa hiyo, lisiwekwe pingamizi hata kidogo kati ya utendaji wa kikazi na
kijaamii kwa upande mmoja, na maisha ya kidini kwa upande mwingine. Mkristo
mwenye kupuuza wajibu zake za hapa duniani anapuuza wajibu zake kwa jirani,
na pia kwa Mungu mwenyewe; na hivyo kuhatarisha uzima wake wa milele. Basi
wakristo wafurahie katika kutekeleza utendaji wao wote wa kidunia wakiufuata
mfano wa Kristo aliyekuwa mtu mwenye ufundi wa kazi. Nao wafungamanishe
bidii za kibinadamu, za kinyumbani, za kiufundi, za kisayansi na za
kiteknolojia katika kuleta mfumo mmoja wenye uhai pamoja na thamani za
kidini. Na chini ya uongozi wa juu sana wa thamani hizo mambo yote
yaunganishwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
Walei ndio wahusika maalumu katika shughuli na utendaji wa kidunia, ingawa
siyo wao peke yao. Kwa hiyo, wakati walei wanapotenda kama raia wa
ulimwengu, wawe kila mmoja peke yake ama kwa kushirikiana kwa pamoja,
wataziheshimu sheria mahususi za kila fani; lakini pia watajitahidi
kujipatia ustadi halisi katika nyanja zile. Tena, watatoa kwa hiari mchango
wa ushirikiano wao kwa wale wote wanaolenga katika shabaha zilezile.
Wakiheshimu madai ya imani na wakijawa na nguvu yake, wabuni maarifa mapya
bila kukoma na, pale panapohitajika, wayatekeleze. Ni wajibu wa dhamiri yao
iliyokwisha kuundwa ipasavyo, kuiandika sheria ya kimungu katika maisha ya
mji wa duniani. Nao, kutoka kwa makuhani, watarajie kupewa mwanga na nguvu
ya kiroho. Lakini wasifikiri kuwa wachungaji wao ni daima mabingwa kuhusu
mambo haya kiasi kwamba wakati wowote wana jawabu tayari kwa kila suala
lijitokezalo; wala huo sio wajibu maalumu [wa wachungaji]. Bali walei
wenyewe washike wajibu zao, katika mwanga wa hekima ya kikristo, na
wazingatie kwa heshima mafundisho ya Majisterio
[97].
Mara nyingi mtazamo wenyewe wa kikristo juu ya mambo ya maisha
utawaongoza kupata jawabu fulani katika hoja mbalimbali. Lakini hata hivyo,
kwa unyofu ulio sawa, waamini wengine wataweza kutoa maoni yaliyo tofauti
mintarafu hoja ileile. Nalo, linatokea mara nyingi na kwa halali. Maana,
kama watu wengi watalinganisha kwa urahisi jawabu moja au jingine na ujumbe
wa Injili, basi walei wakumbuke kuwa hakuna mtu anayeruhusiwa kudai kwamba
uongozi wa Kanisa unahalalisha maoni yake tu. Bali watafute daima njia ya
kuongozana wao kwa wao kwa njia ya mijadala isiyo na hila, wakishikilia
daima upendo na kuyashughulikia awali ya yote manufaa ya wote.
Walei, walio na wajibu za kimatendo katika maisha yote ya Kanisa, hawapaswi
tu kuipenyeza roho ya kikristo katika ulimwengu, bali pia wanaitwa kuwa
mashahidi wa Kristo kati ya watu wote, yaani pia katika jamii ya kibinadamu.
Maaskofu, waliokabidhiwa wajibu wa kuliongoza Kanisa la Mungu, wauhubiri
pamoja na Mapadre wao ujumbe wa Kristo, ili kwamba utendaji wote wa kidunia
wa waamini upate kung’arishwa na mwanga wa Injili. Aidha, wachungaji wote
wakumbuke kuwa, kwa njia ya tabia na ari yao ya kila siku
[98],
wanaudhihirishia ulimwengu uso wa Kanisa, ambao kwa msingi huo wanadamu
wanajitengenezea kauli kuhusu nguvu na ukweli wa ujumbe wa kikristo. Kwa
maisha na maneno [yao] wao, pamoja na watawa na waamini, waonyeshe kuwa
Kanisa, kwa kuwepo kwake tu, pamoja na vipawa vyake vyote vilivyomo ndani
yake, ndiyo chemchemi isiyofifia ya nguvu zile ambazo ulimwengu wa kisasa
unazihitaji sana. Kwa kusoma kwa bidii wajiwezeshe kushika nafasi yao katika
dialogia na ulimwengu huu, na wanadamu wenye rai mbalimbali. Lakini hasa
wayazingatie maneno ya Mtaguso huu: “Kwa kuwa siku hizi wanadamu wanazidi
kufungamana wao kwa wao katika maisha ya kiraia, ya kiuchumi na ya kijamii,
yawapasa Mapadre, kwa kuunganisha juhudi na kazi zao chini ya uongozi wa
Maaskofu na wa Baba Mtakatifu, waondoshe kila sababu ya mfarakano (
dispersionis),
kusudi wanadamu wote waongozwe kwenye umoja wa familia ya Mungu.”
[99]
Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu Kanisa limebaki daima bibiarusi mwaminifu wa
Bwana wake, wala halikuacha kamwe kuwa ishara ya ukombozi hapa duniani.
Lakini hata hivyo Kanisa linajua kuwa, katika mlolongo wa karne zilizopita,
miongoni mwa wanajumuiya wake[100],
makleri kwa walei, hawakukosekana wale ambao hawakuwa waaminifu kwa Roho wa
Mungu. Na hata katika nyakati zetu Kanisa linajua vema jinsi ulivyo mbali
kati yao ujumbe linaouleta na udhaifu wa kibinadamu wa wale waliokabidhiwa
Injili. Lolote liwalo juu ya hukumu ya historia kuhusu makasoro haya, sisi
lazima tuyajue na kuyapinga kwa nguvu usije uenezaji wa Injili ukapata
kikwazo. Kadhalika, Kanisa linafahamu vizuri jinsi linavyopaswa kukomaa
katika mtindo wa mahusiano yake na ulimwengu likisaidiwa na mang’amuzi ya
karne zilizopita. Mama Kanisa, akiongozwa na Roho Mtakatifu hatachoka kamwe
kuwaonya wana wake “wajitakase na kujitengeneza upya, ili ishara ya Kristo
izidi kung’ara kwa nuru angavu juu ya uso wa Kanisa”[101].
Msaada upokewao kutoka kwa ulimwengu wa sasa
44. Kama vile ilivyo muhimu kwa ulimwengu kulitambua Kanisa kama chombo
chenye nafasi ya kijamii katika historia na kama chachu yake, vivyo hivyo
Kanisa nalo linafahamu jinsi lilivyofaidishwa kutokana na historia na
maendeleo ya wanadamu.
Mang’amuzi ya karne zilizopita, maendeleo ya sayansi, na hazina
zinazofichama katika tamaduni mbalimbali za kibinadamu, hayo yote
yanadhihirisha kinaganaga zaidi maumbile ya binadamu mwenyewe. Nayo
yanafungua njia mpya zinazoelekeza katika ukweli na yanalinufaisha pia
Kanisa. Yaani Kanisa, tangu awali ya historia yake, lilijifunza kufafanua
ujumbe wa Kristo likitumia mawazo na lugha za mataifa mbalimbali. Aidha
limejitahidi kuufasiri ujumbe huo kwa njia ya hekima ya wanafalsafa. Katika
harakati hizo Kanisa linanuia kulinganisha ifaavyo Injili na uwezo wa
kuelewa wa watu wote kama vile na madai ya wenye elimu. Na ulinganifu wa
namna hii katika kuhubiri lile Neno lililofunuliwa kwa binadamu lazima
uendelee kuwa kanuni ya kila uenezaji wa Injili. Maana kwa njia hii, katika
kila taifa uwezo wa kufafanua habari ya Kristo unahimizwa kila mahali kwa
namna zake. Na wakati huohuo mawasiliano yenye uhai baina ya Kanisa na
tamaduni mbalimbali yanahamasishwa[102].
Ili kukuza mawasiliano haya, hasa siku hizi ambapo mabadiliko yanafuatana
kwa haraka sana na namna za kufikiri kwa watu zinatofautiana sana, Kanisa
linauhitaji kwa namna ya pekee msaada wa wale ambao, kwa kuishi katika
ulimwengu huu, ni mafundi katika kuvijua vyombo vya dunia hii na katika fani
zake mbalimbali, wawe waamini au wasio waamini. Ni wajibu wa taifa zima la
Mungu, na hasa wa wachungaji na wanateolojia, wakisaidiwa na Roho Mtakatifu,
kuzisikiliza kwa makini, kuzipambanua na kuzifafanua sauti mbalimbali
zinazosikika katika nyakati zetu, na hatimaye kuzichambua (diudicare)
katika mwanga wa Neno la Mungu. Na kazi hiyo yote inakusudia ukweli
uliofunuliwa kwetu uzidi kueleweka kwa undani zaidi, kufahamika zaidi, nao
upate kufafanuliwa kwa namna inayoufaa zaidi.
Kanisa lina muundo wa kijamii unaoonekana, na ambao ni alama ya umoja wake
na Kristo. Hivyo linaweza kutajirishwa – na ndivyo lifanyavyo – na maendeleo
ya maisha ya kijamii, si kana kwamba lingekuwa na kasoro katika muundo
liliopewa na Kristo; bali kusudi lipate kuujua muundo huo kwa undani zaidi;
liuonyeshe kinaganaga zaidi na kuulinganisha na nyakati zetu kwa mafanikio
maridhawa zaidi. Kanisa linahisi kwa roho ya shukrani kuwa linapewa misaada
mbalimbali, kama jumuiya na katika kila mmoja wa watoto wake, kutokana na
watu wa kila kiwango na hali. Awaye yote mwenye kuihamasisha jamii ya
kibinadamu katika nyanja za familia, utamaduni, maisha ya kiuchumi na ya
kijamii, siasa ya kitaifa na kimataifa, huyo huisaidia sana pia jumuiya ya
Kanisa kufuatana na mpango wa Mungu na kwa kadiri jumuiya hii inavyotegemea
mambo yaliyo nje yake. Zaidi, Kanisa linakiri kwamba limenufaishwa sana na
linaweza kuendelea kunufaishwa kutokana na vipingamizi vyenyewe vya wale
wanaolikana na kulidhulumu
[103].
Kristo aliye alfa na omega
45. Kanisa, katika kutoa msaada kwa ulimwengu kama vile katika kupewa mambo
mengi kutoka kwake, linalidhamiria jambo hili tu: Ufalme wa Mungu uje na
wokovu wa wanadamu wote utimizwe. Kila lililo jema, ambalo Kanisa linaipatia
familia ya wanadamu, wakati wa hija yake hapa duniani, linatiririka na
kutokana na kuwa Kanisa ni “sakramenti ya wokovu kwa wote” (
universale
salutis sacramentum)
[104]
ambayo inafunua na kutimiza fumbo la upendo wa Mungu kwa binadamu.
Maana Neno wa Mungu, ambaye kwa njia yake viumbe vyote viliumbwa,
alijifanya mwenyewe mwili ili Yeye, aliye mtu kamili, awaokoe watu wote na
kuvijumlisha vitu vyote ndani yake. Bwana ndiye lengo la historia ya
kibinadamu, “kitovu cha matarajio ya historia na ya ustaarabu”, kiini cha
uzao wa kibinadamu, furaha ya kila moyo, na utimilifu wa matumaini yote[105].
Yeye ndiye ambaye Baba alimfufua kutoka mauti, akamtukuza na kumweka kuumeni
kwake akimfanya hakimu wa walio hai na wafu. Nasi, tukihuishwa na kukusanywa
pamoja katika Roho wake, tunakwenda kama wahujaji kuulaki utimilifu wa
historia ya kibinadamu unaolingana kikamilifu na mpango wa upendo wake,
yaani: “kuvijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya
duniani” (Efe 1:10).
Bwana mwenyewe asema: “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami,
kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni alfa na omega, mwanzo na
mwisho, wa kwanza na wa mwisho” (Ufu 22: 12-13).
SEHEMU YA PILI
BAADHI YA MASWALA YANAYOHITAJIKA KUFAFANULIWA UPESI
Utangulizi
46. Mpaka hapa Mtaguso umeifafanua hadhi iliyomo katika utu wa binadamu, na
wajibu wake anaoitwa kuutekeleza ulimwenguni, uwe wa kibinafsi au wa
kijamii. Hivyo, Mtaguso, katika mwanga wa Injili na mang’amuzi ya
kibinadamu, sasa unawaalika wote kuzingatia baadhi ya masuala ya siku hizi
ambayo ni muhimu sana na ambayo yanawagusa kwa namna ya pekee wanadamu wote.
Miongoni mwa hoja nyingi zinazoamsha juhudi ya watu wote hasa siku hizi,
haya yafuatayo yafaa kuyazingatia hasa: ndoa na familia, utamaduni wa
kibinadamu, maisha ya kiuchumi na ya kijamii, maisha ya kisiasa, ushirikiano
kati ya mataifa, na amani. [Tunapenda kwamba] juu ya kila moja ya masuala
hayo, miongozo na mwanga vitokavyo kwa Kristo ving’arishwe. Hivyo, wakristo
wapate kuongozwa, na wanadamu wote wapate kuangazwa, katika kuyatafuta
masuluhisho kwa hoja nyingi na ngumu namna hii.
Sura ya Kwanza
KUSTAWISHA HESHIMA YA NDOA
NA YA FAMILIA
Ndoa na familia katika ulimwengu wa kisasa
47. Usitawi (
Salus) wa mtu binafsi na wa jamii ya kibinadamu na ya
kikristo hufungamana kabisa na hali njema ya jumuiya ya kindoa na ya
kifamilia. Kwa hiyo wakristo, pamoja na wote wenye kuiheshimu sana jumuiya
hiyo, wanaifurahia kwa moyo mkunjufu misaada mbalimbali ambayo kwayo
wanadamu wa siku za leo waweza kuendelea katika kuistawisha jumuiya hiyo ya
upendo, na katika kuuheshimu uhai. [Misaada hiyo] inawasaidia watu wa ndoa
na wazazi katika kutekeleza jukumu lao muhimu, na kutoka [misaada] hiyo wao
hutarajia kupata manufaa yaliyo bora zaidi, pamoja na kufanya juhudi ili
itolewe.
Lakini hadhi ya ndoa haimuliki kwa mwanga mweupe mahali pote, kwa sababu
hutiwa kivuli na mitara, pigo la talaka, uhuru – inavyosemwa – wa mapenzi,
na maharibifu mengineyo. Licha ya hayo, mara nyingi upendo wa kindoa
unanajisiwa na ubinafsi, upenzitamaa (
hedonismo), na mitindo isiyo
halali ya kuzuia uzazi. Aidha, hali za siku hizi za kiuchumi,
kisaikolojia-kijamii, na za kiraia, huleta machafuko makubwa katika familia.
Kisha, mahali pengine ulimwenguni matatizo yatokanayo na ongezeko la idadi
ya watu yanaleta fadhaa. Kutokana na hayo yote huzuka shida nyingi
zinazofadhaisha dhamiri za watu. Hata hivyo, thamani na uimara wa asasi ya
ndoa na ya familia (
matrimonialis familiarisque instituti) huonyeshwa
siku za leo kwa namna ya pekee. Jambo hilo linatokea kwa sababu mageuzo
makubwa ya jamii za siku hizi, licha ya magumu ambayo kwa kasi hujitokeza
humo, mara nyingi yanadhihirisha kwa njia mbalimbali maumbile halisi ya ndoa
na familia zenyewe.
Kwa hiyo Mtaguso, ukiweka wazi vipengere kadhaa vya msingi vya mafundisho
ya Kanisa, unadhamiria kuwaangaza na kuwaimarisha wakristo na wanadamu wote
wanaojitahidi kulinda na kuhamasisha hadhi ya kimaumbile na thamani ya juu
sana na iliyo takatifu ya hali ya ndoa.
Utakatifu wa ndoa na familia
48. Ushirikiano wa ndani wa maisha na wa upendo wa ndoa uliasisiwa na
[Mungu] Muumbaji na kuratibishwa [naye] kwa sheria maalumu. Nao una asili
yake katika agano la ndoa (foedere coniugii), yaani katika
makubaliano yasiyotanguka ya kila mmoja (consensu personali). Na
hivyo, ndoa ni ushirika unaopata kuwa imara kwa sheria za kimungu na ambao
unazaliwa, hata mbele ya jamii, kutokana na tendo lile la kibinadamu ambalo
kwalo kila mwanandoa anajitoa kwa mwenzake na anampokea. Kifungo hicho
kitakatifu kinachoyakusudia manufaa ya wanandoa, ya watoto na ya jamii,
hakiutegemei uhiari wa kiholela (arbitrio) wa binadamu. Kwani Mungu
mwenyewe ndiye muundaji wa ndoa; nayo ina tunu na malengo mengi[106]
ambayo yote yana umuhimu mkubwa kwa mwendelezo wa uzao wa kibinadamu, kwa
maendeleo ya kibinafsi na kwa kikomo cha milele cha kila mmoja wa
wanafamilia; tena ina umuhimu mkubwa kwa heshima, uthabiti, amani na usitawi
wa familia yenyewe na wa jamii nzima ya wanadamu. Kwa maumbile yake halisi
ndoa yenyewe, na upendo wa kindoa, vimepangwa kwa ajili ya uzazi na malezi
ya watoto; kilele kama hicho, ndilo taji lake [ndoa]. Na hivyo mwanamume na
mwanamke, ambao kwa ajili ya agano la upendo wa kindoa “si wawili tena bali
ni mwili mmoja” (Mt 19:6), wanasaidiana na kutumikiana kwa muungano wa ndani
wa nafsi na wa utendaji wao. Nao wanang’amua umaana wa umoja wao, na
kuufikia kwa utimilifu unaozidi kujikamilisha siku kwa siku. Umoja huo wa
ndani, maadamu ni kujitoa kila mmoja kwa mwenzake, unadai uaminifu kamili
kati ya wanandoa na unataka umoja huu usivunjwe[107].
Na ndivyo ilivyo pia kwa manufaa ya watoto.
Kristo Bwana amemimina baraka zake tele juu ya upendo huo unaojionyesha kwa
namna nyingi. Nao umebubujika katika chemchemi ya upendo wa kimungu na
kujiunda kwa mfano wa umoja uliopo kati ya Kristo na Kanisa. Maana, kama
vile zamani Mungu alivyokutana na taifa lake kwa agano la upendo na uaminifu
[108],
vivyo hivyo Yesu, aliye mkombozi wa wanadamu na Bwanaarusi wa Kanisa
[109],
anawajia wakristo wanandoa kwa njia ya sakramenti ya ndoa. Aidha, anaendelea
kukaa nao ili waweze kupendana wao kwa wao kwa uaminifu, kwa daima na kwa
uradhi wa moyo, kama vile Yesu naye alivyolipenda Kanisa na kujitoa kwake
[110].
Upendo halisi wa kindoa unachukuliwa ndani ya upendo wa kimungu na
unategemezwa na kutajirishwa na nguvu yenye kukomboa ya Kristo pamoja na
utendaji wa wokovu wa Kanisa. Hivyo, wanandoa kweli wanaongozwa kwa Mungu,
wanasaidiwa na kuimarishwa katika jukumu lao bora la kuwa baba na mama
[111].
Kwa sababu hiyo, wakristo wanandoa wanatiwa nguvu na kama kuwekwa wakfu
[112]
na sakramenti maalumu kwa ajili ya wajibu na hadhi ya hali yao. Nao wanapata
kutekeleza wajibu wao wa kindoa na wa kifamilia kwa nguvu ya sakramenti hii,
wakipenyezwa na Roho wa Kristo ambaye kwake maisha yao yote yanajazwa imani,
tumaini na mapendo. Na hatimaye wanaelekea kuufikia ukamilifu wao, kila
mmoja akimtakatifuza mwenzake; na hivyo wanashirikiana pamoja katika
kumtukuza Mungu.
