Index   Back Top Print

[ DE  - EN  - ES  - FR  - IT  - PL  - PT  - SW ]

MAUSIA YA KITUME BAADA YA SINODI

AFRICAE MUNUS

YA BABA MTAKATIFU BENEDIKTO XVI
KWA MAASKOFU, MAKLERI,
WATU WALIO WAKFU
NA WAAMINI WALEI
JUU YA KANISA BARANI AFRIKA
KATIKA KUHUDUMIA UPATANISHO, HAKI NA AMANI

“NINYI NI CHUMVI YA DUNIA ...
NINYI NI NURU YA ULIMWENGU”
(Mt 5:13-14)

 

 

UTANGULIZI

1. Ari ya Afrika kwa Bwana Yesu Kristo ni hazina ya thamani kubwa ambayo ninaiweka mwanzoni mwa hii milenia ya tatu kwa maaskofu, mapadre, mashemasi wa kudumu, watu wa maisha ya wakfu, makatekista na waamini walei wa bara hilo pendwa na visiwa jirani yake. Na utume huo unaielekeza Afrika kutathimini wito wake wa kikristo kwa undani zaidi. Unalialika bara hilo, katika jina la Yesu, kuishi upatanisho kati ya mtu na mtu na jumuiya na kukuza amani na haki katika ukweli kwa wote.

2. Ilikuwa ni nia yangu kwamba Mkutano Maalumu wa Pili kwa ajili ya Afrika wa Sinodi ya maaskofu, ambao ulifanyika kutoka tarehe 4 hadi 25 Oktoba 2009, uendeleze kazi ya Mkutano wa 1994, “ambao ulikusudiwa kuwa fursa ya tumaini na ufufuko, wakati wenyewe hasa ambapo matukio ya kibinadamu yalionekana kuipeleka Afrika kwenye kuvunja moyo na kukata tamaa.”[1] Waraka wa Mausia ya Kitume baada ya Sinodi uitwao Ecclesia in Africa wa mtangulizi wangu, mwenye Heri Yohane Paulo II, ulijumuisha mang’amuzi ya kichungaji na mapendekezo ya mababa wa Sinodi kwa ajili ya uinjilishaji mpya wa bara la Afrika. Ilikuwa wakati mwafaka, baada ya miaka kumi ya kwanza ya milenia hii ya tatu, kuiamsha upya imani na matumaini yetu, ili kusaidia kujenga Afrika iliyopatanishwa kwa kufuata njia za ukweli na haki, upendo na amani (rej. Zab 85:11). Kwa kuungana na mababa wa Sinodi, ninakumbuka kwamba “Bwana asipoijenga nyumba, waijengao wafanya kazi bure” (Zab 127:1).

3. Uhai wa kipekee wa kikanisa na uelewa wa kiteolojia wa Kanisa kama Familia ya Mungu,[2] vilikuwa matunda yanayoonekana wazi zaidi ya Sinodi ya mwaka 1994. Ili kutoa msukumo mpya, uliojaa matumaini na upendo ya kiinjili, kwa Kanisa la Mungu katika bara la Afrika na kwa visiwa jirani yake, niliona ni lazima kuitisha Mkutano wa pili wa kisinodi. Vikitegemezwa na uvuvio wa Roho Mtakatifu na sala za waamini wasiohesabika, vikao vya Sinodi vilizaa matunda ambayo ningependa kuyafikisha kwa njia ya hati hii kwa Kanisa zima, na kwa namna ya pekee kwa Kanisa barani Afrika,[3] ili liweze kweli kuwa “chumvi ya dunia” na “nuru ya ulimwengu” (rej. Mt 5:13-14).[4] Likibidishwa na “imani inayofanya kazi kwa njia ya upendo” (Gal 5:6), Kanisa hutafuta kutoa matunda ya upendo: upatanisho, amani na haki (rej. 1Kor 13:4-7). Huu ni utume wake maalumu.

4. Nilivutiwa sana na ubora wa hotuba zilizotolewa na mababa wa Sinodi na wengine walioongea wakati wa mkutano. Michango yao yalizingatia uhalisia na mtazamo wao wa mbali na kuonyesha ukomavu wa kikristo wa bara la Afrika. Hawakuogopa kuukabili ukweli na walitafuta kutafakari kikwelikweli kuhusu ufumbuzi unaowezekana wa matatizo yanayoyakabili Makanisa yao mahalia na Kanisa lote zima. Pia walitambua kwamba baraka za Mungu, Baba wa wote, hazihesabiki. Mungu hawaachi kamwe watu wake. Sioni ulazima wa kujadili kwa kirefu hali halisi ya kijamii na kisiasa, kimakabila, kiuchumi au kimazingira ambayo Waafrika wanaikabili kila siku na ambayo haiwezi kupuuziwa. Waafrika wanajua vizuri zaidi kuliko mwingine yeyote hali hii inavyoweza mara nyingi kuwa ngumu, ya kukera na hata ya kutisha kabisa. Nawapongeza Waafrika na Wakristo wote wa bara hilo wanaokabili hali hizi kwa ujasiri na utu. Kwa haki kabisa wanataka utu huo utambuliwe na kuheshimiwa. Ninaweza kuwahakikishia kwamba Kanisa linaipenda na linaiheshimu Afrika.

5. Mbele ya changamoto nyingi ambazo Afrika inataka kuzishughulikia ili kuwa zaidi na zaidi nchi ya ahadi, Kanisa, kama Israeli, lingeweza kukata tamaa kirahisi; lakini mababu zetu wa imani wametuonyesha mtazamo sahihi wa kuchukua. Musa, mtumishi wa Bwana, “kwa imani ... alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana” (Ebr 11:27). Kama mwandishi wa waraka kwa Waebrania anavyotukumbusha: “Imani ni hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (11:1). Kwa sababu hii ninaliomba Kanisa zima kuitazama Afrika kwa imani na matumaini. Yesu Kristo, anayetualika kuwa “chumvi ya dunia” na “nuru ya ulimwengu” (Mt 5:13-14), anatupatia nguvu ya Roho kutusaidia kulikaribia lengo hili bora.

6. Ilikuwa nia yangu kwamba maneno ya Kristo: “Ninyi ni chumvi ya dunia ... ninyi ni nuru ya ulimwengu”, yawe mada unganishi ya Sinodi na ya kipindi baada ya Sinodi. Nilipoongea huko Yaoundé kwa waamini wote wa Afrika, nilisema haya: “Katika Yesu, miaka takribani elfu mbili iliyopita, Mungu mwenyewe alileta chumvi na mwanga huko Afrika. Tangu wakati huo na kuendelea, mbegu ya uwepo wake ilipandwa kwenye kilindi cha mioyo ya watu wa bara hili pendwa, na imechanua polepole, nje na ndani ya historia ya mwanadamu.”[5]

7. Mausia ya Baba Mtakatifu Ecclesia in Africa yalifanya la kwake wazo la “Kanisa kama Familia ya Mungu”, ambalo mababa wa Sinodi “walilitambua ... kama msemo unaofaa sana kuhusu hali ya Kanisa, hasa kwa huku Afrika. Kwa kuwa picha hii husisitiza kuwajali wengine, mshikamano, ubora wa mahusiano ya kibinadamu, kupokeana, mazungumzano na kuaminiana.”[6] Hati hiyo ilizialika familia za Afrika kuwa “makanisa ya nyumbani”[7] ili kuzisaidia jumuiya zao kutambua kwamba wao ni viungo vya mwili mmoja. Picha hii ni muhimu siyo tu kwa Kanisa barani Afrika, lakini pia kwa Kanisa lote zima, kwa wakati ambapo familia inatishiwa na wale ambao wanataka kumwondoa Mungu katika maisha ya watu. Kuliondolea bara la Afrika Mungu ni kuliua taratibu, kwa kuliondolea roho yake.

8. Ndani ya mapokeo hai ya Kanisa na kwa kufuata nia iliyoelezwa katika Hati Ecclesia in Afrika,[8] ya kuliona Kanisa kama familia na udugu, ni kurudisha kipengere kimoja cha urithi wake. Katika jumuiya hii ambamo Yesu Kristo, “mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi” (Rum 8:29), aliwapatanisha watu wote na Mungu Baba (rej. Efe 2:14-18) na akammimina Roho Mtakatifu (Yn 20:22), Kanisa kwa upande wake linakuwa mbebaji wa Habari Njema ya kwamba kila mtu ni mtoto wa Mungu. Linaitwa kueneza ujumbe huu kwa watu wote kwa kutangaza wokovu tulioupata kwa njia ya Kristo, kwa kuadhimisha ushirika wetu na Mungu na kwa kuishi katika mshikamano wa kidugu.

9. Afrika inahifadhi uchungu wa kumbukumbu za makovu yaliyoachwa na vita kati ya kikabila, biashara ya utumwa na ukoloni. Leo pia, bara hili linakabiliana na ushindani mbalimbali na aina mpya za utumwa na ukoloni. Mkutano Maalumu wa kwanza ulilifananisha na mhanga wa uporaji, lililoachwa life kando ya barabara (rej. Lk 10:25-37). Ndiyo maana iliwezekana kuongelea “kuwekwa pembezoni” kwa Afrika. Mapokeo yaliyozaliwa katika ardhi ya Afrika yanatambua Msamaria Mwema kuwa ni Bwana Yesu mwenyewe, na yanatoa mwaliko wa kuwa na matumaini. Ni Klementi wa Aleksandria aliyeandika: “Nani, zaidi ya yeye, alituhurumia, wakati sisi sote tulipokuwa mahututi, hali tumejeruhiwa na nguvu za giza, kwa hofu zetu, tamaa mbaya, hasira, maumivu, udanganyifu na anasa? Mganga pekee wa majeraha haya ni Yesu.”[9] Kwa hiyo, kuna sababu nyingi za kutufanya tuwe na matumaini na shukrani. Kwa mfano, licha ya majanga makubwa yanayoangamiza idadi ya watu wake – kama vile malaria, UKIMWI, TB na magonjwa mengine ambayo sayansi bado inahangaika kuyaondoa kabisa, Afrika inahifadhi furaha yake ya kuishi, ikiadhimisha paji la Mungu la uhai kwa kuwakaribisha watoto, kwa kuongeza familia na jumuiya za watu. Ninaona sababu za matumaini pia katika utajiri wa kiakili wa Afrika, utamaduni na urithi wa kidini. Afrika inataka kutunza mambo haya, kuyaimarisha na kuyashirikisha kwa ulimwengu. Kwa kufanya hivyo, itatoa mchango wa msingi na chanya.

10. Mkutano wa Pili wa Sinodi kwa ajili ya Afrika ulishughulikia mada ya upatanisho, haki na amani. Utajiri wa kumbukumbu katika maandishi niliokabidhiwa baada ya vikao – Lineamenta, Instrumentum Laboris, taarifa zilizotayarishwa kabla na baada ya majadiliano, hotuba na mihutasari iliyotayarishwa na makundi yaliyofanya kazi pamoja – “unadai kuigeuza teolojia kuwa huduma ya kichungaji, yaani kuifanya teolojia iguse hali halisi ya huduma ya kichungaji ambamo mitazamo mipana inayopatikana katika Maandiko Matakatifu na katika Mapokeo huongoza utendaji kazi wa maaskofu na mapadre kwa nyakati maalumu na mahali maalumu.”[10]

11. Basi, kwa kujali kama baba na kama mchungaji ninaielekeza hati hii kwa Afrika ya leo, ambayo imeisha kupitia kwenye mateso na migongano ambayo tunaifahamu vizuri sana. Watu wanaundwa na yale yaliyopita, lakini wanaishi na kusafiri katika wakati uliopo na wanatazama mbele. Kama ilivyo duniani kote, Afrika inapitia mshituko wa kiutamaduni ambao unashambulia msingi wa zamani wa maisha ya jamii, na wakati mwingine unafanya iwe vigumu kuendana na usasa. Katika mtikisiko huu wa kijamii ambao bara la Afrika linaukabili, njia za matumaini zitagunduliwa kwa kukuza mazungumzano miongoni mwa washiriki wa jumuiya zake mbalimbali za kidini, kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kisayansi. Afrika itapasika kugundua upya na kukuza dhana ya mtu na uhusiano wake na hali halisi ambayo ni tunda la uamsho wa kiroho wa kina.

12. Katika hati Ecclesia in Africa, Yohane Paulo II alisisitiza kwamba “licha ya ustaarabu wa kisasa wa ‘dunia kuwa kama kijiji kimoja’, katika Afrika kama vile kwingineko duniani roho ya mazungumzano, amani na upatanisho haijakaa bado ndani ya mioyo ya kila mmoja. Vita, migongano na ubaguzi wa rangi na wa kikabila vinatawala mno mahusiano wa kibinadamu.”[11] Tumaini, ambalo ni dalili halisi ya maisha ya kikristo, hutukumbusha kwamba Roho Mtakatifu hutenda kazi kila mahali, pia katika bara la Afrika, na kwamba nguvu za uhai, zinazotokana na upendo, hushinda daima nguvu za kifo (rej. Wim 8:6-7). Hivyo, mababa wa Sinodi waliona kuwa matatizo ambayo yanazikabili nchi na Makanisa mahalia barani Afrika siyo mapingamizi yasiyotatulika, bali ni changamoto zinazochochea vilivyo bora ndani yetu: fikra zetu, akili zetu, wito wetu wa kuzifuata bila masharti nyayo za Yesu Kristo, kumtafuta Mungu, aliye “Upendo wa milele na Ukweli kamili”.[12] Basi, pamoja na wadau wote wa jamii ya Kiafrika, Kanisa hujisikia limeitwa kuzikabili changamoto hizi. Ni, kwa namna fulani, jukumu linalotokana na Injili.

13. Kwa hati hii ninataka kuwapatia wote matunda na maneno ya kutia moyo yaliyopendekezwa na Sinodi, na ninawaalika watu wote wenye mapenzi mema kuiangalia Afrika kwa imani na upendo, ili kuisaidia – kwa njia ya Kristo na kwa njia ya Roho Mtakatifu – iwe nuru wa ulimwengu na chumvi ya dunia (rej. Mt 5:13-14). Hazina ya thamani kubwa iko katika roho ya Afrika – ambako ninaona “ ‘pafu’ la kiroho kwa ubinadamu unaoonekana kuwa katika mtikisiko wa imani na matumaini”[13] – kutokana na utajiri usio na kiasi wa kiutu na wa kiroho wa watoto wake, na tamaduni zake mbalimbali, ardhi yake yenye maliasili tele. Hata hivyo, kama inataka kusimama wima kwa heshima, Afrika inahitaji kusikia sauti ya Kristo ambaye leo anatangaza upendo kwa jirani, upendo hata kwa adui, mpaka kutoa uhai wako: ile sauti ya Kristo anayesali leo kuombea umoja na ushirika wa watu wote katika Mungu (rej. Yn 17:20-21).

 

SEHEMU YA KWANZA
“TAZAMA, NAYAFANYA YOTE KUWA MAPYA”

14. Sinodi iliwezesha kung’amua mihimili ya utume kwa ajili ya Afrika inayotafuta upatanisho, haki na amani. Ni wajibu wa Kanisa mahalia kuitafsiri mihimili hii katika “maazimio motomoto na miongozo kwa ajili ya utendaji”.[14] Kwa kweli ni “katika Kanisa mahalia ambapo kwa namna ya pekee mchanganuo wa mpango wa kichungaji unaweza kutambuliwa – malengo na taratibu, malezi na uwezeshaji wa watu husika, upatikanaji wa rasilimali za lazima – ambao utawezesha utangazaji wa Kristo kuwafikia watu, kuunda jumuiya, na kuwa na msukumo wa kina na wa mkazo katika kushuhudia tunu za Injili ndani ya jamii na utamaduni wa Kiafrika.”[[15]

 

SURA YA I
KATIKA HUDUMA YA UPATANISHO, HAKI NA AMANI

I. WATUMISHI WA KWELI WA NENO LA MUNGU

15. Afrika inayosonga mbele, yenye furaha na uhai, hufanya ionekane sifa ya Mungu, kwa kuwa, kama Mtakatifu Ireneo alivyoandika: “utukufu wa Mungu ni mtu aliye hai”. Lakini mara moja aliongeza: “na uzima wa mtu ni katika kumwona Mungu”.[16] Kwa sababu hiyo, leo pia, kazi ya msingi ya Kanisa ni kuuleta ujumbe wa Injili kwenye moyo wa jamii za Kiafrika, kuwaongoza watu kumwona Mungu. Kama chumvi itiavyo ladha chakula, vivyo hivyo ujumbe huu hufanya wale ambao huuishi wawe mashahidi wa kweli. Wote ambao hukua katika njia hii huwa na uwezo wa kupatanishwa katika Yesu Kristo. Wanakuwa vyanzo vya mwanga kwa ndugu zao. Kwa hiyo, kwa kuungana na mababa wa Sinodi, ninalialika “Kanisa ... barani Afrika kuwa shahidi katika huduma ya upatanisho, haki na amani, kama ‘chumvi ya dunia’ na ‘nuru ya ulimwengu’,”[17] ili maisha yake yawe jibu kwa agizo hili: “Simama, Kanisa barani Afrika, Familia ya Mungu, kwa sababu Baba wa mbinguni anakuita!”[18]

16. Ni kwa maongozi ya Mungu kwamba Sinodi ya Pili kwa ajili ya Afrika ilifanyika baada ya ile iliyohusu Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ilikumbuka wajibu mzito wa kila mfuasi kumfahamu Kristo ambaye anatuita kwa Neno lake. Kwa njia ya Neno hili, waamini, hujifunza kumsikiliza Kristo na kuongozwa na Roho Mtakatifu, ambaye hutufunulia maana ya mambo yote (rej. Yn 16:13). Kwa kweli, “kusoma na kutafakari Neno la Mungu hutufanya tuwe na mizizi ya kina katika Kristo na huongoza huduma yetu kama wahudumu wa upatanisho, haki na amani.”[19] Kama Sinodi ile ilivyotukumbusha, “ili kuwa kaka na dada zake, ni lazima kuwa kama ‘wale wanaolisikia Neno la Mungu na kulitenda’ (Lk 8:21). Usikilizaji halisi ni utii na utendaji; humaanisha kufanya haki na amani kuchanua katika maisha, ni kutoa, katika maisha na katika jamii, ushahidi unaozingatia wito wa manabii, ambao uliendelea kuliunganisha Neno la Mungu na maisha, imani na uadilifu, ibada na majukumu ya kijamii.”[20] Kulisikiliza na kulitafakari Neno la Mungu humaanisha kuliruhusu lipenye na kuyaunda maisha yetu ili kutupatanisha na Mungu, kumruhusu Mungu atuongoze kwenye upatanisho na jirani zetu: njia ya lazima kwa kujenga jumuiya ya watu na ya mataifa. Katika maisha yetu, tunaomba Neno la Mungu litwae mwili kweli!

 

II. KRISTO KATIKA MOYO WA MAISHA YA KIAFRIKA:
CHEMCHEMI YA UPATANISHO, HAKI NA AMANI.

17. Mawazo makuu matatu ya mada iliyochaguliwa kwa ajili ya Sinodi, yaani upatanisho, haki na amani, yaliweka Sinodi mbele ya “wajibu wake wa kiteolojia na kijamii”,[21] na yakawezesha pia kutafakari juu ya mchango wa kijamii wa Kanisa na nafasi yake katika bara la Afrika leo.[22] Tungeweza kusema kwamba upatanisho na haki ndiyo misingi miwili ya amani, na kwamba, kwa hiyo, kwa kiasi fulani, inaeleza hali yake halisi.”[23] Jukumu ambalo tunapaswa kulifafanua si rahisi, kwa sababu linajikita kati ya kujiingiza mara moja katika uwanja wa siasa – kitu ambacho ni nje ya maeneo ya utendaji wa moja kwa moja wa Kanisa – na uwezekano wa kujitoa au kuepa hali ya leo kwa kushikilia nadharia za kiteolojia na kiroho ambazo zinaweza kutumika kama fursa ya kukwepa uwajibikaji halisi wa kihistoria.

18. “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa”, asema Bwana, na anaongeza “niwapavyo mimi, sivyo kama ulimwengu utoavyo” (Yn 14:27). Amani ya kibinadamu inayopatikana bila haki ni ya kudanganya na ya muda mfupi. Haki ya kibinadamu ambayo siyo tunda la upatanisho katika “ukweli wa upendo” (Efe 4:15) inabaki si kamili; si haki halisi. Upendo wa ukweli – “ukweli wote” ambako Roho peke yake anaweza kutuongoza (rej. Yn 16:13) – ndio unaoonyesha njia ambayo haki yote ya kibinadamu lazima ifuate ili iweze kurudisha pingu za mshikamano wa kidugu ndani ya “familia ya kibinadamu, jumuiya ya amani”[24], inayopatanishwa na Mungu kwa njia ya Kristo. Haki kamwe si kitu cha kufikirika tu. Inadai kufungamana na maamuzi ya kibinadamu yasiyo kigeugeu. Upendo unaoshindwa kuheshimu uadilifu na haki za wote ni wa uongo. Kwa hiyo ninawatia moyo Wakristo wawe mfano wa kuigwa katika medani ya haki na upendo (Mt 5:19-20).

A. “Mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:20b)

19. “Upatanisho ni jambo linalotangulia siasa, na kwa sababu hii wenyewe ni muhimu sana kwa kazi ya siasa yenyewe. Bila nguvu ya upatanisho kuumbwa ndani ya mioyo ya watu, majukumu ya kisiasa kwa ajili ya amani yanakosa msingi wake wa ndani. Kwenye Sinodi, Wachungaji wa Kanisa walihangaikia huu utakaso wa ndani wa mtu ambao ni sharti la msingi linalodaiwa kabla ya kujenga haki na amani. Lakini utakasaji huu na ukomavu wa ndani kuelekea utu wa kweli hauwezi kuwepo bila Mungu.”[25]

20. Kwa kweli, ni neema ya Mungu inayotupatia moyo mpya na hutupatanisha naye na sisi kwa sisi.[26] Ni Kristo aliyeurudisha ubinadamu katika upendo wa Baba. Upatanisho chanzo chake ni katika upendo huo; unaotokana na uamuzi wa Baba wa kufanya upya uhusiano wake na wanadamu, uhusiano uliovunjwa na dhambi ya mwanadamu. Katika Yesu Kristo, “katika maisha yake na katika huduma yake, lakini hasa katika kifo na ufufuko wake, Mtume Paulo alimwona Mungu Baba akiupatanisha ulimwengu (vitu vyote mbinguni na duniani) naye, bila kuhesabia dhambi ya binadamu (rej. 2Kor 5:19; Rum 5:10; Kol 1:21-22). Paulo alimwona Mungu Baba akiwapatanisha Wayahudi na watu wa mataifa kwake, akiumba mtu mmoja mpya kwa njia ya msalaba (rej. Efe 2:15; 3:6). Kwa namna hiyo, tendo la upatanisho hujenga ushirika katika ngazi mbili: ushirika muungano kati ya Mungu na wanadamu; na ushirika kati ya watu – kwa kuwa tendo la upatanisho pia hutufanya sisi (kama wanadamu tuliopatanishwa) kuwa ‘mabalozi wa upatanisho’”[27] . Upatanisho, kwa hiyo, si kwamba unaishia katika mpango wa Mungu wa kuleta kwake – katika Kristo kwa njia ya msamaha wa dhambi na kwa upendo – wanadamu waliojitenga naye na walio wenye dhambi. Bali upatanisho unarudisha pia uhusiano kati ya watu kwa njia ya maridhiano ya tofauti zao na kwa kuviondoa vizuizi vya mahusiano yao kwa kuonja kwao upendo wa Mungu.”[28]  Jambo hili limeelezwa wazi na mfano wa mwana mpotevu; katika kurudi kwa yule mwana mdogo (yaani, kuongoka kwake) Mwinjili anatuonyesha hitaji lake la kupatanishwa na baba yake, na pia, kwa kupitia kwa baba yake, na kaka yake (rej. Lk 15:11-32). Ushuhuda wa kusisimua kutoka waamini wa Afrika, “ushuhuda wa mateso na wa upatanisho halisi katika matukio ya kusikitisha yaliyotokea miaka hii barani Afrika”[29], umeonyesha uwezo wa Roho kugeuza mioyo ya wahanga na watesi wao na kwa hiyo kujenga upya udugu.[30]

21. Kwa hakika, ni upatanisho halisi tu unaoweza kuleta amani ya kudumu katika jamii. Hii ni jukumu la lazima la viongozi wa serikali na watemi wa kijadi, lakini inawahusu pia raia wa kawaida. Baada ya kutokea migogoro, upatanisho – ambao mara nyingi hupatikana kimyakimya na bila majigambo – hurudisha umoja wa mioyo na kuishi pamoja kwa utulivu. Kutokana na upatanisho, baada ya vita vya muda mrefu mataifa yanaweza kurudisha amani, na jamii iliyojeruhiwa vikali na vita vya wenyewe kwa wenyewe au na mauaji ya kimbari inaweza kujenga tena umoja wao. Kwa njia ya kutoa na kupokea msamaha[31] kumbukumbu zilizojeruhiwa za watu binafsi na za jumuiya zimepata kupona, na familia ambazo zilikuwa zimegawanyika zimeungana tena kwa utulivu. “Upatanisho hushinda matatizo, hurudisha heshima ya watu binafsi na hufungua njia ya maendeleo na amani ya kudumu kati ya watu katika kila ngazi”[32], kama mababa wa Sinodi walivyokuwa na shauku ya kusisitiza. Ili uwe na ufanisi, upatanisho huu lazima uendane na tendo la kijasiri na la kikweli, lisilo na unafiki ndani yake: ufuatiliaji wa waliohusika na migogoro hii, wa wale ambao waliuwezesha kifedha ukatili huo, pamoja na waliohusika kwa namna yoyote na mipango hiyo, na kuhakikisha jinsi walivyohusika. Wahanga wana haki ya kujua ukweli na kupata haki. Ni muhimu kwa sasa na kwa wakati ujao kusafisha kumbukumbu, ili kuijenga jamii bora zaidi pale ambapo matukio hayo ya kutisha hayarudiwi tena.

