Index

Back Top Print

[AR - BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

KONSTITUSIO YA KICHUNGAJI JUU YA
 KANISA KATIKA ULIMWENGU WA LEO
[1]

Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso mkuu
ataka haya yakumbukwe daima

 

UTANGULIZI

Ushirika wa kiundani wa Kanisa na familia nzima ya wanadamu

1. FURAHA NA MATUMAINI (Gaudium et Spes), uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Wala hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao. Maana jumuiya yao imefanywa na wanadamu ambao, wakijumuika pamoja katika Kristo, huongozwa na Roho Mtakatifu katika hija yao inayouelekea Ufalme wa Baba; nao wamepewa tangazo la ukombozi lililowekwa kwa wote. Kwa hiyo [jumuiya ya wakristo] inajisikia kuwa inashikamana kweli na kwa ndani na binadamu na historia yake.

Ni akina nani wanaoelekezewa maneno ya Mtaguso

2. Kwa sababu hiyo Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano, ukishapenya kwa undani zaidi fumbo la Kanisa, bila kusita unalielekeza neno lake si kwa watoto wa Kanisa tu, wala si kwa wale wote wanaoliitia jina la Kristo tu, bali kwa wanadamu wote bila kutofautisha. Hivyo basi, Mtaguso unatamani kuwawekea wazi mtazamo wake mintarafu kuwepo kwa Kanisa na kazi yake katika ulimwengu wa nyakati zetu.

Kwa hiyo Mtaguso unauzingatia ulimwengu wa wanadamu, yaani jamii nzima ya kibinadamu katika mazingira yote ambamo huishi ndani yake. Nao ni ulimwengu ulio mandhari ya historia ya binadamu; tena unaleta alama ya juhudi zake, kushindwa na kushinda kwake. Huu ndio ulimwengu ambao wakristo huamini kuwa umeumbwa na unaendelea kutunzwa kwa njia ya mapendo ya [Mungu] Muumba. Tena ni ulimwengu ambao umeanguka katika utumwa wa dhambi, lakini ambao umeokolewa na Kristo Msulibiwa na Mfufuka aliyevunja mamlaka ya yule mwovu. [Kwa njia hiyo, ulimwengu huu] unapata kutengenezwa upya kadiri ya azimio la Mungu, na kufikia utimilifu wake.

Kumtumikia binadamu

3. Nyakati zetu binadamu, akipigwa na butwaa kwa sababu ya magunduzi na uwezo wake, huyatokeza masuala yenye kufadhaisha juu ya maendeleo ya kisasa ya ulimwengu; tena juu ya nafasi na wajibu wa binadamu hapa duniani (orbe universo); juu ya maana ya juhudi za kila mmoja na za wote pamoja; kisha juu ya kikomo cha mambo yote na cha wanadamu. Kwa sababu hiyo, Mtaguso unashuhudia na kuieleza imani ya taifa zima la Mungu lililojumuishwa na Kristo; hivyo hauwezi kutoa kielelezo kilicho wazi cha mshikamano, heshima na upendo wake kwa ajili ya jamii nzima ya kibinadamu ambamo linaishi ndani yake kuliko kuanzisha majadiliano ya pamoja (colloquium) na jamii hii kuhusu masuala mbalimbali yaliyodokezwa hapo juu. [Katika majadiliano haya] Mtaguso unaleta mwanga utokao katika Injili na unaweka wazi kwa wanadamu nguvu ziletazo wokovu ambazo Kanisa, likiongozwa na Roho Mtakatifu, linazipokea kutoka kwa Mwasisi wake. Maana binadamu ndiye aliye lazima akombolewe, na jamii ya kibinadamu ndiyo hiyo lazima ijengwe. Hivyo basi, kiini cha maelezo yetu yote ni binadamu: lakini kila binadamu katika hali yake nzima, yaani katika umoja wa mwili na roho, wa moyo na dhamiri, wa akili na utashi.

  Kwa hiyo Mtaguso Mkuu, ukitangaza ukuu wa wito wa binadamu, tena ukithibitisha kuwemo ndani yake kwa mbegu ya kimungu, basi unatoa kwa binadamu msaada (cooperationem) wa Kanisa utolewao kwa moyo mweupe ili kuimarisha udugu ule kati ya wanadamu wote unaolingana na wito huo. Kanisa halisukumwi na tamaa yoyote ya makuu ya kidunia, bali linalenga katika hilo tu: likiongozwa na Roho Mtakatifu, kuendeleza kazi ya Kristo mwenyewe ambaye alikuja ulimwenguni ili kuushuhudia ukweli[2], tena kukomboa wala si kuhukumu, kutumikia wala si kutumikiwa[3].

Maelezo ya kitangulizi

HALI YA BINADAMU KATIKA ULIMWENGU WA SASA

Matumaini na fadhaa

4. Ili kutekeleza jukumu hilo, ni wajibu wa kudumu wa Kanisa kuchunguza ishara za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa Injili hivi kwamba, kwa namna inayolingana na kila kizazi, liweze kuyajibu masuala yarudiayo siku zote mintarafu umaana wa maisha ya kisasa na yale ya wakati ujao, tena namna yanavyohusiana kati yao. Maana hatuna budi kujua na kuelewa ulimwengu tunamoishi kama vile matazamio na matarajio yake, kisha tabia yake iletayo mara nyingi fadhaa. Haya yafuatayo ni maelezo yanayoweza kutolewa kuhusu masuala yenye uzito zaidi katika ulimwengu wa kisasa.

Binadamu anaishi leo katika kipindi kipya cha historia yake, chenye mabadiliko ya haraka na ya ndani yanayoenea polepole ulimwenguni kote. [Mabadiliko] hayo husababishwa na akili na harakati za ugunduzi wa binadamu. Nayo yanamgeukia yeye mwenyewe, yaani mawazo yake, maazimio yake ya kibinafsi na ya kijamii, namna ya kufikiri na namna ya kutenda, kuhusu vitu na watu. Hivyo twaweza kuzungumzia mageuzi halisi ya kijamii na ya kitamaduni yenye kuleta matokeo yake hata katika maisha ya kidini.

Kama inavyotokea kila mara mageuzi yanapofanyika katika harakati za kimaendeleo, hata mabadiliko ya namna hii huleta matatizo makubwa. Hivyo wakati binadamu anapoukuza uwezo wake, ndipo wakati huohuo mara nyingi anashindwa kuuweka chini ya mamlaka yake. Tena binadamu anapofanya bidii ili kujipenyeza zaidi na zaidi katika nafsi yake, mara nyingi huonyesha hali ya kusitasita juu yake mwenyewe. Naye anagundua polepole kwa uwazi zaidi sheria za maisha ya kijamii, lakini anaendelea kuwa mtu mwenye mashaka kuhusu mahali pa kuzielekeza. 

Haijatokea wakati wowote kuwa binadamu amefaidika kwa mali nyingi namna hii, pamoja na kuwa na uwezo wa kiuchumi; na hata hivyo sehemu iliyo kubwa ya wanadamu inataabika kwa njaa na umaskini; makundi makubwa ya watu wasiohesabika hawajui kabisa kusoma na kuandika. Wala haijatokea kamwe wanadamu kuutilia maanani uhuru kama ilivyo leo, na wakati huohuo mitindo mipya ya utumwa wa kijamii na wa kifikara inazidi kustawi. Tena wakati ulimwengu unaoelewa wazi umoja wake na ulazima wa mshikamano, ambapo kwao watu wake wanategemezana wao kwa wao, ulimwengu unasukumwa kwa nguvu na kugawanyika katika pande zinazopingana; maana bado yanaendelea mapigano makali ya kisiasa, ya kijamii, ya kiuchumi, ya kikabila na ya kiitikadi. Wala haijatoweka hatari ya vita vya ulimwengu vyenye uwezo wa kuangamiza kila kitu. Ingawa mawasiliano ya mawazo yanazidi kusitawi, maneno yenyewe yanayoeleza fikra zile muhimu hushika maana zilizo tofauti sana katika itikadi (ideologiis) mbalimbali. Mwishowe, kwa kila jitihada binadamu hutaka kujenga mfumo wa kidunia ulio mkamilifu zaidi, lakini bila kwenda sambamba na mfumo wa maendeleo ya kiroho.

Basi, watu wengi sana wa kizazi chetu, wakizama katika hali za kupingana namna hii, wanashindwa kugundua tunu halisi na za kudumu ili wapate kuzilinganisha ipasavyo na zile zinazogunduliwa katika mwenendo wa kihistoria. Kwa sababu hiyo wanasongwa na uzito wa mashaka na kuhangaishwa kati ya matumaini na fadhaa, hasa wakati wanapojihoji mintarafu mwenendo wa kisasa wa ulimwengu. Na mwenendo huo ndio unaomkabili binadamu, tena humshurutisha ajipatie jibu.

Mabadiliko ya ndani

5. Fadhaa ya kiroho ya nyakati zetu na mabadiliko ya hali ya maisha vinahusiana na geuzo la kimsingi linalojitokeza katika muundo wa elimu. Maana muundo huu mpya kwa upande mmoja watilia mkazo zaidi sayansi za kihesabu, kifizikia, au sayansi zinazomhusu binadamu mwenyewe; na kwa upande wa kimatendo inategemea teknolojia itokanayo na sayansi zilizotajwa hapo juu. Mtazamo huo wa kisayansi unaunda kwa mtindo ulio tofauti na ule wa zamani utamaduni na tabia ya kimawazo. Aidha, teknolojia imesonga mbele kiasi kwamba imeugeuza uso wa dunia na kuufuatilia utawala wa anga.

Tena akili ya binadamu kwa namna fulani inakuza utawala wake hata juu ya nyakati: juu ya nyakati zilizopita kwa njia ya uchunguzi wa kihistoria; juu ya nyakati zijazo kwa ustadi katika kuona mbele na kuratibu mambo. Basi, maendeleo ya kisayansi, ya kibayolojia, ya kisaikolojia, na ya kijamii yanampatia binadamu uwezo wa kujitambua vizuri zaidi. Na licha ya hayo, maendeleo hayo yanampa pia mbinu za kiteknolojia ili kuyatengeneza moja kwa moja maisha ya kijamii. Vilevile binadamu anajishughulisha zaidi na zaidi kutathmini mbele na kudhibiti ongezeko la watu.

Kutokana na hayo, mwenendo wa historia unaharakishwa kiasi kwamba kila binadamu hawezi kufuatilia mwenendo huo kirahisi. Kikomo cha jamii ya wanadamu kinapata kuwa kimoja pasipo kutofautiana tena katika historia mbalimbali. Na hivyo binadamu anapita kutoka utaratibu wa kutogeukageuka, na kuingia katika utaratibu wa kimkikimkiki na wa kusonga mbele. Jambo hilo linasaidia kuzuka kwa wingi kwa matatizo mapya ambayo yanadai bidii za uchunguzi na usanisi mpya.

Mabadiliko katika mfumo wa kijamii

  6. Kutokana na hayo yote, mabadiliko ya ndani yanazidi kutokea katika jamii mahalia za jadi – kama vile jamaa, koo, kabila na vijiji – na pia katika makundi mbalimbali na mahusiano ya maisha ya kijamii.

 Jamii zinazotegemea viwanda zinaenea polepole, nazo zaleta ukwasi (opulentiam) wa kiuchumi kwa baadhi ya nchi na zinabadilisha kiundani mitazamo na hali za maisha ya kijamii zilizokuwepo tangu karne zilizopita. Vilevile tamaa na bidii kwa mfumo wa maisha ya mjini zinakua; tamaa na bidii hizo zinasukumwa na ongezeko la miji na wakazi wake, na pia zinatokana na kuenea kwa [ruwaza za] maisha ya mjini kati ya wakazi wa vijijini.

Tena vyombo vipya na vizuri zaidi vya upashanaji habari vinaleta taarifa kuhusu matukio mbalimbali kwa haraka na kufika sehemu zilizo mbali za dunia. Pia vinasaidia kushamiri kwa mawazo na hisia, pamoja na kuzusha mjibizo (repercussiones) wa mlolongo.

Kisha, usipunguzwe uzito wa kwamba watu wengi sana, wakisukumwa kwa sababu mbalimbali kuhamia katika sehemu mbalimbali, hubadilisha namna zao za kuishi.

Hivyo mahusiano kati ya wanadamu yanaendelea kuongezeka; na kwa upande wake kuhusiana huko, au ujamiisho (socializatio), kunaunda tena mawasiliano mapya; lakini mara chache tu kuhusiana huko kunakwenda sambamba na kukomaa kwa mtu na kusaidia uhusiano wa kila mtu na mwenzake (personalizatio).

Maendeleo ya namna hii yanajitokeza wazi zaidi katika nchi zenye viwango vya juu vya kiuchumi na kiteknolojia. Lakini yanayasukuma mbele hata mataifa yale yanayoendelea na ambayo yanakusudia kupata manufaa kutokana na viwanda na miji. Na mataifa hayo, hasa yakifungamana na mapokeo ya zamani, yanajitahidi vilevile kujitengenezea upya mazoea ya uhuru yaliyokomaa na yenye kumwajibisha kila mtu.

Mabadiliko ya kisaikolojia, kimaadili na kidini

7. Mabadiliko ya fikra na mifumo mara nyingi hujadili desturi za kimapokeo, hasa kati ya vijana ambao mara nyingi hawana saburi na pengine wanakuwa waasi kwa sababu ya kutoridhika. Nao, wakielewa umuhimu wao katika maisha ya kijamii, hutamani kuchukua wadhifa wao mapema iwezekanavyo. Kwa sababu hiyo mara nyingi wazazi na walezi wao wanakumbana kila siku na matatizo makubwa zaidi katika kutekeleza jukumu lao.

Taasisi mbalimbali [za kuliongoza taifa], sheria, namna za kufikiri na kuhisi ambazo zimerithiwa kutoka nyakati zilizopita, si kila mara zinaonekana kuweza kulingana vema na hali ya kisasa. Kwa sababu hiyo machafuko mazito katika tabia na kanuni zenyewe za kimaadili hutokea.

Kisha, hata maisha ya kidini husongwa na hali hii mpya. Kwa upande mmoja, uwezo mkubwa zaidi wa kuyapambanua mambo unayasafisha maisha ya kidini na mitazamo ya mazingaombwe na ushirikina ya ulimwengu inayoendelea kuwepo hadi leo. Tena [uwezo huo mkubwa] hudai daima ambato (adhaesionem) la kila mmoja na la kimatendo kwa imani. Na hivyo ni wengi wanaofikia hatua ya kuhisi kiundani zaidi juu ya Mungu. Lakini kwa upande mwingine umati wa watu wanatengana na dini kimatendo. Tofauti na nyakati zilizopita, suala la kumkana Mungu ama dini, au kutomjali Mungu si suala linalotokea kwa nadra na kwa mtu mmoja mmoja. Maana siku za leo tabia hii mara nyingi inaonyeshwa kama dai la maendeleo ya kisayansi au kama mtindo mpya wa “humanismi” (humanismus). Katika nchi nyingi haya yote yanajitokeza si tu katika masuala ya wanafalsafa, bali hupenya kwa vikubwa katika fasihi, sanaa, ufafanuzi wa sayansi ya kibinadamu na wa historia; kisha hupenya pia katika sheria za kijamii hivi kwamba watu wengi hukanganywa.

Tofauti na migongano katika ulimwengu wa nyakati zetu

8. Mabadiliko ya haraka namna hii, ambayo mara nyingi yanaendeshwa kiholela, pamoja na mang’amuzi ya undani zaidi ya hitilafu zilizomo ulimwenguni huzalisha na kuongeza kinzano na migongano.

Awali ya yote katika mtu mwenyewe mara nyingi huonekana mgongano kati ya fikra za kisasa kimatendo na mfumo wa mawazo kinadharia. Nayo mawazo yanashindwa kuutawala na kuuratibu katika muhtasari wa kufaa ujumla wa mambo anayofahamu. Vilevile hujitokeza mgongano kati ya juhudi kwa mafanikio ya kimatendo na madai ya dhamiri kuhusu maadili. Mara nyingi [kutolingana huko hujitokeza] pia kati ya hali za maisha ya pamoja na madai yatokanayo na uwezo wa kufikiri, na pengine wa kutafakari, wa kila mtu. Na tokea hapo, ndipo unapozaliwa mgongano kati ya ubingwa katika kazi mbalimbali za wanadamu na mtazamo kwa ujumla wa mambo.

Aidha, katika familia mivutano hutokana na hali ngumu za idadi ya watu, za kiuchumi na za kijamii; tena, hutokana na matatizo yanayozuka kati ya vizazi vinavyofuatana; kisha hutokana na uhusiano mpya katika jamii kati ya mwanamume na mwanamke.

Mivutano mikubwa huzuka pia kati ya makabila na hata kati ya tabaka mbalimbali katika jamii; kati ya mataifa tajiri, na yale yenye uwezo mdogo, na yale maskini; mwisho kabisa kati ya taasisi za kiulimwengu, zilizoanzishwa kutokana na hamu ya mataifa ya kupata amani, na tamaa ya kuieneza itikadi yake pamoja na ubinafsi wa kijamii uliopo katika mataifa au katika taasisi nyinginezo.

Tokea hapo huzaliwa kutoaminiana, uadui, vita na uchungu. Chanzo cha hayo yote ni binadamu mwenyewe, na ni binadamu mwenyewe mwenye kudhurika.

Matarajio ya binadamu yaliyoenea zaidi

9. Wakati huohuo linazidi kuaminiwa wazo la kwamba binadamu siyo tu anaweza na anapaswa kuimarisha utawala wake juu ya viumbe, bali pia kwamba ni juu yake kuunda mpango wa kisiasa, kijamii na wa kiuchumi ambao utaweza kuwasaidia watu binafsi na makundi ya watu mbalimbali kupandikiza na kuendeleza hadhi yao.

Tokea hapo hujitokeza madai ya wengi ambao wanaamini kabisa kuwa wamenyimwa mali zao bila haki ama kwa mgawanyo usio sawa. Nchi zinazoendelea au zile zilizoufikia uhuru hivi karibuni zinatamani kushiriki manufaa ya ustaarabu wa kisasa katika vipengele vya kisiasa na kiuchumi. Tena hutamani kutekeleza kwa uhuru wajibu wao katika ulimwengu, lakini wakati huohuo umbali wao na mara nyingi hata kutegemea kwao kiuchumi nchi tajiri, zinazoendelea upesi zaidi, vinazidi kukua siku kwa siku. Mataifa yanayosongwa na njaa yanaziita na kuzihoji nchi tajiri. Wanawake wanadai kuwa sawa na wanaume, si tu kinadharia, bali katika haki na hata katika matendo, pale ambapo usawa haupo. Wafanyakazi na wakulima hawataki kuridhika kwa mahitaji yao ya lazima tu katika maisha, bali wanataka kuendeleza haiba yao kwa njia ya kazi, na hivyo kushika nafasi zao katika mpango wa maisha ya kiuchumi, ya kijamii, ya kisiasa na ya kiutamaduni. Kwa mara ya kwanza katika historia ya wanadamu mataifa yote siku hizi yanasadiki kwamba mapato ya ustaarabu yanaweza na yanapaswa kufikishwa kwa wote. 

Chini ya madai hayo yote imejificha hamu ya ndani na ya upote zaidi: watu binafsi na makundi wanayo kiu ya maisha yaliyo ya uhuru kamili, yanayoustahili utu na yanayoyaweka chini ya utawala wao yale yote ambayo ulimwengu huu unaweza kuyatoa kwa ajili yao kwa wingi. Mataifa nayo yanafanya juhudi zaidi na zaidi ili kuufikia muungano wa kiulimwengu kwa namna fulani.

Mambo yakiwa hivyo, ulimwengu wa leo unajionyesha kwa wakati mmoja kuwa wenye nguvu na mdhaifu, wenye uwezo wa kutenda yaliyo bora au yaliyo mabaya sana. Na wakati huohuo zinafunguliwa mbele yake njia za uhuru au utumwa, maendeleo au kurudi nyuma, udugu au chuki. Licha ya hayo binadamu anaelewa kuwa ni juu yake kuelekeza kwa unyofu nguvu ambazo yeye mwenyewe aliziamsha na ambazo zinaweza kumdhuru ama kumtumikia. Na kwa sababu hiyo anajihoji.

Maswali mazito zaidi ya binadamu

10. Kwa kweli makinzano yanayoutesa ulimwengu wa leo yanahusiana na lile la ndani zaidi lenye mizizi yake katika moyo wa binadamu. Ndani ya binadamu mwenyewe mambo mengi hupingana yenyewe kwa yenyewe. Maana, kwa upande mmoja kiumbe hung’amua kwa namna nyingi mipaka yake; na kwa upande mwingine hujihisi kuwa hana mipaka katika matarajio yake na kuwa ameitwa kwa maisha ya juu zaidi. Akivutwa na tamaa nyingi, hulazimika daima kuzichagua baadhi yake na kuziacha nyingine. Tena, akiwa mdhaifu na mkosefu, mara nyingi hutenda yale ambayo asingetaka kuyatenda na hatendi yale ambayo angetaka kuyatenda[4]. Kwa hiyo huteswa na mgawanyiko huo uliopo ndani yake mwenyewe ambao kutokana nao huzuka pia fitina nyingi na kubwa katika jamii. Hakika watu wengi sana wanaoishi kimatendo katika hali ya uyakinifu (materialismus) wako mbali katika kuelewa vizuri tatizo hilo sugu, au walau wakisongwa na umaskini huzuiliwa kuitafakari hoja hiyo. Wengi hudhani ya kuwa watapata amani kwa njia ya fafanuzi mbalimbali za mambo zilizoletwa kwa namna nyingi. Tena wengine hungoja ukombozi ulio halisi na mkamilifu kutokana na juhudi za kibinadamu tu; nao wameshawishiwa kuwa ufalme ujao wa kibinadamu hapa duniani utakidhi matarajio yote ya mioyo yao. Wala hawakosekani wale ambao, wakishakata tamaa juu ya umaana wa maisha yao, huusifu ujasiri wa wengine ambao, wakiona kuwa maisha ya binadamu hayana umaana halisi, basi hujitahidi kuyafanya yawe na maana kamili kwa njia ya akili yao tu. Hivyo mbele ya mageuzo ya ulimwengu wa kisasa wanazidi kuwa wengi wale wanaojihoji au wanaojihisi kwa mang’amuzi mapya maswali ya kimsingi kama haya yafuatayo: Je, binadamu ni nani? Je, nini maana ya uchungu, uovu na mauti, ambayo yanaendelea kuwepo ingawa kuna maendeleo katika kila fani? Je, ni kwa ajili ya nini mafanikio haya yanayogharimiwa namna hii? Je, mwanadamu atoe mchango gani kwa ajili ya jamii? Je, naye atarajie kupata nini kutokana nayo? Je, baada ya maisha haya ya kidunia kitafuata nini?

Basi, Kanisa huamini kuwa Kristo, aliyekufa na kufufuka kwa ajili ya wote[5], anampa binadamu mwanga na nguvu kwa njia ya Roho wake ili binadamu mwenyewe aweze kuuitikia wito wake ulio bora. Wala hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu liwapasalo wao kuokolewa kwalo[6]. Kadhalika, Kanisa linaamini kupata katika Bwana wake na Mwalimu ufunguo, kiini na kikomo cha historia yote ya binadamu. Aidha, Kanisa linakiri kwamba licha ya mabadiliko yote yapo mambo mengi yasiyobadilika; nayo yanapata msingi wake halisi katika Kristo ambaye ndiye Yeye yule jana na leo na hata milele[7]. Na hivyo, katika nuru ya Kristo, aliye sura ya Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote[8], Mtaguso unadhamiria kunena na watu wote ili kuwaeleza fumbo la binadamu na kushirikiana nao katika utafiti ili kulipata suluhisho la matatizo muhimu zaidi ya nyakati zetu.

SEHEMU YA KWANZA

KANISA NA WITO WA BINADAMU

Kuitikia misukumo ya Roho Mtakatifu

11. Taifa la Mungu linasukumwa na imani, ambayo kwayo linaamini kuwa huongozwa na Roho wa Bwana anayeujaza ulimwengu. Nalo linayashiriki matukio, madai na matarajio pamoja na wanadamu wote wa nyakati zetu. Katika hayo linajibidisha kuzitambua ni zipi ishara halisi za kuwepo kwa Mungu au za mpango wake. Maana imani inayang’arisha mambo yote kwa mwanga mpya, na kuyafunua maazimio ya Mungu mintarafu wito mzima wa binadamu; na hivyo inaiongoza akili kwa masuluhisho ambayo ni ya kiutu kabisa.

Katika mwanga huo, Mtaguso unadhamiria kwanza kuzichambua tunu zinazoheshimiwa sana siku hizi, na kuzielekeza tena katika chemchemi yake ya kimungu. Maana tunu hizo kwa zenyewe ni bora kwa sababu zinatokana na akili ya kibinadamu iliyo kipaji kutoka kwa Mungu. Lakini mara nyingi, kutokana na upotovu wa moyo wa binadamu tunu hizo zinaharibiwa kutoka hali zake halisi, na hivyo zinahitaji kusafishwa.

Je, Kanisa linafikiria nini kuhusu binadamu? [sura ya 1]. Je, ni hatua zipi zinazohimizwa kwa ujenzi wa jamii ya siku hizi? [sura ya 2]. Je, ni nini maana ya ndani ya harakati za binadamu katika ulimwengu? [sura ya 3]. Majibu kwa maswali hayo yanasubiriwa. Baada ya hayo itaonekana wazi zaidi kuwa taifa la Mungu na wanadamu wote ambao kati yao taifa la Mungu linaishi, wanatumikiana wenyewe kwa wenyewe. Hivyo, utume wa Kanisa utajidhihirisha kuwa na tabia ya kidini, na kwa sababu hiyohiyo kuwa pia na tabia halisi ya kibinadamu [sura ya 4].

Sura ya Kwanza

HESHIMA YA BINADAMU

Binadamu ni sura ya Mungu

12. Waamini na wasio waamini hukubaliana karibu kwa kauli moja kwamba yote yaliyomo duniani yamefanywa kwa ajili ya binadamu aliye kiini na kilele chake.

Lakini, je, binadamu ni nani? Naye mwenyewe ametoa, na anaendelea kutoa, maoni mengi juu yake; ambayo pengine hupingana. Maana, ama anajikuza na kujiweka kuwa kama kanuni inayoviongoza vitu vyote, ama anajidhili hata kukata tamaa na hivyo kuingia katika mashaka na fadhaa. Basi Kanisa linajihusisha kiundani kwa matatizo hayo na linaweza kutoa jawabu, likiisha kufundishwa na ufunuo wa Mungu. Nalo jibu linaweza kueleza hali halisi ya binadamu, kuutia maana udhaifu wake, na wakati huohuo kumsaidia binadamu kutambua kwa haki hadhi yake na wito wake. 

Maana Maandiko Matakatifu hufundisha kuwa binadamu ameumbwa “kwa mfano na sura ya Mungu”, mwenye uwezo wa kumjua na kumpenda Muumba wake. Tena [hufundisha] kwamba binadamu aliwekwa na Mungu juu ya viumbe vyote vya duniani kama mtawala wake[9] ili aviongoze na kuvitumia kwa utukufu wa Mungu[10]. “Mtu ni kitu gani hata umkumbuke? Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, umemvika taji ya utukufu na heshima; umemtawaza juu ya kazi za mikono yako. Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake” (Zab 8:4-6).

Lakini Mungu hakumwumba binadamu na kumwacha peke yake, bali tangu mwanzo “mwanamume na mwanamke aliwaumba” (Mwa 1:27), na muungano wao umeunda mtindo wa kwanza wa ushirika kati ya watu. Maana binadamu kwa mtima wa maumbile yake ni kiumbe ambaye anahitaji kushirikiana na wengine; naye hawezi kuishi wala kuvitokeza vipawa vyake pasipo mahusiano na wenzake.

Kwa sababu hiyo Mungu, kama tena ilivyoandikwa kwenye Maandiko Matakatifu, aliona “kila kitu alichokifanya, na tazama, kilikuwa chema sana” (Mwa 1:31).

Juu ya dhambi

13. Ingawa binadamu aliumbwa na Mungu katika hali ya haki, hata hivyo akishawishiwa na Shetani, tangu mwanzo wa historia aliutumia vibaya uhuru wake. Naye akajikweza dhidi ya Mungu na kutamani sana kupata tarajio lake (finem suum) nje ya Mungu. Ijapo walikuwa wamemfahamu Mungu, wanadamu hawakumtukuza kama Mungu, bali mioyo yao isiyo na hekima ilitiwa giza, nao wakakitumikia kiumbe badala ya Muumba[11]. Na yale tunayoarifiwa na ufunuo wa Mungu hulingana na ung’amuzi wenyewe. Maana kama binadamu hujichunguza moyoni mwake anajitambua kuwa anauelekea ubaya na kuzama katika mabaya mengi, ambayo kwa hakika hayawezi kutoka kwa Muumba [wake] ambaye ni mwema. Mara nyingi binadamu, kwa kukataa kumkiri Mungu kama asili yake, umevunja utaratibu uliokuwa wa kufaa kwa kikomo chake, na wakati huohuo utaratibu mzima ndani yake, na pia katika uhusiano wake na watu wenzake na viumbe vyote. 

Hivyo binadamu amegawanyika ndani yake mwenyewe. Hivyo maisha yote ya binadamu, mmoja mmoja na pamoja, hujidhihirisha kama pambano, tena lililo kali, kati ya wema na uovu, kati ya mwanga na giza. Zaidi, binadamu anajikuta hawezi kushinda kabisa peke yake mashambulio ya uovu, hivi kwamba kila mmoja hujisikia kama amefungwa minyororo. Lakini Bwana mwenyewe amekuja kumkomboa binadamu na kumtia nguvu akimwumba upya ndani yake na kumfukuza “mkuu wa ulimwengu huu” (Yn 12:31), aliyekuwa amemfunga katika utumwa wa dhambi[12]. Kwa sababu dhambi humshusha binadamu mwenyewe, ikimzuia asiufikilie utimilifu wake.

Basi, katika mwanga wa Ufunuo huo, wito mkuu na pia udhaifu mkubwa, ambavyo binadamu huvionja, vinapata maana yake halisi.

 
Maumbile ya binadamu  
 
14. Binadamu ni umoja wa mwili na roho. Hivyo kwa hali yake ya kimwili anajumlisha ndani yake vitu asili vya ulimwengu unaoonekana ili kwamba hivyo [vitu] kwa njia yake viweze kuufikia utimilifu wake na kupata sauti ya kumsifu Muumba kwa hiari [13]. Ndiyo maana binadamu haruhusiwi kuudharau uzima wa mwili. Zaidi, anapaswa kuutazama mwili wake kama mwema na wenye kustahili heshima kwa sababu uliumbwa na Mungu na utafufuliwa siku ya mwisho. Japo hivyo, binadamu aliyejeruhiwa na dhambi huonja maasi ya mwili. Kwa hiyo, ni heshima yenyewe ya binadamu inayomdai amtukuze Mungu katika mwili wake [14], wala asiuruhusu ujitumikishe kwa maelekeo mapotovu ya moyo wake.

Lakini binadamu hakosi anapojitambua kuwa yeye ni mkuu kuliko viumbe vingine vyenye mwili, wala anapojijali zaidi kuliko chembe ndogo tu ya ulimwengu, au kuliko mwanajumuiya asiyetambuliwa katika jamii ya watu. Maana binadamu katika undani (interioritate) wake huzidi viumbe vyote; naye anaingia tena katika undani huo anapourudia moyo wake. Ndimo ambamo Mungu anamngojea, Yeye ambaye ndiye mwenye kuichunguza mioyo[15]; tena, ambamo binadamu mbele ya macho ya Mungu huamua bahati yake. Kwa hiyo [binadamu] akitambua kuwa ana nafsi ya kiroho isiyokufa, hakubali kuhadaiwa na mawazo madanganyifu yanayotokana tu na hali za kimaumbile au za kijamii; bali, kinyume chake hufikia kugusa kiundani ukweli wenyewe wa mambo.

 
Heshima ya akili, ukweli, na hekima  
 
15. Binadamu anayo haki kujitambua kuwa mkubwa kuliko viumbe vyote kwa sababu ya akili yake, ambayo kwayo hushiriki nuru ya fikra ( mentis) ya Mungu. Kwa kujibidisha kuitumia akili yake katika mfululizo wa karne, binadamu hakika amejiendeleza katika fani za sayansi, za kiuchunguzi, katika sanaa za kiufundi na za kitaalamu ( artibus technicis et liberalibus). Aidha, nyakati zetu binadamu amefanikiwa kwa vikubwa hasa katika kuutafiti na kuutawala ulimwengu. Na hata hivyo ametafuta na kuuvumbua daima ukweli ulio wa kina zaidi. Maana akili ya binadamu haimalizi kazi yake katika mambo ya ulimwengu huu yanayoonekana tu, bali inamudu kuufikia ukweli unaoweza kueleweka kwa uhakika halisi, ijapokuwa kutokana na dhambi imetiwa kivuli na kudhoofishwa.  
 
Kisha maumbile ya kiakili ya binadamu, yanaufikia ukamilifu wake kadiri ipasavyo kwa njia ya hekima; nayo humvutia kwa upole binadamu ili atafute na kupenda yaliyo kweli na mema. Na hekima hiyo, binadamu akijazwa nayo, humwongoza kwa njia ya yale yaonekanayo kufikia yale yasiyoonekana.  
 
Nyakati zetu zinahitaji hekima hiyo kuliko nyakati zilizopita, ili magunduzi yote mapya yalingane zaidi na hali ya kibinadamu. Kwa kweli mustakabali wa ulimwengu upo katika hatari, kama wasipojitokeza watu wenye hekima zaidi. Licha ya hayo, haina budi kusisitizwa kwamba kuna mataifa mengi, ambayo kiuchumi ni maskini zaidi kuliko mengine, lakini ni matajiri zaidi katika hekima, yanayoweza kuyachangia mengine msaada mkubwa.

Aidha, kwa paji la Roho Mtakatifu, binadamu huweza kuifikia katika imani hatua ya kutazama na kulionja fumbo la mpango wa Mungu[16].

 
Heshima ya dhamiri ya kimaadili

16. Ndani kabisa ya dhamiri yake binadamu hugundua sheria ambayo hakujiwekea mwenyewe, lakini ambayo lazima aitii. Sauti [ya sheria hiyo] inamwita daima kupenda na kutenda mema, na kuepuka uovu; nayo yasikika kusema moyoni mwake wakati unaotakiwa, “fanya hili, epukana na lile”. Kwa kweli binadamu anayo sheria moyoni mwake iliyoandikwa na Mungu; kuitii ndiyo heshima yenyewe ya binadamu, na kadiri ya hiyo atahukumiwa[17]. Dhamiri ndicho kiini cha siri zaidi cha binadamu, na hekalu lake. Humo yeye yumo peke yake pamoja na Mungu, ambaye sauti yake ndimo inamosikika[18]. Tena, kwa njia ya dhamiri inajijulisha kwa namna ya ajabu sheria ile ambayo yapata utimilifu wake katika upendo wa Mungu na wa jirani[19]. Katika uaminifu kwa dhamiri [yao] wakristo wanajiunga na wanadamu wengine, ili kutafuta ukweli na kuyatatua masuala mengi ya kimaadili yanayozuka katika maisha ya binafsi na ya jamii. Kwa hiyo, kadiri dhamiri inavyozidi kuwa nyofu, ndivyo watu na vikundi vinavyozidi kujitenga na uamuzi kipofu na hujaribu kulingana na sheria halisi za uadilifu. Hata hivyo, pengine inatokea kwamba dhamiri inadanganyika kwa sababu ya ujinga usioponyeka; ila ijapo hivi haipotezi heshima yake. Lakini mambo haya hayawezi kusemwa ikiwa binadamu anazembea katika kuutafuta ukweli na wema, tena iwapo dhamiri [yake] karibu imepofuka kutokana na uzoefu wa dhambi.