Wakiongozwa na mfano wa wazazi pamoja na sala katika familia, watoto na wale
wote wanaoishi katika nyumba watapata kwa urahisi zaidi njia ya kulelewa
kiutu, njia ya wokovu na ya utakatifu. Na wafunga ndoa, waliopewa heshima na
wajibu wa kuwa baba na mama, watatekeleza kwa makini wajibu wao wa kulea,
hasa kidini, wajibu ambao kwanza ni wao kuliko wa wengine.
Pia watoto, kama viungo hai vya familia, wanachangia kwa upande wao
kuwatakatifuza wazazi. Maana watawarudishia wazazi upendo uliojaa shukrani
na heshima, na watawaamini; watakuwa karibu nao, kama ifaavyo kwa watoto,
katika taabu na upweke wa uzeeni. Na ujane, ukipokelewa kwa moyo thabiti
kama mwendelezo wa wito wa ndoa, utaheshimiwa na wote[113].
Familia moja itaishirikisha kwa ukarimu familia nyingine utajiri wake wa
kiroho. Kwa hiyo familia ya kikristo inatokana na ndoa, ambayo ni mfano na
ushirikisho wa agano la upendo kati ya Kristo na Kanisa[114];
nayo, kwa njia ya upendo, ya kuzaa wazao bila ubahili, ya umoja, uaminifu wa
wanandoa, na hatimaye kwa ushirikiano wenye upendo wa wanafamilia wake,
itawadhihirishia wote uwepo hai wa Mwokozi wa ulimwengu hapa duniani na
maumbile halisi ya Kanisa.
Upendo ya kindoa
49. Wachumba hualikwa mara nyingi na Neno la Mungu kuulisha na
kuuimarisha uchumba wao kwa upendo safi; na pia wafunga ndoa hualikwa
kuulisha na kuuimarisha muungano wa ndoa kwa upendo usiotengeka[115].
Hata watu wengi wa nyakati zetu wanathamini sana upendo wa kweli kati ya
mume na mke unaojidhihirisha kwa namna mbalimbali kwa mujibu wa desturi
zilizo nyofu za mataifa na nyakati mbalimbali. Upendo wa ndoa ni tendo
halisi la kiutu, kwa maana ni hisia kati ya mtu na mtu itokanayo na utashi
[wao] na inayouhusu wema wa mtu mzima. Kwa sababu hiyo, upendo huo unaweza
kuzitajirisha hisia za rohoni na matendo yake ya kimwili kwa heshima ya
pekee; na pia yaweza kuzitukuza [hisia na matendo hayo] kama ishara na alama
mahsusi za urafiki wa kindoa. [Mungu] Bwana alipenda kuponya, kukamilisha na
kukuza upendo huu kwa kipawa maalum cha neema na ukarimu. Upendo wa namna
hii, unaounganisha pamoja tunu za kibinadamu na za kimungu, huwaongoza
wanandoa kujitoa kwa hiari kila mmoja kwa mwenzie; kadhalika, unathibitishwa
na hisia na vitendo vya upendo mtamu (tenero affecto) na kupenya
vipengele vyote vya maisha ya wanandoa[116].
Zaidi, upendo wa ndoa unatimilika na kukua kwa njia ya utekelezaji wake; na
kwa sababu hiyo ni jambo kubwa kuliko mvutio mtupu wa kimwili (eroticam
inclinationem) ambao, ukilishwa kwa tamaa ya kibinafsi, utafifia vibaya
na mapema.
Upendo huo huonyeshwa na kutimilika kwa namna ya pekee kwa matendo yaliyo
maalum ya ndoa; kwa hiyo yale matendo ambayo kwayo wanandoa wanaungana kati
yao kwa undani na usafi, ni mazuri na ya kuheshimiwa. Nayo, yakifanyika kwa
namna inayoustahili utu wa binadamu, yanachochea kile yanachokiashiria,
yaani kujitoa kila mmoja kwa mwenzie, na yanawatajirisha mume na mke katika
furaha na shukrani. Upendo huo unathibitishwa na ahadi [ya uaminifu ya kila
mmoja] na hasa unaidhinishwa na sakramenti ya Kristo; hivyo unadumu
mwaminifu wala hauwezi kuvunjika katika raha na taabu, kwa upande wa mwili
na wa roho. [Ndiposa] upendo wa ndoa haukubali kabisa uzinzi na talaka. Tena
umoja wa ndoa, uliothibitishwa na Bwana, unaonekana kinaganaga katika hadhi
iliyo sawa ya mume na mke, ambayo ni lazima itambulikane katika upendo
mkamilifu na wa kila mmoja kwa mwenzake. Lakini fadhila ya pekee inadaiwa
ili kuzitekeleza kwa uaminifu wajibu za wito huu wa kikristo. Ndiyo maana
wafunga ndoa, wakiimarishwa na neema [ya Mungu] kwa ajili ya maisha
matakatifu, watauhamasisha bila kukoma uthabiti wa upendo, saburi na roho ya
sadaka. Nao watauomba upendo huo kwa njia ya sala.
Upendo halisi wa ndoa utaheshimiwa zaidi, na watu watafundishwa vema, ikiwa
wanandoa wakristo wanatoa ushuhuda wa uaminifu na wa uelewano katika upendo,
pamoja na ari katika kuwalea watoto. Tena ikiwa wanashika nafasi yao katika
matengenezo ya lazima ya kitamaduni, kisaikolojia na kijamii kwa manufaa ya
ndoa na familia. Pia vijana lazima wafundishwe ifaavyo na mapema, hasa ndani
ya familia yao, kuhusu heshima ya upendo wa ndoa, kama vile juu ya dhima
yake na kujitokeza kwake. Na hivyo wapate kufundishwa kuuheshimu usafi wa
moyo, na hatimaye kuushikilia uchumba ulio mnyofu na baadaye kufunga ndoa.
Uzazi katika ndoa
50. Ndoa na upendo wake kwa maumbile yake inakusudia kuwazaa na kuwalea
watoto. Maana watoto ni zawadi bora ya ndoa, nao wanachangia sana kwa ajili
ya mema ya wazazi wenyewe. Mungu mwenyewe ndiye aliyesema: “Si vema mtu huyu
awe peke yake” (Mwa 2:18); naye “alimwumba mtu mwanzo, aliwaumba mtu mume na
mtu mke” (Mt 19:4), na alitaka kumshirikisha mtu kwa namna ya pekee katika
kazi yake ya kuumba. Pia aliwabariki mwanamume na mwanamke akiwaambia:
“Zaeni, mkaongezeke” (Mwa 1:28). Bila ya kupuuza malengo mengine ya ndoa,
matendo stahivu (
cultus) ya upendo wa kindoa, pamoja na muundo wote
wa maisha ya kifamilia unaotokana nao, unalenga kuwafanya mume na mke
wakubali kwa moyo thabiti kushiriki upendo wa Muumba na Mwokozi ambaye kwa
njia yao anaongeza siku kwa siku familia yake na kuitajirisha.
Wanandoa wanajua kuwa ni washiriki wa upendo wa Mungu Muumba na wafasiri
wake kwa njia ya wajibu wa kuuendeleza uhai wa binadamu na kuulea; nao hauna
budi kutazamwa kama utume wao maalumu. Kwa hiyo watatekeleza kazi yao kwa
uwajibikaji wa kiutu na wa kikristo. Tena, kwa upole na heshima kwa Mungu
watajitengenezea fikra zilizo nyofu kwa njia ya kutafakari na kujibidisha,
wakiyazingatia manufaa yao wenyewe na ya watoto wao, wale waliokwisha zaliwa
kama vile wanaotarajiwa kuzaliwa. Wataipima hali ya maisha ya nyakati zao na
ya wao wenyewe kwa upande wa kimwili na wa kiroho. Na hatimaye watautunza
utaratibu ulio bora wa manufaa ya familia, ya jamii, na ya Kanisa. Ni
wanandoa wenyewe wanaopaswa kuzifikia fikra hizo mbele ya Mungu. Lakini
katika tabia yao wanandoa wakristo ni lazima waelewe kuwa hawawezi kuenenda
kadiri ya hiari yao, bali lazima waongozwe na dhamiri iliyo nyofu na
inayopaswa kujilinganisha na sheria ya Mungu mwenyewe. Kisha waitii
Majisterio ya Kanisa ambayo inafasiri kiukweli sheria ile katika mwanga wa
Injili. Sheria hiyo ya kimungu huionyesha maana kamili ya upendo wa ndoa,
huulinda na kuusukuma mbele kuelekea ukamilifu wake wa kiutu. Hivyo wanandoa
wakristo, wakiyategemea Maongozi ya kimungu na kuilisha roho ya sadaka (spiritum
sacrificii)[117],
wanamtukuza Muumba na wanajielekeza kwenye ukamilifu wa Kristo pale
wanapotekeleza jukumu lao la kuzaa kwa moyo radhi na kwa uwajibikaji wa
kiutu na wa kikristo. Miongoni mwa wanandoa wanaotekeleza wajibu
waliokabidhiwa na Mungu, lazima watajwe wale ambao, kwa uamuzi wenye
utaratibu na wa pamoja, wanapokea kwa moyo mkuu hata idadi kubwa zaidi ya
watoto wanaodai kulelewa ipasavyo[118].
Hata hivyo, ndoa haikuwekwa kwa ajili ya kuwazaa watoto tu; lakini maumbile
[yake] yenyewe ya kuwa agano lisilotengeka kati ya watu wawili na pia
manufaa ya watoto vinadai kuwa upendo kati ya wanandoa uambatane na ishara
zake zenye utaratibu mzuri, yakue na kufikia ukomavu. Kwa hiyo ingawa
pengine watoto, ambao mara nyingi hutamaniwa sana, hawapatikani, hata hivyo
ndoa hudumu kama mazoea na ushirika (
consuetudo et communio) wa
maisha yote; kisha huhifadhi thamani yake na hali yake ya kutotengeka.
Kupatana kwa upendo wa ndoa na heshima ya uhai wa binadamu
51. Mtaguso unajua kuwa mara nyingi wanandoa wanapopanga ipasavyo maisha ya
ndoa, wanazuiliwa na hali mbalimbali za maisha ya kisasa. Tena wanaweza
kupambana na mazingira ambapo haiwezekani kuongeza idadi ya watoto, walau
kwa muda fulani; wala si rahisi kutunza uaminifu wa upendo na hali kamili ya
kifamilia katika maisha yao. Maana, pale ambapo mwandani wa ndoa (
intima
vita conigalis) unakatishwa, mara nyingi uaminifu huhatarishwa, na
manufaa ya watoto huathirika; na hapo ndipo malezi ya watoto hutiwa
mashakani, pamoja na ule ujasiri wa kukubali kupata watoto wengine.
Wapo wengine wanaodai kuyatatua matatizo hayo kwa namna zisizo halali, na
pengine hawakatai hata uuaji. Basi Kanisa linakumbusha kwamba sheria za
kimungu za kuendeleza uhai na wajibu wa kuhamasisha upendo halisi wa kindoa
haviwezi kupingana.
Maana Mungu aliye Bwana wa uhai amewakabidhi wanadamu utume mkuu wa
kuulinda uhai; na utume huo, hauna budi kutekelezwa kwa namna za kiutu. Kwa
hiyo uhai, ukishatungwa, lazima uhifadhiwe kwa juhudi kubwa; kwa hiyo
kuharibu mimba na kuwaua watoto ni mauaji ya kuchukiza kabisa. Maumbile ya
kijinsia katika binadamu na uwezo wake wa kuzaa unayashinda kwa namna ya
ajabu yale yanayotokea katika viumbe vingine vilivyo chini yake. Kwa hiyo
matendo yenyewe halisi ya maisha ya ndoa yameratibiwa kadiri ya hadhi ya
binadamu, nayo ni lazima yastahiwe kwa heshima kubwa. Kwa hiyo, katika suala
la kupatanisha upendo wa ndoa na wajibu wa kutoa uhai, maadili ya mwenendo
[wa wanandoa] hayategemei tu nia yao nyofu wala tathmini ya madhumuni peke
yake; bali [tabia hii] lazima iainishwe na vigezo halisi, vigezo ambavyo
vina misingi yake katika maumbile ya mtu na ya matendo yake; vigezo
vinavyoheshimu maana kamili ya kujitoa mmoja kwa mwingine na ya uzazi wa
binadamu katika maana ya upendo wa kweli. Na hayo yote hayatawezekana ikiwa
fadhila ya usafi wa moyo wa kindoa haitalishwa kwa unyofu wa moyo. Watoto wa
Kanisa, wakiasisiwa katika miongozo hii, hawawezi kushika njia za kuudhibiti
uzazi zinazolaumiwa na Majisterio[119],
iliyo na wajibu wa kufafanua sheria ya kimungu.
Iwe wazi kwa wote kwamba uhai wa binadamu na jukumu la kuuendeleza uhai huo
havifungwi katika mipaka ya maisha ya hapa duniani, wala haviwezi kupimwa na
kueleweka katika ulimwengu huu tu, bali vinahusu daima kikomo cha milele cha
wanadamu.
Ustawi wa ndoa na familia ushughulikiwe na wote
52. Familia ni shule ya kujitajirisha kibinadamu. Lakini, ili familia
iweze kuchota utimilifu wa maisha yake na wa wajibu wake ni lazima wanandoa
wawe na moyo ulio wazi na wenye upendo wa kila mmoja kwa mwenzake. Tena,
inawapasa kuwa na ushirika wa fikra na wa pamoja kati ya mume na mke, na
ushirikiano thabiti kama wazazi katika malezi ya watoto. Uwepo wa baba
mwenye kuishughulikia familia yake unanufaisha sana malezi yao; lakini pia
ni muhimu ziwepo bidii za mama naye katika nyumba yake; hasa kuwashughulikia
watoto walio wadogo zaidi, bila kusahau maendeleo ya kijamii ya mwanamke.
Aidha watoto, kwa njia ya malezi, wajengwe kitabia kwa namna ambayo
itawawezesha kuufikia ukomavu wao na kuufuata wito wao kwa uwajibikaji
kamili, hata ikiwa wito wa kidini. Na hatimaye waweze kuchagua hali ya
maisha yao; kama watachagua hali ya maisha ya ndoa, wapate kuunda familia
yao katika hali ya kimaadili, ya kijamii na ya kiuchumi inayowafaa kweli.
Aidha ni wajibu wa wazazi au walezi kuwaongoza walio vijana zaidi katika
kuiunda familia yao mpya kwa ushauri nasaha unaoelezwa kwa namna
inayowapendeza. Nao walezi waepukane hasa na tabia yenye kuwashurutisha, kwa
mitindo mbalimbali ya ukandamizaji, kushika hali fulani ya maisha au pengine
kumchagua mtu fulani kama mwenzake wa ndoa.
Familia ni mahali ambapo vizazi vilivyo tofauti vinakutana na kusaidiana
kati yao kuifikia busara ya kibinadamu iliyo kamili zaidi, na kuunganisha
pamoja haki za mtu binafsi na madai mengine ya maisha ya kijamii. Hivyo
familia ndio msingi wa jamii. Kwa hiyo, wale wote wenye uwezo wa kuathiri
jamii na makundi yake mbalimbali ni lazima wasaidie kimatendo kwa ajili ya
usitawi wa ndoa na familia. Serikali za nchi zinapaswa kutazama kama wajibu
mkuu kuheshimu, kulinda na kusitawisha maumbile halisi [ya ndoa na familia]
pamoja na maadili ya wote na usitawi wa maisha ya nyumbani. Kwa namna ya
pekee haki ya wazazi ya kuzaa watoto na kuwalea ndani ya familia haitakuwa
na budi kutetewa. Lakini sheria zenye kufaa na mipango mbalimbali vitapaswa
kuwalinda na kuwasaidia ifaavyo wale ambao bahati mbaya hawana familia yao
wenyewe.
Wakristo, wakiukomboa wakati wa sasa
[120]
na kupambanua mambo yadumuyo na yale yapitayo, watajibidisha ili
kuyasitawisha kwa makini mema ya familia; [na watafuatilia lengo hilo] kwa
ushuhuda wa maisha yao na pia kwa kushirikiana kwa moyo na watu [wote] wenye
mapenzi mema. Na hivyo watayashinda matatizo yaliyopo na watayakidhi
mahitaji na manufaa ya familia yanayojitokeza katika nyakati mpya. Kwa lengo
hilo hisia za kikristo za waamini, dhamiri nyofu za kimaadili za wanadamu
pamoja na hekima na umahiri wa wale wanaohusika katika elimu ya dini utaleta
mchango mkubwa.
Wataalamu wa sayansi, hasa za kibayolojia, kiuganga, kijamii na
kisaikolojia, huweza kunufaisha sana ndoa na familia na pia amani ya dhamiri
kama watauunganisha utafiti wao na pia kama watajitahidi kubainisha kwa
undani zaidi hali mbalimbali zinazousaidia uzazi wenye utaratibu na ulio
mnyofu.
Ni wajibu wa mapadre kujipatia elimu iliyo ya lazima mintarafu masuala ya
maisha ya kifamilia, na kuusaidia kwa upendo wito wa wanandoa katika maisha
yao ya kindoa na ya kifamilia. Kwa kusudi hilo watatumia mbinu mbalimbali za
kichungaji: kuhubiri Neno la Mungu, ibada za kiliturujia na misaada mingine
ya kiroho. Tena watawasaidia kwa utu na saburi katika matatizo yao, na
kuwaimarisha katika mapendo ili ziundwe familia zinazong’aa kwelikweli.
Taasisi mbalimbali za kitume, hasa zile zinazoshirikisha familia,
zijibidishe kuwategemeza kwa mafundisho na matendo vijana na wanandoa
wenyewe, hasa familia mpya; tena zifanye juhudi kuwalea kwa maisha ya
kifamilia, ya kijamii na ya kitume.
Kisha, wanandoa wenyewe, walioumbwa kwa sura ya Mungu aliye hai na
waliowekwa katika hadhi halisi ya kila mtu, waunganishwe kwa upendo ulio
sawa wa kila mmoja kwa mwenzie, na nia moja na hatimaye utakatifu wa pamoja[121].
Na hivyo watamfuata Kristo aliye asili ya uzima[122]
katika furaha na majitoleo (gaudis et sacrificiis) ya wito wao. Na
kwa njia ya upendo wao mwaminifu wapate kuwa mashahidi wa lile fumbo la
pendo ambalo Bwana amelifunua kwa ulimwengu, kwa njia ya kifo na ufufuko
wake[123].
Sura ya Pili
KUSTAWISHA MAENDELEO YA UTAMADUNI
Utangulizi
53. Ni sifa maalum ya binadamu kuweza kukifikia kiwango cha maisha
kinacholingana kweli na kikamilifu na hali ya kiutu kwa njia ya utamaduni
tu, yaani kwa kustawisha hazina na tunu za maumbile. Kwa hiyo, kila
kunapokuwa na suala liyahusuyo maisha ya kibinadamu, maumbile na utamaduni
huungana kiundani.
Kwa ujumla neno “utamaduni” lataka kumaanisha mambo yale yote ambayo
kwayo binadamu huboresha na kuvitokeza vipawa vyake vingi vya kimwili na
kiroho. Tena kwa njia yake binadamu hujibidisha kuutawala ulimwengu wenyewe
kwa ujuzi na kazi [yake]. Kadhalika, huyafanya maisha ya kijamii yawe ya
kiutu zaidi, katika familia na pia katika jamii nzima, kwa njia ya maendeleo
ya desturi na ya taasisi mbalimbali. Kisha, katika mfuatano wa majira,
hutokeza, hushirikisha na kuhifadhi katika matendo yake mang’amuzi na
matarajio makuu ya kiroho ili yaweze kuyasaidia maendeleo ya walio wengi au,
zaidi, ya wanadamu wote.