B. Kuwa wenye haki na kujenga mfumo wa kijamii wenye haki

22. Hapana shaka kwamba ujenzi wa mfumo wa kijamii wenye haki ni jukumu la siasa.[33] Hata hivyo moja ya majukumu ya Kanisa barani Afrika ni kuunda dhamiri safi zinazojali madai ya haki, ili wapatikane watu wanaotaka na wanaoweza kuujenga huu mfumo wa kijamii wenye haki kwa mwenendo wa wenye uwajibikaji. Mfano bora kabisa wa kuigwa ni Kristo, namna ya kufikiri ya Kanisa inazingatia mfano huo, na Kanisa linaupendekeza kwa wote.[34] Kwa mujibu wa mafundisho kuhusu jamii, “Kanisa halina majibu ya kitaalamu na kiufundi, wala halidai ‘kuingilia kwa namna yoyote siasa za mataifa.’ Hata hivyo, Kanisa lina utume wa kutekeleza ukweli ... utume ambao Kanisa kamwe haliwezi kuusahau. Mafundisho yake kuhusu jamii ni nafasi maalum ya utangazaji huo wa ukweli: ni huduma ya ukweli inayotuweka huru.”[35]

23. Kwa njia ya Tume za Haki na Amani, Kanisa lilijibidisha kutoa elimu ya uraia kwa wananchi na kusaidia katika mchakato wa uchaguzi katika nchi kadhaa. Kwa njia hii Kanisa huchangia kuwaelimisha watu, likiamsha dhamiri zao na uwajibikaji wao wa kiraia. Nafasi hii ya pekee katika malezi inathaminiwa na nchi nyingi ambazo zinalitambua Kanisa kama mjenga amani, mtendaji wa upatanisho na mtangazaji wa haki. Inafaa kurudia kwamba, ingawa tunatofautisha nafasi ya wachungaji na nafasi ya waamini walei, utume wa Kanisa si katika ngazi ya siasa.[36] Kazi yake ni kuulea ulimwengu kwenye hisia za kidini (religious sense) kwa kumtangaza Kristo. Kanisa linataka kuwa ishara ya hali ya binadamu inayozidi mambo ya hapa duniani tu, na kuihifadhi. Kanisa ni lazima pia liwe mlezi wa watu katika kutafuta ukweli ulio wa juu zaidi kuhusu jinsi walivyo wao wenyewe, na kuhusu maswali yao, ili majibu sahihi kwa matatizo yao yaweze kupatikana.[37]

1. Kuishi kadiri ya Haki ya Kristo

24. Katika uwanja wa kijamii, dhamiri za wanadamu zinakumbana na changamoto zinazotokana na ukosefu mkubwa wa haki uliopo katika ulimwengu wetu kwa ujumla na ndani ya bara la Afrika kwa namna ya pekee. Uporaji wa mali asili unaofanywa na wachache kwa hasara ya watu wote ni kitu kisichokubalika, kwa sababu ni kinyume na maadili. Haki inatulazimisha “kumpa kila mtu anachostahili”: ius suum unicuique tribuere.[38] Ni suala, kwa hiyo, la kutoa haki kwa mataifa yote. Afrika inaweza kumpa kila mtu na kila taifa la bara hilo mazingira ambayo yatawawezesha kushirikishana katika maendeleo.[39] Kwa hiyo Waafrika wataweza kuzitumia talanta zao na utajiri wao walizopewa na Mungu kwa kuwahudumia nchi zao na ndugu zao. Ili haki itawale katika maeneo yote ya maisha, maisha binafsi na maisha ya hadhara, katika mambo ya kiuchumi na ya kijamii, inahitaji kutegemezwa na kanuni ya auni (subsidiarity) na mshikamano (solidarity), na zaidi ya hayo, lazima isukumwe na upendo. “Kwa mujibu wa kanuni ya auni, wala serikali au jamii nyingine yoyote ya ngazi ya juu ina haki ya kujichukulia ubunifu na wajibu wa watu binafsi na mashirika ya ngazi ya kati.”[40] Mshikamano ndio uhakika wa haki na amani, na hivyo ndio uhakika wa umoja, kwa namna ambayo ule “utele wa baadhi ya watu ufidie uhaba wa wengine.”[41] Na upendo, ambao hutuhakikishia mshikamano wetu na Mungu, ni zaidi ya haki ya kugawana. Kwa sababu “kama haki ni fadhila ambayo humpa kila mtu anachostahili ... chochote ambacho humuondoa mtu mbali na Mungu wa kweli hakiwezi kuwa haki.”[42]

25. Mungu mwenyewe hutuonyesha haki ya kweli ni ya namna gani, kwa mfano, tunapomuona Yesu anaingia katika maisha ya Zakayo na hivyo kumpa mdhambi neema ya uwepo wake (rej. Lk 19:1-10), Ni nini, basi, haki hii ya Kristo? Waliokuwepo wakati Yesu alipokutana na Zakayo walimtazama Yesu (rej. Lk 19:7); kunung’unika kwao kwa kutoridhika kuliashiria upendo kwa haki. Hata hivyo, hawa hawajui haki ya upendo ambayo hujitolea mpaka upeo, mpaka kujichukulia yenyewe “laana” iliyowekwa juu ya wanadamu, ili badala yake waweze kupokea “baraka” ambayo ni zawadi ya Mungu (rej. Gal 3:13-14). Haki ya kimungu huiwezesha haki ya kibinadamu, ambayo daima ina mipaka na si kamili, kuwa na mtazamo mpana ili kuweza kuwa kamilifu. Zaidi, inatufanya tutambue unyonge wetu, hitaji letu la kupokea msamaha na la urafiki wa Mungu. Ndivyo tunavyoonja katika Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi, ambazo zinatokana na tendo la wokovu la Kristo. Utendaji huo wa wokovu unatuingiza kwenye aina ya haki ambamo tunayapata mengi zaidi kuliko tulivyoweza kutarajia[kwa kuzingatia haki], kwa kuwa katika Kristo, upendo ni ukamilifu wa sheria (rej. Rum 13:8-10).[43] Kwa njia ya Kristo, aliye mfano pekee wa kuigwa, mwenye haki hualikwa kuingia kwenye mfumo wa upendo – agape.

2. Kuunda mfumo wa haki katika Roho ya Heri Nane

26. Mfuasi wa Yesu, katika kuungana na Mwalimu wake, lazima asaidie kuunda jamii yenye haki ambamo wote wataweza kushiriki kikamilifu, wakizitumia talanta zao, katika maisha ya kijamii na ya kiuchumi. Kwa hiyo wataweza kupata wanachohitaji ili kuishi kulingana na hadhi yao kama binadamu katika jamii ambamo haki inahuishwa na upendo.[44] Kristo hapendekezi aina ya mapinduzi yanayolenga jamii au siasa tu, bali mapinduzi ya upendo, yaliyoletwa kwa kujitoa kwake kikamilifu kwa njia ya kifo chake msalabani na ufufuko wake. Heri Nane zimejengwa juu ya msingi wa mapinduzi haya ya upendo (rej. Mt 5:3-10). Heri Nane zinatoa mtazamo mpya wa haki, uliofunguliwa rasmi katika fumbo la Pasaka, ambao kwa njia yake tunaweza kuwa wenye haki na tunaweza kujenga ulimwengu bora zaidi. Haki ya Mungu, iliyofunuliwa kwetu katika zile Heri, huwapandisha wanyenyekevu na kuwashusha wanaojikweza wenyewe. Kwa kweli, haki hii itakamilishwa katika ufalme wa Mungu utakaokamilika mwisho wa nyakati. Lakini haki ya Mungu tayari huonekana hapa na sasa, ambapo maskini wanafarijiwa na kukaribishwa katika karamu ya uzima.

27. Katika roho ya Heri hizo, upendeleo wa pekee ni lazima utolewe kwa maskini, wenye njaa, wagonjwa – kwa mfano, wenye UKIMWI, kifua kikuu au malaria – kwa wageni, kwa wale wanaonyanyaswa, kwa wafungwa, kwa wahamiaji ambao wanadharauliwa, kwa wakimbizi au waliofukuzwa (rej. Mt 25:31-46). Kujibu katika haki na upendo mbele ya mahitaji ya watu hawa ni juu ya kila mtu. Afrika inategemea kujaliwa namna na familia nzima ya wanadamu, kama vile kutoka kwa watu wake wenyewe.[45] Hata hivyo, ni lazima ianze ndani yake na kwa makusudi mazima ya kuwa na mfumo wa haki ya kisiasa, kijamii na kiutawala; hii ni sehemu ya utamaduni wa kisiasa unaohitajika kwa kuleta maendeleo na amani. Kwa upande wake, Kanisa litatoa mchango wake maalumu kwa kuyaegemea mafundisho ya Heri Nane.

C. Upendo katika ukweli: Chemchemi ya Amani

28. Mtazamo wa kijamii uliopendekezwa na utendaji wa Kristo, ulio na msingi katika upendo, unapita kiwango cha chini cha madai ya haki za kibinadamu, yaani, kumpa kila mtu anachostahili. Mantiki ya ndani ya upendo inavuka haki hii, hata kufikia kiwango cha mtu kutoa kama zawadi mali zake:[46] “Tusipende kwa neno au kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli” (1Yoh 3:18). Kwa mfano wa Mwalimu Bwana wake, mfuasi wa Kristo atakwenda mbali zaidi hata kufikia kiwango cha kuutoa uhai wake kwa ajili ya ndugu zake (rej. 1Yoh 3:16). Hii ndiyo gharama ya amani ya kweli katika Mungu (rej. Efe 2:14).

1. Huduma halisi ya kidugu

29. Hakuna jamii, hata kama imeendelea namna gani, inayoweza kwenda bila huduma ya kidugu inayosukumwa na upendo. “Yeyote atakaye kuuondoa upendo anajitayarisha kumwondoa hata mtu. Daima kutakuwa na mateso yanayolilia faraja na msaada. Daima kutakuwako upweke. Daima kutakuwa na hali ya kuhitaji vitu, ambamo msaada katika hali halisi ya upendo kwa jirani ni wa lazima.”[47]  Ni upendo ambao hutuliza mioyo iliyoumizwa, iliyobaki katika hali ya upweke au iliyotelekezwa. Ni upendo unaozalisha au unaorudisha amani katika mioyo wa watu na kuijenga amani kati yetu.

2. Kanisa kama Mwangalizi

30. Katika hali halisi ya wakati huu barani Afrika, Kanisa linaitwa kuifanya sauti ya Kristo isikike. Linatakiwa kuufuata ushauri wa Yesu kwa Nikodemo, aliyemuuliza inawezekanaje kuzaliwa mara ya pili: “Hamna budi kuzaliwa mara ya pili” (Yn 3:7). Wamisionari waliletea Waafrika njia ya huku kuzaliwa upya “kwa maji na Roho” (Yn 3:5), Habari Njema ambayo kila mtu ana haki ya kuisikia ili kufikia wito wake kikamilifu.[48] Kanisa barani Afrika huchota uhai wake kutoka kwenye urithi huu. Kwa ajili ya Kristo na kwa kuwa waaminifu kwa mafundisho yake ya kimaisha, Kanisa hujisikia kuwa na wajibu wa kuwa kila mahali ambapo watu wanateseka na kufanya kisikike kilio bubu cha wasiokuwa na hatia ambao huteseka kutokana na madhulumu, au cha watu ambao serikali zao hutumia fursa zilizopo sasa na za wakati ujao kwa manufaa yao binafsi.[49] Kwa njia ya uwezo wake wa kuuona uso wa Kristo katika nyuso za watoto, wagonjwa, wahitaji na wanaoteseka, Kanisa linasaidia polepole lakini kwa uimara kuunda Afrika mpya. Katika kazi yake ya kinabii, kila wakati watu wanapolililia: “Ee mlinzi, habari gani za usiku?” (Isa 21:11), Kanisa linataka kuwa tayari kutoa sababu ya tumaini lililo nalo ndani yake (rej. 1Pet 3:15), kwa sababu pambazuko jipya linakuja (rej. Ufu 22:5). Kukataa udhalilishaji wa wanadamu na makubaliano yoyote yanayotokana na woga wa kuteseka au kifodini ndiyo njia pekee Injili ya Ukweli isonge mbele. “Ulimwenguni”, asema Kristo, “mnayo dhiki. Lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu” (Yn 16:33). Amani ya kweli hutoka kwa Kristo (rej. Yn 14:27). Hivyo, haiwezi kulinganishwa na amani ambayo ulimwengu hutoa. Siyo tunda la majadiliano na makubaliano ya kidiplomasia yenye msingi katika faida binafsi. Ni amani ya ubinadamu uliojipatanisha katika Mungu, amani ambayo kwake Kanisa ni sakramenti.[50]

 

SURA YA II
MAHALI PA KUFANYIA KAZI KWA UPATANISHO, HAKI NA AMANI

31. Katika hatua hii, ningependa kuonyesha baadhi ya njia (“karakana”) ambazo mababa wa Sinodi waliziainisha kwa ajili ya utume wa Kanisa leo katika jitihada za kuisaidia Afrika kujikomboa kutoka kwa nguvu zinazoifanya ipooze. Kristo hakusema awali ya yote kwa yule aliyepooza: “Umesamehewa dhambi zako”, na halafu “Inuka!” (Lk 5:20.24)?

1. KUMJALI MTU

A. Metanoia: Uongofu wa kweli

32. Hangaiko kuu la wanasinodi, kadiri walivyoangalia hali ya bara la Afrika, lilikuwa ni kutafuta njia za kutia moyoni mwa Waafrika wafuasi wa Kristo utashi wa kujitoa kikamilifu kuiishi Injili katika maisha yao ya kila siku na katika jamii. Kristo daima anataka metanoia, uongofu.[51] Wakristo wameathiriwa na roho na desturi za nyakati zao na mahali pao. Lakini kwa neema ya Ubatizo wao wanaitwa kuikataa mielekeo isiyofaa na kwenda kinyume na mikondo. Ushahidi wa namna hii unadai majitoleo yasiyotetereka katika “uongofu endelevu kwa Baba, aliye chanzo cha uhai wa kweli, aliye peke yake na uwezo wa kututoa katika uovu na majaribu yote, na kutuweka katika Roho wake, hata katika mapambano dhidi ya nguvu za uovu.”[52] Uongofu kama huo unawezekana tu ikiwa unaegemea imani iliyoimarishwa, ikitegemezwa na katekesi ya kweli. Kwa hiyo inafaa “kutunza muunganiko hai kati ya katekisimu inayokaririwa na katekisimu iliyo hai katika maisha, kwa namna ambayo hutuongoza kwenye uongofu wa maisha wa kina na wa kudumu.”[53] Uongofu huonekana kwa namna ya pekee katika sakramenti ya Upatanisho, unatakiwa kuwa na umakini wa pekee ili iweze kuwa kama “shule ya moyo” ya kweli. Katika shule hii, wanafunzi wa Kristo polepole huunda na kukomaza maisha ya kikristo yaliyokomaa na yaliyo ishara ya umakini katika vipengee vyenye mtazamo wa kimungu na vya kimaadili katika matendo yake, na kwa hiyo huweza “kukabili magumu ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni”[54] kwa njia ya maisha yanayoongozwa na roho ya Injili. Mchango wa Wakristo katika Afrika utakuwa na manufaa ikiwa tu uelewa wao wa imani unajenga uelewa wao wa ulimwengu.[55] Ili iwe hivyo, malezi ya imani ni ya lazima, vinginevyo Kristo litakuwa ni jina jingine tu zaidi linalopamba nadharia zetu. Neno la Mungu na ushahidi wa maisha huenda pamoja.[56] Lakini ushahidi peke yake hautoshi, kwa sababu “hata ule ushahidi mzuri kabisa utaonyesha kushindwa baada ya muda kama haukuelezwa vizuri na kuhalalishwa – kile ambacho Petro hukiita kuwa ‘tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu’ – na kufafanuliwa na utangazaji ulio wazi na wa moja kwa moja wa Bwana Yesu.”[57]

B. Kuuishi ukweli wa Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho

33. Wanasinodi pia walikazia kwamba Wakristo wengi Afrika huchukua msimamo usioeleweka wa sakramenti ya upatanisho, wakati Wakristo walewale mara nyingi wanazingatia kikamilifu na kwa taratibu za ibada za jadi za upatanisho. Ili kuwasaidia waamini Wakatoliki kutembea katika njia halisi ya uongofu (metanoia) wanapoadhimisha sakramenti hii, ambapo mtazamo mzima wa mtu unaelekezwa upya kwenye lengo la kukutana na Yesu,[58] ingefaa maaskofu waagize ufanyike utafiti makini juu ya ibada za jadi za Kiafrika za upatanisho ili kutathimini sehemu zake chanya na mipaka yake. Kwa kweli taratibu hizo ambazo ni kama malezi ya usuluhisho[59] kwa namna yoyote ile haiwezi kuwa badala ya sakramenti ya upatanisho. Mausia ya Kitume baada ya Sinodi iitwayo Reconciliatio et Paenitentia (Upatanisho na Toba) ya mwenye heri Yohane Paulo II waziwazi ilieleza kuhusu mhudumu rasmi na taratibu za sakramenti ya Kitubio na Upatanisho.[60] Taratibu za jadi zinaweza kusaidia tu kupunguza ugumu wanaosikia baadhi ya waamini na kuwasaidia kuwa wazi kwa kina zaidi na kwa ukweli zaidi kwa Kristo, aliye Mpatanishi mkuu pekee, ili kupokea neema ya sakramenti ya Kitubio. Ikiadhimishwa katika imani, sakramenti hii ina nguvu ya kutupatanisha na Mungu na jirani.[61] Hatimaye, ni Mungu ambaye, katika Mwanae, anatupatanisha naye na sisi kwa sisi.

C. Roho ya umoja na ushirika (A spirituality of communion)

34. Upatanisho siyo tendo linalofanyika mara moja tu bali ni mchakato mrefu ambao kwao wahusika wanajengwa tena katika upendo – upendo ambao huponya kwa njia ya kazi ya Neno la Mungu. Upatanisho kwa hiyo huwa kwa wakati huohuo namna ya kuishi na utume. Ili kufikia upatanisho wa kweli na kuweka katika matendo roho ya umoja inayotokana na upatanisho, Kanisa linahitaji mashahidi ambao wamezama kabisa katika Kristo na hulishwa na Neno lake na Masakramenti. Hivyo, kwa kujitahidi kukua katika utakatifu, mashahidi hawa wanaweza kuwa na ari katika ujenzi wa umoja wa familia ya Mungu, wakiwasilisha kwa ulimwengu – kama ni lazima hadi kifodini – roho ya upatanisho, haki na amani, kwa mfano wa Kristo.

35. Hapa ningependa kutaja masharti ya roho ya umoja (spirituality of communion) ambayo Papa Yohane Paulo II alipendekeza kwa Kanisa zima: uwezo wa kuona mwanga wa fumbo la Utatu Mtakatifu uking’aa katika nyuso za ndugu wanaotuzunguka,[62] kuwajali “ndugu zetu wa imani katika umoja wa kina wa Mwili wa Fumbo, na kwa hiyo kama ‘wale ambao ni sehemu yangu’ ili kushiriki furaha na mateso yao, kuyaelewa matarajio yao, kuyashughulikia mahitaji yao, na kuwapa urafiki wa kina na wa kweli”;[63] uwezo pia wa kuyatambua yote yaliyo mazuri katika maisha ya wengine ili kuyakaribisha na kuyachukua kama zawadi ambayo Mungu hunipatia kwa njia ya mtu huyo, kwa namna ambayo inavuka mipaka ya nafsi yake kwa vile anakuwa kama bomba la neema za Mungu; na hatimaye, uwezo “wa kuwatengenezea nafasi ndugu zetu, ‘tukichukuliana mizigo yetu’ (Gal 6:2) na tukikataa kishawishi cha ubinafsi ambacho daima hutusonga na kuuamsha ushindani, kunyang’anyana vyeo, kutoaminiana na wivu.”[64]

Kwa namna hii watu watakua katika imani na umoja, wakionyesha ujasiri katika ukweli na majikatalio, na wakiangaziwa na furaha. Hivyo wanashuhudia kwa namna ya kinabii katika maisha yanayopatana na imani yao. Maria, Mama wa Kanisa, aliyemkaribisha Neno wa Mungu, ndiye mfano wao: Maria, kwa kulisikiliza neno hilo, aliweza kuyaelewa mahitaji ya watu na kuwa mwombezi wao, katika huruma yake.[65]

D. Utamadunisho wa Injili na Uinjilishaji wa utamaduni

36. Ili kuleta umoja na ushirika huo, ingefaa kwamba Mkutano wa kwanza wa Sinodi kwa ajili ya Afrika uliongea juu ya hitaji la utafiti wa kina kuhusu mapokeo na tamaduni za Kiafrika. Wanasinodi walibaini kutengana kwa baadhi ya mapokeo na tamaduni za Kiafrika na madai mahususi ya ujumbe wa Kristo. Katika jitihada zake za kutafuta kufanya mambo yanayoeleweka na yenye kukubalika, Kanisa linahitaji kufanya tathimini ya kina ili kubaini vipengee vya kitamaduni ambavyo ni pingamizi kwa umwilisho wa tunu za Injili, na pia vipengee vinavyokuza tunu hizi.[66]

37. Hata hivyo, lazima tukumbuke kwamba Roho Mtakatifu ndiye mtendaji wa kweli wa utamadunisho, ndiye anayesimamia “kwa namna yenye kuzaa matunda mazungumzano kati ya Neno la Mungu, lililofunuliwa katika Kristo, na maswali ya kina ambayo huibuka miongoni mwa wingi wa watu na tamaduni. Kwa njia hii, tukio la Pentekoste huendelea katika historia, katika umoja wa ile imani moja na ileile iliyotajirishwa na utofauti wa lugha na tamaduni mbalimbali.”[67] Roho Mtakatifu huwezesha Injili kupenya tamaduni zote, bila kuwa mtumishi wa hizo.[68] Maaskofu lazima wawe macho kwa hitaji hili kwa utamadunisho, wakiheshimu kanuni zilizowekwa na Kanisa. Kwa kupambanua mambo yapi katika utamaduni na mapokeo yanapingana na Injili, wataweza kutenganisha mbegu nzuri na magugu (rej. Mt 13:26). Na hivyo Ukristo, wakati ukibaki katika ukweli wake, katika uaminifu kamili kwa ujumbe wa Injili na mapokeo ya Kanisa, utapokea uso wa tamaduni nyingi zisizohesabika za watu ambao miongoni mwao umepokelewa na kuweka mizizi. Na Kanisa litakuwa ikona ya wakati ujao ambao Roho wa Mungu anatutayarishia,[69] ikona ambayo humo Afrika inaweza kutoa mchango wake. Katika mchakato huu wa utamadunisho, ni muhimu kutosahau kazi, ambayo ni muhimu vilevile, ya kuinjilisha ulimwengu wa utamaduni wa kisasa wa Kiafrika.

38. Ubunifu wa Kanisa kwa ajili ya kuthamini na kulinda tamaduni za Kiafrika unafahamika wazi. Ni muhimu sana kitu hiki kiendelee, wakati ambapo kuchanganyikana kwa watu, pamoja na kuwa sababu ya kutajirishana, mara kwa mara hudhoofisha tamaduni na jamii. Utambulisho wa jumuiya za Kiafrika uko hatarini katika mwingiliano wa tamaduni hizi. Inalazimu kwa hiyo kuwajibika katika kueneza tunu ambazo Muumba ameziamsha katika mioyo ya Waafrika tangu mwanzo wa nyakati. Hizi zimesaidia kama chanzo cha kuunda jamii zenye kiwango fulani cha maelewano, kwa kuwa zinajumuisha kanuni za kitamaduni za kuishi pamoja kwa amani. Vipengee hivi chanya kwa hiyo vinahitaji kuthaminiwa, vikiangaziwa kutoka ndani (rej. Yn 8:12), kusudi Wakristo waweze kupokea kikwelikweli ujumbe wa Kristo, na kwa njia hii Mwanga wa Mungu uweze kung’aa mbele ya macho ya wote. Kisha, kwa kuona matendo mema ya Wakristo, watu wataweza kumtukuza “Baba aliye mbinguni” (Mt 5:16).

E. Zawadi ya Kristo: Ekaristi na Neno la Mungu

39. Zaidi ya tofauti za asili au utamaduni, changamoto kubwa kabisa inayotukabili sisi sote ni kutambua katika mwanadamu, aliyependwa na Mungu, msingi wa ushirika ambao huheshimu na huunganisha michango ya pekee ya tamaduni mbalimbali.[70] “Inatubidi tufungue kweli mipaka hii kati ya makabila, makundi ya kiukoo na dini mbalimbali ili zishiriki kwenye upendo wa Mungu.”[71] Watu, katika tofauti za asili, tamaduni, lugha na dini zao, wanaweza kuishi pamoja kwa maelewano.

40. Kwa kweli, Mwana wa Mungu ameweka hema lake miongoni mwetu; amemwaga damu yake kwa ajili yetu. Kwa mujibu wa ahadi yake ya kubaki nasi hadi ukamilifu wa dahari (rej. Mt 28:20), anajitoa mwenyewe kwetu kila siku kama lishe katika Ekaristi na katika Maandiko. Katika Mausia yangu ya Kitume baada ya Sinodi iitwayo Verbum Domini, niliandika kwamba “Neno na Ekaristi vimeunganika kwa kina hivi kwamba hatuwezi kuelewa kimoja bila kingine: Neno la Mungu huchukua mwili kisakramenti katika tukio la Ekaristi: Ekaristi inafungua mlango wa kuelewa Maandiko, kama vile Maandiko kwa upande wake huangazia na kufafanua fumbo la Ekaristi.”[72]

41. Maandiko Matakatifu hushuhudia kwamba damu aliyomwaga Kristo kwa ajili yetu huwa, kwa njia ya Ubatizo, msingi na pingu ya udugu mpya. Udugu huo ni kinyume kabisa na utengano, ukabila, ubaguzi wa rangi na kiburi cha kikabila (rej. Gal 3:26-28). Ekaristi ni nguvu ambayo huleta pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika na kawadumisha katika umoja,[73] “kwani katika mishipa yetu inazunguka Damu yenyewe ya Kristo, ambaye hutufanya watoto wa Mungu, wanafamilia ya Mungu.”[74] Tunapompokea Yesu katika Ekaristi na katika Maandiko, tunatumwa ulimwenguni kumtangaza Kristo kwa kujiweka sisi wenyewe kama watumishi wa wengine (rej. Yn 13:15; 1Yoh 3:16).[75]

 

2. KUISHI KWA MAELEWANO

A. Familia

42. Familia ndiyo “hekalu la uhai” na chembe hai ya jamii na ya Kanisa. Ni hapa ambapo “sura za watu huundwa, ni hapa ambapo wanafamilia hupata mafundisho ya msingi. Wanajifunza kupenda kwa kadiri wanavyopendwa bila masharti, wanajifunza kuwaheshimu wengine kwa kadiri wanavyoheshimiwa, wanajifunza kujua uso wa Mungu kwa kuwa wanapokea ufunuo wa kwanza wa uso huo kutoka kwa baba na mama ambao wanawajali kikamilifu. Kila mara yanapokosekana mambo hayo ya msingi, jamii nzima huteseka kutokana na ukatili huo na huwa chanzo na chimbuko la ziada ya ukatili.”[76]

43. Familia ni mahali panapofaa pa kujifunzia na kuzoeshwa utamaduni wa msamaha, amani na upatanisho. “Katika maisha bora ya kifamilia tunaonja baadhi ya mambo yaliyo muhimu kwa amani: haki na upendo kati ya ndugu, kazi ya mamlaka kama inavyooneshwa na wazazi, huduma yenye upendo kwa wanafamilia ambao ni dhaifu zaidi kwa sababu ya udogo, maradhi, au uzee, kusaidiana katika mahitaji ya maisha, utayari wa kuwapokea wengine na, ikibidi, kuwasamehe. Kwa sababu hii, familia ndiyo mlezi wa kwanza wa amani na nafasi yake haiwezi kuchukuliwa na wengine.”[77] Kwa mujibu wa umuhimu wake wa pekee na kutokana na matishio mbalimbali yanayoinyemelea – kuharibiwa kwa dhana yenyewe ya ndoa na familia, kudharau uzazi na kufanya utoaji wa mimba kuwa jambo jepesi, kutalikiana kirahisi tu, na “maadili mapya” ya kwamba ukweli ni nionavyo mimi (relativism) – familia inahitaji kukingwa na kutetewa,[78] ili iweze kuipa jamii huduma inayoitazamia, yaani kutoa watu wanaoweza kujenga mazingira ya jamii yenye amani na maelewano.