 
Ubora wa uhuru

17. Lakini binadamu anaweza kuugeukia wema katika uhuru tu. Watu wa nyakati zetu wanauzingatia sana uhuru huo na kuutafuta kwa shauku. Na katika hilo wanayo haki. Lakini mara nyingi wanaushughulikia kwa namna isiyofaa, kana kwamba yote yanaruhusiwa ilimradi yapendeze, hata yakiwa ni mabaya. Bali uhuru halisi ndiyo ishara iliyo bora ya sura ya kimungu katika binadamu. Maana Mungu alitaka kumwacha binadamu “aifuate nia yake”[20], hivi kwamba amtafute Muumba wake kwa hiari; na hatimaye aufikie ukamilifu ulio bora na wenye heri, pasipo shuruti na kwa kuambatana naye [Mungu]. Kwa hiyo, hadhi ya binadamu yamtaka atende kadiri ya chaguo lake kwa kujua na kwa uhuru; yaani awe amesukumwa na kuhimizwa kutoka ndani, wala si kwa misukumo yenye upofu ya ndani yake, au kwa shuruti tu za nje. Lakini binadamu anapewa hadhi hiyo anapoliweka mbele lengo lake kwa kuchagua kwa hiari lililo jema, akijibandua mwenyewe na kila utumwa wa tamaa. Kwa juhudi na bidii anajipatia njia zinazofaa lengo lake. Uhuru wa binadamu uliojeruhiwa na dhambi, unaweza kufanikisha kikamilifu mpango huo unaomwelekea Mungu kwa msaada wa neema ya Mungu tu. Aidha, kila binadamu atapaswa kutoa hesabu ya maisha yake mbele ya mahakama ya Mungu, kwa mambo yote aliyoyatenda, kwamba ni mema au mabaya[21].

 
Fumbo la mauti
 
18. Mbele ya kifo fumbo la hali ya binadamu hupata kuwa kubwa sana. Binadamu anafadhaika si tu anapofikiria juu ya kukaribia kwa uchungu na uozo wa mwili, bali zaidi anaposhikwa na hofu juu ya mambo yote kukoma moja kwa moja. Lakini silka ( instinctu) ya moyo wake inamfanya apambanue mambo kwa unyofu, hasa anapolichukia wazo la uharibifu wote na la mwisho kabisa wa utu wake. Mbegu ya umilele iliyo ndani yake, isiyoweza kugeuzwa kuwa kitu tu, hiyo basi huinuka dhidi ya mauti. Juhudi zote za teknolojia, ingawa zinafaa sana, haziwezi kutuliza fadhaa ya binadamu; kurefusha maisha ya kimwili hakuwezi kukidhi hamu ya maisha ya baadaye isiyozimika, iliyomo moyoni mwa binadamu.

Wakati ambapo kila kuwaza kunakoma mbele ya kifo na mauti, hapo Kanisa, likifundishwa na Ufunuo wa kimungu, hukiri kwamba binadamu ameumbwa na Mungu kwa kikomo chenye heri kinachovuka mipaka ya udhaifu wa dunia hii. Zaidi ya hayo, imani ya kikristo hufundisha kwamba kifo cha kimwili, ambacho binadamu angezuiliwa kama asingalitenda dhambi[22], kitashindwa kabisa. Nalo litatimizwa wakati binadamu atakaporudishwa na uweza na huruma ya Mkombozi katika hali aliyoipoteza kwa sababu ya dhambi. Maana Mungu alimwita na anaendelea kumwita binadamu aambatane naye kwa maumbile yake yote katika ushirika wa milele na uzima wa kimungu usioweza kuharibika. Kristo ndiye aliyeupata ushindi huo alipofufuka yu mzima, baada ya kumkomboa binadamu na mauti kwa njia ya kifo chake[23]. Kwa hiyo imani, ikijiweka mbele ya watu kwa mafundisho yenye misingi imara, inawapa wote wanaotaka kutafakari jibu kwa fadhaa zao mintarafu maisha yajayo. Tena wakati huohuo imani inawawezesha kushirikiana katika Kristo na ndugu zao waliokwisha kufa. Nayo [imani] inawapa tumaini la kwamba ndugu hawa wamekwisha fikia uzima wa Mungu.

Namna za ukani Mungu (atheismus), na sababu zake

19. Hadhi ya binadamu kwanza kabisa imo katika wito wake wa kuwa na ushirika na Mungu. Tangu mwanzo wa uwepo wake, binadamu anaitwa kuongea na Mungu; kwani kama binadamu anakuwepo, ni kwa sababu aliumbwa na Mungu kwa upendo [wake]; tena kwa upendo huo anatunzwa naye; wala binadamu hawezi kuishi kikamilifu kulingana na ukweli ikiwa hautambui kwa uhuru upendo huo na hamtegemei Muumba wake. Lakini wengi wa watu wa nyakati zetu hawakielewi katu au wanakikataa waziwazi kiungo hiki cha ndani na kiletacho uzima na Mungu [kwa binadamu]. Hivyo, ukani Mungu lazima utazamwe kama moja ya masuala yaliyo mazito sana ya nyakati zetu, nao unapaswa kuchunguzwa kwa uangalifu mkubwa.

 
Kwa neno “ukani Mungu”, au “atheismi”, hutajwa mambo kadhaa yanayotofautiana sana kati yao. Maana wengine wanamkana Mungu waziwazi; wengine tena hudhani kwamba binadamu hawezi kufahamu neno lolote juu yake; aidha wapo wengine ambao huichunguza hoja kuhusu Mungu kwa njia inayoleta wazo kwamba suala hilo halionekani kuwa na maana yoyote. Wengi, wanavuka isivyofaa mipaka ya sayansi, ama hudai kuyafafanua mambo yote kwa mtazamo wa kisayansi tu; au, kinyume chake, hawakubali kuwa ukweli ulio halisi unaweza kupatikana. Tena wengine wanamtukuza binadamu kiasi ambacho imani kwa Mungu inadhoofishwa; nao inavyoonekana wanapendelea kumkweza binadamu kuliko kumkana Mungu waziwazi. Aidha wengine hujitungia wenyewe mawazo juu ya Mungu kwa namna ambayo hayalingani na ukweli wa Injili, na hivyo fikra mintarafu Mungu wanazozikataa haziwezi kwa namna yoyote ile kumhusu Mungu wa Injili. Kisha wapo wengine ambao hawajishughulishi kamwe na suala juu ya Mungu, kwa sababu hawaonekani kuhisi fadhaa yoyote kuhusu dini na wanashindwa kuelewa kwa nini ingewapasa wajishughulishe nayo. Aidha, mara nyingi kumkana Mungu kuna asili yake katika kuupinga vikali uovu uliopo ulimwenguni; au pengine pale ambapo tunu za kibinadamu zinatiliwa ubora unaozifaa kweli za kimungu ( ipsius absoluti) tu; na hivyo tunu hizo za kibinadamu zinachukua nafasi ya Mungu. Mara nyingi pia ustaarabu wa kisasa unaweza kuleta ugumu katika kumkaribia Mungu, si kwa sababu yake wenyewe, bali kwa kuwa unafungamana mno na mambo ya dunia hii.

Bila shaka wale ambao kwa makusudi wanapania kumfunga Mungu mbali na mioyo yao na kuepukana na hoja za kidini na hivyo wasiufuate mwongozo wa dhamiri yao, hawa basi hawana budi kuwa na kosa. Lakini mara nyingi katika fani hii hata waamini wamechangia. Kwa maana ukani Mungu ukitazamwa kwa ujumla si jambo lililokuwepo tangu asili (non est quid originarium) bali unatokana na sababu mbalimbali. Kati ya hizo [kisa kimojawapo] ni upinzani wenye msingi wake katika malalamiko dhidi ya dini mbalimbali, na hasa, katika nchi kadha wa kadha, dhidi ya dini ya kikristo. Kwa sababu hiyo, katika vyanzo vya ukani Mungu waamini wanaweza kuchangia kwa sehemu ambayo si ndogo. Maana, ama huzembea katika mafunzo ya imani; au hufafanua mafundisho yake kwa namna isiyo sahihi; au kwa makasoro yao katika maisha yao ya kidini, ya kimaadili au ya kijamii. [Kwa sababu hizo zote] hakuna budi kusema kuwa waamini pengine wanauficha uso halisi wa Mungu na wa dini, kuliko kuufunua.

Ukani Mungu wa kimpango  
 
20. Mara nyingi ukani Mungu wa nyakati zetu hujidhihirisha kwa namna ya mpango kamambe. Kadiri ya mpango huo, licha ya sababu nyingine, mvuto wa binadamu kujitawala unakazwa sana, hivi kwamba unaleta ugumu katika kumtegemea Mungu kwa namna yoyote ile. Watu wanaoshikilia nadharia hii ya ukani Mungu hudai kuwa uhuru kwa binadamu ni kuwa mwenyewe kikomo chake ( homo sibi ipse sit finis), yaani yeye peke yake ndiye mtengenezaji na mratibu wa historia yake. Hao hudhani kwamba mtazamo huo haupatani na imani kwa Bwana aliye Muumba na kikomo cha mambo yote; au pengine tu unaifanya batili kabisa [imani hiyo]. Nadharia hiyo yaweza kuhamasishwa na hisia ya kuwa na uwezo mkubwa ambayo inatiwa moyoni mwa binadamu na maendeleo ya kiteknolojia.

Kati ya mitindo mbalimbali ya ukani Mungu wa nyakati zetu, hauna budi kuzingatiwa ule unaotarajia ukombozi wa binadamu kutokana hasa na ukombozi wa kiuchumi na wa kijamii. Inadaiwa kuwa dini kwa maumbile yake yenyewe ni kipingamizi kwa ukombozi huo, kwa maana inaelekeza tumaini la binadamu kwa maisha ya baadaye na yenye udanganyifu, na hivyo inamwondoa binadamu katika harakati za kujenga mji wa dunia hii. Kwa hiyo, wafuasi wa itikadi hiyo wanapofikia hatua ya kushika hatamu za uongozi katika nchi, wanaipinga dini kwa nguvu na kueneza ukani Mungu, kwa kutumia pia vyombo vyao vya dola vinavyowaelemea raia, hasa katika elimu ya vijana.

Msimamo wa Kanisa mbele ya ukani Mungu

21. Kanisa likijishughulisha kiaminifu na wajibu wake mbele za Mungu na wanadamu, halina budi kuyapinga kwa uchungu na kwa nguvu mafundisho na matendo hayo yenye kudhuru, kama lilivyofanya huko nyuma[24]. [Mafundisho na matendo] hayo yanapingana na akili na mang’amuzi ya kawaida ya wanadamu, pamoja na kumwangusha binadamu kutoka cheo chake cha heshima alichoumbiwa.

Lakini Kanisa linajibidisha kuvumbua sababu za kumkana Mungu zinazojificha akilini mwa wakana Mungu; nalo likitambua uzito mkubwa wa masuala yanayozushwa na ukani Mungu, tena likisukumwa na upendo kwa ajili ya watu wote, hudhani kuwa masuala haya yanastahili uchunguzi wenye uzingativu na wa ndani zaidi.

Kanisa linaamini kwamba kumkiri Mungu hakupingi hata kidogo hadhi ya binadamu, kwa vile hadhi hiyo husimikwa na kutimilizika katika Mungu; maana binadamu hupokea kutoka kwa Mungu Muumba vipawa vya akili na uhuru; tena huwekwa kuwa huru katika jamii; lakini hasa huitwa kuungana na Mungu mwenyewe kama mwana [wake] na kushiriki heri yake Yeye. Aidha [Kanisa] linafundisha kuwa tumaini kwa maisha yajayo ( spem eschatologicam) halipunguzi umuhimu wa shughuli za kidunia, bali hutoa sababu mpya zinazosaidia utekelezaji wake. Kinyume chake, ukikosekana msingi wa kimungu na tumaini la uzima wa milele, basi hadhi ya binadamu inaudhiwa sana, kama inavyoonekana mara nyingi siku za leo. Hoja za maisha na mauti, za dhambi na uchungu, huendelea kuwa mafumbo yasiyo na ufumbuzi, kiasi kwamba mara nyingi wanadamu huzama katika kukata tamaa.
 
Wakati huohuo binadamu hubaki kuwa kwake mwenyewe suala lisilo na ufumbuzi, na analolihisi kwa gizagiza. Maana hakuna anayeweza kuepukana kabisa na suala hilo la kujihojihoji katika wakati fulani wa maisha yake, na hasa katika matukio yaliyo mazito zaidi. Mungu peke yake anaweza kutoa jawabu kamili na timilifu kwa hoja hiyo; Yeye ambaye humwita binadamu kwenye fikra za juu na kwenye uchunguzi wenye hali ya kunyenyekea.

Dawa kwa ukani Mungu haina budi kutokana na fafanuzi za kufaa za mafundisho ya Kanisa, na pia kutokana na maisha yake na ya wanajumuiya yake. Maana ni juu ya Kanisa kuleta uwepo wa Mungu Baba na wa Mwanae aliyetwaa mwili, na kuudhihirisha. Na litafanya hivyo likijitengeneza upya na kujirekebisha bila kukoma chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu[25]. Hilo litapatikana kwa ushuhuda wa imani iliyo hai na komavu, yaani imani ambayo imelelewa vizuri hivi kwamba iweze kuyakabili matatizo kwa upambanuzi na kuyashinda. Na mashahidi wengi sana walitoa na wanatoa ushuhuda mtukufu wa imani hiyo. Nayo haina budi kudhihirisha uwezo wake na kuzaa matunda tele, kwa kupenya mfumo mzima wa maisha ya waamini pia katika harakati zake za kidunia. Tena kwa kuwasukuma kufuatilia haki na upendo hasa kwa wahitaji. Kisha, linalochangia kwa vikubwa kuutambua uwepo wa Mungu ndio upendo wa kidugu kati ya waamini ambao kwa roho moja hushirikiana katika kazi kwa ajili ya imani ya Injili[26] na kujidhihirisha kuwa alama ya umoja.

Aidha, ingawa Kanisa linaukataa kabisa ukani Mungu, hata hivyo linatambua kwa moyo mweupe kwamba wanadamu wote, waamini na wasio waamini, wanapaswa kuchangia katika ujenzi wa haki wa ulimwengu huu, ambapo wanaishi wote pamoja. Nalo haliwezi kufanikishwa bila ya mjadala, au dialogia, unaofanyika kwa moyo mnyofu na kwa busara. Kwa hiyo Kanisa hulaumu ubaguzi kati ya waamini na wasio waamini, ambao baadhi ya serikali za nchi zinauingiza pasipo haki. Na sababu yake ni kwamba [serikali hizo] hazitaki kuzitambua haki zile za msingi za binadamu. Tena Kanisa linadai uhuru wa kweli kwa waamini, ili waruhusiwe kulijenga pia hekalu la Mungu katika dunia hii. Na hatimaye linawaalika wakana Mungu wakubali kuizingatia (considerent) Injili ya Kristo kwa moyo ulio wazi.

Kanisa linajua vizuri kabisa kwamba ujumbe wake huuwiana vema na matarajio ya siri kabisa ya moyo wa binadamu linapotetea hadhi ya wito wa binadamu, na hivyo linawarudishia tumaini wale wote waliokata tamaa ya kwamba kuna kikomo kilicho bora kwa ajili yao. Ujumbe wa Kanisa hauwanyimi binadamu kitu chochote, bali unaleta mwanga, uzima na uhuru kwa ajili ya maendeleo yake. Nje ya ujumbe huo hakuna liwezalo kuuridhisha moyo wa binadamu : “Umetuumba kwa ajili yako, ee Bwana, na moyo wetu hautulii, mpaka utulie ndani yako”[27].

Kristo, aliye Mtu Mpya

22. Kwa kweli ni katika fumbo la Neno aliyefanyika mwili tu kwamba fumbo la binadamu linaangazwa. Maana Adamu, mtu wa kwanza, alikuwa mfano wa yule atakayekuja[28], yaani Kristo Bwana. Naye Kristo, aliye Adamu mpya, akilifunua fumbo la [Mungu] Baba na la upendo wake, hudhihirisha kikamilifu kwa binadamu, binadamu alivyo, na kumjulisha wito wake mkuu. Kwa hiyo, sasa, hakuna la kushangaza ikiwa kweli zote zilizokwisha elezwa hapo juu hupata chemchemi yake katika Kristo na [katika Yeye] kukifikia kilele chake.

Naye ndiye “mfano wa Mungu asiyeonekana” (Kol 1:15)[29]. Tena ndiye mtu mkamilifu, aliyewarudishia wana wa Adamu kufanana kwao na Mungu, yaani ile sura iliyoumbuka tangu awali kwa sababu ya dhambi. Maadam katika Kristo hali ya kibinadamu imechukuliwa bila kumezwa[30], basi, vivyo hivyo, hali hiyo imekuzwa hata katika sisi kwenye hadhi iliyo kuu. Kwa njia ya umwilisho [wake] Mwana wa Mungu amejiunga kwa namna fulani na kila binadamu. Alifanya kazi kwa mikono ya kibinadamu, alifikiri kwa akili ya kibinadamu, alitenda kwa utashi wa kibinadamu[31], na alipenda kwa moyo wa kibinadamu. Akizaliwa na Bikira Maria alijifanya kweli mmoja kati yetu, akifanana nasi katika yote isipokuwa katika dhambi[32].

Mwanakondoo asiye na kosa, alitustahilisha uzima kwa damu yake aliyoimwaga kwa hiari; na katika yeye Mungu alitupatanisha naye na kati yetu [33] na alitupokonya katika utumwa wa shetani na wa dhambi. Hivyo kila mmoja wetu anaweza kutamka pamoja na Mtume [Paulo]: Mwana wa Mungu “alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu” (Gal 2:20). Akiteswa kwa ajili yetu, alituachia kielelezo ili tufuate nyayo zake [34], na pia alitufungulia njia ili tunapoifuata, uzima na mauti vitakatifuzwe na kupata maana mpya.

Aidha, mkristo, akiisha fananishwa na sura ya Mwana aliye mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi[35], hupokea “malimbuko ya Roho” (Rum 8:23), ambayo kwayo huwezeshwa kutimiza sheria mpya ya upendo[36]. Kwa njia ya Roho huyo aliye “amana ya urithi wetu” (Efe 1:14), mtu mzima huumbwa upya kiundani mpaka kufikia “ukombozi wa mwili [wake]” (Rum 8:23): “Ikiwa Roho wake Yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, Yeye aliyemfufua Kristo katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu” (Rum 8:11)[37]. Hakika mkristo anasongwa na haja ya kuupinga ubaya akipitia katika matatizo mengi, na hatimaye kufa. Lakini akiungana na fumbo la kipasaka na kushirikishwa kifo cha Kristo ataulaki ufufuko akiimarishwa na tumaini[38].

Jambo hilo haliwahusu wakristo tu bali pia wanadamu wote wenye mapenzi mema, ambao neema ya Mungu hufanya kazi mioyoni mwao, kwa namna isiyoonekana [39]. Maana Kristo alikufa kwa ajili ya watu wote [40] na wito halisi wa binadamu ndio mmoja, ule wa kimungu. Kwa hiyo lazima tuwe na wazo kwamba Roho Mtakatifu anawajalia watu wote uwezekano wa kushiriki fumbo la kipasaka, kwa jinsi anayoijua Mungu.

Fumbo la binadamu ni kuu na la namna ambayo huangazwa machoni pa waamini kwa njia ya Ufunuo wa kikristo. Kwa njia ya Kristo na katika Kristo hata fumbo la uchungu na mauti hupata nuru, nalo ambalo pasipo Injili hutufadhaisha. Kristo amefufuka na kuangamiza mauti kwa mauti yake, naye ametupatia uzima[41] ili, tukiwa wana katika Mwana, tulie katika Roho: Aba, yaani, Baba![42].

Sura ya Pili

JUMUIYA YA WANADAMU

Madhumuni ya Mtaguso

23. Mandhari mojawapo ya muhimu zaidi katika ulimwengu wa sasa ni kuongezeka kwa mawasiliano kati ya watu, nako kunachangiwa kwa vikubwa na maendeleo ya kiteknolojia ya nyakati zetu. Hata hivyo, mjadala wa kidugu kati ya wanadamu hautimiliki katika maendeleo hayo, bali kwa undani zaidi katika jumuiya ya watu. Nayo inadai heshima kati yao na kwa hadhi kamilifu ya roho [ya kila mtu]. Ufunuo wa kikristo unasaidia sana usitawi wa ushirika kati ya watu; wakati huohuo unatuongoza kufahamu kwa undani zaidi sheria zinazoongoza maisha ya kijamii na zilizoandikwa na Muumba katika maumbile ya kiroho na ya kimaadili ya binadamu.

Hati za Majisterio ya Kanisa zilizotolewa hivi karibuni zilifafanua kwa upana zaidi mafundisho ya kikristo kuhusu jamii ya kibinadamu [43]. Kwa sababu hiyo Mtaguso unakumbushia tu baadhi ya kweli zilizo muhimu zaidi na kueleza misingi yake katika mwanga wa Ufunuo. Aidha, unasisitiza baadhi ya mambo yanayotokana na kweli hizo, na yaliyo muhimu zaidi kwa nyakati zetu.
 
Tabia ya kijumuiya ya wito wa binadamu katika mpango wa Mungu
 
24. Mungu, mwenye kutunza watu wote kama baba, alitaka wanadamu wote waunde familia moja na kutendeana [wao kwa wao] kwa roho ya kidugu. Maana, wote wameumbwa kwa sura ya Mungu ambaye “alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mtu mmoja, ili wakae juu ya uso wa nchi yote” (Mdo 17:26); nao huitwa kwa kikomo kimoja kilekile, yaani Mungu mwenyewe.
 
Kwa hiyo, upendo wa Mungu na wa jirani ndiyo amri ya kwanza na iliyo kuu kuliko zote. Maana tunafundishwa na Maandiko Matakatifu ya kuwa upendo wa Mungu hauwezi kutenganishwa na upendo wa jirani. “Na amri nyingine yoyote inajumlishwa katika neno hili: Mpende jirani yako kama nafsi yako. Kwa hiyo, utimilifu wa sheria ndio upendo” (Rum 13:9-10; taz. 1Yoh 4:20). Na jambo hilo lajidhihirisha kuwa la muhimu sana kwa wanadamu wanaozidi kutegemezana wao kwa wao; tena kwa ulimwengu unaozidi kuunganika siku baada ya siku.

Zaidi, Bwana Yesu akimwomba Baba ili “wote wawe na umoja, kama sisi nasi tulivyo umoja” (Yn 17:21-22) anatuwekea upeo mpya uliofumbika kwa akili ya binadamu. Na papo hapo anatudokezea ufanano kati ya umoja wa nafsi [tatu] za Mungu na umoja wa wana wa Mungu katika ukweli na upendo. Ufanano huo unadhihirisha kuwa binadamu, ambaye hapa duniani ni kiumbe pekee alichotaka Mungu kwa ajili yake chenyewe, hawezi kuvumbua kikamilifu ukweli wake, isipokuwa kwa kujitolea mwenyewe kwa moyo mweupe[44].

 
Kutegemezana baina ya mtu na jamii
 
25. Tabia ya kijamii ya binadamu huonyesha kuwa kukamilishwa kwa ubinadamu na maendeleo ya jamii yenyewe vinategemezana. Hivyo binadamu, kwa vile ni yeye ambaye kwa maumbile yake huhitaji sana maisha ya kijamii, ndiye yeye, na lazima awe yeye, msingi, kiini na lengo la taasisi zote za kijamii [45]. Maadamu maisha ya kijamii si kitu kilicho nje ya mtu, basi binadamu hukua katika vipawa vyake vyote na kuweza kuuitikia wito wake kwa mawasiliano na wenzake, kwa kutimiza wajibu zake kwa ajili ya wengine, na kwa mjadala wa kindugu.
 
Kati ya miungano ya kijamii inayokusaidia kukamilishwa kwa binadamu, mingine, kama vile familia na jamii ya kisiasa, inalingana moja kwa moja na tabia ya ndani ya mtu. Mingine tena inatokana zaidi na utashi wake ulio huru. Katika nyakati zetu hizi kuwasiliana na kutegemezana kati ya watu kunaongezeka kwa sababu nyingi; na kutokana na kuongezeka huko vyama na taasisi mbalimbali huundwa, viwe vya kijamii ama vya kibinafsi ( sive publici sive privati iuris). Tendo hilo, liitwalo “ujamiisho” ( socializatio), halina budi kuandamana na hatari zake, lakini pia linaleta manufaa mengi katika kuimarisha na kukuza vipaji vya binadamu na katika kutetea haki zake [46].

Kwa hiyo basi, watu wanapewa mambo mengi kutokana na maisha haya ya kijamii ili kuutimiliza wito wao, hata wa kidini. lakini, kwa upande mwingine, haipingiki kwamba mara nyingi wanadamu wanapotoshwa katika kutenda mema na kusukumwa kutenda mabaya kutokana na mazingira yenyewe ya kijamii wanamoishi na kuzoea tangu utotoni. Ni yakini kwamba machafuko yanayozuka mara kwa mara katika utaratibu wa kijamii husababishwa kwa kiasi fulani na mivutano itokanayo na mifumo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Lakini kwa undani zaidi machafuko haya asili yake ni katika kiburi na ubinafsi wa binadamu, vinavyoathiri mazingira ya kijamii. Na pale ambapo utaratibu wa mambo huharibiwa kwa matokeo ya dhambi, ndipo binadamu, anayeuelekea ubaya tangu kuzaliwa kwake, hupata misukumo mipya ya kutenda dhambi. Nayo haiwezi kushindwa bila ya bidii nyingi na pasipo msaada wa neema [ya Mungu].

Kustawisha manufaa ya wote
 
26. Kutegemezana [kati ya watu] kunazidi kuwaunganisha wanadamu na kuenea polepole ulimwenguni kote. Hivyo hutokea kwamba manufaa ya wote – yaani ujumla wa hali za maisha ya kijamii zinazowawezesha watu, au kama makundi, au kama mtu mmoja mmoja, kufikia utimilifu wao kikamilifu na upesi zaidi – yanazidi kuwahusisha watu wa dunia nzima mintarafu haki na wajibu kwa wanadamu wote. Kwa sababu hiyo, kila kundi lazima lizingatie mahitaji na matarajio ya makundi mengine na pia manufaa ya wote katika familia nzima ya kibinadamu [47].
 
Wakati huohuo watu wanazidi kuelewa hadhi kuu ya utu wa binadamu, aliye mkubwa kuliko vitu vyote na ambaye wajibu na haki zake zinawahusu wote na haziwezi kuvunjwa. Kwa hiyo, inabidi binadamu aweze kuvipata vitu vyote vile vinavyohitajika ili kuendesha maisha yaistahiliyo hadhi yake ya kibinadamu, kama vile chakula, nguo, makazi, haki ya kujichagulia kwa uhuru hali ya maisha, ya kuunda familia, ya kupata elimu, kazi, sifa nzuri, heshima, ujuzi wa habari unaotakiwa, uwezo wa kutenda kadiri ya mwongozo mnyofu utokanao na dhamiri yake; kisha haki ya kulinda maisha ya binafsi na kuishi katika uhuru ulio na haki pia katika masuala ya dini.
 
Kwa hiyo, mfumo wa kijamii na maendeleo yake havina budi kuyapa kipaumbele manufaa ya watu. Maana katika kuyaratibu mambo lazima kuyalinganisha na utaratibu wa watu, wala si kinyume chake. Na ndivyo alivyoelekeza Bwana mwenyewe aliposema kuwa sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato [48]. Basi utaratibu huo unadaiwa kuendelezwa zaidi na zaidi, kuasisiwa katika ukweli, kutekelezwa katika haki; tena lazima uhuishwe na upendo, na kurekebishwa ili uzidi kuuwiana zaidi na zaidi na hali ya kibinadamu katika uhuru [49]. Ili kulifikia lengo hilo yapasa kuanzisha matengenezo ya fikira na mageuzo ya ndani ya jamii.

Roho wa Mungu ambaye, kwa maongozi ya ajabu, huongoza mwenendo wa nyakati na kutengeneza upya uso wa dunia, anasimamia maendeleo hayo. Basi, chachu ya Injili ilichochea na inaendelea kuchochea kiu hii isiyozimika ya heshima [kwa binadamu].

Heshima kwa binadamu
 
27. Mtaguso ukiyazingatia yale yanayotokana na mawazo hayo na yahitajiyo kukabiliwa upesi zaidi, unakazia sana ile heshima kwa binadamu, ili kwamba kila mmoja amwone jirani yake, bila kubagua, kama “nafsi yake” nyingine. Na afanye hivyo akizingatia maisha yake na njia za kuyaishi inavyostahili [50]. Wala asimwige yule tajiri ambaye hakumshughulikia katu Lazaro aliyekuwa maskini [51].  
 
Siku za leo hasa linatusonga sharti la kujifanya jirani wa kila binadamu na la kutoa huduma kimatendo kwa yule anayepita karibu nasi. [Na ndivyo tutakavyomtendea kila mhitaji], awe mzee aliyeachwa na wote au mfanyakazi mgeni anayedharauliwa pasipo haki, au mhamiaji, au mtoto aliyezaliwa na ujamiano usio halali na ambaye anateswa bila kustahili kwa dhambi ambayo hakuitenda mwenyewe; kisha awe mwenye njaa anayehoji dhamiri yetu akikumbushia sauti ya Bwana isemayo: “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” (Mt 25:40).

Aidha, kila tendo linalodhuru uhai wenyewe ndiyo aibu kabisa kama vile kila aina ya uuaji: uuaji wa kabila zima, utoaji mimba, euthanasia au uuaji wa mtu asiyeweza kuponywa, na pia kujiua makusudi. [Tena ni aibu] matendo yote yanayoathiri uzima wa mtu kama vile kutia vilema, kutesa kimwili na kiakili, bidii ya kugandamiza dhidi ya roho ya mtu. [Kisha ni aibu] kila tendo linalovunja heshima ya kibinadamu kama vile hali zile za maisha zisizostahili kwa mtu, [kwa mfano] kufungwa bila hukumu, kuhamishwa, utumwa, ukahaba, uuzaji wa wanawake na vijana; tena hali nyonge ya kazi inayosababisha wafanyakazi watazamwe kama vyombo viletavyo faida tu, wala si kama watu walio huru na wawajibikaji. Haya yote na mengine yanayofanana na hayo huuchafua ustaarabu wa kibinadamu na hasa huwaharibu wenye kuyatenda kuliko wale wenye kuteswa nayo. Kisha huipinga heshima ya Muumba.

Heshima na upendo kwa maadui

28. Heshima na upendo ni lazima viwafikie pia wale wenye kufikiri au kutenda tofauti na sisi katika masuala ya kijamii, kisiasa, na hata ya dini. Maana kadiri tutakavyozidi kupenya katika namna zao za kufikiri, kwa ukarimu na upendo mkubwa, ndivyo tutakavyofanikiwa kirahisi kuingia katika mijadala nao.

Ni kweli kwamba upendo na ukarimu wa namna hii hauwezi kutufanya kwa vyovyote tusiujali ukweli na wema. Naam, ni upendo wenyewe unaowasukuma wafuasi wa Kristo wawatangazie watu wote ukweli wenye kukomboa. Lakini lazima kupambanua baina ya kosa, ambalo daima hukataliwa, na mwenye kukosa ambaye daima hushika hadhi ya kiutu hata pale anapochafuliwa na mawazo madanganyifu na yasiyo kamili kuhusu dini [52]. Mungu peke yake ndiye hakimu na mwenye kuichunguza mioyo; kwa hiyo anatukataza kuhukumu hatia ya ndani ya mtu yeyote [53].

Mafundisho ya Kristo yanatudai sisi tuyasamehe pia matukano[54], na yanawahusisha katika amri ya upendo maadui wote. Amri hiyo ndiyo amri ya sheria mpya, “Mmesikia kwamba imenenwa: Umpende jirani yako, na umchukie adui yako. Lakini mimi nawaambia: Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wanaowachukia; waombeeni wanaowaudhi na kuwasengenya” (Mt 5:43-44).

Usawa wa msingi kati ya wanadamu wote, na haki ya kijamii
 
29. Wanadamu wote wamejaliwa nafsi yenye akili na wameumbwa kwa sura ya Mungu; tena wanashiriki maumbile yaleyale na asili ileile; nao, wakiisha kombolewa na Kristo, wanafurahia wito uleule na kikomo kilekile. Kwa hiyo basi, ni sharti kuzidi kuutambua usawa wa msingi kati ya watu wote.
 
Kwa kweli watu wote si sawa kufuatana na uwezo mbalimbali wa kimwili na tofauti za nguvu, za akili na kimaadili. Lakini hata hivyo kila mtindo wa ubaguzi katika haki za msingi za binadamu – uwe katika uwanja wa kijamii au wa kitamaduni, kuhusu jinsia, kabila, rangi, hali ya kijamii, lugha au dini – lazima uachwe na kung’olewa kama kinyume cha mpango wa Mungu. Kweli, yatupasa kusikitika kwa kuwa haki zile za msingi za binadamu hazijapata kuheshimiwa mahali pote. Kwa mfano mwanamke anaponyimwa fursa ya kuchagua kwa uhuru mume wake, au kuambata hali fulani ya maisha, au tena kuwahi katika elimu na utamaduni unaokubaliwa kwa mwanamume tu.

Licha ya hayo, ingawa kati ya wanadamu zipo tofauti zenye haki, hata hivyo usawa wao wa hadhi kama binadamu wataka tupiganie hali ya maisha iliyo ya haki na ya kiutu zaidi. Maana kuwepo kwa tofauti nyingi mno za kiuchumi na kijamii kati ya wanajamii na kati ya mataifa ya familia iliyo moja ya kibinadamu kunaleta taksiri, au kikwazo. Nako kunaipinga haki ya kijamii, usawa na hadhi ya binadamu, kadhalika amani ya kijamii na kimataifa.

Taasisi za kibinadamu, ziwe za binafsi ama za umma, zifanye juhudi ili zipate kuitumikia hadhi ya binadamu na kikomo chake. Na wakati huohuo zikinze kwa ujasiri kila mtindo wa utumikishaji wa kijamii na wa kisiasa, na pia zizitetee haki za msingi za wanadamu walio chini ya dola yoyote ile. Zaidi, taasisi hizi hupaswa polepole kujilinganisha na ile hali ya kiroho iliyo juu kuliko mambo mengine yote, ijapo pengine zitachukua muda mrefu kulifikia lengo linalotarajiwa.
 
Ulazima wa kuishinda tabia ya kibinafsi
 
30. Hatua za mabadiliko ni za kina na za haraka kiasi kwamba zinadai kwa upesi zaidi asiwepo mtu awaye yote ambaye, akiufumbia macho mkondo wa matukio na kutoujali kwa uvivu, anashikilia tabia ya kibinafsi tu. Wajibu wa haki na upendo utazidi kutimizwa ikiwa kila mmoja atatoa mchango wake kwa ajili ya manufaa ya wote, kulingana na uwezo wake ya mahitaji ya wengine. Na hivyo, atazihamasisha na kuzisaidia pia taasisi za umma na za binafsi zilizopo kwa minajili ya kukuza hali za maisha ya wanadamu. Wapo watu ambao, ingawa wanakiri mawazo mapana na yaliyojaa ukarimu, lakini kimatendo huishi daima kama wasingejali kabisa mahitaji ya jamii. Zaidi, walio wengi katika nchi mbalimbali wanapuuzia sheria na maagizo ya kijamii. Wasio wachache tena hawaoni aibu kuepa zile kodi zilizo halali – kwa mbinu mbalimbali za udanganyifu na ulaghai – au masharti mengine ya kijamii. Hatimaye, wengine hawazingatii kanuni kadhaa za maisha ya kijamii kama vile zile zilizowekwa kwa afya ya wote, au zinazoratibisha uendeshaji wa magari. [Kwa kufanya hivyo] hawaelewi kuwa wanahatarisha maisha yao wenyewe na ya wengine kwa uzembe wao.