Kwa sababu hiyo hutokea kwamba utamaduni ni lazima uwe na mandhari mbili,
yaani ya kihistoria na ya kijamii; na neno “utamaduni” linachukua mara
nyingi maana inayohusu elimujamii (sosiolojia) na sayansi ya makabila
(ethnolojia). Kwa maana hiyo, ndipo inapoongelewa juu ya wingi wa tamaduni
mbalimbali. Hivyo, hali tofauti za maisha ya kawaida na mitindo mbalimbali
ya kuyaratibisha mema yake vina asili yake katika namna tofauti za kutumia
vitu, kufanya kazi, kujieleza, kufuata dini, kuunda desturi, kutunga sheria
na kuzishughulikia, kuendeleza sayansi na sanaa na kuustawisha uzuri. Kwa
hiyo, desturi za kimapokeo zinaunda urithi mahsusi wa kila jumuiya ya
kibinadamu. Kadhalika, yanatengenezwa mazingira maalum ya kihistoria ambamo
wanadamu wa kila taifa na wakati wanaingia, na ambamo kutoka humo huchota
yale mema yanayomwezesha kukuza ustaarabu.
Ibara ya kwanza
HALI YA UTAMADUNI KATIKA ULIMWENGU WA SASA
Mitindo mipya ya maisha
54. Hali za maisha ya siku hizi zimebadilika sana katika nyanja za
kijamii na kiutamaduni, hivi kwamba ni halali kuuita wakati huu kuwa ni
kipindi kipya cha historia ya kibinadamu[124].
Na tokea hapo zinafunguliwa njia mpya za kuboresha na kushamirisha zaidi
utamaduni. Nazo zimeandaliwa kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi ya
kimaumbile, ya watu, na ya kijamii; na pia kutokana na maendeleo ya
kitekniki na ya uvumbuzi na uratibishaji wa mfumo wa vyombo vya upashanaji
habari. Kwa hiyo, tabia ya utamaduni wa siku hizi ina mengine ya pekee kama
haya yafuatayo: sayansi ziitwazo kamili zinakuza sana uwezo wa kupambanua
mambo (iudicium criticum); utafiti wa kisaikolojia wa siku hizi
unaeleza kwa undani zaidi utendaji wa kibinadamu; sayansi za kihistoria
zinafaa sana ili kutathmini mambo katika mtazamo wa mageuzo na maendeleo
yao; mitindo ya maisha na desturi zinazidi kulingana kati yao. Mfumo wa
viwanda (industrializatio), kupanuka kwa uhamiaji mjini (urbanizatio),
na mambo mengine yanayohamasisha maisha ya pamoja kijamii (vitam
communitariam) yanaleta mitindo mipya ya utamaduni (unaolingana kwa wote
= mass-culture). Tangu hapo zinazaliwa namna mpya za kufikiri, za kutenda,
na za kutumia muda wa mapumziko; kukua kwa mawasiliano kati ya mataifa
mbalimbali na kati ya matabaka ya kijamii kunawafungulia wote, na kwa kila
mmoja, hazina za aina mbalimbali za utamaduni. Na hivyo, polepole unaundwa
mtindo wa utamaduni ambao ni wa kiulimwengu zaidi (universalior); nao
utahamasisha na kuonyesha umoja kati ya wanadamu kwa kadiri ileile ambavyo
unavyouheshimu upekee wa tamaduni mbalimbali.
Binadamu mtendaji wa utamaduni
55. Katika kila taifa na tabaka ya kijamii inazidi idadi ya wanaume na
wanawake wanaotambua kuwa ni watengenezaji na watendaji wa utamaduni wa
jumuiya zao. Ulimwenguni kote hisia za kujitegemea na za uwajibikaji
zinazidi kukua; na jambo hilo ni la muhimu sana kwa ukomavu wa kiroho na
kimaadili wa wanadamu. Nalo linajitokeza kinaganaga zaidi tukiuzingatia
muungano wa ulimwengu mzima, pamoja na wajibu unaotulazimu kuijenga dunia
iliyo nzuri zaidi katika ukweli na haki. Hivyo sisi tunashuhudia kuzaliwa
kwa ubinadamu, au humanismi (humanismus), mpya unaomfanya mtu
ajitambulishe kwanza kwa uwajibikaji wake mbele ya wenzake na mbele ya
historia.
Matatizo na wajibu
56. Katika hali ya namna hii haishangazi ikiwa binadamu, anayejisikia mwenye
wajibu katika maendeleo ya utamaduni, huwa na matumaini makubwa zaidi,
lakini vilevile anatazama kwa fadhaa migongano iliyomo na ambayo anapaswa
kuitatua.
Je, yapaswa kufanya nini ili ongezeko la mahusiano ya kiutamaduni lisichafue
maisha ya kijamii, wala lisivunje busara ya mababu na kuhatarisha tabia
maalum ya kila taifa? Maana mahusiano hayo yangepaswa kuleta mjadala wenye
kuzaa matunda kati ya matabaka na mataifa mbalimbali.
Je, ni kwa vipi kasi na kupanuka kwa utamaduni mpya vitaweza kuhamasishwa
bila ya kupoteza uaminifu hai kwa urithi wa mapokeo? Suala hilo linahitaji
utatuzi wa haraka hasa pale ambapo utamaduni unaotokana na maendeleo makubwa
ya kisayansi na kiteknolojia lazima ulinganishwe na ile heshima ya akili
ambayo, kadiri ya mapokeo mbalimbali, inalishwa na elimusanaa (
studiis
classicis).
Fani mbalimbali za sayansi zinaendelea kuongezeka na kutawanyika haraka.
Je, kwa njia ipi mtawanyiko wa fani hizi unaweza kupatanishwa na haja ya
kuzirudisha [hizo fani] katika hali ya usanisi, na haja ya kutunza katika
binadamu uwezo wake wa kutafakari na kushangaa unaomwongoza katika kuifikia
hekima?
Je, inabidi kufanya nini ili wanadamu wa dunia nzima washirikishwe katika
mema ya utamaduni, wakati ambapo utamaduni wa mabingwa unazidi kuwa wa ndani
na changamano?
Kisha je, yatupasa kufanya nini ili kutambua uhalali wa utamaduni wa
kujiratibisha – na ndivyo unavyodai – bila kunaswa na humanismi
inayozingatia mambo ya dunia tu, au pengine unaopinga wazi dini yenyewe?
Hata katika hoja hizo zipinganazo kati yao, siku za leo utamaduni wa
kibinadamu hauna budi kujiendeleza hivi kwamba uweze kustawisha utu wa
binadamu katika uzima wake na kwa utaratibu ufaao. Aidha kwamba uweze
kuwasaidia watu kuyatekeleza majukumu yao ambayo wote, lakini hasa wakristo,
waliounganika kidugu katika familia moja ya kibinadamu, wanaitwa
kuyatimiliza.
Ibara ya pili
KANUNI KADHAA ZIONGOZAZO USTAWISHAJI UFAAO WA UTAMADUNI
Imani na utamaduni
57. Wakristo, wanaosafiri kuuelekea mji wa mbinguni, hupaswa kuyatafuta na
kuyaonja mambo yaliyo juu
[125].
Hata hivyo, jambo hili halipunguzi, bali linakazia umuhimu wa wajibu wao wa
kushirikiana na watu wote, ili kuujenga ulimwengu ulio wa kiutu zaidi. Na ni
yakini kwamba fumbo la imani ya kikristo linawapatia vihimizo na misaada
bora ili kutekeleza wajibu huo kwa juhudi kubwa zaidi. Tena linawahimiza na
kuwasaidia hasa kutambua maana kamili ya kazi hiyo, ambayo kwayo utamaduni
wa kibinadamu utaweza kushika nafasi ya pekee katika wito mzima wa binadamu.
Maana binadamu analima ardhi kwa kazi ya mikono yake au kwa msaada wa
teknolojia ili itoe mazao na ipate kuwa maskani inayoistahili familia ya
dunia nzima. Tena, binadamu anashiriki kwa uwajibikaji maisha ya makundi
mbalimbali ya kijamii. Basi, wakati huohuo anatimiza mpango wa Mungu,
uliodhihirishwa tangu mwanzo wa nyakati, wa kuitawala dunia[126]
na kuukamilisha uhulushi; na hatimaye kujisitawisha yeye mwenyewe. Aidha,
anaishika amri kuu ya Kristo ya kujitoa mhanga kwa utumishi wa ndugu zake.
Licha ya hayo binadamu anajishughulisha na fani mbalimbali za taaluma kama
vile falsafa, historia, hisabati, sayansi ya kimaumbile na sanaa. Na hivyo
huweza kuchangia kwa vikubwa katika kukuza familia ya wanadamu ili izifikie
fikra zilizo bora zaidi mintarafu ukweli, wema na uzuri; tena kusudi iufikie
mtazamo wa thamani za mambo ulio sawa kwa ulimwengu mzima (iudicium
universi valoris). Kwa njia hii familia ya wanadamu itaangazwa wazi
zaidi na ile Hekima ya ajabu iliyokuwa pamoja na Mungu tangu milele,
ikipanga vitu vyote pamoja naye, ikifurahia nchi yote iliyokaliwa, na furaha
yake ikiwa ni kukaa pamoja na wanadamu[127].
Kwa sababu hiyo roho ya kibinadamu ikiwa huru zaidi mbali na utu-mwa wa
mambo ya kidunia inaweza kujiinua upesi zaidi kumwabudu na kumtazama Mungu
Muumba. Na zaidi, ikisukumwa na neema ya Mungu, hujiweka tayari kumtambua
Neno wa Mungu ambaye, kabla ya kutwaa mwili ili kuvikomboa na kuvijumlisha
vyote ndani yake, tayari alikuwepo ulimwenguni kama “nuru halisi
inayomwangaza kila mtu” (Yn 1:9)
[128].
Bila shaka, maendeleo ya nyakati zetu ya sayansi na teknolojia hayawezi
kufumbua sababu za ndani za mambo kwa njia ya mbinu zake; na hivyo yanaweza
kusababisha kustawi kwa namna fulani ya ufenomeni na uagnostiki (
phenomenismo
et agnosticismo) pale ambapo mbinu za utafiti zinazotumika katika fikra
hizi zinakuzwa bila haki kuwa kanuni kuu kupita zote katika harakati za
kuutafuta ukweli wote. Zaidi, kuna hatari ya kwamba binadamu, akiutegemea
mno ugunduzi wa siku za leo, huanza kudhani kuwa anajitosheleza na wala
hayatafuti tena mambo ya juu.
Lakini mambo hayo ya kulaumiwa si lazima yatokane na utamaduni wa kisasa
tu, wala yasitutie katika kishawishi cha kukana tunu zake zilizo nzuri.
Miongoni mwa tunu hizo hutajwa hizi zifuatazo: taaluma ya kisayansi na
uaminifu wa utafiti wake kwa ajili ya ukweli; ulazima wa kushirikiana na
makundi mengine ya mafundi stadi; hisia ya mshikamano wa kimataifa; kustawi
kwa utambuzi wa uwajibikaji wa mafundi katika kuwasaidia na kuwalinda
wanadamu [wenzao]; moyo wa kuboresha zaidi hali za maisha ya wote, hasa ya
wale wanaoteswa kwa kunyimwa uwajibikaji wao ama kwa uduni wa utamaduni.
Mambo hayo yote kwa namna fulani yanaweza kuwa kama maandalizi ya kuipokea
habari ya Injili. Na maandalizi hayo yaweza kukolezwa na Yule aliyekuja
kuukomboa ulimwengu.
Mahusiano ya namna nyingi kati ya Habari Njema ya Kristo na utamaduni
58. Kuna mahusiano ya namna nyingi kati ya ujumbe wa wokovu na utamaduni wa
kibinadamu. Maana, Mungu alipojidhihirisha kwa taifa lake, mpaka utimilifu
wa ufunuo wake katika Mwanae aliyefanyika mwili, alinena kadiri ya utamaduni
halisi wa kila kipindi cha historia.
Kadhalika Kanisa, ambalo limeishi katika mfululizo wa karne nyingi katika
hali mbalimbali, limetumia tamaduni tofauti ili kueneza na kufafanua ujumbe
wa Kristo katika mahubiri yake kwa watu wote. Tena [limetumia tamaduni
mbalimbali] katika kuuchunguza na kuuelewa [ujumbe huo] ili kuuonyesha
vizuri zaidi katika maisha ya kiliturujia na katika mitindo mingi ya maisha
ya jumuiya ya waamini
Lakini wakati huohuo Kanisa, likitumwa kwa mataifa yote ya nyakati zote na
ya mahali pote, halifungamani katu na kabila au taifa moja tu, wala
halifungamani na mtindo mmoja tu maalum wa maisha, wala halifungamani na
desturi ya pekee, iwe ya zamani au mpya. Bali Kanisa ni aminifu kwa mapokeo
yake, na vilevile linauzingatia utume wake wa kiulimwengu; nalo linaweza
kushiriki katika aina za utamaduni zilizo mbalimbali. Aidha, ushirika huu
unalitajirisha Kanisa lenyewe na, vilevile hizo tamaduni mbalimbali.
Habari njema ya Kristo yafanya upya daima maisha na utamaduni wa binadamu
aliyeanguka, na inapinga na kuondosha makosa na mabaya yatokanayo na
mvuto wa dhambi ambao daima huhatarisha maisha ya watu. Tena inayatakasa na
kuyainua maadili ya mataifa bila kukoma; kwa utajiri utokao juu
inazirutubisha kwa undani, inaimarisha, inakamilisha na kuzifanya upya
katika Kristo sifa za kiroho na vipawa vya kila taifa[129].
Kwa njia hii Kanisa linatekeleza utume wake[130],
na papo hapo linahamasisha na kutoa mchango wake kwa utamaduni wa kibinadamu
na wa kijamii; na hatimaye, kwa utendaji wake, hata wa kiliturujia, linamlea
binadamu katika uhuru wa ndani.
Kuoanisha mitindo mbalimbali ya utamaduni
59. Kwa sababu zilizotolewa hapo juu, Kanisa linawakumbusha wote kuwa
utamaduni lazima ulenge katika ukamilifu wa mtu mzima na pia katika manufaa
ya jamii na ya wanadamu wote. Kwa hiyo ni lazima kuistawisha roho [ya
binadamu] ili kwamba uwezo wake wa kushangaa, wa utambuzi wa ndani na wa
taamuli upate kukuzwa; naye ajipatie pia uwezo wa kupambanua mambo, kulisha
utambuzi wake wa kidini, kimaadili na kijamii.
Maana utamaduni, ukitokana na tabia ya kirazini na ya kijamii (
indole
rationali et sociali) ya binadamu, unahitaji daima uhuru ule ulio wa
haki ili usitawi, na pia unatakiwa kutambuliwa una uhalali wa kujiratibisha
kadiri ya kanuni zake wenyewe. Kwa haki basi utamaduni hudai heshima na
ustahilivu wa kuhifadhiwa, ila zitunzwe haki za kiutu na za kijamii za kila
mahali na za ulimwengu mzima, ndani ya mipaka ya manufaa ya wote.
Mtaguso Mkuu unayakumbusha yale yaliyofundishwa katika Mtaguso wa Vatikano I
na kuthibitisha kwamba “kuna taratibu mbili tofauti za ujuzi”,
zisizochangamana, yaani ya imani na ya akili. Na Kanisa halipigi marufuku
kwamba “sanaa za kibinadamu na sayansi zitumie kanuni na mbinu zake kila
moja katika uwanja wake”; kwa hiyo [Kanisa], “likiutambua uhuru huo wa haki”
linauthibitisha uwezo ulio halali wa utamaduni, na hasa wa sayansi, wa
kujiratibisha
[131].
Hayo yote yanadai kwamba pia binadamu, akiheshimu utaratibu wa maadili na
manufaa ya wote, huweza kuuchunguza ukweli kwa uhuru, kujulisha na kueneza
maoni yake na kujishughulisha na sanaa yoyote ile; na hatimaye mambo hayo
yanadai binadamu ataarifiwe vilivyo kadiri ya ukweli wa matukio yauhusuyo
umma
[132].
Sio wajibu wa serikali kuunda sura maalum ya mitindo mbalimbali ya
utamaduni, bali kushughulika ili mazingira na misaada inayoweza kuhamasisha
maisha ya kiutamaduni ya watu wote na ya kila kundi japo dogo katika taifa
ipatikane[133]. Kwa hiyo, ni
lazima kwanza kutilia mkazo kuwa utamaduni usipotoshwe katika kulifuata
lengo lake na usilazimishwe kuvitumikia vyombo vya siasa na vya uchumi.
Ibara ya Tatu
BAADHI YA NYAJIBU MUHIMU ZA WAKRISTO KUHUSU UTAMADUNI
Kutambua haki ya kila mtu kuhusu elimu na utamaduni, na utekelezaji wake
60. Nyakati zetu upo uwezekano wa kuwaokoa watu wengi sana katika hali duni
itokanayo na ujinga. Nao ndio wajibu mkubwa katika siku za leo, hasa kwa
wakristo; yaani kufanya kazi bila kuchoka, ili haki za msingi kwa watu wote
kuhusu utamaduni wa kibinadamu na wa kijamii zitambuliwe na kutekelezwa
popote, katika nyanja za uchumi na siasa, katika kila taifa na kati ya
mataifa. Na hatimaye haki hizo zilingane na hadhi ya kiutu, pasipo ubaguzi
wa kikabila, wa kijinsia, kitaifa, kidini au wa kijamii. Kwa hiyo inatakiwa
kuwapatia watu wote mafaa ya kiutamaduni mengi ya kutosha, hasa yale
yanayounda
utamaduni uitwao wa msingi; hivyo watu wengi sana
wasizuiliwe kutoa mchango wao wa kiutu kwa manufaa ya wote, kutokana na
ujinga wa kutojua kusoma na kuandika au kwa sababu ya kunyimwa utendaji
mwajibifu.
Kwa hiyo, inabidi kufanya kila juhudi ili wote wenye uwezo wapate kuingia
katika masomo ya juu. Nao, kwa njia hii na kwa kadiri iwezekanavyo, wataweza
kushughulikia katika jamii ya kibinadamu na majukumu, wajibu na huduma
zilinganazo na maelekeo yao ya kimaumbile pamoja na ufundi walioupata
[134].
Kwa hiyo, kila mtu na makundi ya kijamii ya kila taifa, wataweza kuyafikia
maendeleo kamili ya maisha yao ya kitamaduni kwa mujibu wa vipawa vyao na
mapokeo yao maalum.
Aidha, lazima kutumia kila jitihada ili kuwafanya watu wote waelewe haki
yao kuhusu elimu na pia wajibu wao wa kujiendeleza na kuwasaidia wengine.
Pengine zipo hali za maisha na za kazi zinazowazuia wanadamu katika bidii
yao ya kujielimisha na hivyo zinaua hamu ya elimu ndani yao. Hilo lawahusu
hasa wakulima na wafanyakazi wa viwandani ambao inabidi wapatiwe hali ya
kazi isiyozuia maendeleo yao ya kielimu na kitamaduni, bali
inayoyahamasisha. Wanawake wameshaanza kufanya kazi katika fani zote za
maisha; ingefaa sasa wapate uwezo wa kuzitekeleza kikamilifu wajibu zao
kadiri ya maumbile yao ya pekee. Na itakuwa wajibu wa wote kufanya
ushirikiano wa wanawake katika maisha ya kitamaduni, ulio maalum na wa
lazima, utambuliwe na kuhamasishwa.
Kumwelimisha binadamu katika utamaduni mzima
61. Siku hizi ni vigumu zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma kuunganisha
katika usanisi fani mbalimbali za sanaa na ujuzi. Maana wakati matawi ya
utamaduni yanapopanuka na kutofautiana, ndipo wakati huohuo uwezo wa kila
mtu wa kuyaelewa na kuyaunganisha pamoja unapungua, hivi kwamba picha ya
“binadamu wa ujuzi wa fani zote” (
imago “hominis universalis”)
inazidi kufifia. Lakini hata hivyo kila mtu anawajibika kushikilia dhana ya
“binadamu katika utu wake mzima”, ambaye ndani yake zinajitokeza tunu za
akili, utashi, dhamiri, na udugu. Nazo zina msingi wake katika Mungu
Muumbaji na zimeponywa na kukuzwa kwa namna ya ajabu ndani yake Kristo.