44. Basi, nazitia moyo kabisa familia zichote mang’amuzi na nguvu kutoka kwenye sakramenti ya Ekaristi, ili kuuishi ule upya wa kina ulioletwa na Kristo katika kiini cha maisha ya kila siku, upya wa maisha unaomwongoza kila mtu kuwa shahidi mwenye uwezo wa kuangaza katika mazingira yake ya kazi na katika jamii kwa ujumla. “Upendo kati ya mwanamume na mwanamke, ukaribishaji wa uhai, na kazi ya malezi ya watoto ni mambo ambamo kwa namna ya pekee Ekaristi inaweza kuionyesha nguvu yake ya kubadilisha maisha na kuyapatia maana yake kamili.”[79] Ni wazi kwamba kushiriki katika Ekaristi siku ya Dominika ni jambo linalodaiwa na dhamiri ya kikristo na wakati huohuo husaidia kuiunda.[80].

45. Zaidi ya hayo, kuipa sala – iwe ya binafsi ama ya kijumuiya – nafasi yake sahihi katika familia inamaanisha kuuheshimu msingi muhimu kabisa wa mtazamo wa kikristo kuhusu maisha: ukipaumbele (primacy) wa neema. Sala daima hutukumbusha ukipaumbele wa Kristo na, kilichounganika na hili, ukipaumbele wa maisha ya utu wa ndani na utakatifu. Mazungumzano na Mungu hufungua moyo kwa chemchemi za neema na huruhusu neno la Kristo kututiririkia na nguvu zake zote. Kwa hiyo, ndani ya familia inahitajika uzoefu wa kudumu katika kusikiliza na kusoma kwa makini Maandiko Matakatifu.[81]

46. Zaidi ya hayo, “utume wa kulea wa familia ya Kikristo” ni “huduma kweli, ambayo kwa njia yake Injili inatangazwa na kuenezwa, ili maisha ya familia yenyewe yawe safari ya imani na kwa namna fulani mfumo wa kuingizwa katika Ukristo na shule ya kumfuata Kristo. Katika familia inayoifahamu zawadi hii, kama Papa Paulo VI alivyoandika, ‘wanafamilia wote huinjilisha na huinjilishwa’. Kwa mujibu wa huduma yao ya kulea, wazazi ni, kwa njia ya ushahidi wa maisha yao, watangazaji wa kwanza wa Injili kwa watoto wao ... wanakuwa wazazi kamili, katika maana kwamba wazazi siyo tu wa maisha ya kimwili lakini pia wa maisha ambayo, kwa njia ya kufanyiwa upya na Roho, hububujika kutoka Msalaba na Ufufuko wa Kristo.”[82]

B. Wazee

47. Katika Afrika, wazee hupewa heshima ya pekee. Hawaondolewi kwenye familia au kuwekwa pembezoni kama ilivyo kwenye tamaduni zingine. Kinyume chake, wanaheshimika na kuunganika kikamilifu ndani ya familia zao, ambamo wao ni kama kilele chake. Jambo hilo zuri katika mazingira ya Afrika linapaswa kuwahamasisha jamii za Magharibi kuwatendea wazee kwa heshima kubwa zaidi. Maandiko Matakatifu husema mara nyingi juu ya wazee. “Ustadi wa uzoefu ni taji ya wazee na utukufu wao ni kumcha Bwana” (YbS 25:6). Uzee, licha ya udhaifu ambao huambatana nao, ni zawadi ambayo ni lazima ipokelewe kila siku kwa utayari wenye utulivu mbele ya Mungu na jirani. Ni wakati pia wa hekima, kwani kuishi miaka mingi hufundisha ukuu na udhaifu wa maisha. Kama mtu wa imani, mzee Simeoni hutangaza kwa furaha na hekima kuyaaga maisha: si kwa huzuni, bali kwa kuimba wimbo wa shukrani kwa Mwokozi wa ulimwengu (rej. Lk 2:25-32).

48. Kwa sababu ya hekima hii, ambayo wakati mwingine imepatikana kwa gharama kubwa, wazee huweza kuwa na ushawishi wa namna mbalimbali kwa kuzivuta familia. Uzoefu wao moja kwa moja huwaongoza kuziba pengo lililopo kati ya kizazi na kizazi, bali huthibitisha pia haja ya watu kutegemeana. Wao ni hazina kwa kila mwanafamilia, hasa kwa wanandoa vijana na kwa watoto ambao huona kwao uelewa na upendo. Siyo tu kwamba wametupatia uhai, bali wanachangia pia kwa matendo yao kuijenga familia yao (rej. Tit 2:2-5), na kwa njia ya sala zao na maisha yao ya imani, wanawatajirisha kiroho wanafamilia wote na jumuiya kwa ujumla.

49. Afrika, udumifu na utaratibu wa kijamii mara nyingi bado umewekwa mikononi mwa baraza la wazee au watemi wa jadi. Kwa njia ya mfumo huo, wazee wanaweza kuchangia kwa ufanisi katika kujenga jamii yenye haki zaidi, na ambayo huendelea, siyo kwa kutegemea mitindo inayoweza kuwa hatari, bali kwa kufuata hatua kwa hatua na kwa msimamo wa hekima na busara. Kwa namna hiyo, wazee wataweza kushiriki kupatanisha watu binafsi na jumuiya kwa kutumia busara yao na uzoefu.

50. Kanisa huwaheshimu sana wazee. Pamoja na Mwenyeheri Yohane Paulo II, napenda niyarudie maneno haya: “Kanisa linawahitaji ninyi! ... Lakini jamii ya kiraia nayo inawahitaji! ... Muweze kutumia kwa ukarimu muda mlio nao na karama mlizopewa na Mungu! Saidieni kutangaza Injili ... Mtenge muda maalumu na nguvu kwa ajili ya kusali.”[83]

C. Wanaume

51. Katika familia, wanaume wamepokea utume wa pekee. Kwa nafasi yao kama waume na baba, wanatimiza wajibu muhimu wa kuipatia jamii tunu inazohitaji kwa njia ya mahusiano ya ndoa na malezi ya watoto.

52. Katika umoja na mababa wa Sinodi, ninawatia moyo akina baba Wakatoliki, ili ndani ya familia zao, wawe na mchango wa kweli katika malezi ya kiutu na ya kikristo ya watoto wao, na katika kuukaribisha na kuulinda uhai tangu kutungwa mimba.[84] Ninawaalika kuujenga mtindo wa kikristo wa maisha, wenye mizizi na msingi katika upendo (rej. Efe 3:17). Pamoja na Mtakatifu Paulo, ninawahimiza tena: “Wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake ... waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa” (Efe 2:25.28-29). Msiogope kuonyesha kwa vitendo kwamba hakuna upendo mkubwa zaidi ya ule wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya anaowapenda (rej. Yn 15:13), yaani, kwanza kabisa, kwa mke wake na watoto. Jengeni mazingira ya furaha nyumbani mwenu! Ndoa ni “zawadi kutoka kwa Mungu”, kwa maneno ya Mtakatifu Fulgentius wa Ruspe.[85] Ushahidi wenu kwa heshima ya kila mwanadamu isiyoweza kamwe kuvunjwa utasaidia kama dawa kwa utendaji wa kitamaduni ambao uko kinyume na Injili na unaowagandamiza hasa akina mama.

53. Kwa kuonyesha na kuishi hapa duniani ubaba wa Mungu (rej. Efe 3:15), mnaitwa kuhakikisha makuzi binafsi ya wanafamilia wote, ambayo ni chimbuko na nyenzo yenye ufanisi mkubwa katika kuifanya jamii iwe ya kiutu na mahali pa kukutana vizazi tofauti tofauti.[86] Kwa nguvu yenye uumbaji ya Neno la Mungu lenyewe,[87] dhamiri ya kuwajibika ikue hadi kufikia hatua ya kushiriki kiutendaji katika Kanisa. Kanisa linahitaji mashahidi wa imani ambao kweli wanaamini na ambao watakuza upatanisho, haki na amani,[88] na watatoa mchango wao wa motomoto na ujasiri ili kuyageuza mazingira ya maisha yao wenyewe na jamii kwa ujumla. Ninyi ndio mashahidi hawa kwa njia ya kazi zenu, ambazo huwawezesha kuzitunza familia zenu na ninyi wenyewe pia. Cha zaidi, kwa kutolea kazi hii kwa Mungu, mnashiriki ile kazi ya ukombozi ya Yesu Kristo ambaye aliipa heshima kubwa kazi kwa kufanya kazi kwa mikono yake Nazareti.[89]

54. Ubora na uwezo wa kuangaza wa maisha yenu ya kikristo hutegemea maisha ya sala ya kina, inayolishwa na Neno la Mungu na masakramenti. Kwa hiyo muwe macho katika kutunza uhai wa kipengele hiki cha wajibu wenu wa kikristo; ni hapo ambapo ushahidi wenu wa imani katika kazi za kila siku na ushiriki wenu katika harakati za kikanisa hupata chimbuko lake! Katika mchakato huu, mnakuwa pia mfano ambao vijana watataka kuuiga, na hivi mtaweza kuwasaidia kupokea wajibu wa maisha ya utu uzima. Msiogope kuongea nao juu ya Mungu na kuwaingiza, kwa mifano yenu wenyewe, katika maisha ya imani na uwajibikaji katika shughuli za kijamii au za huruma, na kwa njia hii kuwaongoza kutambua kwamba wameumbwa kweli kwa sura na mfano wa Mungu. “Alama za sura ya kimungu katika mwanadamu zinaweza kutambuliwa, lakini siyo katika hali ya mwili, ambao unaweza kuharibika, bali katika busara ya akili, katika haki, kiasi, ujasiri, hekima, na elimu.”[90]

D. Wanawake

55. Wanawake huko Afrika hutoa mchango mkubwa kwa familia, kwa jamii na kwa Kanisa kwa vipaji vyao vingi na karama zao za pekee. Kama Yohane Paulo II alivyosema: “mwanamke ni yeye ambaye ndani yake utaratibu wa upendo katika ulimwengu ulioumbwa wa wanadamu huchukua mizizi kwanza.”[91] Kanisa na jamii huhitaji wanawake wazichukue nafasi zao kikamilifu katika ulimwengu “ili watu wote waweze kuishi ulimwenguni bila kupoteza kabisa utu wao.”[92]

56. Ingawa ni ukweli usiopingika kwamba katika baadhi ya nchi za Kiafrika kuna hatua za kimaendeleo zilizochukuliwa kwa kuendeleza wanawake na elimu yao, hata hivyo, kwa jumla, bado heshima ya wanawake na haki zao kama pia mchango wao ulio wa msingi kwa familia na kwa jamii havijakubaliwa kikamilifu au kuthaminiwa. Kwa hiyo wanawake na wasichana mara nyingi wanapewa fursa chache zaidi kuliko wanaume na wavulana. Bado kuna mazoea mengi mno ya kuwabeza na kuwadhalilisha wanawake kwa kisingizio cha mapokeo ya mababu. Pamoja na mababa wa Sinodi, ninawaalika kwa msisitizo Wakristo wote kupiga vita matendo yote ya ukatili dhidi ya wanawake, kusema juu ya haya na kuyalaumu.[93] Katika hilo, ingefaa mienendo iliyo ndani ya Kanisa lenyewe iwe mfano kwa jamii kwa ujumla.

57. Nilipoitembelea Afrika, nilisisitiza kwamba: “ni lazima kuutambua, kuushuhudia na kuutetea usawa wa heshima kati ya mwanamume na mwanamke: wote ni binadamu, tofauti kabisa na viumbe vingine hai ulimwenguni.”[94] Kwa bahati mbaya, mabadiliko ya namna ya kufikiri katika suala hilo ni polepole mno. Kanisa lina wajibu wa kuchangia katika kumtambua na kumkomboa mwanamke kwa kufuata mfano wa Kristo aliyewathamini wanawake (rej. Mt 15:21-28; Lk 7:36-50; 8:1-3; 10:38-42; Yn 4:7-42). Kutengeneza mazingira ambapo wanawake huweza kutoa sauti yao na kuonyesha vipaji vyao kwa njia ya miradi inayoimarisha thamani yake, kujiamini kwake na upekee wake, kungewawezesha wanawake kuchukua nafasi katika jamii sawa kama ile ya wanaume – bila fujo, na bila kusawazisha ule upekee wa kila mmoja – kwa kuwa wote wawili, wanaume na wanawake ni “sura” ya Muumba (rej. Mwa 1:27). Maaskofu waweze kutia moyo na kuendeleza malezi ya wanawake ili wenyewe waweze kuchukua “nafasi yao ya pekee ya uwajibikaji na ushiriki katika maisha ya kijumuiya ya jamii na ... ya Kanisa.”[95] Kwa njia hiyo wanawake watachangia katika kuifanya jamii iwe ya kiutu.

58. Ninyi, akina mama Katoliki, mnaingia katika mapokeo ya kiinjili ya wale wanawake waliomsaidia Yesu na mitume (rej. Lk 8:3)! Katika Kanisa mahalia, ninyi ni kama “uti wa mgongo”,[96] kwa sababu idadi yenu, na uwepo wenu hai na vyama vyenu ni tegemeo kubwa kwa utume wa Kanisa. Amani inapotishiwa, haki inapodharauliwa, umasikini unapoongezeka, ninyi mnasimama kuitetea heshima ya binadamu, familia na tunu za dini. Roho Mtakatifu aweze kuwaibua katika Kanisa bila kukoma wanawake watakatifu na jasiri, ambao wanaweza kutoa mchango wao wa kiroho wenye thamani kubwa kwa maendeleo ya jumuiya zetu!

59. Wapendwa mabinti wa Kanisa, kaeni daima katika shule ya Kristo, kama Maria wa Betania, ili mjifunze kulitambua Neno lake (rej. Lk 10:39). Mkue katika elimu ya katekisimu na mafundisho ya Kanisa kuhusu jamii, ili mjipatie kanuni ambazo zitawasaidia katika kutenda kama wafuasi wa kweli. Hivyo mtaweza kushiriki kwa utambuzi katika miradi mbalimbali inayowahusisha wanawake. Endeleeni kuutetea uhai, kwa sababu Mungu amewafanya milango ya uhai. Kanisa daima litakuwa tegemeo lenu. Wasaidieni wasichana kwa ushauri na mifano yenu, ili wayaendee maisha ya utuuzima kwa utulivu. Saidianeni! Onesheni heshima kwa walio wazee miongoni mwenu. Kanisa linawategemea ninyi ili kuunda “ikolojia ya kibinadamu”[97] kwa njia ya upendo na upole wenu, moyo wa kukaribisha na utulivu, na hatimaye kwa huruma, tunu ambazo mnafahamu namna ya kuziwasilisha kwa watoto wenu, tunu ambazo ulimwengu unazihitaji sana. Kwa njia hii, kwa utajiri wa zawadi zenu zinazotokana na upekee wenu kama wanawake,[98] mtaendeleza upatanisho wa watu na jumuiya.

E. Vijana

60. Vijana ndio walio wengi katika idadi ya watu barani Afrika. Ujana huu ni zawadi na hazina kutoka kwa Mungu ambayo kwayo Kanisa zima linatoa shukrani kwa Bwana wa uhai.[99] Vijana ni lazima wapendwe, wathaminiwe na waheshimiwe. “Ingawa mara nyingine wanaweza wasieleweke, vijana wanaonyesha kuwa na hamu kutoka kwa ndani ya kutafuta tunu za kweli ambazo hupata ukamilifu wake katika Kristo. Si Kristo aliye siri ya uhuru wa kweli na furaha ya kina ya moyo? Si Kristo aliye rafiki mkuu na mlezi wa urafiki wote wa kweli? Kama Kristo akioneshwa kwa vijana kama alivyo kweli, wanamwonja kama jibu la kufaa na wanaweza kuupokea ujumbe wake, hata kama una masharti makali unatangaza Msalaba.”[100]

61. Nikiwafikiria vijana, katika Mausia ya Kitume baada ya Sinodi Verbum Domini, nimeandika maneno haya: “Ujana ni muda ambapo maswali juu ya maana ya maisha na juu ya mwelekeo wake kwa mmoja huibuka kwa nguvu kabisa na kwa unyofu Mungu peke yake anaweza kutoa majibu ya kweli kwa maswali haya. Kuwajali vijana kunadai ujasiri na uwazi katika kuutangaza ujumbe; inatupasa kuwasaidia vijana kuyafahamu na kuyazoea Maandiko Matakatifu ili yawe kama dira inayoelekeza njia ya kufuata. Vijana wanahitaji mashahidi na walezi watakaotembea nao, watakaowaongoza kwenye kuipenda Injili na kuishirikishana, hasa na vijana wenzao, na kwa namna hiyo wenyewe watakuwa wajumbe wa kweli na wakuaminika.”[101]

62. Katika Kanuni yake, Mtakatifu Benedikto anamtaka abate wa monasteri awasikilize walio na umri mdogo zaidi. Kama asemavyo: “Mara nyingi Bwana anamfumbulia yule aliye kijana lililo jema zaidi”.[102] Kusiachwe kuwahusisha vijana moja kwa moja katika maisha ya jamii na ya Kanisa, ili wasishikwe na hisia za kushindwa na za kukataa wanapokabiliana na hali ya kutoweza kupanga maisha yao ya mbele, hasa katika hali zile ambapo vijana wako katika mazingira hatarishi kwa sababu ya kukosa malezi, kukosa ajira, unyonywaji wa kisiasa na namna mbalimbali za kuwa tegemezi.[103]

63. Wapendwa vijana, changamoto wa kila aina zinaweza kuwajaribu: itikadi, makundi, pesa, madawa ya kulevya, uasherati, ukatili... Muwe macho: wale wanaopendekeza mambo haya kwenu wanataka kuwaharibia maisha yenu ya baadaye! Licha ya magumu, msikate tamaa na msiyaache malengo yenu, ari na udumifu katika malezi yenu ya utu, akili na roho! Ili kupata mang’amuzi, nguvu inayohitajika na uhuru wa kuweza kukabiliana na mashinikizo hayo, ninawapa moyo ili mmweke Yesu Kristo kati ya maisha yenu yote kwa njia ya sala, lakini pia kwa njia ya kujifunza Maandiko Matakatifu, ya kupokea sakramenti mara kwa mara, kulelewa katika mafundisho ya Kanisa kuhusu jamii, na pia kwa njia ya ushiriki wenu hai na wa motomoto katika makundi ya kikanisa na vyama vya kitume. Kuzeni ndani yenu tamaa ya udugu, haki na amani. Mustakabali uko mikononi mwa wale ambao hupata sababu za maana kwa kuishi na kwa kuwa na kutumaini. Mkitaka, mustakabali uko mikononi mwenu, kwa sababu zawadi ambazo Bwana amewagawia kila mmoja wenu, zikiwa zimeimarishwa kwa kukutana kwenu na Kristo, zinaweza kuleta matumaini ya kweli ulimwenguni![104]

64. Inapofika wakati wa kuchagua hali ya maisha, mnapojikuta mnafikiria juu ya suala la kujiweka wakfu kikamilifu kwa Kristo – katika huduma ya kipadre au maisha ya wakfu – mgeukieni yeye, mchukueni kama mfano wa kuigwa, sikilizeni Neno lake na muwe na kawaida ya kulitafakari. Wakati wa homilia ya Misa ya ufunguzi wa kipindi changu cha upapa, nilikuambieni maneno ambayo nataka kuyarudia sasa, kwa sababu bado ni muda mwafaka kuyasema: “Kama tukimkaribisha Kristo katika maisha yetu, hatupotezi kitu, hakuna, hakuna kabisa hata kitu kimoja kinachofanya maisha huru, mazuri na bora ambacho kitaenda kupotea. Hakuna! Katika urafiki huu tu milango ya maisha inafunguliwa wazi. Ni katika urafiki huu tu uwezo mkuu wa maisha ya mtu hufunuliwa kikwelikweli ... Wapendwa vijana: Msimwogope Kristo! Hanyang’anyi chochote, na anawapatieni kila kitu. Anayejitoa kwake, hupokea mara mia kutoka kwake. Ndiyo, fungueni, fungueni wazi kabisa milango ili Kristo aingie – na mtapata maisha ya kweli.”[105]

F. Watoto

65. Kama vile vijana, watoto pia ni zawadi ya Mungu kwa wanadamu, hivyo ni lazima wawe ndio lengo la kuhangaika kwa familia zao, Kanisa, jamii na serikali, kwa sababu ndio chanzo cha matumaini na maisha yaliyofanywa upya. Mungu yu karibu nao kwa namna ya pekee na maisha yao ni ya thamani machoni pake, hata wakati ambapo mazingira huonekana magumu au hayawezekaniki (rej. Mwa 17:17-18; 18:12; Mt 18:10).

66. Kwa kweli, “kwa mujibu wa haki ya kuishi, kila mwanadamu asiye na hatia ana haki sawa na wengine. Usawa huu ndio msingi wa mahusiano mengine yote ya kweli ya kijamii. Mahusiano hayo ili yawe ya kweli, ni lazima yawe yana msingi katika ukweli na haki, kwa kumtambua na kumkinga kila mtu kama nafsi na siyo kama kitu cha kutumiwa.”[106]

67. Kama hivi ndivyo, basi, kwa nini tusikemee na kushtaki kwa nguvu matendo yasiyovumilika wanayofanyiwa watoto wengi sana barani Afrika?[107] Kanisa ni mama na lisingeweza kumwacha hata mmoja wao. Ni jukumu letu kuruhusu mwanga wa Kristo ung’ae katika maisha yao kwa kuwapa upendo wake, ili waweze kumsikia akiwaambia: “Wewe ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda” (Isa 43:4). Mungu anataka kila mtoto awe na furaha na tabasamu, na upendeleo wake uwe juu yao, “kwa maana watu walio kama hao ufalme wa Mungu ni wao” (Mk 10:14).

68. Kristo Yesu daima alionyesha upendo wake wa upendeleo kwa wadogo (rej. Mk 10:13-16). Injili yenyewe imejaa mpaka ndani na ukweli juu ya watoto. Ni kitu gani hasa kinachomaanishwa na maneno haya: “msipoongoka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbingu” (Mt 18:3)? Yesu hawafanyi watoto kuwa mfano wa kuigwa, hata kwa watu wazima? Watoto wana kitu ambacho ni lazima wawe nacho wale ambao wanataka kuingia katika ufalme wa mbingu. Mbingu inaahidiwa kwa wasio na makuu, kama watoto, kwa wote ambao, kama watoto, wamejaa roho ya kujiachia kwa kumtegemea Mungu, usafi na wema mkubwa. Wao peke yao ndio wanaoweza kumwona Mungu kama Baba na kuwa, kwa njia ya Yesu, watoto wa Mungu. Watoto wa wazazi wetu, Mungu anatutaka sisi wote tuwe wanae wa kambo kwa neema![108]

 

3. MTAZAMO WA KIAFRIKA KUHUSU MAISHA

69. Katika mtazamo wa Kiafrika wa ulimwengu, uhai, au maisha, unatazamwa kama kitu kinachokumbatia na kujumuisha wahenga, wazima wanaoishi sasa na wale watakaozaliwa, uumbaji wote na viumbe vyote: vinavyoongea na visivyoongea, vinavyofikiri na visivyofikiri. Ulimwengu unaoonekana na usioonekana unachukuliwa kama mahali pa kuishi kwa ajili ya watu, lakini pia kama mahali pa kuungana ambapo vizazi vilivyopita huungana na vizazi vilivyopo, vyenyewe vikiwa mama wa vizazi vijavyo. Uwazi mpana huu wa moyo na roho katika mapokeo ya Kiafrika hukuwekeni tayari, wapendwa kaka na dada, kusikia na kupokea ujumbe wa Kristo, na kulifahamu fumbo la Kanisa, ili kuthamini uhai wa mwanadamu kikamilifu, pamoja na mazingira yanayosaidia uhai huo kuchanua kwa nguvu zote.