Ni tendo takatifu kwa wote kuyaingiza masharti ya kijamii katika wajibu zilizo muhimu zaidi za mtu wa kisasa, na kuzitimiza. Maana, kadiri ulimwengu unavyozidi kuunganika, vivyo hivyo ni wazi kuwa masharti ya wanadamu yanavuka mipaka ya makundi mbalimbali na kuenea polepole ulimwenguni kote. Na jambo hilo haliwezekani ikiwa watu binafsi na makundi yao hawashughulikii ndani yao usitawi wa fadhila za kimaadili na za kijamii na kuzishamirisha katika ujamii. Nalo lilenge katika kujitokeza kwa kizazi kipya cha wanadamu wenye kujenga ubinadamu mpya, kwa msaada ulio wa lazima wa neema ya kimungu.

 
Uwajibikaji na ushirikiano
 
31. Ili kila mtu apate kuutimiza kwa bidii zaidi wajibu wa dhamiri yake ( conscientiae officium) mbele yake mwenyewe na mbele ya makundi mbalimbali ambapo anashiriki, basi lazima kila mmoja alelewe kwa makini na kuelekezwa katika nafsi yake kwenye uwanja wa ustaarabu ulio mpana zaidi. [Kwa kusudi hilo] vitumiwe vyombo vile vingi vinavyopatikana siku za leo kwa binadamu. Awali ya yote, mfumo wa malezi ya vijana wanaotoka katika kila tabaka la kijamii hauna budi kulenga katika kuandaa wanaume na wanawake si zaidi wenye elimu ya juu sana bali hasa walio imara katika utu wao, kama inavyodaiwa kwa nguvu na nyakati zetu.
 
Lakini binadamu anaifikia hisia hii ya uwajibikaji kwa shida, kama hali za maisha hazimwezeshi kuitambua hadhi yake na kuuitikia wito wake katika huduma ya Mungu na ya wengine. Kwa kweli mara nyingi uhuru wa binadamu unadhoofishwa iwapo binadamu anakabiliana na umaskini mtupu. Vilevile yeye naye hudunishwa anapokubali kuishi maisha ya raha mno na hivyo kujifungia katika upweke unaojitosheleza. Kinyume chake, [uhuru wa binadamu] unaimarika wakati mtu anapokubali kupambana na magumu yasiyoepukika ya maisha ya kijamii; tena anapokidhi madai yaliyo mengi ya maisha ya pamoja, kisha anapojihusisha kuitumikia jumuiya ya watu.

Kwa hiyo ni lazima kuamsha utashi wa wote ili wachukue nafasi zao katika shughuli za pamoja; Aidha ni lazima kuisifu mifumo ile ya mataifa ambayo huruhusu wengi wa raia wao kushiriki katika uongozi wa maisha ya umma katika hali ya uhuru kamili. Hata hivyo haina budi kuzingatiwa hali halisi ya kila taifa na uimara wa lazima wa madaraka ya kiserikali. Aidha, ili raia wote waweze kukubali kushiriki maisha ya makundi mbalimbali yanayoiunda jamii, basi ni lazima wapate katika makundi hayo mambo mema yawezayo kuvutia na ya kuwaweka tayari kuwatumikia wengine. Kwa hiyo ni halali kudhani kwamba siku zijazo za binadamu zimo mikononi mwa wale walio na uwezo wa kuvipa vizazi vijavyo sababu za kuishi na za kutumaini.

Neno aliyefanyika mwili na mshikamano wa binadamu

32. Kama vile Mungu alivyowaumba wanadamu si kusudi waishi kama watu binafsi, bali wawekwe ili kuunda umoja wa kijamii, vivyo hivyo “ilimpendeza Mungu kuwatakatifuza na kuwaokoa watu, sio mmoja mmoja na pasipo muungano kati yao, bali kwa kuwaunda kama taifa moja lenye kumjua katika ukweli na kumtumikia kitakatifu”[55]. Tangu mwanzo wa historia ya wokovu Mungu mwenyewe aliwateua watu si kama watu binafsi tu, bali pia kama wana wa jumuiya fulani. Maana Mungu, akifunua azimio lake, akawaita wateule hawa “watu wake” (Kut 3:7-12) ambao alifunga Agano nao katika mlima Sinai[56].

Tabia hii ya kijumuiya imekamilishwa na kutimizwa na kazi ya Yesu Kristo. Neno wa Mungu mwenyewe aliyefanyika mwili alitaka kushiriki katika umoja wa wanadamu. Alihudhuria arusi ya Kana, akaingia nyumbani mwake Zakayo, akala pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi. Alifunua upendo wa Baba na wito bora wa wanadamu akiyazingatia masuala ya kawaida zaidi ya maisha ya kijamii na kutumia lugha na mifano ya maisha ya kila siku. Aliyatakatifuza mahusiano kati ya wanadamu, na kabla ya yote yale ya kifamilia, ambayo katika hayo hutoka mahusiano ya kijamii; kwa hiari alizitii sheria za taifa lake. Alitaka kuishi maisha ya mfanyakazi wa nyakati zake na ya nchi yake.
 
Tena katika kuhubiri kwake aliwaamuru wazi wana wa Mungu wazingatiane wao kwa wao kama ndugu. Katika sala yake akaomba wanafunzi wake wote wawe “kitu kimoja”. Zaidi, Yeye mwenyewe alijitoa kwa ajili ya watu wote hata mauti, akiwa Mkombozi wa wote. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yn 15:13). Aidha, akawaamuru Mitume watangaze habari ya Injili kwa mataifa yote, ili wanadamu wapate kuwa familia ya Mungu, ambapo utimilifu wa sheria utakuwa upendo.
 
Mzaliwa wa kwanza kati ya ndugu wengi, baada ya kifo na ufufuko wake aliunda kwa paji la Roho wake jumuiya mpya ya kidugu kati ya wale wote wanaompokea kwa imani na upendo. Nayo ndiyo jumuiya ya Mwili wake, yaani Kanisa, ambamo washirika wake kama viungo wahudumiane wao kwa wao kadiri ya vipawa mbalimbali walivyojaliwa.

Na mshikamano huu ni lazima uwe unakuzwa zaidi na zaidi hata kufikia siku ya kutimilizwa kwake. Hapo ndipo ambapo wanadamu, wakishaokolewa kwa neema, watampa Mungu utukufu uliokamilika, kama familia iliyopendwa naye, pia na Kristo aliye ndugu yao.

Sura ya Tatu

UTENDAJI WA BINADAMU ULIMWENGUNI

 
Kuwekwa kwa suala  
 
33. Kwa njia ya kazi na maarifa yake binadamu daima amefanya bidii ili kuyaendeleza maisha yake. Aidha, leo, hasa kwa msaada wa sayansi na teknolojia, amepanua na anaendelea kuupanua utawala wake karibu juu ya ulimwengu mzima. Tena, hasa kwa msaada wa ongezeko la njia mbalimbali za mawasiliano kati ya mataifa, familia ya wanadamu imeifikia polepole hatua ya kujitambua na kujitengeneza kama jumuiya moja katika dunia nzima. Matokeo yake ni kwamba sasa binadamu kwa maarifa na nguvu zake tu hujipatia vitu vingi ambavyo hapo zamani alikuwa akivingojea kutoka nguvu za juu.

Mbele ya bidii hii kubwa sana ambayo siku hizi inawasukuma watu wote, masuala mengi yanajitokeza kati ya wanadamu. Je, maana na thamani ya kazi ya binadamu ni ipi? Je, tuvitumieje vitu hivi vyote? Je, hizi juhudi za watu binafsi na za umma zinalenga wapi? Kanisa linahifadhi hazina ya Neno la Mungu na kuchota miongozo ndani yake kwa taratibu za kimaadili na za kidini. Lakini si mara zote Kanisa linalo jibu lililo tayari kwa masuala yote; hivyo linatamani kuunganisha mwanga wa Ufunuo pamoja na mang’amuzi ya watu wote kusudi liangaze njia ambayo wanadamu wameiingia hivi karibuni.

 
Thamani ya utendaji wa binadamu

34. Jambo hili ni la hakika kwa waamini: utendaji wa binadamu, wa binafsi na wa pamoja, ukitazamwa kwa wenyewe hulingana na azimio la Mungu. Nao ndio ile bidii kubwa ambayo kwayo wanadamu katika mfululizo wa karne hufanya juhudi ili kuboresha hali ya maisha yao. Maana binadamu, aliyeumbwa kwa sura ya Mungu, alipewa amri ili aitiishe dunia na vyote viijazavyo na kuutawala ulimwengu katika haki na utakatifu[57]. Kadhalika, aliamriwa kumrejea Mungu mwenyewe na kuurudisha ulimwengu mzima kwake, akimtambua Yeye kama Muumba wa viumbe vyote ili kwamba kwa njia ya utawala wa binadamu juu ya viumbe vyote, jina la Mungu litukuzwe duniani kote[58].

Jambo hili linazihusu pia kazi za kila siku. Maana wanaume kwa wanawake hupata mahitaji kwa ajili yao na ya familia wakifanya kazi, na hivyo pia hutoa huduma ifaayo kwa jamii. Nao huweza kwa haki kufikiri kwamba kwa kazi yao huendeleza kazi ya Muumba, hutoa huduma kwa ndugu zao, pamoja na mchango wa kila mmoja ili kutimiliza mpango wa Mungu katika historia [59].

Kwa hiyo wakristo hawapinganishi kabisa matokeo ya maarifa na uwezo wa binadamu dhidi ya uweza wa Mungu, kana kwamba kiumbe chenye akili kingekuwa mshindani wa Muumba. Bali kinyume chake [wakristo] husadiki kuwa ushindi wa binadamu ni alama ya ukuu wa Mungu na tunda la mpango wake wa ajabu. Na kadiri uwezo wa wanadamu unavyozidi kukua, ndivyo uwajibikaji wao wa binafsi na wa pamoja unavyozidi kupanuka. Tokea hapo huonekana kwamba ujumbe wa kikristo, mbali na kuwatoa wanadamu katika wajibu wao wa kuijenga dunia, tena mbali na kuwahimiza kutojali manufaa ya wenzao, huwahusisha na hayo yote kwa sharti linalowafungamanisha zaidi[60].

Utaratibu wa utendaji wa binadamu
 
35. Kwa kweli utendaji wa binadamu, kama vile unavyotokana na binadamu, vivyo hivyo hulenga katika binadamu. Maana binadamu anapofanya kazi hatengenezi tu mambo na jamii, bali pia hujikamilisha mwenyewe. Anajifunza mengi, anakuza uwezo wake, anasukumwa kutoka katika ubinafsi wake, na kuongeza kipawa chake. Maendeleo hayo, yakieleweka vizuri, yana thamani kubwa kuliko utajiri wa nje unaoweza kulimbikizwa. Binadamu thamani yake ni alivyo, kuliko alivyo navyo [61]. Hali kadhalika yale yote wayatendayo wanadamu ili kupata haki iliyo kubwa zaidi, udugu ulio mpana zaidi, na mfumo wa mahusiano ya kijamii yaliyo ya kiutu zaidi, haya yana thamani kubwa kuliko maendeleo ya kiteknolojia. Nayo maendeleo ya kiteknolojia yatupatia dutu ( materiam) kwa maendeleo ya binadamu, lakini peke yake hayawezi kwa namna yoyote kuyatimiliza [maendeleo ya binadamu].

Hii ndiyo kanuni ya utendaji wa kibinadamu: kwamba utendaji huo ulingane na manufaa halisi ya wanadamu, kadiri ya mpango wa Mungu na mapenzi yake; tena umwezeshe kila binadamu kama mtu binafsi na kama mshirika wa jamii kuusitawisha na kuutekeleza wito wake kikamilifu.

 
Uhalali wa kujiratibisha kwa mambo ya dunia
 
36. Watu wengi wa siku hizi wanaonekana kuhofia kwamba, kama mahusiano kati ya utendaji wa binadamu na dini yanafungamamishwa mno, uwezekano wa kujitawala wa binadamu, jamii na sayansi utazuiliwa.
 
Pengine tunaweza kuelewa kwamba “[tendo la] kujiratibisha kwa mambo ya dunia” ( terrenarum rerum autonomiam) lina msingi kwamba vitu vilivyoumbwa pamoja na jamii zenyewe vina sheria na tunu zake; na binadamu anapaswa polepole kuzivumbua tunu hizo, kuzitumia na kuzipanga. Ikiwa tutaelewa hivyo, basi tendo hilo ni dai lililo halali. Tena dai hilo halitakiwi tu na wanadamu wa nyakati zetu, bali linalingana na mapenzi yake Muumba. Maana ni kwa nguvu yenyewe ya kuumbwa kwao, kwamba viumbe vyote vinapata uthabiti wao wa pekee, ukweli na wema wao pamoja na sheria na utaratibu wao. Mwanadamu apaswa kuyaheshimu hayo yote kwa kuzitambua mbinu mahususi za kila sayansi na ufundi. Kwa hiyo, utafiti wenye mpango ukifanyika katika nyanja mbalimbali za ujuzi, hautapingana kweli na imani, kama ukifanyika kweli kisayansi na kufuata taratibu za kimaadili. Maana mambo ya kidunia na yale ya kiimani, asili yake ni katika Mungu yuleyule [62]. Tena yule ajibidishaye kuzichunguza siri za mambo kwa unyenyekevu na saburi, hata asipojua, mkono wa Mungu ndio unaomwongoza. Maana Mungu ndiye anayevitunza vitu vyote na kuvifanya viwe kama vilivyo. Tupate hapa nafasi ya kulaumu namna kadhaa za fikra, ambazo pengine hazikosekani hata kati ya wakristo, zinazotokana na kutokueleweka kwa kutosha uhalali wa sayansi kuzifuata kanuni zake. Fikra hizo zimezua mapingano, mabishano na kuwavuta wengi mpaka wakafikia hatua ya kudhani kwamba sayansi na imani vinapingana kati yake [63].

Lakini, ikiwa kwa usemi “tendo la kujiratibisha kwa mambo ya dunia” inaeleweka kuwa vitu vilivyoumbwa havimtegemei Mungu, tena kuwa binadamu huweza kuvitumia bila ya kuvielekeza kwa Muumba, [basi ikieleweka hivyo,] wale wote wenye kumwamini Mungu wanahisi jinsi kauli hizo zilivyo za udanganyifu. Maana kiumbe bila Muumba hutoweka. Kwa vyovyote, wote wenye kuamini dini yoyote ile, wamegundua daima sauti ya Mungu na ufunuo wake katika lugha za viumbe. Zaidi, kwa kumsahau Mungu, kiumbe chenyewe kinatiwa giza.

 
Utendaji wa binadamu ulioharibiwa na dhambi
 
37. Maandiko Matakatifu, ambayo mang’amuzi ya karne nyingi hupatana nayo, yanawafundisha watu kuwa, ijapo maendeleo yao ni kitu chema sana kwa binadamu, huleta kishawishi kikubwa ndani yake. Maana mpangilio wa tunu [za binadamu] ( ordine valorum) umevurugwa, ubaya na wema vimechanganyikana, watu binafsi na makundi mbalimbali wanazingatia mambo yao wenyewe tu, wala si yale ya wengine. Hivyo dunia inakoma kuwa mahali pa mahusiano ya kidugu, wakati ambapo kuongezeka kwa uwezo wa kibinadamu kunatishia kuangamiza watu wote.  
 
Maana historia yote ya binadamu imejaa mapambano magumu dhidi ya nguvu za giza. Mapambano haya yalianza tangu mwanzo wa dunia, nayo yataendelea, asemavyo Bwana, mpaka siku ya mwisho [64]. Binadamu, akiwa katika vita hivi, lazima apambane bila kukoma ili aweze kuambatana na mema; wala hataweza kuufikia umoja wake wa ndani, bila juhudi kubwa, pamoja na msaada wa neema ya Mungu.  
 
Kwa sababu hiyo Kanisa la Kristo, likiutegemea mpango wa Muumba, linakubali kuwa maendeleo ya kibinadamu yanaweza kuisaidia heri halisi ya wanadamu. Lakini wakati huohuo halina budi kuyatangaza maneno ya Mtume [Paulo]: “Msitake kuifuatisha namna ya dunia hii” (Rum 12:2), yaani ile roho ya ubatili na ya uovu inayopotosha utendaji wa binadamu uliolengwa katika utumishi wa Mungu na wa mtu, kuwa chombo cha dhambi.

Kama mtu angalituuliza, “Je, ni kwa njia gani hali hii duni ingeweza kushindwa?” Wakristo tungejibu kuwa utendaji wote wa kibinadamu, unaohatarishwa kila siku na kiburi na kujipenda kusiko na utaratibu, lazima usafishwe na kukamilishwa kwa njia ya msalaba na ufufuko wa Kristo. Maana binadamu, akishaokolewa na Kristo na kuwa kiumbe kipya katika Roho Mtakatifu, anaweza na anapaswa kuvipenda pia vitu vile alivyoviumba Mungu. Anavipata kutoka kwa Mungu, anavitazama na kuviheshimu kana kwamba vinatoka wakati huohuo mikononi mwa Mungu. Anamshukuru [Mungu] Mhisani kwa hivyo; na akivitumia na kuvifurahia viumbe hivi katika ufukara na uhuru wa kiroho, huingizwa katika utawala wa ulimwengu kana kwamba ni mtu asiye na kitu, bali yu mwenye vitu vyote[65]: “Maana vyote ni vyenu: nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu” (1Kor 3:22-23).

Utendaji wa binadamu hufikishwa katika ukamilifu wake kwenye fumbo la Pasaka

38. Neno wa Mungu, ambaye kwa njia yake vitu vyote viliumbwa, aliutwaa mwili Yeye mwenyewe, akaja kukaa katika dunia ya wanadamu[66], akaingia katika historia ya ulimwengu kama binadamu kamili, na akaichukua na kuijumlisha ndani yake[67]. Naye hutufunulia kuwa “Mungu ndiye upendo” (1Yoh 4:8) na hutufundisha kuwa sheria ya msingi ya utimilifu wa binadamu, na pia ya mageuzo ya ulimwengu, ndiyo amri mpya ya upendo. Kwa hiyo wale wote wanaouamini upendo wa Mungu, wanahakikishiwa naye kuwa njia ya upendo imewekwa wazi kwa watu wote. Tena wanathibitishwa kwamba juhudi zinazokusudia kutimiza udugu wa wote, si za bure. Vilevile [Neno wa Mungu] anatuhimiza tusienende kwenye njia ya upendo katika mambo makubwa tu, bali hasa katika mazingira ya kawaida ya maisha. Akiyastahimili mauti kwa ajili yetu sisi sote wenye dhambi[68], hutufundisha kwa mfano wake kuwa tunapaswa pia kubeba msalaba. Huo ndio ule msalaba ambao mwili na ulimwengu (caro et mundus) huwatwisha mabegani mwao wote watafutao amani na haki. Kwa njia ya ufufuko wake aliwekwa kuwa Bwana, Yeye aliye Kristo, na akapewa mamlaka yote duniani na mbinguni[69]. Naye anaendelea kufanya kazi hadi leo mioyoni mwa wanadamu kwa nguvu ya Roho wake, si kwa kuamsha tu ari ya ulimwengu ujao, bali pia kwa kuhamasisha, kusafisha, na kuimarisha matarajio mema. Ni kwa njia ya matarajio hayo kwamba familia ya wanadamu inajitahidi kuyafanya maisha yake yawe ya kiutu zaidi na kuitiisha dunia nzima kwa kusudi hilo. Lakini vipawa vya Roho ni vya aina nyingi: watu wengine anawaita kutoa ushuhuda wazi wa makao ya mbinguni kwa njia ya hamu yao [ya kutaka kufika huko]. Kwa njia hiyo wataifanya [hamu hiyo] iendelee kuwa hai kati ya wanadamu. Tena wengine anawaita kujitoa kwa utumishi wa wanadamu hapa duniani ili kwamba kwa huduma hiyo wapate kuzitayarisha njia za ufalme wa mbinguni. Lakini Roho Mtakatifu huwafanya wote wawe watu huru, wenye kukataa ubinafsi na kuzishirikisha nguvu zote za kidunia katika maisha ya kibinadamu. Hivyo [nao] wataweza kujielekeza kwenye maisha yajayo ambapo watu wote watapata kuwa sadaka inayokubalika kwa Mungu[70].

 
Bwana amewaachia wafuasi wake amana ya tumaini hilo na chakula cha safari katika sakramenti ile ya imani ambayo ndani yake vitu vya kawaida vinavyolimwa na binadamu hugeuzwa kuwa Mwili na Damu yake tukufu. Hiyo ndiyo karamu ya ushirika wa kidugu na kama onjo la karamu ya mbinguni.
 
Dunia mpya na mbingu mpya
 
39. Sisi hatujui wakati wa utimilifu wa dunia na wa ubinadamu [71], wala hatujui jinsi ulimwengu utakavyobadilika. Sura ya ulimwengu huu ulioharibiwa na dhambi inapita [72]. Lakini twafundishwa [toka katika ufufuo] kuwa Mungu anatayarisha makao mapya na dunia mpya itakamotawala haki [73], na ambamo heri yake itashibisha na kupita tamaa zote za amani ziibukazo mioyoni mwa watu [74]. Hapo ndipo mauti itakaposhindwa, wana wa Mungu watafufuliwa katika Kristo, na kile kilichopandwa katika udhaifu na uharibifu kitaivaa hali ya kutokufa [75]. Upendo na matunda yake ndivyo vitakavyobaki [76], na mambo yote yaliyoumbwa na Mungu kwa ajili ya binadamu yataokolewa na utumwa wa ubatili [77].
 
Bila shaka tunaonywa kuwa hakuna linalomfaa mtu, ikiwa anaupata ulimwengu wote, lakini anajipoteza mwenyewe [78]. Hata hivyo kungojea dunia mpya, mbali na kuidhoofisha juhudi katika kazi inayoihusu dunia ya sasa, huichochea; mwili wa familia mpya ya wanadamu hukua, ambao tayari unaweza kutoa sura ambayo ni kivuli cha ulimwengu mpya. Kwa sababu hiyo, ni lazima kutofautisha kwa makini maendeleo ya kidunia na ongezeko la Ufalme wa Kristo. Hata hivyo maendeleo hayo yana umuhimu mkubwa kwa Ufalme wa Mungu [79], kwa kadiri yanavyoweza kuchangia kuratibisha vizuri zaidi jamii ya kibinadamu.

Maana, baada ya sisi kueneza duniani [kote] matunda yote mema ya maumbile na utendaji wetu – yaani hadhi ya binadamu, udugu na uhuru – katika Roho wa Bwana na kadiri ya amri yake, basi tutayapata tena baadaye yakiwa sasa yameshafishwa na kila doa, yameng’arishwa na yamegeuzwa, Kristo atakapomkabidhi Baba Ufalme wa milele na wa ulimwengu mzima: “ambao ni ufalme wa ukweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, mapendo na amani”[80]. Basi, hapa duniani Ufalme huo tayari upo katika fumbo; lakini katika ujio wa Bwana utaufikia utimilifu wake.

Sura ya Nne

UTUME WA KANISA KATIKA ULIMWENGU WA SASA

 
Mahusiano ya Kanisa na ulimwengu
 
40. Yote tuliyoyazungumzia hapo juu mintarafu hadhi ya binadamu, jamii ya watu, na maana ya ndani ya utendaji wa binadamu, ndio msingi wa mahusiano kati ya Kanisa na ulimwengu na pia wa dialogia kati yao [81]. Kwa sababu hiyo, katika mwanga wa yale yote yaliyokwisha kutangazwa rasmi na Mtaguso kuhusu fumbo la Kanisa, katika sura hii [Mtaguso] unadhamiria kutafakari juu ya Kanisa lililopo katika ulimwengu na linaloishi na kutenda kazi pamoja nao.

Kanisa linalotoka katika upendo wa Baba wa milele[82], limeanzishwa na Kristo Mwokozi katika ulimwengu wa nyakati, limekusanywa katika Roho Mtakatifu[83], na linalenga katika ukombozi wa maisha ya baadaye ambayo hayawezi kupatikana kikamilifu isipokuwa katika ulimwengu ujao. Aidha, Kanisa lipo hapa duniani na limeundwa na wanadamu ambao ni washiriki wa mji wa dunia hii. Nao huitwa, kuanzia tayari katika historia ya binadamu, kuunda familia ya wana wa Mungu inayopaswa kukua siku kwa siku mpaka Bwana atakapokuja. Familia hiyo, iliyounganishwa kwa ajili ya mema ya mbinguni na inayotajirishwa nayo, “iliundwa na kupangwa kama jamii katika ulimwengu huu”[84]. Nayo imepewa “misaada inayofaa kwa ajili ya umoja uonekanao na wa kijamii”[85]. Kwa hiyo, Kanisa ambalo kwa wakati mmoja ni “kusanyiko linaloonekana na jumuiya ya kiroho”[86] linatembea pamoja na wanadamu wote na linaionja pamoja na ulimwengu bahati ileile ya kidunia. Vilevile Kanisa ni kama chachu na kama roho ya jamii ya kibinadamu[87] inayoelekea kufanyika upya katika Kristo na kugeuka kuwa familia ya Mungu.

Upenyezano wa namna hii kati ya mji wa duniani na mji wa mbinguni hauwezi kuhisika kwa hakika ila kwa njia ya imani. Zaidi, fumbo la historia ya kibinadamu linabaki; nayo historia itaendelea kuchafuliwa na dhambi hadi mwangaza wa wana wa Mungu utakapodhihirika wazi. Ni kweli kwamba Kanisa likifuatilia lengo lake la wokovu halimshirikishi binadamu maisha ya kimungu tu, bali pia linaeneza mwanga wake unaoakisiwa kwa namna fulani duniani kote. Na Kanisa linalifikia lengo hilo kwa sababu linaponya na kuinua hadhi ya binadamu, linaimarisha jamii ya kibinadamu, na kutia maana ya ndani zaidi na kusudi lake katika kazi za kila siku za wanadamu. Hivyo, Kanisa linaamini kuwa, kwa njia ya kila mwanakanisa na ya jumuiya yake kwa pamoja, linaweza kuchangia kwa vikubwa kuifanya familia ya wanadamu na historia yake viwe vya kiutu zaidi.

Aidha, Kanisa katoliki kwa furaha linathamini mchango uliotolewa na unaoendelea kutolewa na Makanisa mengine na jumuiya za kikanisa kwa kusudi la kutekeleza jukumu lilelile. Wakati huohuo Kanisa linasadiki kuwa ulimwengu unaweza kusaidia sana na kwa namna nyingi katika kuweka matayarisho ya Injili. Yaani kila mtu, na jamii wa kibinadamu kwa ujumla, huleta mchango wa vipawa na bidii zake. Basi, hapa Mtaguso unadhamiria kufasiri baadhi ya miongozo iliyo muhimu zaidi ili kuhamasisha ipasavyo katika kubadilishana na kupeana msaada mintarafu masuala ambayo kwa namna fulani yahusu Kanisa na ulimwengu kwa pamoja.

Msaada unaonuiwa kutolewa na Kanisa kwa kila mtu

41. Binadamu wa siku hizi yupo katika njia inayoelekea kuupevusha kikamilifu zaidi utu wake na inayomwezesha kuvumbua wazi zaidi haki zake na kuzifuatilia. Lakini Kanisa limekabidhiwa wajibu wa kudhihirisha fumbo la Mungu ambalo ndicho kikomo cha mwisho cha kila mtu. Kwa hiyo, wakati huohuo Kanisa linamfunulia binadamu umaana wa maisha yake mwenyewe, yaani ukweli wa ndani wa binadamu. Nalo hujua vema kuwa ni Mungu peke yake tu, ambaye kwa utumishi wake linajitolea, anayetoa jibu kwa zile hamu zilizo za ndani zaidi za moyo wa binadamu, usioweza kamwe kushibishwa kikamilifu na mali za kidunia. Tena [Kanisa] hujua kuwa binadamu, akisukumwa pasipo kukoma na Roho wa Mungu, hawezi kamwe kupuuzia suala la dini. Na ndivyo inavyoonyeshwa, si tu na mang’amuzi ya karne zilizopita, bali pia na shuhuda nyingi za nyakati zetu. Maana [binadamu] atatamani daima kujua, hata isivyo dhahiri, maana ya maisha yake, ya kazi yake na ya kifo chake. Nalo Kanisa linakumbushia hoja hizo kwa kuwepo kwake tu hapa duniani. Lakini Mungu peke yake, aliyemwumba binadamu kwa sura yake na kumkomboa kutoka katika dhambi, anatoa jibu maridhawa kabisa kwa masuala haya. Nalo jibu hutolewa kwa njia ya ufunuo upatikanao katika Mwanae aliyefanyika mwili. Yeyote amfuataye Kristo, aliye mtu kamili, yeye naye anazidi kujikamilisha katika utu wake.

Kutokana na imani hiyo, Kanisa linaweza kuopoa hadhi ya binadamu kutoka katika kauli zile zote zenye hali ya kubadilikabadilika, kwa mfano zile ambazo zinatweza mno mwili wa kibinadamu, ama kuukuza mno. Hakuna sheria ya kibinadamu iwezayo kuiweka salama namna hii hadhi ya mtu na uhuru wake kama ifanyavyo Injili ya Kristo iliyokabidhiwa kwa Kanisa. Maana Injili hii inauhubiri na kuutangaza uhuru wa watoto wa Mungu, inakataa kila mtindo wa utumwa utokanao na dhambi [88], inaheshimu hadhi ya dhamiri na hiari yake ya kuamua kama vitu vilivyo vitakatifu. Tena Injili haikomi kuhamasisha kujiongezea talanta za kibinadamu katika utumishi wa Mungu na kwa manufaa ya watu. Kisha, inamkabidhi kila mmoja kwa wengine wote ili wampende [89]. Jambo hilo linalingana na sheria ya msingi ya mpango wa kikristo. Maana Mungu Mkombozi na Mungu Muumbaji ni Mungu yuleyule; tena Bwana wa historia ya kibinadamu na Bwana wa historia ya wokovu ndiye Bwana yuleyule. Lakini hata hivyo katika utaratibu huo wa kimungu, kujitawala kwa haki kwa kiumbe ( iusta creatura autonomia), hasa kwa binadamu, hakuondolewi, bali zaidi kunarudishwa katika hali ya hadhi yake na kuimarishwa katika hiyo.

Kwa sababu hiyo Kanisa, kwa nguvu ya Injili liliyokabidhiwa, linatangaza haki za wanadamu, na linatambua na kuthamini sana juhudi zinazofanyika siku za leo ili haki hizo zikuzwe popote. Lakini uamsho (motus) huo hauna budi kupenywa na roho ya Injili, na kulindwa dhidi ya kila tabia danganyifu inayodai binadamu ajitawale. Maana tunashawishiwa kufikiri kuwa haki za kila mmoja wetu zinahifadhiwa pale tu ambapo tunafunguliwa na kila sharti la sheria ya kimungu. Lakini kwa njia hii hadhi ya binadamu haiwezi kuokolewa; ila zaidi inapotea.

Msaada unaonuiwa kutolewa na Kanisa kwa jamii ya kibinadamu
 
42. Muungano wa familia ya wanadamu unaimarishwa sana na kutimilizwa na umoja wa familia ya watoto wa Mungu inayoasisiwa katika Kristo [90].
 
Bila shaka utume maalum uliokabidhiwa na Kristo kwa Kanisa lake, haupo katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, na kijamii. Maana lengo aliloliweka Kristo kwa ajili ya Kanisa lipo katika uwanja wa kidini [91]. Lakini kutokana na utume huo wa kidini hutiririshwa wajibu, mwanga na nguvu, viwezavyo kuchangia katika kujenga na kuimarisha jamii ya wanadamu kadiri ya sheria ya Mungu. Hivyo, pale panapohitajika na kadiri ya mazingira ya nyakati na mahali, Kanisa nalo huweza na hupaswa kuamsha matendo yakusudiayo katika utumishi wa watu wote, lakini hasa kwa wahitaji; kama vile kufanya matendo ya huruma na mengine yanayofanana na hayo.

Aidha, Kanisa linayatambua yale mema yote yaliyopo katika mkikimkiki wa kijamii (dynamismo sociali) wa siku za leo: na hasa huyatambua maendeleo ya kuufikia umoja, ushirikisho ulio bora na muungano wa kijamii na kiuchumi. Maana kuhamasisha umoja kunawiana na utume halisi wa Kanisa, ambalo “katika Kristo ni kama sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote”[92]. Hivyo Kanisa lenyewe linauonyesha ulimwengu kwamba muungano halisi wa kijamii [unaoonekana] kwa nje hutokana na muungano wa fikara na wa mioyo, yaani hupatikana kutoka katika imani na upendo ambao kwao umoja wake una msingi madhubuti katika Roho Mtakatifu. Maana nguvu ambazo Kanisa linaweza kuzipenyeza katika jamii za kibinadamu za siku hizi ni imani na upendo ambavyo vinapata kugeuzwa kuwa matendo katika maisha; wala nguvu hizo za Kanisa hazimo katika kutawala milki yoyote ile ya kidunia kwa njia za kibinadamu tu.

Aidha, kutokana na utume wake na maumbile yake, Kanisa halifungamani na mtindo wowote wa utamaduni wa kibinadamu, au mfumo wa kisiasa, wa kiuchumi au wa kijamii. Basi kwa sababu ya hali yake ya kuenea pote, Kanisa linaweza kufungamanisha kwa namna ya pekee jamii za kibinadamu na pia mataifa, ilimradi yawe na imani na Kanisa na kuutambua kimatendo uhuru wake halisi wa kutimiliza utume wake. Ndiyo maana Kanisa linawaonya watoto wake, kama vile wanadamu wote, kusuluhisha kila mgogoro kati ya mataifa na makabila katika roho ile ya kifamilia ambayo ndiyo tabia ya watoto wa Mungu. Kadhalika waimarishe kiundani vyama vya wanadamu vilivyo vya haki.

Basi, Mtaguso unazingatia kwa heshima kubwa kila kilicho cha kweli, chema na cha haki, kipatikanacho katika taasisi mbalimbali ambazo wanadamu wamejiundia na wanazoendelea kuzitengeneza. Aidha, Mtaguso unatangaza kuwa Kanisa linataka kuzisaidia na kuzihamasisha taasisi hizo zote, kutegemeana na uamuzi wake na kadiri zinavyolingana na utume wake. Hakuna lolote ambalo Kanisa linalitamani zaidi kuliko kuyatumikia mafaa ya watu wote; tena kuliko kupata uhuru wa kuenea chini ya mfumo wowote wa utawala (quovis regimine) unaoziheshimu haki za msingi za binadamu na za familia na unaoyatambua madai ya manufaa ya wote.