Awali ya yote familia ndiye mama na mlishi wa elimu hii. Ndani yake watoto,
wakiishi katika mazingira ya upendo, hujifunza kwa urahisi utaratibu mnyofu
wa mambo; na papo hapo mitindo ya utamaduni iliyokwisha kuthibitishwa
inapokelewa na roho ya kijana anayekua.
Kwa ajili ya elimu hiyohiyo, katika jamii za kisasa kuna nafasi nyingi
zinazoweza kustawisha utamaduni wa kiulimwengu (
universali culturae).
Na hizo nafasi hutokana hasa na ongezeko la usambazaji wa vitabu pamoja na
vyombo vipya vya upashanaji habari vya kiutamaduni na kijamii. Kupunguzwa
kwa masaa ya kazi karibu mahali pote kunazidisha siku kwa siku nafasi kwa
watu wengi ya kujielimisha. Wakati wa mapumziko (
otio) utumike
ipasavyo kwa kuiburudisha roho na kuiimarisha afya ya kiroho na ya kimwili
kwa njia ya shughuli na masomo ya hiari; tena kwa safari za kitalii katika
nchi nyingine, ambazo kwazo roho ya binadamu inakamilishwa, na watu
wanajitajirisha kwa kufahamiana wao kwa wao. Aidha, afya ya kiroho na ya
kimwili inaweza kuimarishwa kwa mazoezi na kwa mao-nyesho ya michezo, ambayo
inasaidia kudumisha usawa wa kiroho (
equilibrium) pia katika jumuiya.
Pamoja na hayo, huweza pia kutoa mchango wake katika kustawisha mahusiano ya
kidugu kati ya wanadamu wa hali zote, na wa mataifa na makabila mbalimbali.
Basi, wakristo washiriki mambo hayo ili maonyesho na matendo ya kiutamaduni
ya umma ya nyakati zetu yakolezwe na roho ya kiutu na ya kikristo.
Lakini, misaada hiyo yote haiwezi kukamilisha malezi yote ya kiutamaduni
ya binadamu kama wakati huohuo asipojihoji kiundani juu ya maana ya
utamaduni na ya sayansi mintarafu utu wa binadamu.
Ulinganifu kati ya utamaduni wa kibinadamu na mafundisho ya kikristo
62. Kanisa limechangia kwa vikubwa katika maendeleo ya utamaduni; lakini
mang’amuzi huonyesha kwamba, kutokana na sababu nasibu (
ex causis
contingentibus), ulinganifu baina ya utamaduni na malezi ya kikristo
pengine unatekelezwa kwa shida.
Matatizo haya si lazima yaidhuru imani; bali yanaweza kuihimiza roho
kuielewa kwa makini na kwa undani zaidi imani yenyewe. Maana utafiti wa siku
hizi na magunduzi mapya ya sayansi, ya historia na ya falsafa vinazusha
masuala mapya yaletayo matokeo yake pia katika maisha ya kila siku; nayo
yanadai utafiti mpya kwa upande wa wanateolojia. Aidha, wanateolojia
wanaalikwa kuzitafuta daima namna za kufaa zaidi ili kuwaeleza wanadamu wa
nyakati zao mafundisho ya kikristo; ila waheshimu mbinu na madai maalum ya
sayansi ya kiteolojia. Maana kitu kimoja ni hazina au kweli za imani, na
kitu kingine tofauti ni namna hizo [hazina au kweli] zinavyoelezwa; ijapo
kiini na maana yake ya ndani ni vilevile tu
[135].
Tena katika uangalizi wa kichungaji zijulikane na kutumiwa kwa namna
maridhawa kanuni za teolojia na pia ugunduzi wa sayansi za kidunia. Na
miongoni mwake yazingatiwe hasa mang’amuzi ya elimunafsi na elimujamii
(saikolojia na sosiolojia), hivi kwamba hata waamini waongozwe kuyafikia
maisha ya imani yaliyo safi na makomavu zaidi.
Pia fasihi na sanaa, kwa namna zake, ni muhimu sana kwa maisha ya Kanisa.
Maana, zinafanya juhudi ili kuijua tabia mahsusi ya binadamu, pamoja na
matatizo na mang’amuzi yake katika bidii anayoifanya ya kujifahamu na
kujikamilisha mwenyewe na ulimwengu mzima. Tena [fasihi na sanaa]
hujishughulisha kuitambua hali ya binadamu katika historia na katika
ulimwengu, kufafanua unyonge na furaha [zake], na hatimaye kueleza mahitaji
na uwezo wake, pamoja na kuidokeza hali ya kiutu iliyo nzuri zaidi. Na hivyo
sanaa hizo huweza kuyainua maisha ya kibinadamu zinayoyaeleza kwa namna
nyingi, kadiri ya mahali na nyakati.
Kwa hiyo, lazima bidii ifanyike ili wale wanaoshughulikia sanaa hizo
wajisikie kuwa Kanisa linathamini kazi yao; nao, wakiwa na uhuru wenye
utaratibu, waunde mahusiano rahisi zaidi na jumuiya ya kikristo. Tena Kanisa
liitambue mielekeo mipya ya kisanaa ilinganayo na nyakati zetu na iliyo
kadiri ya tabia ya mataifa na nchi mbalimbali. Nayo iingizwe pia katika
majengo kwa ajili ya ibada (sanctuario), iwapo, kwa mtindo ufaao na
kufuatia madai ya kiliturujia[136],
inaziinua kwa Mungu roho [za waamini].
Basi, kwa njia hii habari juu ya Mungu zitadhihirishwa wazi zaidi, na
mahubiri ya kiinjili yataeleweka kinaganaga zaidi katika akili za watu; nayo
yataonekana yanafungamana kiundani na hali ya maisha yao.
Kwa sababu hiyo waamini washirikiane sana na wanadamu wa nyakati zao, na
wajibidishe kupenya kikamilifu namna yao ya kufikiri na kuhisia, ambayo
utamaduni ni kielelezo chake. Na tena [waamini] wapate kuoanisha maarifa ya
sayansi mpya, ya mafundisho mapya na ya magunduzi ya hivi karibuni, na
maadili na fikra za kikristo. Na hivyo maisha ya kidini na unyofu wa
mwenendo viende, ndani yao [waamini], sambamba na elimu ya kisayansi na
maendeleo ya mfululizo ya kiteknolojia, hivi kwamba waweze kupambanua na
kufasiri mambo yote kwa hisia halisi za kikristo.
Wale wanaoshughulikia taaluma za kiteolojia katika seminari na vyuo vikuu
wajitahidi kushirikiana na watu ambao ni mabingwa katika taaluma nyingine,
wakiweka pamoja nguvu na kauli zao. Utafiti wa kiteolojia ujiendeleze katika
ujuzi wa kina wa ukweli uliofunuliwa. Lakini usipuuze kukabiliana na nyakati
zake, ili mabingwa katika fani mbalimbali za ujuzi waweze kusaidiana
kuufikia ufahamu wa imani ulio kamili zaidi. Na ushirikiano huo utaunufaisha
sana malezi ya wahudumu watakatifu kufasiri mafundisho ya Kanisa juu ya
Mungu, binadamu, na ulimwengu kwa namna iwafaayo zaidi watu wa nyakati zetu.
Na hapo wao watakuwa wepesi zaidi kuyapokea maneno yao[137].
Zaidi ya hayo Kanisa linatamani walei wengi wapate malezi yafaayo katika
sayansi za kidini. Na wengi kati yao wajiendeleze katika taaluma hizo na
wajipenyeze ndani yake kwa vyombo vya kisayansi vifaavyo. Lakini, ili waweze
kutekeleza wajibu huo, waamini hawa, wawe wakleri ama walei, wapewe uhuru –
kadiri ya haki – wa kutafiti, kufikiri, kuonyesha kwa unyenyekevu na ujasiri
maoni yao katika tawi la ufundi wao[138].
Sura ya Tatu
MAISHA YA KIUCHUMI NA KIJAMII
Baadhi ya sifa za maisha ya kiuchumi ya siku hizi
63. Pia katika maisha ya kiuchumi kijamii hadhi na wito halisi vya binadamu
lazima viheshimiwe na kusitawishwa, kama vile mafaa ya jamii nzima
.
Maana binadamu ni mtendaji, kiini na ukomo wa maisha ya kiuchumi kijamii.
Uchumi wa siku hizi, kadhalika kama fani nyingine zote za maisha ya kijamii,
una mfumo ambao kwao binadamu anazidi kuitawala huluka. Tena raia, makundi
na mataifa, yanazidi kuwasiliana na kutegemezana kati yao; kisha mamlaka ya
serikali inazidi kujihusisha [na masuala ya umma]. Kwa upande mwingine
maendeleo ya uzalishaji mali na ya mpango wa usambazaji wake pamoja na
huduma mbalimbali, yamefanya uchumi uwe chombo cha kufaa kwa kuyakidhi
vizuri zaidi mahitaji yaliyoongezeka ya familia ya wanadamu.
Hata hivyo, sababu za kuhangaika hazikosekani. Wanadamu wengi, hasa katika
nchi zilizoendelea kiuchumi, wanaonekana kuwa wanatawaliwa na madai ya
uchumi hivi kwamba karibu maisha yao yote ya kibinafsi na kijamii yanapenywa
na mawazo ya kiuchumi. Nazo zinaenea pia katika nchi zenye uchumi wa
kijamaa, pamoja na nchi nyingine. Tunaishi katika kipindi ambacho maendeleo
ya maisha ya kiuchumi yangeweza kupunguza tofauti za kijamii kama
yangeelekezwa na kupangwa kirazini na kulingana na hali za kibinadamu.
Lakini, mara nyingi mno maendeleo haya yanageuka kuwa sababu ya kuongeza
uzito wa tofauti hizo au pengine hata kurudisha nyuma hali za kijamii kwa
walio wanyonge, na hatimaye kuleta dharau kwa maskini. Wakati ambapo umati
mkubwa wa watu unakosa bado mahitaji yake ya lazima, wapo wengine, hata
katika nchi zenye maendeleo hafifu, wanaoishi katika utajiri kupindukia na
kutapanya mali. Anasa na umaskini vinakwenda sambamba. Na wakati watu
wachache wanapokuwa na uwezo mkubwa wa kuamua, basi wengi hukaribia kukosa
kabisa uwezekano wa kutenda kwa hiari yao na kwa uwajibikaji wao wenyewe. Na
hawa mara nyingi hubaki katika hali za maisha na za kazi zisizostahili utu
wa kibinadamu.
Ukosefu wa ulinganifu wa kiuchumi na wa kijamii namna hii unaonekana kati
ya kilimo, viwanda na idara mbalimbali za huduma; kama vile katika kanda
mbalimbali za nchi moja. Migogoro inayozidi siku kwa siku kati ya nchi
zilizoendelea zaidi kiuchumi na nchi nyinginezo inaweza kuihatarisha amani
katika ulimwengu mzima.
Watu wa siku hizi wanazidi kutambua kwa undani tofauti hizi zilizopo, maadam
wanaamini kwamba uwezo wa kiteknolojia na kiuchumi unaozidi kuwa mkubwa
katika ulimwengu wa leo, ungeweza na ungepaswa kusahihisha hali hii mbaya ya
mambo. Kutokana na hayo yanatakiwa mageuzi mengi katika maisha ya kiuchumi
kijamii, pamoja na mabadiliko katika namna ya kufikiri na ya kuishi, kwa
wote. Kwa lengo hilo Kanisa, katika mfululizo wa historia na hasa siku hizi,
limetunga na kuieleza miongozo kuhusu haki na usawa inayotakiwa na utaratibu
wa uadilifu. Nayo miongozo hutokana na mwanga wa Injili na kuyaelekea maisha
ya kibinafsi, ya kijamii na mahusiano ya kimataifa. Mtaguso Mkuu unadhamiria
kuithibitisha miongozo hii kutokana na hali ya siku hizi na kutoa maelekezo
kadhaa, hasa ukizingatia madai ya maendeleo ya kiuchumi
[139].
Ibara ya Kwanza
MAENDELEO YA KIUCHUMI
Maendeleo ya kiuchumi kwa huduma ya binadamu
64. Siku hizi kuliko huko nyuma lipo ongezeko la uzalishaji mali katika
fani za kilimo na viwanda, pamoja na la utoaji huduma mbalimbali. Nalo
linakusudia kwa haki kukidhi ongezeko la idadi ya watu na kutosheleza
matarajio ya wanadamu wote. Kwa hiyo tunapaswa kuhamasisha maendeleo ya
kiteknolojia, moyo wa kuleta mabadiliko, uanzishaji wa shughuli mpya na
ustawishaji wake. Tena tunapaswa kuhamasisha ulinganifu wa mbinu mbalimbali
za uzalishaji mali na bidii kabambe zinazofanywa na wale wanaoshiriki katika
uzalishaji huo. Yaani kwa neno moja, twatakiwa kuyahimiza yale yote
yanayochangia katika maendeleo haya. Zaidi, lengo la mwisho na la msingi la
maendeleo ya namna hii si tu kuongeza bidhaa zinazozalishwa, wala si
kutafuta tu faida na utawala wa uchumi. Bali lengo la mwisho na la msingi
lipo kwa ajili ya huduma ya binadamu, akitazamwa katika utu wake mzima,
yaani yakizingatiwa mahitaji yake ya kimwili pamoja na madai ya maisha yake
ya kifikra, kimaadili, kiroho na kidini. Tena yafaa yazingatiwe mahitaji ya
kila mtu, ya kila kundi, ya kila kabila, hatimaye pande zote za ulimwengu.
Kwa hiyo harakati yote ya kiuchumi lazima itekelezwe kadiri ya sheria na
mbinu maalum za uchumi, lakini katika mipaka ya utaratibu wa kimaadili[140],
ili ilingane na mpango wa Mungu juu ya binadamu[141].
Maendeleo ya kiuchumi kudhibitiwa na binadamu
65. Maendeleo ya kiuchumi lazima yabaki chini ya udhibiti wa binadamu, wala
hayawezi kuachwa chini ya uamuzi wa watu wachache ama makundi yenye uwezo
mkubwa mno wa kutawala uchumi. Tena maendeleo ya kiuchumi hayawezi kuamuliwa
na jamii za siasa tu, wala si na baadhi ya mataifa machache yenye nguvu
zaidi. Kinyume chake, yafaa kwamba idadi kubwa ya watu iwezekanavyo, wa kila
uwanja, washiriki kimatendo katika uongozi wake. Na vilevile, ikiwa ni suala
la mahusiano ya kimataifa, mataifa yote yashirikishwe katika uongozi huo.
Kadhalika, shughuli zote za hiari za watu binafsi na za mashirika yao
mbalimbali ni lazima yaungane na kulinganishwa ifaavyo na juhudi
zinazofanywa na serikali.
Maendeleo ya kiuchumi hayawezi kuachwa yajiongoze yenyewe kadiri ya utendaji
wake wa watu binafsi, wala chini ya uamuzi wa serikali tu. Kwa sababu hiyo,
lazima kukemea makosa ya zile itikadi ambazo, kwa kadiri
ya fikra za
uongo kuhusu uhuru, zinapinga mageuzi yaliyo ya lazima. Tena twapaswa kuonya
makosa ya zile [itikadi] ambazo hufuatisha haki za msingi za watu binafsi na
za makundi nyuma ya mfumo wa ujima wa uzalishaji mali (
organizationi
productionis collectivae)
[142].
Kwa upande mwingine, raia wote wakumbuke kwamba wana haki na wajibu wa
kuchangia katika maendeleo ya jamii yao wenyewe kadiri ya uwezo wao. Na haki
na wajibu hizo inabidi zitambuliwe pia na serikali. Matumizi ya mali zote
zilizopo yanatakiwa hasa katika nchi ambazo maendeleo yake ni duni zaidi.
Basi, papo hapo wale ambao wanalimbikiza mali zao bila kuzitumia, au pengine
wale ambao wanazinyima jamii zao misaada ya kimwili na kiroho inayohitajika
– isipokuwa haki ya kila mtu ya kuhamia – hawa hudhuru vibaya manufaa ya
wote katika jumuiya zao.
Tofauti kubwa za kiuchumi na kijamii zikomeshwe
66. Ili kukidhi madai ya haki na usawa lazima kujitahidi kwa kila hali ili
tofauti kubwa za kiuchumi zilizopo na pengine zinazokua ziondoshwe kwa upesi
iwezekanavyo, ila kwa heshima ya watu na ya tabia maalum ya kila taifa.
Maana tofauti hizi zinaleta ubaguzi katika haki za kibinafsi na katika hali
ya kijamii. Kadhalika, tukizingatia shida za pekee kwa upande wa fani ya
kilimo kuhusu uzalishaji mali na uuzaji wa mazao, tunaona kwamba katika
mahali pengi wakulima lazima wasaidiwe ili kuongeza kiwango cha uzalishaji
mali na uuzaji wake. Tena, wakulima inabidi wasaidiwe kutekeleza mabadiliko
yale yaliyo ya lazima na kubuni mbinu mpya zitakazotumika katika kufikia
kiwango cha mapato kitakiwacho, kusudi wasibaki katika hali duni ya kijamii
kama inavyotokea mara nyingi. Wakulima wenyewe, na hasa vijana, wajibidishe
kujiendeleza katika ustadi wao ambao, pasipo huo, kilimo hakiwezi
kustawishwa
[143].
Haki na usawa vinadai kwamba maisha ya watu binafsi na ya familia zao
yasitiwe mashaka na wasiwasi kwa sababu ya hali ya uhamishaji inayodaiwa
katika maendeleo ya kiuchumi. Kwa hiyo, mipango ya uhamishaji huo iratibiwe
ipasavyo. Aina yoyote ya ubaguzi katika ujira na kazi iepukwe kwa makini
mintarafu wafanyakazi ambao, wakitoka katika mataifa na nchi nyingine, kwa
kazi yao wanachangia kukuza uchumi wa taifa au eneo lilipo tofauti na lile
la asili. Aidha watu wote, na serikali ndiyo wa kwanza, hupaswa kuwapokea
wageni hawa kama binadamu, na wala si kama vyombo vitupu vya uzalishaji mali
tu; tena wote wanapaswa kuwasaidia ili waweze kuichukua familia pamoja nao
na kujitafutia makazi yastahiliyo; na hatimaye wote wanatakiwa kuwasaidia
kwa kuchukuliana na mfumo wa maisha ya kijamii ya taifa au nchi
inayowapokea. Lakini, bidii ifanyike ili nafasi za kazi zipatikane katika
nchi zao wenyewe kadiri iwezekanavyo.
Katika hali ya uchumi unaoendelea, juhudi lazima zifanyike ili kila mmoja
apate nafasi ya kazi ya kutosha na imfaayo pamoja na uwezekano wa kupewa
mafunzo ya kikazi na kiufundi. Kwa mfano, izingatiwe hali mpya ya jamii
inayotegemea uchumi wa viwanda ambapo mitambo inayojiendesha (automatio)
huzidi kutumiwa katika utekelezaji wa kazi. Kisha lazima riziki itolewe, na
heshima ya kiutu ihifadhiwe, kwa wale ambao wapo katika hali ngumu, hasa kwa
sababu ya ugonjwa au uzee.
Ibara ya Pili
KANUNI KADHAA ZA UTARATIBU KATIKA MAISHA YA KIUCHUMI
KIJAMII KWA UJUMLA
Kazi, hali zake na wakati wa mapumziko
67. Binadamu anatekeleza kazi yake ili kuzalisha na kubadilisha mali, na
kutoa huduma mbalimbali za kiuchumi. Kazi hiyo ina thamani kubwa zaidi
kuliko vipengele vingine vya maisha ya kiuchumi, kwa sababu hivi vingine ni
vyombo tu vinavyotumiwa ili kulifikia lengo fulani.