A. Kulinda uhai

70. Miongoni mwa mikakati iliyowekwa kuhusiana na kulinda uhai wa mwanadamu barani Afrika, wanasinodi walizichambua jitihada zilizofanywa na taasisi za kimataifa kwa kusaidia mambo fulani ya maendeleo.[109] Hata hivyo waliona kwa wasiwasi kwamba katika mikutano ya kimataifa msimamo wa kimaadili hauko wazi, mpaka kuwa na lugha za kuchanganya zinazobeba itikadi ambazo zinapingana na mafundisho Katoliki ya maadili. Kanisa daima hujali maendeleo ya jumla “ya kila mtu na ya mtu mzima”, kama Papa Paulo VI alivyosema.[110] Kwa sababu hiyo Mababa wa Sinodi walitaka kuyasisitiza mambo yanayozua wasiwasi na maswali kwenye baadhi ya hati za taasisi za kimataifa, hasa zile zinazohusu afya ya uzazi ya wanawake. Msimamo wa Kanisa kuhusu utoaji mimba ni wazi. Mtoto ndani ya tumbo la uzazi la mama yake ni uhai wa mtu ambao ni lazima ulindwe. Utoaji mimba, ambao ni uuaji wa mtoto asiye na hatia ambaye hajazaliwa bado, ni kinyume cha mapenzi ya Mungu, kwa sababu thamani na heshima ya uhai wa mtu ni lazima ilindwe kutoka kutungwa mimba hadi kifo asilia. Kanisa barani Afrika na visiwa jirani lazima lijitahidi kusaidia na kuwa pamoja na wanawake na wanandoa wanaoshawishika kutoa mimba, na pia kuwa karibu na wale ambao wamekwisha fanya tendo hilo la kuhuzunisha, ili kuwalea wauheshimu uhai. Kanisa linatambua ujasiri wa serikali ambazo zimetunga sheria dhidi ya utamaduni wa kifo – ambao utoaji mimba ni kielelezo cha kusikitisha mno – wakiuenzi utamaduni wa uhai.[111]

71. Kanisa linajua kwamba ni wengi wale ambao – binafsi, mashirika, taasisi maalum au vyama, na serikali – hukataa mafundisho safi kuhusu suala hilo. “Tusiogope uadui au kukosa umaarufu, tunapokataa kulegeza msimamo kwa namna yoyote ile ambao utatufanya sisi tufuatishe namna ya kufikiri ya ulimwengu huu (rej. Rum 12:2). Ni lazima tuwe ulimwenguni lakini si wa ulimwengu (rej. Yn 15:19; 17:16), tukichota nguvu zetu kutoka kwa Kristo, ambaye kwa kifo chake na ufufuko wake ameushinda ulimwengu (rej. Yn 16:33).”[112]

72. Maisha ya watu Afrika yanabeba mzigo wa vitisho vikubwa sana.. Lazima kuipigia kelele, hapa, kama vile kwingineko, madhara ya madawa ya kulevya na unywaji wa pombe wa kupindukia vinavyoharibu uwezo wa mwanadamu katika bara la Afrika na kuwaathiri vijana kwa namna ya pekee.[113] Malaria,[114] na kifua kikuu pia na UKIMWI, vinawatafuna watu wa Afrika na kuathiri kwa kiwango kikubwa sana hali yao ya kijamii na kiuchumi. Tatizo la UKIMWI, kwa namna ya pekee, waziwazi linahitaji majibu yanayotegemea madaktari na madawa. Hata hivyo, hilo halitoshi, kwa sababu tatizo ni la ndani zaidi. Juu ya yote, ni tatizo la kimaadili. Kubadili tabia kunakohitajika – kwa mfano, kujinyima ngono[kabla ya ndoa], kuacha ngono zembe, uaminifu ndani ya ndoa – hatimaye kunatupeleka kwenye suala la maendeleo ya jumla, ambayo hudai Kanisa liwe na mtazamo na jibu pana linalohusisha mambo yote. Kwa maana kama tukitaka ufanisi, kinga dhidi ya UKIMWI lazima iwe na msingi katika malezi ya kijinsia ambayo yenyewe yawe yamesimikwa katika elimu-binadamu (anthropolojia) iliyo na mizizi katika sheria ya asili (natural law) na kuangaziwa na Neno la Mungu na mafundisho ya Kanisa.

73. Kwa jina la uhai – ambao ni wajibu wa Kanisa kuutetea na kuulinda – na kwa kuungana na Mababa wa Sinodi, kwa mara nyingine ninaziunga mkono na kuzielekea taasisi zote za Kanisa na vyama mbalimbali ambavyo hufanya kazi katika uwanja wa afya, hususan kuhusu UKIMWI. Mnafanya kazi nzuri sana na muhimu. Naziomba taasisi za kimataifa kuwatambueni na kuwapa msaada, kwa kuuheshimu upekee wenu na kutenda katika roho ya ushirikiano. Mara nyingine tena nazitia moyo zile taasisi na programu za utafiti wa tiba na madawa unaofanywa kwa lengo la kuyafuta magonjwa yaliyoenea sana. Msibakize jitihada yoyote katika kufikia mapema iwezekanavyo matokeo ya kufa, mkisukumwa na upendo kwa thamani kubwa ya uhai.[115] Tunaomba mpate ufumbuzi na mmpatie kila mmoja uwezekano wa kupata matibabu na dawa, mkizingatia mazingira yalivyo ya wasiwasi! Toka muda mrefu, Kanisa linaunga mkono jitihada ya kuwapatia wahusika wote tiba bora kwa gharama ya chini.[116]

74. Kutetea uhai kunadai pia kuufuta ujinga kwa njia ya uelimishaji na malezi bora ambayo humlenga mtu katika ujumla wake. Kwa kipindi chote cha historia yake, Kanisa Katoliki limeonyesha kujali kwa namna ya pekee malezi. Daima Kanisa limewafungua macho wazazi, likiwapatia ujasiri na msaada katika kuchukua wajibu wao kama walezi wa kwanza wa watoto wao katika maisha na katika imani. Katika Afrika, taasisi za elimu za Kanisa – kama vile shule zake, shule za bweni, shule za sekondari, vyuo vya ufundi, vyuo vikuu na kadhalika – zinawapa nafasi watu waweze kufaidi zana za kujifunzia, bila ubaguzi kwa misingi ya uzawa, uwezo wa kiuchumi, au dini. Kanisa hutoa mchango wake ili kuwezesha karama ambazo Mungu kaziweka katika moyo wa kila mtu zithaminiwe na zizae matunda. Mashirika mengi ya kitawa yalianzishwa kwa lengo hilo. Watakatifu wasiohesabika wametambua kwamba kuwaongoza watu kwenye utakatifu kabla ya yote kunamaanisha kuikuza heshima yao kwa njia ya malezi.

75. Wanasinodi waliona kwamba Afrika, kama vile na kokote ulimwenguni, malezi yameingia utatani.[117] Walikazia hitaji la kuwa na ratiba ya malezi inayounganisha imani na akili (faith and reason) ili kuwatayarisha watoto na vijana kwa maisha ya utuuzima. Misingi na vigezo safi vilivyowekwa kwa namna hiyo imara vitaweza kuwasaidia kufanya maamuzi ya kila siku katika maisha ya utuuzima, yahusuyo jamii, kazi na siasa.

76. Kutojua kusoma na kuandika ni kati ya vikwazo vikubwa vya maendeleo. Ni janga linalofanana na magonjwa yaliyoenea sana. Ni kweli, si kwamba kunaua moja kwa moja, lakini kunachangia kwa sehemu kubwa sana kumtenga mtu na kuwekwa pembezoni – jambo ambalo ni aina fulani ya kifo cha kijamii – na huzuia uwezekano wa kujipatia elimu. Kuwafundisha watu kusoma na kuandika huwafanya kuwa wanajamii kamili na kuwawezesha kutoa mchango wao katika kuijenga.[118] Kwa Wakristo, huwapatia ufunguo wa kuingia kwenye hazina isiyopimika ya Maandiko Matakatifu ambayo hulisha maisha yao ya imani.

77. Nazialika jumuiya na taasisi za Kikatoliki kushughulikia kwa ukarimu changamoto hii kubwa, ambayo ni karakana kwelikweli ambapo utu unajengwa, na kulingana na nyenzo zao, ninawaalika kuongeza bidii, peke yao au kwa kushirikiana na mashirika mengine, ili kuiendeleza miradi yenye ufanisi na zinazoendana na uhitaji wa watu. Jumuiya na taasisi za Kikatoliki zitaweza kushinda katika changamoto hii ikiwa tu zitaudumisha upekee wao wa kikanisa na kubaki waaminifu kabisa katika kuushika ujumbe wa Injili na kuizingatia karama ya mwasisi. Upekee huo wa Kikristo, ni mali yenye thamani ambayo ni lazima ihifadhiwe na kulindwa, chumvi isije kupoteza ladha yake na kuishia kukanyagwa chini ya miguu (rej. Mt 5:13).

78. Kwa hakika, ni lazima kuziamsha serikali ili zisaidie zaidi kusomesha. Kanisa linatambua na linaheshimu jukumu la serikali katika uwanja wa malezi. Hata hivyo, Kanisa, hukiri haki yake halali ya kushiriki, likitoa mchango wake wa pekee. Na inaonekana inafaa kuikumbusha serikali kwamba Kanisa lina haki ya kulea kwa mujibu wa taratibu zake na katika majengo yake. Hii ni haki ambayo ni sehemu ya uhuru wa kutenda “kwa kiasi kile kinachohitajika ili kuwafikishia watu ukombozi”.[119] Serikali nyingi za Kiafrika zinatambua nafasi za juu kabisa, na isiyotafuta faida, ya Kanisa katika kujenga Taifa lao, kutokana na miundombinu yake ya malezi. Kwa hiyo nawatia moyo kabisa watu wa serikali katika ari zao za kusaidia kazi hii ya malezi.

B. Kuheshimu Uumbaji na Mazingira (ecosystem)

79. Pamoja na mababa wa Sinodi, nawaalika wanakanisa wote kutenda na kuwa na msimamo unaopendelea uchumi unaojali maskini na unaopinga utaratibu usio wa haki ambao, kwa kisingizio cha kupunguza umaskini, mara nyingi umechangia kuuongeza umaskini huo. [120] Mungu ameipatia Afrika maliasili muhimu. Ukizingatia umaskini sugu wa watu wake, wahanga wa unyonyaji na ubadhirifu uliosababishwa na wenyeji au wageni, ufahari wa baadhi ya makundi ya watu hushtua dhamiri ya mtu. Makundi haya, yakiwa yamejipanga kutengeneza utajiri katika nchi zao, na si mara chache kwa kushirikiana na walioko madarakani Afrika, mara nyingi mno hujihakikishia usitawi wao binafsi kwa hasara ya usitawi wa watu wenyeji.[121] Likitenda kwa kushirikiana na makundi yote ya jamii ya kiraia, Kanisa ni lazima likemee utaratibu usio wa haki ambao huwazuia watu wa Afrika kuimarisha uchumi wao[122] na “kuendelea kadiri ya tabia ya utamaduni wao”.[123] Zaidi, ni jukumu la Kanisa kupigania ili “kila taifa liwe wakala mkuu wa uchumi wake na wa maendeleo yake ya kijamii ... na ili liweze kushiriki katika kuleta manufaa ya wote kama mwanafamilia hai na mwenye kuwajibika katika jamii ya watu, kwa fursa sawa na mataifa mengine.”[124]

80. Baadhi ya wafanya biashara, serikali na makundi ya kifedha wanajihusisha na miradi ya unyonyaji ambayo huchafua mazingira na husababisha jangwa jinsi ambavyo haijawahi kutokea. Uharibifu mkubwa unafanywa kwa viumbe asilia, misitu, mimea na wanyama, na viumbe vingine vingi vipo katika hatari ya kupotea kabisa. Haya yote yanatishia mfumo mzima wa ikolojia, na hivyo kuhatarisha maisha ya wanadamu.[125] Ninaliomba Kanisa barani Afrika kuwahimiza viongozi wa kisiasa kulinda rasilimali hizi za msingi kama vile ardhi na maji kwa ajili ya maisha ya watu wa sasa na wa vizazi vijavyo[126] na kwa ajili ya amani kati ya watu.

C. Utawala bora wa serikali

81. Muundo wa kisiasa, ambao wajibu wake muhimu ni kuleta na kuongoza mfumo wa haki, unaweza kuwa kati ya zana zilizo muhimu zaidi kwa huduma ya upatanisho, haki na amani.[127] Mfumo huo, kwa upande wake, uko katika huduma ya “wito wa watu kuungana na kushirikiana”.[128] Ili kuweka mfumo huu katika vitendo, Kanisa barani Afrika lazima lisaidie kujenga jamii kwa kushirikiana na mamlaka ya serikali na taasisi za kijamii, ambazo hujishughulisha katika kujenga manufaa ya wote.[129] Viongozi wa jadi wana mchango chanya mkubwa katika kuujenga utawala bora. Kanisa, kwa upande wake, linawajibika kukuza ndani ya mipaka yake na ndani ya jamii utamaduni unaoheshimu utawala wa sheria.[130] Kwa mfano, uchaguzi huwa jukwaa la watu la kuelezea maamuzi yao kisiasa, na ni ishara ya uhalali kwa matumizi ya mamlaka. Chaguzi zinatoa fursa ya upekee kwa ajili ya kueleza maoni tofauti tofauti ya kisiasa kwa amani na utulivu, katika hali ya kuheshimu tofauti za maoni na tofauti za makundi ya kisiasa. Kusaidia ili chaguzi hizi ziiendeshwe vizuri, kutachochea na kutia moyo ushiriki hai na wa kweli wa raia katika maisha ya kisiasa na kijamii. Kushindwa kuiheshimu Katiba ya nchi, sheria au matokeo ya chaguzi, pale ambapo uchaguzi umekuwa huru, wa haki na wazi, kungebaini hitilafu kubwa sana katika utendaji wa serikali na kuashiria ukosefu wa umahiri katika kuongoza mambo ya umma.[131]

82. Leo, watu wengi wanaofanya maamuzi, wanasiasa na wachumi pia, wanadai kwamba wasidaiwe kitu na yeyote isipokuwa na wao wenyewe. “Wanafikiri wao tu wana haki, na mara nyingi wana matatizo makubwa katika kuwajibika kwa ajili ya maendeleo kwa ujumla yanayowahusu wao wenyewe na wengine pia. Kwa sababu hiyo ni muhimu kuichochea tafakari mpya juu ya namna haki zilivyosimikwa juu ya wajibu; bila kuwa hivyo, haki hizo zinageuzwa kuwa ubabe.”[132]

83. Kuongezeka kwa makosa ya jinai katika jamii za watu wanaozidi kuishi mijini ni suala linalowahangaisha sana wale wote wanaowajibika, pamoja na viongozi wa serikali. Basi, ni suala nyeti na la haraka kuiweka mifumo ya mahakama na ya magereza iliyo huru, ili kurudisha haki na kuwarekebisha wakosaji. Zaidi ya hayo, ni lazima kuyaacha kabisa “makosa yanayofanyika mahakamani pamoja na kuwatendea vibaya wafungwa, nafasi nyingi za kutozingatia sheria ambazo ni sawa na kuzivunja haki za binadamu,”[133] na vilevile kufunga watu bila kuwafikisha mahakamani, kabisa au kwa kuchelewa sana. “Kanisa barani Afrika ... linatambua utume wake wa kinabii mbele ya wale walioathiriwa na makosa ya jinai na mbele ya hitaji lao la upatanisho, haki na amani.”[134] Wafungwa ni binadamu ambao, licha ya makosa yao, wanastahili kutendewa kwa staha na heshima. Wanahitaji tuwahangaikie. Kwa sababu hiyo, Kanisa lazima liwe na mkakati wa kutoa huduma ya kichungaji magerezani, kwa ajili ya ustawi wa kimwili na wa kiroho wa wafungwa. Kazi hii ya kichungaji ni huduma kweli ambayo Kanisa hutoa kwa jamii, na ambayo ni lazima isaidiwe na Serikali kwa manufaa ya wote. Pamoja na wana Sinodi, ninaweka wazi mbele ya viongozi wa jamii hitaji la kufanya kila jitihada ili kuondoa adhabu ya kifo,[135] na pia la kuurekebisha mfumo mzima wa adhabu kwa lengo la kuzingatia heshima ya utu wa wafungwa. Wenye kutoa huduma ya kichungaji wana jukumu la kutafiti na kupendekeza kuhusu haki adilishi[yaani, haki inayolenga kurudisha heshima kwa kila mtu] kama njia na mchakato wa kukuza upatanisho, haki na amani, na kuwaingiza tena katika jumuiya wahanga na wakosaji.[136]

D. Wahamiaji, wasio kwao na Wakimbizi

84. Mamilioni ya wahamiaji, watu wanaokaa wasipostahili kukaa (wasio kwao) na wakimbizi wanatafuta nchi na mahali penye amani barani Afrika au katika mabara mengine. Ukubwa wa msafara huo, unaogusa mataifa yote, hufunua aina mbalimbali za umaskini mkubwa uliofichika mara nyingi kutokana na makosa katika uongozi wa umma. Maelfu ya watu wamejaribu na wanaendelea kujaribu kuvuka majangwa na bahari wakitafuta makimbilio yenye amani na ustawi, elimu bora na uhuru mkubwa zaidi. Kwa bahati mbaya, wakimbizi wengi na wasio kwao hukutana na kila aina ya ukatili na unyonyaji, hata kifungo au, mara nyingi mno, kifo. Baadhi ya serikali zimekabiliana na hali hii tete kwa kuweka sheria kandamizi.[137] Hali tete ya hawa watu maskini ingepaswa kuamsha huruma na mshikamano wa ukarimu wa wote; kinyume chake, mara nyingi hali hiyo inazaa woga na hofu. Wengi huwachukulia wahamiaji kama mzigo na huwatazama kwa kuwashuku, wakiwaona tu kama chanzo cha hatari, kukosa usalama na tishio. Mtazamo huu huamsha matendo ya kutovumiliana, chuki ya wageni na ubaguzi wa rangi. Matokeo yake, wahamiaji hawa wanalazimika, kwa njia ya utete wa hali yao, kufanya kazi zenye malipo duni ambazo mara nyingi hazina uhalali, zinazowanyenyekesha na kuwadhalilisha. Mbele ya hali hiyo, dhamiri ya mtu lazima isikitishwe sana tu. Kwa namna hiyo, uhamiaji ndani na nje ya bara huwa tatizo kubwa linalohusisha mambo mengi na ambalo huathiri kwa kiwango kikubwa raslimali watu ya Afrika, likipelekea kutetereka au kuharibika kabisa kwa familia.

85. Kanisa linakumbuka kwamba Afrika imekuwa mahali pa kukimbilia Familia Takatifu walipokuwa wakikimbia siasa wenye kumwaga damu wa Herode,[138] na kupatafuta mahali penye tumaini la kuwapa usalama na amani. Kanisa litaendelea kufanya sauti yake isikike na kujitahidi kuwatetea watu wote.[139]

E. Utandawazi na msaada wa kimataifa

86. Mababa wa Sinodi walieleza wasiwasi wao na mashaka yao kuhusu utandawazi. Tayari nimeangalisha kuhusu jambo hilo kama changamoto inayotakiwa kushughulikiwa. “Ukweli wa utandawazi kama mchakato, na kigezo cha maadili yake msingi, vinapatikana kwa kuzingatia umoja wa familia ya wanadamu na maendeleo yake katika wema. Kwa hiyo uwajibikaji wa kudumu unahitajika ili kukuza mtazamo wa kitamaduni wenye msingi wake katika kuzingatia utu wa kila nafsi wa na kijumuiya. Mtazamo huo, ambao utakuwa wazi kwa mambo yanayozidi yale ya ulimwengu huu, utasaidia kuongoza mchakato ya kuyaunganisha yote yaliyo ulimwenguni.”[140] Kanisa linategemea kwamba utandawazi wa mshikamano utafikia hatua ya kuingiza “katika mahusiano ya kibiashara kanuni ya kutenda bure (gratuitousness) na mantiki ya zawadi kama kielelezo cha udugu”,[141] huku tunakwepa kishawishi cha kuchukulia utandawazi kama namna ya kuweka mtazamo mmoja tu kuhusu maisha, utamaduni, siasa na uchumi, na kuendeleza maadili endelevu ya kuziheshimu hali mbalimbali za watu kwa faida ya ufanisi wa mshikamano wetu.

87. Utandawazi wa mshikamano tayari umeoneshwa kwa kiasi fulani kwa njia ya msaada wa kimataifa. Leo, habari za maafa huenea haraka ulimwenguni kote na mara nyingi hupelekea kuamsha hisia za huruma na matendo ya ukarimu. Kanisa hutoa huduma yenye upendo mkubwa kwa kutetea mahitaji halisi ya walengwa. Kanisa, kwa kutetea haki ya wahitaji na wale wasio na sauti, na kwa heshima na mshikamano ambao wanastahili, linaomba kwamba “taasisi za kimataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali wajitahidi kuwa wazi kabisa” katika kazi zao.[142]

 

4. MAZUNGUMZANO NA USHIRIKA KATI YA WAAMINI

88. Kama makundi mengi ya kijamii yanavyoonyesha, amani Afrika, kama vile kwingineko, inategemea mahusiano baina ya dini mbalimbali. Kwa hiyo ni muhimu kwa Kanisa kukuza mazungumzano kama utayari wa kiroho, ili waamini waweze kujifunza kufanya kazi pamoja, kwa mfano katika vyama vinavyotenda kwa haki na amani, katika roho ya kuaminiana na kusaidiana. Lazima familia zielimishwe kujifunza kusikia wengine kwa uangalifu, kuwa na roho ya udugu na kuheshimiana bila kuogopana.[143] Kitu kimoja tu ni cha lazima (Lk 10:42) na kinachoweza kutuliza kiu ya kila mtu ya umilele na matamanio ya wa binadamu wote ya umoja: upendo na kumtazama yeye ambaye Mtakatifu Augustino alimlilia kwa sauti: “Ukweli wa milele, Upendo wa kweli, Umilele mpendwa!”[144]

A. Mazungumzano ya kiekumeni (Ecumenical dialogue) na changamoto ya madhehebu mapya ya kidini

89. Kwa kuwakaribisha katika mkutano wa Sinodi ndugu zetu Wakristo – wa Orthodoksi, wa Koptiki Orthodoksi, wa Kilutheri, wa Anglikana, wa Methodisti, na kwa namna ya pekee Mheshimiwa sana (His Holiness) Abuna Paulos, Patriaki wa Kanisa la Tewahedo la Orthodoksi la Ethiopia, moja ya jumuiya za kikristo za kale zaidi barani Afrika – nilitaka kuweka wazi kwamba njia inayoelekea upatanisho ni lazima kwanza ipitie ushirika kati ya wafuasi wa Kristo. Ukristo uliogawanyika unabaki ni kikwazo, kwa kuwa, kwa vitendo, hupinga mapenzi ya Mwalimu wa Kimungu (rej. Yn 17:21). Mazungumzano ya kiekumeni, kwa hiyo, yataka kuongoza safari yetu ya pamoja kuelekea umoja wa kikristo, kama tunavyosikiliza kila mara neno la Mungu, tukiwa waaminifu kwa ushirika wa kidugu, kumega mkate na sala (rej. Mdo 2:42). Ninaomba jumuiya yote ya familia ya kikanisa – makanisa mahalia, taasisi za maisha ya wakfu, na vuguvugu na vyama vya waamini walei – kuchukua njia hii kwa ari kubwa zaidi, katika roho ya, na juu ya msingi wa, maelekezo ya Mwongozo wa Kiekumeni na kwa njia ya vyama mbalimbali vya kiekumeni vilivyopo. Naomba pia vingine vipya vianzishwe popote pale ambapo vinaweza kusaidia kwa ajili ya utume. Kwa pamoja tufanye kazi ya upendo na tuhifadhi urithi wa dini yetu, ambao kwa njia ya huo wanafunzi wa Kristo wanapata nguvu ya kiroho wanayohitaji ili kuijenga familia ya kibinadamu![145]

90. Katika miongo ya hivi karibuni, Kanisa Afrika limekuwa likijiuliza maswali mengi juu ya kuibuka na kukua kwa jumuiya zisizo za Kikatoliki ambazo wakati mwingine zinajulikana kama African Independent Chruches (Makanisa huru ya Kiafrika). Jumuiya hizo, ambazo mara nyingi hutokana na Makanisa ya kikristo ya kimapokeo na jumuiya za kikanisa, zinachukua vipengee vya tamaduni za kimapokeo za Kiafrika. Makundi haya yameonekana katika uwanja wa ekumeni. Wachungaji wa Kanisa Katoliki hawatakuwa na budi kuzingatia jambo hilo jipya lihusulo ukuzaji wa umoja wa kikristo Afrika, na hivi watatakiwa kupata majibu yatakayokidhi hali hii, kwa ajili ya uinjilishaji wa kina kama njia ya kueneza kwa ufanisi ukweli wa Kristo kwa watu wa Afrika.

91. Makundi ya mchanganyo-dini na vidhehebu mbalimbali vimeibuka Afrika katika miongo ya hivi karibuni. Wakati mwingine ni vigumu kupambanua kama ni kweli vya kikristo au kama ni matokeo tu ya kupagawa kwa kiongozi wao akidai kuwa na karama za pekee. Majina yao na misamiati yao huleta utata mara moja, na kuweza kuwapotosha hata watu wenye roho nyofu. Huu utitiri wa vidhehebu hutumia mwanya wa miundombinu ya kijamii isiyo kamili, mmomonyoko wa mshikamano wa kimapokeo wa kifamilia na upungufu wa katekesi, ili kujinufaisha kwa ujinga wa kidini wa watu, na kubandika jina la dini juu ya imani za kizushi za aina mbalimbali zisizo za kikristo. Wanaharibu amani ya wanandoa na ya familia kwa njia ya unabii na maono ya uongo. Hata wanawashawishi viongozi wa kisiasa. Teolojia ya Kanisa na huduma yake ya kichungaji lazima zibaini sababu ya jambo hili, siyo tu ili kuzuia waamini wasihamie kutoka parokia zetu kwenda kwenye vidhehebu hivyo, lakini pia ili kuweka msingi wa jibu la kichungaji kwa kivutio ambacho vidhehebu hivyo vinacho kwa watu. Kwa mara nyingine tena, hilo linaashiria hitaji la uinjilishaji wa kina wa roho ya Kiafrika.

B. Mazungumzano kati ya dini

1. Dini za kimapokeo ya Kiafrika

92. Kanisa huishi kila siku pamoja na wafuasi wa dini za kimapokeo za Kiafrika. Kwa kutilia mkazo uhusiano na wahenga, na aina ya ushenga kati ya mtu na Uwepo wa kimungu (Immanence), dini hizi ni rutuba nzuri ya kiutamaduni na kiroho ambamo kutoka humo Wakristo walio wengi huongoka na ambayo wanaendelea kuwa na mahusiano ya kila siku nayo. Ni jambo la maana kuchagua baadhi ya watu walioongoka wenye maarifa maalum, ambao wangeweza kulipatia Kanisa mwongozo katika kupata elimu sahihi na ya kina ya mila, utamaduni na dini za kimapokeo. Hii ingerahisisha kubainisha mambo ambayo ni tofauti kweli na imani ya kikristo. Ingesaidia pia kuweka wazi tofauti muhimu kati ya utamaduni na ibada na kuondoa yale mambo ya kishirikina ambayo husababisha mgawanyiko na kuharibu familia na jamii. Katika suala hili, Mtaguso Mkuu wa Vatikano ulifundisha kwamba Kanisa “linawahimiza wanae ili, kwa busara na mapendo, kwa njia ya dialogia na ushirikiano na wafuasi wa dini nyinginezo, watoe ushuhuda wa imani na wa maisha ya kikristo, na tena watambue, wahifadhi na kukuza mema ya kiroho na ya kimaadili, na tunu za kijamii na za kitamaduni, ambazo zapatikana kati ya wasio Wakristo.”[146] Ingesaidia kuonyesha hazina za maisha ya kisakramenti ya Kanisa na za karama zake za kiroho (spirituality) katika kina chake na kuzipitisha kwa ufanisi zaidi katika katekesi, kama Kanisa litaweza kuendeleza majifunzo ya kiteolojia ya mambo yale ya tamaduni za kimapokeo za Kiafrika yanayolingana na mafundisho ya Kristo.