Msaada unaonuiwa kutolewa na Kanisa kwa utendaji wa binadamu kwa njia ya wakristo

43. Mtaguso unawahimiza wakristo, walio raia wa miji yote miwili, [yaani mji wa duniani na mji wa mbinguni], wafanye bidii kutekeleza kwa uaminifu wajibu zao za kidunia, wakiongozwa na roho ya Injili. Wapo waamini ambao, wakijua kuwa wao hawana uraia wa kudumu hapa duniani bali wanautafuta ule ujao,[93] wanadhani kwamba kwa sababu hiyo wanaweza kuzembea wajibu zao za kidunia. Hao basi wanakosa, wala hawafikirii kuwa ni imani yenyewe inayowashurutisha zaidi kuzitekeleza, kadiri ya wito wa kila mmoja[94]. Lakini vilevile wanakosa ambao, kinyume chake, hudhani kuwa wanaweza kujizamisha kabisa katika shughuli za kidunia, kana kwamba hizo zingekuwa geni sana kwa maisha ya kidini. Nayo hutazamwa tu machoni pao kama mkusanyiko wa ibada mbalimbali na masharti kadhaa ya kimaadili. Utengano unaoonekana katika fikra za wengi kati ya imani wanayoikiri na maisha yao ya kila siku hauna budi kuhesabiwa kati ya makosa makubwa zaidi ya nyakati zetu. Tangu Agano la Kale manabii walikuwa wanatoa kwa nguvu makaripio yao dhidi ya kikwazo hicho[95]. Na zaidi sana katika Agano Jipya, Yesu Kristo mwenyewe alitoa tishio la adhabu kali [kwa wenye fikra za namna hii][96]. Kwa hiyo, lisiwekwe pingamizi hata kidogo kati ya utendaji wa kikazi na kijaamii kwa upande mmoja, na maisha ya kidini kwa upande mwingine. Mkristo mwenye kupuuza wajibu zake za hapa duniani anapuuza wajibu zake kwa jirani, na pia kwa Mungu mwenyewe; na hivyo kuhatarisha uzima wake wa milele. Basi wakristo wafurahie katika kutekeleza utendaji wao wote wa kidunia wakiufuata mfano wa Kristo aliyekuwa mtu mwenye ufundi wa kazi. Nao wafungamanishe bidii za kibinadamu, za kinyumbani, za kiufundi, za kisayansi na za kiteknolojia katika kuleta mfumo mmoja wenye uhai pamoja na thamani za kidini. Na chini ya uongozi wa juu sana wa thamani hizo mambo yote yaunganishwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

Walei ndio wahusika maalumu katika shughuli na utendaji wa kidunia, ingawa siyo wao peke yao. Kwa hiyo, wakati walei wanapotenda kama raia wa ulimwengu, wawe kila mmoja peke yake ama kwa kushirikiana kwa pamoja, wataziheshimu sheria mahususi za kila fani; lakini pia watajitahidi kujipatia ustadi halisi katika nyanja zile. Tena, watatoa kwa hiari mchango wa ushirikiano wao kwa wale wote wanaolenga katika shabaha zilezile. Wakiheshimu madai ya imani na wakijawa na nguvu yake, wabuni maarifa mapya bila kukoma na, pale panapohitajika, wayatekeleze. Ni wajibu wa dhamiri yao iliyokwisha kuundwa ipasavyo, kuiandika sheria ya kimungu katika maisha ya mji wa duniani. Nao, kutoka kwa makuhani, watarajie kupewa mwanga na nguvu ya kiroho. Lakini wasifikiri kuwa wachungaji wao ni daima mabingwa kuhusu mambo haya kiasi kwamba wakati wowote wana jawabu tayari kwa kila suala lijitokezalo; wala huo sio wajibu maalumu [wa wachungaji]. Bali walei wenyewe washike wajibu zao, katika mwanga wa hekima ya kikristo, na wazingatie kwa heshima mafundisho ya Majisterio [97].

Mara nyingi mtazamo wenyewe wa kikristo juu ya mambo ya maisha utawaongoza kupata jawabu fulani katika hoja mbalimbali. Lakini hata hivyo, kwa unyofu ulio sawa, waamini wengine wataweza kutoa maoni yaliyo tofauti mintarafu hoja ileile. Nalo, linatokea mara nyingi na kwa halali. Maana, kama watu wengi watalinganisha kwa urahisi jawabu moja au jingine na ujumbe wa Injili, basi walei wakumbuke kuwa hakuna mtu anayeruhusiwa kudai kwamba uongozi wa Kanisa unahalalisha maoni yake tu. Bali watafute daima njia ya kuongozana wao kwa wao kwa njia ya mijadala isiyo na hila, wakishikilia daima upendo na kuyashughulikia awali ya yote manufaa ya wote.

Walei, walio na wajibu za kimatendo katika maisha yote ya Kanisa, hawapaswi tu kuipenyeza roho ya kikristo katika ulimwengu, bali pia wanaitwa kuwa mashahidi wa Kristo kati ya watu wote, yaani pia katika jamii ya kibinadamu.
 
Maaskofu, waliokabidhiwa wajibu wa kuliongoza Kanisa la Mungu, wauhubiri pamoja na Mapadre wao ujumbe wa Kristo, ili kwamba utendaji wote wa kidunia wa waamini upate kung’arishwa na mwanga wa Injili. Aidha, wachungaji wote wakumbuke kuwa, kwa njia ya tabia na ari yao ya kila siku [98], wanaudhihirishia ulimwengu uso wa Kanisa, ambao kwa msingi huo wanadamu wanajitengenezea kauli kuhusu nguvu na ukweli wa ujumbe wa kikristo. Kwa maisha na maneno [yao] wao, pamoja na watawa na waamini, waonyeshe kuwa Kanisa, kwa kuwepo kwake tu, pamoja na vipawa vyake vyote vilivyomo ndani yake, ndiyo chemchemi isiyofifia ya nguvu zile ambazo ulimwengu wa kisasa unazihitaji sana. Kwa kusoma kwa bidii wajiwezeshe kushika nafasi yao katika dialogia na ulimwengu huu, na wanadamu wenye rai mbalimbali. Lakini hasa wayazingatie maneno ya Mtaguso huu: “Kwa kuwa siku hizi wanadamu wanazidi kufungamana wao kwa wao katika maisha ya kiraia, ya kiuchumi na ya kijamii, yawapasa Mapadre, kwa kuunganisha juhudi na kazi zao chini ya uongozi wa Maaskofu na wa Baba Mtakatifu, waondoshe kila sababu ya mfarakano ( dispersionis), kusudi wanadamu wote waongozwe kwenye umoja wa familia ya Mungu.” [99]

Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu Kanisa limebaki daima bibiarusi mwaminifu wa Bwana wake, wala halikuacha kamwe kuwa ishara ya ukombozi hapa duniani. Lakini hata hivyo Kanisa linajua kuwa, katika mlolongo wa karne zilizopita, miongoni mwa wanajumuiya wake[100], makleri kwa walei, hawakukosekana wale ambao hawakuwa waaminifu kwa Roho wa Mungu. Na hata katika nyakati zetu Kanisa linajua vema jinsi ulivyo mbali kati yao ujumbe linaouleta na udhaifu wa kibinadamu wa wale waliokabidhiwa Injili. Lolote liwalo juu ya hukumu ya historia kuhusu makasoro haya, sisi lazima tuyajue na kuyapinga kwa nguvu usije uenezaji wa Injili ukapata kikwazo. Kadhalika, Kanisa linafahamu vizuri jinsi linavyopaswa kukomaa katika mtindo wa mahusiano yake na ulimwengu likisaidiwa na mang’amuzi ya karne zilizopita. Mama Kanisa, akiongozwa na Roho Mtakatifu hatachoka kamwe kuwaonya wana wake “wajitakase na kujitengeneza upya, ili ishara ya Kristo izidi kung’ara kwa nuru angavu juu ya uso wa Kanisa”[101].

Msaada upokewao kutoka kwa ulimwengu wa sasa
 
44. Kama vile ilivyo muhimu kwa ulimwengu kulitambua Kanisa kama chombo chenye nafasi ya kijamii katika historia na kama chachu yake, vivyo hivyo Kanisa nalo linafahamu jinsi lilivyofaidishwa kutokana na historia na maendeleo ya wanadamu.

Mang’amuzi ya karne zilizopita, maendeleo ya sayansi, na hazina zinazofichama katika tamaduni mbalimbali za kibinadamu, hayo yote yanadhihirisha kinaganaga zaidi maumbile ya binadamu mwenyewe. Nayo yanafungua njia mpya zinazoelekeza katika ukweli na yanalinufaisha pia Kanisa. Yaani Kanisa, tangu awali ya historia yake, lilijifunza kufafanua ujumbe wa Kristo likitumia mawazo na lugha za mataifa mbalimbali. Aidha limejitahidi kuufasiri ujumbe huo kwa njia ya hekima ya wanafalsafa. Katika harakati hizo Kanisa linanuia kulinganisha ifaavyo Injili na uwezo wa kuelewa wa watu wote kama vile na madai ya wenye elimu. Na ulinganifu wa namna hii katika kuhubiri lile Neno lililofunuliwa kwa binadamu lazima uendelee kuwa kanuni ya kila uenezaji wa Injili. Maana kwa njia hii, katika kila taifa uwezo wa kufafanua habari ya Kristo unahimizwa kila mahali kwa namna zake. Na wakati huohuo mawasiliano yenye uhai baina ya Kanisa na tamaduni mbalimbali yanahamasishwa[102]. Ili kukuza mawasiliano haya, hasa siku hizi ambapo mabadiliko yanafuatana kwa haraka sana na namna za kufikiri kwa watu zinatofautiana sana, Kanisa linauhitaji kwa namna ya pekee msaada wa wale ambao, kwa kuishi katika ulimwengu huu, ni mafundi katika kuvijua vyombo vya dunia hii na katika fani zake mbalimbali, wawe waamini au wasio waamini. Ni wajibu wa taifa zima la Mungu, na hasa wa wachungaji na wanateolojia, wakisaidiwa na Roho Mtakatifu, kuzisikiliza kwa makini, kuzipambanua na kuzifafanua sauti mbalimbali zinazosikika katika nyakati zetu, na hatimaye kuzichambua (diudicare) katika mwanga wa Neno la Mungu. Na kazi hiyo yote inakusudia ukweli uliofunuliwa kwetu uzidi kueleweka kwa undani zaidi, kufahamika zaidi, nao upate kufafanuliwa kwa namna inayoufaa zaidi.

Kanisa lina muundo wa kijamii unaoonekana, na ambao ni alama ya umoja wake na Kristo. Hivyo linaweza kutajirishwa – na ndivyo lifanyavyo – na maendeleo ya maisha ya kijamii, si kana kwamba lingekuwa na kasoro katika muundo liliopewa na Kristo; bali kusudi lipate kuujua muundo huo kwa undani zaidi; liuonyeshe kinaganaga zaidi na kuulinganisha na nyakati zetu kwa mafanikio maridhawa zaidi. Kanisa linahisi kwa roho ya shukrani kuwa linapewa misaada mbalimbali, kama jumuiya na katika kila mmoja wa watoto wake, kutokana na watu wa kila kiwango na hali. Awaye yote mwenye kuihamasisha jamii ya kibinadamu katika nyanja za familia, utamaduni, maisha ya kiuchumi na ya kijamii, siasa ya kitaifa na kimataifa, huyo huisaidia sana pia jumuiya ya Kanisa kufuatana na mpango wa Mungu na kwa kadiri jumuiya hii inavyotegemea mambo yaliyo nje yake. Zaidi, Kanisa linakiri kwamba limenufaishwa sana na linaweza kuendelea kunufaishwa kutokana na vipingamizi vyenyewe vya wale wanaolikana na kulidhulumu [103].
 
Kristo aliye alfa na omega
 
45. Kanisa, katika kutoa msaada kwa ulimwengu kama vile katika kupewa mambo mengi kutoka kwake, linalidhamiria jambo hili tu: Ufalme wa Mungu uje na wokovu wa wanadamu wote utimizwe. Kila lililo jema, ambalo Kanisa linaipatia familia ya wanadamu, wakati wa hija yake hapa duniani, linatiririka na kutokana na kuwa Kanisa ni “sakramenti ya wokovu kwa wote” ( universale salutis sacramentum) [104] ambayo inafunua na kutimiza fumbo la upendo wa Mungu kwa binadamu.

Maana Neno wa Mungu, ambaye kwa njia yake viumbe vyote viliumbwa, alijifanya mwenyewe mwili ili Yeye, aliye mtu kamili, awaokoe watu wote na kuvijumlisha vitu vyote ndani yake. Bwana ndiye lengo la historia ya kibinadamu, “kitovu cha matarajio ya historia na ya ustaarabu”, kiini cha uzao wa kibinadamu, furaha ya kila moyo, na utimilifu wa matumaini yote[105]. Yeye ndiye ambaye Baba alimfufua kutoka mauti, akamtukuza na kumweka kuumeni kwake akimfanya hakimu wa walio hai na wafu. Nasi, tukihuishwa na kukusanywa pamoja katika Roho wake, tunakwenda kama wahujaji kuulaki utimilifu wa historia ya kibinadamu unaolingana kikamilifu na mpango wa upendo wake, yaani: “kuvijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani” (Efe 1:10).

 
Bwana mwenyewe asema: “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni alfa na omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho” (Ufu 22: 12-13).

SEHEMU YA PILI

BAADHI YA MASWALA YANAYOHITAJIKA KUFAFANULIWA UPESI

 
Utangulizi
 
46. Mpaka hapa Mtaguso umeifafanua hadhi iliyomo katika utu wa binadamu, na wajibu wake anaoitwa kuutekeleza ulimwenguni, uwe wa kibinafsi au wa kijamii. Hivyo, Mtaguso, katika mwanga wa Injili na mang’amuzi ya kibinadamu, sasa unawaalika wote kuzingatia baadhi ya masuala ya siku hizi ambayo ni muhimu sana na ambayo yanawagusa kwa namna ya pekee wanadamu wote.

Miongoni mwa hoja nyingi zinazoamsha juhudi ya watu wote hasa siku hizi, haya yafuatayo yafaa kuyazingatia hasa: ndoa na familia, utamaduni wa kibinadamu, maisha ya kiuchumi na ya kijamii, maisha ya kisiasa, ushirikiano kati ya mataifa, na amani. [Tunapenda kwamba] juu ya kila moja ya masuala hayo, miongozo na mwanga vitokavyo kwa Kristo ving’arishwe. Hivyo, wakristo wapate kuongozwa, na wanadamu wote wapate kuangazwa, katika kuyatafuta masuluhisho kwa hoja nyingi na ngumu namna hii.

Sura ya Kwanza

KUSTAWISHA HESHIMA YA NDOA NA YA FAMILIA

 
Ndoa na familia katika ulimwengu wa kisasa
 
47. Usitawi ( Salus) wa mtu binafsi na wa jamii ya kibinadamu na ya kikristo hufungamana kabisa na hali njema ya jumuiya ya kindoa na ya kifamilia. Kwa hiyo wakristo, pamoja na wote wenye kuiheshimu sana jumuiya hiyo, wanaifurahia kwa moyo mkunjufu misaada mbalimbali ambayo kwayo wanadamu wa siku za leo waweza kuendelea katika kuistawisha jumuiya hiyo ya upendo, na katika kuuheshimu uhai. [Misaada hiyo] inawasaidia watu wa ndoa na wazazi katika kutekeleza jukumu lao muhimu, na kutoka [misaada] hiyo wao hutarajia kupata manufaa yaliyo bora zaidi, pamoja na kufanya juhudi ili itolewe.
 
Lakini hadhi ya ndoa haimuliki kwa mwanga mweupe mahali pote, kwa sababu hutiwa kivuli na mitara, pigo la talaka, uhuru – inavyosemwa – wa mapenzi, na maharibifu mengineyo. Licha ya hayo, mara nyingi upendo wa kindoa unanajisiwa na ubinafsi, upenzitamaa ( hedonismo), na mitindo isiyo halali ya kuzuia uzazi. Aidha, hali za siku hizi za kiuchumi, kisaikolojia-kijamii, na za kiraia, huleta machafuko makubwa katika familia. Kisha, mahali pengine ulimwenguni matatizo yatokanayo na ongezeko la idadi ya watu yanaleta fadhaa. Kutokana na hayo yote huzuka shida nyingi zinazofadhaisha dhamiri za watu. Hata hivyo, thamani na uimara wa asasi ya ndoa na ya familia ( matrimonialis familiarisque instituti) huonyeshwa siku za leo kwa namna ya pekee. Jambo hilo linatokea kwa sababu mageuzo makubwa ya jamii za siku hizi, licha ya magumu ambayo kwa kasi hujitokeza humo, mara nyingi yanadhihirisha kwa njia mbalimbali maumbile halisi ya ndoa na familia zenyewe.

Kwa hiyo Mtaguso, ukiweka wazi vipengere kadhaa vya msingi vya mafundisho ya Kanisa, unadhamiria kuwaangaza na kuwaimarisha wakristo na wanadamu wote wanaojitahidi kulinda na kuhamasisha hadhi ya kimaumbile na thamani ya juu sana na iliyo takatifu ya hali ya ndoa.

 
Utakatifu wa ndoa na familia

48. Ushirikiano wa ndani wa maisha na wa upendo wa ndoa uliasisiwa na [Mungu] Muumbaji na kuratibishwa [naye] kwa sheria maalumu. Nao una asili yake katika agano la ndoa (foedere coniugii), yaani katika makubaliano yasiyotanguka ya kila mmoja (consensu personali). Na hivyo, ndoa ni ushirika unaopata kuwa imara kwa sheria za kimungu na ambao unazaliwa, hata mbele ya jamii, kutokana na tendo lile la kibinadamu ambalo kwalo kila mwanandoa anajitoa kwa mwenzake na anampokea. Kifungo hicho kitakatifu kinachoyakusudia manufaa ya wanandoa, ya watoto na ya jamii, hakiutegemei uhiari wa kiholela (arbitrio) wa binadamu. Kwani Mungu mwenyewe ndiye muundaji wa ndoa; nayo ina tunu na malengo mengi[106] ambayo yote yana umuhimu mkubwa kwa mwendelezo wa uzao wa kibinadamu, kwa maendeleo ya kibinafsi na kwa kikomo cha milele cha kila mmoja wa wanafamilia; tena ina umuhimu mkubwa kwa heshima, uthabiti, amani na usitawi wa familia yenyewe na wa jamii nzima ya wanadamu. Kwa maumbile yake halisi ndoa yenyewe, na upendo wa kindoa, vimepangwa kwa ajili ya uzazi na malezi ya watoto; kilele kama hicho, ndilo taji lake [ndoa]. Na hivyo mwanamume na mwanamke, ambao kwa ajili ya agano la upendo wa kindoa “si wawili tena bali ni mwili mmoja” (Mt 19:6), wanasaidiana na kutumikiana kwa muungano wa ndani wa nafsi na wa utendaji wao. Nao wanang’amua umaana wa umoja wao, na kuufikia kwa utimilifu unaozidi kujikamilisha siku kwa siku. Umoja huo wa ndani, maadamu ni kujitoa kila mmoja kwa mwenzake, unadai uaminifu kamili kati ya wanandoa na unataka umoja huu usivunjwe[107]. Na ndivyo ilivyo pia kwa manufaa ya watoto.

 
Kristo Bwana amemimina baraka zake tele juu ya upendo huo unaojionyesha kwa namna nyingi. Nao umebubujika katika chemchemi ya upendo wa kimungu na kujiunda kwa mfano wa umoja uliopo kati ya Kristo na Kanisa. Maana, kama vile zamani Mungu alivyokutana na taifa lake kwa agano la upendo na uaminifu [108], vivyo hivyo Yesu, aliye mkombozi wa wanadamu na Bwanaarusi wa Kanisa [109], anawajia wakristo wanandoa kwa njia ya sakramenti ya ndoa. Aidha, anaendelea kukaa nao ili waweze kupendana wao kwa wao kwa uaminifu, kwa daima na kwa uradhi wa moyo, kama vile Yesu naye alivyolipenda Kanisa na kujitoa kwake [110]. Upendo halisi wa kindoa unachukuliwa ndani ya upendo wa kimungu na unategemezwa na kutajirishwa na nguvu yenye kukomboa ya Kristo pamoja na utendaji wa wokovu wa Kanisa. Hivyo, wanandoa kweli wanaongozwa kwa Mungu, wanasaidiwa na kuimarishwa katika jukumu lao bora la kuwa baba na mama [111]. Kwa sababu hiyo, wakristo wanandoa wanatiwa nguvu na kama kuwekwa wakfu [112] na sakramenti maalumu kwa ajili ya wajibu na hadhi ya hali yao. Nao wanapata kutekeleza wajibu wao wa kindoa na wa kifamilia kwa nguvu ya sakramenti hii, wakipenyezwa na Roho wa Kristo ambaye kwake maisha yao yote yanajazwa imani, tumaini na mapendo. Na hatimaye wanaelekea kuufikia ukamilifu wao, kila mmoja akimtakatifuza mwenzake; na hivyo wanashirikiana pamoja katika kumtukuza Mungu.
 
Wakiongozwa na mfano wa wazazi pamoja na sala katika familia, watoto na wale wote wanaoishi katika nyumba watapata kwa urahisi zaidi njia ya kulelewa kiutu, njia ya wokovu na ya utakatifu. Na wafunga ndoa, waliopewa heshima na wajibu wa kuwa baba na mama, watatekeleza kwa makini wajibu wao wa kulea, hasa kidini, wajibu ambao kwanza ni wao kuliko wa wengine.

Pia watoto, kama viungo hai vya familia, wanachangia kwa upande wao kuwatakatifuza wazazi. Maana watawarudishia wazazi upendo uliojaa shukrani na heshima, na watawaamini; watakuwa karibu nao, kama ifaavyo kwa watoto, katika taabu na upweke wa uzeeni. Na ujane, ukipokelewa kwa moyo thabiti kama mwendelezo wa wito wa ndoa, utaheshimiwa na wote[113]. Familia moja itaishirikisha kwa ukarimu familia nyingine utajiri wake wa kiroho. Kwa hiyo familia ya kikristo inatokana na ndoa, ambayo ni mfano na ushirikisho wa agano la upendo kati ya Kristo na Kanisa[114]; nayo, kwa njia ya upendo, ya kuzaa wazao bila ubahili, ya umoja, uaminifu wa wanandoa, na hatimaye kwa ushirikiano wenye upendo wa wanafamilia wake, itawadhihirishia wote uwepo hai wa Mwokozi wa ulimwengu hapa duniani na maumbile halisi ya Kanisa.

 
Upendo ya kindoa

49. Wachumba hualikwa mara nyingi na Neno la Mungu kuulisha na kuuimarisha uchumba wao kwa upendo safi; na pia wafunga ndoa hualikwa kuulisha na kuuimarisha muungano wa ndoa kwa upendo usiotengeka[115]. Hata watu wengi wa nyakati zetu wanathamini sana upendo wa kweli kati ya mume na mke unaojidhihirisha kwa namna mbalimbali kwa mujibu wa desturi zilizo nyofu za mataifa na nyakati mbalimbali. Upendo wa ndoa ni tendo halisi la kiutu, kwa maana ni hisia kati ya mtu na mtu itokanayo na utashi [wao] na inayouhusu wema wa mtu mzima. Kwa sababu hiyo, upendo huo unaweza kuzitajirisha hisia za rohoni na matendo yake ya kimwili kwa heshima ya pekee; na pia yaweza kuzitukuza [hisia na matendo hayo] kama ishara na alama mahsusi za urafiki wa kindoa. [Mungu] Bwana alipenda kuponya, kukamilisha na kukuza upendo huu kwa kipawa maalum cha neema na ukarimu. Upendo wa namna hii, unaounganisha pamoja tunu za kibinadamu na za kimungu, huwaongoza wanandoa kujitoa kwa hiari kila mmoja kwa mwenzie; kadhalika, unathibitishwa na hisia na vitendo vya upendo mtamu (tenero affecto) na kupenya vipengele vyote vya maisha ya wanandoa[116]. Zaidi, upendo wa ndoa unatimilika na kukua kwa njia ya utekelezaji wake; na kwa sababu hiyo ni jambo kubwa kuliko mvutio mtupu wa kimwili (eroticam inclinationem) ambao, ukilishwa kwa tamaa ya kibinafsi, utafifia vibaya na mapema.

Upendo huo huonyeshwa na kutimilika kwa namna ya pekee kwa matendo yaliyo maalum ya ndoa; kwa hiyo yale matendo ambayo kwayo wanandoa wanaungana kati yao kwa undani na usafi, ni mazuri na ya kuheshimiwa. Nayo, yakifanyika kwa namna inayoustahili utu wa binadamu, yanachochea kile yanachokiashiria, yaani kujitoa kila mmoja kwa mwenzie, na yanawatajirisha mume na mke katika furaha na shukrani. Upendo huo unathibitishwa na ahadi [ya uaminifu ya kila mmoja] na hasa unaidhinishwa na sakramenti ya Kristo; hivyo unadumu mwaminifu wala hauwezi kuvunjika katika raha na taabu, kwa upande wa mwili na wa roho. [Ndiposa] upendo wa ndoa haukubali kabisa uzinzi na talaka. Tena umoja wa ndoa, uliothibitishwa na Bwana, unaonekana kinaganaga katika hadhi iliyo sawa ya mume na mke, ambayo ni lazima itambulikane katika upendo mkamilifu na wa kila mmoja kwa mwenzake. Lakini fadhila ya pekee inadaiwa ili kuzitekeleza kwa uaminifu wajibu za wito huu wa kikristo. Ndiyo maana wafunga ndoa, wakiimarishwa na neema [ya Mungu] kwa ajili ya maisha matakatifu, watauhamasisha bila kukoma uthabiti wa upendo, saburi na roho ya sadaka. Nao watauomba upendo huo kwa njia ya sala.
 
Upendo halisi wa ndoa utaheshimiwa zaidi, na watu watafundishwa vema, ikiwa wanandoa wakristo wanatoa ushuhuda wa uaminifu na wa uelewano katika upendo, pamoja na ari katika kuwalea watoto. Tena ikiwa wanashika nafasi yao katika matengenezo ya lazima ya kitamaduni, kisaikolojia na kijamii kwa manufaa ya ndoa na familia. Pia vijana lazima wafundishwe ifaavyo na mapema, hasa ndani ya familia yao, kuhusu heshima ya upendo wa ndoa, kama vile juu ya dhima yake na kujitokeza kwake. Na hivyo wapate kufundishwa kuuheshimu usafi wa moyo, na hatimaye kuushikilia uchumba ulio mnyofu na baadaye kufunga ndoa.
 
Uzazi katika ndoa
 
50. Ndoa na upendo wake kwa maumbile yake inakusudia kuwazaa na kuwalea watoto. Maana watoto ni zawadi bora ya ndoa, nao wanachangia sana kwa ajili ya mema ya wazazi wenyewe. Mungu mwenyewe ndiye aliyesema: “Si vema mtu huyu awe peke yake” (Mwa 2:18); naye “alimwumba mtu mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke” (Mt 19:4), na alitaka kumshirikisha mtu kwa namna ya pekee katika kazi yake ya kuumba. Pia aliwabariki mwanamume na mwanamke akiwaambia: “Zaeni, mkaongezeke” (Mwa 1:28). Bila ya kupuuza malengo mengine ya ndoa, matendo stahivu ( cultus) ya upendo wa kindoa, pamoja na muundo wote wa maisha ya kifamilia unaotokana nao, unalenga kuwafanya mume na mke wakubali kwa moyo thabiti kushiriki upendo wa Muumba na Mwokozi ambaye kwa njia yao anaongeza siku kwa siku familia yake na kuitajirisha.

Wanandoa wanajua kuwa ni washiriki wa upendo wa Mungu Muumba na wafasiri wake kwa njia ya wajibu wa kuuendeleza uhai wa binadamu na kuulea; nao hauna budi kutazamwa kama utume wao maalumu. Kwa hiyo watatekeleza kazi yao kwa uwajibikaji wa kiutu na wa kikristo. Tena, kwa upole na heshima kwa Mungu watajitengenezea fikra zilizo nyofu kwa njia ya kutafakari na kujibidisha, wakiyazingatia manufaa yao wenyewe na ya watoto wao, wale waliokwisha zaliwa kama vile wanaotarajiwa kuzaliwa. Wataipima hali ya maisha ya nyakati zao na ya wao wenyewe kwa upande wa kimwili na wa kiroho. Na hatimaye watautunza utaratibu ulio bora wa manufaa ya familia, ya jamii, na ya Kanisa. Ni wanandoa wenyewe wanaopaswa kuzifikia fikra hizo mbele ya Mungu. Lakini katika tabia yao wanandoa wakristo ni lazima waelewe kuwa hawawezi kuenenda kadiri ya hiari yao, bali lazima waongozwe na dhamiri iliyo nyofu na inayopaswa kujilinganisha na sheria ya Mungu mwenyewe. Kisha waitii Majisterio ya Kanisa ambayo inafasiri kiukweli sheria ile katika mwanga wa Injili. Sheria hiyo ya kimungu huionyesha maana kamili ya upendo wa ndoa, huulinda na kuusukuma mbele kuelekea ukamilifu wake wa kiutu. Hivyo wanandoa wakristo, wakiyategemea Maongozi ya kimungu na kuilisha roho ya sadaka (spiritum sacrificii)[117], wanamtukuza Muumba na wanajielekeza kwenye ukamilifu wa Kristo pale wanapotekeleza jukumu lao la kuzaa kwa moyo radhi na kwa uwajibikaji wa kiutu na wa kikristo. Miongoni mwa wanandoa wanaotekeleza wajibu waliokabidhiwa na Mungu, lazima watajwe wale ambao, kwa uamuzi wenye utaratibu na wa pamoja, wanapokea kwa moyo mkuu hata idadi kubwa zaidi ya watoto wanaodai kulelewa ipasavyo[118].

Hata hivyo, ndoa haikuwekwa kwa ajili ya kuwazaa watoto tu; lakini maumbile [yake] yenyewe ya kuwa agano lisilotengeka kati ya watu wawili na pia manufaa ya watoto vinadai kuwa upendo kati ya wanandoa uambatane na ishara zake zenye utaratibu mzuri, yakue na kufikia ukomavu. Kwa hiyo ingawa pengine watoto, ambao mara nyingi hutamaniwa sana, hawapatikani, hata hivyo ndoa hudumu kama mazoea na ushirika ( consuetudo et communio) wa maisha yote; kisha huhifadhi thamani yake na hali yake ya kutotengeka.
 
Kupatana kwa upendo wa ndoa na heshima ya uhai wa binadamu
 
51. Mtaguso unajua kuwa mara nyingi wanandoa wanapopanga ipasavyo maisha ya ndoa, wanazuiliwa na hali mbalimbali za maisha ya kisasa. Tena wanaweza kupambana na mazingira ambapo haiwezekani kuongeza idadi ya watoto, walau kwa muda fulani; wala si rahisi kutunza uaminifu wa upendo na hali kamili ya kifamilia katika maisha yao. Maana, pale ambapo mwandani wa ndoa ( intima vita conigalis) unakatishwa, mara nyingi uaminifu huhatarishwa, na manufaa ya watoto huathirika; na hapo ndipo malezi ya watoto hutiwa mashakani, pamoja na ule ujasiri wa kukubali kupata watoto wengine.
 
Wapo wengine wanaodai kuyatatua matatizo hayo kwa namna zisizo halali, na pengine hawakatai hata uuaji. Basi Kanisa linakumbusha kwamba sheria za kimungu za kuendeleza uhai na wajibu wa kuhamasisha upendo halisi wa kindoa haviwezi kupingana.

Maana Mungu aliye Bwana wa uhai amewakabidhi wanadamu utume mkuu wa kuulinda uhai; na utume huo, hauna budi kutekelezwa kwa namna za kiutu. Kwa hiyo uhai, ukishatungwa, lazima uhifadhiwe kwa juhudi kubwa; kwa hiyo kuharibu mimba na kuwaua watoto ni mauaji ya kuchukiza kabisa. Maumbile ya kijinsia katika binadamu na uwezo wake wa kuzaa unayashinda kwa namna ya ajabu yale yanayotokea katika viumbe vingine vilivyo chini yake. Kwa hiyo matendo yenyewe halisi ya maisha ya ndoa yameratibiwa kadiri ya hadhi ya binadamu, nayo ni lazima yastahiwe kwa heshima kubwa. Kwa hiyo, katika suala la kupatanisha upendo wa ndoa na wajibu wa kutoa uhai, maadili ya mwenendo [wa wanandoa] hayategemei tu nia yao nyofu wala tathmini ya madhumuni peke yake; bali [tabia hii] lazima iainishwe na vigezo halisi, vigezo ambavyo vina misingi yake katika maumbile ya mtu na ya matendo yake; vigezo vinavyoheshimu maana kamili ya kujitoa mmoja kwa mwingine na ya uzazi wa binadamu katika maana ya upendo wa kweli. Na hayo yote hayatawezekana ikiwa fadhila ya usafi wa moyo wa kindoa haitalishwa kwa unyofu wa moyo. Watoto wa Kanisa, wakiasisiwa katika miongozo hii, hawawezi kushika njia za kuudhibiti uzazi zinazolaumiwa na Majisterio[119], iliyo na wajibu wa kufafanua sheria ya kimungu.

Iwe wazi kwa wote kwamba uhai wa binadamu na jukumu la kuuendeleza uhai huo havifungwi katika mipaka ya maisha ya hapa duniani, wala haviwezi kupimwa na kueleweka katika ulimwengu huu tu, bali vinahusu daima kikomo cha milele cha wanadamu.
 
Ustawi wa ndoa na familia ushughulikiwe na wote

52. Familia ni shule ya kujitajirisha kibinadamu. Lakini, ili familia iweze kuchota utimilifu wa maisha yake na wa wajibu wake ni lazima wanandoa wawe na moyo ulio wazi na wenye upendo wa kila mmoja kwa mwenzake. Tena, inawapasa kuwa na ushirika wa fikra na wa pamoja kati ya mume na mke, na ushirikiano thabiti kama wazazi katika malezi ya watoto. Uwepo wa baba mwenye kuishughulikia familia yake unanufaisha sana malezi yao; lakini pia ni muhimu ziwepo bidii za mama naye katika nyumba yake; hasa kuwashughulikia watoto walio wadogo zaidi, bila kusahau maendeleo ya kijamii ya mwanamke. Aidha watoto, kwa njia ya malezi, wajengwe kitabia kwa namna ambayo itawawezesha kuufikia ukomavu wao na kuufuata wito wao kwa uwajibikaji kamili, hata ikiwa wito wa kidini. Na hatimaye waweze kuchagua hali ya maisha yao; kama watachagua hali ya maisha ya ndoa, wapate kuunda familia yao katika hali ya kimaadili, ya kijamii na ya kiuchumi inayowafaa kweli. Aidha ni wajibu wa wazazi au walezi kuwaongoza walio vijana zaidi katika kuiunda familia yao mpya kwa ushauri nasaha unaoelezwa kwa namna inayowapendeza. Nao walezi waepukane hasa na tabia yenye kuwashurutisha, kwa mitindo mbalimbali ya ukandamizaji, kushika hali fulani ya maisha au pengine kumchagua mtu fulani kama mwenzake wa ndoa.

Familia ni mahali ambapo vizazi vilivyo tofauti vinakutana na kusaidiana kati yao kuifikia busara ya kibinadamu iliyo kamili zaidi, na kuunganisha pamoja haki za mtu binafsi na madai mengine ya maisha ya kijamii. Hivyo familia ndio msingi wa jamii. Kwa hiyo, wale wote wenye uwezo wa kuathiri jamii na makundi yake mbalimbali ni lazima wasaidie kimatendo kwa ajili ya usitawi wa ndoa na familia. Serikali za nchi zinapaswa kutazama kama wajibu mkuu kuheshimu, kulinda na kusitawisha maumbile halisi [ya ndoa na familia] pamoja na maadili ya wote na usitawi wa maisha ya nyumbani. Kwa namna ya pekee haki ya wazazi ya kuzaa watoto na kuwalea ndani ya familia haitakuwa na budi kutetewa. Lakini sheria zenye kufaa na mipango mbalimbali vitapaswa kuwalinda na kuwasaidia ifaavyo wale ambao bahati mbaya hawana familia yao wenyewe.
 
Wakristo, wakiukomboa wakati wa sasa [120] na kupambanua mambo yadumuyo na yale yapitayo, watajibidisha ili kuyasitawisha kwa makini mema ya familia; [na watafuatilia lengo hilo] kwa ushuhuda wa maisha yao na pia kwa kushirikiana kwa moyo na watu [wote] wenye mapenzi mema. Na hivyo watayashinda matatizo yaliyopo na watayakidhi mahitaji na manufaa ya familia yanayojitokeza katika nyakati mpya. Kwa lengo hilo hisia za kikristo za waamini, dhamiri nyofu za kimaadili za wanadamu pamoja na hekima na umahiri wa wale wanaohusika katika elimu ya dini utaleta mchango mkubwa.

Wataalamu wa sayansi, hasa za kibayolojia, kiuganga, kijamii na kisaikolojia, huweza kunufaisha sana ndoa na familia na pia amani ya dhamiri kama watauunganisha utafiti wao na pia kama watajitahidi kubainisha kwa undani zaidi hali mbalimbali zinazousaidia uzazi wenye utaratibu na ulio mnyofu.

Ni wajibu wa mapadre kujipatia elimu iliyo ya lazima mintarafu masuala ya maisha ya kifamilia, na kuusaidia kwa upendo wito wa wanandoa katika maisha yao ya kindoa na ya kifamilia. Kwa kusudi hilo watatumia mbinu mbalimbali za kichungaji: kuhubiri Neno la Mungu, ibada za kiliturujia na misaada mingine ya kiroho. Tena watawasaidia kwa utu na saburi katika matatizo yao, na kuwaimarisha katika mapendo ili ziundwe familia zinazong’aa kwelikweli.
 