Maana kazi [ya binadamu], iwe inafanywa kwa kujitegemea, ama chini ya
uongozi wa watu wengine, hutokana moja kwa moja na mtu mwenyewe ambaye
anavitia viumbe kama muhuri wake na kuvitiisha chini ya utashi wake. Kwa
kazi yake, kwa kawaida mtu hupata riziki kwa ajili yake na ya familia yake,
hushirikiana na wenzie na kuwahudumia wanadamu nduguze; tena huweza kuishi
kwa upendo halisi na kuchangia kwa utendaji wake mwenyewe katika
kuukamilisha uhulushi wa kimungu. Zaidi, twajua kuwa binadamu, akimtolea
Mungu kazi yake, hushirikiana na tendo la ukombozi wa Yesu Kristo, ambaye
ameiweka kazi katika hali ya heshima kubwa akifanya kazi kwa mikono yake
mwenyewe huko Nazarethi. Hutokana na hayo, kwa kila mtu, wajibu wa kufanya
kazi kiaminifu, pamoja na haki ya kufanya kazi. Kadhalika, kwa upande
mwingine, ni wajibu wa jamii – kadiri ya hali yake – kuwasaidia raia ili
waweze kupata nafasi ya kazi ya kutosha. Aidha, kazi haina budi kulipwa kwa
kiasi kitoshacho ili kumpatia mtu binafsi na familia yake vifaa vya kutosha
kwa kuishi maisha yenye heshima kimwili, kijamii, kiutamaduni na kiroho. Na
mishahara hiyo ilingane na aina ya kazi pamoja na kiwango cha uzalishaji
mali cha kila mtu; kisha izingatiwe hali ya mwajiri na pia manufaa ya wote
[144].
Maadamu utendaji wa kiuchumi mara nyingi hutekelezwa kwa ushirikiano wa
watu wengi, basi si haki wala hailingani na hali ya kiutu kupanga kazi hiyo
kwa mfumo na utaratibu unaowanyanyasa wafanyakazi wawao wote. Lakini mara
nyingi mno, hata siku hizi, hutokea kwamba wafanyakazi wanafanywa kuwa
watumwa wa kazi zao. Jambo hilo haliwezi kabisa kupata udhuru yake kutokana
na sheria ziitwazo za kiuchumi. Basi, ni lazima kulinganisha mfumo wa kazi
yenye uzalishaji mali na madai ya binadamu pamoja na mtindo wa maisha yake,
kuanzia na maisha ya nyumbani, hasa kwa upande wa akina mama wenye familia.
Na vilevile jinsia na umri daima vizingatiwe. Aidha, wafanyakazi wapewe
fursa ya kutumia vipawa na hulka yao katika utekelezaji wa kazi yenyewe.
Wafanyakazi wote watekeleze kazi yao kwa uwajibikaji utakiwao wakitumia muda
na bidii yao; lakini hawa lazima wapewe pia muda wa kutosha kwa kupumzika na
kustarehe ili wapate kuyashughulikia maisha ya kifamilia, kiutamaduni,
kijamii na kidini. Zaidi wafanyakazi wote inabidi wapewe nafasi ya
kuzistawisha, kwa shughuli za hiari, zile nguvu na vipawa ambavyo pengine
haviwezi kukuzwa katika kazi zile walizopewa na waajiri wao.
Ushirikiano katika amala za biashara na katika mfumo wa kiuchumi kwa
ujumla. Migongano katika kazi
68. Katika makampuni ya kiuchumi wanaungana watu, yaani wanadamu walio huru
na wenye hiari ya kujiamulia mambo, walioumbwa kwa sura ya Mungu. Kwa hiyo
ushirikiano wa kimatendo wa wote katika kuendesha kampuni (inceptorum
curatione) lao uhamasishwe[145],
kwa mtindo unaopaswa kuamuliwa kwa namna ifaayo. Ila wadhifa wa kila mmoja –
yaani mmilikaji, mwajiri, viongozi na wafanyakazi – uzingatiwe, na umoja wa
uongozi unaodaiwa uhifadhiwe. Lakini mara nyingi maamuzi mintarafu hali za
kijumla zihusuzo masuala ya kiuchumi na kijamii hayachukuliwi katika kiwango
cha makampuni yenyewe, bali katika kile kiwango cha juu zaidi cha vyombo
maalum vinavyohusika na uongozi. Basi, maadamu mategemeo ya baadaye ya
wafanyakazi na ya watoto wao hutokana na maamuzi hayo, ni lazima hawa
washirikishwe kimatendo, wao wenyewe ama wawakilishi waliochaguliwa kwa
uhuru.
Miongoni mwa haki za msingi za binadamu hazina budi kuhesabiwa haki ya
wafanyakazi ya kuunda vyama vyao kwa uhuru, vinavyoweza kweli kuwawakilisha
na kuchangia katika kuratibu ipasavyo maisha ya kiuchumi. Tena, ihesabiwe
haki yao ya kuushiriki kwa uhuru utendaji wa vyama hivyo bila ya kuingia
katika hatari ya kuadhibiwa. Hivyo, wote watazidi kuelewa nafasi na
uwajibikaji wao kwa msaada wa ushirikiano ulioratibiwa namna hii, pamoja na
elimu ya kiuchumi na kijamii yenye kuongezeka. Kwa njia hiyo wafanyakazi
watajisikia kuwa ndio watendaji, kadiri ya uwezo na mwelekeo wa kila mmoja,
katika mfumo mzima wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na wa ujenzi wa manufaa
ya wote duniani kote.
Ikiwa itatokea migongano ya kiuchumi kijamii, kila juhudi lazima ifanyike,
ili kuufikia usuluhishi wa amani. Njia ya kwanza iwe ni mijadala ya kweli
kati ya makundi yanayohusika. Lakini hata hivyo katika mazingira ya siku
hizi mgomo unaweza kubaki kama njia pekee na ya lazima, ingawa ni ya mwisho,
ili kutetea haki za wafanyakazi na kukidhi matarajio yao ya haki. Lakini
njia zifaazo ili kuanzisha tena mijadala kwa maafikiano na usuluhishi
zifuatiliwe upesi iwezekanavyo.
Mali za dunia ni kwa ajili ya watu wote
69. Mungu ameiweka dunia na vyote viijazavyo kwa ajili ya matumizi ya
wanadamu wote na mataifa yote, hivi kwamba vitu vyote vilivyoumbwa lazima
vigawanywe kwa wote kwa kipimo kilicho sawa, haki ikiwa kiongozi na upendo
ukiwa mwenzi[146]. Kwa hiyo,
ni lazima daima kuridhisha makusudio ya kiumma ya mali (bonorum
universalem destinationem), bila kujali namna mbalimbali za umilikaji,
kulingana na kawaida zilizo halali za mataifa na kadiri ya mtazamo wa
mazingira mbalimbali yanayobadilika. Binadamu, katika kutumia mali hizo
anapaswa kutambua kuwa mali anazozimiliki kwa halali hazipo kwa ajili yake
tu, bali pia kwa ajili ya wengine kwa pamoja, kwa maana kwamba zinaweza
kumsaidia si yeye peke yake tu, bali pia wengine[147].
Licha ya hayo, ni haki ya watu wote kushiriki sehemu ya kutosha ya mali kwa
ajili yao na ya familia zao. Na ndivyo walivyoona kuwa ni haki Mababa na
Walimu wa Kanisa walipokuwa wakifundisha kwamba wanadamu wanalo sharti la
kuwasaidia maskini, wala si tu kuwapa yaliyo ya ziada[148].
Yule aliyepo katika shida ya lazima kabisa (extrema necessitate degit)
anayo haki ya kujipatia mahitaji kutokana na utajiri wa wengine[149].
Mtaguso Mkuu, ukizingatia idadi kubwa sana ya watu wanaoelemewa na njaa,
unawasihi hima wote, watu binafsi kwa serikali, ili wakumbuke tamko la
mababa, “Umlishe aliye kufani kwa njaa, maana kama hukumlisha umemwua”[150].
Hivyo, wote wawashirikishe kweli wengine mali zao na kuzitumia ifaavyo, kila
mmoja kadiri ya uwezo wake, hasa kwa kuwapatia watu binafsi na mataifa vifaa
ambavyo kwavyo wataweza kujiruzuku na kujiendeleza.
Mara nyingi katika jamii ambazo zina maendeleo duni kiuchumi, makusudio ya
kiumma ya mali yanazingatiwa walau kwa kiasi katika ujumla wa desturi na
kawaida za kijumuiya; maana hizo zinanuia kumsaidia mwanajumuiya katika
kupata mahitaji yaliyo ya lazima. Hata hivyo, haifai kudhani kwamba desturi
kadhaa haziwezi kubadilishwa katu ikiwa hazilingani tena na madai ya wakati
wa sasa. Na kwa upande mwingine, si vema kutenda lolote kiholela dhidi ya
desturi zile zilizo nyofu na ambazo hazikomi kuleta manufaa, ilimradi
zilingane ifaavyo na mazingira ya sasa. Kadhalika, katika nchi zilizoendelea
sana kiuchumi, mfumo wa taasisi za kijamii zinazoushughulikia misaada na
usalama wa kijamii unaweza kuchangia kiasi chake katika kuwafikishia watu
wote mali [hizo]. Aidha, ni muhimu sana kustawisha zaidi taasisi
ziihudumiazo familia na mahitaji ya kijamii, na hasa zile zizishughulikiazo
fani za utamaduni na elimu. Lakini katika harakati za kuzipanga taasisi hizo
lazima kukaa macho ili raia wasisukumwe kushikilia tabia ya wivu kuhusu
jamii, wala tabia inayopuuza uwajibikaji katika kazi, au inayokataa kutoa
huduma.
Vitegauchumi na fedha
70. Kwa upande wake vitegauchumi lazima vichangie katika kuwapatia watu
nafasi ya kufanya kazi, pamoja na mshahara wa kutosha kwa sasa na kwa siku
za mbele. Wale wote wanaowajibika katika vitegauchumi hivi na katika
kuratibisha maisha ya uchumi kwa ujumla – wawe watu binafsi, ama makundi, au
serikali – inawabidi wayazingatie malengo hayo na kuelewa wajibu wao mzito.
Nao wajibu utakuwa, kwa upande mmoja, kuangalia ili kila mtu na jumuiya
nzima wapate riziki zinazodaiwa kwa maisha yenye kustahili; kwa upande
mwingine, utakuwa muhimu kutambua mahitaji ya baadaye. Na hivyo wataleta
uwiano mzuri kati ya mahitaji ya sasa ya kibinafsi na ya kijamii na madai ya
kuweka vitegauchumi kwa ajili ya kizazi cha baadaye. Aidha, yazingatiwe
daima mahitaji ya haraka ya mataifa au nchi ambazo bado zina maendeleo duni.
Katika uwanja wa fedha kila mmoja ajihadhari na tendo la kudhuru manufaa ya
nchi yake au ya nchi nyingine. Kisha, suala la wale ambao ni wadhaifu
kiuchumi halina budi kushughulikiwa ili wasiathiriwe pasipo haki na
mabadiliko ya thamani ya fedha.
Haki ya kumiliki vitu, na mali ya binafsi; na juu ya mashamba makubwa ya
kibepari
71. Kumiliki vitu na aina nyingine za umilikaji wa kibinafsi juu ya mali za
nje (
bona exteriora) vinachangia kujidhihirisha kwa vipawa alivyo
navyo mtu. Aidha, vinampatia binadamu fursa ya kutoa mchango wake wa
uwajibikaji katika jamii na uchumi. Kwa sababu hiyo, ni muhimu sana
kuwasaidia watu wote, watu binafsi na makundi, wawe na kiasi fulani cha
umilikaji wa mali za nje.
Mali za binafsi au aina kadhaa za umilikaji wa mali za nje zinampatia mtu
nafasi iliyo ya lazima ya kujitegemea yeye na familia yake; tena hazina budi
kuhesabiwa kama mwendelezo wa uhuru wa binadamu. Nazo hatimaye,
zikiwahimiza watu kushikilia haki na wajibu zao, zinapata kuwa sharti
mojawapo la uhuru wa kiraia[151].
Namna za umilikaji huo na za mali hizi [za binafsi] zinajitokeza siku za leo
kwa mitindo mbalimbali na zinazidi kutofautiana kati yao siku kwa siku. Na
ingawa ipo misaada ya kijamii, haki na huduma zinazotolewa na jamii, hata
hivyo namna zote za umilikaji huo na za mali za binafsi zinaendelea kuwa
sababu kubwa za usalama. Na jambo hilo halihusu tu umilikaji wa mali
yakinifu (
proprietatibus materialibus), bali pia umilikaji wa
mali-akili, kama ulivyo ustadi katika nyanja mbalimbali za ufundi.
Haki ya kuwa na mali za binafsi haipingani na ile ya mitindo mbalimbali ya
umilikaji wa kiserikali (
proprietatum publicam). Lakini utaifishaji
wa mali hauwezi kutekelezwa isipokuwa na chombo chenye mamlaka, kadiri ya
madai ya manufaa ya wote na ndani ya mipaka yake, na hatimaye kwa fidia
iliyo ya haki. Aidha, ni juu ya serikali kuzuia mtu awaye yote asitumie
isivyo halali haki yake ya kumiliki mali, akihatarisha manufaa ya wote
[152].
Umilikaji-mali wa binafsi wenyewe kwa maumbile yake una dhima yake katika
jamii; nao una msingi wake katika sheria ya makusudio ya kiumma ya mali
[153].
Tukipuuza umuhimu wa dhima hiyo [ya mali ya binafsi katika jamii], umilikaji
unaweza ukawa chanzo cha choyo na cha fujo kali kwa namna nyingi. Na hivyo,
wapinzani wake wanaweza kwa urahisi kujipatia kisa cha kuhujumu haki yenyewe
ya umilikaji mali.
Katika nchi nyingi ambazo zina maendeleo duni kiuchumi, kunapatikana
umilikaji wa mashamba makubwa na pengine mapana sana, ambayo yanalimwa
kidogo tu au yanalala bure na kutunzwa kama akiba kwa sababu ya ulanguzi (lucri
causa), bila kulimwa. Na wakati huohuo umati wa watu hawana mashamba ya
kulima au wanatumia vishamba vidogo mno. Kwa upande mwingine haja ya
kuongeza uzalishaji wa mazao ni tatizo ambalo linadai kutatuliwa mapema.
Mara nyingi hutokea kwamba wale wanaoajiriwa na mabwana wao, yaani wale
wanaolima sehemu ya ardhi kwa kukabidhiwa tu, hao hupata mishahara au aina
nyingine za thawabu ambazo hazistahili hadhi ya binadamu, wala hawana makazi
ya heshima au hunyonywa na wanyapara. Na hivyo wakinyimwa usalama, huishi
katika hali ya kumtegemea mwingine kiasi kwamba wanazuiliwa kila uwezekano
wa kutenda kwa hiari na kwa kujiwajibisha wao wenyewe. Tena wanakatazwa kila
endeleo la kiutamaduni na kila ushirikiano wa kimatendo katika maisha ya
kijamii na ya kisiasa. Kwa hiyo, kadiri ya mazingira mbalimbali, yanadaiwa
mageuzi yanayokusudia kukuza mishahara, kuboresha hali katika kazi,
kustawisha uhakika wa ajira, na kuhamasisha hali ya kujituma kwa kila mmoja.
Aidha, yanadaiwa mageuzi yatakayowezesha kugawa yale mashamba yanayomilikiwa
tu bila kulimwa, kwa manufaa ya wale wenye uwezo wa kuzalisha. Kwa suala
hili, lazima vitolewe vifaa na vyombo vinavyodaiwa kwa lengo hilo, na hasa
misaada ya kielimu na kwa ajili ya kuunda mashirika (cooperativae)
yenye kuleta manufaa. Na pale ambapo manufaa ya wote yanadai kutaifishwa kwa
mali, basi fidia ihesabiwe kwa haki yakizingatiwa mazingira yote
yanayohusika.
Utendaji wa kiuchumi kijamii, na Ufalme wa Kristo
72. Wakristo wanaoshiriki kimatendo katika maendeleo ya kiuchumi kijamii ya
siku hizi na wanaotetea haki na mapendo, waamini kuwa wanaweza kuchangia kwa
vikubwa katika ustawi wa wanadamu na amani ya ulimwengu. Katika harakati za
namna hii watoe mfano bora, wakitenda kama watu binafsi ama kwa pamoja. Kwa
hiyo, wakishajipatia ujuzi na mang’amuzi yaliyo ya lazima kabisa, wakifanya
shughuli hizi za kidunia wauhifadhi utaratibu ulio mnyofu, wakiwa waaminifu
kwa Kristo na Injili yake. Na hivyo maisha yao yote, ya kibinafsi na ya
kijamii, yakolezwe na roho ya heri za kiinjili, hasa na roho ya umaskini.
Yule amfuataye Kristo kiaminifu huutafuta kwanza Ufalme wa Mungu. Naye
huchota kwake upendo imara na safi zaidi ili kuwasaidia ndugu zake wote na
kuyatimiza matendo ya haki chini ya uongozi wa mapendo[154].
Sura ya Nne
MAISHA YA JUMUIYA YA KISIASA
Maisha ya hadhara ya siku hizi
73. Katika nyakati zetu mageuzo ya ndani yanaonekana pia katika mifumo na
vyombo vya uongozi wa mataifa; nayo yanatokana na maendeleo ya kiutamaduni,
kiuchumi na kijamii ya mataifa. Mageuzo hayo yanaathiri sana maisha ya
jumuiya ya kisiasa, hasa katika uwanja wa wajibu na haki za watu wote kuhusu
matumizi ya uhuru wa kiraia na katika kupania manufaa ya wote. Tena, yana
nguvu kubwa juu ya uratibishaji wa mahusiano baina ya raia wenyewe na pia
kati ya raia na serikali.
Utambuzi hai wa hadhi ya binadamu katika mahali pengi duniani unaamsha
juhudi ya kuunda utaratibu wa kisiasa na kisheria ambapo haki za binadamu
katika maisha ya hadhara (
vita publica) zinalindwa vema zaidi. Nazo
ndizo haki za kujumuika na kuunda umoja kwa uhuru, haki ya kila mmoja kutoa
maoni yake na kukiri imani yake akiwa peke yake au hadharani. Maana, ulinzi
wa haki za binadamu ni sharti la lazima ili raia, kila mmoja peke yake au
kama wanachama, waweze kushiriki kimatendo maisha ya umma na uongozi wa
mambo yanayoyahusu.
Pamoja na maendeleo ya kiutamaduni, kiuchumi na kijamii, hamu ya walio wengi
ya kuchukua wajibu mkubwa zaidi katika kuratibu maisha ya jumuiya ya kisiasa
inazidi kupata nguvu. Katika dhamiri ya watu wengi bidii ya kuhifadhi haki
za makundi ya wachache katika nchi zao inastawi, lakini bila ya makundi hayo
ya wachache kusahau wajibu zao mbele ya jumuiya ya kisiasa. Aidha, inazidi
kukua heshima mbele ya watu wenye maoni au dini tofauti. Na wakati huohuo
ushirikiano mpana zaidi unaundwa; nao unalenga kwa raia wote – siyo kwa
wachache tu wenye marupurupu – ili wapate kutumia kimatendo haki zao za
binafsi.
Aidha, inalaumiwa mitindo yote ya kiserikali iliyomo katika nchi kadhaa
inayozuia uhuru wa kiraia au wa kidini, inayoongeza idadi ya wale wanaouawa
kwa choyo na jinai za kisiasa, na inayopotosha utekelezaji wa mamlaka kuhusu
manufaa ya wote ili kulinufaisha kundi moja au watawala wenyewe.
Ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya kibinadamu, hakuna lililo
bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upendo na huduma
kwa manufaa ya wote. Pia ni kuuimarisha msimamo (persuasiones) wa
msingi mintarafu maumbile halisi ya jumuiya ya kisiasa; tena kuhusu lengo,
matumizi ya halali na mipaka ya wajibu wa serikali.