93. Uchawi, ambao msingi wake ni dini za kimapokeo, kwa hivi karibuni hutiwa tena nguvu. Woga wa zamani unaibuka tena na unatengeneza pingu poozeshi za kutojiamini. Wasiwasi kuhusu afya, ustawi, watoto, hali ya hewa, na kujikinga na pepo wabaya mara nyingine hupelekea watu kukimbilia kwenye mazoezi fulani ya dini za kimapokeo za Kiafrika ambayo hayapatani na mafundisho ya kikristo. Tatizo la “kujisajili kuwili” – kwenye Ukristo na kwenye dini za kimapokeo za Kiafrika – linabaki ni changamoto. Kwa njia ya katekesi na utamadunisho wa kina, Kanisa huko Afrika linahitaji kuwasaidia watu kugundua ukamilifu wa tunu za Injili. Ni muhimu kuweka wazi maana ya kina ya mazoezi haya ya ushirikina kwa kuainisha mambo mengi ya kiteolojia, kijamii na kiuchungaji yanayohusu janga hili.

2. Uislamu

94. Mababa wa Sinodi walitilia mkazo kwamba uwepo wa Waislamu barani Afrika ni suala changamani (complexity). Katika baadhi ya nchi, mahusiano mazuri yapo kati ya Wakristo na Waislamu; katika nchi zingine, Wakristo mahalia wanachukuliwa kama raia wa daraja la pili, na Wakatoliki kutoka nje, watawa na walei, wanaona shida kupata visa na kibali cha kukaa nchini (residence permit); katika baadhi ya nchi, kuna tofauti ndogo kati ya uwanja wa kidini na uwanja wa kisiasa; mwishowe, i katika baadhi ya nchi, kuna hali ya chuki. Ninaliomba Kanisa, katika hali zote, kushikilia msimamo wa kuwaheshimu “Waislamu, wanaomwabudu Mungu aliye mmoja, mwenye uhai na mwenye kuwepo, rahimu na mwenyezi, Muumba wa mbingu na dunia, aliyenena na wanadamu”[147] . Kama sisi sote tunaomwamini Mungu tunataka kukuza upatanisho, haki na amani, ni lazima tufanye kazi pamoja ili kuondoa kila aina ya ubaguzi, kutovumiliana na imani kali (religious fundamentalism). Katika utume wake wa kijamii, Kanisa halitofautishi dini. Linakuja kuwasaidia wahitaji, wawe ni Wakristo, Waislamu au wafuasi wa dini za kimapokeo. Kwa njia hii hutoa ushahidi wa upendo wa Mungu, muumba wa wote, na linahamasisha wafuasi wa dini zingine kuonyesha heshima na kubadilishana masuala mbalimbali kwa roho ya kuheshimiana. Ninaliomba Kanisa zima, kwa njia ya mazungumzano ya kuvumiliana na Waislamu, lijitahidi ili uhuru wa kidini utambuliwe kisheria na kivitendo, ili kila mwananchi barani Afrika aweze kuwa na haki, siyo tu ya kuchagua dini anayotaka bila shuruti[148] na kuabudu, lakini pia haki ya uhuru wa dhamiri.[149] Uhuru wa kidini ni barabara inayoelekea kwenye amani.[150]

C. Kuwa “chumvi ya dunia” na “nuru ya Ulimwengu”

95. Kwa utume wake wa uinjilishaji, Kanisa barani Afrika linachota chemchemi kadhaa: Maandiko Matakatifu, Mapokeo na maisha ya sakramenti. Kama wengi wa mababa wa Sinodi walivyoona, huduma ya Kanisa hujengwa kwa ufanisi juu ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Zaidi ya hayo, Mkusanyiko wa Mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu Jamii ni mwongozo kwa utume wa Kanisa kama “Mama na Mwalimu” ulimwenguni na katika jamii, na kwa hiyo ni zana za kichungaji za ngazi ya kwanza.[151] Waamini ambao huchota kutoka kwenye chemchemi halisi, Kristo, wanabadilishwa naye kuwa “nuru ya ulimwengu” (Mt 5:14), na wanamsambaza ambaye ndiye yeye mwenyewe “nuru ya ulimwengu” (Yn 8:14). Uelewa wao ni lazima upewe sura na upendo. Elimu kwa kweli, “kama inataka kuwa hekima inayoweza kumwongoza mtu kutoka mwanzo wake hadi kufikia lengo lake la mwisho... lazima ‘ikolezwe na chumvi ya upendo.”[152]

96. Ili kukamilisha kazi ambayo tumeitwa kuifanya, ni lazima tuyafanye ya kwetu mawaidha ya Mtakatifu Paulo, “Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani, zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani; ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho”( Efe 6:14-18).

 

SEHEMU YA PILI
“LAKINI KILA MMOJA HUPEWA UFUNUO WA ROHO KWA KUFAIDIANA”
(1Kor 12:7)

97. Ule mwongozo wa utume ambao nimeuonyesha hivi punde utakuwa kitu halisi ikiwa tu Kanisa linatenda, kwa upande mmoja, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, na kwa upande mwingine, kama mwili mmoja, tukitumia picha ya Mtakatifu Paulo, ambaye anaonyesha haya masharti mawili katika njia moja unganifu (integrated way). Ndani ya Afrika kwa kweli ambamo mna mambo yanayokinzana, Kanisa lazima lioneshe wazi njia ya kumwelekea Kristo. Lazima lioneshe namna ya kuishi, katika uaminifu kamili kwa Kristo Yesu, umoja katika tofauti alivyofundisha Mtume: “ Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.” (1Kor 12:4-7). Kwa kumhimiza kila mwana familia wa Kanisa kuwa “chumvi ya dunia” na “nuru ya ulimwengu” (Mt 5:13-14), ninataka kukazia kwamba kwa “kuwa hivyo” ni lazima watende, kwa njia ya Roho Mtakatifu, kwa faida ya umma. Mtu hawezi kuwa Mkristo pe Zawadi zilizotolewa na Bwana kwa kila mmoja – maaskofu, mapadre, mashemasi na watawa, makatekista na walei – lazima zichangie katika kujenga uelewano, muungano na amani katika Kanisa lenyewe na jamii kwa ujumla.

98. Wote tunafahamu wazi simulizi la yule mgonjwa aliyekuwa amepooza aliyepelekwa kwa Yesu ili aponywe (rej. Mk 2:1-12). Kwetu sisi leo, mtu huyu anawakilisha ndugu zetu wote wa Afrika na mahali kwingineko ambao wamepooza kwa namna mbalimbali na kwa kusikitisha, mara nyingi, katika uchungu mkubwa. Katika mwanga wa changamoto ambayo nimeilezea kwa kifupi, nikichukua kwenye maelezo ya mababa wa Sinodi, hebu tutafakari juu ya maelekeo ya wale waliokuwa wamembeba yule mgonjwa aliyepooza. Yeye mwenyewe hakuweza kufika karibu na Yesu bila msaada wa wale watu wanne wenye imani waliovunja vipingamizi vya kimwili kama ishara ya mshikamano wao na imani yao kamili katika Yesu. Kristo “aliiona imani yao.” Yeye anaondoa vizuizi vya kiroho anapomwambia yule mgonjwa: “Umesamehewa dhambi zako.” Anaondoa kile kilichokuwa kikimzuia yule mgonjwa kusimama tena. Mfano huu unatualika kukua katika imani na, matokeo yake, kuonyesha mshikamano na ubunifu katika kuwapatia ahueni wabebao mizigo mizito, ili kuwafungua kwenye ukamilifu wa uhai katika Kristo (Mt 11:28). Mbele ya vipingamizi, vya kimwili na vya kiroho, vinavyosimama mbele yetu, hebu tukusanye nguvu za kiroho za Kanisa zima ambalo ni mwili wa Kristo, tukiamini kwamba Kristo atatenda kwa njia ya Roho Mtakatifu katika kila mmoja wetu tulio sehemu ya mwili wake.

 

SURA YA I
WANAKANISA

99. Wapendwa wanakanisa, hasa ninyi, wapendwa waamini wa Afrika, upendo wa Mungu umewajaza kila aina ya baraka na umewawezesha kutenda kama chumvi ya dunia. Ninyi nyote, kama wanakanisa, lazima mtambue kwamba amani na haki hutokana kwanza na upatanisho wa kina wa mwanadamu katika nafsi yake mwenyewe na vilevile na Mungu. Kristo mwenyewe ndiye “Mfalme pekee na wa kweli wa Amani.” Kuzaliwa kwake ni uthibitisho wa amani ya kimasiha iliyotangazwa na manabii (rej. Isa 9:5-6;57:19; Mik 5:4, Efe 2:14-17). Amani hii haiji kutoka kwetu sisi wenyewe ila kwa Mungu. Ni zawadi ya kimasiha haswa. Amani hii hutuongoza kwenye ile haki ya ufalme, ambayo ni lazima itafutwe wakati unaofaa na wakati usiofaa, katika kila tufanyalo (rej. Mt 6:33), ili katika mazingira yote utolewe utukufu kwa Mungu (rej. Mt.5:16). Sasa sisi tunajua kwamba mtu mwenye haki ni mwaminifu kwa sheria ya Mungu kwa sababu ameongolewa (rej. Lk 15:7; 18:14). Uaminifu huu mpya umeletwa na Kristo ili kutufanya watu “wasio na lawama wala udanganyifu” (Flp 2:15).

I. MAASKOFU

100. Ndugu zangu katika daraja la uaskofu, utakatifu ambao askofu anaitiwa unadai kuishi maisha ya fadhila – katika nafasi ya kwanza, fadhila za kimungu – na kuishi mashauri ya injili,[153] utakatifu wenu binafsi ni lazima uwe wa pekee, kwa faida ya wale waliowekwa chini ya uangalizi wenu wa kichungaji, ambao ni lazima muwatumikie. Maisha yenu ya sala yatalisha utume wenu kutoka ndani. Askofu ni lazima awe mtu ambaye anampenda Kristo. Mamlaka ya kiroho na hadhi ambayo hutegemeza utendaji wenu wa mamlaka ya kisheria yana uwezo kutokana tu na utakatifu wa maisha yenu.

101. Mtakatifu Sipriani wa Kartago, katikati ya milenia ya tatu, alisema: “Kanisa linao Maaskofu kama mihimili inayolishikilia, na mwenendo wake wote hufuata maelekezo ya hao maaskofu.”[154] Maungano, umoja na ushirikiano na mapadre vitakuwa mwongozo dhidi ya mgawanyiko na vitawasaidia kumsikiliza pamoja Roho Mtakatifu. Atawaongoza kwenye njia iliyo kweli (rej. Zab 22:3). Wapendeni na waheshimuni mapadre wenu!. Ni watenda kazi pamoja nanyi wastahiki katika huduma yenu ya uaskofu. Mwigeni Kristo! Alitengeneza mduara wa urafiki ukimzunguka, upendo wa kidugu na maungano ambavyo alichota kutoka kwenye kina cha fumbo la Utatu. “ninawaalika kuendelea kuwasaidia mapadre wenu kuishi katika muungano wa karibu na Kristo. Maisha haya ya kiroho ni msingi wa maisha yao ya utume. Wahimizeni kwa upole kusali kila siku, kuadhimisha masakramenti inavyostahili, hasa Ekaristi na Upatanisho, kama Mtakatifu Francis wa Sales alivyofanya kwa mapadre wake ... mapadre wenu wanahitaji upendo wenu, kuwatia moyo na kuwajali.”[155]

102. Muwe wamoja na halifa wa Petro, pamoja na mapadre wenu na waamini wote. Msipoteze nguvu zenu za kibinadamu na za kichungaji kwa kutafuta majibu kwa maswali ambayo hayawahusu moja kwa moja, au katika kutafuta utaifa ambao kwa urahisi unaweza kuwapofusha. Ni rahisi zaidi kufuata kinyago hiki, au kuufanya utamaduni wa Kiafrika ni kila kitu, kuliko kufuata madai ya Kristo. Vinyago kama hivyo ni udanganyifu mtupu. Na zaidi, ni vishawishi vya kutusadikisha kwamba jitihada za kibinadamu peke yake zinaweza kuleta ufalme wa furaha ya milele duniani.

103. Wajibu wenu wa kwanza ni kuipeleka Habari Njema ya wokovu kwa watu wote, na kuwapa waamini katekesi ambayo huwaongoza hadi kwenye elimu ya kina zaidi ya Yesu Kristo. Hakikisheni kwamba waamini walei wanajipatia ufahamu wa kweli juu ya utume wao wa kikanisa na kuwahimiza kujihusisha nao kwa kuwajibika daima kwa kutafuta maslahi ya umma. Programu za kudumu za mafunzo zinazotolewa kwa walei, na zaidi ya yote programu zinazotolewa kwa viongozi wa kisiasa na kiuchumi, lazima zisisitize uongofu kama sharti la lazima kwa kuubadili ulimwengu. Inafaa ziwe zinaanza kwa sala na kisha kuendelea na katekesi ambayo itawafikisha kwenye utendaji. Kutengeneza mfumo, kama unahitajika kweli kutakuja baadaye; kwa vile hauwezi kuchukua nafasi ya nguvu ya sala!

104. Wapendwa maaskofu, mkifuata nyayo za Kristo Mchungaji Mwema, iweni wachungaji wema na watumishi wa kundi mlilokabidhiwa kulitunza, kwa mfano wa maisha na mwenendo wenu. Uongozi mzuri wa majimbo yenu unahitaji uwepo wenu. Kufanya ujumbe wenu uaminike, hakikisheni kwamba majimbo yenu yanakuwa mifano katika mwenendo wa watumishi, katika uwazi na utawala mzuri wa mali. Msisite kuomba msaada kutoka kwa wataalamu katika kukagua mahesabu, ili kuonyesha mfano kwa waamini na kwa jamii kwa ujumla. Hamasisheni utendaji mzuri wa wahudumu mbalimbali wa Kanisa waliowekwa kwa mujibu wa sheria za Kanisa katika ngazi ya kijimbo na kiparokia. Kwenu kwa nafasi ya kwanza mna kazi ya kutafuta umoja, haki na amani kwa kuwa mna wajibika kwa makanisa mahalia.

105. Sinodi inakumbuka kwamba “Kanisa ni muungano ambao huzaa mshikamano wa kichungaji. Maaskofu, katika umoja na askofu wa Roma, ndio watu wa kwanza kuhamasisha muungano na ushirikiano katika utume wa Kanisa.”[156] Mabaraza ya maaskofu yamekabidhiwa utume wa kuimarisha muungano huo na kuhamasisha mshikamano huu wa kichungaji.

106. Ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na muonekano mkubwa, udumifu na ufanisi wa kazi ya kichungaji ya Kanisa katika jamii, Sinodi iliona hitaji la kuwa na mshikamano mkubwa zaidi katika utendaji kwa ngazi zote. Ingekuwa vizuri mabaraza ya maaskofu, na mkutano wa hierakia Katoliki ya Misri (ACHE), kutazama upya uwajibikaji wao katika kuchukuliana mizigo kiurika.[157] Hili linamaanisha ushiriki katika shughuli za muundo huu, hususani watumishi na fedha. Kwa njia hii Kanisa litashuhudia kwa vitendo umoja ambao Kristo aliomba (rej. Yn 17:20-21).

107. Aidha ninaona ni kitu muhimu kwa maaskofu kusaidia, kwa ufanisi na kwa upendo, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Afrika na Madagaska”, yaani SECAM, kama muundo wa kibara wa mshikamano na umoja wa kikanisa.[158] Vilevile, mahusiano mazuri lazima yadumishwe na Shirikisho la Mashirika ya kitawa na kazi ya kitume barani Afrika na Madagaska, yaani COSMAM, na chama cha vyuo vikuu Katoliki na makundi mengine ya kikanisa .

II. MAPADRE

108. Kama wafanya kazi wa lazima na wa karibu na maaskofu, mapadre[159] wamepewa jukumu la kuendeleza kazi ya uinjilishaji. Mkutano wa Pili wa Sinodi kwa ajili ya Afrika ulifanyika mwaka ule nilioutangaza kuwa wa Upadre, nikihimiza kwa namna ya pekee kukua katika utakatifu. Wapendwa mapadre, kumbukeni kwamba ushuhuda wenu wa kuishi pamoja kwa amani, ndani ya koo zenu na tofauti za utaifa wenu, unaweza kugusa nyoyo.[160] Wito wa kuwa watakatifu unatudai tuwe wachungaji kufuatana na moyo wa Mungu,[161] tukiwalisha kondoo wetu kwa haki (rej. Eze 34:16). Kujisalimisha kuwa viongozi wa kisiasa[162] au mawakala wa kijamii kungekuwa ni sawa na kusaliti utume wenu wa kipadre na kuinyima huduma jamii, ambayo inatarajia neno lenu la kinabii na matendo yenu ya kinabii. Kama Mtakatifu Sipriani alivyosema nyakati zake: “wale walio na heshima ya ukuhani mtakatifu...lazima watoe huduma zao tu kwa huduma ya altare na watolee muda wao kusali peke yake.”[163]

109. Kwa kujitoa kwenu kwa ajili ya wale ambao Bwana amewaweka chini yenu ili ya muunde fadhila zao za kikristo na kuwaongoza katika njia ya utakatifu, si tu mtawaleta kwa Kristo lakini pia mtawafanya wanaharakati wa jamii ya Kiafrika iliyofanywa upya. Tukizingatia mazingira magumu ambayo mnakumbana nayo, ninawaomba mwimarishe kwa kina maisha yenu ya sala na malezi endelevu ya kiakili na malezi ya kiroho. Iweni daima na uelewa zaidi wa maandiko matakatifu, ambayo ni neno la Mungu ambalo kila siku mwalitafakari na kulifafanua kwa waamini. Kueni katika ujuzi wenu wa katekisimu, hati za Majisterio na mafundisho ya Kanisa juu ya jamii. Kwa namna hiyo mtaweza kuwalea Wakristo wengine katika jumuiya ya kikristo ambamo moja kwa moja mnawajibika, ili, waweze kuwa wafuasi halisi na mashahidi wa Kristo.

110. Ishini bila makuu utii kwa Askofu wa Jimbo lenu katika maisha ya unyenyekevu na upendo wa kimwana. “Mkisukumwa na heshima kwa yule aliyetupenda, ni sahihi muwaheshimu bila unafiki, kwa maana siyo askofu ambaye tunamwona ambaye twamdanganya, lakini ni yule asiyeonekana. Kwa hali hii, siyo suala la mwili, bali la Mungu ambaye anajua yaliyofichika.”[164] Katika muktadha wa malezi endelevu ya maklero, ninaona ni muhimu kusoma tena na kutafakari katika hati kama zile za dikrii ya Huduma na Maisha ya Mapadre, Presbyterorum Ordinis, au Mausia ya Kitume baada ya Sinodi Pastores Dabo Vobis, Mwongozo juu ya Huduma na Maisha ya Mapadre na maelekezo yaitwayo Padre, Mchungaji na Kiongozi wa Jumuiya ya Parokia.

111. Jengeni jumuiya za kikristo kwa mifano yenu, kuishi katika ukweli, na furaha ya majukumu yenu ya kipadre, useja katika usafi kamili na kujinasua kutoka kwenye kung’ang’ania mali. Ishara hizi mkiziishi katika ukomavu na amani, kwa kupatanisha na mtindo wa maisha ya Yesu, mtaonyesha “kujitoa kama zawadi kamilifu na bila kujibakiza, kwa Kristo, kwa Kanisa na kwa ufalme wa Mungu.”[165] Wajibikeni kwa bidii zaidi kuweka katika vitendo mpango wa kichungaji wa kijimbo kwa ajili ya upatanisho, haki na amani, hasa kwa njia ya kuadhimisha sakramenti ya Kitubio na Ekaristi, katekesimu, malezi ya walei na mazungumzano endelevu na wale wanaoshikilia nafasi za majukumu katika jamii. Kila padre lazima afurahie kulihudumia Kanisa.

112. Kumfuasa Kristo katika njia ya upadre kunamaanisha kufanya maamuzi. Siyo rahisi kila mara kuliishi hili. Madai ya kiinjili yaliyoratibishwa kwa karne na karne kwa mafundisho ya Majisterio huonekana magumu machoni pa ulimwengu. Wakati mwingine ni vigumu kuyafuata, lakini siyo kwamba haiwezekani. Kristo anatuambia kwamba hatuwezi kutumikia mabwana wawili (rej. Mt 6:24). Ni wazi anaongelea pesa, hazina ya kiulimwengu ambayo inaweza kuziteka nyoyo zetu (rej. Lk 12:14), lakini pia anaongelea mambo mengine mengi yasiyo hesabika tunayomiliki, kama vile maisha yetu, familia zetu, elimu yetu, mahusiano yetu ya kichungaji. Haya yote ni mambo muhimu ambayo ni sehemu ya unafsi wetu. Lakini Kristo anawataka wale anaowaita kujikana wenyewe kikamilifu ili kujiweka chini ya maongozi ya Mungu. Anadai kufanya uamuzi mgumu (rej. Mt 7:13-14) ambao wakati mwingine tunauona ni mgumu kuuelewa na kuuishi. Hata hivyo, kama Mungu ni hazina yetu – ile lulu yenye thamani kubwa ambayo lazima tuipate kwa gharama yo yote ile, hata ile ya sadaka kubwa (Mt 13:45-46) – kwa hiyo, tunataka mioyo yetu na mili yetu, akili zetu na mawazo yetu yawe kwa ajili yake tu. Tendo hili la imani hutuwezesha kuona kila kitu ambacho huonekana muhimu kwetu katika mwanga mwingine, na kuonja uhusiano wetu na miili yetu, na mahusiano yetu katika familia au miongoni mwa marafiki, katika mwanga wa wito wa Mungu na wa kile kinachotakiwa katika huduma ya Kanisa. Hii inadai kufanya tafakari ya kina. Tafakari hiyo ni lazima ianzie seminarini na iendelee siku zote katika maisha ya upadre wetu. Kristo anatuambia, kwa njia ya kutuhamasisha, maana anajua uwezo na udhaifu wa mioyo yetu. “Tafuteni kwanza ufalme wa mbingu na haki yake, na mengine yote mtapewa kwa ziada” (Mt 6:33)

III. WAMISIONARI

113. Wamisionari wasio wa Afrika, wakiitikia kwa ukarimu wito wa Bwana kwa ari kubwa ya kitume, walikuja kushirikisha furaha ya ufunuo. Wakifuata nyayo zao, Waafrika leo ni wamisionari katika mabara mengine. Tunawezaje kushindwa kuwasifu kwa namna ya pekee kwa hili? Wamisionari waliokuja Afrika – mapadre, wanawake na wanaume wa maisha ya wakfu na walei – walijenga makanisa, mashule na zahanati, na walifanya mengi kutengeneza uso wa utamaduni wa Kiafrika wa leo, lakini zaidi ya yote waliujenga mwili wa Kristo na wakaitajirisha maskani ya Bwana. Walifahamu vizuri namna ya kushirikisha chumvi ya neno na wakaeneza mwanga wa masakramenti. La maana zaidi kuliko yote, waliipatia Afrika hazina yao ya thamani kuliko zote: Yesu Kristo. Shukrani kwao kwa kuzikomboa tamaduni nyingi za kimapokeo kutoka kwenye hofu za kihenga (ancestor) na roho wachafu (rej. Mt 10:1). Kutokana na ile mbegu njema waliyopanda (rej. Mt. 13:24)waliibuka watakatifu wengi wa Kiafrika, ambao bado ni mfano na wanapaswa kutuhamasisha zaidi na zaidi. Ingekuwa kitu cha faida kurudia na kukuza ibada kwa watakatifu hawa. Uwajibikaji wao kwa kazi ya Injili wakati mwingine ulioneshwa kwa hali ya ushujaa, hata kwa gharama ya maisha yao. Mara nyingine tena maneno ya Tertuliano yanadhihirika kuwa kweli: “damu ya mashahidi ni mbegu ya Wakristo.”[166] Ninamshukuru Mungu kwa ajili ya hawa wanaume na wanawake watakatifu wote, ishara ya uhai wa Kanisa barani Afrika.

114. Ninawahimiza wachungaji wa makanisa mahalia kutambua miongoni mwa wahudumu wa Injili barani Afrika wale ambao wangeweza kutangazwa watakatifu kwa mujibu wa kanuni za Kanisa, siyo tu ili kuongeza idadi ya watakatifu Waafrika, lakini pia kupata waombezi wapya mbinguni kujiunga na kanisa katika safari yake ya kihija na kuomba mbele ya Mungu kwa ajili ya bara la Afrika. Ninaliweka chini ya watakatifu wa hili bara pendwa Kanisa linaloishi hapa.

IV. MASHEMASI WA KUDUMU

115. Umuhimu wa wito walioupokea mashemasi wa kudumu inabidi usisitizwe. Katika uaminifu kwa umisionari wa kale, ninawakaribisha kufanya kazi kwa unyenyekevu na kwa ushirikiano wa karibu na maaskofu.[167] Ninawaomba kwa upendo kuendelea kutoa kile ambacho Kristo anatufundisha katika Injili: kujivunia kazi iliyofanywa vizuri,[168] nguvu ya kimaadili kwa kuheshimu tunu, uaminifu, ukweli, furaha ya mmoja kuongeza jiwe lake katika jengo la Kristo na jamii, kulinda uasili, kujali maslahi ya wote. Isaidieni jamii ya Kiafrika katika kila ngazi kuhimiza uwajibikaji; Kwa upande wa wanaume ambao ni waume na mababa, kuheshimu wanawake ambao ni sawa na wanaume kwa heshima, na kujali watoto walioachwa bila elimu.

116. Msikose kutoa uangalizi wa pekee kwa wale ambao ni wagonjwa, kiakili au kimwili,[169] wale ambao ni dhaifu na maskini wa jumuiya zenu. Upendo wenu na uwe wa kufikirika (imaginative)! Katika kazi ya kichungaji ya maparokia, Kumbukeni kwamba maisha mazuri ya kiroho huruhusu Roho wa Kristo kumkomboa mtu ili aweze kutenda kwa ufanisi katika jamii. Maaskofu watakuwa waangalifu kuhakikisha kwamba mnapata malezi yenu endelevu ili yaweze kuchangia kuboresha utendaji wa huduma yenu[170]. Kama Mtakatifu Stefano, Mtakatifu Laurenti na Mtakatifu Vinsenti, mashemasi na mashahidi, hutafuta kutambua na kukutana na Kristo katika Ekaristi na katika maskini. Huduma hii ya Altare na ya upendo itawafanya mtazamie kukutana na Bwana aliyepo altareni na katika maskini. Na hivi mtaweza kujitoa maisha yenu kwa ajili yake hata kifo.