Taasisi mbalimbali za kitume, hasa zile zinazoshirikisha familia, zijibidishe kuwategemeza kwa mafundisho na matendo vijana na wanandoa wenyewe, hasa familia mpya; tena zifanye juhudi kuwalea kwa maisha ya kifamilia, ya kijamii na ya kitume.

Kisha, wanandoa wenyewe, walioumbwa kwa sura ya Mungu aliye hai na waliowekwa katika hadhi halisi ya kila mtu, waunganishwe kwa upendo ulio sawa wa kila mmoja kwa mwenzie, na nia moja na hatimaye utakatifu wa pamoja[121]. Na hivyo watamfuata Kristo aliye asili ya uzima[122] katika furaha na majitoleo (gaudis et sacrificiis) ya wito wao. Na kwa njia ya upendo wao mwaminifu wapate kuwa mashahidi wa lile fumbo la pendo ambalo Bwana amelifunua kwa ulimwengu, kwa njia ya kifo na ufufuko wake[123].

Sura ya Pili

KUSTAWISHA MAENDELEO YA UTAMADUNI

Utangulizi
 
53. Ni sifa maalum ya binadamu kuweza kukifikia kiwango cha maisha kinacholingana kweli na kikamilifu na hali ya kiutu kwa njia ya utamaduni tu, yaani kwa kustawisha hazina na tunu za maumbile. Kwa hiyo, kila kunapokuwa na suala liyahusuyo maisha ya kibinadamu, maumbile na utamaduni huungana kiundani.

Kwa ujumla neno “utamaduni” lataka kumaanisha mambo yale yote ambayo kwayo binadamu huboresha na kuvitokeza vipawa vyake vingi vya kimwili na kiroho. Tena kwa njia yake binadamu hujibidisha kuutawala ulimwengu wenyewe kwa ujuzi na kazi [yake]. Kadhalika, huyafanya maisha ya kijamii yawe ya kiutu zaidi, katika familia na pia katika jamii nzima, kwa njia ya maendeleo ya desturi na ya taasisi mbalimbali. Kisha, katika mfuatano wa majira, hutokeza, hushirikisha na kuhifadhi katika matendo yake mang’amuzi na matarajio makuu ya kiroho ili yaweze kuyasaidia maendeleo ya walio wengi au, zaidi, ya wanadamu wote.

Kwa sababu hiyo hutokea kwamba utamaduni ni lazima uwe na mandhari mbili, yaani ya kihistoria na ya kijamii; na neno “utamaduni” linachukua mara nyingi maana inayohusu elimujamii (sosiolojia) na sayansi ya makabila (ethnolojia). Kwa maana hiyo, ndipo inapoongelewa juu ya wingi wa tamaduni mbalimbali. Hivyo, hali tofauti za maisha ya kawaida na mitindo mbalimbali ya kuyaratibisha mema yake vina asili yake katika namna tofauti za kutumia vitu, kufanya kazi, kujieleza, kufuata dini, kuunda desturi, kutunga sheria na kuzishughulikia, kuendeleza sayansi na sanaa na kuustawisha uzuri. Kwa hiyo, desturi za kimapokeo zinaunda urithi mahsusi wa kila jumuiya ya kibinadamu. Kadhalika, yanatengenezwa mazingira maalum ya kihistoria ambamo wanadamu wa kila taifa na wakati wanaingia, na ambamo kutoka humo huchota yale mema yanayomwezesha kukuza ustaarabu.

Ibara ya kwanza

HALI YA UTAMADUNI KATIKA ULIMWENGU WA SASA

 
Mitindo mipya ya maisha

54. Hali za maisha ya siku hizi zimebadilika sana katika nyanja za kijamii na kiutamaduni, hivi kwamba ni halali kuuita wakati huu kuwa ni kipindi kipya cha historia ya kibinadamu[124]. Na tokea hapo zinafunguliwa njia mpya za kuboresha na kushamirisha zaidi utamaduni. Nazo zimeandaliwa kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi ya kimaumbile, ya watu, na ya kijamii; na pia kutokana na maendeleo ya kitekniki na ya uvumbuzi na uratibishaji wa mfumo wa vyombo vya upashanaji habari. Kwa hiyo, tabia ya utamaduni wa siku hizi ina mengine ya pekee kama haya yafuatayo: sayansi ziitwazo kamili zinakuza sana uwezo wa kupambanua mambo (iudicium criticum); utafiti wa kisaikolojia wa siku hizi unaeleza kwa undani zaidi utendaji wa kibinadamu; sayansi za kihistoria zinafaa sana ili kutathmini mambo katika mtazamo wa mageuzo na maendeleo yao; mitindo ya maisha na desturi zinazidi kulingana kati yao. Mfumo wa viwanda (industrializatio), kupanuka kwa uhamiaji mjini (urbanizatio), na mambo mengine yanayohamasisha maisha ya pamoja kijamii (vitam communitariam) yanaleta mitindo mipya ya utamaduni (unaolingana kwa wote = mass-culture). Tangu hapo zinazaliwa namna mpya za kufikiri, za kutenda, na za kutumia muda wa mapumziko; kukua kwa mawasiliano kati ya mataifa mbalimbali na kati ya matabaka ya kijamii kunawafungulia wote, na kwa kila mmoja, hazina za aina mbalimbali za utamaduni. Na hivyo, polepole unaundwa mtindo wa utamaduni ambao ni wa kiulimwengu zaidi (universalior); nao utahamasisha na kuonyesha umoja kati ya wanadamu kwa kadiri ileile ambavyo unavyouheshimu upekee wa tamaduni mbalimbali.

Binadamu mtendaji wa utamaduni

55. Katika kila taifa na tabaka ya kijamii inazidi idadi ya wanaume na wanawake wanaotambua kuwa ni watengenezaji na watendaji wa utamaduni wa jumuiya zao. Ulimwenguni kote hisia za kujitegemea na za uwajibikaji zinazidi kukua; na jambo hilo ni la muhimu sana kwa ukomavu wa kiroho na kimaadili wa wanadamu. Nalo linajitokeza kinaganaga zaidi tukiuzingatia muungano wa ulimwengu mzima, pamoja na wajibu unaotulazimu kuijenga dunia iliyo nzuri zaidi katika ukweli na haki. Hivyo sisi tunashuhudia kuzaliwa kwa ubinadamu, au humanismi (humanismus), mpya unaomfanya mtu ajitambulishe kwanza kwa uwajibikaji wake mbele ya wenzake na mbele ya historia.

Matatizo na wajibu
 
56. Katika hali ya namna hii haishangazi ikiwa binadamu, anayejisikia mwenye wajibu katika maendeleo ya utamaduni, huwa na matumaini makubwa zaidi, lakini vilevile anatazama kwa fadhaa migongano iliyomo na ambayo anapaswa kuitatua.  
 
Je, yapaswa kufanya nini ili ongezeko la mahusiano ya kiutamaduni lisichafue maisha ya kijamii, wala lisivunje busara ya mababu na kuhatarisha tabia maalum ya kila taifa? Maana mahusiano hayo yangepaswa kuleta mjadala wenye kuzaa matunda kati ya matabaka na mataifa mbalimbali.
 
Je, ni kwa vipi kasi na kupanuka kwa utamaduni mpya vitaweza kuhamasishwa bila ya kupoteza uaminifu hai kwa urithi wa mapokeo? Suala hilo linahitaji utatuzi wa haraka hasa pale ambapo utamaduni unaotokana na maendeleo makubwa ya kisayansi na kiteknolojia lazima ulinganishwe na ile heshima ya akili ambayo, kadiri ya mapokeo mbalimbali, inalishwa na elimusanaa ( studiis classicis).

Fani mbalimbali za sayansi zinaendelea kuongezeka na kutawanyika haraka. Je, kwa njia ipi mtawanyiko wa fani hizi unaweza kupatanishwa na haja ya kuzirudisha [hizo fani] katika hali ya usanisi, na haja ya kutunza katika binadamu uwezo wake wa kutafakari na kushangaa unaomwongoza katika kuifikia hekima?

Je, inabidi kufanya nini ili wanadamu wa dunia nzima washirikishwe katika mema ya utamaduni, wakati ambapo utamaduni wa mabingwa unazidi kuwa wa ndani na changamano?
 
Kisha je, yatupasa kufanya nini ili kutambua uhalali wa utamaduni wa kujiratibisha – na ndivyo unavyodai – bila kunaswa na humanismi inayozingatia mambo ya dunia tu, au pengine unaopinga wazi dini yenyewe?

Hata katika hoja hizo zipinganazo kati yao, siku za leo utamaduni wa kibinadamu hauna budi kujiendeleza hivi kwamba uweze kustawisha utu wa binadamu katika uzima wake na kwa utaratibu ufaao. Aidha kwamba uweze kuwasaidia watu kuyatekeleza majukumu yao ambayo wote, lakini hasa wakristo, waliounganika kidugu katika familia moja ya kibinadamu, wanaitwa kuyatimiliza.

Ibara ya pili

KANUNI KADHAA ZIONGOZAZO USTAWISHAJI UFAAO WA UTAMADUNI

 
Imani na utamaduni
 
57. Wakristo, wanaosafiri kuuelekea mji wa mbinguni, hupaswa kuyatafuta na kuyaonja mambo yaliyo juu [125]. Hata hivyo, jambo hili halipunguzi, bali linakazia umuhimu wa wajibu wao wa kushirikiana na watu wote, ili kuujenga ulimwengu ulio wa kiutu zaidi. Na ni yakini kwamba fumbo la imani ya kikristo linawapatia vihimizo na misaada bora ili kutekeleza wajibu huo kwa juhudi kubwa zaidi. Tena linawahimiza na kuwasaidia hasa kutambua maana kamili ya kazi hiyo, ambayo kwayo utamaduni wa kibinadamu utaweza kushika nafasi ya pekee katika wito mzima wa binadamu.

Maana binadamu analima ardhi kwa kazi ya mikono yake au kwa msaada wa teknolojia ili itoe mazao na ipate kuwa maskani inayoistahili familia ya dunia nzima. Tena, binadamu anashiriki kwa uwajibikaji maisha ya makundi mbalimbali ya kijamii. Basi, wakati huohuo anatimiza mpango wa Mungu, uliodhihirishwa tangu mwanzo wa nyakati, wa kuitawala dunia[126] na kuukamilisha uhulushi; na hatimaye kujisitawisha yeye mwenyewe. Aidha, anaishika amri kuu ya Kristo ya kujitoa mhanga kwa utumishi wa ndugu zake.

Licha ya hayo binadamu anajishughulisha na fani mbalimbali za taaluma kama vile falsafa, historia, hisabati, sayansi ya kimaumbile na sanaa. Na hivyo huweza kuchangia kwa vikubwa katika kukuza familia ya wanadamu ili izifikie fikra zilizo bora zaidi mintarafu ukweli, wema na uzuri; tena kusudi iufikie mtazamo wa thamani za mambo ulio sawa kwa ulimwengu mzima (iudicium universi valoris). Kwa njia hii familia ya wanadamu itaangazwa wazi zaidi na ile Hekima ya ajabu iliyokuwa pamoja na Mungu tangu milele, ikipanga vitu vyote pamoja naye, ikifurahia nchi yote iliyokaliwa, na furaha yake ikiwa ni kukaa pamoja na wanadamu[127].

Kwa sababu hiyo roho ya kibinadamu ikiwa huru zaidi mbali na utu-mwa wa mambo ya kidunia inaweza kujiinua upesi zaidi kumwabudu na kumtazama Mungu Muumba. Na zaidi, ikisukumwa na neema ya Mungu, hujiweka tayari kumtambua Neno wa Mungu ambaye, kabla ya kutwaa mwili ili kuvikomboa na kuvijumlisha vyote ndani yake, tayari alikuwepo ulimwenguni kama “nuru halisi inayomwangaza kila mtu” (Yn 1:9) [128].
 
Bila shaka, maendeleo ya nyakati zetu ya sayansi na teknolojia hayawezi kufumbua sababu za ndani za mambo kwa njia ya mbinu zake; na hivyo yanaweza kusababisha kustawi kwa namna fulani ya ufenomeni na uagnostiki ( phenomenismo et agnosticismo) pale ambapo mbinu za utafiti zinazotumika katika fikra hizi zinakuzwa bila haki kuwa kanuni kuu kupita zote katika harakati za kuutafuta ukweli wote. Zaidi, kuna hatari ya kwamba binadamu, akiutegemea mno ugunduzi wa siku za leo, huanza kudhani kuwa anajitosheleza na wala hayatafuti tena mambo ya juu.

Lakini mambo hayo ya kulaumiwa si lazima yatokane na utamaduni wa kisasa tu, wala yasitutie katika kishawishi cha kukana tunu zake zilizo nzuri. Miongoni mwa tunu hizo hutajwa hizi zifuatazo: taaluma ya kisayansi na uaminifu wa utafiti wake kwa ajili ya ukweli; ulazima wa kushirikiana na makundi mengine ya mafundi stadi; hisia ya mshikamano wa kimataifa; kustawi kwa utambuzi wa uwajibikaji wa mafundi katika kuwasaidia na kuwalinda wanadamu [wenzao]; moyo wa kuboresha zaidi hali za maisha ya wote, hasa ya wale wanaoteswa kwa kunyimwa uwajibikaji wao ama kwa uduni wa utamaduni. Mambo hayo yote kwa namna fulani yanaweza kuwa kama maandalizi ya kuipokea habari ya Injili. Na maandalizi hayo yaweza kukolezwa na Yule aliyekuja kuukomboa ulimwengu.

Mahusiano ya namna nyingi kati ya Habari Njema ya Kristo na utamaduni
 
58. Kuna mahusiano ya namna nyingi kati ya ujumbe wa wokovu na utamaduni wa kibinadamu. Maana, Mungu alipojidhihirisha kwa taifa lake, mpaka utimilifu wa ufunuo wake katika Mwanae aliyefanyika mwili, alinena kadiri ya utamaduni halisi wa kila kipindi cha historia.  
 
Kadhalika Kanisa, ambalo limeishi katika mfululizo wa karne nyingi katika hali mbalimbali, limetumia tamaduni tofauti ili kueneza na kufafanua ujumbe wa Kristo katika mahubiri yake kwa watu wote. Tena [limetumia tamaduni mbalimbali] katika kuuchunguza na kuuelewa [ujumbe huo] ili kuuonyesha vizuri zaidi katika maisha ya kiliturujia na katika mitindo mingi ya maisha ya jumuiya ya waamini  
 
Lakini wakati huohuo Kanisa, likitumwa kwa mataifa yote ya nyakati zote na ya mahali pote, halifungamani katu na kabila au taifa moja tu, wala halifungamani na mtindo mmoja tu maalum wa maisha, wala halifungamani na desturi ya pekee, iwe ya zamani au mpya. Bali Kanisa ni aminifu kwa mapokeo yake, na vilevile linauzingatia utume wake wa kiulimwengu; nalo linaweza kushiriki katika aina za utamaduni zilizo mbalimbali. Aidha, ushirika huu unalitajirisha Kanisa lenyewe na, vilevile hizo tamaduni mbalimbali.

Habari njema ya Kristo yafanya upya daima maisha na utamaduni wa binadamu aliyeanguka, na inapinga na kuondosha makosa na mabaya yatokanayo na mvuto wa dhambi ambao daima huhatarisha maisha ya watu. Tena inayatakasa na kuyainua maadili ya mataifa bila kukoma; kwa utajiri utokao juu inazirutubisha kwa undani, inaimarisha, inakamilisha na kuzifanya upya katika Kristo sifa za kiroho na vipawa vya kila taifa[129]. Kwa njia hii Kanisa linatekeleza utume wake[130], na papo hapo linahamasisha na kutoa mchango wake kwa utamaduni wa kibinadamu na wa kijamii; na hatimaye, kwa utendaji wake, hata wa kiliturujia, linamlea binadamu katika uhuru wa ndani.

Kuoanisha mitindo mbalimbali ya utamaduni

59. Kwa sababu zilizotolewa hapo juu, Kanisa linawakumbusha wote kuwa utamaduni lazima ulenge katika ukamilifu wa mtu mzima na pia katika manufaa ya jamii na ya wanadamu wote. Kwa hiyo ni lazima kuistawisha roho [ya binadamu] ili kwamba uwezo wake wa kushangaa, wa utambuzi wa ndani na wa taamuli upate kukuzwa; naye ajipatie pia uwezo wa kupambanua mambo, kulisha utambuzi wake wa kidini, kimaadili na kijamii.

Maana utamaduni, ukitokana na tabia ya kirazini na ya kijamii ( indole rationali et sociali) ya binadamu, unahitaji daima uhuru ule ulio wa haki ili usitawi, na pia unatakiwa kutambuliwa una uhalali wa kujiratibisha kadiri ya kanuni zake wenyewe. Kwa haki basi utamaduni hudai heshima na ustahilivu wa kuhifadhiwa, ila zitunzwe haki za kiutu na za kijamii za kila mahali na za ulimwengu mzima, ndani ya mipaka ya manufaa ya wote.
 
Mtaguso Mkuu unayakumbusha yale yaliyofundishwa katika Mtaguso wa Vatikano I na kuthibitisha kwamba “kuna taratibu mbili tofauti za ujuzi”, zisizochangamana, yaani ya imani na ya akili. Na Kanisa halipigi marufuku kwamba “sanaa za kibinadamu na sayansi zitumie kanuni na mbinu zake kila moja katika uwanja wake”; kwa hiyo [Kanisa], “likiutambua uhuru huo wa haki” linauthibitisha uwezo ulio halali wa utamaduni, na hasa wa sayansi, wa kujiratibisha [131].
 
Hayo yote yanadai kwamba pia binadamu, akiheshimu utaratibu wa maadili na manufaa ya wote, huweza kuuchunguza ukweli kwa uhuru, kujulisha na kueneza maoni yake na kujishughulisha na sanaa yoyote ile; na hatimaye mambo hayo yanadai binadamu ataarifiwe vilivyo kadiri ya ukweli wa matukio yauhusuyo umma [132].

Sio wajibu wa serikali kuunda sura maalum ya mitindo mbalimbali ya utamaduni, bali kushughulika ili mazingira na misaada inayoweza kuhamasisha maisha ya kiutamaduni ya watu wote na ya kila kundi japo dogo katika taifa ipatikane[133]. Kwa hiyo, ni lazima kwanza kutilia mkazo kuwa utamaduni usipotoshwe katika kulifuata lengo lake na usilazimishwe kuvitumikia vyombo vya siasa na vya uchumi.

Ibara ya Tatu

BAADHI YA NYAJIBU MUHIMU ZA WAKRISTO KUHUSU UTAMADUNI

Kutambua haki ya kila mtu kuhusu elimu na utamaduni, na utekelezaji wake
 
60. Nyakati zetu upo uwezekano wa kuwaokoa watu wengi sana katika hali duni itokanayo na ujinga. Nao ndio wajibu mkubwa katika siku za leo, hasa kwa wakristo; yaani kufanya kazi bila kuchoka, ili haki za msingi kwa watu wote kuhusu utamaduni wa kibinadamu na wa kijamii zitambuliwe na kutekelezwa popote, katika nyanja za uchumi na siasa, katika kila taifa na kati ya mataifa. Na hatimaye haki hizo zilingane na hadhi ya kiutu, pasipo ubaguzi wa kikabila, wa kijinsia, kitaifa, kidini au wa kijamii. Kwa hiyo inatakiwa kuwapatia watu wote mafaa ya kiutamaduni mengi ya kutosha, hasa yale yanayounda utamaduni uitwao wa msingi; hivyo watu wengi sana wasizuiliwe kutoa mchango wao wa kiutu kwa manufaa ya wote, kutokana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika au kwa sababu ya kunyimwa utendaji mwajibifu.
 
Kwa hiyo, inabidi kufanya kila juhudi ili wote wenye uwezo wapate kuingia katika masomo ya juu. Nao, kwa njia hii na kwa kadiri iwezekanavyo, wataweza kushughulikia katika jamii ya kibinadamu na majukumu, wajibu na huduma zilinganazo na maelekeo yao ya kimaumbile pamoja na ufundi walioupata [134]. Kwa hiyo, kila mtu na makundi ya kijamii ya kila taifa, wataweza kuyafikia maendeleo kamili ya maisha yao ya kitamaduni kwa mujibu wa vipawa vyao na mapokeo yao maalum.

Aidha, lazima kutumia kila jitihada ili kuwafanya watu wote waelewe haki yao kuhusu elimu na pia wajibu wao wa kujiendeleza na kuwasaidia wengine. Pengine zipo hali za maisha na za kazi zinazowazuia wanadamu katika bidii yao ya kujielimisha na hivyo zinaua hamu ya elimu ndani yao. Hilo lawahusu hasa wakulima na wafanyakazi wa viwandani ambao inabidi wapatiwe hali ya kazi isiyozuia maendeleo yao ya kielimu na kitamaduni, bali inayoyahamasisha. Wanawake wameshaanza kufanya kazi katika fani zote za maisha; ingefaa sasa wapate uwezo wa kuzitekeleza kikamilifu wajibu zao kadiri ya maumbile yao ya pekee. Na itakuwa wajibu wa wote kufanya ushirikiano wa wanawake katika maisha ya kitamaduni, ulio maalum na wa lazima, utambuliwe na kuhamasishwa.

 
Kumwelimisha binadamu katika utamaduni mzima
 
61. Siku hizi ni vigumu zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma kuunganisha katika usanisi fani mbalimbali za sanaa na ujuzi. Maana wakati matawi ya utamaduni yanapopanuka na kutofautiana, ndipo wakati huohuo uwezo wa kila mtu wa kuyaelewa na kuyaunganisha pamoja unapungua, hivi kwamba picha ya “binadamu wa ujuzi wa fani zote” ( imago “hominis universalis”) inazidi kufifia. Lakini hata hivyo kila mtu anawajibika kushikilia dhana ya “binadamu katika utu wake mzima”, ambaye ndani yake zinajitokeza tunu za akili, utashi, dhamiri, na udugu. Nazo zina msingi wake katika Mungu Muumbaji na zimeponywa na kukuzwa kwa namna ya ajabu ndani yake Kristo.
 
Awali ya yote familia ndiye mama na mlishi wa elimu hii. Ndani yake watoto, wakiishi katika mazingira ya upendo, hujifunza kwa urahisi utaratibu mnyofu wa mambo; na papo hapo mitindo ya utamaduni iliyokwisha kuthibitishwa inapokelewa na roho ya kijana anayekua.
 
Kwa ajili ya elimu hiyohiyo, katika jamii za kisasa kuna nafasi nyingi zinazoweza kustawisha utamaduni wa kiulimwengu ( universali culturae). Na hizo nafasi hutokana hasa na ongezeko la usambazaji wa vitabu pamoja na vyombo vipya vya upashanaji habari vya kiutamaduni na kijamii. Kupunguzwa kwa masaa ya kazi karibu mahali pote kunazidisha siku kwa siku nafasi kwa watu wengi ya kujielimisha. Wakati wa mapumziko ( otio) utumike ipasavyo kwa kuiburudisha roho na kuiimarisha afya ya kiroho na ya kimwili kwa njia ya shughuli na masomo ya hiari; tena kwa safari za kitalii katika nchi nyingine, ambazo kwazo roho ya binadamu inakamilishwa, na watu wanajitajirisha kwa kufahamiana wao kwa wao. Aidha, afya ya kiroho na ya kimwili inaweza kuimarishwa kwa mazoezi na kwa mao-nyesho ya michezo, ambayo inasaidia kudumisha usawa wa kiroho ( equilibrium) pia katika jumuiya. Pamoja na hayo, huweza pia kutoa mchango wake katika kustawisha mahusiano ya kidugu kati ya wanadamu wa hali zote, na wa mataifa na makabila mbalimbali. Basi, wakristo washiriki mambo hayo ili maonyesho na matendo ya kiutamaduni ya umma ya nyakati zetu yakolezwe na roho ya kiutu na ya kikristo.

Lakini, misaada hiyo yote haiwezi kukamilisha malezi yote ya kiutamaduni ya binadamu kama wakati huohuo asipojihoji kiundani juu ya maana ya utamaduni na ya sayansi mintarafu utu wa binadamu.

Ulinganifu kati ya utamaduni wa kibinadamu na mafundisho ya kikristo
 
62. Kanisa limechangia kwa vikubwa katika maendeleo ya utamaduni; lakini mang’amuzi huonyesha kwamba, kutokana na sababu nasibu ( ex causis contingentibus), ulinganifu baina ya utamaduni na malezi ya kikristo pengine unatekelezwa kwa shida.
 
Matatizo haya si lazima yaidhuru imani; bali yanaweza kuihimiza roho kuielewa kwa makini na kwa undani zaidi imani yenyewe. Maana utafiti wa siku hizi na magunduzi mapya ya sayansi, ya historia na ya falsafa vinazusha masuala mapya yaletayo matokeo yake pia katika maisha ya kila siku; nayo yanadai utafiti mpya kwa upande wa wanateolojia. Aidha, wanateolojia wanaalikwa kuzitafuta daima namna za kufaa zaidi ili kuwaeleza wanadamu wa nyakati zao mafundisho ya kikristo; ila waheshimu mbinu na madai maalum ya sayansi ya kiteolojia. Maana kitu kimoja ni hazina au kweli za imani, na kitu kingine tofauti ni namna hizo [hazina au kweli] zinavyoelezwa; ijapo kiini na maana yake ya ndani ni vilevile tu [135]. Tena katika uangalizi wa kichungaji zijulikane na kutumiwa kwa namna maridhawa kanuni za teolojia na pia ugunduzi wa sayansi za kidunia. Na miongoni mwake yazingatiwe hasa mang’amuzi ya elimunafsi na elimujamii (saikolojia na sosiolojia), hivi kwamba hata waamini waongozwe kuyafikia maisha ya imani yaliyo safi na makomavu zaidi.
 
Pia fasihi na sanaa, kwa namna zake, ni muhimu sana kwa maisha ya Kanisa. Maana, zinafanya juhudi ili kuijua tabia mahsusi ya binadamu, pamoja na matatizo na mang’amuzi yake katika bidii anayoifanya ya kujifahamu na kujikamilisha mwenyewe na ulimwengu mzima. Tena [fasihi na sanaa] hujishughulisha kuitambua hali ya binadamu katika historia na katika ulimwengu, kufafanua unyonge na furaha [zake], na hatimaye kueleza mahitaji na uwezo wake, pamoja na kuidokeza hali ya kiutu iliyo nzuri zaidi. Na hivyo sanaa hizo huweza kuyainua maisha ya kibinadamu zinayoyaeleza kwa namna nyingi, kadiri ya mahali na nyakati.

Kwa hiyo, lazima bidii ifanyike ili wale wanaoshughulikia sanaa hizo wajisikie kuwa Kanisa linathamini kazi yao; nao, wakiwa na uhuru wenye utaratibu, waunde mahusiano rahisi zaidi na jumuiya ya kikristo. Tena Kanisa liitambue mielekeo mipya ya kisanaa ilinganayo na nyakati zetu na iliyo kadiri ya tabia ya mataifa na nchi mbalimbali. Nayo iingizwe pia katika majengo kwa ajili ya ibada (sanctuario), iwapo, kwa mtindo ufaao na kufuatia madai ya kiliturujia[136], inaziinua kwa Mungu roho [za waamini].

Basi, kwa njia hii habari juu ya Mungu zitadhihirishwa wazi zaidi, na mahubiri ya kiinjili yataeleweka kinaganaga zaidi katika akili za watu; nayo yataonekana yanafungamana kiundani na hali ya maisha yao.
 
Kwa sababu hiyo waamini washirikiane sana na wanadamu wa nyakati zao, na wajibidishe kupenya kikamilifu namna yao ya kufikiri na kuhisia, ambayo utamaduni ni kielelezo chake. Na tena [waamini] wapate kuoanisha maarifa ya sayansi mpya, ya mafundisho mapya na ya magunduzi ya hivi karibuni, na maadili na fikra za kikristo. Na hivyo maisha ya kidini na unyofu wa mwenendo viende, ndani yao [waamini], sambamba na elimu ya kisayansi na maendeleo ya mfululizo ya kiteknolojia, hivi kwamba waweze kupambanua na kufasiri mambo yote kwa hisia halisi za kikristo.

Wale wanaoshughulikia taaluma za kiteolojia katika seminari na vyuo vikuu wajitahidi kushirikiana na watu ambao ni mabingwa katika taaluma nyingine, wakiweka pamoja nguvu na kauli zao. Utafiti wa kiteolojia ujiendeleze katika ujuzi wa kina wa ukweli uliofunuliwa. Lakini usipuuze kukabiliana na nyakati zake, ili mabingwa katika fani mbalimbali za ujuzi waweze kusaidiana kuufikia ufahamu wa imani ulio kamili zaidi. Na ushirikiano huo utaunufaisha sana malezi ya wahudumu watakatifu kufasiri mafundisho ya Kanisa juu ya Mungu, binadamu, na ulimwengu kwa namna iwafaayo zaidi watu wa nyakati zetu. Na hapo wao watakuwa wepesi zaidi kuyapokea maneno yao[137]. Zaidi ya hayo Kanisa linatamani walei wengi wapate malezi yafaayo katika sayansi za kidini. Na wengi kati yao wajiendeleze katika taaluma hizo na wajipenyeze ndani yake kwa vyombo vya kisayansi vifaavyo. Lakini, ili waweze kutekeleza wajibu huo, waamini hawa, wawe wakleri ama walei, wapewe uhuru – kadiri ya haki – wa kutafiti, kufikiri, kuonyesha kwa unyenyekevu na ujasiri maoni yao katika tawi la ufundi wao[138].

Sura ya Tatu

MAISHA YA KIUCHUMI NA KIJAMII

Baadhi ya sifa za maisha ya kiuchumi ya siku hizi
 
63. Pia katika maisha ya kiuchumi kijamii hadhi na wito halisi vya binadamu lazima viheshimiwe na kusitawishwa, kama vile mafaa ya jamii nzima . Maana binadamu ni mtendaji, kiini na ukomo wa maisha ya kiuchumi kijamii.
 
Uchumi wa siku hizi, kadhalika kama fani nyingine zote za maisha ya kijamii, una mfumo ambao kwao binadamu anazidi kuitawala huluka. Tena raia, makundi na mataifa, yanazidi kuwasiliana na kutegemezana kati yao; kisha mamlaka ya serikali inazidi kujihusisha [na masuala ya umma]. Kwa upande mwingine maendeleo ya uzalishaji mali na ya mpango wa usambazaji wake pamoja na huduma mbalimbali, yamefanya uchumi uwe chombo cha kufaa kwa kuyakidhi vizuri zaidi mahitaji yaliyoongezeka ya familia ya wanadamu.
 
Hata hivyo, sababu za kuhangaika hazikosekani. Wanadamu wengi, hasa katika nchi zilizoendelea kiuchumi, wanaonekana kuwa wanatawaliwa na madai ya uchumi hivi kwamba karibu maisha yao yote ya kibinafsi na kijamii yanapenywa na mawazo ya kiuchumi. Nazo zinaenea pia katika nchi zenye uchumi wa kijamaa, pamoja na nchi nyingine. Tunaishi katika kipindi ambacho maendeleo ya maisha ya kiuchumi yangeweza kupunguza tofauti za kijamii kama yangeelekezwa na kupangwa kirazini na kulingana na hali za kibinadamu. Lakini, mara nyingi mno maendeleo haya yanageuka kuwa sababu ya kuongeza uzito wa tofauti hizo au pengine hata kurudisha nyuma hali za kijamii kwa walio wanyonge, na hatimaye kuleta dharau kwa maskini. Wakati ambapo umati mkubwa wa watu unakosa bado mahitaji yake ya lazima, wapo wengine, hata katika nchi zenye maendeleo hafifu, wanaoishi katika utajiri kupindukia na kutapanya mali. Anasa na umaskini vinakwenda sambamba. Na wakati watu wachache wanapokuwa na uwezo mkubwa wa kuamua, basi wengi hukaribia kukosa kabisa uwezekano wa kutenda kwa hiari yao na kwa uwajibikaji wao wenyewe. Na hawa mara nyingi hubaki katika hali za maisha na za kazi zisizostahili utu wa kibinadamu.

Ukosefu wa ulinganifu wa kiuchumi na wa kijamii namna hii unaonekana kati ya kilimo, viwanda na idara mbalimbali za huduma; kama vile katika kanda mbalimbali za nchi moja. Migogoro inayozidi siku kwa siku kati ya nchi zilizoendelea zaidi kiuchumi na nchi nyinginezo inaweza kuihatarisha amani katika ulimwengu mzima.

Watu wa siku hizi wanazidi kutambua kwa undani tofauti hizi zilizopo, maadam wanaamini kwamba uwezo wa kiteknolojia na kiuchumi unaozidi kuwa mkubwa katika ulimwengu wa leo, ungeweza na ungepaswa kusahihisha hali hii mbaya ya mambo. Kutokana na hayo yanatakiwa mageuzi mengi katika maisha ya kiuchumi kijamii, pamoja na mabadiliko katika namna ya kufikiri na ya kuishi, kwa wote. Kwa lengo hilo Kanisa, katika mfululizo wa historia na hasa siku hizi, limetunga na kuieleza miongozo kuhusu haki na usawa inayotakiwa na utaratibu wa uadilifu. Nayo miongozo hutokana na mwanga wa Injili na kuyaelekea maisha ya kibinafsi, ya kijamii na mahusiano ya kimataifa. Mtaguso Mkuu unadhamiria kuithibitisha miongozo hii kutokana na hali ya siku hizi na kutoa maelekezo kadhaa, hasa ukizingatia madai ya maendeleo ya kiuchumi [139].

Ibara ya Kwanza

MAENDELEO YA KIUCHUMI

 
Maendeleo ya kiuchumi kwa huduma ya binadamu

64. Siku hizi kuliko huko nyuma lipo ongezeko la uzalishaji mali katika fani za kilimo na viwanda, pamoja na la utoaji huduma mbalimbali. Nalo linakusudia kwa haki kukidhi ongezeko la idadi ya watu na kutosheleza matarajio ya wanadamu wote. Kwa hiyo tunapaswa kuhamasisha maendeleo ya kiteknolojia, moyo wa kuleta mabadiliko, uanzishaji wa shughuli mpya na ustawishaji wake. Tena tunapaswa kuhamasisha ulinganifu wa mbinu mbalimbali za uzalishaji mali na bidii kabambe zinazofanywa na wale wanaoshiriki katika uzalishaji huo. Yaani kwa neno moja, twatakiwa kuyahimiza yale yote yanayochangia katika maendeleo haya. Zaidi, lengo la mwisho na la msingi la maendeleo ya namna hii si tu kuongeza bidhaa zinazozalishwa, wala si kutafuta tu faida na utawala wa uchumi. Bali lengo la mwisho na la msingi lipo kwa ajili ya huduma ya binadamu, akitazamwa katika utu wake mzima, yaani yakizingatiwa mahitaji yake ya kimwili pamoja na madai ya maisha yake ya kifikra, kimaadili, kiroho na kidini. Tena yafaa yazingatiwe mahitaji ya kila mtu, ya kila kundi, ya kila kabila, hatimaye pande zote za ulimwengu. Kwa hiyo harakati yote ya kiuchumi lazima itekelezwe kadiri ya sheria na mbinu maalum za uchumi, lakini katika mipaka ya utaratibu wa kimaadili[140], ili ilingane na mpango wa Mungu juu ya binadamu[141].

Maendeleo ya kiuchumi kudhibitiwa na binadamu
 
65. Maendeleo ya kiuchumi lazima yabaki chini ya udhibiti wa binadamu, wala hayawezi kuachwa chini ya uamuzi wa watu wachache ama makundi yenye uwezo mkubwa mno wa kutawala uchumi. Tena maendeleo ya kiuchumi hayawezi kuamuliwa na jamii za siasa tu, wala si na baadhi ya mataifa machache yenye nguvu zaidi. Kinyume chake, yafaa kwamba idadi kubwa ya watu iwezekanavyo, wa kila uwanja, washiriki kimatendo katika uongozi wake. Na vilevile, ikiwa ni suala la mahusiano ya kimataifa, mataifa yote yashirikishwe katika uongozi huo. Kadhalika, shughuli zote za hiari za watu binafsi na za mashirika yao mbalimbali ni lazima yaungane na kulinganishwa ifaavyo na juhudi zinazofanywa na serikali.
 