Maumbile na lengo la jumuiya ya kisiasa
74. Wanadamu, familia na makundi mbalimbali, wanaounda jumuiya ya kiraia
wanaelewa vema kuwa peke yao hawawezi kujenga kikamilifu maisha ya kiutu.
Nao wanaona ulazima wa kuunda jumuiya iliyo pana zaidi, ambapo wote wataleta
mchango wa vipawa vyao kila siku[155],
ili kuyafikia zaidi na zaidi manufaa ya wote. Ndiyo maana hawa wanaunda
jumuiya ya kisiasa kadiri ya mitindo yake mbalimbali. Na jumuiya hiyo
imewekwa kwa ajili ya yale manufaa ya wote ambayo kwa ajili yake [jumuiya]
yenyewe inapata sababu na umaana wake kikamilifu. Hivyo, tokea hayo inapata
pia utaratibu wake wa kisheria, maalum na wa kimsingi. Na manufaa ya wote ni
ujumla wa zile hali za maisha ya kijamii ambazo kwazo wanadamu, familia na
vyama mbalimbali huweza kupata kikamilifu na upesi zaidi utimilifu wake[156].
Lakini, katika jumuiya ya kisiasa watu wengi hukusanyika pamoja walio
tofauti kati yao; nao kwa halali huweza kuelekea maamuzi yanayohitilafiana.
Ili jumuiya ya kisiasa isidhuriwe na tofauti za maoni ya kila mmoja basi ni
lazima uwepo uongozi wenye uwezo wa kuzielekeza nguvu za raia wote kuyafikia
manufaa ya wote. Nalo litekelezwe si kama mashine (mechanice), wala
si kwa mabavu, bali hasa kama nguvu ya kimaadili yenye msingi wake katika
uhuru na hisia ya uwajibikaji kwa jukumu lililochukuliwa.
Basi, ni wazi kwamba jumuiya ya kisiasa na mamlaka ya kiserikali vimeasisiwa
katika hali ya binadamu; navyo, kwa sababu hii, vimo katika utaratibu
uliowekwa na Mungu, ijapo uchaguzi wa utawala wa kisiasa, pamoja na uteuzi
wa watawala huachiwa maamuzi huru ya raia
[157].
Hufuata kuwa utawala wa kisiasa, uwe unatekelezwa na jumuiya yenyewe au na
vyombo vinavyowakilisha dola (
rem publicam), ni lazima daima ufanyike
ndani ya mipaka ya sheria ya kimaadili. Na lengo lake ni kuyafikia manufaa
ya wote, tena manufaa yenye maendeleo yake, kadiri ya kanuni za utaratibu wa
kisheria uliokwisha kuwekwa, au wa kuwekwa. Na hapo ndipo raia
wanapolazimishwa kutii kwa sababu ya dhamiri zao
[158].
Tokea hapo hueleweka wazi uwajibikaji, wadhifa na umuhimu wa uongozi wa
serikali.
Na pale raia wanapoonewa na serikali inayovuka mipaka ya madaraka yake,
ndipo wasikatae [kutii] kama yale yanayodaiwa ni kwa manufaa ya wote. Lakini
ni halali kwao kutetea haki zao na za raia wenzao dhidi ya matumizi mabaya
ya madaraka hayo, kwa kuheshimu mipaka iliyowekwa na sheria ya maumbile na
ya kiinjili.
Namna mbalimbali ambazo kwazo jumuiya ya kisiasa inaratibisha miundo yake
na utekelezaji wa madaraka ya kisiasa zaweza kutofautiana, kadiri ya tabia
za mataifa zilivyo mbalimbali, na ya maendeleo ya kihistoria. Lakini, daima
ni lazima zikusudie katika kumuunda mtu mwadilifu, mtulivu, na mkarimu kwa
wote, kwa manufaa ya familia nzima ya wanadamu.
Ushirikiano wa wote katika maisha ya hadhara
75. Inalingana kikamilifu na maumbile ya binadamu kwamba ipatikane miundo ya
kisiasa na kisheria inayowawezesha zaidi na zaidi raia wote – bila ubaguzi
wowote – kushiriki kwa uhuru na kwa matendo katika kutengeneza misingi ya
kisheria ya jumuiya ya kisiasa, katika kuongoza mambo ya dola, katika
kuainisha uwanja wa kazi na mipaka yake kwa taasisi mbalimbali, na hatimaye
katika kuwachagua viongozi
[159].
Kwa sababu hiyo, raia wote wakumbuke haki yao, ambayo pia ni wajibu, ya
kutumia kura yao huru kwa minajili ya kuhamasisha manufaa ya wote. Kanisa
linasifu na kuthamini wale ambao, kwa ajili ya kuwatumikia wanadamu,
wanajitoa kwa manufaa ya dola na kubeba uzito wa wajibu husika.
Ili ushirikiano wa raia pamoja na hisia zao za uwajibikaji ziweze kuleta
matokeo mazuri katika maisha ya kisiasa ya kila siku, utaratibu mzuri wa
kisheria unatakiwa, ambao utasaidia kupanga mgawanyo ufaao wa majukumu na wa
vyombo vya utawala pamoja na ulinzi imara na huru wa haki [za raia]. Haki za
watu, za familia na za makundi, pamoja na utekelezaji wake, ni lazima
zitambuliwe, ziheshimiwe na kuhamasishwa
[160];
kama vile pia wajibu zinazomkalia kila raia. Miongoni mwa wajibu hizi ni
vema kukumbushia wajibu wa kujishughulisha na mambo yauhusuyo umma na kutoa
huduma za kimatendo na kibinafsi zinazotakiwa kwa manufaa ya wote. Na
viongozi wajiepushe na kuweka vizuizi dhidi ya familia, makundi ya kijamii
na kiutamaduni, mashirika au taasisi za kati (
instituta intermedia);
wala wasiwanyime uwezo wao ulio halali na wenye manufaa wa kutenda kazi,
bali, kinyume chake, wavihamasishe vyombo hivyo kwa hiari na utaratibu. Na
kwa upande wao raia, kila mmoja binafsi na katika makundi, wasiipe serikali
uwezo mkubwa mno, wala wasiiombe masilahi kubwa mno isivyofaa. Maana hapo
kuna hatari ya kupunguza uwajibikaji wa watu, familia na makundi ya kijamii.
Katika nyakati zetu ugumu wa masuala yanayojitokeza unazilazimisha
serikali kujihusisha zaidi katika fani za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni
ili kuleta mazingira yanayofaa zaidi kusudi raia na makundi waweze
kuyafuatilia kwa bidii na kwa uhuru manufaa kamili ya binadamu. Uhusiano
kati ya ujamiisho (socializationem)[161]
na uwezo wa kujiratibisha na kujiendeleza kwa mtu binafsi unaweza kufikiriwa
kwa namna tofauti katika nchi mbalimbali za ulimwengu na kwa mujibu wa
maendeleo ya mataifa. Lakini pale ambapo utekelezaji wa haki unapunguzwa kwa
muda kwa ajili ya manufaa ya wote, basi mazingira yanapobadilika uhuru
urejeshwe mapema iwezekanavyo. Aidha, si ubinadamu kwa serikali kutumia
namna za utawala wa mabavu au za udikteta zinazovunja haki za mtu ama za
makundi ya kijamii.
Raia wastawishe upendo kwa taifa lao kwa ari na unyofu, lakini si kwa
mtazamo mfinyu, yaani hivi kwamba wayazingatie daima mema ya familia nzima
ya wanadamu inayounganika kwa vifungo mbalimbali kati ya makabila, mataifa
na nchi.
Wakristo wote hawana budi kufahamu kwa undani wito wao maalum katika jumuiya
ya kisiasa. Nao lazima wawe kielelezo angavu, wakikuza ndani yao hisia ya
uwajibikaji na ya kujitoa kwa manufaa ya wote. Na hivyo wabainishe pia kwa
matendo jinsi yanavyoweza kuafikiana mamlaka na uhuru, uanzishaji wa
kibinafsi na mshikamano wa mwili mzima wa kijamii, na hatimaye umoja ufaao
na utofauti uletao faida. Tena wakristo wanapaswa kukubali wingi wa maoni
ulio halali na tofauti zake mintarafu mambo ya dunia, na kuwaheshimu raia
ambao, hata katika makundi, hutetea kauli zao kwa unyofu. Vyama vya siasa
navyo havina budi kuyahamasisha yale yanayodaiwa na manufaa ya wote, kadiri
ya mtazamo wao; lakini kamwe si halali kutanguliza maslahi yao mbele ya
manufaa ya wote.
Aidha inapasa kushughulikia kwa bidii elimu ya kiraia na kisiasa iliyo ya
lazima siku za leo kwa watu wote, na hasa kwa vijana, ili raia wote waweze
kushika nafasi zao katika maisha ya jumuiya ya kisiasa. Wale walio tayari
kuishughulikia fani ya siasa iliyo ngumu lakini pia yenye ustahivu[162],
ama wale wanaoweza kujizatiti kwa ajili ya kazi hiyo, basi wajiandae na
kujibidisha ili kuitekeleza bila ya kujali manufaa yao wala maslahi ya pesa.
Nao watende kwa unyofu na busara dhidi ya udhalimu na uonevu, [dhidi ya]
utawala wa mabavu na ujeuri usio mvumilivu wa mtu mmoja au wa chama kimoja
tu; na hatimaye, wajitolee kiaminifu na pasina ubaguzi katika kutoa huduma
kwa wote, tena kwa mapendo na uimara utakiwao katika maisha ya kisiasa.
Jumuiya ya kisiasa na Kanisa
76. Ni muhimu sana hasa katika jamii inayozingatia wingi wa maoni na wa
taasisi (
societas pluralistica), kuchukulia kwa mtazamo ulio mnyofu
mahusiano kati ya jumuiya ya kisiasa na Kanisa. Tena, kuna umuhimu mkubwa
kutofautisha wazi kati ya matendo ambayo waamini wanayafanya kwa jina lao,
kibinafsi au katika makundi, kama raia wanaoongozwa na dhamiri ya kikristo,
na matendo wayafanyayo kwa jina la Kanisa katika umoja na wachungaji wao.
Kanisa halichangamani katu na jumuiya ya kisiasa, wala halifungamani na
mtindo wowote wa mfumo wa kisiasa kwa sababu ya majukumu na uhalali wake (
sui
muneris et competentiae). Nalo ni alama, pia ni ulinzi, wa tabia ya juu
kabisa ya binadamu.
Jumuiya ya kisiasa na Kanisa zina uhuru na mamlaka kila moja katika uwanja
wake. Na zote mbili zipo kwa ajili ya kutumikia wito wa binadamu, wake
binafsi na katika jamii, ijapo ni kwa msingi ulio tofauti. Nazo zitatekeleza
huduma zao hizi kwa ajili ya watu wote kwa namna inayozidi kuleta mafanikio
kwa kadiri ushirikiano kati yao unavyozidi kusitawishwa, na kulingana na
mazingira ya mahali na wakati. Binadamu hafungwi katika mipaka ya dunia hii
tu, bali, akiishi katika historia ya kibinadamu, huhifadhi kikamilifu wito
wake wa milele. Na Kanisa, lenye msingi wake katika upendo wa Mkombozi,
linachangia uenezaji wa haki na upendo katika kila taifa na kati ya mataifa
yote. Nalo huhubiri ukweli wa kiinjili na kuziangaza fani zote za utendaji
wa kibinadamu kwa mafundisho yake na kwa ushuhuda unaotolewa na wakristo. Na
hivyo, linaheshimu na kuhamasisha pia uhuru wa kisiasa na uwajibikaji wa
raia.
Mitume pamoja na waandamizi na wasaidizi wao, huku wakitumwa kuwahubiria
wanadamu Kristo, Mwokozi wa ulimwengu, katika kutekeleza utume wao
wanautegemea uweza wa Mungu, ambao mara nyingi sana hudhihirisha nguvu ya
Injili katika udhaifu wa mashahidi [wake]. Na wale wote wanaojitolea katika
utumishi wa Neno la Mungu, lazima watumie njia na mbinu maalum za Injili
ambazo zinahitilafiana katika sehemu nyingi na mbinu maalum za mji wa dunia
hii (
terrenae civitatis).
Ni kweli kwamba mambo ya dunia na yale ambayo, katika hali ya kibinadamu,
yanavuka mipaka ya ulimwengu huu, yameunganika kiundani. Na Kanisa lenyewe
linatumia mambo ya dunia kwa kiasi kitakiwacho na utume wake. Lakini, hata
hivyo haliweki tumaini lake katika fadhili (privilegiis) linazopewa
toka serikalini. Tena, litayaacha matumizi ya haki kadhaa lilizozipata kwa
halali pale ambapo litaona kuwa matumizi hayo yanaleta mashaka juu ya unyofu
wa ushuhuda wake au pale ambapo mazingira mapya yanadai utaratibu tofauti.
Lakini daima na popote iwe haki ya Kanisa kuihubiri imani kwa uhuru wa kweli
na kutoa mafundisho yake kuhusu jamii. Tena iwe haki yake kutekeleza utume
wake kati ya wanadamu bila vizuizi na kutoa hukumu zake za kimaadili, hata
juu ya masuala yahusuyo utaratibu wa kisiasa wakati jambo hilo linatakiwa na
haki za msingi za binadamu pamoja na wokovu wa roho za watu. Kanisa
litafanya hivi likizitumia njia zote, na zile tu, zinazolingana na Injili na
manufaa ya watu wote, kufuatana na tofauti za nyakati na za mazingira.
Nalo Kanisa, ambalo katika uaminifu wake kwa Injili na katika kutekeleza
utume wake ulimwenguni, limewajibika kuhamasisha na kukuza yale yote yaliyo
kweli, mema na mazuri katika jumuiya ya wanadamu
[163],
laimarisha amani kati ya watu kwa utukufu wa Mungu
[164].
Sura ya Tano
KUHAMASISHA AMANI
NA KUSTAWISHA JUMUIYA YA KIMATAIFA
Utangulizi
77. Katika miaka hii yetu mahangaiko na fadhaa vinavyotokana na mwendelezo
wa ukali wa vita au na tishio la vita linalotukabili, vinaendelea kuwasumbua
sana wanadamu. Na jamii nzima ya kibinadamu imeufikia wakati ulio muhimu
sana katika maendeleo ya ukomavu wake. Kwa upande mmoja wanadamu polepole
wanaendelea kuungana kati yao na mahali pote wanazidi kuelewa umoja wao.
Lakini wakati huohuo watashindwa kutimiza kazi inayotakiwa nao – yaani
kujenga ulimwengu uwe wa kiutu kwelikweli kwa watu wote na duniani pote –
kama wanadamu wenyewe hawataiongokea amani halisi kwa moyo mpya. Kwa sababu
hii habari ya Injili, maadamu inalingana na matarajio na malengo ya juu
zaidi ya wanadamu, inang’ara kwa mwangaza mpya inapowatangaza wenye heri
wanaofanya amani, “kwa maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mt 5:9).
Kwa hiyo Mtaguso, ukifafanua maumbile halisi na ya juu ya amani,
unashutumu ubaya usio na kipimo wa vita (belli immanitate damnata).
Tena unadhamiria kuwasihi kwa moyo wote wakristo ili, kwa msaada wa Kristo
ambaye ndiye mwenye kufanya amani, washirikiane na watu wote kusudi waasisi
kati ya wanadamu amani yenye msingi wake katika haki na upendo. Na hatimaye
waandae nyenzo za lazima ili kuifikia amani hiyo.
Maumbile ya amani
78. Amani siyo tu kutokuwepo kwa vita, wala haiwezi kupunguzwa kuwa tendo la
kudumisha uwiano kati ya nguvu zipinganazo. Tena amani si tu matokeo ya
utawala wa mabavu, bali inaitwa kwa usahihi kamili “kazi ya haki” (Isa
32:17). Amani ndilo tunda la utaratibu uliowekwa katika jamii ya wanadamu na
Mwasisi wake; nao hauna budi kutekelezwa na wanadamu watarajiao sana haki
iliyo kamili zaidi siku kwa siku. Maana manufaa ya pamoja ya wanadamu
yameratibiwa katika kiini chake na sheria ya milele, lakini katika
mwendelezo wa muda manufaa hayo hubadilika mara kwa mara kuhusu matakwa yake
ya kila siku. Ndiyo maana amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali
inadaiwa kujengwa siku kwa siku. Aidha, maadam utashi wa binadamu ni dhaifu
na umejeruhiwa na dhambi, kuleta amani kunadai siku zote kila mtu azitawale
tamaa zake, na serikali ijihusishe katika kulinda amani.
Lakini hayo hayatoshi. Hiyo amani haiwezi kupatikana hapa duniani ikiwa
mafaa ya watu hayalindwi na kama wanadamu hawawezi kubadilishana kwa
kuaminiana na kwa uhuru utajiri wa roho na akili zao. Utashi imara wa
kustahi utu wa watu wengine na mataifa mengine, pamoja na uzingativu thabiti
wa udugu wa wanadamu ni vya lazima kabisa katika kuijenga amani. Na hivyo
amani ndilo pia tunda la upendo unaozidi uwezo wa haki tupu.
Amani ya kidunia itokanayo na upendo kwa jirani ni mfano na matokeo ya amani
ya Kristo itokayo kwa Mungu Baba. Maana Mwana aliyefanyika mwili, Mfalme wa
amani, kwa njia ya msalaba wake amewapatanisha watu wote na Mungu. Naye,
akiurudisha umoja wa wote katika taifa moja na mwili mmoja, akaiua chuki
mwilini mwake
[165] na
hatimaye, katika utukufu wa ufufuko wake, akapuliza Roho wa mapendo mioyoni
mwa wanadamu.
Kwa hiyo wakristo wote wanaitwa kwa nguvu “kuishika kweli katika upendo”
(Efe 4:15) na kujiunga na wanadamu waipendayo kwa moyo amani ili kuomba
amani na kuitekeleza.
Tukisukumwa na Roho yuleyule, sisi hatuna budi kuwasifu wale ambao,
wakikataa utumiaji nguvu (actioni violentae) katika kudai haki zao,
huzishikilia zile njia za kujitetea ambazo, kwa vyovyote zinapatikana pia
kwa walio wadhaifu zaidi. Ila kazi hii ifanyike pasipo kudhuru haki na
wajibu wa watu wengine au wa jumuiya.
Wanadamu, maadam ni wakosefu, wapo na wataendelea daima kuwa chini ya tishio
la vita hadi Kristo atakapokuja. Lakini madhali wanaweza kuishinda dhambi
wakiunganika katika upendo, wanaweza pia kuushinda utumiaji nguvu hata
kulitimiza lile neno la Mungu lisemalo, “Watafua panga zao ziwe majembe, na
mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala
hawatajifunza vita tena kamwe” (Isa 2:4).
Ibara ya kwanza
KUEPUKANA NA VITA
Kuzuia ukatili wa vita
79. Ingawa vita vya hivi karibuni vimeuletea ulimwengu wetu maharibifu
makubwa sana ya kimwili na kiroho, hata hivyo mpaka leo kila siku mahali
kadha wa kadha pa dunia vita vinaendelea kuleta maangamizi yake. Hasa zaidi,
zinapotumika silaha za kisayansi za kila aina, tabia mbaya sana ya vita
inatishia kuwapeleka wapinganao kwa uovu unaopita sana ule wa nyakati za
nyuma. Aidha mchangamano mkubwa wa hali za dunia ya sasa na msokotano wa
mahusiano ya kimataifa huvifanya vita vilivyoanzishwa viendelezwe kwa muda
mrefu na kuendeshwa kwa mbinu mpya, zenye kudhuru kwa siri na ziletazo
uharibifu. Mara nyingi pia kutumia mbinu za ugaidi kunatazamwa kama namna
mpya ya kupiga vita.