V. WATU WA MAISHA YA WAKFU

117. Kwa njia ya nadhiri ya usafi kamili, umaskini na utii, maisha ya watu wa maisha ya wakfu huwa ushahidi wa kinabii. Kwa hiyo wanaweza kuwa mifano katika maeneo ya upatanisho, haki na amani, hata katika mazingira ambayo ni ya wasiwasi mkubwa.[171] Maisha ya jumuiya hutuonyesha kwamba inawezekana kuishi kama kaka na dada, na kuunganika licha ya tofauti zetu za kizawa na rangi (rej. Zab 133:1). Maisha ya jumuiya yanaweza na ni lazima yawawezeshe watu kuona na kuamini kwamba leo barani Afrika, wale akina baba na wakina mama wanaomfuata Kristo Yesu hupata ndani yake siri ya kuishi kwa furaha pamoja: kupendana na muungano wa kidugu, unaoimarishwa kila siku na Ekaristi na sala ya Kanisa.

118. Wapendwa watu wa maisha ya wakfu, ninawaomba mwendelee kuishi karama zenu kwa ari ya kweli ya kitume katika maeneo mbalimbali yaliyoainishwa na waanzilishi wenu! Kwa namna hiyo mtakuwa zaidi na zaidi macho katika kutunza taa zenu zikiwaka! Waanzilishi wenu walitaka kumfuata Kristo kikweli kweli na kuitikia mwito wake. Zile kazi njema mbalimbali zilizojitokeza kama matokeo ni nakshi ambazo hulipamba Kanisa.[172] Hivi, ni lazima mziendeleze kwa kufuata kwa uaminifu kadiri inavyowezekana karama za waanzilishi wenu, mawazo yao na mipango yao. Hapa ningependa kusisitiza mchango muhimu wa watu wa maisha ya wakfu katika maisha ya Kanisa na katika kazi yake ya umisionari. Wao ni msaada wa lazima na wa thamani kwa kazi ya kichungaji ya Kanisa lakini pia ni kielelezo cha uhalisia kwa kina kabisa wa wito wetu wa Kikristo.[173] Kwa sababu hiyo, ninawaalika, wapendwa watu wa maisha ya wakfu, kuendelea katika muungano wa karibu na kanisa mahalia na pamoja na Askofu wa Roma.

119. Afrika ni hori la maisha ya tafakari ya kikristo. Tangu nyakati za mwanzo katika Afrika ya Kaskazini, hasa Misri na Ethiopia, ilipata mizizi katika Afrika Kusini mwa Sahara wakati wa karne ya mwisho. Bwana awabariki wanaume na wanawake ambao wameamua kumfuata bila masharti! Maisha yao yaliyofichika ni kama chachu katika unga. Sala zao za daima zitategemeza jitihada za kitume za maaskofu, mapadre, watu wengine wa maisha ya wakfu, makatekista na kanisa zima.

120. Maana mbalimbali za mabaraza ya kitaifa ya wakuu wa mashirika na wale wa COMSAM, husaidia kuvuta tafakari zenu, siyo tu ili kufanikisha malengo ya hizo taasisi mbalimbali, wakati wanatunza uhuru wa kila mmoja wapo, tabia na roho ya kila moja peke yake, lakini pia kusaidia kufanya kazi kwa pamoja katika mazingira ya udugu na mshikamano. Inafaa kukuza roho ya kikanisa iliyo na msingi kwenye ushirikiano mzuri na mabaraza ya maaskofu.

VI. WASEMINARI

121. Mababa wa Sinodi walitoa umakini wa pekee kwa waseminari. Bila kupuuzia malezi ya kiteolojia na kiroho, ambayo ni wazi ndiyo ya msingi, walisisitizia umuhimu wa makuzi ya kiakili na kiutu ya kila mseminari. Mapadre wa baadaye ni lazima wakuze uelewa sahihi wa tamaduni zao wakati wakiwa hawafungwi na mipaka yao ya kikabila na kiutamaduni.[174] Ni lazima wazidi kuwa na mizizi imara katika tunu za kiinjili ili kuimarisha kujitoa kwao katika uaminifu na ibada kwa Kristo. Uaminifu wao kwa utume wao ujao kwa kiasi kikubwa utategemea muungano wao wa kina na Kristo, juu ya ubora wa maisha yao ya sala na maisha yao ya ndani, na katika utu, tunu za kiroho na za kimaadili walizojipatia wakati wa malezi yao. Tunaomba waseminari wote wawe watu wa Mungu anayetafuta na kuishi “haki, imani, upendo, udumifu, na utaratibu” (1Tim 6:11).

122. “Waseminari lazima wajifunze kuishi kwenye jumuiya kiasi kwamba maisha ya pamoja yaweze baadaye kupelekea kwenye muonjo wa kweli wa upadre kama udugu wa karibu wa kipadre.”[175] Walimu w wa seminari na walezi watafanya kazi kwa pamoja, wakifuata maelekezo ya maaskofu, kuhakikisha waseminari waliowekwa chini ya uangalizi wao wanapata malezi unganifu (integral formation). Katika kuchagua watakaji, uangalifu makini na uongozi bora lazima viwepo, ili wale waliosajiliwa kwenye upadre wawe wafuasi wa kweli wa Kristo na watumishi wa kweli wa Kanisa. Uangalifu unatakiwa katika kuwaingiza katika utajiri usio na mipaka wa Kanisa wa kibiblia, kiteolojia, kiroho, kiliturujia, kimaadili na kisheria.

123. Katika kuhitimisha mwaka wa Mapadre, Juni 2010, niliandika barua kwa waseminari,[176] ambamo niliongea juu ya utambulisho, mambo ya kiroho na utume wa padre. Kwa moyo nilihimiza kwamba kila mseminari aisome na kutafakari juu ya hati hii fupi iliyoelekezwa kwake binafsi; walezi wataifanya iweze kusomeka. Seminari inawakilisha muda wa matayarisho kwa upadre, muda wa kujifunza. Ni muda wa kufanya maamuzi, malezi na maendeleo ya kiutu na kiroho. Waseminari wanatakiwa kutumia kwa busara muda huu ambao unatolewa kwa ajili yao kujijengea uwezo wa kiroho na kiutu ili kutoka humo waweze baadaye kuchota kwa njia ya maisha yao ya kipadre.

124. Wapendwa waseminari, iweni mitume wa vijana wa kizazi chenu kwa kuwakaribisha kumfuata Kristo katika maisha ya upadre. Msiogope! Sala za watu wengi zinawasindikiza na kuwategemeza (rej. Mt 9:37-38).

VII. MAKATEKISTA

125. Makatekista siyo mawakala wa kupuuzwa wa uchungaji katika utume wa uinjilishaji. Mchango wao ulikuwa muhimu sana wakati wa uinjilishaji wa mwanzo, kuwatayarisha wakatekumeni na kuwaongoza na kuzitegemeza jumuiya. “Katika njia asilia walileta utamadunisho fanisi ambao umetoa matunda mengi ajabu (rej. Mk 4:20). Makatekista wameiruhusu nuru yao kung’ara mbele za watu (Mt 5:16), sababu, kwa kuona mema wanayofanya, watu huweza kumtukuza Baba yetu aliye mbinguni. Kwa hakika, Waafrika wamewainjilisha Waafrika.”[177] Mchango huu, uliokuwa muhimu hivi zamani, unabaki muhimu hata wakati huu wa sasa na wakati ujao wa Kanisa. Nawashukuru kwa upendo wao kwa Kanisa.

126. Nawataka maaskofu na mapadre kujihusisha na malezi ya makatekista kiakili, kimafundisho, kimaadili na kiuchungaji. Lazima waitazame kwa umakini mkubwa hali ya maisha ya makatekista,[178] ili kuhakikisha heshima yao inalindwa. Wala wasipuuzie mahitaji yao kama wanandoa, kwa maana mfanya kazi mwaminifu shambani mwa Bwana anastahili ujira wake (Mt 20:1-6), wakati wanasubiri ujira wao kutoka kwa Bwana kwa kuwa yeye peke yake ni mwenye haki na aijua mioyo yetu.

127. Wapendwa makatekista, kumbukeni kwamba kwa jumuiya zilizo nyingi ninyi ndio picha ya mfuasi mwenye bidii na mfano wa maisha ya kikristo. Ninawahimiza kutangaza, kwa mifano yenu, kwamba maisha ya familia yanastahili heshima kubwa, kwamba malezi ya kikristo huwatayarisha vijana kuishi katika jamii kama watu ambao ni waaminifu na wa kuaminika katika kuhusiana na watu wengine. Kwa kuwakaribisha wote bila ubaguzi: matajiri na maskini, wazawa na wageni, Wakatoliki na wasio Wakatoliki (rej. Yak 2:1). Msioneshe upendeleo (rej. Mdo 10:34; Rum 2:11, Gal 2:6, Efe 6:9). Kwa njia ya kuyaishi maandiko matakatifu na mafundisho ya majisterio mtaweza kutoa katekesi safi, kuongoza vikundi vya sala na kupendekeza masomo ya kiroho kwa jumuiya katika uangalizi wenu. Kazi yenu baadaye itakuwa endelevu, stahimilivu na chanzo cha uvuvio. Kama ninavyo wakumbuka kwa shukrani watangulizi wenu, ninawasalimu nyote na ninawahimiza kufanya kazi leo bila ubinafsi kama wao, kwa ujasiri wa kitume kama wao na imani kama yao. Kwa kujitahidi kuwa waaminifu kwa utume wenu, mtachangia siyo tu kwa utakatifu wenu, lakini pia kwa namna fanisi, kujenga mwili wa Kristo, Kanisa.

VIII. WALEI

128. Kwa njia ya waamini walei, Kanisa limo na linafanya kazi ulimwenguni. Waamini walei wana mchango muhimu katika Kanisa na katika jamii. Kuwawezesha itakiwavyo kutoa mchango wao, inatakiwa vituo vya malezi ya kibiblia, kiroho, kiliturujia na kichungaji viwemo majimboni. Ni hamu ya moyo wangu kwamba waamini walei wenye majukumu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii watayarishwe kwa kupatiwa elimu ya kutosha ya mafundisho ya kanisa kuhusu jamii, ambayo yanaweza kuwapatia kanuni za kutenda sawasawa na Injili. Walei wanaume na wanawake, kwa kweli, ni “mabalozi wa Kristo” (2Kor 5:20) katika uwanja wa hadhara, katika moyo wa ulimwengu![179] Ushuhuda wao wa kikristo utakuwa wa kuaminika tu kama ni wanataaluma wenye uwezo na ni waaminifu.

129. Waamini walei wanaitwa, zaidi ya yote kuwa watakatifu, utakatifu ambao watauishi ulimwenguni. Wapendwa sehemu ya waamini wote: jengeni maisha yenu ya ndani na mahusiano yenu na Mungu, ili Roho Mtakatifu awaangaze katika kila mazingira. Ili kuhakikisha kwamba maslahi ya mtu binafsi na maslahi ya wote yanabaki katika kiini cha ubinadamu, kisiasa, kiuchumi au kijamii. Imarisheni muungano wenu na Kristo, ili mmjue na mmpende, mkitenga muda kwa ajili ya Mungu katika Sala na katika kupokea masakramenti. Jiruhusuni kuangaziwa na kuelekezwa na Mungu na neno lake.

130. Ningependa kwenda ndani zaidi katika kuelezea vidokezo vya maisha ya kitaaluma ya kikristo. Kwa kifupi, inamaanisha kutoa ushuhuda kwa Kristo ulimwenguni kwa kuonyesha, kwa njia ya mfano, kwamba kazi inaweza kuwa mazingira chanya sana kwa ajili ya maendeleo binafsi na siyo kimsingi njia ya kujipatia faida. Kazi zenu huwawezesha kushiriki katika kazi ya uumbaji na kuwatumikia ndugu kaka na dada zenu. Mkitenda kwa namna hiyo, mtakuwa “chumvi ya dunia” na nuru ya ulimwengu”, kama Bwana anavyotutaka. Katika maisha ya kila siku, wekeni katika vitendo kipaumbele kwa maskini, bila kujali nafasi yenu katika jamii, sawasawa na roho ya zile heri (rej. Mt 5:3-12), ili kuona ndani yao uso wa Kristo ambaye anawaita kumtumikia (rej. Mt 25:31-46).

131. Ingefaa kuunda vyama ili kuendelea kuunda dhamiri zenu za kikristo na kutegemezana katika kutafuta haki na amani. Jumuiya ndogondogo za kikristo (JNNK) na zile “jumuiya mpya”[180] ni muundo msingi kwa kutegemeza moto wa ubatizo wenu. Leteni utaalam wenu katika maisha na kazi za vyuo vikuu Katoliki, ambavyo vinaendelea kukua vikifuata pendekezo la Mausia ya Kitume Ecclesia in Africa.[181] Ninawahimiza pia kuwa na uwepo hai na wa kijasiri katika maeneo ya maisha ya kisiasa, utamaduni, sanaa, vyombo vya mawasiliano na vyama mbalimbali. Msisite au kuona aibu juu ya uwepo huu, lakini muujivunie na mkijua mchango wake wa thamani kubwa kwa maslahi ya umma!

 

SURA YA II
MAENEO MUHIMU YA UTUME

132. Bwana ametukabidhi utume maalumu, na hajatuacha bila nyenzo za kufanikisha utume huo. Siyo tu kwamba amempatia kila mmoja wetu vipaji binafsi kwa ajili ya kuujenga Mwili wake ambao ni Kanisa, lakini pia ameipatia jumuiya nzima ya kanisa karama za pekee ambazo huiwezesha kuendeleza utume wake. Zawadi yake kuu ni Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Roho tunaunda mwili mmoja na “katika nguvu ya Roho Mtakatifu tu tunaweza kugundua kilicho sahihi na baadaye kukifanya.”[182] Nyenzo fulani zinatuhitaji kwa hizo kazi ; hata hivyo hizi zinabaki kuwa hazitoshi isipokuwa Mungu mwenyewe anatuweka tayari kushirikiana katika kazi yake ya upatanisho kwa njia ya “uwezo wetu wa kufikiri, kuongea, kusikiliza na kutenda.”[183] Kwa njia ya Roho Mtakatifu, tunakuwa kweli “chumvi ya dunia” na “nuru ya ulimwengu” (Mt 5:13-14)

I. KANISA KAMA UWEPO WA KRISTO

133. “Katika Kristo Kanisa ni kama sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mungu na cha kuleta umoja kati ya wanadamu wote.”[184] Kama jumuiya ya wafuasi wa Kristo, tunaweza kufanya upendo wa Mungu uonekane na tuushiriki. Upendo “ndio mwanga wa dunia, hasa mwanga wake wa pekee. Huo tu waweza kuuangazia utusitusi wake, na kutupatia ushujaa tuendelee kuishi na kuchapa kazi.”[185] Hili linaonekana dhahiri katika Kanisa lote zima (universal Church), katika majimbo, katika maparokia, katika jumuiya ndogondogo za kikristo,[186] katika vyama, na hata katika familia ya kikristo yenyewe, ambayo imeitwa kuwa ‘kanisa la nyumbani’, mahali pa imani, pa sala na pa upendo unaojali kwa ajili ya maslahi ya kweli na ya kudumu ya kila mwanafamilia,”[187] jumuiya ambayo huishi alama ya amani.[188] Pamoja na parokia, jumuiya ndogondogo za kikristo na vyama vya kitume vinaweza kuwa mahali pa msaada ili kupokea na kuishi zawadi ya upatanisho iliyotolewa na Kristo aliye amani yetu. Kila mwanajumuiya lazima awe “mlinzi na mwenyeji” wa mwenzake: hii ndiyo maana ya ishara ya amani katika adhimisho la Ekaristi.[189]

II. ULIMWENGU WA ELIMU

134. Shule Katoliki ni raslimali ya thamani kubwa kwa kujifunza tangu utoto namna ya kutengeneza mshikamano wa umoja na utulivu katika jamii, kwa kuwa zinawafundisha watoto tunu za Kiafrika ambazo zinaendelezwa na zile za Injili. Ninawahimiza maaskofu na taasisi za maisha ya wakfu kuwawezesha watoto wa umri unaotakiwa kuingia shule: hili ni suala la haki kwa kila mtoto na hasa wakati ujao wa Afrika unategemea suala hilo. Wakristo, na vijana kwa namna ya pekee, inawapasa wapate elimu wakiwa na lengo la kurithisha elimu iliyojaa ukweli: siyo tu kujua namna ya kufanya lakini elimu ya kweli ya maisha, iliyovuviwa na mtazamo wa kikristo ulioundwa na mafundisho ya Kanisa kuhusu jamii. Ingefaa pia kuhakikisha kwamba wale wanaoajiriwa katika taasisi za elimu za Kanisa wapo, na kwa kweli waajiriwa wote wa Kanisa, wapate ujira wa haki, ili kuimarisha kuaminika kwa Kanisa.

135. Ukizingatia hali halisi ya kuchanganyika kwa watu, tamaduni na dini tulizo nazo nyakati zetu hizi, vyuo vikuu Katoliki na taasisi za kitaaluma (academic institutions) zina mchango wa maana kwa utafiti mvumilivu wa bidii na wa kinyenyekevu wa kutafuta mwanga ambao hutoka kwenye Ukweli. Ukweli tu unaozidi kiwango cha kibinadamu, kilicho na mipaka inayokiathiri, huleta amani kwa watu binafsi na upatanisho kwa jamii. Kwa sababu hii, ingesaidia kuanzisha vyuo vikuu Katoliki vipya ambapo havipo. Wapendwa kaka na dada zangu katika vyuo vikuu Katoliki na taasisi za kitaaluma, inawaangukia, kwa upande mmoja, kazi ya kutengeneza akili na mioyo ya kizazi cha vijana katika mwanga wa Injili na, kwa upande mwingine, kuzisaidia jamii za Kiafrika vizuri zaidi kujua changamoto zinazozikabili leo kwa kuipa Afrika, kwa njia ya utafiti wenu na uchunguzi, mwanga ambao inahitaji.

136. Utume ambao Mausia ya kitume Ecclesia in Africa yanakabidhi kwa taasisi Katoliki za elimu ya juu siyo kitu kipya. Ndani yake mtangulizi wangu aliandika: “Vyuo vikuu vya Kikatoliki na vituo vya elimu ya juu katika Afrika vina wajibu mahususi katika kutangaza Neno la Mungu lenye wokovu. Vinaonyesha ishara ya kukua kwa Kanisa mradi utafiti wao ukamilishe ukweli na uzoefu wa imani na uvisaidie kiundani. Vinahudumia Kanisa kwa kutoa wataalamu, kwa kuchunguza masuala muhimu ya kiteolojia na kitamaduni kwa minajili ya ufanisi wa Kanisa, kwa kusitawisha teolojia ya Kiafrika, kwa kuendeleza kazi ya utamadunisho, ... kwa kutoa vitabu na kutangaza hadharani ukweli wa ukatoliki, kwa kushughulikia maagizo yanayotolewa na Maaskofu na kwa kushiriki kwenye utafiti wa tamaduni kisayansi.” ... “Vituo vya utamaduni vya Kikatoliki hupatia Kanisa uwezekano wa kuwepo na utekelezaji kwenye uwanja wa mabadilishano ya kitamaduni. Vituo hivi vinasimamia kweli mabaraza ya hadhara yanayoliwezesha Kanisa kutangaza waziwazi kwa njia ya majadiliano ya kujenga imani za Kikristo kuhusu mwanamume, mwanamke, familia, kazi, uchumi, jamii, siasa, maisha ya kimataifa mazingira”. Hivyo, hizi ni sehemu za kusikiliza, heshima na ustahimilivu.”[190] Maaskofu watakuwa waangalifu kwamba taasisi hizi za elimu ya juu zinatunza utambulisho wao Katoliki kwa kwenda daima katika mwelekeo sawa na mafundisho ya Majisterio ya Kanisa.

137. Ili kutoa mchango imara na sahihi kwa jamii ya Kiafrika, ni lazima wanafunzi wafundishwe mafundisho ya Kanisa kuhusu jamii. Hilo litalisaidia Kanisa la Afrika kwa utulivu kutayarisha mpango wa kichungaji ambao unagusa mioyo ya Waafrika na kuwawezesha kupatanishwa na nafsi zao wenyewe kwa kumfuata Kristo. Mara nyingine tena, ni juu ya maaskofu kutegemeza mipango ya kichungaji kwa akili na ufahamu ili kuhamasisha tabia ya mazungumzano ya kiakili na uchanganuzi yakinifu ndani ya jamii na katika Kanisa. Kama nilivyosema huko Yaoundé, “Yamkini karne hii itaruhusu, kwa neema ya Mungu, kuzaliwa upya katika bara lenu, ingawa kwa hakika kwa namna mpya na tofauti, ile Shule mashuhuri ya Aleksandria. Kwa nini tusitegemee kwamba itaweza kuwapatia Waafrika wa leo na Kanisa lote zima wanateolojia wakuu na walimu wa kiroho ambao wangeweza kuchangia utakatifu wa wakazi wa bara hili na wa Kanisa lote zima?”[191]

138. Ni vema maaskofu wategemeze uchapleni ndani ya vyuo vikuu vya Kanisa na shule, na kuuweka katika vyuo vikuu na shule za serikali pia . Kikanisa kitakuwa, kama ilivyokuwa, moyo wa taasisi hizo. Kitawawezesha wanachuo kukutana na Mungu na kusimama mbele zake. Pia kitamruhusu chapleni, ambaye ni lazima achaguliwe kwa uangalifu mkubwa kwa fadhila zake za kipadre, kufanya kazi yake ya kichungaji ya kufundisha na kutakatifuza.

III. ULIMWENGU WA HUDUMA YA AFYA

139. Kanisa daima limekuwa likijihusisha na afya. Linafuata mfano wa Kristo mwenyewe aliyetangaza neno na akawaponya wagonjwa, na kisha akawapa wafuasi wake mamlaka yaleyale “kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina” (Mt 10:1; rej. 14:35; Mk 1:32, 34; 6:13, 55). Kwa njia ya taasisi zake za huduma ya afya, Kanisa huendelea kuonyesha moyo huohuo wa kuwajali wagonjwa na wote wanaoteseka. Kama mababa wa Sinodi walivyokazia, Kanisa kwa makusudi mazima linajihusisha na vita dhidi ya udhaifu wa kila namna, magonjwa na maradhi tandavu (pandemics).[192]

140. Taasisi za Kanisa za huduma ya afya na wahudumu wake wote lazima wajitahidi kuona kwa kila mgonjwa kiungo kinachoteseka cha Mwili wa Kristo. Magumu ya kila namna yanajitokeza katika mwendo wenu: ongezeko la idadi ya wagonjwa, upungufu wa vifaa na raslimali fedha, kujiondoa kwa taasisi zilizokuwa zikiwasaidieni kwa muda wa miaka mingi, na sasa zinawaacha; huenda yote haya yanaweza kuwapa picha kwamba kazi yenu haitoi matokeo yoyote yanayoonekana. Wapendwa wahudumu wa afya, leteni upendo wenye huruma wa Yesu kwa wale wanaoteseka! Iweni wavumilivu, simameni imara na msife moyo! Kuhusu maradhi tandavu, ni wazi kwamba rasilimali fedha na vifaa vinazidi kuwa vya lazima, lakini pamoja na hayo jaribuni pia daima kuwalea na kuwapa taarifa sahihi watu, hasa vijana.[193]

141. Taasisi za huduma ya afya zinahitaji kuongozwa kufuatana na kanuni za maadili za Kanisa, zikitoa huduma ambazo hupatana na mafundisho yake na daima ni chaguo la uhai (pro-life). Hazipaswi kuwa vyanzo vya kujitajirisha kwa wachache. Menejimenti ya misaada inayotolewa lazima ilenge kwenye uwazi na kimsingi huhudumia maslahi ya wagonjwa. Mwisho, kila taasisi ya huduma ya afya lazima iwe na kikanisa, ambacho uwepo wake utawakumbusha wote wanaofanya kazi pale (uongozi, staff, waganga na wauguzi), hali kadhalika wagonjwa wenyewe, kwamba Mungu peke yake ndiye Bwana wa uhai na mauti. Ingefaa kuongeza, kwa kiasi kikubwa inavyowezekana, idadi ya zahanati ndogondogo ambazo hutoa huduma kwa watu mahalia na msaada wa dharura.

IV. ULIMWENGU WA TEKNOLOGIA YA TAARIFA NA MAWASILIANO (INFORMATION TECHNOLOGY AND COMMUNICATION)

142. Hati ya kitume Ecclesia in Africa iliona vyombo vya habari vya kisasa si tu kama vifaa vya mawasiliano, lakini pia kama “ulimwengu unaohitaji kuenezewa Injili.”[194] Vyombo vya habari (media) lazima vihudumie mawasiliano ya kweli, ambayo ni kipaumbele kwa Afrika, kwa kuwa ni nguvu kubwa kwa maendeleo ya bara hilo[195] na kwa uinjilishaji. “Media zinaweza kutoa mchango muhimu kuelekea kukua kwa muunganiko wa familia ya wanadamu na utamaduni wa jamii zinapotumika kukuza ushiriki wa pamoja katika utafiti wa pamoja wa kile ambacho ni haki.”[196]

143. Kila mmoja anajua kwamba tekinolojia mpya za taarifa (information technologies) zina uwezo wa kuwa nyenzo zenye nguvu kwa ajili ya umoja na amani, lakini pia zinaweza kutumika kwa kuharibu na kugawanya. Kwa mtazamo wa kimaadili, zinaweza zikatoa au huduma au kuharibu huduma, kusambaza ukweli hali kadhalika kusambaza uongo, kupendekeza kile ambacho ni kibaya au kile ambacho ni kizuri. Mafuriko ya habari au ya zisizo habari, bila kusema juu ya picha mbalimbali, yanaweza kuwa kwa ajili ya kufikisha ujumbe fulani lakini pia yanaweza kuwa nyenzo zenye nguvu ya kupotosha ukweli. Taarifa zinaweza kwa urahisi kuwa upotoshaji wa taarifa, na malezi kuwa kutengua malezi (deformation). Media zinaweza kuwa nguvu kwa ajili ya kujenga utu wa kweli, lakini pia zinaweza kutumiwa kwa urahisi ili kuharibu ubinadamu.

144. Media zinaweza kukwepa hatari hii “kama zinaelekezwa kwenye muono (vision) wa mtu na ya maslahi ya umma ambao hutoa taswira ya kweli ya tunu za jumla. Kwa sababu tu mawasiliano ya kijamii huongeza uwezekano wa mahusiano kati ya watu wa mahali tofauti na kusambaza mawazo, haifuati kimantiki kwamba zinakuza uhuru au kufanya maendeleo yawe ya kimataifa na demokrasia kwa wote. Kufikia malengo kama haya, zinahitaji kulenga kwenye kukuza heshima ya nafsi na watu; zinahitaji kuvuviwa waziwazi na upendo na kuwekwa katika huduma ya ukweli, ya wema, na ya udugu asilia na udugu wa kiroho.”[197]

145. Kanisa linahitaji kuwepo zaidi na zaidi katika media ili kuzifanya siyo tu zana za kuenezea Injili lakini pia kwa ajili ya kuelimisha watu wa Afrika juu ya upatanisho katika ukweli, na kukuza haki na amani. Malezi makini katika maadili na ukweli yatasaidia waandishi wa habari kuepuka mvuto kwa mambo ya kushangaza, na kishawishi cha kupotosha habari na kutengeneza pesa za haraka haraka. Waandishi wa habari Wakristo wasiogope kuonyesha imani yao! Ni lazima waionee fahari! Uwepo na shughuli za waamini walei wenye uwezo katika ulimwengu wa vyombo vya mawasiliano vya umma na vya binafsi ni lazima uhimizwe. Kama chachu katika unga, wataendelea kushuhudia mchango chanya na wa kujenga ambao mafundisho ya Kristo na ya Kanisa lake huyatoa kwa ulimwengu.