Maendeleo ya kiuchumi hayawezi kuachwa yajiongoze yenyewe kadiri ya utendaji wake wa watu binafsi, wala chini ya uamuzi wa serikali tu. Kwa sababu hiyo, lazima kukemea makosa ya zile itikadi ambazo, kwa kadiri ya fikra za uongo kuhusu uhuru, zinapinga mageuzi yaliyo ya lazima. Tena twapaswa kuonya makosa ya zile [itikadi] ambazo hufuatisha haki za msingi za watu binafsi na za makundi nyuma ya mfumo wa ujima wa uzalishaji mali ( organizationi productionis collectivae) [142].

Kwa upande mwingine, raia wote wakumbuke kwamba wana haki na wajibu wa kuchangia katika maendeleo ya jamii yao wenyewe kadiri ya uwezo wao. Na haki na wajibu hizo inabidi zitambuliwe pia na serikali. Matumizi ya mali zote zilizopo yanatakiwa hasa katika nchi ambazo maendeleo yake ni duni zaidi. Basi, papo hapo wale ambao wanalimbikiza mali zao bila kuzitumia, au pengine wale ambao wanazinyima jamii zao misaada ya kimwili na kiroho inayohitajika – isipokuwa haki ya kila mtu ya kuhamia – hawa hudhuru vibaya manufaa ya wote katika jumuiya zao.

 
Tofauti kubwa za kiuchumi na kijamii zikomeshwe
 
66. Ili kukidhi madai ya haki na usawa lazima kujitahidi kwa kila hali ili tofauti kubwa za kiuchumi zilizopo na pengine zinazokua ziondoshwe kwa upesi iwezekanavyo, ila kwa heshima ya watu na ya tabia maalum ya kila taifa. Maana tofauti hizi zinaleta ubaguzi katika haki za kibinafsi na katika hali ya kijamii. Kadhalika, tukizingatia shida za pekee kwa upande wa fani ya kilimo kuhusu uzalishaji mali na uuzaji wa mazao, tunaona kwamba katika mahali pengi wakulima lazima wasaidiwe ili kuongeza kiwango cha uzalishaji mali na uuzaji wake. Tena, wakulima inabidi wasaidiwe kutekeleza mabadiliko yale yaliyo ya lazima na kubuni mbinu mpya zitakazotumika katika kufikia kiwango cha mapato kitakiwacho, kusudi wasibaki katika hali duni ya kijamii kama inavyotokea mara nyingi. Wakulima wenyewe, na hasa vijana, wajibidishe kujiendeleza katika ustadi wao ambao, pasipo huo, kilimo hakiwezi kustawishwa [143].
 
Haki na usawa vinadai kwamba maisha ya watu binafsi na ya familia zao yasitiwe mashaka na wasiwasi kwa sababu ya hali ya uhamishaji inayodaiwa katika maendeleo ya kiuchumi. Kwa hiyo, mipango ya uhamishaji huo iratibiwe ipasavyo. Aina yoyote ya ubaguzi katika ujira na kazi iepukwe kwa makini mintarafu wafanyakazi ambao, wakitoka katika mataifa na nchi nyingine, kwa kazi yao wanachangia kukuza uchumi wa taifa au eneo lilipo tofauti na lile la asili. Aidha watu wote, na serikali ndiyo wa kwanza, hupaswa kuwapokea wageni hawa kama binadamu, na wala si kama vyombo vitupu vya uzalishaji mali tu; tena wote wanapaswa kuwasaidia ili waweze kuichukua familia pamoja nao na kujitafutia makazi yastahiliyo; na hatimaye wote wanatakiwa kuwasaidia kwa kuchukuliana na mfumo wa maisha ya kijamii ya taifa au nchi inayowapokea. Lakini, bidii ifanyike ili nafasi za kazi zipatikane katika nchi zao wenyewe kadiri iwezekanavyo.

Katika hali ya uchumi unaoendelea, juhudi lazima zifanyike ili kila mmoja apate nafasi ya kazi ya kutosha na imfaayo pamoja na uwezekano wa kupewa mafunzo ya kikazi na kiufundi. Kwa mfano, izingatiwe hali mpya ya jamii inayotegemea uchumi wa viwanda ambapo mitambo inayojiendesha (automatio) huzidi kutumiwa katika utekelezaji wa kazi. Kisha lazima riziki itolewe, na heshima ya kiutu ihifadhiwe, kwa wale ambao wapo katika hali ngumu, hasa kwa sababu ya ugonjwa au uzee.

Ibara ya Pili

KANUNI KADHAA ZA UTARATIBU KATIKA MAISHA YA KIUCHUMI KIJAMII KWA UJUMLA

 
Kazi, hali zake na wakati wa mapumziko
 
67. Binadamu anatekeleza kazi yake ili kuzalisha na kubadilisha mali, na kutoa huduma mbalimbali za kiuchumi. Kazi hiyo ina thamani kubwa zaidi kuliko vipengele vingine vya maisha ya kiuchumi, kwa sababu hivi vingine ni vyombo tu vinavyotumiwa ili kulifikia lengo fulani.
 
Maana kazi [ya binadamu], iwe inafanywa kwa kujitegemea, ama chini ya uongozi wa watu wengine, hutokana moja kwa moja na mtu mwenyewe ambaye anavitia viumbe kama muhuri wake na kuvitiisha chini ya utashi wake. Kwa kazi yake, kwa kawaida mtu hupata riziki kwa ajili yake na ya familia yake, hushirikiana na wenzie na kuwahudumia wanadamu nduguze; tena huweza kuishi kwa upendo halisi na kuchangia kwa utendaji wake mwenyewe katika kuukamilisha uhulushi wa kimungu. Zaidi, twajua kuwa binadamu, akimtolea Mungu kazi yake, hushirikiana na tendo la ukombozi wa Yesu Kristo, ambaye ameiweka kazi katika hali ya heshima kubwa akifanya kazi kwa mikono yake mwenyewe huko Nazarethi. Hutokana na hayo, kwa kila mtu, wajibu wa kufanya kazi kiaminifu, pamoja na haki ya kufanya kazi. Kadhalika, kwa upande mwingine, ni wajibu wa jamii – kadiri ya hali yake – kuwasaidia raia ili waweze kupata nafasi ya kazi ya kutosha. Aidha, kazi haina budi kulipwa kwa kiasi kitoshacho ili kumpatia mtu binafsi na familia yake vifaa vya kutosha kwa kuishi maisha yenye heshima kimwili, kijamii, kiutamaduni na kiroho. Na mishahara hiyo ilingane na aina ya kazi pamoja na kiwango cha uzalishaji mali cha kila mtu; kisha izingatiwe hali ya mwajiri na pia manufaa ya wote [144].

Maadamu utendaji wa kiuchumi mara nyingi hutekelezwa kwa ushirikiano wa watu wengi, basi si haki wala hailingani na hali ya kiutu kupanga kazi hiyo kwa mfumo na utaratibu unaowanyanyasa wafanyakazi wawao wote. Lakini mara nyingi mno, hata siku hizi, hutokea kwamba wafanyakazi wanafanywa kuwa watumwa wa kazi zao. Jambo hilo haliwezi kabisa kupata udhuru yake kutokana na sheria ziitwazo za kiuchumi. Basi, ni lazima kulinganisha mfumo wa kazi yenye uzalishaji mali na madai ya binadamu pamoja na mtindo wa maisha yake, kuanzia na maisha ya nyumbani, hasa kwa upande wa akina mama wenye familia. Na vilevile jinsia na umri daima vizingatiwe. Aidha, wafanyakazi wapewe fursa ya kutumia vipawa na hulka yao katika utekelezaji wa kazi yenyewe. Wafanyakazi wote watekeleze kazi yao kwa uwajibikaji utakiwao wakitumia muda na bidii yao; lakini hawa lazima wapewe pia muda wa kutosha kwa kupumzika na kustarehe ili wapate kuyashughulikia maisha ya kifamilia, kiutamaduni, kijamii na kidini. Zaidi wafanyakazi wote inabidi wapewe nafasi ya kuzistawisha, kwa shughuli za hiari, zile nguvu na vipawa ambavyo pengine haviwezi kukuzwa katika kazi zile walizopewa na waajiri wao.

Ushirikiano katika amala za biashara na katika mfumo wa kiuchumi kwa ujumla. Migongano katika kazi  

68. Katika makampuni ya kiuchumi wanaungana watu, yaani wanadamu walio huru na wenye hiari ya kujiamulia mambo, walioumbwa kwa sura ya Mungu. Kwa hiyo ushirikiano wa kimatendo wa wote katika kuendesha kampuni (inceptorum curatione) lao uhamasishwe[145], kwa mtindo unaopaswa kuamuliwa kwa namna ifaayo. Ila wadhifa wa kila mmoja – yaani mmilikaji, mwajiri, viongozi na wafanyakazi – uzingatiwe, na umoja wa uongozi unaodaiwa uhifadhiwe. Lakini mara nyingi maamuzi mintarafu hali za kijumla zihusuzo masuala ya kiuchumi na kijamii hayachukuliwi katika kiwango cha makampuni yenyewe, bali katika kile kiwango cha juu zaidi cha vyombo maalum vinavyohusika na uongozi. Basi, maadamu mategemeo ya baadaye ya wafanyakazi na ya watoto wao hutokana na maamuzi hayo, ni lazima hawa washirikishwe kimatendo, wao wenyewe ama wawakilishi waliochaguliwa kwa uhuru.

Miongoni mwa haki za msingi za binadamu hazina budi kuhesabiwa haki ya wafanyakazi ya kuunda vyama vyao kwa uhuru, vinavyoweza kweli kuwawakilisha na kuchangia katika kuratibu ipasavyo maisha ya kiuchumi. Tena, ihesabiwe haki yao ya kuushiriki kwa uhuru utendaji wa vyama hivyo bila ya kuingia katika hatari ya kuadhibiwa. Hivyo, wote watazidi kuelewa nafasi na uwajibikaji wao kwa msaada wa ushirikiano ulioratibiwa namna hii, pamoja na elimu ya kiuchumi na kijamii yenye kuongezeka. Kwa njia hiyo wafanyakazi watajisikia kuwa ndio watendaji, kadiri ya uwezo na mwelekeo wa kila mmoja, katika mfumo mzima wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na wa ujenzi wa manufaa ya wote duniani kote.

Ikiwa itatokea migongano ya kiuchumi kijamii, kila juhudi lazima ifanyike, ili kuufikia usuluhishi wa amani. Njia ya kwanza iwe ni mijadala ya kweli kati ya makundi yanayohusika. Lakini hata hivyo katika mazingira ya siku hizi mgomo unaweza kubaki kama njia pekee na ya lazima, ingawa ni ya mwisho, ili kutetea haki za wafanyakazi na kukidhi matarajio yao ya haki. Lakini njia zifaazo ili kuanzisha tena mijadala kwa maafikiano na usuluhishi zifuatiliwe upesi iwezekanavyo.

Mali za dunia ni kwa ajili ya watu wote

69. Mungu ameiweka dunia na vyote viijazavyo kwa ajili ya matumizi ya wanadamu wote na mataifa yote, hivi kwamba vitu vyote vilivyoumbwa lazima vigawanywe kwa wote kwa kipimo kilicho sawa, haki ikiwa kiongozi na upendo ukiwa mwenzi[146]. Kwa hiyo, ni lazima daima kuridhisha makusudio ya kiumma ya mali (bonorum universalem destinationem), bila kujali namna mbalimbali za umilikaji, kulingana na kawaida zilizo halali za mataifa na kadiri ya mtazamo wa mazingira mbalimbali yanayobadilika. Binadamu, katika kutumia mali hizo anapaswa kutambua kuwa mali anazozimiliki kwa halali hazipo kwa ajili yake tu, bali pia kwa ajili ya wengine kwa pamoja, kwa maana kwamba zinaweza kumsaidia si yeye peke yake tu, bali pia wengine[147]. Licha ya hayo, ni haki ya watu wote kushiriki sehemu ya kutosha ya mali kwa ajili yao na ya familia zao. Na ndivyo walivyoona kuwa ni haki Mababa na Walimu wa Kanisa walipokuwa wakifundisha kwamba wanadamu wanalo sharti la kuwasaidia maskini, wala si tu kuwapa yaliyo ya ziada[148]. Yule aliyepo katika shida ya lazima kabisa (extrema necessitate degit) anayo haki ya kujipatia mahitaji kutokana na utajiri wa wengine[149]. Mtaguso Mkuu, ukizingatia idadi kubwa sana ya watu wanaoelemewa na njaa, unawasihi hima wote, watu binafsi kwa serikali, ili wakumbuke tamko la mababa, “Umlishe aliye kufani kwa njaa, maana kama hukumlisha umemwua”[150]. Hivyo, wote wawashirikishe kweli wengine mali zao na kuzitumia ifaavyo, kila mmoja kadiri ya uwezo wake, hasa kwa kuwapatia watu binafsi na mataifa vifaa ambavyo kwavyo wataweza kujiruzuku na kujiendeleza.

Mara nyingi katika jamii ambazo zina maendeleo duni kiuchumi, makusudio ya kiumma ya mali yanazingatiwa walau kwa kiasi katika ujumla wa desturi na kawaida za kijumuiya; maana hizo zinanuia kumsaidia mwanajumuiya katika kupata mahitaji yaliyo ya lazima. Hata hivyo, haifai kudhani kwamba desturi kadhaa haziwezi kubadilishwa katu ikiwa hazilingani tena na madai ya wakati wa sasa. Na kwa upande mwingine, si vema kutenda lolote kiholela dhidi ya desturi zile zilizo nyofu na ambazo hazikomi kuleta manufaa, ilimradi zilingane ifaavyo na mazingira ya sasa. Kadhalika, katika nchi zilizoendelea sana kiuchumi, mfumo wa taasisi za kijamii zinazoushughulikia misaada na usalama wa kijamii unaweza kuchangia kiasi chake katika kuwafikishia watu wote mali [hizo]. Aidha, ni muhimu sana kustawisha zaidi taasisi ziihudumiazo familia na mahitaji ya kijamii, na hasa zile zizishughulikiazo fani za utamaduni na elimu. Lakini katika harakati za kuzipanga taasisi hizo lazima kukaa macho ili raia wasisukumwe kushikilia tabia ya wivu kuhusu jamii, wala tabia inayopuuza uwajibikaji katika kazi, au inayokataa kutoa huduma.
 
Vitegauchumi na fedha

70. Kwa upande wake vitegauchumi lazima vichangie katika kuwapatia watu nafasi ya kufanya kazi, pamoja na mshahara wa kutosha kwa sasa na kwa siku za mbele. Wale wote wanaowajibika katika vitegauchumi hivi na katika kuratibisha maisha ya uchumi kwa ujumla – wawe watu binafsi, ama makundi, au serikali – inawabidi wayazingatie malengo hayo na kuelewa wajibu wao mzito. Nao wajibu utakuwa, kwa upande mmoja, kuangalia ili kila mtu na jumuiya nzima wapate riziki zinazodaiwa kwa maisha yenye kustahili; kwa upande mwingine, utakuwa muhimu kutambua mahitaji ya baadaye. Na hivyo wataleta uwiano mzuri kati ya mahitaji ya sasa ya kibinafsi na ya kijamii na madai ya kuweka vitegauchumi kwa ajili ya kizazi cha baadaye. Aidha, yazingatiwe daima mahitaji ya haraka ya mataifa au nchi ambazo bado zina maendeleo duni. Katika uwanja wa fedha kila mmoja ajihadhari na tendo la kudhuru manufaa ya nchi yake au ya nchi nyingine. Kisha, suala la wale ambao ni wadhaifu kiuchumi halina budi kushughulikiwa ili wasiathiriwe pasipo haki na mabadiliko ya thamani ya fedha.

Haki ya kumiliki vitu, na mali ya binafsi; na juu ya mashamba makubwa ya kibepari
 
71. Kumiliki vitu na aina nyingine za umilikaji wa kibinafsi juu ya mali za nje ( bona exteriora) vinachangia kujidhihirisha kwa vipawa alivyo navyo mtu. Aidha, vinampatia binadamu fursa ya kutoa mchango wake wa uwajibikaji katika jamii na uchumi. Kwa sababu hiyo, ni muhimu sana kuwasaidia watu wote, watu binafsi na makundi, wawe na kiasi fulani cha umilikaji wa mali za nje.

Mali za binafsi au aina kadhaa za umilikaji wa mali za nje zinampatia mtu nafasi iliyo ya lazima ya kujitegemea yeye na familia yake; tena hazina budi kuhesabiwa kama mwendelezo wa uhuru wa binadamu. Nazo hatimaye, zikiwahimiza watu kushikilia haki na wajibu zao, zinapata kuwa sharti mojawapo la uhuru wa kiraia[151].

Namna za umilikaji huo na za mali hizi [za binafsi] zinajitokeza siku za leo kwa mitindo mbalimbali na zinazidi kutofautiana kati yao siku kwa siku. Na ingawa ipo misaada ya kijamii, haki na huduma zinazotolewa na jamii, hata hivyo namna zote za umilikaji huo na za mali za binafsi zinaendelea kuwa sababu kubwa za usalama. Na jambo hilo halihusu tu umilikaji wa mali yakinifu ( proprietatibus materialibus), bali pia umilikaji wa mali-akili, kama ulivyo ustadi katika nyanja mbalimbali za ufundi.
 
Haki ya kuwa na mali za binafsi haipingani na ile ya mitindo mbalimbali ya umilikaji wa kiserikali ( proprietatum publicam). Lakini utaifishaji wa mali hauwezi kutekelezwa isipokuwa na chombo chenye mamlaka, kadiri ya madai ya manufaa ya wote na ndani ya mipaka yake, na hatimaye kwa fidia iliyo ya haki. Aidha, ni juu ya serikali kuzuia mtu awaye yote asitumie isivyo halali haki yake ya kumiliki mali, akihatarisha manufaa ya wote [152].
 
Umilikaji-mali wa binafsi wenyewe kwa maumbile yake una dhima yake katika jamii; nao una msingi wake katika sheria ya makusudio ya kiumma ya mali [153]. Tukipuuza umuhimu wa dhima hiyo [ya mali ya binafsi katika jamii], umilikaji unaweza ukawa chanzo cha choyo na cha fujo kali kwa namna nyingi. Na hivyo, wapinzani wake wanaweza kwa urahisi kujipatia kisa cha kuhujumu haki yenyewe ya umilikaji mali.

Katika nchi nyingi ambazo zina maendeleo duni kiuchumi, kunapatikana umilikaji wa mashamba makubwa na pengine mapana sana, ambayo yanalimwa kidogo tu au yanalala bure na kutunzwa kama akiba kwa sababu ya ulanguzi (lucri causa), bila kulimwa. Na wakati huohuo umati wa watu hawana mashamba ya kulima au wanatumia vishamba vidogo mno. Kwa upande mwingine haja ya kuongeza uzalishaji wa mazao ni tatizo ambalo linadai kutatuliwa mapema. Mara nyingi hutokea kwamba wale wanaoajiriwa na mabwana wao, yaani wale wanaolima sehemu ya ardhi kwa kukabidhiwa tu, hao hupata mishahara au aina nyingine za thawabu ambazo hazistahili hadhi ya binadamu, wala hawana makazi ya heshima au hunyonywa na wanyapara. Na hivyo wakinyimwa usalama, huishi katika hali ya kumtegemea mwingine kiasi kwamba wanazuiliwa kila uwezekano wa kutenda kwa hiari na kwa kujiwajibisha wao wenyewe. Tena wanakatazwa kila endeleo la kiutamaduni na kila ushirikiano wa kimatendo katika maisha ya kijamii na ya kisiasa. Kwa hiyo, kadiri ya mazingira mbalimbali, yanadaiwa mageuzi yanayokusudia kukuza mishahara, kuboresha hali katika kazi, kustawisha uhakika wa ajira, na kuhamasisha hali ya kujituma kwa kila mmoja. Aidha, yanadaiwa mageuzi yatakayowezesha kugawa yale mashamba yanayomilikiwa tu bila kulimwa, kwa manufaa ya wale wenye uwezo wa kuzalisha. Kwa suala hili, lazima vitolewe vifaa na vyombo vinavyodaiwa kwa lengo hilo, na hasa misaada ya kielimu na kwa ajili ya kuunda mashirika (cooperativae) yenye kuleta manufaa. Na pale ambapo manufaa ya wote yanadai kutaifishwa kwa mali, basi fidia ihesabiwe kwa haki yakizingatiwa mazingira yote yanayohusika.

Utendaji wa kiuchumi kijamii, na Ufalme wa Kristo
 
72. Wakristo wanaoshiriki kimatendo katika maendeleo ya kiuchumi kijamii ya siku hizi na wanaotetea haki na mapendo, waamini kuwa wanaweza kuchangia kwa vikubwa katika ustawi wa wanadamu na amani ya ulimwengu. Katika harakati za namna hii watoe mfano bora, wakitenda kama watu binafsi ama kwa pamoja. Kwa hiyo, wakishajipatia ujuzi na mang’amuzi yaliyo ya lazima kabisa, wakifanya shughuli hizi za kidunia wauhifadhi utaratibu ulio mnyofu, wakiwa waaminifu kwa Kristo na Injili yake. Na hivyo maisha yao yote, ya kibinafsi na ya kijamii, yakolezwe na roho ya heri za kiinjili, hasa na roho ya umaskini.

Yule amfuataye Kristo kiaminifu huutafuta kwanza Ufalme wa Mungu. Naye huchota kwake upendo imara na safi zaidi ili kuwasaidia ndugu zake wote na kuyatimiza matendo ya haki chini ya uongozi wa mapendo[154].

Sura ya Nne

MAISHA YA JUMUIYA YA KISIASA

 
Maisha ya hadhara ya siku hizi

73. Katika nyakati zetu mageuzo ya ndani yanaonekana pia katika mifumo na vyombo vya uongozi wa mataifa; nayo yanatokana na maendeleo ya kiutamaduni, kiuchumi na kijamii ya mataifa. Mageuzo hayo yanaathiri sana maisha ya jumuiya ya kisiasa, hasa katika uwanja wa wajibu na haki za watu wote kuhusu matumizi ya uhuru wa kiraia na katika kupania manufaa ya wote. Tena, yana nguvu kubwa juu ya uratibishaji wa mahusiano baina ya raia wenyewe na pia kati ya raia na serikali.

Utambuzi hai wa hadhi ya binadamu katika mahali pengi duniani unaamsha juhudi ya kuunda utaratibu wa kisiasa na kisheria ambapo haki za binadamu katika maisha ya hadhara ( vita publica) zinalindwa vema zaidi. Nazo ndizo haki za kujumuika na kuunda umoja kwa uhuru, haki ya kila mmoja kutoa maoni yake na kukiri imani yake akiwa peke yake au hadharani. Maana, ulinzi wa haki za binadamu ni sharti la lazima ili raia, kila mmoja peke yake au kama wanachama, waweze kushiriki kimatendo maisha ya umma na uongozi wa mambo yanayoyahusu.
 
Pamoja na maendeleo ya kiutamaduni, kiuchumi na kijamii, hamu ya walio wengi ya kuchukua wajibu mkubwa zaidi katika kuratibu maisha ya jumuiya ya kisiasa inazidi kupata nguvu. Katika dhamiri ya watu wengi bidii ya kuhifadhi haki za makundi ya wachache katika nchi zao inastawi, lakini bila ya makundi hayo ya wachache kusahau wajibu zao mbele ya jumuiya ya kisiasa. Aidha, inazidi kukua heshima mbele ya watu wenye maoni au dini tofauti. Na wakati huohuo ushirikiano mpana zaidi unaundwa; nao unalenga kwa raia wote – siyo kwa wachache tu wenye marupurupu – ili wapate kutumia kimatendo haki zao za binafsi.
 
Aidha, inalaumiwa mitindo yote ya kiserikali iliyomo katika nchi kadhaa inayozuia uhuru wa kiraia au wa kidini, inayoongeza idadi ya wale wanaouawa kwa choyo na jinai za kisiasa, na inayopotosha utekelezaji wa mamlaka kuhusu manufaa ya wote ili kulinufaisha kundi moja au watawala wenyewe.

Ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya kibinadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upendo na huduma kwa manufaa ya wote. Pia ni kuuimarisha msimamo (persuasiones) wa msingi mintarafu maumbile halisi ya jumuiya ya kisiasa; tena kuhusu lengo, matumizi ya halali na mipaka ya wajibu wa serikali.

Maumbile na lengo la jumuiya ya kisiasa

74. Wanadamu, familia na makundi mbalimbali, wanaounda jumuiya ya kiraia wanaelewa vema kuwa peke yao hawawezi kujenga kikamilifu maisha ya kiutu. Nao wanaona ulazima wa kuunda jumuiya iliyo pana zaidi, ambapo wote wataleta mchango wa vipawa vyao kila siku[155], ili kuyafikia zaidi na zaidi manufaa ya wote. Ndiyo maana hawa wanaunda jumuiya ya kisiasa kadiri ya mitindo yake mbalimbali. Na jumuiya hiyo imewekwa kwa ajili ya yale manufaa ya wote ambayo kwa ajili yake [jumuiya] yenyewe inapata sababu na umaana wake kikamilifu. Hivyo, tokea hayo inapata pia utaratibu wake wa kisheria, maalum na wa kimsingi. Na manufaa ya wote ni ujumla wa zile hali za maisha ya kijamii ambazo kwazo wanadamu, familia na vyama mbalimbali huweza kupata kikamilifu na upesi zaidi utimilifu wake[156].

Lakini, katika jumuiya ya kisiasa watu wengi hukusanyika pamoja walio tofauti kati yao; nao kwa halali huweza kuelekea maamuzi yanayohitilafiana. Ili jumuiya ya kisiasa isidhuriwe na tofauti za maoni ya kila mmoja basi ni lazima uwepo uongozi wenye uwezo wa kuzielekeza nguvu za raia wote kuyafikia manufaa ya wote. Nalo litekelezwe si kama mashine (mechanice), wala si kwa mabavu, bali hasa kama nguvu ya kimaadili yenye msingi wake katika uhuru na hisia ya uwajibikaji kwa jukumu lililochukuliwa.

Basi, ni wazi kwamba jumuiya ya kisiasa na mamlaka ya kiserikali vimeasisiwa katika hali ya binadamu; navyo, kwa sababu hii, vimo katika utaratibu uliowekwa na Mungu, ijapo uchaguzi wa utawala wa kisiasa, pamoja na uteuzi wa watawala huachiwa maamuzi huru ya raia [157].
 
Hufuata kuwa utawala wa kisiasa, uwe unatekelezwa na jumuiya yenyewe au na vyombo vinavyowakilisha dola ( rem publicam), ni lazima daima ufanyike ndani ya mipaka ya sheria ya kimaadili. Na lengo lake ni kuyafikia manufaa ya wote, tena manufaa yenye maendeleo yake, kadiri ya kanuni za utaratibu wa kisheria uliokwisha kuwekwa, au wa kuwekwa. Na hapo ndipo raia wanapolazimishwa kutii kwa sababu ya dhamiri zao [158]. Tokea hapo hueleweka wazi uwajibikaji, wadhifa na umuhimu wa uongozi wa serikali.
 
Na pale raia wanapoonewa na serikali inayovuka mipaka ya madaraka yake, ndipo wasikatae [kutii] kama yale yanayodaiwa ni kwa manufaa ya wote. Lakini ni halali kwao kutetea haki zao na za raia wenzao dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka hayo, kwa kuheshimu mipaka iliyowekwa na sheria ya maumbile na ya kiinjili.

Namna mbalimbali ambazo kwazo jumuiya ya kisiasa inaratibisha miundo yake na utekelezaji wa madaraka ya kisiasa zaweza kutofautiana, kadiri ya tabia za mataifa zilivyo mbalimbali, na ya maendeleo ya kihistoria. Lakini, daima ni lazima zikusudie katika kumuunda mtu mwadilifu, mtulivu, na mkarimu kwa wote, kwa manufaa ya familia nzima ya wanadamu.

Ushirikiano wa wote katika maisha ya hadhara
 
75. Inalingana kikamilifu na maumbile ya binadamu kwamba ipatikane miundo ya kisiasa na kisheria inayowawezesha zaidi na zaidi raia wote – bila ubaguzi wowote – kushiriki kwa uhuru na kwa matendo katika kutengeneza misingi ya kisheria ya jumuiya ya kisiasa, katika kuongoza mambo ya dola, katika kuainisha uwanja wa kazi na mipaka yake kwa taasisi mbalimbali, na hatimaye katika kuwachagua viongozi [159]. Kwa sababu hiyo, raia wote wakumbuke haki yao, ambayo pia ni wajibu, ya kutumia kura yao huru kwa minajili ya kuhamasisha manufaa ya wote. Kanisa linasifu na kuthamini wale ambao, kwa ajili ya kuwatumikia wanadamu, wanajitoa kwa manufaa ya dola na kubeba uzito wa wajibu husika.
 
Ili ushirikiano wa raia pamoja na hisia zao za uwajibikaji ziweze kuleta matokeo mazuri katika maisha ya kisiasa ya kila siku, utaratibu mzuri wa kisheria unatakiwa, ambao utasaidia kupanga mgawanyo ufaao wa majukumu na wa vyombo vya utawala pamoja na ulinzi imara na huru wa haki [za raia]. Haki za watu, za familia na za makundi, pamoja na utekelezaji wake, ni lazima zitambuliwe, ziheshimiwe na kuhamasishwa [160]; kama vile pia wajibu zinazomkalia kila raia. Miongoni mwa wajibu hizi ni vema kukumbushia wajibu wa kujishughulisha na mambo yauhusuyo umma na kutoa huduma za kimatendo na kibinafsi zinazotakiwa kwa manufaa ya wote. Na viongozi wajiepushe na kuweka vizuizi dhidi ya familia, makundi ya kijamii na kiutamaduni, mashirika au taasisi za kati ( instituta intermedia); wala wasiwanyime uwezo wao ulio halali na wenye manufaa wa kutenda kazi, bali, kinyume chake, wavihamasishe vyombo hivyo kwa hiari na utaratibu. Na kwa upande wao raia, kila mmoja binafsi na katika makundi, wasiipe serikali uwezo mkubwa mno, wala wasiiombe masilahi kubwa mno isivyofaa. Maana hapo kuna hatari ya kupunguza uwajibikaji wa watu, familia na makundi ya kijamii.

Katika nyakati zetu ugumu wa masuala yanayojitokeza unazilazimisha serikali kujihusisha zaidi katika fani za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni ili kuleta mazingira yanayofaa zaidi kusudi raia na makundi waweze kuyafuatilia kwa bidii na kwa uhuru manufaa kamili ya binadamu. Uhusiano kati ya ujamiisho (socializationem)[161] na uwezo wa kujiratibisha na kujiendeleza kwa mtu binafsi unaweza kufikiriwa kwa namna tofauti katika nchi mbalimbali za ulimwengu na kwa mujibu wa maendeleo ya mataifa. Lakini pale ambapo utekelezaji wa haki unapunguzwa kwa muda kwa ajili ya manufaa ya wote, basi mazingira yanapobadilika uhuru urejeshwe mapema iwezekanavyo. Aidha, si ubinadamu kwa serikali kutumia namna za utawala wa mabavu au za udikteta zinazovunja haki za mtu ama za makundi ya kijamii.

Raia wastawishe upendo kwa taifa lao kwa ari na unyofu, lakini si kwa mtazamo mfinyu, yaani hivi kwamba wayazingatie daima mema ya familia nzima ya wanadamu inayounganika kwa vifungo mbalimbali kati ya makabila, mataifa na nchi.
 
Wakristo wote hawana budi kufahamu kwa undani wito wao maalum katika jumuiya ya kisiasa. Nao lazima wawe kielelezo angavu, wakikuza ndani yao hisia ya uwajibikaji na ya kujitoa kwa manufaa ya wote. Na hivyo wabainishe pia kwa matendo jinsi yanavyoweza kuafikiana mamlaka na uhuru, uanzishaji wa kibinafsi na mshikamano wa mwili mzima wa kijamii, na hatimaye umoja ufaao na utofauti uletao faida. Tena wakristo wanapaswa kukubali wingi wa maoni ulio halali na tofauti zake mintarafu mambo ya dunia, na kuwaheshimu raia ambao, hata katika makundi, hutetea kauli zao kwa unyofu. Vyama vya siasa navyo havina budi kuyahamasisha yale yanayodaiwa na manufaa ya wote, kadiri ya mtazamo wao; lakini kamwe si halali kutanguliza maslahi yao mbele ya manufaa ya wote.

Aidha inapasa kushughulikia kwa bidii elimu ya kiraia na kisiasa iliyo ya lazima siku za leo kwa watu wote, na hasa kwa vijana, ili raia wote waweze kushika nafasi zao katika maisha ya jumuiya ya kisiasa. Wale walio tayari kuishughulikia fani ya siasa iliyo ngumu lakini pia yenye ustahivu[162], ama wale wanaoweza kujizatiti kwa ajili ya kazi hiyo, basi wajiandae na kujibidisha ili kuitekeleza bila ya kujali manufaa yao wala maslahi ya pesa. Nao watende kwa unyofu na busara dhidi ya udhalimu na uonevu, [dhidi ya] utawala wa mabavu na ujeuri usio mvumilivu wa mtu mmoja au wa chama kimoja tu; na hatimaye, wajitolee kiaminifu na pasina ubaguzi katika kutoa huduma kwa wote, tena kwa mapendo na uimara utakiwao katika maisha ya kisiasa.

Jumuiya ya kisiasa na Kanisa
 
76. Ni muhimu sana hasa katika jamii inayozingatia wingi wa maoni na wa taasisi ( societas pluralistica), kuchukulia kwa mtazamo ulio mnyofu mahusiano kati ya jumuiya ya kisiasa na Kanisa. Tena, kuna umuhimu mkubwa kutofautisha wazi kati ya matendo ambayo waamini wanayafanya kwa jina lao, kibinafsi au katika makundi, kama raia wanaoongozwa na dhamiri ya kikristo, na matendo wayafanyayo kwa jina la Kanisa katika umoja na wachungaji wao.
 
Kanisa halichangamani katu na jumuiya ya kisiasa, wala halifungamani na mtindo wowote wa mfumo wa kisiasa kwa sababu ya majukumu na uhalali wake ( sui muneris et competentiae). Nalo ni alama, pia ni ulinzi, wa tabia ya juu kabisa ya binadamu.
 
Jumuiya ya kisiasa na Kanisa zina uhuru na mamlaka kila moja katika uwanja wake. Na zote mbili zipo kwa ajili ya kutumikia wito wa binadamu, wake binafsi na katika jamii, ijapo ni kwa msingi ulio tofauti. Nazo zitatekeleza huduma zao hizi kwa ajili ya watu wote kwa namna inayozidi kuleta mafanikio kwa kadiri ushirikiano kati yao unavyozidi kusitawishwa, na kulingana na mazingira ya mahali na wakati. Binadamu hafungwi katika mipaka ya dunia hii tu, bali, akiishi katika historia ya kibinadamu, huhifadhi kikamilifu wito wake wa milele. Na Kanisa, lenye msingi wake katika upendo wa Mkombozi, linachangia uenezaji wa haki na upendo katika kila taifa na kati ya mataifa yote. Nalo huhubiri ukweli wa kiinjili na kuziangaza fani zote za utendaji wa kibinadamu kwa mafundisho yake na kwa ushuhuda unaotolewa na wakristo. Na hivyo, linaheshimu na kuhamasisha pia uhuru wa kisiasa na uwajibikaji wa raia.
 
Mitume pamoja na waandamizi na wasaidizi wao, huku wakitumwa kuwahubiria wanadamu Kristo, Mwokozi wa ulimwengu, katika kutekeleza utume wao wanautegemea uweza wa Mungu, ambao mara nyingi sana hudhihirisha nguvu ya Injili katika udhaifu wa mashahidi [wake]. Na wale wote wanaojitolea katika utumishi wa Neno la Mungu, lazima watumie njia na mbinu maalum za Injili ambazo zinahitilafiana katika sehemu nyingi na mbinu maalum za mji wa dunia hii ( terrenae civitatis).