Mbele ya hali hii ya kujidhili ya binadamu, Mtaguso unadhamiria kukumbusha
kwanza thamani isiyofifia ya kanuni asilia ya mataifa na ubora wa sheria
zake za msingi na za wote. Dhamiri yenyewe ya binadamu hutangaza sheria hizi
kwa uthabiti unaozidi kukua siku kwa siku. Kwa hiyo matendo yapingayo kwa
makusudi sheria hizi na pia zile amri zinazoagiza matendo hayo ndiyo jinai;
wala utii mtupu hauwezi kabisa kuhesabiwa kama udhuru kwa wale watendao
mambo hayo. Miongoni mwa matendo haya ni ya kutajwa kwanza yale yanayoleta
maangamizi ya mpangilio kwa taifa zima, nchi au kabila dogo. Na hilo ndilo
kosa la jinai ovu sana ambalo lazima lishutumiwe kwa ukali mkubwa; na hauna
budi kusifiwa ujasiri wa wale wasioogopa kuwapinga waziwazi hao wanaoyaamuru
matendo mabaya namna hii.
Mintarafu vita, yapo maafikiano ya kimataifa yaliyotiwa sahihi na nchi
nyingi; nayo hulenga katika kupunguza ukatili wa matendo ya vita na matokeo
yake. Maafikiano hayo yanahusu namna ya kuwatendea askari waliojeruhiwa au
waliotekwa, na mengineyo kama hayo; nayo lazima yahifadhiwe. Na wote, hasa
serikali na wataalamu, wanapaswa kufanya kila jitihada, kadiri ya uwezo wao,
ili maafikiano hayo yakamilishwe kusudi yaweze kuzuia makatili ya vita kwa
namna ifaayo zaidi na yenye mafanikio. Aidha, inaonekana kuwa jambo la haki
kuwepo kwa sheria zinazowashughulikia kiutu wale wanaokataa matumizi ya
silaha kwa sababu ya dhamiri zao, lakini wanakubali kutoa aina nyingine ya
huduma kwa ajili ya jamii ya wanadamu.
Bahati mbaya vita bado havijang’olewa katika maisha ya binadamu. Na pindi
hatari ya vita inaendelea kuwako, wala hakuna mamlaka ya kimataifa yenye
madaraka na nguvu zinavyotakiwa, basi haitawezekana kuzikatalia serikali
haki ya kujitetea kwa halali, pale juhudi zote za usuluhishi wa amani
zinapokuwa zimeshindikana. Viongozi wa serikali na wote wanaoshiriki katika
uongozi wa dola wamewajibika kulinda usalama wa mataifa waliyokabidhiwa, na
kuyakabili masuala muhimu namna hii kwa hisi za uwajibikaji mkubwa. Lakini
kitu kimoja ni kutumia silaha kwa kuzitetea haki za mataifa, na kitu kingine
tofauti ni kutaka kutawala kwa nguvu juu ya nchi nyingine. Tena nguvu na
zana za vita hazihalalishi kila matumizi yake ya kijeshi na kisiasa; wala si
kila tendo kati ya wapiganaji linakuwa halali, ikiwa vita, bahati mbaya,
vimekwisha zuka.
Aidha, wale wanaoapishwa kutumikia nchi yao katika jeshi wajitambue kama
wahudumu wa usalama na uhuru wa mataifa. Nao, wakitekeleza wajibu wao kwa
unyofu, wanachangia kweli katika kuimarisha amani.
Vita kamili
80. Maendeleo ya silaha za kisayansi yameongeza sana ubaya na ukatili wa
vita. Maana matendo ya kivita, yakiendeshwa kwa vyombo hivyo, yaweza kuleta
maangamizi makubwa sana na ya vitu vyote; nayo yanapita kabisa haki ya
kujitetea kwa halali (
legitimae defensionis). Tena, kama silaha za
namna hii zinazopatikana katika ghala za mataifa yenye uwezo zingetumika
bila kizuizi, uangamizi kamili wa pande zote zipiganazo ungetokea. Aidha,
matumizi ya silaha hizo yangesababisha uharibifu mwingi duniani kote na
matokeo yaletayo vifo vingi.
Mambo haya yote yanatulazimu kulizingatia suala la vita kwa mtazamo mpya
kabisa[166]. Wanadamu wa
nyakati hizi wajue kuwa watapaswa kutoa hesabu kamili ya matendo yao ya
vita, kwa maana namna vizazi vijavyo vitakavyoendelea itayategemea kwa
vikubwa maamuzi yao ya leo.
Baada ya kuzingatia vema mambo haya, Mtaguso Mkuu huu unajiunga na Mababa
Watakatifu wa nyakati zetu katika kulaumu (condemnationes) vita
kamili[167], na hivyo
unatamka haya yafuatayo:
Kila tendo la vita linalokusudia kuangamiza ovyo miji mizima au maeneo
makubwa pamoja na wakazi wake, ni kosa dhidi ya Mungu na wanadamu; nalo
linastahili kulaumiwa vikali na bila kusita.
Hatari maalum ya vita vya kisasa ni kwamba vita hivyo vinawapa wale wenye
silaha za kisayansi kali zaidi fursa ya kutenda mauaji hayo; na vilevile
vinaanzisha mfululizo wa mambo usioweza kusimamishwa na unaosukuma utashi wa
watu kuyafikia maamuzi yenye ukatili mkubwa. Basi, ili mambo hayo yasije
yakatokea tena wakati ujao, Maaskofu wa ulimwengu mzima waliokutanika hapa
wanawasihi watu wote, hasa viongozi wa serikali na wakuu wa majeshi,
wazingatie daima mbele ya Mungu na wanadamu uzito mkubwa sana wa wajibu wao.
Mashindano ya kujipatia silaha
81. Ni kweli kwamba silaha za kisayansi hazilimbikizwi tu kwa lengo la
kutumiwa wakati wa vita tu. Maana inadhaniwa kuwa uwezo imara wa taifa
fulani wa kujikinga unautegemea uwezekano wake wa kuwavamia mara maadui
wanaolishambulia. Hivyo, limbikizo la silaha la namna hii linaloongezeka
mwaka hadi mwaka linaweza kuwashawishi kwa njia hii isiyo kawaida maadui
waondokane na mipango yao. Na walio wengi wanaitazama mbinu hii kama njia
yenye mafanikio zaidi na inayodumisha amani kwa kiasi fulani kati ya
mataifa.
Lakini maoni yoyote yale mtu aliyo nayo juu ya mbinu hii [ya kuwashawishi
maadui wasianzishe vita], basi wanadamu waelewe kuwa mashindano ya kujipatia
silaha (cursum ad arma apparanda) yanayofanywa na mataifa mengi, siyo
njia salama ya kulinda amani iliyo imara. Tena hali ya usawa wa nguvu (aequilibrium)
itokanayo nayo mashindano haiwezi kutazamwa kama hali ya amani iliyo ya
kweli na ya kudumu. Maana, sababu zinazozusha vita haziondolewi na
ulimbikizaji huo, kinyume chake zinaweza kuongezeka polepole. Na wakati
ambapo fedha nyingi sana zinatumika kwa kujipatia daima silaha zilizo mpya,
ndipo haitawezekana kutoa msaada maridhawa kwa umaskini mkubwa wa dunia ya
sasa. Na hatimaye, badala ya kusuluhisha kimsingi migogoro kati ya mataifa,
hiyo itazagaa pia mahali pengine ulimwenguni. Hivyo, yatupasa tutafute njia
mpya, tukianzia na matengenezo ya roho za watu, ili kikwazo hicho [cha vita]
kiweze kuondolewa, na ulimwengu, ukiisha okolewa na fadhaa inayouelemea,
upate kurudishiwa amani ya kweli.
Kwa sababu hiyo ni lazima kutangaza tena kwamba mashindano ya kujipatia
silaha ni kidonda kimojawapo kibaya zaidi katika jumuiya ya wanadamu; nayo
yanawadhuru maskini kwa namna isiyovumilika. Na tishio kubwa ndilo kwamba
mashindano hayo, ikiwa yataendelea, siku moja yatasababisha mauaji yale yote
ambayo zana zake zimeshaanza kuyaandaa.
Basi, tukionywa na misiba iliyosababishwa na wanadamu hapo nyuma,
tuchukue nafasi hii ya shwari tuliyojaliwa na Mungu ili tuelewe vizuri zaidi
wajibu wetu na kutafuta njia ya kusuluhisha migogoro yetu kwa namna
inayomstahili zaidi binadamu. Maongozi ya Mungu yanatudai kwa mkazo kuwa
sisi tujiokoe na utumwa wa kale wa vita. Nasi, tukikataa kufanya juhudi hii,
hatujui njia hii potovu tuliyoishika itatufikisha wapi.
Kulaumu kabisa vita. Juhudi za kimataifa ili vita viepukwe
82. Ni dhahiri kwamba tunapaswa kujitahidi kwa kila bidii ili kukiandaa
kipindi ambapo, kwa mapatano ya kimataifa, itawezekana kuharimisha kabisa
kila aina ya vita. Bila shaka jambo hilo hudai halmashauri ya kiulimwengu
yenye mamlaka iundwe; nayo ikubaliwe na mataifa yote na iwe na madaraka na
enzi ya kulinda nchi zote katika usalama, utekelezaji wa haki, na heshima ya
sheria. Lakini, kabla ya halmashauri hii inayotarajiwa haijapata kuundwa, ni
lazima mabaraza ya kimataifa yaliyopo yajishughulishe kwa bidii zote
kutafuta njia zifaazo zaidi ili kuleta usalama kwa wote. Amani haina budi
itokane na mahusiano yenye uaminifu kati ya mataifa kuliko kulazimishwa kwa
tishio la silaha. Hivyo watu wote hupaswa kufanya bidii ili hatimaye
mashindano ya kujipatia silaha yakomeshwe, na mpunguzo wa zana za vita
uanzishwe kimatendo. Nao uendelezwe si kwa upande mmoja tu, bali sawasawa
kwa pande zote, juu ya msingi wa maafikiano ya pamoja na kwa kuhakikishwa
kwa udhamini wa kweli na wenye nguvu[168].
Kwa sasa hivi yasihesabiwe pungufu majaribio yaliyokwisha fanywa na
yanayoendelea kufanywa ili kuondosha hatari ya vita. Na zaidi watiwe moyo
walio wengi wenye mapenzi mema ambao, ijapo wanaelemewa na wajibu mzito wa
madaraka yao makuu, hata hivyo hujishughulisha kuondosha vita
wanavyovichukia, ingawa hawawezi kupuuza ugumu na upana wa masuala yaliyopo.
Inabidi kumwelekezea Mungu maombi bila kukoma ili awajalie watu hao nguvu ya
kushika kazi hii kwa uthabiti na kuitimiza kwa ushujaa. Nayo ni kazi
iliyojaa upendo mkubwa kwa wanadamu na ambayo kwayo amani hujengwa kwa
uhodari. Lakini kazi hii [iletayo amani] hudai wenye kujishughulisha nayo
wapanue fikra zao na mioyo yao hata kuvuka mipaka ya nchi zao wenyewe. Tena
hudai kuondokana na kila aina ya utaifa pamoja na kila tamaa ya kutawala juu
ya nchi nyingine. Nao waishughulikiao amani walishe hisi za heshima kwa
wanadamu wote ambao wanaelekea kuunda kwa bidii nyingi umoja mkubwa zaidi.
Mashauriano (
perscrutationes) na mikutano ya kimataifa mintarafu
masuala yahusuyo amani na ondoleo la silaha imekwisha anza kufanyika kwa
juhudi na bila kuchoka. Nayo haina budi kutazamwa kama hatua za kwanza
kuuelekea usuluhishi wa hoja nzito namna hii; tena kwa wakati ujao itapaswa
kuhamasishwa kwa mkazo na bidii nyingi zaidi ili mafanikio yapatikane.
Lakini wanadamu wajihadhari na tabia ya kuzitegemea juhudi za baadhi ya
watu, pasipo kuzingatia hisia zao wenyewe. Maana viongozi wa mataifa, ambao
ndio wadhamini wa manufaa ya wote katika nchi zao na pia wenye kuyahamasisha
manufaa ya wanadamu wote, huyategemea kwa vikubwa maoni na hisia za
makutano. Maana ni bure wao wajibidishe kuijenga amani kwa uhodari iwapo
hisia za uadui, dharau, mashaka, chuki ya kikabila na itikadi kaidi
vinaendelea kuwatenga watu na kuwaweka katika hali ya uadui kati yao. Tokea
hapo inaonekana kwamba ni jambo la lazima na la haraka kuzilea upya roho za
watu na kutoa maelekezo mapya katika maoni ya umma. Nao wanaoyashughulikia
malezi, hasa ya vijana, pamoja na wale wanaochangia katika kujenga maoni ya
umma wazingatie kama wajibu wao muhimu sana kazi ya kupenyeza mioyoni mwa
watu hisia mpya ziletazo amani. Aidha, kila mmoja wetu hana budi kujitahidi
kuugeuza moyo wake, akizingatia ulimwengu mzima na pia majukumu yale
tunayoweza kutimiza kwa pamoja ili kuiongoza jamii yetu katika kikomo
kilicho kizuri zaidi.
Wala tumaini la uongo lisitudanganye. Maana kama maafikiano ya amani ya
kiulimwengu yaliyo imara na manyofu hayatafanyika; tena ikiwa watu
hawataacha kila chuki na uadui, basi wanadamu wote ambao, ijapo wameyafikia
magunduzi ya ajabu katika uwanja wa sayansi, wapo tayari katika hatari
kubwa, pengine wataifikia kwa uchungu saa ile ambayo hawataionja amani
nyingine, ila amani yenye shari. Lakini hata hivyo Kanisa la Kristo,
lililowekwa katikati ya fadhaa za wakati huo, linapoeleza matatizo hayo,
haliachi kushikilia tumaini lililo imara. Nalo Kanisa linadhamiria daima na
daima kuwaelezea [wanadamu wa] nyakati zetu ujumbe wa Mtume [Paulo], wawe
wanaupokea ama wanaukataa kama kitu kisichofaa, usemao, “Wakati uliokubalika
ndio sasa” ili wageuze mioyo yao; “Tazama, siku za wokovu ndizo sasa”[169].
Ibara ya Pili
KUJENGA JUMUIYA YA KIMATAIFA
Sababu za magomvi na tiba yake
83. Ujenzi wa amani unadai, kabla ya yote, zing’olewe sababu za fitina
kati ya wanadamu zizushazo vita, kuanzia na ukosefu wa haki. Sababu nyingi
za magomvi hutokana na tofauti tele zilizopo katika hali ya kiuchumi pamoja
na kukawia katika kushughulikia tiba yake inayohitajika. Tena sababu
nyinginezo huzaliwa kutoka katika roho ya utawala na dharau ya watu; na
hatimaye, tukidokeza zile sababu zilizofichika zaidi, hutokana na wivu wa
kibinadamu, mashaka, kiburi na tamaa nyingine za kiubinafsi. Maadamu
wanadamu hawawezi kuvumilia machafuko mengi namna hii, basi hutokea kuwa
ulimwengu, hata pasipo vita, unaendelea kutawaliwa na mapigano na matendo ya
kijeuri kati ya wanadamu. Basi, maovu hayohayo yanapatikana pia katika
mahusiano kati ya mataifa. Kwa hiyo, ili kushinda na kubananga maovu haya;
tena ili kukomesha matumizi mabaya ya nguvu, ni sharti kabisa taasisi za
kimataifa zizidi kushirikiana katika kazi yao na kuwasiliana kwa mpango ulio
imara zaidi. Kisha ni lazima kuchochea bila kuchoka uundaji wa vyombo, au
mabaraza (organismorum), vya kufaa kwa minajili ya kuhamasisha amani.
Jumuiya ya mataifa na taasisi za kimataifa
84. Siku za leo mahusiano ya kutegemezana kati ya raia wote na baina ya
mataifa ya ulimwengu mzima yanazidi kuongezeka na kufungamanisha watu wao
kwa wao. Tena kutafuta na kupata manufaa ya wote duniani kwa mafanikio
mazuri zaidi kunazidi kudai kuwa jumuiya ya mataifa ijipangie utaratibu
ulinganao na majukumu yake ya kisasa, zikizingatiwa hasa nchi zile nyingi
zinazoelemewa hadi leo na hali ya unyonge usiovumulika.
Ili kuyafikia malengo haya, taasisi za jumuiya ya kimataifa lazima yakidhi
mahitaji mbalimbali ya watu, kila moja kwa nafasi yake, katika uwanja wa
maisha ya kijamii, yaani mintarafu chakula, afya, elimu na kazi; kadhalika
katika hali za pekee zinazojitokeza hapa na pale, kama vile sharti la
kuhamasisha usitawi wa maendeleo kwa ujumla ya nchi zinazoendelea; tena
sharti la kuwatuliza maafa ya wakimbizi waliotawanyika duniani pote. Na
hatimaye sharti la kuwasaidia wahamiaji na familia zao.
Taasisi za kimataifa, za kiulimwengu na za kinchi zilizokwisha undwa
zimetoa huduma nyingi kwa watu. Nayo ndilo tunda la jitihada za kwanza
zilizofanyika ili kuiweka misingi ya kimataifa ya jumuiya nzima ya wanadamu
kwa kusudi la kuyatatua masuala mazito zaidi ya siku za leo. Tena ili
kuhamasisha maendeleo popote duniani na kuzuia vita vya kila aina. Katika
nyanja hizo zote Kanisa linaifurahia roho ya udugu halisi inayostawi kati ya
wakristo na wasio wakristo; roho ambayo hukuza bidii zinazolenga katika
kutuliza unyonge mkubwa uliopo duniani.
Ushirikiano wa kimataifa katika mambo ya uchumi
85. Mshikamano wa siku hizi kati ya watu unadai uwepo pia ushirikiano wa
kimataifa mkubwa zaidi katika uwanja wa uchumi. Maana, ikiwa karibu nchi
zote zimekwisha pata uhuru wa kisiasa, hata hivyo ziko mbali na kujipatia
uhuru kutoka katika hali ya kuwa na tofauti kubwa mno na toka katika kila
aina ya kutegemea kusikofaa, na kwamba zote ziweze kuikimbia hatari ya
matatizo makubwa yaliyopo nchini.
Maendeleo ya nchi fulani hutegemea misaada ya watu na ya fedha. Ni lazima
kuwaandaa raia wa kila nchi kwa njia ya elimu na mafunzo ya kikazi ili
waweze kushika majukumu mbalimbali katika maisha ya kiuchumi na kijamii.
Basi, kwa lengo hilo, unatakiwa msaada wa mafundi watokao ng’ambo ambao,
pale wanapofanya kazi yao, wawe na tabia ya wasaidizi na washiriki, wala si
ya watawala. Tena pasipo mabadiliko ya ndani katika mtindo wa kuendesha
uchumi wa kimataifa siku za leo, nchi zinazoendelea hazitaweza kamwe kupata
misaada yakinifu. Aidha, misaada mingine ya ziada lazima itolewe kwao toka
kwa nchi zenye maendeleo kwa namna ama ya zawadi, au mikopo au vitegauchumi.
Na misaada hiyo kwa upande mmoja ifanyike kwa ufadhili, wala si kwa uchoyo;
nayo, kwa upande mwingine, ipokelewe kwa unyofu kamili.
Ili kuunda utaratibu halisi wa kiuchumi wa kiulimwengu, itapaswa kuacha
tamaa ya faida iliyo kubwa mno, tena tamaa ya kiutaifa na ya utawala wa
kisiasa. Na hatimaye itabidi kufuta mipango ya mkakati ya kijeshi na njama
za kushamirisha na kutawaza kwa nguvu itikadi kadha wa kadha. Mifumo
mbalimbali ya kiuchumi na kijamii hupendekezwa; basi, inatarajiwa kuwa
wataalamu wataweza kupata ndani yake msingi wa maisha safi ya kiuchumi ufaao
kwa dunia nzima. Na kazi hii itasahilishwa ikiwa kila mmoja ataziacha chuki
bila sababu (praeiudicia) na atajiweka tayari kwa hiari kwa ajili ya
mazungumzo, na pasipo udanganyifu.
Kanuni kadha wa kadha zenye kufaa
86. Kwa kuufuatilia ushirikiano huo, kanuni hizi zifuatazo zimeonekana
kufaa:
a) Mataifa yanayoendelea yalenge hasa katika kuwakamilisha kiutu raia zake.