146. kwa njia hii, uamuzi wa ule Mkutano Maalumu wa kwanza kwa ajili ya Afrika wa kufikiri mawasiliano kama mmoja wa mihimili mikuu ya uinjilishaji umeonyesha mafanikio kwa maendeleo ya media Katoliki. Ingekuwa labda pia inafaa kuratibu miundo iliyopo, kama inavyofanyika tayari katika maeneo fulani fulani. Uboreshaji kama huo katika matumizi ya media utachangia kwa kiasi kikubwa kutangaza tunu zilizo jadiliwa katika Sinodi: amani, haki na upatanisho barani Afrika,[198] na utaliwezesha bara kushiriki katika maendeleo ya sasa ya ulimwengu.

SURA YA III
“SIMAMA, JITWIKE GODORO LAKO, UENDE”
(Yn 5:8)

I. MAFUNDISHO YA YESU KWENYE BIRIKA LA BETHZATHA

147. Wapendwa ndugu zangu Maaskofu, wapendwa wana na binti za Afrika, baada ya kuwa tumeangalia upya mhimili mkuu wa utendaji na baadhi ya nyenzo ambazo Mkutano Maalumu kwa ajili ya Afrika wa Sinodi ya Maaskofu ulipendekeza kwa ajili ya utekelezaji wa utume wa Kanisa, ningependa kurudi kwenye pointi fulani ambazo tayari nimezigusia.

148. Ile sura ya tano ya Injili ya Yohane inatuletea picha inayogusa kwa namna ya pekee kabisa: lile birika la Bethzatha, na yale matao yake matano ambamo “jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete na waliopooza” (a. 3). Haya ndiyo mazingira ya uponywaji ambao karibu unatokea. “Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane” (a. 5), lakini hakuwa na mtu wa kumweka katika birika. Hapo Yesu anaingia katika maisha yake. Mambo yote yanabadilika mara Yesu anapomwambia: “Simama, jitwike godoro lako, uende” (a. 8). “Mara moja”, mwinjili anatuambia, “yule mtu akawa mzima” (a. 9). Hakuhitaji tena maji ya birika.

149. Kwa kumpokea Yesu, Afrika inaweza kupokea uponyaji usio kifani na wa kina. Nikirudia yale aliyosema Mtume Petro katika Matendo ya Mitume (3:6), ninasisitiza: Afrika inachohitaji zaidi ya yote wala si dhahabu wala fedha; inataka kusimama juu, kama yule mtu katika birika la Bethzatha; inataka kujiamini na kuwa na imani katika hadhi yake kama watu wanaopendwa na Mungu wao. Ni kukutana huku na Yesu ambako Kanisa ni lazima litoe kwa walioumizwa na waliojeruhiwa mioyo wakitamani upatanisho na amani, na wakiionea kiu haki. Ni lazima tutoe na tutangaze neno la Kristo ambalo huponya, huweka huru na kupatanisha.

II. NENO LA MUNGU NA SAKRAMENTI ZAKE

A. Maandiko Matakatifu

150. Kadiri ya Mtakatifu Jerome, “kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo.”[199] Kusoma na kutafakari neno la Mungu siyo tu hutupa “uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu” (Flp 3:8), lakini pia hutupa mizizi ya kina zaidi katika Kristo na huongoza huduma yetu ya upatanisho, haki na amani. Adhimisho la Ekaristi, ambalo sehemu yake ya kwanza ni Liturujia ya Neno, ni chanzo na kilele chake. Kwa sababu hiyo, ninapendekeza kwamba Utume wa Biblia uhamasishwe katika kila jumuiya ya Kikristo, katika familia na katika vyama vya kitume.

151. Kila mmoja wa waamini wa Kristo anapaswa kukua katika mazoea ya kusoma Biblia kila siku! Usomaji makini wa Mausia ya Kitume ya hivi karibuni Verbum Domini unaweza kutoa baadhi ya viashiria vya kufaa vya kiuchungaji. Uangalifu unatakiwa kuchukuliwa kuwaingiza waamini katika mapokea ya zamani na yenye kuzaa tunda ya masomo matakatifu (lectio divina). Neno la Mungu linaweza kutuongoza kwenye kumjua Yesu Kristo na kuleta uongofu ambao huzaa upatanisho, kwa kuwa lina uwezo wa kuyachunguza “mawazo na makusudi ya moyo”. Mababa wa Sinodi walihimiza jumuiya za kiparokia, JNNK, familia na vyama vya kitume kutenga muda kwa ajili ya kushirikishana neno la Mungu.[200] Kwa njia hii, sehemu hizi zitazidi kuwa mahali ambapo neno la Mungu, ambalo huijenga jumuiya ya wafuasi wa Kristo, linasomwa, linatafakariwa na kuadhimishwa. Neno hili daima huchachua muungano wa kidugu (rej. 1Pet 1:22-25).

B. Ekaristi Takatifu

152. Njia yenye ufanisi kuliko zote kwa kujenga jamii iliyopatanishwa, ya haki na amani, ni maisha ya muungano wa kina na Mungu na watu wengine. Meza ya Bwana huunganisha pamoja waume na wake wa kutoka sehemu na kabila tofauti tofauti, wenye tamaduni, rangi na lugha tofauti. Kwa kupokea Mwili na Damu ya Kristo, wanakuwa kweli umoja. Katika Kristo Ekaristi, wanakuwa na mahusiano ya damu na hivi kaka na dada wa kweli, kwa njia ya neno na ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo yuleyule. Kifungo hiki cha udugu ni imara zaidi kuliko kile cha familia za kibinadamu, kuliko kile cha kabila zetu. “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi” (Rum 8:29). Mfano wa Yesu unawawezesha kupendana na kutoa maisha yao kila mmoja kwa ajili ya wengine, maana upendo ule ambao kwao mmoja anapendwa unatakiwa kushirikiwa kwa matendo na katika ukweli.[201] Inafuata kwamba, adhimisho la kijumuiya la Dominika, Siku ya Bwana, na la Sikukuu zilizoamriwa ni la lazima.

153. Sikusudii kuweka hapa maelezo ya kiteolojia juu ya Ekaristi. Katika Mausia ya Kitume baada ya Sinodi Sacramentum Caritatis nimeonyesha baadhi ya mambo muhimu yanayohusu Ekaristi. Hapa ninalihimiza Kanisa zima huko Afrika kuonyesha uangalifu wa pekee kwa adhimisho la Ekaristi, kumbukumbu ya sadaka ya Kristo Yesu, ishara ya umoja na kifungo cha upendo, karamu ya Pasaka na amana ya uzima wa milele. Ekaristi ni lazima iwe inaadhimishwa kwa heshima na uzuri, kulingana na kanuni zilizowekwa. Kuabudu Ekaristi, kwa mmoja mmoja na katika jumuiya, kutapelekea kulithamini kwa kina fumbo hili kubwa. Katika mwelekeo huu, Makongamano ya kibara ya Ekaristi yanaweza kuadhimishwa. Hili lingeimarisha jitihada za Wakristo kushuhudia tunu msingi za muungano katika kila jamii ya Kiafrika.[202]

154. Ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na heshima kwa fumbo la Ekaristi, mababa wa Sinodi walikumbusha kwamba makanisa na vikanisa ni mahali patakatifu, pa kutumiwa kwa ajili ya maadhimisho ya kiliturujia tu, kwa kukwepa iwezekanavyo kuyafanya yawe mahali pa makusanyiko ya kijamii au mahali pa kitamaduni tu. Kuna hitaji kukazia matumizi yake msingi, ambayo ni yale ya kuwa mahali palipopendelewa pa kukutana kati ya Mungu na watu wake, kati ya Mungu na kiumbe chake mwaminifu. Kuna pia hitaji la kuhakikisha kwamba majengo matakatifu haya yanakuwa katika hali inayolingana na fumbo linaloadhimishwa humo na kulingana na sheria za Kanisa na mtindo mahalia. Ni lazima yajengwe kwa uangalizi wa maaskofu, baada ya kusikiliza mawazo ya watu wenye uwezo katika liturujia na usanifu majengo. Watu wanapoingia katika majengo haya waweze kusema: “Kweli Bwana yupo mahali hapa... Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbingu” (Mwa 28:16-17)! Yatatimiza pia madhumuni yake kama yatasaidia jumuiya, iliyozaliwa upya katika Ekaristi na sakramenti zingine, kuendeleza adhimisho katika maisha ya jamii kwa kuendeleza daima mfano wa Kristo mwenyewe (rej. Yn 13:15).[203] Huo “msimamo wa kiekaristi”[204] unaipa changamoto kila dhamiri ya Kikristo (rej. 1Kor 11:17-22).

C. Upatanisho

155. Ili kuzisaidia jamii za Kiafrika kuponya majeraha ya utengano na chuki, mababa wa Sinodi walilitaka Kanisa likumbuke kwamba linachukua ndani yake lenyewe majeraha na maumivu yaleyale. Kwa hiyo, nalo linahitaji uponyaji wa Bwana, ili liweze kushuhudia kwa kuaminika kwamba sakramenti ya Upatanisho huunganisha na kuponya mioyo iliyojeruhiwa. Sakramenti hii hurekebisha vifungo vilivyokatika kati ya mtu na Mungu, na hutengeneza tena vifungo ndani ya jamii. Pia huifundisha mioyo yetu na roho zetu kuishi katika “umoja wa mioyo, huruma, kupendana kindugu, upole na unyenyekevu” (1Pet 3:8).

156. Hapa napenda kukumbusha umuhimu wa maungamo ya mtu mmoja peke yake, ambayo hakuna matendo mengine ya upatanisho au liturujia fulani yanayoweza kuwa badala yake. Ninawahimiza waamini wote wa Kanisa, maklero, watu wa maisha ya wakfu na walei, kuirudisha kwenye nafasi yake ya kweli sakramenti ya Upatanisho katika nyanja zake mbili, ya mtu peke yake na ya kimuungano kama jumuiya.[205] Jumuiya zinazokosa mapadre kwa sababu ya umbali mkubwa au kwa sababu nyingine yoyote zinaweza kuonja ile tabia ya kikanisa ya Kitubio na Upatanisho kwa njia ya aina isiyokuwa ya kisakramenti. Kwa njia hii, Wakristo waliojifungia masakramenti wanaweza pia kushiriki katika safari ya toba ya Kanisa. Kama mababa wa Sinodi walivyoonyesha, zile aina za Kitubio zisizo za kisakramenti zinaweza kufikiriwa kama njia ya kuwatayarisha waamini kwa ajili ya kupokea sakramenti kunakozaa matunda,[206] lakini kamwe haiwezi kuwa utaratibu wa kawaida, zaidi, hauwezi kuwa utaratibu mbadala wa sakramenti yenyewe. Nawahimiza mapadre kung’amua sakramenti hii katika maisha yao na kufanya kila liwezekanalo kuwa tayari kwa adhimisho lake.

157. Ili kuhamasisha upatanisho katika jumuiya, kwa moyo ninapendekeza, kama mababa wa Sinodi walivyopendekeza, kwamba kila nchi iwe inaadhimisha kila mwaka “siku au wiki ya upatanisho, kwa namna ya pekee wakati wa Majilio au Kwaresima”.[207] SECAM itasaidia kufanikisha hili na, kwa kuafikiana na Kiti Kitakatifu, uhamasishwe kibara zima Mwaka wa Upatanisho ili kumwomba Mungu msamaha wa pekee kwa maovu yote na maumivu yote tuliyotendeana hapa Afrika, na kwa upatanisho wa watu na vikundi ambao wameumizwa katika Kanisa na katika jamii nzima.[208] Huu ungekuwa ni Mwaka maalumu wa Jubilei “ambamo Kanisa barani Afrika na katika visiwa jirani linamshukuru Mungu pamoja na Kanisa lote zima na kuomba vipaji vya Roho Mtakatifu”,[209] hasa zawadi ya upatanisho, haki na amani.

158. Kwa ajili ya maadhimisho haya, ingesaidia kufuata ushauri wa mababa wa Sinodi: “Tunaomba kumbukumbu ya mashahidi wakubwa waliotolea maisha yao kwa ajili ya huduma ya Injili na maslahi ya umma, au kwa ajili ya kutetea ukweli na haki za binadamu, itunzwe hai na ikumbukwe kwa uaminifu.”[210] Kwa sababu watakatifu ni nyota za kweli za maisha yetu, wale ambao “waliishi maisha mazuri. Ni mianga ya matumaini. Kwa hakika, Yesu Kristo ndiye nuru ya kweli, jua lililochomoza juu ya kila kivuli cha historia. Lakini ili kumfikia yeye tunahitaji pia mianga inayokuwa karibu – watu ambao wanang’aa kwa mwanga wake na kwa hiyo hutuongoza kwenye njia yetu.”[211]

III. UINJILISHAJI MPYA

159. Kabla ya kuhitimisha hati hii, ningependa kurudi tena kwenye kazi inayolikabili Kanisa barani Afrika: uwajibikaji katika uinjilishaji, kwa missio ad gentes, na kwa uinjilishaji mpya, ili sura ya bara la Afrika iweze kuundwa upya tena na tena kulingana na mafundisho ya Kristo, aliye kweli “nuru ya ulimwengu” na aliye halisi “chumvi ya dunia” yanayotufikia kila mara kwa wakati mwafaka.

A. Wanaombeba Kristo, aliye “mwanga wa ulimwengu”

160. Kazi ya uinjilishaji, ambayo ndiyo kipaumbele, inafanywa kwa njia mbalimbali sawasawa na tofauti za hali na mazingira ya kila nchi. “Katika maana yake halisi, uinjilishaji ni utume kwa mataifa (missio ad gentes) unaoelekezwa kwa wale ambao hawamjui Kristo. Katika maana pana zaidi, neno uinjilishaji hutumika kuelezea kazi za kawaida za kichungaji, wakati msemo “uinjilishaji mpya” unamaanisha shughuli za kichungaji kwa wale ambao hawaishi tena imani ya Kikristo.[212] Uinjilishaji uliovuviwa na nguvu ya Roho Mtakatifu tu ndio unaoweza kuwa “sheria mpya ya Injili” na kuzaa matunda ya kiroho.[213] Roho ya kazi zote za uinjilishaji ni utangazaji wa nafsi ya Yesu, Neno wa Mungu aliyetwaa mwili (rej. Yn 1:14) ambaye alikufa na kufufuka tena na daima yupo katika jumuiya ya waamini, yaani Kanisa lake (rej. Mt 28:20). Hili ni jukumu linalotusukuma tufanye kazi mara moja siyo tu kwa Afrika, lakini kwa ulimwengu mzima, maana utume ambao Kristo Mkombozi aliukabidhi kwa Kanisa lake bado haujatimilika.

161. “Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu” (Mk 1:1) ni njia ya uhakika kwa kukutana na nafsi ya Bwana Yesu. Kuyachunguza Maandiko hutuwezesha zaidi na zaidi kugundua uso wa kweli wa Yesu, aliye ufunuo wa Mungu Baba (rej. Yn 12:45), na kazi yake ya ukombozi. “Kugundua upya ukiini wa neno la Mungu katika maisha ya Kikristo hutuongoza kwenye kuthamini upya ule wito ambao Papa Yohane Paulo II aliutoa kwa ari: kutekeleza missio ad gentes na kuanza kwa nguvu kabisa kazi ya uinjilishaji mpya.”[214]

162. Likiongozwa na Roho Mtakatifu, Kanisa barani Afrika ni lazima litangaze fumbo la wokovu – kwa kuliishi – kwa wale ambao hawajajifunza kuhusu hilo. Roho Mtakatifu ambaye Wakristo walimpokea katika Ubatizo ni moto wa upendo unaotusukuma kufanya kazi ya uinjilishaji. Baada ya Pentekoste, wanafunzi, “wakiwa wamejazwa Roho Mtakatifu” (Mdo 2:4), walitoka kwenye chumba cha Karamu ya Mwisho, ambako walikuwa wamekimbilia kwa sababu ya hofu, na wakatangaza Habari Njema ya Yesu Kristo. Tukio la Pentekoste hutuwezesha kuelewa vizuri zaidi utume wa Wakristo kama “nuru ya ulimwengu” na “chumvi ya dunia” barani Afrika. Ni tabia ya mwanga kusambazwa na kung’ara juu ya kaka na dada zetu walio wengi ambao bado wako gizani. Missio ad gentes inadai uwajibikaji kwa upande wa Wakristo wote wa Afrika. Wakisukumwa na Roho, wanamleta Yesu Kristo, “nuru ya ulimwengu”, kila mahali barani na maeneo mengine yote ya maisha ya mtu binafsi, ya familia na ya kijamii. Mababa wa Sinodi walisisitiza “hitaji la uinjilishaji, ambalo ni utume na utambulisho halisi wa Kanisa.[215]

B. Mashahidi wa Kristo Mfufuka

163. Leo pia, Bwana Yesu anawataka Wakristo wa Afrika watangaze kwa jina lake “toba na ondoleo la dhambi kwa mataifa yote” (Lk 24:47). Kwa sababu hii, wanaitwa kuwa mashahidi wa Bwana Mfufuka (rej. Lk 24:48). Mababa wa Sinodi walisisitiza kwamba uinjilishaji “kimsingi unahusika na kutoa ushahidi kwa Kristo katika nguvu ya Roho kwa njia ya maisha ya kila mmoja wetu, baadaye kwa maneno ya kila mmoja wetu, katika roho ya uwazi na mazungumzano ya kuheshimiana na wengine, wakati huohuo tukishikilia kwa nguvu zile tunu za Injili.”[216] Kwa suala la Kanisa barani Afrika, ushuhuda huu unahitaji kuwa katika huduma ya upatanisho, haki na amani.

164. Utangazaji wa Injili lazima urudishe ari ya mwanzoni mwa uinjilishaji wa bara la Afrika, ambao unaelekezwa kwa mwinjili Marko na kuendelezwa na “watakatifu wengi wasiohesabika, mashahidi, waungama na mabikira”.[217] Kuna hitaji kwa kukumbuka kwa shukrani kubwa na kuiga ari ya wamisionari wengi ambao, kwa muda wa karne nyingi, walitolea sadaka maisha yao ili kuileta Habari Njema kwa kaka na dada zao barani Afrika. Kwa miaka ya hivi karibuni Kanisa katika nchi mbalimbali limefanya kumbukumbu ya miaka mia moja ya uinjilishaji. Kanisa limefanya upya uwajibikaji wake wa kuileta Injili kwa wale ambao bado hawajalijua jina la Yesu Kristo.

165. Katika jitihada ya kuwa na ufanisi zaidi, ile missio ad gentes lazima iende sambamba na uinjilishaji mpya. Barani Afrika pia, hali zinazodai kuieleza Injili kwa namna mpya, “mpya katika ari yake, mbinu na vielelezo”,[218] si haba. Kwa namna ya pekee, uinjilishaji mpya unahitaji kuunganisha uwanja wa kiakili wa imani na mang’amuzi hai ya kukutana na Yesu Kristo aliyepo na akifanya kazi ndani ya jumuiya ya kikanisa. Kuwa Mkristo si matokeo ya kufanya uamuzi wa kimaadili au ya mawazo fulani ya hali ya juu, lakini ni kukutana na tukio, nafsi, ambaye huyapa maisha mtazamo mpya na mwelekeo mkataa. Kwa hiyo, katekesi lazima iunganishe nadharia zake, ambazo hujihusisha na dhana za kujifunza kwa moyo, na utendaji wake, ambao hung’amuliwa katika ngazi za kiliturujia, kiroho, kikanisa, kiutamaduni na kiutendaji huruma, ili mbegu ya neno la Mungu mara inapoanguka katika ardhi yenye rutuba, iweze kuzamisha mizizi kwa kina hadi kufikia ukomavu.

166. Ili jambo hilo litokee, ni muhimu kutumia mbinu mpya zilizopo kwetu leo. Kuhusu njia za mawasiliano ya jamii, ambazo nimekwisha kuziongelea, ningependa kukumbusha wazo moja nililosisitiza katika Mausia ya Kitume baada ya Sinodi ya hivi karibuni iitwayo Verbum Domini: “Mtakatifu Tomaso [wa Akwino], akimrejea Mtakatifu Augustino, anasisitiza kwamba ‘herufi, hata ile ya Injili, ingeua, kama kusingekuwa na neema ya imani iponyayo’.”[219] Tukizingatia hilo, lazima pia ikumbukwe daima kwamba njia yoyote ya mawasiliano haiwezi wala haitakiwi kuwa njia mbadala ya kukutana moja kwa moja, ya kutangaza kwa maneno na kutoa ushuhuda wa maisha yaliyo ya Kikristo kwelikweli. Kuwasiliana kwa kukutana moja kwa moja na kutangaza kwa kuongea kunahitaji kudhihirisha imani hai ambayo hufungamana na maisha ya watu na kuyabadilisha, hali kadhalika na upendo wa Mungu ambao humfikia na kumgusa kila mmoja kama alivyo.

167. Kanisa linalosafiri barani Afrika pia linaitwa kuchangia katika uinjilishaji mpya kwenye nchi zilizoacha imani, ambazo zamani zilitoa wamisionari wengi lakini leo kwa masikitiko zimekosa miito ya upadre na ya maisha ya wakfu. Kwa sasa, idadi kubwa ya wanaume na wanawake Waafrika wamekubali mwaliko wa Bwana wa mavuno (rej. Mt 9:37-38) kufanya kazi katika shamba lake (rej. Mt 20:1-16). Bila kudhoofisha msukumo wa kimisionari ad gentes katika nchi mbalimbali, na hata katika bara zima, maaskofu wa Afrika lazima waitikie kwa ukarimu maombi ya maaskofu wenzao katika nchi zisizokuwa na miito na wawasaidie waamini wasiokuwa na mapadre. Namna hii ya kushirikiana, ambayo ni lazima iratibiwe na makubaliano kati ya Kanisa linalotuma na Kanisa linalopokea, inakuwa ishara wazi ya ufanisi wa missio ad gentes. Kwa vile inavyobarikiwa na Bwana, aliye Mchungaji Mwema (rej. Yn 10:11-18), hutoa msaada wa maana kwa ajili ya uinjilishaji mpya katika nchi za mapokea ya Ukristo ya zamani.

168. Utangazaji wa Habari Njema huzaa ndani ya Kanisa mambo mengine yanayopatana na mahitaji, tamaduni na matazamio ya nyakati zetu. Barani Afrika pia, Roho Mtakatifu daima anainua watu ambao, wakiwa wamekusanyika katika vyama, taasisi na jumuiya mbalimbali, hutolea maisha yao kwa ajili ya uenezaji wa Injili ya Yesu Kristo. Katika mwanga wa maonyo ya Mtakatifu Paulo: “Msimzimishe Roho, msitweze unabii; jaribuni mambo yote; lishikilieni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna” (1The 5:19-22), wachungaji wana wajibu wa kuhakikisha kwamba haya matokeo mapya ya uwezo wa daima wa Injili wa kuzaa matunda yameunganishwa katika kutenda kazi ya kitume ya maparokia na majimbo.

169. Wapendwa kaka na dada, mada ya Mkutano Maalumu wa Pili kwa ajili ya Afrika inatukumbusha kwamba uinjilishaji mpya hasa unahusu huduma ya Kanisa ya upatanisho, haki na amani. Kwa hiyo, kuna haja ya kuikaribisha neema ya Roho Mtakatifu ambaye hutusihi: “Mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:20). Wakristo wote wanaonywa wapatanishwe na Mungu. Kwa njia hii ninyi mtakuwa watendaji wa upatanisho ndani ya jumuiya za kikanisa na za kijamii ambamo mnaishi na kufanya kazi. Uinjilishaji mpya unachukulia kwamba Wakristo wamepatanishwa na Mungu na wao kwa wao. Unadai tuwe tumepatanishwa na majirani zetu, na tuwe tumeshinda kila aina ya vikwazo, ikiwa ni pamoja na vile ambavyo vinaibuka kutokana na lugha, tamaduni na kabila. Sisi sote ni watoto wa Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye “huwaangazia jua lake waovu na wema, na huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki (Mt 5:45).

170. Mungu ataubariki moyo uliopatanishwa kwa kuupatia amani yake. Wakristo kwa hiyo watakuwa wapatanishi (rej. Mt 5:9) kiasi kwamba, wakiwa na msingi katika neema za Mungu, wanashirikiana na Muumba wao katika kujenga na kuimarisha zawadi ya amani. Kama watu waliopatanishwa, waamini pia watahamasisha haki kila mahali, hasa ndani ya jamii za Afrika zilizogawanyika na zilizotishiwa na ukatili na vita, na bado wana njaa na kiu ya haki ya kweli. Bwana anatuhimiza: “Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu, na haki yake, na mengine yote mtapewa kwa ziada” (Mt 6:33).

171. Uinjilishaji mpya ni kazi inayodai kutekelezwa mara moja na Wakristo wa Afrika kwa sababu wao pia wanahitaji kuamsha upya ari yao ya kuwa wanakanisa. Wakiongozwa na Roho ya Bwana Mfufuka, wameitwa kuiishi Habari Njema kama mtu mmoja mmoja, katika familia zao na katika jamii, na kuitangaza kwa ari mpya kwa watu walio karibu na walio mbali, kwa kutumia mbinu mpya ambazo tumejaliwa na Mungu kwa ajili ya kuieneza. Katika kumsifu Mungu Baba kwa maajabu ambayo anaendelea kufanya katika Kanisa lake na katika kila mwanakanisa, waamini wameitwa kuchochea wito wao wa kikristo katika uaminifu kwa Mapokeo hai ya Kanisa. Tukiwa wazi kwa maongozi ya Roho Mtakatifu ambaye anaendelea kuamsha karama mbalimbali katika Kanisa, Wakristo lazima watafute kwa makusudi mazima kuchukua njia ya utakatifu, na hivi zaidi na zaidi kuwa mitume wa upatanisho, haki na amani.