Ni kweli kwamba mambo ya dunia na yale ambayo, katika hali ya kibinadamu, yanavuka mipaka ya ulimwengu huu, yameunganika kiundani. Na Kanisa lenyewe linatumia mambo ya dunia kwa kiasi kitakiwacho na utume wake. Lakini, hata hivyo haliweki tumaini lake katika fadhili (privilegiis) linazopewa toka serikalini. Tena, litayaacha matumizi ya haki kadhaa lilizozipata kwa halali pale ambapo litaona kuwa matumizi hayo yanaleta mashaka juu ya unyofu wa ushuhuda wake au pale ambapo mazingira mapya yanadai utaratibu tofauti. Lakini daima na popote iwe haki ya Kanisa kuihubiri imani kwa uhuru wa kweli na kutoa mafundisho yake kuhusu jamii. Tena iwe haki yake kutekeleza utume wake kati ya wanadamu bila vizuizi na kutoa hukumu zake za kimaadili, hata juu ya masuala yahusuyo utaratibu wa kisiasa wakati jambo hilo linatakiwa na haki za msingi za binadamu pamoja na wokovu wa roho za watu. Kanisa litafanya hivi likizitumia njia zote, na zile tu, zinazolingana na Injili na manufaa ya watu wote, kufuatana na tofauti za nyakati na za mazingira.

Nalo Kanisa, ambalo katika uaminifu wake kwa Injili na katika kutekeleza utume wake ulimwenguni, limewajibika kuhamasisha na kukuza yale yote yaliyo kweli, mema na mazuri katika jumuiya ya wanadamu [163], laimarisha amani kati ya watu kwa utukufu wa Mungu [164].

Sura ya Tano

KUHAMASISHA AMANI

NA KUSTAWISHA JUMUIYA YA KIMATAIFA

Utangulizi
 
77. Katika miaka hii yetu mahangaiko na fadhaa vinavyotokana na mwendelezo wa ukali wa vita au na tishio la vita linalotukabili, vinaendelea kuwasumbua sana wanadamu. Na jamii nzima ya kibinadamu imeufikia wakati ulio muhimu sana katika maendeleo ya ukomavu wake. Kwa upande mmoja wanadamu polepole wanaendelea kuungana kati yao na mahali pote wanazidi kuelewa umoja wao. Lakini wakati huohuo watashindwa kutimiza kazi inayotakiwa nao – yaani kujenga ulimwengu uwe wa kiutu kwelikweli kwa watu wote na duniani pote – kama wanadamu wenyewe hawataiongokea amani halisi kwa moyo mpya. Kwa sababu hii habari ya Injili, maadamu inalingana na matarajio na malengo ya juu zaidi ya wanadamu, inang’ara kwa mwangaza mpya inapowatangaza wenye heri wanaofanya amani, “kwa maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mt 5:9).

Kwa hiyo Mtaguso, ukifafanua maumbile halisi na ya juu ya amani, unashutumu ubaya usio na kipimo wa vita (belli immanitate damnata). Tena unadhamiria kuwasihi kwa moyo wote wakristo ili, kwa msaada wa Kristo ambaye ndiye mwenye kufanya amani, washirikiane na watu wote kusudi waasisi kati ya wanadamu amani yenye msingi wake katika haki na upendo. Na hatimaye waandae nyenzo za lazima ili kuifikia amani hiyo.

Maumbile ya amani
 
78. Amani siyo tu kutokuwepo kwa vita, wala haiwezi kupunguzwa kuwa tendo la kudumisha uwiano kati ya nguvu zipinganazo. Tena amani si tu matokeo ya utawala wa mabavu, bali inaitwa kwa usahihi kamili “kazi ya haki” (Isa 32:17). Amani ndilo tunda la utaratibu uliowekwa katika jamii ya wanadamu na Mwasisi wake; nao hauna budi kutekelezwa na wanadamu watarajiao sana haki iliyo kamili zaidi siku kwa siku. Maana manufaa ya pamoja ya wanadamu yameratibiwa katika kiini chake na sheria ya milele, lakini katika mwendelezo wa muda manufaa hayo hubadilika mara kwa mara kuhusu matakwa yake ya kila siku. Ndiyo maana amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali inadaiwa kujengwa siku kwa siku. Aidha, maadam utashi wa binadamu ni dhaifu na umejeruhiwa na dhambi, kuleta amani kunadai siku zote kila mtu azitawale tamaa zake, na serikali ijihusishe katika kulinda amani.
 
Lakini hayo hayatoshi. Hiyo amani haiwezi kupatikana hapa duniani ikiwa mafaa ya watu hayalindwi na kama wanadamu hawawezi kubadilishana kwa kuaminiana na kwa uhuru utajiri wa roho na akili zao. Utashi imara wa kustahi utu wa watu wengine na mataifa mengine, pamoja na uzingativu thabiti wa udugu wa wanadamu ni vya lazima kabisa katika kuijenga amani. Na hivyo amani ndilo pia tunda la upendo unaozidi uwezo wa haki tupu.
 
Amani ya kidunia itokanayo na upendo kwa jirani ni mfano na matokeo ya amani ya Kristo itokayo kwa Mungu Baba. Maana Mwana aliyefanyika mwili, Mfalme wa amani, kwa njia ya msalaba wake amewapatanisha watu wote na Mungu. Naye, akiurudisha umoja wa wote katika taifa moja na mwili mmoja, akaiua chuki mwilini mwake [165] na hatimaye, katika utukufu wa ufufuko wake, akapuliza Roho wa mapendo mioyoni mwa wanadamu.
 
Kwa hiyo wakristo wote wanaitwa kwa nguvu “kuishika kweli katika upendo” (Efe 4:15) na kujiunga na wanadamu waipendayo kwa moyo amani ili kuomba amani na kuitekeleza.

Tukisukumwa na Roho yuleyule, sisi hatuna budi kuwasifu wale ambao, wakikataa utumiaji nguvu (actioni violentae) katika kudai haki zao, huzishikilia zile njia za kujitetea ambazo, kwa vyovyote zinapatikana pia kwa walio wadhaifu zaidi. Ila kazi hii ifanyike pasipo kudhuru haki na wajibu wa watu wengine au wa jumuiya.

Wanadamu, maadam ni wakosefu, wapo na wataendelea daima kuwa chini ya tishio la vita hadi Kristo atakapokuja. Lakini madhali wanaweza kuishinda dhambi wakiunganika katika upendo, wanaweza pia kuushinda utumiaji nguvu hata kulitimiza lile neno la Mungu lisemalo, “Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe” (Isa 2:4).

Ibara ya kwanza

KUEPUKANA NA VITA

 
Kuzuia ukatili wa vita
 
79. Ingawa vita vya hivi karibuni vimeuletea ulimwengu wetu maharibifu makubwa sana ya kimwili na kiroho, hata hivyo mpaka leo kila siku mahali kadha wa kadha pa dunia vita vinaendelea kuleta maangamizi yake. Hasa zaidi, zinapotumika silaha za kisayansi za kila aina, tabia mbaya sana ya vita inatishia kuwapeleka wapinganao kwa uovu unaopita sana ule wa nyakati za nyuma. Aidha mchangamano mkubwa wa hali za dunia ya sasa na msokotano wa mahusiano ya kimataifa huvifanya vita vilivyoanzishwa viendelezwe kwa muda mrefu na kuendeshwa kwa mbinu mpya, zenye kudhuru kwa siri na ziletazo uharibifu. Mara nyingi pia kutumia mbinu za ugaidi kunatazamwa kama namna mpya ya kupiga vita.
 
Mbele ya hali hii ya kujidhili ya binadamu, Mtaguso unadhamiria kukumbusha kwanza thamani isiyofifia ya kanuni asilia ya mataifa na ubora wa sheria zake za msingi na za wote. Dhamiri yenyewe ya binadamu hutangaza sheria hizi kwa uthabiti unaozidi kukua siku kwa siku. Kwa hiyo matendo yapingayo kwa makusudi sheria hizi na pia zile amri zinazoagiza matendo hayo ndiyo jinai; wala utii mtupu hauwezi kabisa kuhesabiwa kama udhuru kwa wale watendao mambo hayo. Miongoni mwa matendo haya ni ya kutajwa kwanza yale yanayoleta maangamizi ya mpangilio kwa taifa zima, nchi au kabila dogo. Na hilo ndilo kosa la jinai ovu sana ambalo lazima lishutumiwe kwa ukali mkubwa; na hauna budi kusifiwa ujasiri wa wale wasioogopa kuwapinga waziwazi hao wanaoyaamuru matendo mabaya namna hii.

Mintarafu vita, yapo maafikiano ya kimataifa yaliyotiwa sahihi na nchi nyingi; nayo hulenga katika kupunguza ukatili wa matendo ya vita na matokeo yake. Maafikiano hayo yanahusu namna ya kuwatendea askari waliojeruhiwa au waliotekwa, na mengineyo kama hayo; nayo lazima yahifadhiwe. Na wote, hasa serikali na wataalamu, wanapaswa kufanya kila jitihada, kadiri ya uwezo wao, ili maafikiano hayo yakamilishwe kusudi yaweze kuzuia makatili ya vita kwa namna ifaayo zaidi na yenye mafanikio. Aidha, inaonekana kuwa jambo la haki kuwepo kwa sheria zinazowashughulikia kiutu wale wanaokataa matumizi ya silaha kwa sababu ya dhamiri zao, lakini wanakubali kutoa aina nyingine ya huduma kwa ajili ya jamii ya wanadamu.

 

Bahati mbaya vita bado havijang’olewa katika maisha ya binadamu. Na pindi hatari ya vita inaendelea kuwako, wala hakuna mamlaka ya kimataifa yenye madaraka na nguvu zinavyotakiwa, basi haitawezekana kuzikatalia serikali haki ya kujitetea kwa halali, pale juhudi zote za usuluhishi wa amani zinapokuwa zimeshindikana. Viongozi wa serikali na wote wanaoshiriki katika uongozi wa dola wamewajibika kulinda usalama wa mataifa waliyokabidhiwa, na kuyakabili masuala muhimu namna hii kwa hisi za uwajibikaji mkubwa. Lakini kitu kimoja ni kutumia silaha kwa kuzitetea haki za mataifa, na kitu kingine tofauti ni kutaka kutawala kwa nguvu juu ya nchi nyingine. Tena nguvu na zana za vita hazihalalishi kila matumizi yake ya kijeshi na kisiasa; wala si kila tendo kati ya wapiganaji linakuwa halali, ikiwa vita, bahati mbaya, vimekwisha zuka.

Aidha, wale wanaoapishwa kutumikia nchi yao katika jeshi wajitambue kama wahudumu wa usalama na uhuru wa mataifa. Nao, wakitekeleza wajibu wao kwa unyofu, wanachangia kweli katika kuimarisha amani.

Vita kamili
 
80. Maendeleo ya silaha za kisayansi yameongeza sana ubaya na ukatili wa vita. Maana matendo ya kivita, yakiendeshwa kwa vyombo hivyo, yaweza kuleta maangamizi makubwa sana na ya vitu vyote; nayo yanapita kabisa haki ya kujitetea kwa halali ( legitimae defensionis). Tena, kama silaha za namna hii zinazopatikana katika ghala za mataifa yenye uwezo zingetumika bila kizuizi, uangamizi kamili wa pande zote zipiganazo ungetokea. Aidha, matumizi ya silaha hizo yangesababisha uharibifu mwingi duniani kote na matokeo yaletayo vifo vingi.

Mambo haya yote yanatulazimu kulizingatia suala la vita kwa mtazamo mpya kabisa[166]. Wanadamu wa nyakati hizi wajue kuwa watapaswa kutoa hesabu kamili ya matendo yao ya vita, kwa maana namna vizazi vijavyo vitakavyoendelea itayategemea kwa vikubwa maamuzi yao ya leo.

Baada ya kuzingatia vema mambo haya, Mtaguso Mkuu huu unajiunga na Mababa Watakatifu wa nyakati zetu katika kulaumu (condemnationes) vita kamili[167], na hivyo unatamka haya yafuatayo:

Kila tendo la vita linalokusudia kuangamiza ovyo miji mizima au maeneo makubwa pamoja na wakazi wake, ni kosa dhidi ya Mungu na wanadamu; nalo linastahili kulaumiwa vikali na bila kusita.

Hatari maalum ya vita vya kisasa ni kwamba vita hivyo vinawapa wale wenye silaha za kisayansi kali zaidi fursa ya kutenda mauaji hayo; na vilevile vinaanzisha mfululizo wa mambo usioweza kusimamishwa na unaosukuma utashi wa watu kuyafikia maamuzi yenye ukatili mkubwa. Basi, ili mambo hayo yasije yakatokea tena wakati ujao, Maaskofu wa ulimwengu mzima waliokutanika hapa wanawasihi watu wote, hasa viongozi wa serikali na wakuu wa majeshi, wazingatie daima mbele ya Mungu na wanadamu uzito mkubwa sana wa wajibu wao.

Mashindano ya kujipatia silaha
 
81. Ni kweli kwamba silaha za kisayansi hazilimbikizwi tu kwa lengo la kutumiwa wakati wa vita tu. Maana inadhaniwa kuwa uwezo imara wa taifa fulani wa kujikinga unautegemea uwezekano wake wa kuwavamia mara maadui wanaolishambulia. Hivyo, limbikizo la silaha la namna hii linaloongezeka mwaka hadi mwaka linaweza kuwashawishi kwa njia hii isiyo kawaida maadui waondokane na mipango yao. Na walio wengi wanaitazama mbinu hii kama njia yenye mafanikio zaidi na inayodumisha amani kwa kiasi fulani kati ya mataifa.

Lakini maoni yoyote yale mtu aliyo nayo juu ya mbinu hii [ya kuwashawishi maadui wasianzishe vita], basi wanadamu waelewe kuwa mashindano ya kujipatia silaha (cursum ad arma apparanda) yanayofanywa na mataifa mengi, siyo njia salama ya kulinda amani iliyo imara. Tena hali ya usawa wa nguvu (aequilibrium) itokanayo nayo mashindano haiwezi kutazamwa kama hali ya amani iliyo ya kweli na ya kudumu. Maana, sababu zinazozusha vita haziondolewi na ulimbikizaji huo, kinyume chake zinaweza kuongezeka polepole. Na wakati ambapo fedha nyingi sana zinatumika kwa kujipatia daima silaha zilizo mpya, ndipo haitawezekana kutoa msaada maridhawa kwa umaskini mkubwa wa dunia ya sasa. Na hatimaye, badala ya kusuluhisha kimsingi migogoro kati ya mataifa, hiyo itazagaa pia mahali pengine ulimwenguni. Hivyo, yatupasa tutafute njia mpya, tukianzia na matengenezo ya roho za watu, ili kikwazo hicho [cha vita] kiweze kuondolewa, na ulimwengu, ukiisha okolewa na fadhaa inayouelemea, upate kurudishiwa amani ya kweli.

Kwa sababu hiyo ni lazima kutangaza tena kwamba mashindano ya kujipatia silaha ni kidonda kimojawapo kibaya zaidi katika jumuiya ya wanadamu; nayo yanawadhuru maskini kwa namna isiyovumilika. Na tishio kubwa ndilo kwamba mashindano hayo, ikiwa yataendelea, siku moja yatasababisha mauaji yale yote ambayo zana zake zimeshaanza kuyaandaa.

Basi, tukionywa na misiba iliyosababishwa na wanadamu hapo nyuma, tuchukue nafasi hii ya shwari tuliyojaliwa na Mungu ili tuelewe vizuri zaidi wajibu wetu na kutafuta njia ya kusuluhisha migogoro yetu kwa namna inayomstahili zaidi binadamu. Maongozi ya Mungu yanatudai kwa mkazo kuwa sisi tujiokoe na utumwa wa kale wa vita. Nasi, tukikataa kufanya juhudi hii, hatujui njia hii potovu tuliyoishika itatufikisha wapi.

Kulaumu kabisa vita. Juhudi za kimataifa ili vita viepukwe

82. Ni dhahiri kwamba tunapaswa kujitahidi kwa kila bidii ili kukiandaa kipindi ambapo, kwa mapatano ya kimataifa, itawezekana kuharimisha kabisa kila aina ya vita. Bila shaka jambo hilo hudai halmashauri ya kiulimwengu yenye mamlaka iundwe; nayo ikubaliwe na mataifa yote na iwe na madaraka na enzi ya kulinda nchi zote katika usalama, utekelezaji wa haki, na heshima ya sheria. Lakini, kabla ya halmashauri hii inayotarajiwa haijapata kuundwa, ni lazima mabaraza ya kimataifa yaliyopo yajishughulishe kwa bidii zote kutafuta njia zifaazo zaidi ili kuleta usalama kwa wote. Amani haina budi itokane na mahusiano yenye uaminifu kati ya mataifa kuliko kulazimishwa kwa tishio la silaha. Hivyo watu wote hupaswa kufanya bidii ili hatimaye mashindano ya kujipatia silaha yakomeshwe, na mpunguzo wa zana za vita uanzishwe kimatendo. Nao uendelezwe si kwa upande mmoja tu, bali sawasawa kwa pande zote, juu ya msingi wa maafikiano ya pamoja na kwa kuhakikishwa kwa udhamini wa kweli na wenye nguvu[168].

Kwa sasa hivi yasihesabiwe pungufu majaribio yaliyokwisha fanywa na yanayoendelea kufanywa ili kuondosha hatari ya vita. Na zaidi watiwe moyo walio wengi wenye mapenzi mema ambao, ijapo wanaelemewa na wajibu mzito wa madaraka yao makuu, hata hivyo hujishughulisha kuondosha vita wanavyovichukia, ingawa hawawezi kupuuza ugumu na upana wa masuala yaliyopo. Inabidi kumwelekezea Mungu maombi bila kukoma ili awajalie watu hao nguvu ya kushika kazi hii kwa uthabiti na kuitimiza kwa ushujaa. Nayo ni kazi iliyojaa upendo mkubwa kwa wanadamu na ambayo kwayo amani hujengwa kwa uhodari. Lakini kazi hii [iletayo amani] hudai wenye kujishughulisha nayo wapanue fikra zao na mioyo yao hata kuvuka mipaka ya nchi zao wenyewe. Tena hudai kuondokana na kila aina ya utaifa pamoja na kila tamaa ya kutawala juu ya nchi nyingine. Nao waishughulikiao amani walishe hisi za heshima kwa wanadamu wote ambao wanaelekea kuunda kwa bidii nyingi umoja mkubwa zaidi.

Mashauriano ( perscrutationes) na mikutano ya kimataifa mintarafu masuala yahusuyo amani na ondoleo la silaha imekwisha anza kufanyika kwa juhudi na bila kuchoka. Nayo haina budi kutazamwa kama hatua za kwanza kuuelekea usuluhishi wa hoja nzito namna hii; tena kwa wakati ujao itapaswa kuhamasishwa kwa mkazo na bidii nyingi zaidi ili mafanikio yapatikane. Lakini wanadamu wajihadhari na tabia ya kuzitegemea juhudi za baadhi ya watu, pasipo kuzingatia hisia zao wenyewe. Maana viongozi wa mataifa, ambao ndio wadhamini wa manufaa ya wote katika nchi zao na pia wenye kuyahamasisha manufaa ya wanadamu wote, huyategemea kwa vikubwa maoni na hisia za makutano. Maana ni bure wao wajibidishe kuijenga amani kwa uhodari iwapo hisia za uadui, dharau, mashaka, chuki ya kikabila na itikadi kaidi vinaendelea kuwatenga watu na kuwaweka katika hali ya uadui kati yao. Tokea hapo inaonekana kwamba ni jambo la lazima na la haraka kuzilea upya roho za watu na kutoa maelekezo mapya katika maoni ya umma. Nao wanaoyashughulikia malezi, hasa ya vijana, pamoja na wale wanaochangia katika kujenga maoni ya umma wazingatie kama wajibu wao muhimu sana kazi ya kupenyeza mioyoni mwa watu hisia mpya ziletazo amani. Aidha, kila mmoja wetu hana budi kujitahidi kuugeuza moyo wake, akizingatia ulimwengu mzima na pia majukumu yale tunayoweza kutimiza kwa pamoja ili kuiongoza jamii yetu katika kikomo kilicho kizuri zaidi.

Wala tumaini la uongo lisitudanganye. Maana kama maafikiano ya amani ya kiulimwengu yaliyo imara na manyofu hayatafanyika; tena ikiwa watu hawataacha kila chuki na uadui, basi wanadamu wote ambao, ijapo wameyafikia magunduzi ya ajabu katika uwanja wa sayansi, wapo tayari katika hatari kubwa, pengine wataifikia kwa uchungu saa ile ambayo hawataionja amani nyingine, ila amani yenye shari. Lakini hata hivyo Kanisa la Kristo, lililowekwa katikati ya fadhaa za wakati huo, linapoeleza matatizo hayo, haliachi kushikilia tumaini lililo imara. Nalo Kanisa linadhamiria daima na daima kuwaelezea [wanadamu wa] nyakati zetu ujumbe wa Mtume [Paulo], wawe wanaupokea ama wanaukataa kama kitu kisichofaa, usemao, “Wakati uliokubalika ndio sasa” ili wageuze mioyo yao; “Tazama, siku za wokovu ndizo sasa”[169].

Ibara ya Pili

KUJENGA JUMUIYA YA KIMATAIFA

Sababu za magomvi na tiba yake

83. Ujenzi wa amani unadai, kabla ya yote, zing’olewe sababu za fitina kati ya wanadamu zizushazo vita, kuanzia na ukosefu wa haki. Sababu nyingi za magomvi hutokana na tofauti tele zilizopo katika hali ya kiuchumi pamoja na kukawia katika kushughulikia tiba yake inayohitajika. Tena sababu nyinginezo huzaliwa kutoka katika roho ya utawala na dharau ya watu; na hatimaye, tukidokeza zile sababu zilizofichika zaidi, hutokana na wivu wa kibinadamu, mashaka, kiburi na tamaa nyingine za kiubinafsi. Maadamu wanadamu hawawezi kuvumilia machafuko mengi namna hii, basi hutokea kuwa ulimwengu, hata pasipo vita, unaendelea kutawaliwa na mapigano na matendo ya kijeuri kati ya wanadamu. Basi, maovu hayohayo yanapatikana pia katika mahusiano kati ya mataifa. Kwa hiyo, ili kushinda na kubananga maovu haya; tena ili kukomesha matumizi mabaya ya nguvu, ni sharti kabisa taasisi za kimataifa zizidi kushirikiana katika kazi yao na kuwasiliana kwa mpango ulio imara zaidi. Kisha ni lazima kuchochea bila kuchoka uundaji wa vyombo, au mabaraza (organismorum), vya kufaa kwa minajili ya kuhamasisha amani.

Jumuiya ya mataifa na taasisi za kimataifa

84. Siku za leo mahusiano ya kutegemezana kati ya raia wote na baina ya mataifa ya ulimwengu mzima yanazidi kuongezeka na kufungamanisha watu wao kwa wao. Tena kutafuta na kupata manufaa ya wote duniani kwa mafanikio mazuri zaidi kunazidi kudai kuwa jumuiya ya mataifa ijipangie utaratibu ulinganao na majukumu yake ya kisasa, zikizingatiwa hasa nchi zile nyingi zinazoelemewa hadi leo na hali ya unyonge usiovumulika.

Ili kuyafikia malengo haya, taasisi za jumuiya ya kimataifa lazima yakidhi mahitaji mbalimbali ya watu, kila moja kwa nafasi yake, katika uwanja wa maisha ya kijamii, yaani mintarafu chakula, afya, elimu na kazi; kadhalika katika hali za pekee zinazojitokeza hapa na pale, kama vile sharti la kuhamasisha usitawi wa maendeleo kwa ujumla ya nchi zinazoendelea; tena sharti la kuwatuliza maafa ya wakimbizi waliotawanyika duniani pote. Na hatimaye sharti la kuwasaidia wahamiaji na familia zao.

Taasisi za kimataifa, za kiulimwengu na za kinchi zilizokwisha undwa zimetoa huduma nyingi kwa watu. Nayo ndilo tunda la jitihada za kwanza zilizofanyika ili kuiweka misingi ya kimataifa ya jumuiya nzima ya wanadamu kwa kusudi la kuyatatua masuala mazito zaidi ya siku za leo. Tena ili kuhamasisha maendeleo popote duniani na kuzuia vita vya kila aina. Katika nyanja hizo zote Kanisa linaifurahia roho ya udugu halisi inayostawi kati ya wakristo na wasio wakristo; roho ambayo hukuza bidii zinazolenga katika kutuliza unyonge mkubwa uliopo duniani.

Ushirikiano wa kimataifa katika mambo ya uchumi
 
85. Mshikamano wa siku hizi kati ya watu unadai uwepo pia ushirikiano wa kimataifa mkubwa zaidi katika uwanja wa uchumi. Maana, ikiwa karibu nchi zote zimekwisha pata uhuru wa kisiasa, hata hivyo ziko mbali na kujipatia uhuru kutoka katika hali ya kuwa na tofauti kubwa mno na toka katika kila aina ya kutegemea kusikofaa, na kwamba zote ziweze kuikimbia hatari ya matatizo makubwa yaliyopo nchini.
 
Maendeleo ya nchi fulani hutegemea misaada ya watu na ya fedha. Ni lazima kuwaandaa raia wa kila nchi kwa njia ya elimu na mafunzo ya kikazi ili waweze kushika majukumu mbalimbali katika maisha ya kiuchumi na kijamii. Basi, kwa lengo hilo, unatakiwa msaada wa mafundi watokao ng’ambo ambao, pale wanapofanya kazi yao, wawe na tabia ya wasaidizi na washiriki, wala si ya watawala. Tena pasipo mabadiliko ya ndani katika mtindo wa kuendesha uchumi wa kimataifa siku za leo, nchi zinazoendelea hazitaweza kamwe kupata misaada yakinifu. Aidha, misaada mingine ya ziada lazima itolewe kwao toka kwa nchi zenye maendeleo kwa namna ama ya zawadi, au mikopo au vitegauchumi. Na misaada hiyo kwa upande mmoja ifanyike kwa ufadhili, wala si kwa uchoyo; nayo, kwa upande mwingine, ipokelewe kwa unyofu kamili.

Ili kuunda utaratibu halisi wa kiuchumi wa kiulimwengu, itapaswa kuacha tamaa ya faida iliyo kubwa mno, tena tamaa ya kiutaifa na ya utawala wa kisiasa. Na hatimaye itabidi kufuta mipango ya mkakati ya kijeshi na njama za kushamirisha na kutawaza kwa nguvu itikadi kadha wa kadha. Mifumo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii hupendekezwa; basi, inatarajiwa kuwa wataalamu wataweza kupata ndani yake msingi wa maisha safi ya kiuchumi ufaao kwa dunia nzima. Na kazi hii itasahilishwa ikiwa kila mmoja ataziacha chuki bila sababu (praeiudicia) na atajiweka tayari kwa hiari kwa ajili ya mazungumzo, na pasipo udanganyifu.

 
Kanuni kadha wa kadha zenye kufaa

86. Kwa kuufuatilia ushirikiano huo, kanuni hizi zifuatazo zimeonekana kufaa:

 
 

 
a) Mataifa yanayoendelea yalenge hasa katika kuwakamilisha kiutu raia zake. Na yatekeleze wazi wajibu huo na kwa nia imara; na lengo hilo liwe kikomo cha maendeleo yake. Kadhalika [haya mataifa] yakumbuke kuwa maendeleo hayo huasilika kwanza na kupata nguvu yake katika kazi na maarifa ya watu wake yenyewe, hasa kwa sababu yanategemea kabla ya yote si misaada ya nje tu, bali zaidi ustawishaji mkamilifu wa rasilimali zilizomo ndani. Na hatimaye maendeleo haya hayana budi kutegemea busara na desturi za wananchi, ambazo nazo hupaswa kukuzwa.
 
Mintarafu suala hilo, wenye uwezo mkubwa zaidi wa kuwaathiri wengine lazima watoe mfano bora.
 
b) Ni wajibu mzito sana wa mataifa yaliyoendelea kuzisaidia nchi zinazoendelea kusudi zitekeleze kazi zao zilizotajwa hapo juu. Kwa lengo hili mataifa yaliyoendelea hayana budi kufanya kwa hiari marekebisho ya kiroho na kimatendo ( mentales et materiales), yanayodaiwa ili kuunda ushirikiano huo wa kiulimwengu.
 
Hivyo, katika biashara mataifa yaliyoendelea yanapaswa kuyazingatia manufaa ya nchi zilizo nyonge na maskini zaidi. Maana nchi hizi zinaegemea mapato yanayotokana na uuzaji wa bidhaa zao kusudi zipate zenyewe riziki yao.
 
c) Ni wajibu wa jumuiya ya kimataifa kuratibu na kuchochea maendeleo, lakini kwa kufuatilia ufanisi timamu na haki kamili katika ugawaji wa rasilimali zinazowekwa kwa madhumuni hayo. Tena ni wajibu wake kuratibisha shughuli za kiuchumi duniani pote kwa mujibu wa masharti ya haki, ila pasipo kuhalifu kanuni ya auni ( principio subsidiarietatis).

Tena ziundwe taasisi maalum na zenye kufaa kwa minajili ya kuhamasisha na kuratibu biashara ya kimataifa, hasa na nchi zenye maendeleo hafifu. Na taasisi hizo zilenge pia katika kufidia matatizo yatokanayo na tofauti kubwa mno ya uweza iliyopo baina ya mataifa. Na hatimaye utaratibu wa mtindo huo hauna budi kuzishirikisha nchi zilizomo katika njia ya maendeleo rasilimali zinazohitajika, pamoja na msaada wa kiufundi, kitamaduni na kifedha, ili kusudi zipate ustawi maridhawa wa uchumi wao.

d) Mara nyingi kazi inayotakiwa kufanywa kwa haraka ndiko kutengeneza upya miundo ya kiuchumi na kijamii. Lakini inapaswa kujitahadhari na fumbuzi za kistadi ambazo hazijakomaa vizuri; na hasa zile ambazo, pale zimleteapo binadamu manufaa ya kimwili, ndipo hupinga maumbile yake na manufaa yake ya kiroho. Maana “Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu” (Mt 4:4). Aidha, kila tawi la familia ya kibinadamu lina chochote, ndani yake na ndani ya mapokeo yake, cha ile hazina ya kiroho ambayo Mungu ameukabidhi ubinadamu, ijapokuwa wengi hawaelewi ni asili ipi inakotoka.
 
Ushirikiano wa kimataifa kuhusu ongezeko la watu
 
87. Ushirikiano wa kimataifa ni wa lazima hususan yanapotazamwa mataifa ambayo siku hizi, mara nyingi, yanasongwa kwa namna ya pekee na matatizo yatokanayo na ongezeko la kasi la idadi ya watu, pamoja na shida nyingine nyingi. Hivyo ni dharura na lazima, kwa ushirikiano kamili na wenye nguvu wa wote, hasa wa nchi tajiri zaidi, kubuni mbinu za kuyapata yale yanayohitajika kwa ajili ya riziki na elimu ya kufaa ya kila mtu; na hatimaye kuishirikisha jamii nzima ya wanadamu mambo hayo. Mataifa mengi yangeweza kuiendeleza sana hali yao ya maisha ikiwa yangefunzwa ipasavyo ili kuzigeuza maarifa za zamani za kilimo na kuzishikilia mbinu za uzalishaji mali zilizo mpya na za kiteknolojia. Ila [yatekeleze mageuzo hayo] kwa utaratibu na kwa bidii ya kuyalinganisha na mazingira yao yenyewe; tena wakati huohuo yatengeneze mfumo wa kijamii ulio bora zaidi na kuutekeleza mgawanyo wa ardhi ulio wa haki zaidi.
 
Na serikali mbalimbali hakika zina haki na wajibu zihusuzo matatizo ya idadi ya watu katika nchi zao; ila zisivuke mipaka ya madaraka yao; kwa mfano mintarafu sheria za kijamii na kifamilia, tena uhamaji toka shambani kuelekea mjini; au hatimaye mintarafu upashanaji habari kuhusu hali na mahitaji ya nchi. Siku hizi watu wanafadhaishwa sana rohoni na matatizo kama hayo. Hivyo wakatoliki wenye ustadi kuhusu masuala hayo yote wanatarajiwa waendeleze kwa bidii utafiti na juhudi zao na kuzikomaza zaidi, hasa katika vyuo vikuu.

Aidha, wengi hukazia kuwa ongezeko la watu duniani, au walau katika baadhi ya nchi, halina budi kupunguzwa kabisa kwa kila njia na kwa mbinu yoyote ile chini ya mamlaka ya serikali; hivyo basi, Mtaguso unawahimiza wote waepukane na fumbuzi zipinganazo sheria za kimaadili, ziwe zinahamasishwa ama kuwekwa kwa shuruti hadharani au faraghani. Maana, kwa nguvu ya haki isiyoachanika (inalienabile) ya mtu kufunga ndoa na kuzaa watoto, uamuzi kuhusu idadi ya watoto wa kuzawa ni juu ya upambanuzi mnyofu wa wazazi; wala kwa vyovyote vile hauwezi kuachiwa upambanuzi wa serikali. Nao upambanuzi wa wazazi huitegemea dhamiri iliyokomaa vizuri; hivyo ni muhimu sana kuwapatia watu wote nyenzo za kujikomaza katika uwajibikaji mnyofu unaowafaa kabisa wanadamu, kwa mujibu wa sheria ya Mungu na kwa kuyazingatia mazingira ya mahali na nyakati. Na hayo yote hudai popote pale maendeleo ya hali ya malezi na ya kijamii; na hasa yatakiwa malezi ya kidini au walau malezi manyofu ya kimaadili. Vilevile watu wataarifiwe ipasavyo kuhusu maendeleo ya kisayansi katika uwanja wa utafiti wa zile mbinu zitakazoweza kuwasaidia wazazi mintarafu udhibiti wa mpango wa uzazi. Ila kwanza ithibitishwe kwa bidii uthabiti wa hizo mbinu na uhakikishwe uhalali wake wa kimaadili.

Jukumu la wakristo katika kutoa misaada
 
88. Kwa hiari na kwa moyo wote wakristo washiriki katika kujenga utaratibu wa kimataifa wenye kuheshimu uhuru ulio halali na udugu wa kirafiki wa watu wote. Nalo ni la maana zaidi kutokana na kwamba sehemu kubwa zaidi ya dunia huuhangaikia umaskini mkubwa sana kiasi kwamba Kristo mwenyewe anaonekana kuulilia mapendo ya wanafunzi wake kwa midomo ya fukara. Na kikwazo hiki kiepukwe: kwamba mataifa mengine, ambayo wakaazi wake karibu wote hujiita wakristo, yamejaa wingi wa mali, na wakati huohuo mataifa mengine yanakosa mahitaji muhimu kwa maisha na yanahangaika kwa njaa, magonjwa na unyonge wa kila aina. Maana roho ya ufukara na mapendo ndio utukufu na ushuhuda wa Kanisa la Kristo.
 
Basi, wasifiwe na kutiwa moyo wale wakristo, hasa vijana, ambao kwa hiari hujitolea kuwasaidia watu wengine na nchi nyingine. Na zaidi, ni jukumu la Taifa lote la Mungu, kwa kufuata neno na mfano wa maaskofu wake, kuunyanyua unyonge wa nyakati zetu, kufuatana na uwezo wake; yaani kwa kutoa si tu kutoka kinachozidi, bali pia kilicho cha lazima, kufuatana na desturi za Kanisa za tangu zamani.

Michango na ugawaji wa misaada mbalimbali inabidi vifanyike kadiri ya utaratibu wa kijimbo, kitaifa na kimataifa; ila si lazima vipangwe kwa mtindo mmoja tu na usiobadilika. Na pale iwezekanapo, vitekelezwe kwa kazi ya pamoja ya wakatoliki pamoja na ndugu wakristo wengine. Maana, roho ya upendo haipingani hata kidogo na utekelezaji wenye busara na utaratibu wa shughuli za kijamii na kifadhili; bali, kinyume chake, inaudai. Hivyo ni lazima wale watakao kujibidisha katika kuzitumikia nchi zinazoendelea, wapewe mafunzo yafaayo katika taasisi zenye utaalamu.