Na yatekeleze wazi wajibu huo na kwa nia imara; na lengo hilo liwe kikomo
cha maendeleo yake. Kadhalika [haya mataifa] yakumbuke kuwa maendeleo hayo
huasilika kwanza na kupata nguvu yake katika kazi na maarifa ya watu wake
yenyewe, hasa kwa sababu yanategemea kabla ya yote si misaada ya nje tu,
bali zaidi ustawishaji mkamilifu wa rasilimali zilizomo ndani. Na hatimaye
maendeleo haya hayana budi kutegemea busara na desturi za wananchi, ambazo
nazo hupaswa kukuzwa.
Mintarafu suala hilo, wenye uwezo mkubwa zaidi wa kuwaathiri wengine lazima
watoe mfano bora.
b) Ni wajibu mzito sana wa mataifa yaliyoendelea kuzisaidia nchi
zinazoendelea kusudi zitekeleze kazi zao zilizotajwa hapo juu. Kwa lengo
hili mataifa yaliyoendelea hayana budi kufanya kwa hiari marekebisho ya
kiroho na kimatendo (
mentales et materiales), yanayodaiwa ili kuunda
ushirikiano huo wa kiulimwengu.
Hivyo, katika biashara mataifa yaliyoendelea yanapaswa kuyazingatia manufaa
ya nchi zilizo nyonge na maskini zaidi. Maana nchi hizi zinaegemea mapato
yanayotokana na uuzaji wa bidhaa zao kusudi zipate zenyewe riziki yao.
c) Ni wajibu wa jumuiya ya kimataifa kuratibu na kuchochea maendeleo, lakini
kwa kufuatilia ufanisi timamu na haki kamili katika ugawaji wa rasilimali
zinazowekwa kwa madhumuni hayo. Tena ni wajibu wake kuratibisha shughuli za
kiuchumi duniani pote kwa mujibu wa masharti ya haki, ila pasipo kuhalifu
kanuni ya auni (
principio subsidiarietatis).
Tena ziundwe taasisi maalum na zenye kufaa kwa minajili ya kuhamasisha na
kuratibu biashara ya kimataifa, hasa na nchi zenye maendeleo hafifu. Na
taasisi hizo zilenge pia katika kufidia matatizo yatokanayo na tofauti kubwa
mno ya uweza iliyopo baina ya mataifa. Na hatimaye utaratibu wa mtindo huo
hauna budi kuzishirikisha nchi zilizomo katika njia ya maendeleo rasilimali
zinazohitajika, pamoja na msaada wa kiufundi, kitamaduni na kifedha, ili
kusudi zipate ustawi maridhawa wa uchumi wao.
d) Mara nyingi kazi inayotakiwa kufanywa kwa haraka ndiko kutengeneza upya
miundo ya kiuchumi na kijamii. Lakini inapaswa kujitahadhari na fumbuzi za
kistadi ambazo hazijakomaa vizuri; na hasa zile ambazo, pale zimleteapo
binadamu manufaa ya kimwili, ndipo hupinga maumbile yake na manufaa yake ya
kiroho. Maana “Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika
kinywa cha Mungu” (Mt 4:4). Aidha, kila tawi la familia ya kibinadamu lina
chochote, ndani yake na ndani ya mapokeo yake, cha ile hazina ya kiroho
ambayo Mungu ameukabidhi ubinadamu, ijapokuwa wengi hawaelewi ni asili ipi
inakotoka.
Ushirikiano wa kimataifa kuhusu ongezeko la watu
87. Ushirikiano wa kimataifa ni wa lazima hususan yanapotazamwa mataifa
ambayo siku hizi, mara nyingi, yanasongwa kwa namna ya pekee na matatizo
yatokanayo na ongezeko la kasi la idadi ya watu, pamoja na shida nyingine
nyingi. Hivyo ni dharura na lazima, kwa ushirikiano kamili na wenye nguvu wa
wote, hasa wa nchi tajiri zaidi, kubuni mbinu za kuyapata yale
yanayohitajika kwa ajili ya riziki na elimu ya kufaa ya kila mtu; na
hatimaye kuishirikisha jamii nzima ya wanadamu mambo hayo. Mataifa mengi
yangeweza kuiendeleza sana hali yao ya maisha ikiwa yangefunzwa ipasavyo ili
kuzigeuza maarifa za zamani za kilimo na kuzishikilia mbinu za uzalishaji
mali zilizo mpya na za kiteknolojia. Ila [yatekeleze mageuzo hayo] kwa
utaratibu na kwa bidii ya kuyalinganisha na mazingira yao yenyewe; tena
wakati huohuo yatengeneze mfumo wa kijamii ulio bora zaidi na kuutekeleza
mgawanyo wa ardhi ulio wa haki zaidi.
Na serikali mbalimbali hakika zina haki na wajibu zihusuzo matatizo ya idadi
ya watu katika nchi zao; ila zisivuke mipaka ya madaraka yao; kwa mfano
mintarafu sheria za kijamii na kifamilia, tena uhamaji toka shambani
kuelekea mjini; au hatimaye mintarafu upashanaji habari kuhusu hali na
mahitaji ya nchi. Siku hizi watu wanafadhaishwa sana rohoni na matatizo kama
hayo. Hivyo wakatoliki wenye ustadi kuhusu masuala hayo yote wanatarajiwa
waendeleze kwa bidii utafiti na juhudi zao na kuzikomaza zaidi, hasa katika
vyuo vikuu.
Aidha, wengi hukazia kuwa ongezeko la watu duniani, au walau katika
baadhi ya nchi, halina budi kupunguzwa kabisa kwa kila njia na kwa mbinu
yoyote ile chini ya mamlaka ya serikali; hivyo basi, Mtaguso unawahimiza
wote waepukane na fumbuzi zipinganazo sheria za kimaadili, ziwe
zinahamasishwa ama kuwekwa kwa shuruti hadharani au faraghani. Maana, kwa
nguvu ya haki isiyoachanika (inalienabile) ya mtu kufunga ndoa na
kuzaa watoto, uamuzi kuhusu idadi ya watoto wa kuzawa ni juu ya upambanuzi
mnyofu wa wazazi; wala kwa vyovyote vile hauwezi kuachiwa upambanuzi wa
serikali. Nao upambanuzi wa wazazi huitegemea dhamiri iliyokomaa vizuri;
hivyo ni muhimu sana kuwapatia watu wote nyenzo za kujikomaza katika
uwajibikaji mnyofu unaowafaa kabisa wanadamu, kwa mujibu wa sheria ya Mungu
na kwa kuyazingatia mazingira ya mahali na nyakati. Na hayo yote hudai
popote pale maendeleo ya hali ya malezi na ya kijamii; na hasa yatakiwa
malezi ya kidini au walau malezi manyofu ya kimaadili. Vilevile watu
wataarifiwe ipasavyo kuhusu maendeleo ya kisayansi katika uwanja wa utafiti
wa zile mbinu zitakazoweza kuwasaidia wazazi mintarafu udhibiti wa mpango wa
uzazi. Ila kwanza ithibitishwe kwa bidii uthabiti wa hizo mbinu na
uhakikishwe uhalali wake wa kimaadili.
Jukumu la wakristo katika kutoa misaada
88. Kwa hiari na kwa moyo wote wakristo washiriki katika kujenga utaratibu
wa kimataifa wenye kuheshimu uhuru ulio halali na udugu wa kirafiki wa watu
wote. Nalo ni la maana zaidi kutokana na kwamba sehemu kubwa zaidi ya dunia
huuhangaikia umaskini mkubwa sana kiasi kwamba Kristo mwenyewe anaonekana
kuulilia mapendo ya wanafunzi wake kwa midomo ya fukara. Na kikwazo hiki
kiepukwe: kwamba mataifa mengine, ambayo wakaazi wake karibu wote hujiita
wakristo, yamejaa wingi wa mali, na wakati huohuo mataifa mengine yanakosa
mahitaji muhimu kwa maisha na yanahangaika kwa njaa, magonjwa na unyonge wa
kila aina. Maana roho ya ufukara na mapendo ndio utukufu na ushuhuda wa
Kanisa la Kristo.
Basi, wasifiwe na kutiwa moyo wale wakristo, hasa vijana, ambao kwa hiari
hujitolea kuwasaidia watu wengine na nchi nyingine. Na zaidi, ni jukumu la
Taifa lote la Mungu, kwa kufuata neno na mfano wa maaskofu wake, kuunyanyua
unyonge wa nyakati zetu, kufuatana na uwezo wake; yaani kwa kutoa si tu
kutoka kinachozidi, bali pia kilicho cha lazima, kufuatana na desturi za
Kanisa za tangu zamani.
Michango na ugawaji wa misaada mbalimbali inabidi vifanyike kadiri ya
utaratibu wa kijimbo, kitaifa na kimataifa; ila si lazima vipangwe kwa
mtindo mmoja tu na usiobadilika. Na pale iwezekanapo, vitekelezwe kwa kazi
ya pamoja ya wakatoliki pamoja na ndugu wakristo wengine. Maana, roho ya
upendo haipingani hata kidogo na utekelezaji wenye busara na utaratibu wa
shughuli za kijamii na kifadhili; bali, kinyume chake, inaudai. Hivyo ni
lazima wale watakao kujibidisha katika kuzitumikia nchi zinazoendelea,
wapewe mafunzo yafaayo katika taasisi zenye utaalamu.
Uwepo wenye kufaa wa Kanisa katika jumuiya ya kimataifa
89. Kanisa, kwa nguvu ya utume wake wa kimungu, huhubiri Injili na kugawa
hazina za neema kwa watu wote. Hivyo, hutoa mchango wake katika kuimarisha
amani popote pale duniani, likiweka ujuzi wa sheria za Mungu na ya maumbile
uwe msingi thabiti wa ushirikiano wa kidugu kati ya wanadamu na kati ya
mataifa. Ndiyo sababu Kanisa linapasika kabisa kuwepo ndani ya jumuiya
yenyewe ya mataifa, ili liwaamshe na kuwahimiza watu wasaidiane wao kwa wao.
Nalo litafanyika kwa njia ya taasisi zake zenye madaraka rasmi na pia kwa
ushirikiano kamili na mnyofu wa wakristo wote, likichochewa na hamu ile moja
ya kuwatumikia watu wote.
Ili kufikia lengo hilo kwa namna inayofaa zaidi, waamini, wakielewa
jukumu lao la kiutu na kijamii, watapaswa kufanya bidii ili kuiamsha nia ya
kushirikiana kwa uhodari na jumuiya ya kimataifa, kuanzia na mazingira yao
wenyewe wanamoishi. Na juhudi ya pekee ifanyike kusudi vijana wafunzwe
kuhusu suala hilo katika malezi yao ya kidini na kiraia.
Ushirikiano wa wakristo katika taasisi za kimataifa
90. Hakika mtindo mmojawapo ulio bora wa wakristo kujihusisha na shughuli za
kimataifa ndiyo kazi ifanyikayo kwa kushiriki, iwe kibinafsi ama kijumuiya,
ndani ya taasisi zilizokwisha undwa au zinazotarajiwa kuundwa; nayo kazi
idhamirie kuhamasisha ushirikiano kati ya mataifa. Aidha, vyama mbalimbali
vya kikatoliki vya kimataifa huweza pia kuutumikia kwa njia nyingi ujenzi wa
jumuiya ya kimataifa katika amani na udugu. Ndiyo maana itabidi kuviimarisha
[hivyo vyama] kwa kuongeza idadi ya wanachama wenye malezi mazuri. Nalo
litekelezwe kwa kutumia misaada inayohitajika na pia kwa kuratibisha nguvu
zake kwa namna ya kufaa. Maana siku hizi mafanikio katika utendaji, na
ulazima wa dialogia, vinadai shughuli zifanyike kwa kushirikiana pamoja. Na
licha ya hayo, vyama vya namna hii hunufaisha kwa vikubwa katika kutia
mioyoni mwa watu zile hisia za kiulimwengu zinazowafaa sana wakatoliki; tena
husaidia sana katika kuamsha katika dhamiri ya watu [umaana wa] ushirikiano
na uwajibikaji wa kiulimwengu.
Na hatimaye ni tumaini kwamba wakatoliki watapania ushirikiano wa
kimatendo na wenye kufaa na ndugu waliojitenga, ambao nao hukiri mapendo ya
kiinjili; tena na wanadamu wote wanaoitamani amani ya kweli. Basi, kwa njia
hizi watautimiza iwapasavyo wajibu wao ndani ya jumuiya ya kimataifa.
Aidha, Mtaguso huyazingatia mabalaa makubwa sana ambayo bado yawataabisha
sehemu kubwa zaidi ya jamii ya wanadamu; hivyo hudhania kuwa yafaa sana
kuunda taasisi fulani ya kiulimwengu ya Kanisa ili kuchochea popote pale
haki na upendo wa Kristo kwa maskini. Nayo taasisi itakusudia kuchochea
jumuiya ya wakatoliki ili ihamasishe maendeleo ya nchi zenye kuhitaji na
haki ya kijamii kati ya mataifa.
TAMATI
Jukumu la kila mwamini na la Makanisa mahalia
91. Mambo yote yanayoelezwa na Sinodi hii Takatifu ni sehemu ya hazina ya
mafundisho ya Kanisa; nayo hudhamiria kuwasaidia watu wote wa nyakati zetu,
wale wanaomwamini Mungu na wale wasiomtambua wazi; ili kusudi hao wote
wagundue kinagaubaga madai ya wito wao mzima na hivyo wafanye kazi ili
kulinganisha zaidi dunia hii na hadhi kuu ya binadamu. Tena ili kusudi
wapanie udugu wa wote na wenye asili ya juu. Na hatimaye waweze kuiitikia
mialiko ya dharura zaidi ya siku za leo, kwa msukumo wa upendo na kwa bidii
nyingi na za pamoja.
Lakini kwa makusudi, katika vipengele vyake vingi, maelezo hayo
yametolewa kwa mtazamo wa kijumla, kwa sababu ya utofauti mkubwa sana wa
mazingira mbalimbali na wa mitindo ya utamaduni uliopo katika dunia nzima.
Na zaidi, ingawa hapa yameelezwa mafundisho yaliyokwisha pokelewa katika
Kanisa, haya yatapaswa kuendelezwa na kupanuliwa, madhali mara nyingi yahusu
mada zenye kubadilikabadilika. Twategemea kuwa yale mengi tuliyoyaeleza
katika msingi wa Neno la Mungu na wa roho ya Injili yataweza kutoa msaada
wenye kufaa kwa watu wote; na hasa baada ya wakristo kutekeleza jukumu la
kuyalinganisha hayo (adaptatio) na hali ya mataifa na tamaduni
mbalimbali. Nayo wayafanye wakiongozwa na Wachungaji wao.
Dialogia kati ya wanadamu wote
92. Kanisa lilipewa utume wa kuuangaza ulimwengu mzima kwa ujumbe wa
kiinjili, tena wa kuwakusanya katika Roho mmoja wanadamu wote wa kila taifa,
kabila na utamaduni; basi, kwa nguvu ya utume huo Kanisa linakuwa ishara ya
ule udugu unaowezesha na kuimarisha dialogia iliyo nyofu.
Suala hilo ladai kwamba kuanzia katika Kanisa lenyewe tuhamasishe
kuheshimiana, staha na uelewano; tukitambua kila tofauti iliyo halali
iliyopo, kusudi tuanzishe dialogia inayozidi kuwa ya kina kati yao wote
wanaounda lile taifa moja la Mungu; wawe wachungaji au waamini wakristo
wengine. Maana, yana nguvu zaidi yale yanayowaunganisha waamini kuliko
yanayowatenganisha; kuwepo umoja katika mambo ya lazima, uhuru katika yale
yasiyo hakika, na mapendo katika yote[170].
Aidha, mawazo yetu yanawaendea ndugu wasioishi bado katika ushirika kamili
na sisi, pamoja na jumuiya zao; lakini twaunganika nao katika kumkiri
[Mungu] Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, tena katika kiungo cha mapendo;
tukikumbuka kuwa siku za leo umoja wa wakristo unatarajiwa na kutamaniwa
hata na wengi wasiomwamini Kristo. Maana, kadiri umoja huo utakavyokithiri
katika ukweli na upendo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kwa kiasi hichohicho
utakuwa taraja la umoja na amani kwa ulimwengu mzima. Kwa hiyo, tuunganishe
nguvu zetu na kutumia mitindo na mbinu vinavyofaa zaidi na zaidi katika
nyakati za sasa ili kulifikilia vizuri lengo bora namna hii; hivyo, kwa
kuifuata zaidi na zaidi Injili, tujitahidi kushirikiana kidugu katika
kuitumikia familia ya wanadamu inayoitwa kugeuka kuwa familia ya wana wa
Mungu, katika Kristo.
Na hatimaye tuwaelekezee mawazo yetu wote wanaomwamini Mungu ambao huzitunza
tunu za kidini na kiutu katika mapokeo yao; tujitakie kuwa dialogia wazi
iweze kutuhimiza kupokea kwa uaminifu misukumo ya Roho Mtakatifu na
kuitimiliza kwa ari.
Hamu ya kuianzisha dialogia inayoongozwa tu na upendo kwa ajili ya ukweli
na kuendelezwa kwa utaratibu wa kufaa, kwa upande wetu haimkatai mtu awaye
yote: [haiwakatai] wenye kuziheshimu tunu bora za kibinadamu, wajapokuwa
hawamtambui bado Mtunzi wake; wala [haiwakatai] wenye kupinga Kanisa na
kulidhulumu kwa namna mbalimbali. Madhali Mungu Baba ndiye chanzo na kikomo
cha wote, basi sote huitwa kuwa ndugu. Ndiyo maana twaitwa kuushiriki wito
uo huo wa kibinadamu na kimungu pasipo ujeuri wala udanganyifu; nasi twaweza
na twapaswa kutenda kazi pamoja ili kuujenga ulimwengu katika amani ya
kweli.
Ulimwengu unaotakiwa kujengwa na kufikishiwa kikomo chake
93. Wakristo wakiyakumbuka maneno ya Bwana, “Hivyo watu wote watatambua
ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yn
13:35), wasikitamani chochote kwa shauku kuliko kuwatumikia wanadamu wa
ulimwengu wa sasa kwa ukarimu na ufanisi unaozidi siku kwa siku. Kwa hiyo,
waambatane kiaminifu na Injili na kuchota nguvu kutoka kwake; na pia
waunganike nao wote wanaopenda na kuitafuta haki; maana wamebeba wajibu
mkubwa sana hapa duniani: kuhusu huo watapasika kutoa hesabu kwa Yule
atakayewahukumu watu wote siku ya mwisho. Maana si wote wasemao, “Bwana,
Bwana”, wataingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni wao wafanyao mapenzi ya
[Mungu] Baba[171] na kunyosha
mkono kwa kutenda kazi. Kwa sababu [Mungu] Baba hutaka sisi katika wanadamu
wote tumtambue na kumpenda kwa manufaa – yaani kwa neno na tendo – ndugu
yetu Kristo; na hivyo tutoe ushuhuda kwa ukweli na kuwashirikisha wengine
fumbo la upendo wa Baba wa mbinguni. Nasi, tukifanya hivyo, tutaliamsha tena
katika wanadamu wote wa dunia tumaini lenye uhai, ndilo kipaji cha Roho
Mtakatifu, ili siku moja wote hatimaye wachukuliwe katika amani na heri kuu,
katika nchi yetu inayong’ara utukufu wa Bwana.
“Basi atukuzwe Yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote
tuyaombayo au tuyawezayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam
atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na
milele. Amina” (Efe 3:20-21).
Mambo yote yaliyoamuliwa katika konstitusio hii ya kichungaji, na kila
moja kati yake, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya
mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa,
katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na kuyathibitisha. Na
yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa
utukufu wa Mungu.
Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 7 Desemba 1965
Mimi mwenyewe Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki.
(Zinafuata sahihi za Mababa)