 

HITIMISHO
“JIPE MOYO; INUKA, ANAKUITA”
(Mk 10:49)

172. Wapendwa kaka na dada zangu, neno la mwisho la Sinodi lilikuwa wito kwa matumaini ulioelekezwa kwa Afrika. Wito huu utakuwa bure isipokuwa una mizizi katika upendo wa Utatu Mtakatifu. Kutoka kwa Mungu, Baba wa wote, tunapata utume wa kuipelekea Afrika upendo ambao kwa huo Kristo, Mwana mzaliwa wa kwanza, ametupenda, ili kazi zetu, zikisukumwa na Roho wake Mtakatifu, ziongozwe na matumaini na kuwa chanzo cha matumaini. Wakati tunatamani kwa nguvu kusaidia kuweka katika vitendo maelekezo ya Sinodi juu ya masuala motomoto kama vile upatanisho, haki na amani, ninapenda kusema kuwa nina imani kwamba “wanateolojia wataendelea kutafiti kina cha fumbo la Utatu Mtakatifu na maana yake kwa maisha ya kila siku ya Kiafrika”.[220] Kwa kuwa wito wa wanadamu wote ni mmoja, haitupasi kupoteza ari yetu kwa upatanisho wa ubinadamu na Mungu kwa njia ya fumbo la wokovu wetu katika Kristo. Ukombozi wetu ni sababu ya uhakika na uthabiti wa matumaini yetu, ambayo “kwa mujibu wa hiyo tunaweza kuukabili wakati wetu uliopo: wakati uliopo, hata kama ni mgumu, unaweza kupendwa na kupokelewa ikiwa unaongoza kwenye lengo, ikiwa twaweza kuwa na uhakika juu ya lengo hili, na kama lengo hili ni kubwa ya kutosha kuhalalisha jitihada ya safari”.[221]

173. Kwa mara nyingine tena nasema: “Simama, Kanisa barani Afrika ... kwa sababu unaitwa na Baba wa mbinguni, ambaye wahenga wenu walimtambua kama Muumba hata kabla ya kujua ukaribu wake wa kihuruma uliofunuliwa katika Mwanae wa pekee, Yesu Kristo. Iweni katika njia ya uinjilishaji mpya kwa ujasiri ambao unawajieni kutoka kwa Roho Mtakatifu.”[222]

174. Uinjilishaji leo unachukua jina la upatanisho, “sharti la lazima ili kuamsha katika Afrika haki miongoni mwa watu, na kujenga amani ya haki na ya kudumu ambayo huheshimu kila mtu na watu wote; amani ambayo... iko wazi kwa mchango wa watu wote wenye mapenzi mema bila kujali dini zao, ukabila, lugha, utamaduni na jamii walimokulia.”[223] Tunaomba Kanisa Katoliki lote liandamane kwa upendo na ndugu zake wa bara la Afrika! Watakatifu wa Afrika wawategemeze kwa sala na maombezi yao![224]

175. “Mtakatifu Yosefu, msimamizi mwema wa nyumba yake, ambaye binafsi anajua maana ya kufikiria, kwa umakini na kwa matumaini, mwelekeo wa familia kwa siku zijazo,[na ambaye] kwa upendo alitusikiliza na akatusindikiza kwenye Sinodi yenyewe”,[225] alilinde na kulisindikiza Kanisa katika utume wake wa kuihudumia Afrika, nchi ambapo alipata kimbilio na hifadhi kwa ajili ya Familia Takatifu (rej. Mt 2:13-15)! Naomba Bikira Maria Mtakatifu, Mama wa Neno wa Mungu na Mama yetu wa Afrika, aendelee kulisindikiza Kanisa zima kwa maombezi yake na kwa mwaliko wake wa kufanya chochote ambacho Mwanae anatuambia (rej. Yn 2:5)! Na sala za Maria, Malkia wa Amani, ambaye moyo wake daima unaelekea mapenzi ya Mungu, ategemeze kila jitihada ya uongofu; aimarishe kila mpango wa upatanisho na atie nguvu kila jitihada ya kuleta amani katika ulimwengu ambao una njaa na kiu ya haki (rej. Mt 5:6).[226]

176. Wapendwa kaka na dada, kwa njia ya Mkutano Maalumu wa Pili kwa ajili ya Afrika wa Sinodi ya Maaskofu, Bwana wetu, katika wema na huruma yake unawakumbusheni kwa ari kwamba “Ninyi ni chumvi ya dunia ... Ninyi ni nuru ya ulimwengu” (Mt 5:13.14) Maneno haya yawakumbusheni hadhi ya wito wenu kama watoto wa Mungu na viungo vya Kanisa lililo moja, takatifu, katoliki na la Mitume! Wito huo ni wito wa kung’arisha katika ulimwengu huu, ambao mara nyingi hukaa kwenye giza, mwangaza wa Injili na nuru ya Yesu Kristo, ambaye ndiye mwanga halisi “amtiaye nuru kila mtu” (Yn 1:9). Wakristo wanapaswa kuwapa kila mtu shauku ya Mungu Baba, furaha ya uwepo wake bunifu katika ulimwengu. Wenyewe waitwa pia kushirikiana na neema ya Roho Mtakatifu, kusudi mwujiza wa Pentekoste upate kuenea katika bara zima la Afrika, na kila mtu aweze kuwa zaidi na zaidi mtume wa upatanisho, haki na amani.

177. Kanisa barani Afrika liwe daima pafu la kiroho kwa ubinadamu, na kupata kuwa kila siku baraka kubwa zaidi na zaidi kwa ajili ya bara bora la Afrika na kwa ulimwengu mzima.

Imetolewa Ouidah, huko Benin, tarehe 19 Novemba, mwaka 2011, wa saba wa Upapa wangu.

 

BENEDIKTO XVI


 

Tanbihi:

[1] John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Ecclesia in Africa (14 September 1995), 1:AAS 88 (1996), 5.

[2] Cf. First Special Assembly for Africa of the Synod of Bishops, Final Message (6 May 1994), 24-25; John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Ecclesia in Africa (14 September 1995), 63: AAS 88 (1996), 39-40.

[3] Cf. Second Special Assembly for Africa of the Synod of Bishops, Propositio 1.

[4] Cf. Propositio 2.

[5] Benedict XVI, Address to Members of the Special Council for Africa of the Synod of Bishops (Yaoundé, 19 March 2009): AAS 101 (2009), 310.

[6] John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Ecclesia in Africa (14 September 1995), 63:AAS 88 (1996), 39-40.

[7] Cf. No. 92: AAS 88 (1996), 57-58; cf. Second Vatican Ecumenical Council, Dogmatic Constitution on the Church Lumen Gentium, 11; Decree on the Apostolate of the LaityApostolicam Actuositatem, 11; John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Familiaris Consortio (22 November 1981), 21: AAS 74 (1982), 104-106.

[8] Cf. No. 63:AAS 88 (1996), 39-40.

[9] Quis dives salvetur 29; PG 9, 633.

[10] Benedict XVI, Address to the Roman Curia (21 December 2009): AAS 102 (2010), 35.

[11] No. 79: AAS 88 (1996), 51.

[12] Benedict XVI, Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 1: AAS 101 (2009), 641.

[13] Id., Homily at the Opening Mass of the Second Special Assembly for Africa of the Synod of Bishops (4 October 2009): AAS 101 (2009), 907.

[14] John Paul II, Apostolic Letter Novo Millennio Ineunte (6 January 2001), 3: AAS 93 (2001), 267.

[15] Ibid., 29: AAS 93 (2001), 286.

[16] Adversus Haereses IV, 20, 7: PG 7, 1037.

[17] Propositio 34.

[18] Benedict XVI, Homily at the Closing Mass of the Second Special Assembly for Africa of the Synod of Bishops (25 October 2009): AAS 101 (2009), 918.

[19] Propositio 46.

[20] Twelfth Ordinary General Assembly of the Synod of Bishops, Final Message (24 October 2008), 10.

[21] Benedict XVI, Address to the Roman Curia (21 December 2009): AAS 102 (2010), 35.

[22] Cf. Id., Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 5-9: AAS 101 (2009), 643-647.

[23] Id., Address to the Roman Curia (21 December 2009): AAS 102 (2010), 35.

[24] Id., Message for the 2008 World Day of PeaceAAS 100 (2008), 38-45.

[25] Id., Address to the Roman Curia (21 December 2009): AAS 102 (2010), 37.

[26] Cf. Propositio 5.

[27] Relatio ante disceptationem, II, a.

[28] Ibid.

[29] Benedict XVI, Address to the Roman Curia (21 December 2009): AAS 102 (2010), 35.

[30] Cf. Id., Homily at the Closing Mass of the Second Special Assembly for Africa of the Synod of Bishops (25 October 2009): AAS 101 (2009), 916.

[31] Cf. John Paul II, Message for the 1997 World Day of Peace, 1: AAS 89 (1997), 1.

[32] Propositio 5.

[33] Cf. Benedict XVI, Encyclical Letter Deus Caritas Est (25 December 2005), 28: AAS 98 (2006), 238-240.

[34] Cf. Propositio 14.

[35] Benedict XVI, Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 9: AAS 101 (2009), 646-647.

[36] Cf. Id., Encyclical Letter Deus Caritas Est (25 December 2005), 28-29: AAS 98 (2006), 238-240; International Theological Commission, Select Questions on the Theology of God the Redeemer (29 November 1994), 14-20: Enchiridion Vaticanum 14, Nos. 1844-1850.

[37] Cf. Second Vatican Ecumenical Council, Pastoral Constitution on the Church in the Modern World Gaudium et Spes, 40; Pontifical Council for Justice and Peace, Compendium of the Social Doctrine of the Church, 49-51.

[38] Cf. Saint Thomas Aquinas, Summa Theol., IIa-IIae, q. 58, a. 1.

[39] Cf. John Paul II, Encyclical Letter Centesimus Annus (1 May 1991), 35: AAS 83 (1991), 837.

[40] Catechism of the Catholic Church, 1894.

[41] Lineamenta, 44.

[42] Saint Augustine, De Civitate Dei, XIX, 21,1: PL 41, 649.

[43] Cf. Benedict XVI, Message for Lent 2010 (30 October 2009): Insegnamenti V/2 (2009), 454.

[44] Cf. ibid.

[45] Cf. Propositio 17.

[46] Cf. Benedict XVI, Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 6: AAS 101 (2009), 644.

[47] Id., Encyclical Letter Deus Caritas Est (25 December 2005), 28: AAS 98 (2006), 240.

[48] Cf. Paul VI, Apostolic Exhortation Evangelii Nuntiandi (8 December 1975), 53, 80: AAS 68 (1976), 41-42, 73-74; John Paul II, Encyclical Letter Redemptoris Missio (7 December 1990), 46: AAS 83 (1991), 293.

[49] Cf. Final Message, 36.

[50] Cf. Second Vatican Ecumenical Council, Dogmatic Constitution on the Church Lumen Gentium, 1.

[51] Cf. Congregation for the Doctrine of the Faith, Doctrinal Note on some Aspects of Evangelization (3 December 2007), 9: AAS 100 (2008), 497-498.

[52] Lineamenta, 48.

[53] Propositio 43.

[54] Ibid.

[55] Cf. Benedict XVI, Address to the Pontifical Council for the Laity (21 May 2010):Insegnamenti VI/1 (2010), 758.

[56] Cf. Second Vatican Ecumenical Council, Decree on the Missionary Activity of the Church Ad Gentes, 15.

[57] Paul VI, Apostolic Exhortation Evangelii Nuntiandi (8 December 1975), 22: AAS 68 (1976), 20.

[58] Cf. Propositio 9.

[59] Cf. Propositio 8.

[60] Cf. Nos. 28-34: AAS 77 (1985), 250-273. This teaching was confirmed by the Apostolic Letter issued Motu proprio Misericordia Dei (2 May 2002): AAS 94 (2002), 452-459.

[61] Cf. Propositio 7.

[62] Cf. Apostolic Letter Novo Millennio Ineunte (6 January 2001), 43: AAS 93 (2001), 297.

[63] Ibid.

[64] Ibid.

[65] Cf. Propositio 9.

[66] Cf. Propositio 33.

[67] Congregation for the Doctrine of the Faith, Doctrinal Note on some Aspects of Evangelization (3 December 2007), 6: AAS 100 (2008), 494.

[68] Cf. Paul VI, Apostolic Exhortation Evangelii Nuntiandi (8 December 1975), 19-20: AAS 68 (1976), 18-19.

[69] Cf. John Paul II, Apostolic Letter Novo Millennio Ineunte (6 January 2001), 40: AAS 93 (2001), 295.

[70] Cf. Propositio 32.

[71] Benedict XVI, Second Special Assembly for Africa of the Synod of Bishops: Meditation after the Hour of Terce (5 October 2009): AAS 101 (2009), 924.

[72] No. 55: AAS 102 (2010), 734-735.

[73] Cf. Propositio 45.

[74] Benedict XVI, Address to Members of the Special Council for Africa of the Synod of Bishops (Yaoundé, 19 March 2009): AAS 101 (2009), 313.

[75] Cf. Id., Post-Synodal Apostolic Exhortation Sacramentum Caritatis (22 February 2007), 51: AAS 99 (2007), 144.

[76] Congregation for the Doctrine of the Faith, Letter to the Bishops of the Catholic Church on the Collaboration of Men and Women in the Church and in the World (31 May 2004), 13:AAS 96 (2004), 682.

[77] Benedict XVI, Message for the 2008 World Day of Peace, 3: AAS 100 (2008), 38-39.

[78] Cf. Propositio 38.

[79] Benedict XVI, Post-Synodal Apostolic Exhortation Sacramentum Caritatis (22 February 2007), 79: AAS 99 (2007), 165-166.

[80] Cf. ibid., 73.

[81] Cf. John Paul II, Apostolic Letter Novo Millennio Ineunte (6 January 2001), 38 and 39: AAS93 (2001), 293-294.

[82] John Paul II, Apostolic Exhortation Familiaris Consortio, 39: AAS 74 (1982), 130-131; cf. Paul VI, Apostolic Exhortation Evangelii Nuntiandi (8 December 1975), 71: AAS 68 (1976), 60-61.

[83] John Paul II, Homily for the Jubilee of the Elderly (17 September 2000), 5: AAS 92 (2000), 876; cf. Id., Letter to the Elderly (1 October 1999): AAS 92 (2000), 186-204.

[84] Cf. Final Message, 26.

[85] Epistula 1, 11: PL 65, 306C.

[86] Cf. John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Familiaris Consortio, 25, 43: AAS 74 (1982), 110-111; 134-135.

[87] Cf. Propositio 45.

[88] Cf. Final Message, 26.

[89] Cf. Second Vatican Ecumenical Council, Pastoral Constitution on the Church in the Modern World Gaudium et Spes, 67.

[90] Origen, De Principiis, IV, 4, 10, SC 268, 427.

[91] John Paul II, Apostolic Letter Mulieris Dignitatem (15 August 1988), 29: AAS 80 (1988), 1722; cf. Benedict XVI, Meeting with Catholic Movements for the Promotion of Women(Luanda, 22 March 2009): Insegnamenti V/1 (2009), 484.

[92] Benedict XVI, Meeting with Catholic Movements for the Promotion of Women (Luanda, 22 March 2009): Insegnamenti V/1 (2009), 484.

[93] Cf. Propositio 47.

[94] Benedict XVI, Meeting with Catholic Movements for the Promotion of Women (Luanda, 22 March 2009): Insegnamenti V/1 (2009), 484.

[95] Second Ordinary General Assembly of the Synod of Bishops, Document Justitia in Mundo(30 November 1971), 45: AAS 63 (1971), 933; cf. John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Ecclesia in Africa, 121: AAS 88 (1996), 71-72.

[96] Final Message, 25.

[97] Benedict XVI, Message for the 2010 World Day of Peace, 11: AAS 102 (2010), 49; cf. Id., Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 51: AAS 101 (2009), 687.

[98] Cf. John Paul II, Apostolic Letter Mulieris Dignitatem (15 August 1988), 31: AAS 80 (1988), 1727-1729; ID., Letter to Women (29 June 1995), 12: AAS 87 (1995), 812.

[99] Cf. Final Message, 27-28.

[100] John Paul II, Apostolic Letter Novo Millennio Ineunte (6 January 2001), 9: AAS 93 (2001), 271-272.

[101] No. 104: AAS 102 (2010), 772.

[102] Rule III, 3; cf. John Paul II, Apostolic Letter Novo Millennio Ineunte (6 January 2001), 45:AAS 93 (2001), 298-299.

[103] Cf. Propositio 48.

[104] Cf. Benedict XVI, Message for the XXV World Youth Day (22 February 2010), 7: AAS102 (2010), 253-254; Id., Post-Synodal Apostolic Exhortation Verbum Domini (30 September 2010), 104: AAS 102 (2010), 772-773.

[105] AAS 97 (2005), 712.

[106] John Paul II, Encyclical Letter Evangelium Vitae (25 March 1995), 57: AAS 87 (1995), 466.

[107] The Synod Fathers referred to different situations, including those involving: children killed before birth, unwanted children, orphans, albinos, street children, abandoned children, child soldiers, child prisoners, children forced into labour, children ill-treated on account of physical or mental handicap, children said to be witches or warlocks, children said to be serpents, children sold as sex slaves, traumatized children without any future prospects, etc. Cf. Propositio 49.

[108] Cf. John Paul II, Letter to Children (13 December 1994): Insegnamenti XVII/2 (1994), 1077.

[109] Cf. Final Message, 30.

[110] Encyclical Letter Populorum Progressio (26 March 1967), 14: AAS 59 (1967), 264; cf. Benedict XVI, Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 18: AAS 101 (2009), 653-654.

[111] Cf. Propositio 20.

[112] John Paul II, Encyclical Letter Evangelium Vitae (25 March 1995), 82: AAS 87 (1995), 495.

[113] Cf. Propositio 53.

[114] Cf. Propositio 52.

[115] Cf. Propositio 51.

[116] Cf. Final Message, 31.

[117] Cf. Propositio 19.

[118] Cf. Benedict XVI, Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 21: AAS 101 (2009), 655-656.

[119] Second Vatican Ecumenical Council, Declaration on Religious Freedom Dignitatis Humanae, 13.

[120] Cf. Propositiones 17 and 29.

[121] Cf. Final Message, 32.

[122] Cf. Benedict XVI, Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 42: AAS 101 (2009), 677-678; cf. Propositio 15.

[123] Second Ordinary General Assembly of the Synod of Bishops, Document Justitia in Mundo(30 November 1971), Proposition 8a: AAS 63 (1971), 941.

[124] Ibid., Propositions 8b and 8c: AAS 63 (1971), 941.

[125] Cf. Propositio 22.

[126] Cf. Propositio 30.

[127] Cf. Congregation for the Doctrine of the Faith, Doctrinal Note on Some Questions Regarding the Participation of Catholics in Political Life (24 November 2002): AAS 96 (2004), 359-370.

[128] Catechism of the Catholic Church, 2419.

[129] Cf. Propositio 24; Benedict XVI, Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 58, 60, 67: AAS 101 (2009), 693-694, 695, 700-701; Catechism of the Catholic Church, 1883, 1885.

[130] Cf. Propositio 25.

[131] Cf. Propositio 26.

[132] Benedict XVI, Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 43: AAS 101 (2009), 679.

[133] Cf. Propositio 54.

[134] Ibid.

[135] Cf. Propositio 55.

[136] Cf. Propositio 54.

[137] Cf. Propositio 28.

[138] Cf. Benedict XVI, Address to Members of the Special Council for Africa of the Synod of Bishops (Yaoundé, 19 March 2009): AAS 101 (2009), 310.

[139] Cf. Id., Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 62: AAS 101 (2009), 696-697.

[140] Ibid., 42: AAS 101 (2009), 677.

[141] Ibid., 36: AAS 101 (2009), 672.

[142] Ibid., 47: AAS 101 (2009), 684; cf. Propositio 31.

[143] Cf. Propositiones 10, 11, 12, 13.

[[144] Confessions, VII, 10, 16: PL 32, 742.

[145] Cf. Propositio 10.

[146] Declaration on the Relation of the Church to Non-Christian Religions Nostra Aetate, 2; cf.Propositiones 3 and 13.

[147] Second Vatican Ecumenical Council, Declaration on the Relation of the Church to Non-Christian Religions Nostra Aetate, 3.

[148] Cf. Final Message, 41.

[149] Cf. Propositio 12.

[150] Cf. Benedict XVI, Message for the 2011 World Day of Peace, AAS 103 (2011), 46-58.

[151] Cf. Propositio 18.

[152] Benedict XVI, Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 30: AAS 101 (2009), 665.

[153] Congregation for Bishops, Directory for the Pastoral Ministry of Bishops Apostolorum Successores (22 February 2004), 33-48; Enchiridion Vaticanum 22, Nos. 1650-1676.

[154] Ep. 33, 1: PL 4, 297.

[155] Benedict XVI, Address to the Bishops of France, Lourdes (14 September 2008):Insegnamenti IV/2 (2008), 321.

[156] Propositio 3.

[157] Cf. Propositio 4.

[158] Cf. ibid.

[159] Cf. Propositio 39.

[160] Cf. Final Message, 20.

[161] Cf. Propositio 39.

[162] Cf. Benedict XVI, Address to the Roman Curia (21 December 2009): AAS 102 (2010), 35.

[163] Ep. 66,1: PL 4, 398.

[164] Saint Ignatius of Antioch, Ad Magnesios, III, 2; ed. F.X. FUNK, 233.

[165] Benedict XVI, Post-Synodal Apostolic Exhortation Sacramentum Caritatis (22 February 2007), 24: AAS 99 (2007), 125.

[166] Apologeticum, 50,13: PL 1, 603.

[167] Cf. Congregation for Catholic Education, Fundamental Norms for the Formation of Permanent Deacons (22 February 1998), 8: Enchiridion Vaticanum 17, No. 167; Congregation for the Clergy, Directory for the Ministry and Life of Permanent Deacons (22 February 1998), 6, 8 and 48: Enchiridion Vaticanum 17, Nos. 291, 294-297, 376-378.

[168] Cf. Lineamenta, 89.

[169] Cf. Propositio 50.

[170] Cf. Propositio 41.

[171] Cf. Propositio 42.

[172] Cf. Second Vatican Ecumenical Council, Dogmatic Constitution on the Church Lumen Gentium, 46.

[173] Cf. Id., Decree on the Missionary Activity of the Church Ad Gentes, 18.

[174] Cf. Propositio 40.

[175] Ibid.

[176] Cf. Letter to Seminarians (18 October 2010): L’Osservatore Romano (18-19 October 2010), p. 12.

[177] Benedict XVI, Address to Members of the Special Council for Africa of the Synod of Bishops (Yaoundé, 19 March 2009): AAS 101 (2009), 311-312.

[178] Cf. Propositio 44; John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Ecclesia in Africa (14 September 1995), 91, AAS 88 (1996), 57.

[179] Cf. John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Christifideles Laici (30 December 1988), 15 and 17: AAS 81 (1989), 413-416 and 418-421.

[180] Propositio 37.

[181] No. 103: AAS 88 (1996), 62-63.

[182] Benedict XVI, Second Special Assembly for Africa of the Synod of Bishops. Meditation during Terce (5 October 2009): AAS 101 (2009), 920.

[183] Ibid.

[184] Second Vatican Ecumenical Council, Dogmatic Constitution on the Church Lumen Gentium, 1.

[185] Benedict XVI, Encyclical Letter Deus Caritas Est (25 December 2005), 39: AAS 98 (2006), 250.

[186] Cf. Propositio 35.

[187] Benedict XVI, Homily in Nazareth (14 May 2009): AAS 101 (2009), 480.

[188] Cf. Id., Post-Synodal Apostolic Exhortation Sacramentum Caritatis (22 February 2007), 49: AAS 99 (2007), 143.

[189] Cf. Propositio 36.

[190] No. 103: AAS 88 (1996), 62-63.

[191] Benedict XVI, Address to Members of the Special Council for Africa of the Synod of Bishops (Yaoundé, 19 March 2009): AAS 101 (2009), 312.

[192] Cf. Final Message, 31.

[193] Ibid.

[194] Cf. John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Ecclesia in Africa (14 September 1995), 124: AAS 88 (1996), 72-73.

[195] Cf. Propositio 56.

[196] Benedict XVI, Encyclical Letter Caritas in Veritate (29 June 2009), 73: AAS 101 (2009), 705.

[197] Ibid., 73: AAS 101 (2009), 704-705.

[198] Cf. Propositio 56.

[199] Commentarium in Isaiam prophetam, Prologus: PL 24, 17.

[200] Cf. Propositio 46.

[201] Benedict XVI, Post-Synodal Apostolic Exhortation Sacramentum Caritatis (22 February 2007), 82: AAS 99 (2007), 168-169; Id., Encyclical Letter Deus Caritas Est (25 December 2005), 14: AAS 98 (2006), 228-229.

[202] Cf. Propositio 8.

[203] Cf. Post-Synodal Apostolic Exhortation Sacramentum Caritatis (22 February 2007), 51:AAS 99 (2007), 144.

[204] Ibid., 83: AAS 99 (2007), 169.

[205] Cf. Propositio 5.

[206] Cf. Propositio 6; John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Reconciliatio et Poenitentia (2 December 1984), 23: AAS 77 (1985), 233-235.

[207] Propositio 8.

[208] Cf. ibid.

[209] Ibid.

[210] Propositio 9.

[211] Benedict XVI, Encyclical Letter Spe Salvi (30 November 2007), 49: AAS 99 (2007), 1025.

[212] Congregation for the Doctrine of the Faith, Doctrinal Note on some Aspects of Evangelization (3 December 2007), 12: AAS 100 (2008), 501.

[213] Cf. Saint Thomas Aquinas, Summa Theologiae, Ia-IIae, q. 106, a. 1.

[214] Benedict XVI, Post-Synodal Apostolic Exhortation Verbum Domini (30 September 2010), 122: AAS 102 (2010), 785.

[215] Propositio 34.

[216] Ibid; cf. Paul VI, Apostolic Exhortation Evangelii Nuntiandi (8 December 1975), 21: AAS68 (1976), 19-20.

[217] John Paul II, Post-Synodal Apostolic Exhortation Ecclesia in Africa (14 September 1995), 31: AAS 88 (1996), 21.

[218] Id., Address to the Members of the Latin American Episcopal Council (9 March 1983):AAS 75 (1983), 778.

[219] Cf. No. 29: AAS 102 (2010), 708.

[220] Benedict XVI, Address to the Members of the Special Council of the Synod for Africa of the Synod of Bishops (Yaoundé, 19 March 2009): AAS 101 (2009), 312.

[221] Id., Encyclical Letter Spe Salvi (30 November 2007), 1: AAS 99 (2007), 985.

[222] Id., Homily at the Final Mass of the Second Special Assembly for Africa of the Synod of Bishops (25 October 2009): AAS 101 (2009), 918.

[223] Ibid.

[224] Cf. ibid.

[225] Benedict XVI, Address to the Roman Curia (21 December 2009): AAS 102 (2010), 34.

[226] Cf. Propositio57.

 

 

© Copyright 2011 - Libreria Editrice VaticanaCopyright © Dicastero per la Comunicazione - Libreria Editrice Vaticana