Uwepo wenye kufaa wa Kanisa katika jumuiya ya kimataifa
 
89. Kanisa, kwa nguvu ya utume wake wa kimungu, huhubiri Injili na kugawa hazina za neema kwa watu wote. Hivyo, hutoa mchango wake katika kuimarisha amani popote pale duniani, likiweka ujuzi wa sheria za Mungu na ya maumbile uwe msingi thabiti wa ushirikiano wa kidugu kati ya wanadamu na kati ya mataifa. Ndiyo sababu Kanisa linapasika kabisa kuwepo ndani ya jumuiya yenyewe ya mataifa, ili liwaamshe na kuwahimiza watu wasaidiane wao kwa wao. Nalo litafanyika kwa njia ya taasisi zake zenye madaraka rasmi na pia kwa ushirikiano kamili na mnyofu wa wakristo wote, likichochewa na hamu ile moja ya kuwatumikia watu wote.

Ili kufikia lengo hilo kwa namna inayofaa zaidi, waamini, wakielewa jukumu lao la kiutu na kijamii, watapaswa kufanya bidii ili kuiamsha nia ya kushirikiana kwa uhodari na jumuiya ya kimataifa, kuanzia na mazingira yao wenyewe wanamoishi. Na juhudi ya pekee ifanyike kusudi vijana wafunzwe kuhusu suala hilo katika malezi yao ya kidini na kiraia.

Ushirikiano wa wakristo katika taasisi za kimataifa
 
90. Hakika mtindo mmojawapo ulio bora wa wakristo kujihusisha na shughuli za kimataifa ndiyo kazi ifanyikayo kwa kushiriki, iwe kibinafsi ama kijumuiya, ndani ya taasisi zilizokwisha undwa au zinazotarajiwa kuundwa; nayo kazi idhamirie kuhamasisha ushirikiano kati ya mataifa. Aidha, vyama mbalimbali vya kikatoliki vya kimataifa huweza pia kuutumikia kwa njia nyingi ujenzi wa jumuiya ya kimataifa katika amani na udugu. Ndiyo maana itabidi kuviimarisha [hivyo vyama] kwa kuongeza idadi ya wanachama wenye malezi mazuri. Nalo litekelezwe kwa kutumia misaada inayohitajika na pia kwa kuratibisha nguvu zake kwa namna ya kufaa. Maana siku hizi mafanikio katika utendaji, na ulazima wa dialogia, vinadai shughuli zifanyike kwa kushirikiana pamoja. Na licha ya hayo, vyama vya namna hii hunufaisha kwa vikubwa katika kutia mioyoni mwa watu zile hisia za kiulimwengu zinazowafaa sana wakatoliki; tena husaidia sana katika kuamsha katika dhamiri ya watu [umaana wa] ushirikiano na uwajibikaji wa kiulimwengu.

Na hatimaye ni tumaini kwamba wakatoliki watapania ushirikiano wa kimatendo na wenye kufaa na ndugu waliojitenga, ambao nao hukiri mapendo ya kiinjili; tena na wanadamu wote wanaoitamani amani ya kweli. Basi, kwa njia hizi watautimiza iwapasavyo wajibu wao ndani ya jumuiya ya kimataifa.

 
Aidha, Mtaguso huyazingatia mabalaa makubwa sana ambayo bado yawataabisha sehemu kubwa zaidi ya jamii ya wanadamu; hivyo hudhania kuwa yafaa sana kuunda taasisi fulani ya kiulimwengu ya Kanisa ili kuchochea popote pale haki na upendo wa Kristo kwa maskini. Nayo taasisi itakusudia kuchochea jumuiya ya wakatoliki ili ihamasishe maendeleo ya nchi zenye kuhitaji na haki ya kijamii kati ya mataifa.

TAMATI

 
Jukumu la kila mwamini na la Makanisa mahalia
 
91. Mambo yote yanayoelezwa na Sinodi hii Takatifu ni sehemu ya hazina ya mafundisho ya Kanisa; nayo hudhamiria kuwasaidia watu wote wa nyakati zetu, wale wanaomwamini Mungu na wale wasiomtambua wazi; ili kusudi hao wote wagundue kinagaubaga madai ya wito wao mzima na hivyo wafanye kazi ili kulinganisha zaidi dunia hii na hadhi kuu ya binadamu. Tena ili kusudi wapanie udugu wa wote na wenye asili ya juu. Na hatimaye waweze kuiitikia mialiko ya dharura zaidi ya siku za leo, kwa msukumo wa upendo na kwa bidii nyingi na za pamoja.

Lakini kwa makusudi, katika vipengele vyake vingi, maelezo hayo yametolewa kwa mtazamo wa kijumla, kwa sababu ya utofauti mkubwa sana wa mazingira mbalimbali na wa mitindo ya utamaduni uliopo katika dunia nzima. Na zaidi, ingawa hapa yameelezwa mafundisho yaliyokwisha pokelewa katika Kanisa, haya yatapaswa kuendelezwa na kupanuliwa, madhali mara nyingi yahusu mada zenye kubadilikabadilika. Twategemea kuwa yale mengi tuliyoyaeleza katika msingi wa Neno la Mungu na wa roho ya Injili yataweza kutoa msaada wenye kufaa kwa watu wote; na hasa baada ya wakristo kutekeleza jukumu la kuyalinganisha hayo (adaptatio) na hali ya mataifa na tamaduni mbalimbali. Nayo wayafanye wakiongozwa na Wachungaji wao.

Dialogia kati ya wanadamu wote

92. Kanisa lilipewa utume wa kuuangaza ulimwengu mzima kwa ujumbe wa kiinjili, tena wa kuwakusanya katika Roho mmoja wanadamu wote wa kila taifa, kabila na utamaduni; basi, kwa nguvu ya utume huo Kanisa linakuwa ishara ya ule udugu unaowezesha na kuimarisha dialogia iliyo nyofu.

Suala hilo ladai kwamba kuanzia katika Kanisa lenyewe tuhamasishe kuheshimiana, staha na uelewano; tukitambua kila tofauti iliyo halali iliyopo, kusudi tuanzishe dialogia inayozidi kuwa ya kina kati yao wote wanaounda lile taifa moja la Mungu; wawe wachungaji au waamini wakristo wengine. Maana, yana nguvu zaidi yale yanayowaunganisha waamini kuliko yanayowatenganisha; kuwepo umoja katika mambo ya lazima, uhuru katika yale yasiyo hakika, na mapendo katika yote[170].

Aidha, mawazo yetu yanawaendea ndugu wasioishi bado katika ushirika kamili na sisi, pamoja na jumuiya zao; lakini twaunganika nao katika kumkiri [Mungu] Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, tena katika kiungo cha mapendo; tukikumbuka kuwa siku za leo umoja wa wakristo unatarajiwa na kutamaniwa hata na wengi wasiomwamini Kristo. Maana, kadiri umoja huo utakavyokithiri katika ukweli na upendo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kwa kiasi hichohicho utakuwa taraja la umoja na amani kwa ulimwengu mzima. Kwa hiyo, tuunganishe nguvu zetu na kutumia mitindo na mbinu vinavyofaa zaidi na zaidi katika nyakati za sasa ili kulifikilia vizuri lengo bora namna hii; hivyo, kwa kuifuata zaidi na zaidi Injili, tujitahidi kushirikiana kidugu katika kuitumikia familia ya wanadamu inayoitwa kugeuka kuwa familia ya wana wa Mungu, katika Kristo.
 
Na hatimaye tuwaelekezee mawazo yetu wote wanaomwamini Mungu ambao huzitunza tunu za kidini na kiutu katika mapokeo yao; tujitakie kuwa dialogia wazi iweze kutuhimiza kupokea kwa uaminifu misukumo ya Roho Mtakatifu na kuitimiliza kwa ari.

Hamu ya kuianzisha dialogia inayoongozwa tu na upendo kwa ajili ya ukweli na kuendelezwa kwa utaratibu wa kufaa, kwa upande wetu haimkatai mtu awaye yote: [haiwakatai] wenye kuziheshimu tunu bora za kibinadamu, wajapokuwa hawamtambui bado Mtunzi wake; wala [haiwakatai] wenye kupinga Kanisa na kulidhulumu kwa namna mbalimbali. Madhali Mungu Baba ndiye chanzo na kikomo cha wote, basi sote huitwa kuwa ndugu. Ndiyo maana twaitwa kuushiriki wito uo huo wa kibinadamu na kimungu pasipo ujeuri wala udanganyifu; nasi twaweza na twapaswa kutenda kazi pamoja ili kuujenga ulimwengu katika amani ya kweli.

Ulimwengu unaotakiwa kujengwa na kufikishiwa kikomo chake

93. Wakristo wakiyakumbuka maneno ya Bwana, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yn 13:35), wasikitamani chochote kwa shauku kuliko kuwatumikia wanadamu wa ulimwengu wa sasa kwa ukarimu na ufanisi unaozidi siku kwa siku. Kwa hiyo, waambatane kiaminifu na Injili na kuchota nguvu kutoka kwake; na pia waunganike nao wote wanaopenda na kuitafuta haki; maana wamebeba wajibu mkubwa sana hapa duniani: kuhusu huo watapasika kutoa hesabu kwa Yule atakayewahukumu watu wote siku ya mwisho. Maana si wote wasemao, “Bwana, Bwana”, wataingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni wao wafanyao mapenzi ya [Mungu] Baba[171] na kunyosha mkono kwa kutenda kazi. Kwa sababu [Mungu] Baba hutaka sisi katika wanadamu wote tumtambue na kumpenda kwa manufaa – yaani kwa neno na tendo – ndugu yetu Kristo; na hivyo tutoe ushuhuda kwa ukweli na kuwashirikisha wengine fumbo la upendo wa Baba wa mbinguni. Nasi, tukifanya hivyo, tutaliamsha tena katika wanadamu wote wa dunia tumaini lenye uhai, ndilo kipaji cha Roho Mtakatifu, ili siku moja wote hatimaye wachukuliwe katika amani na heri kuu, katika nchi yetu inayong’ara utukufu wa Bwana.

“Basi atukuzwe Yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawezayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina” (Efe 3:20-21).

Mambo yote yaliyoamuliwa katika konstitusio hii ya kichungaji, na kila moja kati yake, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na kuyathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa utukufu wa Mungu.

 

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 7 Desemba 1965

 

Mimi mwenyewe Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki.

(Zinafuata sahihi za Mababa)[1] Konstitusio ya kichungaji iitwayo “Kanisa katika ulimwengu wa leo” ni hati yenye sehemu mbili, lakini zinazofungamana pamoja kuwa kitu kimoja.

Nayo inaitwa “ya kichungaji” kwa sababu inadhamiria kueleza tabia ya Kanisa mbele ya ulimwengu na wanadamu wa nyakati zetu kadiri ya msingi wa mafundisho yake. Kwa hiyo katika sehemu ya kwanza ya hati hii halikosekani lengo la kichungaji (intentio pastoralis), wala katika sehemu ya pili halikosekani lile la kimafundisho (intentio doctrinalis).

Katika sehemu ya kwanza Kanisa linaeleza mafundisho yake juu ya binadamu na ulimwengu anamoishi; tena juu ya mahusiano yake na mambo hayo yote. Katika sehemu ya pili vipengele mbalimbali vya maisha ya siku hizi na ya jamii ya binadamu vinafikiriwa kwa jirani zaidi, hasa masuala na matatizo yanayoonekana yanastahili kupewa kipaumbele. Ndiyo maana katika sehemu hiyo ya pili masuala yanayotazamwa katika mwanga wa mafundisho ya Kanisa yana baadhi ya vipengele vyenye kudumu na vingine tena vinavyolingana na hali ya siku za leo tu.

Basi, kwa sababu hiyo Konstitusio hii lazima ifasiriwe kadiri ya kanuni za jumla za ufafanuzi wa kiteolojia. Na hatimaye, hasa katika sehemu yake ya pili, hati hii lazima ifasiriwe yakizingatiwa mazingira yenye kubadilikabadilika ambayo hoja hizo, kwa tabia yake, zinahusika.

[2] Taz. Yn 18:37
[3] Taz. Yn 3:17; Mt 20:28; Mk 10:45
[4] Taz. Rum 7:14nk.
[5] Taz. 2Kor 5:15.
[6] Taz. Mdo 4:12.
[7] Taz. Ebr 13:8.
[8] Taz. Kol 1:15.
[9] Taz. Mwa 1:26; Hek 2:23.
[10] Taz. YbS 17:3-10.
[11] Taz. Rum 1:21-25.
[12] Taz. Yn 8:34.
[13] Taz. Dan 3:57-90.
[14] Taz. 1Kor 6:13-20.
[15] Taz. 1Fal 16:7; Yer 17:10.
[16] Taz. YbS 17:7-8.
[17] Taz. Rum 2:14-16.
[18] Taz. Pius XII, Tangazo kwa redio juu ya malezi ya dhamiri adilifu ya kikristo katika vijana, 23 machi 1952: AAS 44 (1952) uk. 271.
[19] Taz. Mt 22:37-40; Gal 5:14.
[20] Taz. YbS 15:14.
[21] Taz. 2Kor 5:10.
[22] Taz. Hek 1:13; 2:23-24; Rum 5:21; 6:23; Yak 1:15.
[23] Taz. 1Kor 15:56-57.
[24] Taz. Pius XI, Litt. Encicl. Divini Redemptoris, 19 machi 1937: AAS 29 (1937), uk. 65-106. – Pius XII, Litt. Encicl. Ad Apostolorum Principis, 29 juni 1958: AAS 50 (1958), uk. 601-614. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 451-453. – Paulus VI, Litt. Encicl. Ecclesiam Suam, 6 agosti 1964: AAS 56 (1964), uk. 651-653.
[25] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. I, n. 8: AAS 57 (1965), uk. 12.
[26] Taz. Flp 1:27.
[27] Mt. Augustinus, Confess. I, 1: PL 32, 661.
[28] Taz. Rum 5:14. – Taz. Tertullianus, De carnis resurr. 6: “Umbo lolote ulilofinyangwa ule udongo, ndani yake alifikiriwa Kristo aliye mwanadamu mpya”: PL 2, 802 (848); CSEL 47, uk. 33, l. 12-13.
[29] Taz. 2Kor 4:4.
[30] Taz. Conc. Constantinop. II, can. 7: “Bila ya Mungu Neno kugeuzwa kuwa na maumbile ya mwili, wala bila mwili kubadilishwa kuwa na maumbile ya Neno”: Denz. 219 (428). – Taz. pia Conc. Constantinop. III: “Kama vile mwili wake mtakatifu sana na safi kabisa wenye uhai, ungawa wa kimungu ( deificata), haukubatilishwa (qewqe‹sa oÙk ¢nhršqh), bali umeendelea kuwa na hali na tabia yake”: Denz. 291 (556). – Taz. Conc. Chalced.: “[Yesu Kristo] lazima akiriwe katika maumbile mawili yasiyochanganyikana, wala kubadilika, wala wagawanyika, wala kutenganika”: Denz. 148 (302).
[31] Taz. Conc. Constantinop. III: “Vivyo hivyo mapenzi yake ya kibinadamu, ingawa yakawa ya kimungu ( deificata), hayakubatilishwa”: Denz. 291 (556).
[32] Taz. Ebr 4:15.
[33] Taz. 2Kor 5:18-19; Kol 1:20-22.
[34] Taz. 1Pet 2:21; Mt 16:24; Lk 14:27.
[35] Taz. Rum 8:29; Kol 1:18.
[36] Taz. Rum 8:1-11.
[37] Taz. 2Kor 4:14.
[38] Taz. Flp 3:10; Rum 8:17.
[39] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. II, n. 16: AAS 57 (1965), uk. 20.
[40] Taz. Rum 8:32.
[41] Taz. Liturgia Paschalis Byzantina.
[42] Taz. Rum 8:15 na Gal 4:6; taz. pia Yn 1:12 na 1Yoh 3:1-2.
[43] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 401-464. – Id., Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 257-304. – Paulus VI, Litt. Encicl. Ecclesiam Suam, 6 agosti 1964: AAS 56 (1964), uk. 609-659.
[44] Taz. Lk 17:33.
[45] Taz. Mt. Thomas, In I Ethic., Lec. 1.
[46] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 418. – Taz. pia Pius XI, Litt. Encicl. Quadragesimo anno, 15 mei 1931: AAS 23 (1931), uk. 222 ss.
[47] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 417.
[48] Taz. Mk 2:27.
[49] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 266.
[50] Taz. Yak 2:15-16.
[51] Taz. Lk 16:19-31.
[52] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 299-300.
[53] Taz. Lk 6:37-38; Mt 7:1-2; Rum 2:1-11; 14:10-12.
[54] Taz. Mt 5:43-47.
[55] Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. II, n. 9: AAS 57 (1965), uk. 12-13.
[56] Taz. Kut 24:1-8.
[57] Taz. Mwa 1:26-27; 9:2-3; Hek 9:2-3.
[58] Taz. Zab 8:7 na 10.
[59] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 297.
[60] Taz. Tangazo la Mababa wa Mtaguso lililotolewa kwa watu wote mwanzoni mwa Mtaguso Mkuu Vatikano II, 20 oktoba 1962: AAS 54 (1962) uk. 822-823.
[61] Taz. Paulus VI, Alloc. ad Corpus diplomaticum, 7 jenuari 1965: AAS 57 (1965) uk. 232.
[62] Taz. Conc. Vat. I, Const. dogm. De fide cath. Dei Filius, cap. III: Denz. 1785-1786 (3004-3005).
[63] Taz. Mons. Pio Paschini, Vita e opere di Galileo Galilei, 2 vol., Pont. Accademia delle Scienze, Città del Vaticano, 1964.
[64] Taz. Mt 24:13; 13:24-30 na 36-43.
[65] Taz. 2Kor 6:10.
[66] Taz. Yn 1:3 na 14.
[67] Taz. Efe 1:10.
[68] Taz. Yn 3:14-16; Rum 5:8-10.
[69] Taz. Mdo 2:36; Mt 28:18.
[70] Taz. Rum 15:16.
[71] Taz. Mdo 1:7.
[72] Taz. 1Kor 7:31. – Mt. Irenaeus, Adversus Haereses, V, 36, 1: PG 7, 1222.
[73] Taz. 2Kor 5:2; 2Pet 3:13.
[74] Taz. 1Kor 2:9; Ufu 21:4-5.
[75] Taz. 1Kor 15:42 na 53.
[76] Taz. 1Kor 13:8; 3:14.
[77] Taz. Rum 8:19-21.
[78] Taz. Lk 9:25.
[79] Taz. Pius XI, Litt. Encicl. Quadragesimo anno, 15 mei 1931: AAS 23 (1931), uk. 207
[80] Missale romanum, Utangulizi wa Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme.
[81] Taz. Paulus VI, Litt. Encicl. Ecclesiam Suam, III: AAS 56 (1964), uk. 637-659.
[82] Taz. Tit 3:4: filanqrwpia.
[83] Taz. Efe 1:3, 5-6, 13-14, 23.
[84] Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. I, n. 8: AAS 57 (1965), uk. 12.
[85] Ibidem, cap. II, n. 9: AAS 57 (1965), uk. 14; taz. n. 8, l.c., uk 11.
[86] Ibidem, cap. I, n. 8: AAS 57 (1965), uk. 11.
[87] Taz. ibidem, cap. IV, n. 38: AAS 57 (1965), uk. 43, pamoja na dondoo n. 120.
[88] Taz. Rum 8:14-17.
[89] Taz. Mt 22:39.
[90] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. II, n. 9: AAS 57 (1965), uk. 12-14.
[91] Taz. Pius XII, Allocutio ad cultores historiae et artis, 9 machi 1956: AAS 48 (1956) uk. 212: “Mwanzilishi wa Kanisa, yaani Yesu Kristo aliye Mungu, hakulikabidhi Kanisa utume wa mfumo wa kiutamaduni wala kuweka kusudi la aina hiyo. Lengo Kristo alilolipatia ni la kidini tu.... Kanisa lapaswa kuwaongoza watu kwa Mungu, ili wajikabidhi kabisa kwake.... Kanisa haliwezi kuacha kukazia macho lengo hilo lililo la kidini tu, na la kimungu. Maana ya utendaji wake wote, hadi kanuni ya mwisho ya Kodisi-Sheria yake lazima ilielekee moja kwa moja au kwa njia nyingine lengo hilo”.
[92] Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. I, n. 1: AAS 57 (1965), uk. 5.
[93] Taz. Ebr 13:14.
[94] Taz. 2The 3:6-13; Efe 4:28.
[95] Taz. Isa 58:1-12.
[96] Taz. Mt 23:3-33; Mk 7: 10-13.
[97] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, IV: AAS 53 (1961), uk. 456-457; na I: l.c., uk 407, 410-411.
[98] Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. III, n. 28: AAS 57 (1965), uk. 34-35.
[99] Ibidem, uk. 35-36.
[100] Taz. Mt. Ambrosius, De virginitate, cap. VIII, n. 48: PL 16, 278.
[101] Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. II, n. 15: AAS 57 (1965), uk. 20.
[102] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. II, n. 13: AAS 57 (1965), uk. 17.
[103] Taz. Iustinus, Dialogus cum Tryphone, cap. 110: PG 6, 729; ed. Otto, 1897, uk. 391-393: “...kadiri tunavyoteswa sisi mateso haya, vivyo wanavyokuwa waamini na watauwa zaidi wengine kwa jina la Yesu”. – Taz. Tertullianus, Apologeticus, cap. L, 13: PL 1, 534; Corpus Christ., ser. lat. I, uk. 171: “Kila tunapovunwa nanyi tunafanywa kuwa hata wengi zaidi; damu ya wakristo ndiyo mbegu”. – Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. II, n. 9: AAS 57 (1965), uk. 14.
[104] Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. VII, n. 48: AAS 57 (1965), uk. 53.
[105] Taz. Paulus VI, Allocutio, ya tarehe 3 februari 1965: L’Osservatore Romano, 4 februari 1965.
[106] Taz. Mt. Augustinus, De bono coniugali: PL 40, 375-376 na 394. – Mt. Thomas, Summa theol., Suppl., quaest. 49, art. 3 ad 1. – Conc. Flor., Decretum pro Armenis: Denz. 702 (1327). – Pius XI, Litt. Enc., Casti Connubii: AAS 22 (1930), uk. 543-555; Denz. 2227-2238 (3703-3714).
[107] Taz. Pius XI, Litt. Enc., Casti Connubii: AAS 22 (1930), uk. 546-547; Denz. 2231 (3706).
[108] Taz. Hos 2; Yer 3:6-13; Eze 16 na 23; Isa 54.
[109] Taz. Mt 9:15; Mk 2:19-20; Lk 5:34-35; Yn 3:29; 2Kor 11:2; Efe 5:27; Ufu 19:7-8; 21:2 na 9.
[110] Taz. Efe 5:25.
[111] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, nn. 11, 35 na 41: AAS 57 (1965), uk. 15-16; 40-41; 47.
[112] Taz. Pius XI, Litt. Enc., Casti Connubii: AAS 22 (1930), uk. 583.
[113] Taz. 1Tim 5:3.
[114] Taz. Efe 5:32.
[115] Taz. Mwa 2:22-24; Mit 5:18-20; 31:10-31; Tob 8:4-8; Wim 1:1-3; 2:16; 4:16-5:1; 7:8-11; 1Kor 7:3-6; Efe 5:25-33.
[116] Taz. Pius XI, Litt. Enc., Casti Connubii: AAS 22 (1930), uk. 547-548; Denz. 2232 (3707).
[117] Taz. 1Kor 7:5.
[118] Taz. Pius XII, Allocutio Tra le visite, 20 jenuari 1958: AAS 50 (1958) uk 91.
[119] Taz. Pius XI, Litt. Enc., Casti Connubii: AAS 22 (1930), uk. 559-561; Denz. 2239-2241 (3716-3718). – Taz. Pius XII, Allocutio kwa mkutano wa Umoja wa wauguzi wa Italia, 29 oktoba 1951: AAS 43 (1951) uk 835-854. – Paulus VI, Allocutio kwa Makardinali, 23 juni 1964: AAS 56 (1964) uk 581-589. Masuala yale yanayohitaji upekuzi kwa wingi na kwa uangalifu zaidi, kwa amri ya Baba Mtakatifu yamekabidhiwa kwa Tume ya utafiti wa idadi ya watu, familia, na uzazi, ili, itakapotimiza kazi yake, Baba Mtakatifu atoe hukumu juu yake. Kwa vile ndivyo ilivyo hali ya Majisterio kwa sasa, Mtaguso Mkuu hauna nia ya kutoa mara moja utatuzi wa kiutendaji.
[120] Taz. Efe 5:16; Kol 4:5.
[121] Taz. Sacramentarium gregorianum: PL 78, 262.
[122] Taz. Rum 5:15 na 18; 6:5-11; Gal 2:20.
[123] Taz. Efe 5:25-27.
[124] Taz. Maelezo ya kitangulizi ya Konstitusio hii, nn. 4-10.
[125] Taz. Kol 3:1-2.
[126] Taz. Mwa 1:28.
[127] Taz. Mit 8:30-31.
[128] Taz. Mt. Irenaeus, Adversus Haereses, III, 11, 8: ed. Sagnard, uk. 200; taz. Ib., 16, 6: uk. 290-292; 21, 10-22: uk. 370-372; 22, 3: uk. 378; n.k.
[129] Taz. Efe 1:10.
[130] Taz. maneno ya Pius XI kwa Mhe. Roland-Gosselin: “Ni lazima tusisahau kamwe kwamba lengo la Kanisa ndilo kutangaza habari ya Injili wala si kustaarabisha. Ikiwa Kanisa linastaarabisha, hilo linatokea kwa njia ya uinjilishaji”. ( Semaines sociales de France, Versailles 1936, uk. 461-462).
[131] Conc. Vat. I, Const. dogm. De fide cath. Dei Filius, cap. IV: Denz. 1795, 1799 (3015, 3019). – Taz. Pius XI, Litt. Encicl. Quadragesimo anno, 15 mei 1931: AAS 23 (1931), uk. 190.
[132] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 260.
[133] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 283. – Pius XII, Tangazo kwa redio, 24 desemba 1941: AAS 34 (1942) uk. 16-17.
[134] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 260.
[135] Taz. Ioannes XXIII, Hotuba ya tarehe 11 oktoba 1962, katika uzinduzi wa Mtaguso Mkuu Vatikano II: AAS 54 (1962), uk. 792.
[136] Taz. Conc. Vat. II, Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Conciliu, n. 123: AAS 56 (1964), uk. 131. – Paulus VI, Hotuba kwa wanasanaa wa mji wa Roma, 7 mei 1964: AAS 56 (1964), uk. 439-442.
[137] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De institutione sacerdotali, Optatam totius, na Declaratio De educatione christiana, Gravissimum educationis.
[138] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, cap. IV, n. 37: AAS 57 (1965), uk. 42-43.
[139] Taz. Pius XII, Nuntius ya tarehe 23 machi 1952: AAS 44 (1952), uk. 273. – Ioannes XXIII, Hotuba kwa A.C.L.I., 1 mei 1959: AAS 51 (1959), uk. 358.
[140] Taz. Pius XI, Litt. Encicl. Quadragesimo anno, 15 mei 1931: AAS 23 (1931), uk. 194 ss. – Pius XII, Nuntius ya tarehe 23 machi 1952: AAS 44 (1952), uk. 276 ss. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 450. – Conc. Vat. II, Decr. De instrumentis communicationis socialis, Inter mirifica, cap. I, n. 6: AAS 56 (1964), uk. 147.
[141] Taz. Mt 16:26; Lk 16:1-31; Kol 3:17.
[142] Taz. Leo XIII, Litt. Encicl. Libertas praestantissimum, 20 juni 1888: ASS 20 (1887-1888), uk. 597 ss. – Pius XI, Litt. Encicl. Quadragesimo anno, 15 mei 1931: AAS 23 (1931), uk. 191 ss. – Id., Litt. Encicl. Divini Redemptoris, 19 machi 1937: AAS 29 (1937), uk. 65 ss. – Pius XII, Nuntius ya Sikikuu ya Noeli 1941: AAS 34 (1942), uk. 10 ss. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 401-464.
[143] Kuhusu matatizo ya kilimo, taz. hasa Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 431 ss.
[144] Taz. Leo XIII, Litt. Encicl. Rerum Novarum: ASS 23 (1890-1891), uk. 649-662. – Pius XI, Litt. Encicl. Quadragesimo anno, 15 mei 1931: AAS 23 (1931), uk. 200-201. – Id., Litt. Encicl. Divini Redemptoris, 19 machi 1937: AAS 29 (1937), uk. 92. – Pius XII, Nuntius kwa redio katika kesha la Sikikuu ya Noeli 1942: AAS 35 (1943), uk. 20 – Id., Allocutio ya tarehe 13 juni 1943: AAS 35 (1943), uk. 172. – Id., Nuntius kwa redio iliyotolewa kwa ajili ya wafanyakazi wa Hispania, 11 machi 1951: AAS 43 (1951), uk. 215. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 419.
[145] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 408, 424, 427; neno la “ curatione” (= kuendesha kampuni) limechukuliwa katika matini ya kilatini ya Litt. Encicl. Quadragesimo anno: AAS 23 (1931), uk. 199. Kuhusu maendeleo ya suala lenyewe, taz. pia: Pius XII, Allocutio, 3 juni 1950: AAS 42 (1950), uk 485-488; Paulus VI, Allocutio, 8 juni 1964: AAS 56 (1964), uk 574-579.
[146] Taz. Pius XII, Epist. Encicl. Sertum laetitiae: AAS 31 (1939), uk. 642. – Ioannes XXIII, Allocutio concistorialis: AAS 52 (1960), uk. 5-11. – Id., Litt. Encicl. Mater et Magistra: AAS 53 (1961), uk. 411.
[147] Taz. Mt. Thomas, Summa theol., II-II, q. 32, a. 5 ad 2. – Ibidem, q. 66, a. 2. – Taz. ufafanuzi katika Leo XIII, Litt. Encicl. Rerum Novarum: ASS 23 (1890-1891), uk. 651. – Taz. pia Pius XII, Allocutio ya tarehe 1 juni 1941: AAS 33 (1941), uk. 199. – Id., Nuntius kwa redio katika Sikikuu ya Noeli 1954: AAS 47 (1955), uk. 27.
[148] Taz. Mt. Basilius, Hom. in illud Lucae “Destruam horrea mea”, n. 2: PL 31, 263. – Lactantius, Divinarum Institutionum, lib. V, de iustitia: PL 6, 565B. – Mt. Augustinus, In Ioann. Ev., tr. 50, n. 6: PL 35, 1760. – Id., Enarratio in Ps. CXLVII, 12: PL 37, 1922. – Mt. Gregorius M., Homiliae in Ev., hom. 20, 12: PL 76, 1165. – Id., Regulae Pastoralis liber, pars III, c. 21: PL 77, 87. – Mt. Bonaventura, In III Sent., d. 33, dub. 1: ed. Quaracchi III, 728. – Id., In IV Sent., d. 15, p. II, a. 2, q. 1: ibid. IV, 371b. – Id., Quaest. de superfluo: ms. Assisi, Bibl. Comun. 186, ff. 112a-113a. – Mt. Albertus M., In III Sent., d. 33, a. 3, sol. 1: ed. Borniet XXVIII, 611. – Id., In IV Sent., d. 15, a. 16: ibid. XXIX, 494-497. – Kuhusu kuainisha maana ya yaliyo ya ziada ( superflui) kwa nyakati zetu, taz. Ioannes XXIII, Nuntius ya redio na televisheni ya tarehe 11 septemba 1962: AAS 54 (1962), uk. 682: “Ni wajibu wa kila mtu, wajibu wa lazima wa mkristo, kuyahesabu yaliyo ya ziada kwa kiasi cha mahitaji ya wengine, na kuangalia kwa makini ili usimamiaji na ugawaji wa mali za ulimwengu ufanyike kwa ajili ya manufaa ya watu wote”.
[149] Hapo ina nguvu kawaida hii ya kale: “katika haja za kuzidi kiasi, mali zote ni za wote, yaani ni za kugawanywa”. Lakini, kuhusu tabia, upanuzi na namna ya kuitumia kawaida hiyo, vilivyodokezwa katika matini ya konstitusio, taz. Mt. Tomas, Summa teol. II-II, q. 66, a. 7, licha ya waandishi wa kisasa waliokubalika. Ni dhahiri kwamba, ili kuitumia vema kanuni hii, lazima yatekelezwe masharti ya kimaadili yaliyopo.
[150] Taz. Gratiani, Decretum, c. 21, dist. 86: ed. Friedberg, I, 302. Usemi huo hupatikana tayari katika PL 54, 491A na PL 56, 1132B. Taz. Antonianum 27 (1952), uk. 349-366.
[151] Taz. Leo XIII, Litt. Encicl. Rerum Novarum: ASS 23 (1890-1891), uk. 643-646. – Pius XI, Litt. Encicl. Quadragesimo anno, 15 mei 1931: AAS 23 (1931), uk. 191. – Pius XII, Nuntius kwa redio ya tarehe 1 juni 1941: AAS 33 (1941), uk. 199. – Id., Nuntius kwa redio katika kesha la Sikikuu ya Noeli 1942: AAS 35 (1943), uk. 17 – Id., Nuntius kwa redio, 1 septemba 1944: AAS 36 (1944), uk. 253. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 428-429.
[152] Taz. Pius XI, Litt. Encicl. Quadragesimo anno, 15 mei 1931: AAS 23 (1931), uk. 214. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 429.
[153] Taz. Pius XII, Nuntius kwa redio ya tarehe 1 juni 1941 (Pentekoste): AAS 33 (1941), uk. 199. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 430.
[154] Kuhusu kuzitumia vema mali kadiri ya mafundisho ya Agano Jipya, taz. Lk 3:11; 10:30 ss.; 11:41; 1Pet 5:3; Mk 8:36; 12:29-31; Yak 5:1-6; 1Tim 6:8; Efe 4:28; 2Kor 8:13nk; 1Yoh 3:17-18.
[155] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 417.
[156] Taz. Id., ibid.
[157] Taz. Rum 13:1-5.
[158] Taz. Rum 13:5.
[159] Taz. Pius XII, Tangazo kwa redio, 24 desemba 1942: AAS 35 (1943), uk. 9-24; 24 desemba 1944: AAS 37 (1945), uk. 11-17. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 263, 271, 277-278.
[160] Taz. Pius XII, Nuntius kwa redio ya tarehe 1 juni 1941: AAS 33 (1941), uk. 200. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 271 na 274.
[161] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961), uk. 415-418.
[162] Taz. Pius XI, Allocutio kwa viongozi wa Umoja wa Wasomi wa Vyuo Vikuu Wakatoliki: Discorsi di Pio XI: ed. Bertetto, Torino, vol. I, 1960, uk. 743.
[163] Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 13: AAS 57 (1965), uk. 17.
[164] Taz. Lk 2:14.
[165] Taz. Efe 2:16; Kol 1:20-22.
[166] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 291: “Katika nyakati zetu, zinazojivunia juu ya uwezo wa kiatomi, si akili kufikiri kwamba vita vinafaa ili kuzirudisha tena haki zilizovunjwa”.
[167] Taz. Pius XII, Allocutio, 30 septemba 1954: AAS 46 (1954), uk 589. – Id., Nuntius kwa redio katika kesha la Sikikuu ya Noeli 1954: AAS 47 (1955), uk. 15 ss. – Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, 11 aprili 1963: AAS 55 (1963), uk. 286-291. – Paulus VI, Hotuba kwenye Mkutano wa Umoja wa mataifa, 4 oktoba 1965: AAS 57 (1965), uk 877-885.
[168] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Pacem in terris, ambamo zinatajwa habari za kupunguza silaha za vita: AAS 55 (1963), uk. 287.
[169] Taz. 2Kor 6:2.
[170] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encicl. Ad Petri Cathedram, 29 juni 1959: AAS 51 (1959), uk. 513.
[171] Taz. Mt 7:21.